Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (12 total)

MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mwaka 2013 Serikali iliuza hatifungani ya thamani ya Dola za Kimarekani milioni mia sita (USD 600m) kupitia benki ya Standard yenye tawi hapa nchini (Stanbic); Shirika la Corruption Watch la Uingereza kwa kutumia vyanzo kama IMF imeonesha kwamba hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanzania hasara ya Dola za Kimarekani milioni themanini (USD) 80.m) na Serikali imelipwa faini Dola za Kimarekani milioni sita (USD Six Million) tu.
Je, kwa nini Serikali haiichukulii hatua Stanbic Bank ili walipe faini zaidi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mahitaji yaliyofanywa na serious fraud office ya Uingereza dhidi ya Standard Bank Group, Serious Fraud Office ilitambua kiasi cha Dola za Kimarekani milioni sita, sawa na asilimia moja ya mkopo ambao Tanzania haikupaswa kutozwa. Tozo (arrangement fee) iliyotakiwa kulipwa kwa Standard Bank Group ni asilimia 1.4. Badala yake tozo iliyoingizwa kwenye mkataba ni aslimia 2.4, na ilithibitika kwamba tozo ya asilimia moja ya ziada haikuwa halali.
Katika hukumu iliyotolewa na Mahakama huko Uingereza Standard Bank Group iliamriwa kulipa faini ya Dola za Kimarekani milioni thelathini na mbili nukta mbili. Kati ya hizo kiasi cha Dola milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania, Dola za milioni sita zikiwa ni fidia na Dola milioni moja ikiwa ni riba.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia taarifa ya hasara kwa Serikali ya Tanzania ya Dola za Kimarekani milioni themanini iliyotajwa na Mheshimiwa Zitto Mbunge wa Kigoma Mjini na hatukupata usahihi wake. Hata hivyo, taarifa ya hasara ya dola milioni themanini imetajwa katika taarifa yenye kichwa cha habari How Tanzania was Short Changed in Stanbic Bribery Payback iliyochapishwa katika gazeti la The Guardian la tarehe 16 Disemba, 2015, likinukuu taarifa ya Corruption Watch ya Uingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa haikutoa maelezo ya namna hasara ya dola milioni themanini ilivyopatikana na kwa kuwa, taarifa iliyonukuliwa kutoka corruption watch pia haielezi jinsi hasara hiyo ilivyokokotolewa, Serikali inashauri Mheshimiwa Mbunge awasilishe taarifa alizonazo tuone iwapo ina vigezo vya kutosha kuisaidia Serikali kujenga hoja ya madai ya hasara hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Benki Kuu imeiandikia Benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni tatu kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za benki na taasisi za fedha. Aidha, sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kimekwisha tarehe 30 Januari. Kwamba Stanbic imewasilisha taarifa ya utetezi wao Benki Kuu na utetezi wao unafanyiwa kazi kwa sasa. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi huo Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. KABWE Z. R. ZITTO) aliuliza:-
Je, ni lini Mradi wa kuzalisha umeme wa Malagarasi utaanza?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya tafiti za kimazingira kuonesha kuwa utekelezaji wa miradi wa kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi katika maeneo ya Igamba Na. III ungekuwa na athari za kumazingira, Serikali itafute eneo lingine. Eneo la Igamba Na. III, lilipatikana na Mkandarasi Mshauri ESBI alianza kazi ya upembuzi yakinifu mwezi Juni, 2010 kupitia ufadhili wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC I). Upembuzi yakinifu na usanifu wa awali (preliminary design) ulikamilika mwaka 2012 na kubainika kuwa maporomoko ya sehemu hiyo yana uwezo wa kuzalisha MW 44.8 na Mkandarasi Mshauri alipewa kazi ya kufanya upembuzi yakinifu na utekelezaji wa miradi kufanywa na Mfadhili mwingine.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa TANESCO inaendelea na taratibu za kumpatia Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina yaani (detail design) na kutengeneza nyaraka za zabuni (tender document) zitakazotumika kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kazi hiyo. Mradi huu unakusudiwa kutekelezwa kwa njia ya EPC (Uhandisi, Manunuzi pamoja na Ujenzi).
