Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Albert Ntabaliba Obama (20 total)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ALBERT O. NTABALIBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha Hoja ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, kama tulivyoiwasilisha leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe Mwenyekiti kwa kuongoza vizuri, lakini naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri waliochangia hoja hii, pia nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuchangia tena hoja hii. Tumepata wachangiaji 16 kwenye hoja hii na wengine 14 wamechangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata hoja za wachangiaji tofauti na mchangiaji wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Joseph Haule ameongelea mikataba ya Chuo Kikuu na Mlimani City, ameongelea mikataba ya TANESCO, ameongelea mikopo inayodaiwa na TANESCO na PSPF. Kamati inakubaliana na yeye kwamba hii mikataba kama tulivyosema kwenye ripoti yetu iweze kuangaliwa upya kwa sababu tunaamini kwamba hii asilimia kumi wanayoipokea katika miaka 50 ni ndogo sana, huenda thamani halisi baadae ikawa siyo nzuri. Kwa hiyo, tunaamini kwamba mapendekezo ya Kamati yaweze kuzingatiwa na yaweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba ya TANESCO kama Mheshimiwa Waziri alivyoongea na Kamati yetu imeongea vizuri, ni mategemeo yangu kwanza kipengele cha mikataba kama AG alivyosema nayo Kamati inashauri iweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ambayo Serikali inadaiwa na PSPF tunakushukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeongea, ni concern ya Kamati kwamba speed inayotumiwa kuhakiki na kulipa madeni ni ndogo sana. Kwa hiyo, Kamati inaona kwamba Serikali bado hapa haijafanya juhudi kubwa, tunaomba kwamba Serikali iweze kuendelea na juhudi kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wameongelea vile vile Ofisi ya TR kwamba kwa nini Ofisi ya TR iwe ni msimamizi wa mifuko. Waheshimiwa Wabunge ndiyo tuliotunga sheria hii mwaka 2010, Cap. 370 tulitunga ambayo mifuko inawekeza fedha nyingi na TR ndiye msimamizi wa Serikali. Kwa hiyo, ni wajibu wa TR kuhakikisha kwamba shughuli zote za Serikali na mashirika yake inaziangalia, na ni hakika kwamba Msajili ni kazi yake kuziangalia hizi sheria. Ukiangalia sheria inayounda Mifuko ya Hifadhi inaangaliwa vile vile na Benki Kuu na SSRA, lakini ni kazi ya TR tena kufanya uhakiki wa mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wengi wameongelea kuhusu bodi na wengine wameenda mbele zaidi kuongelea mambo ya TANAPA. Kamati tumesema bayana, hatujaficha, Serikali ni wavivu katika kuteua bodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Mamlaka ya Uteuzi nafikiri haipelekewi mapendekezo mapema kiasi kwamba, mfano kwenye mashirika 41 tuliyokutana nayo; mashirika 13 yalikuwa hayana bodi na yapo mashirika mengine tuliamua kuyarudisha kwa sababu Mwenyekiti wa Bodi hakuwepo. Kwa hiyo, ni vizuri mamlaka zinazohusika ziweze kuteua bodi. Hata hivyo, tunaipongeza Serikali mmeanza kuchukua hatua, tunaomba hiyo hatua iendelee ili muweze kukamilisha mashirika yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la National Housing, Mheshimiwa Omary Mgumba amesema haiwezekani National Housing ijenge, isimamie yenyewe, ikague ubora na kila kitu. Kwa hiyo, Wajumbe wana wasiwasi kwamba lazima kuwe na chombo kingine cha kuihakiki National Housing ili kuangalia accountability kwa sababu ni shirika hilo hilo linaloshughulikia mambo yote. Kamati imependekeza na iko kwenye mapendekezo ili Serikali iweze kuyaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata mchango mwingine unaohusiana na TBA kwamba sasa hivi kuna mwamko TBA iweze kujenga majengo, je, nani anaikagua hii kampuni na haitoi gawio kwa Serikali. Kwa hiyo, nalo hilo Wajumbe wamelichangia nalo tunahisi kwamba Serikali iweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo walioonesha masikitiko makubwa. Waheshimiwa Wabunge, Serikali hii ina mashirika na taasisi 264 na mtaji wa mashirika haya yote ya Tanzania ukiyajumlisha ni trilioni 23 lakini faida kwa mwaka kwa mashirika yote ya Tanzania yenye mtaji wa trilioni 23 yanaleta faida ya bilioni 422 ambayo ni asilimia 1.83 ambayo Kamati hairidhiki. Huwezi kuwa na mtaji wa trilioni 23 ukaleta faida kidogo namna hii. Hata kama ingeweza kuleta ten percent ingeweza kuiingiza Serikali trilioni 2.3 ikaweza ku-boost mapato ya Serikali. Kwa hiyo, TR anayo kazi kubwa kuhakikisha kwamba mchango wa mashirika haya lazima uongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wameongelea tena mashirika mengine kama STAMICO ambayo kwa kweli na sisi ni kampuni ambayo tuliihoji inaenda kwa hasara, inatumia ruzuku ya Serikali na huku ni msimamizi wa madini. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kama Wizara iweze kuipa nguvu hili Shirika la STAMICO na kuipa mitaji ili iweze kujiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lulida ameongelea jambo moja pale la kusema pale kuna mwekezaji kwenye national housing pale Kawe ni kweli. Kamati tumetembelea pale ule uwekezaji wote uliopo Kawe wa National Housing yuko mwekezaji mmoja mmbia ambaye viwanja vile kweli alinunua kwa milioni sita mwaka 1995 nafikiri. Lakini yeye ameingia ubia na National Housing kwa fifty fifty, miradi ile ni mikubwa lakini yeye ametumia bilioni sita kuingia kwenye mikataba mikubwa. Haya ni mambo ambayo yanaendelea kwenye uwekezaji wa mitaji ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru tena Wizara kwa kuteua Bodi ya TANAPA, kama Mheshimiwa Nsanzugwanko alivyosema kuna kesi iliamuliwa pale ambayo ilitakiwa shilingi bilioni 10 ziwe zimeletwa Serikalini kwa ajili ya kutoza, lakini nashukuru kwamba imechelewa kwa miaka mitatu hatujui Kamati tunajiuliza kesi inaamuliwa kwamba shilingi bilioni 10 ziingie Serikalini lakini bodi haiteuliwi ili iweze ku-effect hizo fedha zije, zinakaa miaka mitatu, Kamati inajiuliza kulikuwa na nini? Kwa hiyo, tunashukuru sana kwamba Mheshimiwa Waziri amesema sasa bodi imeteuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni; Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyaongelea vizuri lakini yapo madeni ya majeshi, maji kwenye taasisi za Serikali, hayo nayo ni muhimu sana muweze kuyafanyia malipo ili kunasua hizi taasisi za umma ziweze kujiendesha. Kwa kweli ukikutana nao wanasikitika, tungeomba muweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mwongozo wa TR ambao unasema mashirika ya umma yaweze kutumia asilimia kumi tu ya mapato yote, lakini yapo mashirika katika uchambuzi wetu tumekuta yanatumia zaidi ya asilimia kumi. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu kwenye mapendekezo kwamba Serikali itaweza kuyachukua.
Lipo pendekezo moja la Mheshimiwa Elibariki Kingu ambaye ameenda kinyume, anasema haafiki kabisa kwamba TR aweze kusimamia mifuko ya jamii kwa sababu TR anayo mashirika mengi. Tukumbuke Mheshimiwa Kingu ni kwamba tulishatunga sheria, mpaka sheria itakapobadilishwa. Ni haki ya TR kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nayo anaiangalia kwa sababu inaweka uwekezaji na Serikali ndiyo inadhamini hata kama watakuwa wameshindwa kulipa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha sasa naomba Bunge lako likubali maazimio na mapendekezo ya Kamati kama yalivyopendekezwa kwenye kitabu chetu. Baada ya kusema hayo nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ALBERT O. NTABALIBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA MITAJI YA UMMA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha kufika muda huu lakini kipekee nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi asubuhi hii kuweza kuwasilisha taarifa ya Kamati. Kipekee niwashukuru Wabunge wote kwanza kwa kusikiliza taarifa yenyewe na pili kwa kuweza kuisoma na kuijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi niende kuwashukuru waliochangia taarifa hii. Taarifa hii imechangiwa na watu wengi, nitaenda mmoja baada ya mwingine. Naomba nianze kipekee kuwashukuru Serikali kwa response yao ya hotuba yetu na michango ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, naomba nianze na hoja za Serikali na nianze na hoja aliyowasilisha Waziri wa Fedha kwenye majibu yake, pale Kamati tulipoomba kwamba Gavana asiwe Mwenyekiti wa Bodi na tukawa tumependekeza kwamba kwa sababu ya good governance zitenganishwe hizi pillar mbili lakini kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameonesha kwamba ni vizuri iendelee kuwa hivyo kama ilivyo na ame-cite kwamba 90% ya survey waliyoifanya Gavana ndiyo Mwenyekiti wa Bodi.

