Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 57 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 470 2017-06-30

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Wanariadha wa baadhi ya nchi ambazo kijiografia mazingira yao yanafanana na baadhi ya maeneo katika nchi yetu wamekuwa wakishiriki katika mashindano ya riadha ya majiji makubwa duniani kama vile New York Marathon, Tokyo Marathon na kadhalika na hivyo kuzitangaza nchi zao ipasavyo.
Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa inafufua mchezo wa riadha ili kutumia kutangaza utalii wa nchi yetu?

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa baadhi ya nchi zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano makubwa duniani na hivyo kuzitangaza nchi zao ipasavyo. Hata hivyo, nchi yetu imeanza kufanya vizuri katika mashindano ya riadha kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma kupitia kwa wanariadha wake kama vile Francis Naal, Samson Ramadhani, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui na Filbert Bayi. Mathalani, nchi yetu imeweza kupata mafanikio katika riadha hivi karibuni kupitia wanariadha wake kama ifuatavyo:-
(a) Alphonce Simbu aliyekuwa mshindi wa kwanza na kupata medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Standard Chartered Mumbai Marathon, India tarehe 15 Januari, 2017;
(b) Cecilia Ginoka Panga aliyeshinda Beijing International Half Marathon yaliyofanyika tarehe 16 Aprili, 2017; na
(c) Emmanuel Giniki Gisamoda aliyeshinda Shanghai International Half Marathon yaliyofanyika tarehe 23 Aprili, 2017.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuleta maendeleo endelevu ya mchezo wa riadha na michezo yote kwa ujumla, pamoja na mambo mengine, Wizara inakamilisha mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 ili kuhakikisha inaendana na mahitaji ya sasa katika maendeleo ya michezo ikiwemo kuimarisha uendeshaji na usimamizi katika ngazi zote, ugharamiaji pamoja na uibuaji na uendelezaji wa vipaji katika ngazi mbalimbali.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendesha mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA ambayo pamoja na mambo mengine, yanalenga kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika mchezo wa riadha. Aidha, hivi sasa Wizara yangu inakamilisha taratibu za kuandaa miongozo ya Kiserikali ili kuwezesha wadau wote kuendesha kuendesha shughuli zao katika mazingira ya weledi na stadi bora za michezo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia kwa kushirikiana na wadau inatekeleza programu mbalimbali za kuendeleza mchezo wa riadha nchini ikiwemo Kilimanjaro Marathon, Bagamoyo Marathon, Tulia Marathon, Heart Marathon na kadhalika ambayo hushirikisha wanarisha kutoka ndani na nje ya nchi. (Makofi)