Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Albert Ntabaliba Obama (13 total)

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, kupongeza Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. Kwanza pongezi zimuendee Mheshimiwa Rais mwenyewe, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuikazania barabara hii alipokuwa Waziri wa ujenzi. Lakini niendelee kupongeza Wizara ya TAMISEMI, nayo imechukua juhudi hiyo ili iweze kujengwa. Lakini naomba nimpongeze tena Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuiweka kwenye mpango barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali moja dogo la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye Jimbo letu na Wilaya yetu ya Buhigwe makao makuu ya Wilaya yamebadilika kutoka Kasulu kwenda Buhigwe lakini tunazo barabara nyingine ndani ya Halmashauri yetu ambazo inabidi zichongwe kwa ajili ya kufika makao makuu na kupunguza urefu wa kuzunguka. Tunazo barabara kama nane ambazo zinahitaji kama shilingi milioni 950. Naomba ushauri wako.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukiweka rekodi sawa, Mheshimwa Obama toka kipindi chote cha miaka mitano ambapo alikuwa kama partner wangu wa karibu zaidi alikuwa akizungumzia maeneo haya ya barabara zake na amefanikiwa kuhakikisha kwamba wamehamisha makao makuu. Lakini nikijua wazi kwamba Sera ya Barabara tunaanza kipaombele katika zile barabara za kwanza zilizokuwa bora zaidi. Maana sera ya barabara ndiyo ilivyo hivyo; zile barabara ambazo hazijafunguliwa zinapewa kipaumbele cha mwisho zaidi.
Mheshimiwa Mweyekiti, sasa kwa sababu barabara hii kwa jinsi Mheshimiwa Mbunge alivyouliza ni barabara mpya, lengo ni ku-connect vizuri, kurahisisha ule umbali uwe mfupi zaidi. Nimsihi Mheshimiwa Mbunge, hili ni jambo jema, wananchi lazima wapate huduma, lakini nipende kuwahamasisha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo mumuunge mkono Mbunge huyu sasa katika vile vipaumbele vya kufungua barabara hizo mpya; kwa sababu hii ni barabara ya ndani ya Halmashauri, jambo hili katika Kamati ya Uchumi hali kadhalika katika Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani muangalie jinsi gani sasa mtatumia own source japo angalau kuanza kulifungua. Ofisi ya Rais TAMISEMI katika suala zima la kufungua barabara zake za vikwazo tutaangalia jinsi gani kwa njia moja au nyingine zile Halmashauri za pembezoni zote ambazo zina changamoto kubwa za miundombinu ya barabara tutaziangalia kwa jicho la karibu ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii katika maeneo yao.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza naomba nipongeze juhudi za Serikali katika kutatua tatizo la maji nchini, lakini namba mbili naomba niendelee kuipongeza Wizara ya maji kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Mnanila, wananchi wa Kata ya Mwayaya na Kata Mkatanga katika majibu ya Waziri anasema utekelezaji wa maradi huu utaanza katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji, watu wale hawaelewi programu ya pili, ya tatu hawaelewi. Swali lao, je, mradi huu unaanza kutekelezwa lini?
