Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 8 Questions to Prime Minister Maswali kwa Waziri Mkuu 1 2020-02-06

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni miaka minne sasa tangu Serikali yenu imeweka zuio kwa vyama vya siasa kufanya wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi. Na tunachozungumza leo Mheshimiwa Waziri Mkuu ni siku 262 zimebaki kufika tarehe 24, 25 Oktoba siku ambayo nchi yetu itafanya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa busara zako binafsi na ni Serikali ambayo wewe ni kiongozi mwandamizi, mnafikiri ni lini mtaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi kujiandaa kwa uchaguzi Mkuu?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili Serikali ina mpango gani wa kuwezesha Taifa kupata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itahakikisha kwamba uchaguzi huu unakuwa huru wa haki na wa halali? (Makofi)

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbowe Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa anaomba kujua ni lini vyama vya siasa vitaruhusiwa kufanya shughuli zake za kisiasa. Vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake, ila tumeweka taratibu muhimu unaowezesha vyama kufanya shughuli zake za kisiasa kama ambavyo tumetoa, kumekuwa na uhuru pia wale wote wanasiasa wote ambao waliomba ridhaa kwenye maeneo yao wakapata ridhaa hiyo kuendelea kufanya shughuli na maeneo yao ambayo wamepata ridhaa. Kama vile Madiwani, Wabunge wanaendelea kufanya shughuli zao za siasa kwenye maeneo yao kama ambavyo wao wanapaswa kufanya shughuli hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia lini tunajiandaa kwa ajili ya uchaguzi, ratiba za uchaguzi zitatolewa na ratiba hizi zitaeleza kuanzia lini shughuli za kampeni zitaanza mpaka lini ili vyama viende sasa kama chama kikaeleze sera zake kwenye maeneo yote ili sasa wananchi waweze kupata fursa ya kuendelea kufanya maamuzi ya sera ipi ya chama gani, inafaa kutuletea maendeleo nchini. Kwa hiyo hilo linaendelea na wote mnajua hata kulipokuwa na chaguzi ndogo pale ratiba ilipokuwa inatolewa kila chama kilikuwa kinaendelea kushiriki na huo ndio utaratibu ambao unaifanya hata nchi kuwa imetulia na watu wote kufanya shughuli zao kama kawaida na tutaendelea kufanya hivyo kwa vyama vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu suala la Tume Huru. Jambo hili hata Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu juzi alitoa maelezo hapa, na mimi nataka nirudie tu; kwamba tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba wa sheria, na kwa mujibu wa Katiba ya nchi kipengele 74 (7), (11), (12) inaeleza kwamba hiki ni chombo huru.

Kimeelezwa pia kwenye Katiba pale kinaundwaje; na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote; iwe Rais wa nchi, iwe chama chochote cha kisiasa au Mamlaka nyingine yoyote ile haipaswai kuiingilia. Kama ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba ndiyo Tume huru. Sasa kunaweza kuwa kuna tofauti ya neno huru hili linataka litambulike vipi lakini chombo kipo kinajitegemea kinafanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu yoyote, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Mwaka 1977. Hayo ndiyo maelezo sahihi na ndiyo ambayo yapo kupitia Katiba na sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe. Ahsante. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Question 1

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu unajua vizuri sana, Serikali yako inajua vizuri sana, Watanzania wanajua vizuri sana kwamba vyama vya siasa vya upinzani vimezuiwa kwa miaka minne sasa kufanya kazi zake za siasa za uenezi. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu unapotupa maelezo ndani ya Bunge ya kuhalalisha kilichofanyika na ukasema ni utaratibu ambao mmejiwekea mmejiwekea kwa sheria ipi. Najua yote hayo unajua vizuri sana, kwamba Tume ya Uchaguzi unayoiita ni huru kwa sababu imeandikwa kwenye katibu si huru na watendaji wake vilevile wamekuwa ni partisan sana na masuala haya yamejitokeza wazi na yanaonekana.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE.FREEMAN A. MBOWE: Weweee!!!

MHE. ESTER A. BULAYA: Naomba muwe na adabu.

MHE.FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu haya ni majibu mepesi ambayo kuna siku mtakuja kujuta katika nchi hii kwa majibu haya mepesi. Je…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ESTER A. BULAYA: Keleleni huko!

MHE.FREEMAN A. MBOWE:… Mheshimiwa Waziri Mkuu, narudia kwa mara nyingine hamuoni ni muda mwafaka sasa Serikali ikaona umuhimu wa wadau mbalimbali ambao wanahusika na masuala ya uchaguzi katika nchi hii kukaa na kutafuta njia bora zaidi ya kwenda kwenye uchaguzi Oktoba kuliko kwenda kibabe kwa namna ambavyo tunataka kwenda?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbowe Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikanushe kwamba Serikali inaongoza kibabe, haiongozi kibabe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbowe ni kiongozi tunazungumza, tunabadilishana mawazo; sote tunapobadilishana mawazo tunalenga kulifanya Taifa hili liwe na usalama, liwe tulivu ili shughuli zetu ziweze kwenda lakini muhimu zaidi Watanzania wanahijtai maendeleo. Kwa maana hiyo tunapoweka utaratibu wa namna ya kuwafikia wananchi na kupata maendeleo jambo hili si la chama kimoja ni kwa nchi nzima. Hakuna Mbunge wala Diwani aliyezuiliwa kwenye eneo lake kufanya siasa na watu wake. Kunaweza kuwa labda kama kuna tatizo mahali fulani kwa utaratibu ule tunaozungumza tunakutana tuambizane wapi kuna shida. Kama wiki iliyopita Mheshimiwa Sugu alieza kwamba kule Mbeya anazuio na OCD na mimi nilimuita hapa tumezungumza. Mkuu wa Mkoa ameungana naye, Mkuu wa Polisi Mkoa ameungana naye. Shida kama ziko kwenye ngazi ndogondogo huko ni suala kuzungumza kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani; tunakuheshimu sana, tunatambua una majukumu kwa chama chako lakini Serikali yetu inaendelea kushirikiana na Viongozi wote kwa Mamlaka zao ili kufanya taifa hili liendelee kuwa salama na tulivu, pale ambako kuna shida ya namna hiyo tuendelee kuwasiliana Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi za Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili suala la Tume hii kuonwa kwamba si huru ni mtizamo wa mtu lakini Kikatiba na utendaji wake uiko huru. Pale ambako panaonekana kuna shida basi kwa utaratibu ule paelezwe kwamba hapa kuna shida lakini hatujawahi kuona Rais akiingilia, chama cha siasa kikiinglia ile Tume iko huru na inafanya kazi yake kama ambavyo imetakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kukiwa na jambo lolote lile unao uhuru wa kubadilishana mawazo ili tuone wapi tusaidie katika kufanya jambo hilo liweze kwenda sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)