Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 53 Justice and Constitutional Affairs Wizara ya Katiba na Sheria 440 2017-06-22

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Katika Jimbo zima la Mlimba hakuna Mahakama hata moja, jambo linalosababisha mahabusu kupelekwa Jimbo la Kilombero umbali wa takriban kilometa 260 kuhudhuria mahakama:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama katika Jimbo la Mlimba ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu katafuta huduma ya Mahakama?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo nchini unaongozwa na Sheria ya Mahakimu, Sura 11 ya Sheria za Tanzania (The Magistrate Courts Act, Cap. 11) of the laws of Tanzania. Kifungu cha 3(1) kinaeleza kuwa katika kila Wilaya kutaanzishwa Mahakama za Mwanzo; Kifungu cha 4(1) kinaeleza kuwa kutaanzishwa Mahakama za Wilaya katika kila Wilaya na Kifungu cha 5(1) kinampa mamlaka Jaji Mkuu kutoa amri ya kuanzisha Mahakama za Hakimu Mkazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mlimba, Tarafa ya Mlimba ipo Mahakama ya Mwanzo inayoendelea kutoa huduma hadi hivi sasa. Serikali inatambua kuwa miundombinu ya Mahakama hiyo hairidhishi na hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 tumepanga kujenga Mahakama ya Mwanzo mpya katika Tarafa ya Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umbali na ukubwa wa Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo ya Kilombero na Mlimba na itajitahidi kuhakikisha kwa kadri ya uwezo utakavyokuwa kujenga Mahakama za Mwanzo za kutosha katika Wilaya nzima ya Kilombero ili kusogeza huduma za Mahakama na utoaji haki karibu zaidi na wananchi.