Swali la pili Jimbo letu la Buhigwe bado lina vijiji na Kata ambazo kwa kweli bado tuna matatizo makubwa ya maji. Je, Waziri anaweza akatuma wataalamu wake kwenda kwenye Kata ya Rusaba Kibande, Kilelema, Mgera, Kibigwa na Nyaruboza ili kufanya tathimini ya gharama za kupeleka maji katika vijiji vile ili navyo tuweze kuviingiza kwenye programu hapa baadaye?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza hii Programu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inaanza lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya Kwanza ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tuliianza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2006/2007 ambayo imekamilika mwaka 2015 Disemba na katika programu hiyo tulikuwa na wadau wanaotuchangia fedha pamoja na Serikali yenyewe nayo imekuwa inatoa fedha kwa ajili ya utekelezajiwa miradi ya maji. Katika programu hiyo Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi kwamba miradi ya Munzenze, Kirungu na Nyamgali, ilianza kutekelezwa na sasa hivi ina maendeleo mazuri tu katika hiyo programu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa programu ya pili tumeianza mwezi Januari, 2016, inaendelea, nayo itadumu kwa muda wa miaka mitano na katika programu hiyo wadau wa maendeleo tayari wameshatoa ahadi ya kutuchangia dola bilioni tatu na nukta tatu. Lakini hiyo ni pamoja na Serikali nayo itaendelea kukusanya fedha na kuchangia kwenye utekelezaji wa miradi kwenye vijiji ambavyo bado havijapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna vijiji ambavyo bado havijafikiwa na hii programu na Mheshimiwa Mbunge ameomba kwamba je, tutatuma wataalam lini? Mheshimiwa Mbunge natambua kwamba unayo Halmashauri ya Buhigwe, lakini Halmashauri ya Buhigwe bado ni changa, tutakachofanya na ambacho tumeshaanza kufanya sasa hivi ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, inaendelea kuajiri wataalam na kuwapeka katika Halmashauri yako na Halmashauri nyingine zote ambazo zina upungufu wa wataalam. Ili tuwe na wataalam maeneo husika kuliko kuwachukua wataalam kutoka Wizarani. Lakini pale inapohitajika kama utaalamu unahitajika zaidi basi tutakuwa tuko tayari Mheshimiwa Mbunge kuja kutoa utaalamu zaidi kwenye eneo lako.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niipongeze Wizara kwa majibu mazuri, baada ya hapo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Manyovu - Kasulu imekuwa ni kero kubwa sana hasa wakati huu wa mvua na sasa hivi nauli ya kutoka Manyovu - Kasulu imefikia mpaka shilingi 10,000; na tunayo barabara nyingi ya lami ya kutoka Kigoma mpaka Manyovu yenye urefu wa kilometa 60 ambayo nauli yake ni shilingi 3,000. Kwa hiyo, umuhimu wa kujenga barabara hii na kuianza mapema inajionyesha kwa vigezo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua, Wizara imekiri kwamba inafanya upembuzi yakifu, wananchi wa Buhigwe wanataka kujua upembuzi yakinifu unaisha lini na ujenzi unaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Rais alipokuwa akijinadi tuliita vijiji vya Mlela, Buhigwe, Kavomo, Nyankoloko, Bwelanka na akaahidi kwamba atajenga barabara ya kilometa tano katika Wilaya ya Buhigwe, je, ni lini ahadi hiyo itatimizwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Ntabaliba kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia miradi mbalimbali ya Miundombinu katika Wilaya yake na Jimbo lake, nikupongeze sana. Mimi ninakuhakikishia kama ambavyo tumekuwa tukiwahikishia katika ofisi zetu mimi na Waziri wangu, kwamba tutashirikiana na wewe kuhakikisha mambo yote ambayo tuliyaahidi katika Wilaya yako yanatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la msingi, ujenzi utaanza baada ya kukamilika upembuzi na usanifu wa kina, kwa maana unaofanywa na kufuatiliwa na wenzetu wa AfDB. Nikuombe tu kwa kuwa anayefanya si Serikali, kazi hii inafanya na AfDB chini ya Afrika Mashariki suala la lini ni gumu kukueleza isije ikaonekana tunasema uongo hapa Bungeni. Nikuhakikishie suala hili litakamilika katika kipindi kifupi kijacho na baada ya hapo shughuli za ujenzi zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, nimuhakikishie, kama ambavyo tulimuhakikishia ofisini, kwamba kilometa zake tano ambazo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi zitatekelezwa mara baada ya masuala haya ya miradi ambayo ni kiporo yatakapokamilika; na uzuri wake sehemu kubwa za viporo zinakamilika mwaka huu ujao wa fedha baada ya hapo tutakamilisha ahadi zingine zote ambazo Mheshimiwa Rais aliziahidi hasa za kilometa tano, kilometa sita katika sehemu mbalimbali za Miji ya Tanzania hii.