Mheshimiwa Spika, taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri zitakamilika mwezi Juni, 2016, kazi ya usanifu wa kina pamoja na taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi itachukua miezi sita. Mkandarasi atakayepatikana ataanza kazi Februari, 2017 na utekelezaji wa mradi utachukua miaka mitatu, fedha zitakazotengwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa utekelezaji wa mradi huu ni shilingi bilioni tano.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji unaogharimu shilingi bilioni 32 ambao unafadhiliwa na Shirika la KFW la Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya ulipangwa kukamilika mwezi Machi, 2015:-
(a) Je, kwa nini mradi huo umechelewa kukamilika kwa mujibu wa mkataba?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani dhidi ya Mkandarasi kwa kuchelewa kukamilisha mradi huo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Manispaa ya Kigoma unaogharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KFW kwa gharama ya Euro milioni 16.32 sawa na shilingi bilioni 39.13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi huu unaotekelezwa na Mkandarasi Spencon Services Limited ulianza mwezi Machi, 2013 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2015. Hata hivyo, baada tu ya kuanza kwa ujenzi Mkandarasi alichelewa kupewa eneo la ujenzi kutokana na matatizo ya fidia. Hali hii ilisababisha Mkandarasi kupewa nyongeza ya muda wa kazi hadi kufikia mwezi Disemba, mwaka 2015. Pia, kubadilika kwa Menejimenti ya Spencon Services Limited na mtaji mdogo kifedha kumechangia kuchelewa kwa ukamilishaji wa mradi wa maji ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba, 2016 utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 66.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia masharti ya mkataba Serikali imechukua hatua dhidi ya Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kumkata fedha (Liquidated Damages) ya Euro 1,632,315.27 sawa na shilingi bilioni 3.9 ambayo ni asilimia 10 ya mkataba kuanzia mwezi Januari, 2016. Vilevile Mkandarasi ameagizwa kuongeza nguvu kazi, vifaa na pia kufanya kazi muda wa ziada zikiwemo siku za mapumziko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mkandarasi ameandikiwa barua ya kumfahamisha kuwa Wizara imemweka katika kundi la Non Performing Contractors, (Makandarasi wasioweza kufanya kazi) na Mamlaka zinazohusika za PPRA na CRB zimejulishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, miundombinu ya msingi kama matenki amekwishajenga, pampu zote ameleta, wananchi wa Kigoma Mjini wataanza kupata maji kuanzia mwezi Aprili, 2017.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mwezi Juni, 2015 Serikali ya Falme ya Kuwait kupitia Wakfu ya Kuwait iliijulisha Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuwa wapo tayari kufadhili mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Delta ya Mto Luiche.
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi huo ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, kujenga viwanda vidogo vya mazao ya kilimo na kuondoa umaskini kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kilimo cha umwagiliaji unaopendekezwa katika Bonde la Mto Luiche, Manispaa ya Kigoma Ujiji una wastani wa eneo la hekta 3,000 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga. Mnamo mwaka 2015 Serikali iliwasilisha ombi kwa Serikali ya Falme ya Kuwait kuhusu uendelezaji wa mradi huo ambapo Serikali ya Falme ya Kuwait ilikubali kwa masharti ya kupewa taarifa ya upembuzi yakinifu (feasibility study report) na maoni kutoka kwa nchi zinazotumia maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hii, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu wa awali mwaka 2015. Hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya manunuzi ya mtaalamu mshauri kwa ajili ya kazi ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hii ikikamilika Serikali itawasilisha taarifa ya kina ya kiwango cha maji kinachohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y MHE. KABWE Z. R. ZITTO) aliuliza:-
Nchi ya DRC inaitegemea Kigoma kiuchumi kwa kiwango kikubwa hususan katika soko la bidhaa na huduma ya bandari ya Kigoma na hivyo wananchi wengi wa Kigoma kutembelea Congo na wale wa Congo kutembelea Kigoma. Changamoto kubwa ni gharama za biashara kutokana na viza kati ya nchi hizo mbili licha ya kwamba nchi hizo zote ni wanachama wa SADC na nchi za SADC hazina viza kwa raia wake.
Je, ni kwa nini Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haziondoi viza kwa raia wake ili kudumisha biashara kati ya wananchi wake kwa lengo la kukuza Kigoma kuwa Kituo cha Biashara cha Maziwa Makuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge napenda kumfahamisha kuwa suala la kutotozana viza ni la kimakubaliano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na si kwamba nchi za SADC hazina viza kwa raia wanaotaka katika nchi moja kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, katika nchi za SADC ilikubaliwa kuwa kila nchi wanachama ziwekeane utaratibu na namna bora ya kuondoa hitaji la viza kwa raia wao. Kwa sasa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wenye pasipoti za kidiplomasia na utumishi hawahitaji kulipia viza kuingia Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Tanzania na DRC zimekuwa katika mazungumzo ya muda mrefu kuhusu namna bora ya kuondoa malipo ya viza kwa raia wake wenye pasipoti za kawaida, lakini mazungumzo hayo yamechelewa kukamilika kutoka na migogoro ya ndani iliyoko katika nchi ya DRC. Hata hivyo, ni mategemeo kuwa kupatikana kwa suluhisho la kudumu la migogoro iliyoko ndani ya nchi ya DRC kutawezesha kukamilishwa kwa taratibu za kuondoa hitaji la viza baina ya hizo nchi hizi mbili kwa haraka.
