Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Peter Joseph Serukamba (7 total)

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majawabu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mradi wa Kalinzi huu ni mwaka wa tatu mfululizo zinawekwa fedha kwenye bajeti hazijawahi kuja, naomba leo Waziri alieleze Bunge lako, sasa fedha zilizotengwa mwaka huu zitakuja ili mradi huu uweze kutekelezwa?
Swali la pili, tunalo tatizo kubwa sana la mazingira, vijiji vyote alivyovitaja vinategemea kupata maji kwenye mito na ikifika kiangazi karibu yote inakauka, kwa hiyo tatizo linarudi kuwa palepale. Sasa, Serikali haioni imefika wakati kutumia maji ya Lake Tanganyika ili yaweze kuchukuliwa ili kupeleka maji kwenye vijiji vyote hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inatenga fedha kila mwaka kama alivyosema, lakini kutokana na matatizo ya upatikanaji wa fedha, na sisi sote ni mashahidi, uchumi umekumba dunia yote, kwa hiyo hali ya upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo mgumu. Lakini kwa sasa baada ya kuanza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inakusanya fedha vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa fedha itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, na pili kwenye Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji ambayo tunashirikiana na wadau, mwezi Januari mwaka huu tayari tumeanza Programu ya Pili na tuna ahadi za kutosha za kupatiwa fedha kutoka kwa wadau tunaoshirikiana nao.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo sasa utatekelezwa na utafiti umeshakamilika kama nilivyojibu kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili ni kweli kwamba kipindi cha kiangazi maeneo mengi ya Jimbo lako, mito ile inayotiririsha maji inakauka. Lakini pia wewe mwenyewe ni shahidi kwamba sasa hivi kuna mradi mkubwa wa maji ambao tunajenga Mji wa Kigoma na tunachukua maji kutoka Ziwa Tanganyika na mpango huo kwa sasa Wizara ya Maji inataka kutumia vyanzo vyote vya maji ambavyo viko karibu na miji ambayo imepata bahati ya kuwa karibu na vyanzo vizuri vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tumeanza mradi wa maji Mjini Kigoma, na kadri jinsi tutakavyokuwa tunakwenda, yale maeneo ambayo hayatakuwa na chanzo kizuri cha maji tutaendelea kutumia maji ya Lake Tanganyika kufika mpaka kwenye maeneo yenu.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majawabu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, mradi huu wa maji wa Kigoma Mjini utakuwa unazalisha zaidi ya lita milioni 42 kwa siku, Matumizi ya Mji wa Kigoma haitazidi zaidi ya lita milioni 24, wanasema mpaka 25. Mheshimiwa Waziri haoni sasa na hili swali naliuliza mara ya tatu kwamba, mradi huu sasa waongeze vijiji vya jirani ambavyo ni Vijiji vya Mwandiga, Kibingo mpaka Bigabiro pamoja na kwenda Msimba ili na sisi tufaidike kwa sababu, tatizo la maji kwa Jimbo la Kigoma Kaskazini ni kubwa sana?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi huu utazalisha maji mengi zaidi ya lita milioni 42 kwa siku, zaidi ya mahitaji ya wananchi wa Kigoma Mjini. Lengo la Serikali la kuweka mradi huu ni kwamba, lazima tusambaze katika vijiji ambavyo vinazunguka mji ule, ikiwepo na Mwandiga. Kwa hiyo, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itazingatia ombi lake na tutahakikisha kwamba, maji haya yanafika mpaka maeneo hayo aliyoyataja.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa sana nimemshangaa kidogo Naibu Waziri. Kwanza inaonekana historia ya barabara hii haifahamu. Nitaomba kabla sijauliza maswali mawili madogo, niseme kilichotokea.
Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi wa barabara hii ya Mwandiga - Manyovu unaanza, kuna watu waliambiwa na Serikali wabomoe wakafuata sheria wakabomoa, wale waliogoma kubomoa wote walilipwa na Serikali hii. Hapa naulizia wale waliotii sheria.
Mheshimiwa Spika, sasa niulize masawli mawili ya nyongeza.