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Uharibifu wa vyanzo vya maji katika Taifa letu la Tanzania ni mkubwa mno. Namshukuru Mheshimiwa Waziri amesema vizuri kwamba sheria tunazo lakini namna ya kusimamia hizo sheria ili vyanzo visiharibike ndiyo hafifu. Je, Wizara sasa inajipambanua vipi kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa kwa nguvu zote hapa nchini Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna wakati ambao Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kulinda vyanzo vya maji kwa nguvu zote ni Serikali ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie wewe na Watanzania wote wanaotusikiliza, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliunda Task Force ikaenda kwenye Great Ruaha ambako walikuwa wanaharibu vyanzo vya maji kuhakikisha kwamba wanafanya usimamizi, kutoa mafunzo na kuwaelekeza wananchi. Pia tumeenda Bonde la Usangu na Ihefu, tumeondoa wafugaji wote kwa maana ya kutumia nguvu kubwa kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinaimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Januari Makamba, ule Mto wa pale Katavi ambao ulikuwa umeziba kabisa, Mto Kachima, alienda pale akakuta mkulima mmoja ameweka banio amezuia maji viboko wanataka kufa njaa na watumiaji wengine hawana maji, akazibua na sasa maji yanaendelea kutoka. Kwa hiyo, tutaendelea kutumia nguvu na sheria kuhakikisha kwamba hakuna atakayevunja sheria. Yeyote atakayevunja sheria hatasalimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenu ninyi nitoe darasa la MEMKWA kwa wale walioikosa yaani Mpango Maalum kwa Walioikosa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria niliyoisema Na.20 ya mwaka 2004, kifungu cha 57, Waziri anaweza akatoa kibali kwenye maeneo ya mita 60 kutokana na changamoto aliyoiona. Ndiyo maana wakati mwingine mnaona hoteli zinajengwa ndani ya mita 60 ni kutokana na vibali. Kwa hiyo, Rais wetu hajavunja sheria na ninyi mtakapowachochea wananchi kuvunja sheria, sheria ya Rais Magufuli itapambana na ninyi. Ahsante sana. (Kicheko/Makofi)
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Bunge lililopita tulitunga sheria ya kufuta hotel levy, lakini katika Mkoa wa Dar-es-Salaam hotel levy imeendelea kutozwa. Na Mheshimiwa Waziri anakiri na kusema kwamba, Sheria za Bunge zinazotungwa ziheshimiwe. Nini kauli ya Waziri?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile Sheria ya Hotel Levy inajieleza, ukiisoma vizuri kuna definition ya hoteli, inatakiwa iwe na sifa ipi ili ikidhi kuwa hoteli. Sasa kumekuwa na mchanganyiko kati ya hoteli na guest house. Ukiisoma Sheria ya Hotel Levy inaelekeza wale ambao ni VAT registered hawatakiwi kutoa hotel levy, lakini wale ambao wako chini ya Halmashauri bado sheria imesimama. Kwa hiyo, ni suala tu la kusoma sheria vizuri na kuitafsiri vile inavyotakiwa.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa napenda tu kutoa msisitizo kuhusiana na masuala yale ya kutoza ushuru. Nilikuwa naomba Halmashauri kwa kuwa, zenyewe ndio zinazoweka maeneo ya vizuizi na kukagua juu ya masuala ya kutoza ushuru ni vema sasa kuwe na mizani ambayo itawezesha hawa wananchi kuona kwamba mzigo wao una hiyo tani moja iliyoruhusiwa au la. Kinyume na hapo kwa kuangalia tu magunia kwa upande mmoja inakuwa inawafanya aidha wananchi wananyanyasika au wenyewe Halmashauri kutokupata ushuru ulio sahihi.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize maswali mawili ya nyongeza na ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwamba kuanzia mwaka ule mlipatambua kwamba pana umuhimu wa kuwa na soko la kimataifa na ni ukweli ulio wazi kwamba sisi tuko mpakani na tumepakana kwa ukaribu na tunafanya biashara ya pamoja. Lakini huu mpango mliokuwanao wa masoko ya mpakani bado ni muhimu sana kutekelezwa katika maeneo haya ya Mnanila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu niseme eneo tulilokuwa tumelitoa halikuwa na fidia yoyote. Sasa nataka kujua Wizara sasa itafanyaje kwa sababu umetuomba Halmashauri tuweze kuliweka kwenye mpango, lakini fedha zinazohitajika kujenga soko hili ni kubwa.