Kwa mtazamo wa Kamati tuliona kwamba huenda vingetenganishwa vingeweza kuleta ufanisi lakini naomba nikubaliane na majibu ya Serikali kwamba kama wataendelea kuifikiria na kuiona hivyo bado inaleta ufanisi, basi tunaiomba tuiache hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kabisa nimpongeze Profesa Luoga, tulipoita Benki Kuu kuja kwenye Kamati yetu hakuweza kufika lakini kwa kweli alionesha concern kwa nini hakufika na akawa amesikitika kwa nini hakufika, aliwatuma Magavana wake. Tunaomba tumpongeze kwa sababau alionesha concern kubwa ya kuheshimu Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili ambalo Mheshimiwa Waziri amesema ni huduma za mashirika kwamba mashirika mengine ni kwa ajili ya ruzuku. Kama Kamati tunakubaliana na majibu ya Serikali issue yetu ni kwamba kama mmesema kwamba mtaipa ruzuku na yanasaidia, kwa nini hampeleki fedha? Ndiyo hoja yetu. Tunajua mashirika 175 kati ya 269 yanapewa ruzuku lakini kwa nini Mheshimiwa Waziri fedha za kuendesha mashirika haya haziendi kwa wakati? Hiyo ndiyo hoja yetu, kwa hiyo, tunaomba mwendelee kuifanyia kazi ili muweze kui-solve hii changamoto ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji mwingine alikuwa ni Mheshimiwa Sixtus Mapunda aliyejaribu kuelezea vigezo na kwa nini ATCL. Sisi tumesema kwenye ripoti yetu ATCL ni kampuni ambayo ina umuhimu mkubwa lakini katika miaka mitatu imeendelea kupata hasara. Hata kama itakuwa na faida nyingine kwa sekta nyingine lakini kama shirika na sisi kama Kamati ya Uwekezaji ni lazima tui-task management na bodi ihakikishe kwamba inaleta faida ina- turn out hizi loss ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakubaliana na mawazo ya mchangiaji kwamba inazo faida nyingine kwa sekta nyingine, hizo hatukatai tunajua kwamba intention ya Rais ya kununua ndege na ataendelea kununua ndege na sisi tunaunga mkono katika ku-boost utalii lakini tunapokuja kwenye shirika lenyewe lile nalo tunalitaka liweze kuwa na faida. Tunapoangalia mizania yake tunataka na lenyewe shirika liwe na faida pamoja na kwamba lina other profits kwenye sekta nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ameongelea mitaji, nipongeze nia nzuri ya Serikali, 2016 Serikali hii ilikuwa imewekeza trilioni 23 ambapo mwaka jana tulipata faida ya bilioni 422.9 lakini kwa 2017 mtaji umeweza kuongezeka mpaka kuwa trilioni 47.8 ambapo tumeweza ku-realize gawio la bilioni 845. Kwa hiyo, hii ni achievement kubwa, lakini tunaposema generally faida bado ni 1.9% ambayo ni ndogo. Kwa hiyo, bado ni wito wetu kuhakikisha kwamba wanaoendesha mashirika wana-task ya kuhakikisha faida ya mashirika hayo inaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine aliyechangia ni Mheshimiwa Mary Deo Muro, yeye alikuwa anaongelea Bodi ya mashirika hasa aliongelea RAHCO na Elimu Kibaha. Kwenye ripoti yetu tumesema vizuri na ukiangalia kwenye bodi bado tunai-task Serikali, mfano, MSD ina miaka karibu miwili haina Bodi na sasa hivi nia njema ya Mheshimiwa Magufuli, Rais wetu ya kupeleka fedha ya kununulia dawa, nia njema aliyonayo Waziri wa Afya na Serikali nzima inapeleka fedha nyingi lakini hamna bodi iliyopo pale. Ni wajibu wetu kuwakumbusha kwamba bodi ya MSD iweze kuteuliwa. Wanashindwa kufanya investment kwa sababu decision zingine za investment zinahitaji endorsement ya bodi. Sasa bodi hamna tunashangaa kwa nini uteuzi haufanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Lolesia Bukwimba na Mheshimiwa Juma Hija wameongelea mambo ya madeni makubwa ambayo Serikali inadaiwa. Kwa hiyo, tunawakumbusha, kwenye ripoti yetu tuko so clear kwamba Serikali iweze kuanza kuchukua hatua za kuyalipa madeni hayo kwa mpangilio ambao inaona inaweza kuanza kuyalipa. Madeni yamekuwa makubwa, yanafanya makampuni, mashirika na taasisi zetu zishindwe kujiendesha na ku-meet target zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mashirika ya umma ya Serikali ambayo ni wakandarasi lakini Sheria ya Manunuzi iliyopo inawaona kama ni mashirika au taasisi wanaonunua lakini kumbe ni wakandarasi. Tunayo TBA, DDCA, JKT, haya yote ni makampuni makandarasi, lakini kulingana na Sheria ya Manunuzi wanaonekana kama ni wanunuzi. Kwa hiyo, tunaomba kupitia Ofisi ya TR iweze kuandaa mapendekezo mazuri ambayo yataendana na mashirika haya kwani yanakosa biashara nyingi kwa sababu sheria inawabana na shughuli zinakuwa za muda mfupi. Kwa hiyo, Kamati bado inasisitiza hilo liweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mashirika au kampuni ambazo hazijamtambua Msajili wa Hazina. Hapa ni msisitizo kwamba kupitia Ofisi ya TR basi aweze kuzikumbusha kwa sababu sheria zilizoanzisha mashirika haya nyingine ni za muda mrefu na TR ameanza kupewa uwezo muda siyo mrefu. Kwa hiyo, tungependa zile sheria ziweze kuwa reviewed iweze kuwekwa addendum ya sheria nyingine ili iweze kuzitambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wito wetu kwa Wizara ya Fedha kwani haitendi haki kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina. Kwanza hawana manpower, hawana watu wengi wenye weledi wa kuweza kuchambua mambo yote yaliyopo kwenye uwekezaji wa mitaji ya umma. Tuisihi Wizara ya Fedha iweze ku-empower Ofisi hii na iweze kuipa bajeti ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Ofisi ya TR ilitakiwa iwe imetupa ripoti ya mwaka na hiyo ripoti ingeweza kuletwa kwa Waziri wa Fedha ambaye angeileta Bungeni na baadaye Kamati kupewa, lakini sasa ni miaka miwili na nusu hatujapokea ripoti hii. Sasa tunaiomba Wizara ya Fedha iweze kuijali na kuipa kipaumbele Ofisi ya TR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine makubwa yaliyoongelewa ni madeni, mambo ya ndege, Bodi za Wakurugenzi tumeiongelea, iko kwenye ripoti yetu, Sheria ya Manunuzi tumeisema iko so clear na iko kwenye ripoti yetu. Kwa hiyo, nawashukuru hawa walioboresha ripoti yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rhoda Kunchela amezungumzia Serikali kutolipa madeni kwa wakati, ni kweli, yako mashirika madeni ya DAWASCO, DUWASA na umeme. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo yanaweza yakazungumzwa ndani ya Serikali na tukaondokana na hizi embarrassment. Wananchi wanakatiwa huduma za maji kwenye visima, wanakuta kuna mgogoro Serikali haijalipa umeme, ni mambo ambayo mnaweza mkayaongelea ndani ya Serikali ili wananchi wasiweze kuathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Janet Mbene ameongelea mashirika yaendeshwe kibiashara, ni kweli na sisi tunasisitiza hilo na ndiyo maana ya kuanzisha Kamati hii ili iweze kuangalia mujarabu wa biashara kwenye mashirika haya. Kuhusu vigezo vya appointment, kuona mtu mwenye uwezo wa kuongoza shirika, nafikiri hilo nalo liendelee kuzingatiwa kama ulivyolitolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengine ni ya jumla ambayo kwa kweli tunashukuru kwamba yameweza kuboreshwa, mengine wote walikuwa wanarudia karibu maeneo yaleyale. Kitu muhimu tunachosisitiza kama Mitaji ya Umma tunaomba mapendekezo tuliyoyatoa kwenye ripoti yetu Bunge iyaazimie, iyachukue na yawe ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa niliombe Bunge lako Tukufu liweze kukubali mapendekezo yetu na hoja zetu ambazo zimetolewa ndani ya ripoti yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa asilimia mia moja. Naomba kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Waziri unatambua kwamba Wizara yako iliahidi kushughulikia wizi uliofanywa na Karinzi Coffee Organic kwa kununua kahawa kwa wakulima 435 wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Manyovu 2014/2015 ambapo Serikali iliwaahidi kulipa malipo hayo ya dola za Kimarekani 75,000. Karinzi Coffee Organic inasema Kiwanda cha Kubangua Kahawa hawajawalipa. Tunakuomba kufuatilia suala hili kwani ni kero inayokatisha tamaa wakulima wa kahawa, tunakualika ufike Manyovu ukutane na wakulima wa kahawa kwani wewe utakuwa mkombozi wao.
Naomba ufuatilie juu ya kero ya pembejeo, muda wa pembejeo hizo kulingana na maeneo. Mkoa wa Kigoma unapokea mbolea nje ya muda ambapo tija yake haipatikani. Pili, wajibisha na tumbua majipu ya wezi wa pembejeo, Mawakala na Wakuu wa Wilaya.
Mwisho, nawatakia mafanikio mema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze hotuba nzuri ya Waziri wa Elimu. Kwa ufupi naomba nichangie yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa Walimu. Tunaomba Wizara isimamie vyuo vya Walimu kwa karibu kwani vyuo vingi ubora umepungua sana:-
(i) Maabara za sayansi hakuna katika baadhi ya vyuo, kufanya Walimu kukosa umahiri wa ufundishaji; na
(ii) Walimu wa Hesabu. Ubora wa Walimu wa hesabu umepungua na kufanya output kuwa hafifu. Nashauri programu maalum ya hamasa kwa Walimu wa hesabu Kitaifa na kutoa zawadi maalum kwa wakufunzi wa hesabu. Hesabu ni tatizo kubwa kwa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa VETA. Tunaomba kuleta maombi ya kujengewa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Buhigwe kwani ni Sera ya Wizara yako ya kujenga Chuo cha VETA kila Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa Nyumba za Walimu/Madarasa. Kwa kuwa, bajeti ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI ni ndogo, kwa nini Wizara ya Elimu isishirikiane na Social Security Fund (Mifuko) ili iwasaidie kujenga na Serikali kuwalipa yearly?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TCU na Bodi ya Mikopo. Nashauri Wizara isiishie tu kufukuza, naomba uchunguzi uende mbele zaidi kwani inaonekana rushwa ipo kubwa kwenye sekta hizi mbili; maamuzi ya kubadili Secretaries ni muhimu sana, nao wanaweza kuwa ni chanzo cha rushwa. Bodi ya Mikopo wapewe malengo makubwa ya kukusanya mapato kuliko kuachwa kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri zaidi:-
(1) Fanya ziara za kushtukiza katika taasisi zako.
(2) Komesha siasa mashuleni.
(3) Toa zawadi kwa vyuo bora kwa vigezo vya Wizara.