Je, Rais Magufuli ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi, Sheria ya Babaraba hii anaijua vizuri sana, na Waziri Magufuli alipokuja pale kuomba kura eneo la Kalinzi, tarehe 19, mwezi wa Septemba alisema yafuatayo wakati akisema tungependa vitu gani atusaidie atakapokuwa Rais. Moja ya mambo makubwa manne aliyoambiwa mojawapo ilikuwa ni suala la fidia ya wale watu ambao walitii sheria walipwe. Rais Magufuli alisema maneno yafuatayo, alisema; “Ninajua mgogoro wa barabara hii, wale ambao hawakulipwa wameenda mahakamani, ninawaomba mfute kesi tukimaliza uchaguzi na ninyi mtalipwa.” Wale wote wamefuta kesi. Sasa nimuulize Naibu Waziri, kesi imefutwa, Rais aliahidi, sasa tujiulize, Rais alitudanganya au wewe ndiye unayetudanganya hapa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwahakikishie wananchi wale walioathirika wa kati ya Mwandiga na Manyovu, wakati wanaahidiwa na Mheshimiwa Rais kwamba atawalipa fedha kama wahanga wa ile barabara alikuwa hadanganyi, alikuwa anasema kutoka katika sakafu ya moyo wake.
Pili, tunapolijibu swali hili, kwa sababu swali hili eneo lililopewa nguvu ni eneo la fidia, sasa ukitoa nguvu katika swali kwenye eneo la fidia wakati huku unajua kwamba hawa watu hawastahili fidia inakuwa ni tatizo. Kwa sababu hatuwezi tuka-create precedent, maeneo mengi sana tumewataka watu wa mita 30 toka hifadhi ya barabara wabomoe nyumba zao bila fidia, kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini tunapoongelea kuwalipa wahanga ni kitu kingine na ahadi ya Rais ni kitu kingine.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wale wahanga kwamba Mheshimiwa Rais atatekeleza ahadi yake ya kuwalipa, anawalipa kama wahanga, hatuwalipi fidia. Fidia hatulipi ndani ya eneo la mita 30 au mita 22.5 kwa kipindi kile cha chini ya mwaka 2007, na kwa sasa hatulipi ndani ya mita 30 kila upande.
Ninaomba tukileta precedent hapa tutaleta matatizo katika nchi hii, kama ahadi ya Rais kwa specific case ya eneo la Mwandiga mpaka Manyovu, itatekelezwa kwa asilimia 100 kama ambavyo ahadi nyingine zote za Rais tutahakikisha zinatekelezwa katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majawabu mazuri ya Naibu Waziri anaweza sasa leo akawaelekeza Halmashauri zote nchini kwamba kila mwaka ni mandatory lazima kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa kuwasaidia vijana kupata mitaji na mikopo, tunayo mifuko mingi sana. Moja wa mfuko ambao nimeusema hapa ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao umekuwa ukishirikiana na Halmashauri kupitia SACCOS mbalimbali na vijana wengi wamekuwa wakipata mikopo kupitia katika SACCOS hizo.