Je, Wizara itafanya nini sasa kuhakikisha kwamba, soko hili linajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumejenga soko lingine la mpakani ambalo liko maeneo ya Kijiji cha Nyamugali; tulikuwa na mpango vilevile Kibande na Kilelema, lakini tuna changamoto ya daraja sasa hivi kwenye Soko la Nyamugali ambalo Wizara yako ilijenga, ili watu wa Burundi waweze kuingia nchini. Je, Wizara iko tayari kutujengea daraja Nyamugali pale, ili wafanyabiashara waweze kupita kirahisi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Obama, kwamba suala la masoko ya mipakani ni suala muhimu na linaongeza tija katika uzalishaji na ukuzaji wa mazao ya viwanda ambayo Serikali yetu ndicho inachokisisitiza. Sasa kama ambavyo nimemueleza awali, ni kwamba nimuombe aweke uhitaji wa soko hilo katika bajeti ya halmashauri, na wakati huo kama tulivyoahidi tutaendelea kuwatafuta wahisani mbalimbali ili kuweza kusaidia ujenzi wa soko hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Daraja la Mto Kigale, kama sikosei ulivyotamka, ni kwamba kama ambavyo tunazidi kusisitiza kwamba biashara za mipakani kati ya nchi na nchi mbali tu ya kufanya shughuli za kibiashara zinajenga pia mahusiano na kuziwezesha nchi hizi mbili kuishi vizuri na kuondoa umaskini kwa pamoja. Kwa hiyo, mimi suala hilo nalichukua na litaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa vikundi vingi vimehamasika na wengi wanahitaji mkopo na uwezo wa Halmashauri yetu siyo mkubwa kiasi hicho na katika Wizara mbalimbali tunazo fedha kwa ajili ya maendeleo ya vijana katika mifuko mbalimbali.
Ni lini TAMISEMI itaunganisha nguvu na Wizara nyingine ili sasa na sisi kule fedha hizo ziweze kuwafikia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kila siku tunasikia kwenye vitabu vya CAG na Wabunge wakilalamika kwamba hizi fedha haziendi kwa wananchi kutoka kwenye halmashauri. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba sheria hii ya asilimia kumi kwenda kwa akina mama, vijana na walemavu itatekelezwa kiufasaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza juu ya uwezo mdogo wa Halmashauri na kuitaka Serikali kuunganisha nguvu kupitia fursa tofauti tofauti, naomba nimhakikishie kama ambavyo amesema yeye mwenyewe kuna fursa kwa mikopo kwa vijana kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu ambayo iko chini ya Mheshimiwa Mhagama ni fursa ambayo ni vizuri wananchi wa Buhigwe wakaitumia katika kuweza ku-access mikopo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili juu ya halmashauri kusuasua katika kutenga asilimia 10, anataka kauli ya Serikali. Kama ambavyo nimekuwa nikisema na leo narudia hata kama ingepatikana shilingi moja kinachotakiwa ni asilimia kumi ya shilingi moja hiyo itengwe. Kama ambavyo nilishawahi kujibu hapa katika moja ya maswali wakati tunaenda kukamilisha Finance Bill kuna kipengele ambacho kitampa Waziri mwenye dhamana ili iwe ni takwa la kisheria na kama kuna Mkurugenzi yeyote atashindwa kutenga fungu hilo hatua ziweze kuchukuliwa.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu mazuri na kihakika kama Wizara wanaonesha wanalitambua suala hili vizuri. Kwa hilo, nawapongeza sana kwa majibu haya.