(4) Toa zawadi kwa wanaofaulu hesabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza Mawaziri wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Napenda kusisitiza kwamba kwa kazi nzuri mnayoifanya ingawa bajeti yako ni ndogo sana kulingana na mahitaji ya nchi hii, ninayo machache ya kuchangia:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati ni ukombozi wa wananchi wengi ndani ya nchi hii. Tunaomba Serikali ilifanyie kazi kwani sasa ni hitaji kwa wananchi na kusafirisha mizigo mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mnamila – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, tunaomba ipewe umuhimu wa kipekee kwani ni kero kubwa sana. Kigoma nayo ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais aliahidi kutupatia fedha za kupasua barabara mpya za Nyakimue hadi Muhinda, Rusaba hadi Nyamboze, Kibande hadi Nyamugali, Kilelema hadi Mugera, Munzeze hadi Kwitanga, Kajana hadi Kasumo, Mwayaya hadi Buhigwe. Tunaomba fedha za kupunguza urefu kwenda makao makuu ya Wilaya, kwani ni kero kubwa sana, bajeti ya Wilaya hairuhusu kupasua barabara mpya. Tunaomba mtusaidie na ahadi ya Rais iweze kutekelezwa. Tunaomba special fund na wataalam waje wapitie barabara hizi na cost analysis iweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunawatakia mafanikio mema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa Wizara hii. Napenda kuchangia yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Buhigwe Makao Makuu tunashukuru umeme umefika na baadhi ya vijiji umeme umefika. Tatizo ni kwamba kati ya vijiji 48 tumefikisha umeme vijiji tisa tu. Tunaomba kipaumbele kwani Mkoa wa Kigoma tumeachwa sana na mikoa na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA III, tunaomba vijiji vyangu vya Wilaya ya Buhigwe vipate kuwekewa umeme kwani imeanza kuwa kero na siasa kupamba moto kwamba CCM hawawapendi. Kata ambazo hazijapata umeme Buhigwe ni Muhinda, Janda, Munzeze, Mkatanga, Kibwigwa, Kibande, Munyegera, Kilelema, Kajana, Mugera, Bukuba, Kinazi na Rusaba
Mheshimiwa Naibu Spika, jamani tuoneeni huruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawakumbusha kuwa vijiji vyetu ni vikubwa sana na wananchi ni wengi, tunaomba transformer za kutosha kwani vijiji vilivyopata vitongoji, wengine wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Wizara kwa uamuzi wa kuzalisha umeme pale Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawatakia ufanisi bora wa kazi zenu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri ya bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisoma bajeti hii, naiona katika mambo yafuatayo:-
Kwanza, bajeti hii inajaribu kutuambia kwamba lazima watu wawajibike. Watu walioomba fedha kwenye Taasisi, Wizara, lazima wawajibike! Hata hivyo, nikiiangalia inajaribu kutuonesha kwamba nidhamu ya matumizi kwa walichopangiwa ni kitu muhimu sana. Pia inanionesha kwamba fedha zilizopangwa zinabadili mwelekeo kwa yale tuliyoyazoea na hatimaye kuwaza mambo mapya. Jambo la mwisho naiona kama inaenda kulenga maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nimesoma kitabu chake cha Hali ya Uchumi ukurasa wa 10 pale, kuna kitu amekisema kizuri sana pale. Hali ya umaskini; ametaja mikoa yeye mwenyewe kwamba kuna mikoa ambayo kipato chake ni kidogo. Mikoa mitano yenye umaskini mkubwa wa kipato ni Kigoma, asilimia 48.9, Geita asilimia 43.7, Kagera asilimia 39.3, Singida asilimia 38.2, Mwanza asilimia 35.3. Sasa nataka nimuulize; je, anafurahia kuitaja tu humu au ana mikakati gani aliyoipangia mikoa hii? Hii Mikoa ambayo anafurahia kuiandika kwenye vitabu vyake, kwenye bajeti ili aweze kuikomboa amepanga kitu gani? Hiyo ndiyo, ningependa atuambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu naangalia Mkoa wangu wa Kigoma, Mheshimiwa Waziri ameutaja kwamba ni maskini. Jimbo langu lina mgogoro na Serikali yake, vibanda 120 katika Kijiji cha Mnanila walijenga kwa kupewa ramani na Halmashauri yao, lakini TANROADS wakaja wakavunja na mpaka sasa wanawadai, kila kibanda milioni nane, jumla yake ni shilingi milioni 960, wamewafanya maskini, hawataki kuwalipa, lakini kuwaandika kwenye vitabu kwamba ni maskini wanapenda! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wakulima 435, Waziri wa Kilimo yupo hapa Mwigulu Nchemba nimemwona, wamelima kahawa yao wameuza, wamepeleka kwenye vyama vyao vya ushirika ambavyo wamewapa leseni mpaka sasa wakulima hao tangu msimu uliopita fedha zao hawajalipwa. Bado anapenda awaandike kwamba hao watu wa Obama au watu wa Kigoma ni maskini na watu wanalima hawawapi hela zao! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kigoma katika mipango ya REA, Kigoma ni kati ya mikoa ambayo mpaka sasa hivi performance yake ni ndogo sana, ni Serikali yake hiyo anayoandika kitabu kwamba Kigoma wako nyuma na huku hawataki kuwapelekea fedha. Hivyo hivyo ukienda kwenye data za maji, ukienda kwenye pembejeo, Mkoa wa Kigoma tunapata pembejeo kidogo na zinakuja zimepitwa na wakati, lakini wanapenda watuandike kwamba sisi ni maskini! Kwa hiyo, hayo mambo mengine tunaomba mikakati ya kuokoa mikoa hii sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo hizi fedha milioni 50 ambazo mmesema, najua na nina uhakika, Mkoa wa Kigoma haujapangiwa kuanza na hizi fedha. Mnapeleka kule ambapo ni matajiri. Je, kama mnaionea hii mikoa kwa nini tusianze na hizi fedha zikaenda kwenye mikoa hiyo waliyoitaja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili sikupendezwa nalo ni kuhusu madhehebu ya dini kwamba wanapoagiza vitu vyao walipie kodi kwanza halafu ndiyo waje wa claim! Tujue kwamba nature ya madhehebu yetu mengine yana shule, mengine yana hospitali na hawana fedha, kwa hiyo, ningeomba hilo mliangalie ili tusije kuwa na matatizo na madhehebu yetu ya dini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye pay as you earn, katika kitabu page 60, Rais alikubali kwamba pay as you earn itakuwa digit kutoka 11 kwenda tisa lakini ukiangalia ile schedule watumishi wa Serikali wanaonufaika na hiyo asilimia tisa ni wachache sana kwa sababu inatakiwa uwe chini ya 170,000. Kwa hiyo, watumishi kule wanafurahia kwamba Serikali imepunguza lakini digit za pale juu ni kuanzia asilimia 20, asilimia 25 mpaka asilimia 30, kwa hiyo kile kilio cha watumishi wengi hata Walimu wanaokuwa wanafurahia hakitaweza kuwafaidisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tumeandika kwenye hotuba yetu ya Kamati ya Bajeti, nami nilikuwa sehemu ya Kamati, sina mengi ya kusema nilitaka nimkumbushe Waziri kuhusu hiyo mikoa maskini anayoisema ana mikakati nayo ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mpango wetu wa 2018/2019. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kupongeza Wizara, kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kutuletea mpango ili tuweze kuuboresha. Mpango huu umekuja kama mapendekezo kwa hiyo, ni kazi yetu kuuboresha. Badala ya kuuboresha wala tusiweke majembe, tuuboreshe mpango wetu ili uweze kwenda kutekelezwa 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niipongeze Serikali hii nzima kwa mafanikio ambayo wameyapata 2017/2018 ni juhudi ambazo zinatokana na michango yetu Wabunge lakini na usimamizi mkubwa wa Serikali. Kwa hiyo, niwapongeze kabisa sitaki kuingia kwa yale waliyoyaandika, yote ni mazuri tusonge mbele, twende mbele!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda tu nirudi jimboni kwangu, kwanza niishukuru Serikali. Wizara ya Uchukuzi kwa kutupandishia hadhi ya barabara zetu ambazo zilikuwa zinatuletea shida, barabara ya Buhigwe-Muyama- Katundu imepandishwa kuwa TANROADS, tunawashukuru sana. Pia tunawashukuru kwa kutupandishia barabara nyingine ya Mnanila mpaka Janda ambayo kwa kweli tunategemea fedha nyingi kupatikana ili tuweze kuitengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwamba tunajenga hospitali yetu ya wilaya. Tunachokiomba sasa kwenye Serikali ni kutuongezea fedha. Mmetupa shilingi milioni 500, tumeanza na ujenzi, Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa wako wanajenga pale lakini sasa ile milioni 500 ni kidogo. Tunaomba mtuongezee angalau bilioni moja na nusu mkupuo ili twende na ujenzi wa hospitali yetu kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza kwamba vituo vyetu vya afya vimeendelea kuboreshwa. Tuwashukuru World Vision kwa kuendelea kutuchangia sana kwenye kituo chetu kile cha Muyama lakini tuishukuru Serikali nao wametupatia milioni 500 kwa ajili ya kituo chetu cha Janda. Tunaomba kwa kweli mwendelee kutu-support ili tuweze kuendelea na ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la ujenzi wa Halmashauri yetu ya Wilaya, ofisi zetu za watendaji tumewapata hawa TBA, tumeshawalipa karibu milioni 400 lakini speed yao ya kutengeneza ni ndogo sana. Kwa hiyo, tunaomba kwa sababu tunapowalipa sisi kama Halmashauri fedha zinaenda Benki Kuu. Zinapokwenda Benki Kuu nafikiri wana tatizo la kurudishiwa fedha ili shirika liweze kuendelea na mradi. Kwa hiyo, tunawaomba kwa kweli muweze ku- release fedha ili waweze kuendelea na mradi na tunaomba mwendelee kutu-support. Tumewalipa pesa zote karibu bilioni moja na milioni 200 tumewalipa cash lakini ujenzi unasuasua. Tunaomba Wizara ya Fedha muweze kuruhusu waweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya maji. Mheshimiwa Waziri kwa bahati nzuri wewe unatokea jimbo langu, mimi ndiye Mbunge wako wa Jimbo. Kwa hiyo, ningetegemea kwamba miradi iliyoko pale na fedha ambazo mnatupa ni kidogo sana tunaomba fedha ziweze kuongezwa kwenye miradi yetu ya maji katika vijiji vyetu mbalimbali tunalo tatizo la maji sitaki kwenda mbali kwa sababu mengine tutayaongea kwa sababu ni mpango; mengine tutayaleta na mengine tutayaweka kwenye bajeti zetu za halmashauri, lakini generally tuna matatizo makubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma sasa hivi mnaposikia kwamba, Mpango umeandika kwamba kuleta umeme vijijini. Sisi Mkoa wa Kigoma hatujazindua mpango wa REA III na hatujazindua walitupa barua ya kuhudhuria uzinduzi lakini baadaye ukaahirishwa lakini kwa taarifa tulizonazo ni kwamba, kuna mgogoro uliopo kati ya CCRB na wakandarasi. Tunaomba Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Fedha, hebu ingilieni mgogoro huu, mkoa mzima unaadhibiwa na mradi wa vijiji haufanyiki, hatuna umeme!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Rais akisema, Wakuu wa Mikoa waangalie ujenzi wa viwanda sasa mkoa mzima hamna umeme unaoenda pale unategemea yeye hapo afanye namna gani? Kwa hiyo, tunamwomba kabisa Mheshimiwa Waziri na ni kilio cha mkoa. Mkoa wa Kigoma ikifikia maendeleo tunataka kuendelea kuna watu wanatokea ku-sabotage maendeleo yetu. Sasa ifike mwisho na Mheshimiwa Waziri yuko hapo na wao ndio wanakaa kwenye Baraza la Mawaziri, hebu ashughulikie hilo, tuna uchungu nalo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tumeanzisha TARURA, ni jambo jema, mimi napongeza kwa sababu ubora wa barabara zetu utakuwa mzuri. Tatizo langu, kuna Sheria ya TARURA ambayo hairuhusu kupasua barabara mpya. Sasa ningeomba hilo nalo waliangalie. Kwenye maeneo yetu tuna barabara ambazo tunatakiwa kupasua ni mpya kwa sababu wilaya zenyewe ni mpya ili kuleta mawasiliano mazuri, lakini Sheria inawabana kwamba hawawezi kufanya namna hiyo. Kwa hiyo, tunaomba Sheria nayo ya TARURA ya kupasua barabara mpya iweze kuongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa elimu, kwenye mpango tunakokwenda sasa hivi watu wa kidato cha nne wanafaulu vizuri, kwa hiyo, watatakiwa kwenda kidato cha tano. Sioni kama Taifa kwenye mpango na kupitia kwa Waziri wa Elimu kama tuna bajeti ya kuweza sasa kujenga majengo ya kidato cha tano angalau kila kata kwa sababu sasa tumeshatoka kwenye sekondari kila kijiji sasa angalau kidato cha tano kila kata. Kwa hiyo tunategemea mpango huu uweze kuongeza bajeti ya ujenzi wa madarasa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti iliyopita hotel levy tuliitoa, tulisema kwamba, haitakuwepo, lakini sasa nimeona kwa Dar-es-Salaam na sehemu nyingine kuna waraka ambao unafuta ile waive tuliyoitoa ndani ya Bunge letu. Sasa tungependa Waziri atuambie hotel levy bado ipo au ameifuta? Maana upo waraka, watu wanatozwa hela, watu hatuelewi, tunaomba a seme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo wa viwanda nakubaliana nao na hakuna ambaye anaubishia, ila wito wangu ni kwamba, intelligence ya masoko na ubora wa mazao ambayo sasa yataanza kuzalishwa ni lazima uwe makini kwa sababu, tutakuja kuwa na bidhaa ambazo watu wataanza kulia hawana mahali pa kuuza. Kwa hiyo, ni vizuri sana sasa watu wa masoko waweze kuwa macho na kuanza kujua namna ya ku-market bidhaa zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya SIDO. SIDO tumeipa jukumu kubwa sana la kusimamia viwanda vidogo vidogo, lakini ubora wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya SIDO ni mdogo. Kwa hiyo, tungependa eneo hilo Waziri wa Viwanda aweze kulisimamia vizuri ili ubora wa bidhaa zetu uweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho sijaona kwenye mpango wa Mheshimiwa Mpango kwenye kilimo, msukumo wa zao la michikichi. Sioni akiliongelea kabisa na ni zao ambalo linawafaidisha watu wa Kigoma, watu wanaokula mawese pamoja na kahawa. Kwa hiyo, ni vizuri nayo iweze ku-reflect kwenye mpango huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa barabara za lami ambavyo tumeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Kwanza tunampongeza, tunamtia moyo, nia yake ya kuufungua Mkoa wa Kigoma tunaipongeza kwelikweli. Tunamshukuru alikuja kwenye ziara, tulimpokea vizuri, kwa hiyo, tunaomba msukume maendeleo na watu wa Kigoma waweze kubadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja hii tuweze kwenda na maendeleo zaidi. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba hii nzuri ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kipekee kabisa kwanza nimpongeze Waziri na timu yake ya Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wote kwenye sekta hizi, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, niipongeze Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inatekeleza, hii ya standard gauge, mambo ya ndege, upanuzi wa viwanda, viwanja vya ndege na kuboresha mawasiliano kwa ujumla mnafanyakazi nzuri. Kwa kuwa dakika tano ni chache basi naomba tu niipongeze Serikali kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, mimi ninatokea Buhigwe, mawasiliano kwenye vijiji vyangu viwili yanahitajika. Tumeshaleta maombi kwa Naibu Waziri na ndani ya ofisi ya mawasiliano, Kijiji cha Katundu na Kijiji cha Kajana mawasiliano ni hafifu na kule wamenituma muweze kupeleka mnara ili waweze kwenda vizuri.