MHE. KASUKU S. BILAGO (K.n.y. MHE. ZITTO Z. R. KABWE) aliuliza:-
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafirishaji wa Ardhini na Majini (SUMATRA) hutoa vibali vya usafiri kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika.
(a) Je, ni kifungu gani cha sheria kinaipa mamlaka SUMATRA kutoza ushuru kwa wavuvi na wakati huo huo haifanyi hivyo kwa matrekta kwenye kilimo?
(b) Je, Serikali haioni kuwa inadidimiza wavuvi kwa kuwarundikia tozo nyingi na kuwafanya waendelee kuwa maskini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) haitoi vibali wala haitozi ushuru kwa vyombo vya usafiri majini nchini ikiwa ni pamoja na wavuvi wa Ziwa Tanganyika, ila kwa mujibu wa Sehemu ya III, Kanuni ya 18 ya Kanuni za Sheria, zinazoitwa: The Merchant Shipping (Small Ships, Local Cargo Ship Safety, Small Ships Safety, Survey and Inspection for Vessels engaged on Local and Coastal Voyages Inland Waters) Regulations 2006, GN. 106, SUMATRA inalo jukumu la kukagua ubora wa vyombo vya usafiri majini kwa pamoja na vya uvuvi na kutoa Cheti cha Ubora (Seaworthness Certificate) na usajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya majukumu ya msingi ya SUMATRA katika vyombo vya usafiri majini na vya uvuvi ni kuhakikisha kuwa vyombo hivyo ni salama kabla havijaanza kutoa huduma au kufanya shughuli za majini.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, SUMATRA inapokagua vyombo vya usafiri majini kwa mujibu wa Sehemu ya II, Kanuni ya 9 ya Kanuni za Sheria, zinazoitwa: (The Merchant Shipping (Fees) Regulations, 2005), wenye vyombo vya usafiri majini ikiwa ni pamoja na vya uvuvi hutakiwa kulipa ada ya ukaguzi kwa SUMATRA kwa ajili ya ukaguzi uliofanyika. Hivyo, Serikali haikusudii kudidimiza wavuvi wala haijawarundikia tozo nyingi ambazo zitawafanya wawe masikini bali inawahakikishia wavuvi hao mazingira salama kwa ajili ya kufanya shughuli zao za uvuvi.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi kiasi cha kumwagiwa sifa duniani; na moja ya silaha kubwa dhidi ya rushwa ni uwazi.
Je, ni kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujiondoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP)?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Kuendesha Shughuli wa Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership) ulitokana na wazo la Rais wa Marekani wakati huo Mheshimiwa Barack Obama aliyekuwa na nia na lengo la kuzifanya nchi mbalimbali duniani kuwa wazi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo ulizinduliwa kama Taasisi Isiyo ya Kiserikali (NGO) tarehe 20 Septemba, 2011 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijiunga tarehe 21 Septemba 2011 baada ya kukidhi vigezo vya kujiunga ambavyo ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora. Mpango huo ni wa hiari ambapo nchi inaweza kujiunga baada ya kutimiza masharti na hata kujitoa bila kuwepo na kizuizi chochote.