Mheshimiwa Spika, kuanzia 2011 - 2018 ni miaka saba sasa, hawa wakulima 435 wanaodai zaidi ya milioni 150 au Dola 74,000 bado wanadai. Kwa kuwa Bodi ya Kahawa ilifanya makosa kumlipa mtu mwingine na Mheshimiwa Waziri amekiri kwenye majibu yako kwamba iko kwa Mwanasheria, wakulima hawa wanataabika na hii ni Serikali ya wakulima, ni lini fedha hizo zitapatikana na Mwanasheria ataweza kuliharakisha suala hili?
Mheshimiwa Spika, la pili kwa kuwa hii inatokana na matatizo ya soko hili la kahawa, ni mkakati gani uliopo wa bei na masoko ya kahawa kwa wakulima wetu? Wananchi wanataka kusikia. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana suala zima la zao hili la kahawa katika jimbo lake. Kwenye maswali yake madogo mawili ya nyongeza, mimi nimejibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba hili suala liko Mahakamani na jambo linapokuwa Mahakamani, sisi kama Serikali tunaviachia vyombo vya sheria viweze kuchukua mkondo wake na ukizingatia pia Mwanasheria Mkuu ndiyo in charge katika suala zima hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la nyongeza, ni kwamba, kama Serikali hata zao la kahawa tumejipanga na tumesema tunafufua, tunaimarisha Vyama vya Ushirika kuhakikisha kwamba wakulima wetu wa Kitanzania hawaonewi na wanakuwa na strong bargaining power kupitia Vyama vya Ushirika ili bei zao ziwe nzuri na mazao yaweze kuwa bora. Nashukuru.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tunacho Kituo cha Mlyama ambacho kimejengwa kwa muda mrefu sasa hakijamalizika na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani analijua hilo na pale Wilayani tuna kituo ambacho kinatumiwa kwenye nyumba ambayo siyo nzuri na haitoshi; na kwa majibu haya kwamba wametenga eneo; swali linauliza kwamba ni lini wanaanza kujenga? Hayo maeneo tunashukuru wanayo, lakini swali, wanaanza kujenga lini?
Mheshimiwa Spika, la pili; tuna matukio makubwa sana ya ujambazi yanayotokea hasa baada ya Wakimbizi kurudishwa kwenda Burundi na Jimbo langu linavamiwa kila siku iendayo kwa Mungu na juzi mwanajeshi mmoja ameuawa baada ya kuwa wameenda ku-intervene mashambulio hayo na vitendea kazi ni hafifu.
Je, ni lini sasa vitendea kazi vya magari na pikipiki vitaongezwa kwenye Wilaya ile? Yeye mwenyewe anayo taarifa kwamba ujambazi ni kila siku. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini kituo hiki kitajengwa; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua changamoto ya location ya Jimbo lake, pale ambapo tutapata fedha ni katika vituo ambavyo tutavipa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kujibu swali lake la pili ambalo litahusisha vilevile pamoja na upelekaji wa vitendea kazi ili tuweze kukabiliana na changamoto ambayo ameizungumza ambayo tunaitambua na tumeshaanza kushughulika nayo.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kabisa Wizara hii inafanya kazi kubwa na ya kutukuka, lakini ni ukweli unaojulikana kwamba sisi katika Mkoa wa Kigoma na Katavi na hasa wananchi wangu wa Buhigwe umeme umechelewa kufika. Hivyo kwa commitment hii sasa ya Serikali kwamba ule mgogoro mtakuwa mmeumaliza kwamba Mei Mkandarasi atakuwa site. Kwanza kwa hatua hiyo kwa niaba ya wananchi wa Buhigwe na Mkoa wa Kigoma tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; viko vijiji kama ulivyovitaja mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba vimeshapatiwa umeme lakini kwenye vitongoji umeme