La pili, niipongeze Wizara kwa kuipandisha hadhi barabara zangu miaka iliyopita, ya Buhigwe, Muyama, Mgera na Katundu, mmeanza kuitengeneza vizuri. Nimpongeze kwa dhati kabisa Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kigoma anafanyakazi nzuri sana. Miongoni mwa mameneja ambao wanatakiwa uwapandishe na uwape mshahara mkubwa ni meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, anafanyakazi nzuri sana, ni debe kwa sababu anafanyakazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe meneja wa TANROADS pale kwenye mto Mlangilizi pale kutokea Kijiji cha Migongo kwenda Mgera, tuna mto mkubwa ambao wameanza kuweka maandalizi ya kujenga lile daraja. Kwa hiyo naomba waweze kulimalizia kwasbabu bado ni kero kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna daraja lingine kwenye barabara hiyo, Mlela yeye anajua, ukitokea Buhigwe kwenda Muyama kuna daraja bovu sana pale tunalo; kwa sababu ile barabara imepanda hadhi; tungependa aweze kuimalizia. Vile vile barabara ile ya Mnanila - Mwayaya - Mbanga mpaka Janda ambayo ni ya TANROADS nayo tungeomba kwa safari hii iwekewe fedha ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha TANROADS kwa sababu Wilaya wana uwezo mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sijaona ahadi ya kilometa tano za lami kwenye kitabu chako, kwa sababu Mheshimiwa Rais alishaahidi kwamba atazitengeneza, sasa sioni kama iko kwako na kama kwenye kitabu chako hatuoona kilomita tano zinatengenezwa kwa namna gani, tungependa utupe ufafanuzi utakapokuwa una-wind up. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni ushauri. Shirika letu la TRC linafanya kazi nzuri na limeanza kwenda vizuri. Tunachokiomba wanapoahirisha watoe taarifa kwa wasafiri kwa sababu wanasumbuka sana, hawajui reporting yao na hamja-improve vizuri. Hata mnapofika Dodoma hamwendi Dar es Salaam basi muwataarifu, wanakaa waka- hang, wanatupigia simu, muwe mnawataarifu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho; ningeomba muweze kumalizia jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma, kwa sababu uwanja umeshakuwa mzuri basi muweze kumalizia jengo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengine, nawashukuru, endeleeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa hotuba nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu Buhigwe, Wilaya ya Buhigwe, tunao wanajeshi wanaolinda mipaka vizuri lakini hawana vitendea kazi kama magari na pikipiki. Ombi langu ni kupatiwa vitendea kazi na kwamba makazi hafifu viboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniform za wanamgambo tunaomba ziboreshwe kwani ni walinzi imara katika maeneo yetu, wengi hawana uniform na taratibu ya namna ya kuzipata hawaelewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ya Nishati katika mapato watenge fedha za ukarabati wa ukuta wa Mererani kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia Wizara hii vizuri. Nawapongeza pia kwa kumpandisha cheo Mkuu wangu wa Wilaya ya Buhigwe.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu, lakini pili niendelee kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na timu yake ndani ya Wizara na taasisi zao. Kipekee kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwamba wanafika sana kwenye Kamati yetu na kwa kweli kwa upande huo wanajitahidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako makosa ambayo sasa Wizara inataka kuanza kufanya. Kosa la kwanza ambalo Wizara inataka kufanya ni kuua Ofisi ya Mipango. Mheshimiwa Waziri wa Fedha kabla hajawa, alikuwa kwenye Tume ya Mipango, lakini sasa kwa kuwa ameingia yeye sasa, anatumia cheo hicho kuua Ofisi ya Mipango. Tungependa kuona kwamba Ofisi ya Mipango yenye Fungu Namba 66 inarejeshwa. Hatuwezi kukubali kuwa chini yako, chini ya Fungu Namba 50 kwa sababu mikakati mingi inakufa sasa. Kwa hiyo, hilo ni namba moja ambalo kwa kweli tungeomba lirejeshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili kwa uendelevu wa ukosefu wa mipango, hata mfano ukiangalia fedha tunazozipeleka kwenye Bodi ya Mikopo, ushauri wetu tungependa aidha, waanzishe mfuko wa elimu ya kusomesha vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwenye tangazo juzi kwamba vijana wetu wa diploma hawapati fedha za mikopo. Sasa haya ni mambo ambayo hayakubaliki, mtu anatangazaje na sisi tumeshajitoa kwenye fedha na vijana wanajua tayari watapata fedha? Sasa hii ni ukosefu wa planning unit ambapo kila mtu mwenye taasisi anaamua kusema mwenyewe. Kwa hiyo, tunaomba hilo nalo liweze kurudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Wizara ya Fedha kuna mahali wanaanza kukiuka kufuata sheria. Sheria tumezitunga wenyewe. Tuna sheria za mifuko ambapo mifuko mingine iko ring-fenced ambapo sasa mna- temper nazo zile fedha. Mfano iko Mifuko ya REA, Maji, TANROADS na Reli. Hiyo Mheshimiwa Waziri hamwendi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapenda kuona kwamba mnaenda vizuri zaidi, zile fedha ziheshimiwe, ziweze kwenda kama zilivyotarajiwa. Miradi mingi ambayo wakandarasi tumewa-commit mikataba, kazi hazianzi. Miezi tisa mtu ana mkataba lakini haanzi. Kwa hiyo, tunapenda hapo muweze ku-improve. Ipo mingine ambayo tumeiweka tu kimatamko; mfano, asilimia 15 ya refund za watu wa viwanda vya sukari mnashindwa kuwapa, wanadai mpaka shilingi bilioni 30 zinaenda mpaka shilingi bilioni 40. Sasa ni vizuri nazo muweze kuona.

Mheshimiwa Spika, tunazo fedha karibu shilingi bilion 600 kwenye kampuni za madini nazo hamjaweza kuwapa refund yao. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri aweze kujipanga namna ya kuwarudishia angalau kila mwezi.

Mheshimiwa Spika, tuna huu ugonjwa wa uhakiki. Naipongeza Wizara ya Fedha kuhakiki kulipa fedha ambazo zimetumia, lakini hebu wapeni uwezo hizi Wizara. Mlitoa mfano siku moja kwenye Kamati, tukasema Wizara ya Maji imeleta certificate za shilingi bilioni 109 lakini mmejiridhisha kwamba shilingi bilioni 17 tu ndizo zinatakiwa kulipwa.