Hadi sasa nchi wanachama dunia nzima ziko 70 tu na kati ya nchi hizo kumi tu ndizo zinatoka Barani Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kushiriki utekelezaji wa mpango kwa zaidi ya miaka minne imeamua kujitoa. Tanzania si nchi pekee iliyojiunga na mpango huo na kisha kujitoa, nchi nyingine kama Hungary na Urusi zilijiunga na baadae kujitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ya Tanzania tangu kupata uhuru imekuwa na mashirikiano ya kikanda na kimataifa katika kutekeleza falsafa ya uwazi na uwajibikaji. Katika kutekeleza falsafa hii , Serikali imejiunga na kutekeleza mipango ya kikanda na kimataifa kama vile Mpango wa Nchi za Kiafrika wa Kujithamini katika Nyanja za Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa (APRM), Shirikisho la Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki na Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana Rushwa kwa Nchi za Jumuiya za Madola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali yetu imesaini mikataba mbalimbali ya mapambano dhidi ya rushwa kama vile African Union Advisory Board on Anti- Corruption pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa. Ni maoni ya Serikali kuwa shughuli zinazotekelezwa kupitia vyombo hivyo zinatosha kwa nchi kuendelea kujijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi, kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania kujitoa katika Mpango wa Kimataifa wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) hakuna madhara yoyote. Mipango inayotekelezwa ndani ya nchi kama ilivyoelekezwa hapo juu inajitosheleza kuendeleza na kuimarisha misingi ya uwazi na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
MHE. ANTHONY C. KOMU (K.n.y. MHE. ZITTO Z. R. KABWE) aliuliza:-
Mnamo tarehe 26 Julai, 2017, Mawaziri wa Uchukuzi wa Uganda, Burundi, Congo DRC na Tanzania walifanya mkutano katika Manispaa ya Ujiji-Kigoma na kuazimia kuwa kuanzia Januari, 2018, Bandari ya Kigoma itakuwa bandari ya mwisho kwa bidhaa ya Burundi na Mashariki ya DRC (Kigoma Port of Destination CIF Kigoma). Pamoja na Azimio hilo, mradi wa Bandari ndogo za Ujiji na Kibirizi zilipaswa kujengwa na kuiwezesha miradi kama ya Ujiji City-Great Lakes Trade and Logistics Centre:-
Je, Serikali mpaka sasa imefikia hatua gani ya kiforodha na kibandari kuiwezesha CIF-Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Mkutano wa Mawaziri wa Uchukuzi wa Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania waliazimia kuwa kuanzia Januari, 2018 Bandari ya Kigoma itakuwa Bandari ya mwisho kwa bidhaa za Burundi na Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaani Kigoma Port of Destination.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa bandari hii pia ni muhimu sana kwa uchumi na ustawi wa Mkoa wa Kigoma na ndiyo inategemewa na wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya jirani katika utaoji wa huduma ya usafirishaji wa bidhaa zinazopitia reli ya kati kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tena kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - Tanzania katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza Bandari ndogo za Ujiji na Kibirizi ili zikikamilika ziwezeshe miradi kama vile Ujiji City –Great Lakes Trade and Logistics Centre. Zabuni za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa bandari hizi zilitangazwa. Hata hivyo, kwa bahati mbaya hakuna mzabuni hata mmoja aliyejitokeza kuomba kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Machi, 2018, TPA imetangaza upya zabuni hizo Kimataifa ili kumpata mzabuni atakayefanya kazi za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na athari za kimazingira. Zabuni hizo zimefunguliwa tarehe 3 Aprili, yaani juzi na jumla ya makampuni 21 yameonyesha nia ya kufanya kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kazi inayoendelea ni kufanya tathmini ya wazabuni ili kumpata mzabuni anayefaa kufanya kazi hiyo. Ni matarajio yetu kuwa kazi itaanza mara baada ya kumalizika kazi ya tathmini na kumpata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo na hivyo kunyanyua kiwango cha utendaji wa Bandari ya Kigoma.
MHE. KIZA H. MAYEYE (k. n. y MHE. ZITTO KABWE) aliuliza:-
Kigoma Ujiji ni Mji wa kibiashara kwa kuwa ni Lango la Magharibi la nchi yetu kuelekea nchi jirani za Maziwa Makuu. Kutokana na hali hiyo Serikali ya Japan kupitia JICA imekuwa ikiandaa mradi wa kuboresha Bandari ya Kigoma kwa miaka kadhaa sasa:-
(a) Je, Mchakato wa mradi huo umefikia hatua gani hadi sasa?
(b) Je, mradi huo utagharimu kiasi gani cha fedha na utaboresha maeneo gani ya Bandari ya Kigoma?
(c) Je, mradi huo utaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Ruyagwa Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa JICA imekuwa ikiandaa mradi wa kuboresha bandari ya Kigoma ambapo tarehe 29 Juni, 2018 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali ya Japan kupitia JICA zilisaini makubaliano ya kitaalam ya utekelezaji ya ujenzi wa gati la abiria, jengo la kusubiria abiria, ghala la kutunzia mizigo na barabara itakayoelekea kwenye gati jipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa JICA inasubiri kibali cha ufadhili huo kutoka Serikali ya Japan. Mchakato wa kumpata mkandarasi umepangwa kuanza Novemba, 2018 kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali yetu na JICA.
(b) Gharama halisi ya mradi zitajulikana baada ya kusaini makubaliano ya ufadhili na kumpata mkandarasi wa ujenzi.
(c) Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Juni, 2019 kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali yetu na JICA.
MHE. KABWE R. Z. ZITTO aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini Serikali ya Tanzania inazuia wawekezaji wa uvuvi kuvua kwa kutumia purseiner katika Ziwa Tanganyika ilhali nchi za Burundi, Zambia na DRC zinazopakana na ziwa hilo huruhusu uvuvi huo?