bado haujaenda. Nataka kufahamu mkandarasi huyu atakayeenda kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki je, atapeleka kwenye vitongoji, kwenye vijiji ambavyo tayari vimeshapewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, nini commitment ya Serikali kwa sababu sisi mmetucheleweshea umeme kwa muda mrefu na wananchi wangu wanahitaji umeme kwenye vijiji vyao. Je, mkandarasi hamtaweza kumkwamisha kwamba hamna hela? Naomba commitment ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwape pole wakazi wa Mikoa ya Kigoma na Katavi, lakini niwashukuru sana Wabunge wa maeneo hayo ya Mkoa wa Kigoma, Jimbo la Buhigwe, Kasulu, Uvinza pamoja na Kigoma Vijijini pamoja na majimbo ya Mkoa wa Katavi kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia suala hili na kuwa na matumaini na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati pia nimepokea pongezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake yalikuwa mawili ambalo moja lilijielekeza vijiji ambavyo vimepatiwa umeme kama ambavyo jibu langu la msingi limesema, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo ambayo Serikali inatambua yapo maeneo ya vijiji yalipata umeme lakini vipo vitongoji havikupata huduma hiyo na ndiyo maana Serikali imekuwa ikitekeleza mradi wa densification yaani ujazilizi na kwa sasa kwa mwaka unaokuja wa fedha 2018/2019 Serikali imeandaa mpango wa densification awamu ya pili ambayo itaenda kwenye mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa huu wa Kigoma. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi ambao wote vitongoji ambavyo havina umeme kwenye vijiji vyenye umeme vitapatiwa huduma hiyo kupitia mradi wa densification.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mkandarasi huyu atakapoanza kazi Mei, 2018 hatakwamishwa kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Fedha mpaka sasa imeshatoa pesa zaidi ya shilingi bilioni 221 ambavyo imetokana na chanzo hiki cha umeme (REA) ambao umetokana na tozo ya mafuta. Kwa hiyo, nimthibitishie Mbunge kwamba tatizo la pesa halipo, asante. (Makofi)
MHE. ALBERT N. OBAMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nishukuru majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli kwamba tuna upungufu mkubwa nchi nzima wa Walimu wa sayansi na hesabu na kwenye jibu lake la msingi ameonesha kwamba Buhigwe ina upungufu wa asilimia 46. Sasa na hiki kimekuwa ni kikwazo ambacho kinatufanya kwamba ufaulu wetu uwe mdogo na kule ni pembezoni, kwamba watoto hawawezi kupata namna ya kuweza ku--access namna ya kujisomea kwa kufundishana. Je, ni lini itaweka umuhimu wa kuongeza Walimu wa sayansi katika Wilaya ya Buhigwe?

Mheshimiwa Spika, la pili nipongeze wananchi wa Wilaya ya Buhigwe kwa juhudi na kujitolea kujenga maabara na kujenga madarasa. Je, ni lini Serikali italeta sasa vifaa vya maabara kwa sababu tunaendelea kukamilisha sasa maabara katika shule nyingine, ni lini italeta vifaa hivyo kwa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Obama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna upungufu wa Walimu wa masomo ya sayansi na hisabati na kama nilivyoongea kwenye jibu langu la msingi ni kwamba sasa hivi tunafanya mchakato wa kumalizia kuajiri Walimu zaidi ya 4,500 na tumeyaweka mahsusi kabisa kwamba maeneo haya, Wilaya yako ya Kongwa, kule Buhigwe na maeneo mengine, tutazingatia maeneo ambayo yana upungufu mkubwa zaidi.