Je, swali hapo kama Wizara ya Maji inaweza ikaleta vitu ambavyo karibu shilingi bilioni 92 ni fake; je, hiyo Wizara kwa nini hamjaivunja? Kwa hiyo, ni vizuri uhakiki uweze kuwa empowered kwenye Wizara zote ili hiki kipengele cha kujifichia cha uhakiki kiweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako madeni mengine ni halali. Yako madeni ya TANESCO na Maji, nayo mnahakiki. TANESCO wakileta bili ya umeme unahikiki nini? Je, zile Wizara nazo haziaminiki? Kwa hiyo, hapo napo muweze ku-improve vizuri ili muweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, fedha za kulipa wakandarasi, hili ni jambo lime-stuck uchumi. Wewe unataka makusanyo lakini ume-stuck uchumi. Wakandarasi hawapati hela, walio-supply hawapati hela, kila kitu kime-stuck. Sasa hayo mapato wewe unayapata wapi? Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli Wizara hii iweze ku-improve mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuimarisha Ofisi ya TR. Ofisi ya TR inasimamia karibu shilingi trilioni 47 ya investment. Investment kubwa iko pale, lakini hamuipi wataalam, hamuwapi empowerment, bajeti mnayowapa ni ndogo, sasa hata kutoa ripoti ya mwaka kwa Ofisi ya TR inakuwa ni shida. Wapeni fedha ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalo bomu lingine la mwisho. Hizi fedha za CDG mmesumbua Maafisa Mipango, Wabunge na Madiwani, fedha haziendi. Fedha za Maendeleo ya mwaka 2017/2018 hamjapeleka hata hela yoyote na huu ni mwezi wa sita unaisha. Kwa hiyo, ukisimama hapa utuambie, u-declare kwamba mwaka 2017/2018 kwenye Halmashauri zetu hakuna fedha ya maendeleo iliyoenda. Hili ni bomu kwetu sisi tuliochaguliwa. Tumeahidi tunaenda kuboresha zahanati hamna, shule, hamna; sasa tunaenda vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba hizo fedha hata kama zikitolewa, hata kama mkizitoa mwezi huu, basi tunaomba hizo fedha zitumike na mzidai zirudi baada ya mwaka. Mzipe grace period ya miezi sita ziendelee kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo ushauri wangu. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake yote, kwa kweli wanatupa ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti. Vilevile niendelee kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati na Makamu wake kwa kutuendesha vizuri ndani ya Kamati kwani tumeendelea kutoa maoni yetu kwenye sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa miradi inayotekelezwa na waliyoipanga kwenye bajeti hii sisi tumeibariki, tunaona kwamba haina matatizo, ni miradi muhimu. Miradi ya ndege, meli kwenye maziwa na bahari huko na miradi mingine ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze bajeti kwani lengo linaonesha kwamba mnataka kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha uzalishaji. Kwa hiyo, hilo nalo tunawapongeza na tunampongeza Rais kwa dhamira njema ya kuleta bajeti nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo machache tu kwenye ushauri ambayo napenda niyaseme. Kwanza ni namna ambavyo tumeanza kuua halmashauri zetu. Nilikuwa nafikiri mpaka muda huu tungekuwa tumeshaleta sheria ya kufuta local government kwa sababu sasa hivi meno yote yameondoka. Ukiangalia vyanzo vingi vimechukuliwa, miradi mingi ya maji imekwenda Wizara ya Maji, kilimo ndiyo hivyo na mambo mengine. Kwa hiyo, ifike hatua mlete sheria ya kuua huu ugatuaji ambao tuliupigania kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa na Waziri wa Fedha tumeongea naye juu ya namna ya kuanzisha akaunti ya pamoja ndani ya Wizara ya Fedha, hii ambayo inaonesha kwamba halmashauri zetu zitakufa. Kwa hiyo, nashauri kwamba tulete sheria tuweze kufuta halmashauri zetu mara moja ili tuweze kuendelea na centralization ambayo tunaitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu wakulima wa zabibu wa Mkoa wa Dodoma. Kodi zilizopo kwenye zabibu na mvinyo unaotengeneza pombe kali kama valour zinazotokana na zabibu iko juu, tunaomba iangaliwe. Wakulima wa zabibu Mkoa wa Dodoma wanalia kwelikweli, tunaomba kwa kweli iweze kuiangaliwa ili kwenye Finance Bill muweze kuleta amendment kama Serikali ili tuweze kuwaokoa. Walikuwa wamezoea kodi ya Sh.450 sasa mmepeleka karibu Sh.3,315. Kwa hiyo, tunaomba hilo eneo waweze kuliangalia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kuhusu ETS. Kwenye ETS Mheshimiwa Waziri tumekaa naye kwa muda mrefu, mmetufundisha kama Kamati ya Bajeti lakini kuna maeneo ambayo bado tunaona kwamba kwenye bidhaa, bia, sigara hamkuongeza lakini mmeiongezea kwenye gharama ya kuweka hizo stempu ambapo wafanyabiashara itabidi waingie gharama kubwa kuliko waliyokuwa wanalipa ili kuweza kuweka hizo stempu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hilo kwa kweli mliangalie, hizo gharama ziweze kuwa revised. Kwa kuwa production inaonekana itakuwa kubwa, kwa hiyo, tunashauri ile rate iweze kuwa ndogo. Tulifikiri teknolojia itaweza kuleta gharama ndogo zaidi kwani teknolojia haiwezi kuleta gharama kubwa. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli muendelee kuliangalia. Nimesikia, kuna mtu ameniambia anafikiri Mheshimiwa Rais amesema itakuwa miaka miwili lakini mmewapa miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2 Februari, Serikali yetu hii ili-publish regulations ambazo Kamati ya Bajeti ndiyo tumeziona leo. Hatujawahi kuona regulation ya ETS ambayo ndiyo hii hapa ilikuwa published lakini hatujawahi kuiongea kabisa. Nasi tumeisoma leo kidogo bado hatujamaliza na hatuwezi kusema mengi zaidi kwa sababu tutakutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tujiangalie sana na mifumo maana kwenye sheria humu inasema kama mtu amefungiwa huo mtambo, wakati wa kuzalisha ikitoa hitilafu anatakiwa asimamishe uzalishaji. Wanasema TRA itaweza ku-respond katika saa 48. Tukumbuke raw material za viwandani zingine zina expire baada ya saa mawili au matatu, kama yameshakorogwa yanatakiwa yazalishwe. Sasa ikisimama inakuaje, hizo gharama nani ata-incur? Mheshimiwa Waziri ana timu nzuri, naomba muendelee kuliangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kodi ya ardhi. Wako watu wenye mashamba makubwa ya katani, pamba, tumbaku, mmetoa gharama ya land free kutoka 400 mpaka 1,000, watu wana mashamba makubwa, kutengeneza shamba kwa muda mwaka inamchukua gharama nyingi na gharama nyingine tena ni ya kodi. Ardhi tulipewa na Mungu bure, ingekuwa sehemu ya mtaji wa mtu aendelee. Watu wana mashamba ya chai, land rent ni bei kubwa kuliko zao lililopandwa pale juu. Kwa kweli nashauri Waziri aweze kuliangalia hili na hata Waziri wa Ardhi aweze kuliangalia, msitumie ardhi kama ndiyo mtaji wa kila kitu na huku tulipewa na Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba wakandarasi walipwe. Kwa wale wakandarisi mliowahakiki muwalipe fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linatuudhi sisi watu wa Dar es Salam tunapokuwa tuko kule na katika Mikoa mingine ya Mwanza na kadhalika ni kufunga madukasaa 12.00 asubuhi mpaka saa 4.00 ya kila Jumamosi iendayo kwa Mungu katika mikoa yote ya Tanzania. Hebu tujaribu kufanya utafiti kuona hasara tunazozipata, kodi tunazozipoteza, unaamka asubuhi unataka kutumia fedha ya mtu anasafiri hakuna kibanda cha kutuma fedha. Watu tulizoea supu za asubuhi, hatuwezi kunywa supu Jumamosi. Mheshimiwa Waziri hebu mlipitie, sheria ya usafi tunaiheshimu, ingeweza ikatokea hata kwa mwezi mara moja, haiwezi kila Jumamosi ni matatizo huwezi kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja na Waziri ajue challenge kubwa ni kwamba tuna fedha kidogo lakini mipango ni mingi, lazima ifike mahali tu- compromise. Watu nao ni muhimu, kipato cha watu ni muhimu, kwa hiyo, tu-balance mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hizi mbili ambazo zimewasilisha hoja zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa naomba niwapongeze na hasa nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendesha Serikali yake vizuri, lakini wakisaidiana na Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nitoe pongezi kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Jafo na Naibu Mawaziri wake wawili, Kandege na Kakunda lakini na Mzee wetu Mheshimiwa Mkuchika, hongereni kwa kazi nzuri sana. Vile vile tuwape pongezi Makatibu Wakuu wao wanaowasaidia kwenye shughuli zao, Mungu awape wepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mkuu wangu wa Wilaya, Kanali Gaguti ambaye ameteuliwa jana kuwa Brigedia Jenerali; amefanya kazi nzuri sana kwenye Wilaya yetu, sasa Rais na Amiri Jeshi Mkuu amempandisha hadhi na ameambiwa aweze ku-report Makao Makuu ya Jeshi. Kwa hiyo Wilaya yetu itabaki bila kuwa na Mkuu wa Wilaya lakini tunamtakia mafanikio mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru TAMISEMI kwa kazi nzuri ambayo amefanya kwenye Jimbo la Buhigwe. Kazi nyingi zimefanyika katika muda mfupi na huku Wilaya yenyewe bado ni changa. Naomba niwapongeze kwamba tunajenga Ofisi ya Mkurugenzi na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inaendelea vizuri, kwa hiyo hiyo ni complementary yao. Ujenzi wa hospitali ya Wilaya unaendelea ambapo wametupatia milioni mia nne hamsini, wametupatia milioni mia tano na sasa wametupangia bilioni 1.5, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo ch afya milioni mia nne, nashukuru sana Mheshimiwa Jafo kwa kutupatia kituo hiki. Pia nimpongeze Mheshimiwa Kandege kwa kwenda kukikagua na kukiona na niwashukuru sana kinaendelea vizuri na wananchi wanafurahia, wanabaki wanasubiri tu watendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunacho Kituo kingine cha Afya cha Muyama ambacho tulisaidiana na World Vision ambacho sasa nacho kimeshaimarika na kinaendelea na upasuaji. Hiyo yote ni juhudi ya Serikali, tunaomba tuwapongeze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari za wagonjwa kwenye Jimbo la Buhigwe zinatosha kwa sababu kila kituo kilichopo kina gari jipya, kwa hiyo tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya maji inayoendelea ambayo ni juhudi zenu, lazima niziseme kama Mwana CCM. Tunayo miradi ya Nyamugari inaendelea, Nzeze, Kirungu, Mbanga, Myegela, Mgela, Kasumo, Nyanga hii yote ni miradi ya maji ambayo inaendelea kwenye Jimbo langu, kwa hiyo kwa kweli kwenye maji bado tuko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunao mradi mmoja wa Mnanila unaokwenda Mkatanga na Kata ya Mwayaya; huu ni kati ya ndugu zetu Wabelgiji ambapo kwa kweli wa mradi huu bado hauja-take off, tungeomba Ofisi ya RAS-Mkoa ambayo ndiyo link na hawa Wabelgiji ili tuweze kuendelea na mradi huu kwa sababu watu wa Manyovu na Mnanila wanauhitaji huu mradi. Vile vile tunaendelea, kwa kibali chenu, tunaendeleza kupeleka maji Kilelema na Migongo, Wakandarasi bado wanaendelea kutafutwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasambaza maji, tumepeleka andiko kwa Mheshimiwa Waziri na kupitia Waziri wa Maji, maji ya Mji wa Buhigwe ambao utaweza kusaidia Vijiji vya Songambele, Kavomo, Mlela, Buhigwe, Bwelanka na Kibande, hilo andika tunasubiri majibu tuweze kuona kwenye bajeti ya 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya ningependa kuomba yafuatayo:-