Kwa hiyo, nimuondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba kupitia Mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana, kila mwaka tumekuwa tukikopesha vijana na wengi wamefaidika kama nilivyosema hapa isipokuwa tu katika zile asilimia tano za kila Halmashauri ambazo ni utaratibu mwingine tofauti, nako tumekuwa tukitoa msisitizo mkubwa kuhakikisha kwamba Halmashauri zinatenga asilimia tano za mapato yao ya ndani kwa ajili ya vikundi vya vijana.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majawabu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Mto Makere hali yake ni mbaya sana pamoja na Mto Malagarasi, lakini sababu kubwa kuna mifugo mingi sana imeingia huko na hakuna anayeitoa. Nataka kujua ni lini sasa Serikali tutakwenda kutoa mifugo iliyovamia kwenye vyanzo vya Mto Makere pamoja na Mto Malagarasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijajibu swali la nyongeza, nitoe maelezo ya utangulizi. Wananchi wote nchi nzima kwa mujibu wa Sheria yetu ya Na.20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Uhifadhi wa Mazingira kila Mtanzania ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira. Sheria yetu pia inatoa haki kwa kila Mtanzania aishi katika mazingira safi, salama na ya kiafya. Kwa hiyo, sheria inazuia watu wengine wasiwakere watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Makere ni kweli kabisa kwamba mto ule kwenye vyanzo vyake ulivamiwa lakini uvamizi ule ulikuwa unafanywa na wale wahamiaji haramu ambao wanakuja kule Kasulu, wanawakodi wananchi wa Kasulu halafu wengine wanaenda wanakata miti usiku wengine wanalima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Wilaya ya Kasulu tumeweza kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yamevamiwa na kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi mifugo yote tumeiondoa na hata hivyo kuhusu miti; Nyarugusu, Makere yenyewe, Kwamba, Mwadivano na Kalimungoma, katika maeneo yote yale wamepanda miti zaidi ya 50,500,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Watanzania pamoja na vyombo vya habari wameanza kupotosha kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa jana kule Kagera kwamba sasa wananchi ni ruksa kwenda kuvamia maeneo oevu, maeneo ya vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kauli ya Rais isije ikapotoshwa wananchi wakaenda kuvamia maeneo ya mito na kuanza kulima. Kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais Watanzania waelewe vyanzo vya maji ndivyo uhai wetu, mito yote itakauka, hakuna anayeruhusiwa kwenda kwenye chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Rais ametumia kifungu cha 57 cha sheria hiyo kwamba pale ambapo kunakuwa na changamoto, wananchi wale ambao wako Karagwe wamekuwepo pale hawana ardhi, Rais ametuomba tushirikiane na uongozi wa mkoa kuhakikisha wale wananchi wanapatiwa maeneo mengine lakini siyo kuwaondoa.
Kwa hiyo, hamruhusiwi na msije mkasema kwamba Rais amewaruhusu wananchi kinyume na sheria. Ahsante.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, Mfuko wa Mawasiliano Vijijini haujapewa pesa za kutosha lakini Waziri anasema vijiji hivi vimeingia kwenye Mfuko wa Mawasiliano Vijijini. Je, nataka kujua kama kweli umeingia kazi hii inaaza lini?
Swali la pili, nilidhani Serikali ingekuja na jibu la kusema badala ya kutegemea bajeti ya Serikali, waongee na makampuni ya simu kama Halotel, Airtel, Vodacom na Tigo ili waweze kupeleka mawasiliano kwenye vijiji hivyo kwasababu mbele ya Kazinga kuna Mwamgongo ambayo Mwamgongo tayari kuna mawasiliano na huwezi kufika Mwamgongo lazima uanzie Kazinga. Kwa hiyo, nilitarajia Serikali badala ya kutegemea bajeti peke yake, nikuombe uende ukaongee na makampuni ya simu ili yaweze kupeleka huduma hiyo kwenye vijiji hivyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyoeleza katika jibu la swali la msingi kwamba ujenzi wa Miundombinu kwa ajili ya mawasiliano utafanyika mara baada ya fedha za mradi zitakapopatikana na vijiji hivi vyote tulivyovitaja tayari vimo katika mpango, vimeingia katika mpango vinasubiri upatikanaji wa fedha. Lini? Ni mara fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ombi lake la pili, labda tu nimfahamishe kwamba, mfuko wa mawasiliano kwa wote unatekeleza miradi mbalimbali kupitia Kampuni hizo hizo za Halotel, Tigo, Airtel na Vodacom, wao hawatekelezi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya yanapata ugumu wa kupeleka mawasiliano katika vijiji kwa sababu wanasema havina faida na hivyo Serikali inatoa ruzuku kupitia mfuko huu wa mawasiliano kwa wote na fedha zinapopatikana tunatangaza tender na makampuni hayo ndiyo yanayoomba hizo zabuni kupeleka mawasiliano hayo katika maeneo hayo.