(b) Je, kwa nini Serikali inawaelekeza wawekezaji wa uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuhamisha uwekezaji wao na kuupeleka mahali pengine nchini na je, huu sio makakati wa kukwamisha maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na watu wake?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Ruyagwa Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini lenye kipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimwa Naibu Spika, si lengo la Serikali kuzuia uwekezaji wa uvuvi wa kutumia purseiner katika Ziwa Tanganyika. Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wake husuani wavuvi wadogo na wazawa wananufaika na rasimali za uvuvi katika kuwaletea maendeleo, inazingatia msingi ya uvunaji endelevu unaoendana na wingi wa rasilimali zilizopo.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, tathimini ya wingi wa rasimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika (stock assessment) iliyofanya mwaka 1998 ilionesha wingi wa samaki ulikadiriwa kuwa tani 295,000. Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kujua wingi wa samaki kwa sasa kabla ya kuridhia shughuli za uvuvi mkubwa ili usiathiri wavuvi wadogo wadogo, wananchi wa kawaida na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kuwa Serikali ina mkakata wa kukwamisha maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na watu wake, isipokuwa kwa sasa hatuna hakika na wingi wa samaki uliopo katika Ziwa Tanganyika kwani mara ya mwisho tafiti ya tathimini ya wingi wa samaki ilifanyika ya Ziwa Tanganyika ilifanyika mwaka 1998. Iwapo tafiti itaridhia uvuvi huu bila kufanya tathmini ya wingi wa samaki wadogo, wazawa wa Kigoma na mazingira yanawaweza yakaathirika.
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y MHE. KABWE Z. R. ZITTO) aliuliza:-

Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapata changamoto za huduma za uhamiaji kutokana na Balozi zetu takribani zote kutokuwa na Maafisa Uhamiaji.

Je, ni lini Serikali itapeleka Maafisa Uhamiaji kuhudumu kwenye Balozi zetu ili kutoa huduma bora kwa raia wa Tanzania kwenye nchi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Kabwe Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji inawajibika kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapata huduma bora za uhamiaji wanapofika kwenye Balozi zetu nje ya nchi. Maafisa Uhamiaji waliokuwa wanatoa huduma za uhamiaji katika Balozi zetu ama wamestaafu au wamemaliza muda wao wa kuhudumu katika Balozi walizokuwa na wamerejea nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha huduma bora za uhamiaji zinaendelea kutolewa kwa raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi, tayari Serikali imewateua maafisa watano kutoka Idara ya uhamiaji ambao wamepatiwa mafunzo ya kuhudumu katika Balozi. Kwa sasa Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wako katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwapeleka Maafisa hao kwenda kuhudumu katika Balozi walizopangiwa.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-

Katika kutekeleza mpango wa kutuma fedha za elimu moja kwa moja mashuleni Serikali hutuma shilingi bilioni 18 kila mwezi kwenye akaunti za shule nchini kwa mujibu wa maelezo ya viongozi kwa umma?

(a) Je, Serikali imeshatuma kiasi gani cha fedha kati ya Januari – Desemba, 2016, 2017 na 2018 kwenda kwenye shule nchini?

(b) Je, Serikali imefanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo na kama zilizotoka Hazina zilifika kwenye shule husika; Je, Serikali ipo tayari kuleta Bungeni Ripoti za Ukaguzi huo?

(c) Kama Serikali haijafanya ukaguzi huo; Je, ipo tayari kuagiza ukaguzi maalum utakaofanywa na CAG na kuweka Taarifa ya Ukaguzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Mpango wa Elimu msingi Bila Malipo kuanzia Januari, 2016 hadi Disemba, 2018 jumla ya Sh.798,170,400,005.04 zimetolewa na Serikali na kutumwa moja kwa moja shuleni. Fedha hizo zimejumuisha chakula kwa wanafunzi, fidia ya ada, uendeshaji wa shule, posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu na Maafisa Elimu wa Kata. Fedha hizi zinajumuisha pia fedha zinazokwenda Baraza la Mitihani kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya Kitaifa kwa ngazi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu wa kawaida wa ukaguzi wa fedha za Serikali, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali hufanya ukaguzi katika Wizara, Taasisi, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mwaka. Kwa kuwa, fedha za Elimu Msingi Bila Malipo ni sehemu ya fedha zinazotumwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwa kuwa fedha hizo hutengwa kwenye bajeti kila mwaka wa fedha, ni dhahiri kuwa fedha hizo hukaguliwa na CAG pale anapofanya ukaguzi kwenye mamlaka husika. Ahsante.