Tulikuwa na mkataba wa hospitali yetu ya Heri Mission ambayo iliingia mikataba na halmashauri kwa ajili ya kusaidia akinamama, watoto na wazee, kwa sababu yale
maeneo hatukuwa na kituo cha afya, lakini kwa maelezo yao walileta mkataba wa kusitisha ili huduma hii isiendelee. Sasa wananchi wanapata adha kwa sababu hakuna hopsitali ya karibu kwa sababu hospitali ya wilaya sasa ndiyo tunajenga. Tungeomba waturudishie hii huduma, ule mkataba ambao Katibu Mkuu aliandika ili akinamama hawa waendelee kupata huduma la sivyo, tutapata shida, lakini tutakapomaliza hospitali ya Wilaya wanaweza waka-cancel mkataba huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuishukuru Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, tumetengewa bilioni mbili na milioni mia nne kwa ajili ya kujenga soko zuri la Kimataifa pale Mnanila. Hili ni soko ambalo litakuwa na vyumba 300 vya kuuzia bidhaa, tutakuwa na vizimba vya kuuzia bidhaa 500, kutakuwa na vyumba vya Benki, kwa hiyo ni jambo kubwa. Tunachoomba, hiki kitakuwa ni chanzo cha mapato ya halmashauri lakini pia wafanyabiashara watapata eneo la kufanyia biashara. Tunaahidi kwamba tutautendea haki mradi huu, tunahitaji, tungependa tuone fedha hizi mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu; naomba tu pamoja na changamoto zote zilizopo kwenye Wilaya yangu ya Buhigwe; Wilaya yangu ya Buhigwe kwenye ufaulu katika nchi hii ni ya 21 katika Halmashauri 189. Kwa hiyo ningependa tu niwapongeze Walimu kwa changamoto zilizopo lakini Buhigwe sisi kwenye ufaulu katika nchi hii ni watu wa 21 kati ya 189. Kwa hiyo nawapongeza na waendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma, kwa wale ambao hamna taarifa ni Mkoa wa 10 katika mikoa ya Tanzania hii. Kwa hiyo msije mkafikiri tuko nyuma sana mkafikiri kwamba watu hawafanyi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya maboma ya madarasa kuezekwa; tungependa kuwe na special program. Wananchi wamejitolea, tunayo maboma karibu 17 kwenye Jimbo langu sasa tungependa kupata nguvu angalau tuweze kuezeka. Ilani ya Mheshimiwa Waziri ilisema kwamba tukiweza kufikisha kwenye lenta wao wanaweza wakatusaidia kuezeka. Kwa hiyo, nalo hilo tungeomba watusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu tunataka kupandisha shule nne ili ziwe kidato cha tano. Shule ya Myama, shule ya Buyenzi, shule ya Mkoza, pamoja na shule ya Munzeze tungepanda nazo zipande kuwa kidato cha tano kwa sababu sasa watu wanafaulu vizuri ili waweze kupata sehemu ya kwenda kusomea elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA miundombinu. Mheshimiwa Rais JPM alikubali kwamba kwa kuwa wilaya yetu tumehamisha makao makuu, vijiji namna ya kuungana imekuwa ni tatizo; alikubali kwamba ataweza kutupasulia barabara mpya ili ziweze kuunganisha vijiji na vijiji na Sheria ya TARURA inasema kwamba wao hawawezi kupasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapeleka ombi na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais; tunayo ya kutoka Kijiji cha Nyakimwe kwenda Muhinda, Munzeze kwenda Kwitanga, Rusaba kwenda Nyarubanda, Myegera kwenda Songambele,
Kilelema kwenda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja na hiyo ndiyo ilikuwa hoja yangu ya mwisho. Nakushukuru.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia mpango huu.

Kwanza kabisa nimpongeze Waziri kwa wasilisho lake zuri, kwa kweli mpango tumeupitia, mpango wako ni mzuri kwa sababu umejaribu kupitia tulipotoka tulipo na tunakoenda. Kwa hiyo, nikupongeze kweli kweli na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, lakini kipekee naipongeza Kamati yetu ya Bajeti na mimi nipo kwenye Kamati hiyo tumeipitia bajeti yetu, tumetoa maoni yetu kwenye Kamati yetu ya bajeti nafikiri maoni yetu unayo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi sitaki hata kupita sana kwa sababu yote tulishayasema kwenye Kamati na mengine tumekushauri ndani ya Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee niipongeze Serikali kwa mipangilio ambayo imeshatekelezwa na miradi iliyokwisha tekelezwa ni ukweli usiofichikwa kwamba mmefanya kazi nzuri na miradi hii ni miradi mikubwa ambayo kwa kweli inahitaji kuwa serious ili uweze kui-achieve, kama hautakuwa serious hautaweza ku-achieve kwa sababu inahitaji fedha ngingi. kwa hiyo nakupongeza sana Waziri nampongeza Rais, napongeza na chama changu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye mpango wenyewe kwenye sheria pale kwenye Sheria ya PPP. Pale umeandika kwenye page 43 kuna miradi ya maji nayo ambayo inatakiwa kwenda na PPP. Sasa mimi wazo langu ni kwamba ile miradi sasa ambayo ya maji ambayo unataka iende kwa PPP katika ile orodha ya miradi ambayo unataka iweze kuwepo kuwa solicited au iko solicited na Serikali hatujaweza kuipata, ni vizuri kwenye mpango unaokuja tuweze kuona kwenye maji, miradi ya maji ulivyoitaja ukurasa wa 43 ni miradi gani hiyo ili tuweze kuielewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, page ya 47 ya hotuba ya Waziri kuhusu miundombinu amesema tuweze kuunganisha Tanzania na nchi jirani kwa upande wa miundombinu. Wazo langu langu pale sasa Mheshimiwa Waziri kwa sisi ambao tuko mpakani tunaomba kwenye mpango wako utuwekee madaraja kuunganisha nchi na nchi, tunayo matatizo specifically kwenye Jimbo la Mheshimiwa Obama pale tunatenganishwa Burundi na Tanzania na mto ambao sasa ule mto ni mkubwa tunahitaji madaraja. Kwa hiyo katika kupitia page yako ya 45 tunaomba madaraja pale uweze kuyaweka ili angalau iweze ku-facilitate biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa page 37 ya hotuba yako upande wa kilimo umetaja mambo ya michikichi tungeomba kwa sababu Waziri Mkuu alikuja kwa heshima kubwa sana Mkoa wa Kigoma akawa ameimiza michikichi. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Kilimo iweze kulichukulia hilo na wewe umeliweka kwenye mpango ili iweze kuwa serious Mkoa wetu wa Kigoma michikichi mbegu na utafiti viweze kuwa vimeimarishwa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo amelisema Ndugu yangu Silinde kwenye hotuba yake ame- challenge sana pale kwenye hotuba yako ukurasa wa 34 aliposema changamoto umezieleza pale, sasa siamini kama mpango wowote ule ambao unaweza ukawa umepita ambao changamoto hazipo. Sasa kutupia tu kwamba changamoto zipo sisi tulitegemea kama Wabunge sasa tutoke pale tumpe mawazo namna ya kwenda kwenye mpango unaokuja. Lakini kusema kwamba changamoto kwenye mpango wowote hamna mimi nafikiri siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni mifano ambayo sasa tunaanza kuingizia mfano nchi ya Rwanda, sisi ni Wabunge wa Tanzania tuko proud na mambo yetu ya Tanzania. Kusema kwamba Rais Kagame anawashauri wengine nchi za nje siyo sahihi na sina uhakika JPM kama anahitaji washauri kwa sababu kama niwashauri Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi bado yuko hai, Benjamin William Mkapa bado yuko hai, Jakaya Mrisho Kikwete bado tuko hai Chama cha Mapinduzi ambacho ni imara bado kiko hai, Kamati Kuu bado iko iamara Wabunge wa CCM tuko imara, tutaendelea kumshauri tuhakikishe kwamba nchi yetu inaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye taarifa hizi mbili. Kwanza nawashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote hizi mbili kwa ripoti nzuri ambayo wameweza kutuletea hapa mbele yetu; lakini pili niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kutuletea maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuanza na moja hili la Mheshimiwa Msigwa ambalo alisema, economic growth haiendani na development growth; ikiwa na maana kwamba anaongelea pato la Taifa. Kwanza tuipongeze Serikali yetu kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2015, 2016 na 2017 uchumi umeendelea ku-grow kwa 7% ambapo ni kitu kikubwa sana, lazima tujipongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa ameendelea kuchanganya, haelewei maana ya pato la Taifa kukua. Viashiria vya uchumi kukua ni kuongezeka kwa miundombinu hii ambayo inaendelea katika nchi yetu. Kwa hiyo, unapoona miundombinu inaendelea kukua, ni moja ya kiashiria kwamba uchumi umekua na maendeleo sasa yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya kupatikana umeme wa uhakika kuliko tulipotoka, vilevile ni kiashiria cha kwamba pato limeongezeka na huduma ya umeme sasa inakuwa nzuri vilevile na huduma za jamii. Hivyo, vyote ni viashiria ambavyo vinaonyesha uchumi wa nchi kukua. Kwa hiyo, haina uhusiano wa moja kwa moja na fedha zake za mfukoni kama hufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niendelee kuipongeza Serikali kupitia TRA, wamefanya kazi nzuri chini ya Mkurugenzi, Mheshimiwa Kichele. Ukiangalia mwenendo wa makusanyo ya nchi yetu, mapato yameendelea kuwa mazuri. Naendelea kumpongeza Waziri wa Fedha na timu yake ya wataalam wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wamekuja kwenye Kamati yetu, wamejaribu kuonyesha mapato ya nusu mwaka: Je, wameweza kufanyaje katika makusanyo? Ukienda kwenye mapato yanayotokana na kodi, jumla yake wameweza ku-achieve kwa asilimia 91, lazima tuwapigie makofi kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma namba mbili, kuhusu ushuru wa forodha lengo la mwaka ni shilingi bilioni 1.2, lakini wameweza kukusanya shilingi bilioni 588 ambayo ni asilimia 88.7. Ni jambo kubwa ambalo inabidi tuwapongeze. Kwa hiyo, TRA mnafanya kazi nzuri, hongereni sana na Waziri wa Fedha mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye mwenendo wa misaada na mikopo nafuu hadi Desemba, ukiwapima kwa miezi sita ufanisi wao ukoje? Watu wanasema wafadhili hawatupi fedha, mikopo haiji; naomba niwaambie wameweza ku-achieve kwa lengo la nusu mwaka, wamefikia asilimia 66.4. Wapigieni makofi kwamba Serikali inafanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuendelee kuwapigia makofi kwa sababu ukiangalia mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki, sisi sasa Januari tumeweza kufika 3%. Mpaka Desemba, Kenya walikuwa 5.7% ambao wako juu, sisi tuko chini, ni lazima tuwe proud na tunachokifanya. Kwa hiyo, ni jambo zuri, tuendelee kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpima, Mheshimiwa Waziri Mpango, kaka yangu: Je, fedha anazokusanya anapeleka zinapoitajika? Kwa miezi sita mfano, kwa matumizi ya kawaida kwa lengo lake alivyojipangia kwa nusu mwaka amefikisha 62.7%. Kwa nini usimpe haki yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia na madeni mengine; ulipaji wa madeni ya ndani na nje, malipo na riba za ndani amefikia asilimia 32. Malipo ya riba na mitaji ya nje amelipa kwa asilimia 53 ya lengo. Kwa hiyo, naweza nikasema, Wizara ya Fedha ukiipima na nchi nzima kwa ujumla tunavyotekeleza bajeti yetu, Mheshimiwa Zitto unacho hiki kitabu umesoma, tunaenda vizuri na uende kwenye media na uwaambie Watanzania tunaenda vizuri. Kwa hiyo, ukiwapima, wanaenda vizuri kwa viashiria vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali kwa kazi nzuri sana inayofanya chini ya uongozi wa Jemedari JPM.