Kwa hiyo, nadhani ni kweli Halotel, Airtel, Voda hata kama tutakwenda kuwashawishi siyo rahisi wao kukubali kwasababu wanajua hakuna faida katika maeneo hayo na hivyo inahitajika ruzuku ya Serikali na ruzuku ya Serikali tunaitoa kupitia mfuko huu wa Mawasiliano kwa Wote.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwanza KACOFA iko kwenye Kata yangu, Organic iko Kalinze ambako ni Kata yangu. Kwa masikitiko makubwa Waziri anasema kesi iko Mahakamani, si kweli hakuna kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kilichotokea, KACOFA walipeleka Kahawa na hawa Organic-Kalinze walipeleka Kahawa. Kile kiwanda kilipouza Kahawa ile kikawalipa KACOFA, hakikuwalipa Kalinze Organic. Kalinze Organic walipoanza kufuatilia pesa zao wamefanya usuluhishi Wizarani na Bodi ya Kahawa mwisho wake Kiwanda kikasema kitawalipa, naomba nitoe maelezo haya; kitawalipa Organic taratibu.
Mheshimiwa Spika, toka mwaka 2011 kiwanda kile ambacho kilikubali kuanza kuwalipa watu wa Kalinze Organic, kwamba tutawalipa taratibu mpaka leo hakijalipa. Waziri anakuja leo hapa anasema suala lipo kwa Attorney General wakati wameshakubaliana waanze kuwalipa taratibu.
Mheshimiwa Spika, swali langu; naomba Wizara isimamie watu wa Kalinze Organic waweze kulipwa fedha zao kwa sababu makosa haya yamefanywa na kiwanda kile cha Moshi.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi alivyojibu hili swali la msingi la Mheshimiwa Albert Obama. Jambo hili ni la siku nyingi na hatua za awali kama anavyozisema Mheshimiwa Serukamba ni kweli zilichukuliwa namna hiyo. Kosa lililofanyika ni ku-identify nani anatakiwa kulipwa baada ya yule kupeleka ile kahawa kule mnadani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Bodi ya Kahawa ilivyopokea yale malipo ikapeleka kwa mtu ambaye alitajwa na mtu aliyeleta kahawa kwamba ndiye beneficiary wa hiyo kahawa; kwa hivyo wakamlipa na wale watu wakapokea pesa isiyo yao na wakaitumia.
Mheshimiwa Spika, baadaye ilipoonekana kwamba wamepokea pesa isiyo yao na wametumia, kwanza wakatakiwa wasuluhishwe tu amicably, wakaitwa, wakakiri kwamba watalipa msimu utakaofuata, kwamba watakapouza kahawa msimu unaofuata watalipa hilo deni. Wale waliokuwa wanadai Mheshimiwa Serukamba wakakubaliana na hiyo position, kwamba watapewa pesa yao msimu utakaofuata.
Mheshimiwa Spika, msimu uliofuata wale mabwana wa KACOFA hawakupeleka kahawa, kwa hivyo sasa kukawa na default ya makubaliano hayo; na baada ya hapo ndipo taratibu zikaanza. Nikiri tu kwamba jambo hili lilienda polepole lakini sisi safari hii tulichokifanya tumelipeleka kwenye vyombo vya uchunguzi kwanza tujiridhishe kwa nini walitumia hela ambayo si yao at a time wakati ya kwao walishalipwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, humu ndani kuna jinai katikati ya hili jambo, kwamba mtu amekuta benki fedha ambayo si kwake lakini bila kuuliza benki hela hii imetoka wapi, ameitumia, Sheria za Fedha ziko wazi, umeona! Sasa katika hatua hiyo ndiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali atatushauri sasa hivi tuendelee na hatua gani.
Mheshimiwa Spika, kama atatushauri tuwapeleke Mahakamani ili wale viongozi wa ule Ushirika waweze kuchukuliwa hatua wachukuliwe hatua, kwa sababu as we speak hawa hela ya kuwalipa wale wenzao mara moja, kwamba tungewaambia leteni hizi pesa tuwalipe wale ambao wanastahiki ya kupata hizo pesa.