Tunaomba tupate taarifa kwa sababu kuna mahali unakuta kweli shule nzima haina hata Mwalimu wa hesabu, au baiolojia, kemia au fizikia, tutaweka vipaumbele maeneo hayo ambayo yana changamoto kubwa. Hii ni awamu ya kwanza ya ajira, awamu ya pili ikipatikana pia tutakuwa tunapeleka Walimu kadri uwezo utakavyokuwa unapatikana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza habari ya kumalizia maboma ya maabara. Nimesema kwenye majibu yangu ya msingi ni kwamba tayari hapa tulipo tunasambaza vifaa, tenda imeshatangazwa, kazi inafanyika. Inawezekana wakati tunaomba taarifa kwenye halmashauri mbalimbali labda watu wetu kule hawakuleta taarifa hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Obama kama ana wasiwasi kwa hili la kupeleka vifaa vya maabara kwenye eneo lake, basi naomba tuwasiliane ili tuweze kuzingatia maombi yake. Ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Naishukuru Serikali kwa majibu yao mazuri kabisa, sina wasiwasi na majibu kwani mmejibu vizuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa inavyoonekana future transport logistic kati ya Tanzania na Burundi itapitia Manyovu. Ameonesha kabisa kwamba Dar- es-Salaam – Kabanga ni kilometa 1330 na Dar-es-Salaam – Tabora – Manyovu ni 1273, kwa hiyo, katika mpango wetu wa Blueprint na Easy of Doing Business inaonesha kwamba siku za mbele wafanyabiashara watapitia Manyovu kupitia Tabora. Kwa kuwa iko hivyo, ni maandalizi gani sasa mmeyafanya kwa ajili ya kupokea biashara hiyo? Najua Serikali mtaendelea kujitahidi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, amesema kuna changamoto ya barabara kwa ajili ya kurahisisha biashara kwenda Burundi. Je, Wizara ya Ujenzi ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hivi vipande vya barabara vinaisha haraka?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kitu cha kwanza Mheshimiwa Obama anawatetea kweli ndugu zetu kule, napenda tu nimjulishe kwamba katika utaratibu wa ujenzi wa barabara ambayo inatoka Burundi - Manyovu – Kasulu - Nyakanazi, moja ya vipengele vya barabara ile baadhi ya huduma ambazo zitajengwa kwa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika ni pamoja na kujenga Kituo cha Pamoja cha Forodha pale Manyovu ambacho kwa hakika itakuwa ni mkombozi wa kuharakisha biashara kati ya Tanzania na Burundi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa upande wa Wizara ya Ujenzi pamoja na sisi kama Wizara ya Fedha karibu tumekamilisha jitihada za kupata fedha za kukamilisha vile vipande ambavyo vimebaki vya barabara ambayo inatoka Manyoni - Tabora - Kigoma. Fedha zimekwishapatikana, tunakamilisha taratibu za ujenzi kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi. Ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwamba huu mradi wa Kilelema na Migongo, mmetupatia fedha na kama ulivyosema mwenyewe ni sawa kabisa tunatekeleza mradi ule pamoja na mradi wa kusambaza maji katika Wilaya ya Buhigwe pale mjini. Maswali yangu ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vijiji vya Rusaba, Nyaruboza na Kibwigwa kama ulivyosema nilitaka tu kupata commitment yako kwamba mwaka 2021 utahakikisha kwamba vipo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunao mradi wa vijiji 26 wa kati ya Serikali ya Ubelgiji na Tanzania ambao unatekeleza miradi ya vijiji 26 Mkoa wa Kigoma na katika Kata zangu za Mnanila, Mkatanga na Mwayaya, mradi ule bado haujaanza pamoja na kwamba tumesaini mkataba wa BTC. Je, ni lini sasa mradi huo utaweza kufanikiwa ili na maji pale yaweze kutoka kwenye vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Albert Obama kwa kazi kubwa anayoifanya pale Buhigwe lakini kikubwa ambacho nataka nimhakikishie kuhusu eneo lake lile la Rusaba, sisi ni Wizara ya maji, nasisitiza tena na si Wizara ya ukame!

Nataka nimhakikishie akapofika mwaka 2020 wananchi wake wa Rusaba tutahakikisha wanapata huduma hii ya maji. Maji ni uhai na sisi kama Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa Wana Buhigwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la mradi huu wa Ubelgiji, tupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa taratibu. Nataka nimhakikishie taratibu zitakavyokuwa zimekamilika mradi ule tutauanza na wannachi wake wataweza kupata huduma ya maji.