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, nami niweze kuunga mkono azimio hili la kupandisha haya mapori na kuwa hifadhi. Kilichonisukuma niweze kuunga mkono maazimio haya, sisi Mkoa wa Kigoma tumeathiriwa sana na hili pori lililokuwa la Biharamulo. Hili pori la Biharamulo lilikuwa linatufanya mabasi yanapopita pale ya abiria lazima uende na Askari wakiwa wanalinda. Ukiwa na gari lako la binafsi, uende na Askari wakulinde mpaka utakapofika maeneo ya Kibondo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kulipandisha hadhi hili kuwa hifadhi, tuna uhakika kwamba mambo yataanza kuwa mazuri kwa sababu majambazi kutoka Burundi na Rwanda wamekuwa wakijificha mle. Kwa hiyo, ndiyo sababu iliyonifanya nivutike kuunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, hata haya mapori mengine tunazo faida nyingi za kiuchumi kwa sababu nazo zitakuwa ni sehemu ya utalii, lakini tour guide wetu watapata ajira na mahoteli yataweza kuwekwa pale kwenye baadhi ya maeneo na vile vile mapato utalii nayo yataongezeka. Faida nyingine, tutaendelea kutunza mazingira kwa sababu, kwa kuwa ni mapori watu wamekuwa wakienda kufanya shughuli mbalimbali za ufugaji, wanalima, wanakata miti, wanakata mkaa ndani ya yale mapori. Kwa hiyo, hifadhi nzima inakuwa imeharibika. Kwa hiyo, sababu hizo zinasababisha tuweze kuunga mkono azimio hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa zaidi ni faida za kiuchumi tutakazozipata kwenye mapori haya. Mengine nashukuru kwamba kwa kuwa yanaenda TANAPA na tuna Mkurugenzi pale Kijazi yuko imara kuweza kuyasimamia, kwa hiyo, naye tunampa wito kwamba aweze kuyawekeza miundombinu ndani ya hifadhi ili nayo hadhi yake iweze kuwepo. Zaidi elimu iweze kutolewa kwa vijiji vinavyozunguka kwa sababu wengine walikuwa wanakidhi mahitaji yao mle. Kwa hiyo, elimu iweze kutolewa kwa vile vjiji vinayozunguka ili faida ya hifadhi hizi ziweze kuonekana.

Mheshimiwa Spika, sitaki kupoteza muda, naunga mkono maazimio haya. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia mpango ulioko mbele yetu. Nianze tu kwa kuipongeza Serikali na sisi wenyewe kama Wabunge kwa sababu hii mipango yote imekuwa ikipita mikononi mwetu hapa ndani ya Bunge na wote tumeitendea haki katika kuichangia

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko Kamati ya Bajeti, tumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na ofisi nzima kwa ushirikiano mzuri waliotupa na maelekezo na ndani ya mjadala ule yalikuwa ni mengi tumeyaongea, lakini kwa kweli naishukuru Wizara inafanya kazi nzuri na wako very responsive katika masuala yetu katika vikao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ya kusema. Tukiangalia viashiria vya uchumi, kwa kweli ni hakuna namna zaidi tu ya kuwapongeza kwa sababu dalili za viashiria vya uchumi vyote viko vizuri na tunaenda vizuri. Ukuaji wa uchumi kulingana na malengo yetu ni kwamba ifikapo mwaka 2021 tunataka uchumi wetu ufike asilimia 10. Sasa hivi ni mwaka 2018/2019 tumefika 7%, tuna-gap ya 3% pale ambayo nahisi kwamba tunaenda vizuri, progress iko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye mfumuko wa bei, bado tuko chini, sasa tumefikia asilimia 3.2 ambayo kwa kweli tunaona tunaenda vizuri. Hata hivyo, hapa ni lazima tuangalie, pamoja na kwamba tunaminya ule mfumuko wa chakula usiwe mkubwa ambapo unachangia kwa asilimia zaidi ya asilimia 28 sasa ni vizuri tuone, kwa sababu hapa inaonyesha kwamba kwa wawekezaji inawapa mileage nzuri kwa sababu they can plan. Vilevile kwa wazalishaji inaonyesha kwamba bei haibadiliki kwa kiasi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri wataalam waioanishe na riba tunazozipata kwenye mikopo. Kama inflation ya 3.2 siyo kubwa, vile vile na riba za kupata mikopo ili uweze ku-invest gharama zako na kupata faida, ni vizuri sasa pale wachumi muweze kutuchanganulia ili tuweze kuipata vizuri. Inaonekana kwamba huenda faida ya kuzalisha inakuwa ni ndogo kwa sababu mfumuko nao umebana sana, kama interest rate ya kwenye mabenki hujaibana vizuri. Kwa hiyo, hapo napo wataalam wetu wa mipango mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye Sekta ya Kilimo, target yetu ni mwaka 2021 tunataka ukuaji uwe wa 7.6%. Sasa hivi tumefika 5.3%, tunakwenda, lakini Mheshimiwa Waziri wa Mipango tuangalie kwa kina ukuaji huu wa kilimo ambao unaajiri watu wengi hebu mkae mfanye retreat mwone ni wapi tunakosea? Kwa nini huu ukuaji usipande? Kwa sababu lengo letu tunataka tufike 7.6. Tutakapofika 7.6 kidogo mwananchi ataanza kuona pato kwenye mfuko wake. La sivyo, kama hatuwezi kwenda kwa namna hiyo na ku-invest na kutoa fedha kwenye vipaumbele vya Wizara hii, ukiangalia trend ya utoaji wa fedha kwenye za maendeleo kwenye kilimo saa nyingine hatufanyi vizuri, kwa hiyo lazima twende sasa tuweze kuwekeza pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi za mazao ambazo zinashughulika na kilimo cha wananchi wetu ni vizuri na ninashauri kwamba kwa kuwa sasa Serikali imeweka macho na Waziri Mkuu yuko huko kwa ajili mambo ya ushirika, tuongeze nguvu, tusipunguze nguvu ili wakulima wetu waweze kufaidi matunda yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija sasa kwenye mpango wenyewe ukiangalia mpango wetu kila kitu ambacho kinafanywa na Serikali ya CCM nchi hii, kiko kwenye mpango; lakini utakuta watu wanabeza au kuona kwamba hiki kitu ni kipya, hakikuwepo kwenye mpango. Mheshimiwa Waziri nakuomba, elimu ya mpango wowote tunaoutoa inaonekana haufiki kwa watu. Kitu kikija wanaona kwamba Serikali imekurupuka, hakikuweko kwenye mpango. Sasa ni vizuri bajeti ya kutoa elimu kwa ajili ya kuelimisha wananchi kwenye mpango, aidha Wizara yako, Kitengo chako kile cha Mpango ukipe bajeti kiwe kinaeleza mipango ya Serikali kwa kila sekta kwa miaka inayokuja ili wote tuweze kwenda pamoja. Inaonekana bado kuna information gap kati ya wananchi na mpango wenyewe.

Mimi bado najiuliza kitu kimoja, naipongeza Serikali, mnatoa fedha nyingi na zinaenda kwenye miradi, lakini utakuta mwenge wa uhuru ukipita kwa dakika tano kwenye mradi wanagundua kosa. Mwenge ukipita kwa dakika tano kwenye eneo lako, wanagundua kosa. Wizara walikuwa wapi? Wataalam walikuwa wapi? Mkuu wa Wilaya alikuwa wapi? Mkuu wa Mkoa alikuwa wapi? Waziri mhusika wa sekta alikuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi vitu tunaweza tukaendelea kusema kwamba tuna fedha nyingi lakini kumbe miradi yote tunayoipelekea fedha inakuwa haina tija. Kwa hiyo, naomba kwa kweli tuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitunga Sheria ya Uhujumu Uchumi, sasa itoke kwa wafanyabiashara, iende sasa kwa wataalam. Wahujumu uchumi wawe ni wataalam ambao hawasimamii miradi vizuri. Fedha hizi zinakusanywa kwa wananchi kwa nguvu kubwa na tunatoa kodi kubwa, hii sheria sasa iingie maofisini, Waziri ajikute naye ameingia kwenye uhujumu uchumi, kwa sababu hakusimamia fedha alizozipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, nirudi kwenye miradi hii ya kawaida. Mheshimiwa Waziri ulikopa fedha Euro milioni nane za maji katika mikoa ya Kigoma. Ubelgiji walitoa hizo fedha lakini miradi ile nayo haiendi. Sasa tukuulize na utuambie: Je, zile fedha zimeshatoka au imekuwaje? Maana yake miradi haiendi na hakuna kazi yoyote inayofanyika. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli uangalie hiyo miradi ya maji ambayo mmekopa fedha Euro milioni nane ili tuweze kwenda vizuri na miradi kote ilikopangwa iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya PPP haitoshi Tanzania. Tunacho kitengo kizuri sana pale Wizara ya Fedha ambacho kinachushughulika na miradi ya PPP. Miradi ile tunaisoma kila wakati, hakuna kitu kinachofanyika. Tangu nimeingia Kamati ya Bajeti miradi ile inaletwa kwetu, tunaisoma, inachakatwa inafanyiwa nini, hakuna kinachoenda. Lazima PPP ifanye kazi iweze kuachia fedha za Serikali ili nazo zifanye kazi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mpango huu wa mwaka 2015 – 2021 tulisema unakuwa financed na shilingi trilioni 107. Tukasema watu binafsi watachangia shilingi trilioni 48. Tumeingia kwenye Kamati, Wizara haina data inayoonyesha private people wamechangia kiasi gani na hiyo miradi iko wapi? Sasa kama huwezi ku-track miradi iliyochangiwa na wawekezaji binafsi, lakini uliiweka kwenye mpango, hilo ni eneo ambalo lazima huo udhaifu tuweze kuuondoa. Tunataka kuona shilingi trilioni 48 za private sector imechangia wapi? Sehemu gani? Mradi gani? Kiwanda gani? Au project gani? Kwa hiyo, hiyo naomba kwa kweli tuweze kulii-improve vizuri ili tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya umeme, barabara na afya, tunaomba speed ya ukopaji, kwa sababu wakati mwingine fedha ni za watu, kwa hiyo, tuongeze kasi ya kutafuta fedha hii miradi iweze kuendelea. Vijiji tunavyotajiwa ni vijiji ambavyo tunapeleka umeme, vinatugombanisha na wananchi kwamba umeme uko sehemu ya center, lakini kwenye vijiji ndani haujaingia. Kwa hiyo, ni vizuri tutafute fedha. Pamoja kwamba tumekopa mpaka tumefikia shilingi trilioni 53, tusiogope kwa sababu deni letu bado linahimilika, tuendelee kufanya hii miradi iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango sijaona mahali ambapo mafunzo kwa vijana yamesisitizwa sana. Vyuo vya VETA mna mpango wa kuvijenga, lakini kwenye mpango hakuna mahali ambapo pamesisitizwa sana. Naomba hapo kwenye Mpango tutakapourekebisha tuweze kuona mafunzo kwa vijana na ajira baadaye inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kusema mengi, mengi tumeyaandika kwenye ripoti yetu ya Kamati, nafikiri inatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi hii niweze kuchangia hii Wizara, kwanza kabisa nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu na Wakuu wa Vitengo vyote vya ndani ya Wizara hii, kwa kweli wameendelea kutupa ushirikiano ndani ya Kamati ya Bajeti, naomba niwapongeze sana. Lakini niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwapa mwongozo mzuri katika usimamizi wa fedha ambayo ni jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kabisa nipongeze Kamishna Mkuu wa TRA, kwa taarifa zake za ukusanyaji wa mapato hasa ukiangalia kule kwenye jedwali la makusanyo ukurasa wa 180 utaona kwamba average yake imekuwa ni asilimia 87 ambayo ni nzuri, kwa hiyo nampongeza sana. Lakini niendelee kumpongeza Magavana wote wa Benki Kuu kwa kazi nzuri wanayoendelea kutoa miongozi ya fedha katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kumuuliza Mheshimiwa Waziri ukiangalia page yake 178 Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa asilimia 17 ya fedha za OC, sasa nilitaka kujua ni kitu gani kinawafanya wakati Wizara zako na Taasisi zako zilizoko kwako zina asilimia 70, 60 hao wana asilimia 17 na wanasimamia mashirika ya umma. Ni kitu gani wamefanya makosa au ni shughuli gani hawaifanyi mpaka sasa wasiweze kupata fedha? Hilo nilitaka Mheshimiwa Waziri uweze kutupa ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine ni uhakiki, Wizara ya Fedha imechukua majukumu ya kuhakiki fedha, sasa wito wito kwamba speed ya kuhakiki imekuwa ni ndogo na kama kuna timu za uhakiki basi muweze ku-recruit watu wengine kutoka kwenye Wizara nyingine kwa sababu kwa kweli malipo ya wazabuni, wakandarasi yamechelewa sana na halafu hatuna deadline ya kuona ni lini tutaweza kuhakiki. Lakini feedback kwa wale ambao hawakufanikiwa hakuna utaratibu ambao mmeuleza kwenye Kamati ambao unawapa feedback wale ambao madai yao hayakupita qualification zenu, kwa hiyo kule wanaendelea kubaki wanakijua wanadai kumbe ninyi mmeshayatupa pembeni.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuna sheria hii ya asilimia 15 kama wanazo-deposit hawa wenye viwanda vya sukari, hebu tunaomba maana yake wanakuja kwenye Kamati zetu, wanaonesha mitaji yao imeyumba. Sasa Serikali inahimiza viwanda lakini inachukua fedha zao, lakini haiwarudishii sasa unachohimiza ni nini na unachotaka kufanya ni nini.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako yote ni control, hakuna mahali kwenye Wizara hapa unachosema kwamba nitahamasisha wafanyabiashara wafanye hivi, nitahamasisha wakulima wafanye hivi. Sasa ni mambo umejaza mambo ya kodi tu ambayo kwa kweli ni vizuri huko mbele style hii na wanaposikia hotuba yako wapate faraja wafanyabiashara, wachimbaji waone faraja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nipongeze BOT kwa hatua yao kwa kupitia Sheria hii ya Bureau De Change sisi tuwape nguvu tuwaombe waendelee walete kanuni na wale wanafanya biashara ya Bureau De Change ambao hawana makosa basi waweze kufunguliwa waweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuchelewa kwa madai ya wastaafu. Wastaafu wanadai, wastaafu inachukua mwaka mzima bado hajalipwa fedha zake, hebu tunakuomba hicho kitengo kinachoshughulikia wastaafu kwa sababu ile database ya watu wanaostaafu Mheshimiwa Waziri mnayo kila Idara na kila sekta. Kwa hiyo, ni vizuri nayo hii iweze kuangaliwa vizuri iweze kwenda haraka.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho ni mambo ya business license. Sasa hivi Watanzania wote hatuwezi kuajiriwa, watu wanatafuta namna ya kujiajiri, lakini bureaucracy iliyopo unapotaka leseni mpaka unaambiwa uende kwenye TRA ukapate tax clearance; tax clearance unaipataje na hujaanza biashara?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri huu mfumo uliopo hebu tuurahisishe mtu akienda kutafuta leseni siku hiyohiyo au siku ya pili aweze kuipata, lakini kuliko kuzunguka aende TRA kumbe hajaanza biashara na akifika kule anaanza kukadiriwa biashara, unataka kufanya biashara gani? Unaanza kukadiriwa kodi na huku biashara haujaanza, kwa hiyo, ni vizuri sana muweze kuiangalia hiyo, ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisiseme mengi. Mengi tumeyasema kwenye Kamati yetu ya Bajeti na nisipende kuyarudia kwa sababu tumeyaandika na Wabunge wote wameyaona. Nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niwezeze kuchangia muswada ulioko mbele yetu wa kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016.
Kwanza kabisa naomba nipongeze Serikali, nimpongeze Waziri na Naibu wake, kwa kutuletea sheria nzuri kabisa ambayo itaweza kutuokolea fedha nyingi. Kwenye bajeti ya mwaka huu tumepitisha asilimia 40 ya fedha zote kwenye shughuli za maendeleo; sasa kama tumepitisha asilimia 40 maana yake ni fedha nyingi. Fedha nyingi hizi, bila kuwa na sheria ya kuzilinda hazitafikia wananchi. Kwa hiyo naomba niipongeze Wizara kwa kweli, na Mheshimiwa Waziri Mpango, kwa kuleta mpango mzuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya muswada huu wa kupunguza gharama na kuleta ufanisi ni jambo jema ambalo wote Wabunge lazima tuliunge mkono ili sheria hii iweze kufanya kazi. Lakini nipongeze kipekee kwa sheria hii kuja kuangalia wazawa, kwamba wale wenye makampuni ya wazawa, local waweze kupewa kipaumbele, nalipongeza sana na naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kujali makundi mbalimbali, kina mama, walemavu, wazee ni jambo jema na Serikali makini lazima iangalie watu wake na makundi yake waweze kushiriki kwenye uchumi huu, kwa hiyo nalo nisuala ambalo nimesimama kuipongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ku-promote local production ya bidhaa zetu ni jambo zuri ambalo kwa kweli nahamasisha kwamba Wabunge wengine tuweze kuiunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria imekwenda mbele zaidi kwa kurekebisha ushiriki wa Madiwani kwenye manunuzi. Mimi naishurukuru Serikali kwamba kazi ya Madiwani iwe ni kuisimamia Serikali kwa maamuzi iliyoyafanya, siyo na Madiwani kuwa wanashiriki kwenye tender ambacho kinakosesha ile roho yenyewe ya usimamizi wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu uko kwenye bei ya soko. Hatuna tafsiri ya bei ya soko na sioni kama kuna mtu yeyote anajua bei ya soko. Bei ya soko inategemeana na bidhaa yenyewe, lakini kwa kuwa ni manunuzi ya Serikali, mimi nilikuwa napenda kwamba Serikali iwapongeze wazabuni na wakandarasi wote, kwa sababu wakandarasi hawa wanaikopesha Serikali, kabla hawajawalipa. Kwa hiyo wana umuhimu mkubwa sana katika Serikali hii, kwamba wanafanya vitu in advance kwa kutumia fedha zao, Serikali inakuja kuwalipa baadaye. Kwa hiyo hawa ni wabia muhimu sana; na hasa kwenye PPP tunayoisema kila siku, kwa hiyo mimi naona kwamba bei ya soko ili tuweze kuipata Waziri inabidi sasa ujipange, je, unazo fedha za kuwalipa wakandarasi kwa muda ili waweze kukupa bei ya soko?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama unawalipa baada ya mwaka, miezi sita hakuna mfanya biashara yeyote mwenye kampuni ambaye anaweza ku-predict bei ya vifaa baada ya mwaka mmoja, kwa hiyo lazima aweke bei ambayo itakuja ku-compensate loss yoyote ile atakayo ipata. Lakini ni vizuri ujipange sasa kwa fedha hizi uweze kuwalipa wazabuni, na wenyewe watakupa bei ya soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipengele cha kujadiliana ni kipengele kizuri, lakini wasiwasi wangu itakuja kuleta migongano ya makampuni kulingana na ulivyofanya majadiliano, kama ulijadili na kampuni moja ambayo unaitaka ipate na ikashusha bei na ukaiacha nyingine, hapa ndio utakuwa ni kwenye mgogoro. Kwa hiyo hiki kipengele ni vizuri tukiangalie kwa makini, tuweze kujua namna ya kuja kutatua migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali kwenye ujenzi kwa nini isiboreshe vituo vyake vya ujenzi, kwa kununua mitambo, ma-grader ili gharama ya kutengeneza barabara iweze kupungua. Kama mnataka gharama zipungue basi ningeshauri kwamba mboreshe kila Wilaya ipelekewe mitambo ya ukandarasi, iwepo kitengo cha ujenzi, na iwe inatengeneza barabara wawe weka mafuta na madereva wanaajiriwa. Hiyo inawezekana, kama mmeamua kwamba tuweze kupunguza gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko emergency procurement ambayo kwa kweli naona kwenye muswada huu haijasema vizuri, labda kwenye kanuni za Waziri, Hospitali huwa zinaishiwa gloves, zinashindwa kununua kwa sababu mlolongo wa manunuzi umekuwa mrefu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninakuomba kwenye ununuzi wa ghafla hasa kwenye dawa hospitali, MSD ni vitu muhimu lazima uziweke kwenye kanuni, kama hujaweka kwenye kanuni mtu anaweza akafa nashindwa mtu kuchukua hela ofisini au ndani ya kituo kwa sababu milolongo ya manunuzi iko mbali; kwa hiyo kanuni tunaomba uweze kuiweka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sina mengi, ninashukuru na sheria ni nzuri tuipe nguvu tuipe support, nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye kwa kutuandalia sheria nzuri, na mara nyingi amekuwa akifanya hivyo, naye tunampongeza sana.