Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Selemani Moshi Kakoso (105 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo lipo kwenye maeneo mengi katika nchi yetu ni miradi ya maji ambayo Serikali ilianzisha kushindwa kutekelezwa. Jimboni kwangu kuna miradi ya maji katika Kijiji cha Majalila na Igagala na imeanza kufanyiwa kazi na imefikia asilimia 70. Sasa hivi miundombinu ya miradi ile imeanza kuharibika kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ile miradi ambayo kimsingi ingewasaidia wananchi kwenye maeneo hayo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ipo miradi mingi, tuna miradi zaidi ya 508 ambapo katika awamu ya kwanza ya programu haijakamilika. Hivi sasa ipo katika hatua mbalimbali, ipo kwenye asilimia 99 na mengine 60. Sasa hivi tumeingia awamu ya pili ya programu lakini lazima kwanza tukamilishe ile miradi ambayo ipo mbioni kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi fedha zimeshaanza kupatikana kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi ambao walikuwa katika hatua mbalimbali na maeneo mengine walikuwa yamesimama, kwa hiyo, tunawalipa ili kusudi wakamilishe miradi hiyo. Nilihakikishie Bunge lako kwamba Serikali itakwenda kukamilisha miradi yote ili wananchi wetu waweze kupata maji kama ilivyokusudiwa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ambayo Serikali imetoa ya hatua ya awali ya ujenzi wa hospitali ya Mkoa.
Swali langu la msingi nimeuliza kwa kuwa, hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ndiyo iliyobeba uzito wa kuhudumia takribani wagonjwa zaidi ya laki tano wanaotumia bajeti ya Halmashauti ya Wilaya ya Mpanda, ni lini Serikali itaharakisha mchakato wa ujenzi huo wa hospitali ya Mkoa ili kuepusha Halmashauri ya Mpanda inayotumia bajeti ya Halmashauri kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wengi kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuisaidia hospitali hii ili iweze kukidhi mahitaji kwa sasa?
Lakini swali la pili…
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili naomba kuweka uzito, tunavyo vituo vya afya ambavyo kama vingeimarishwa vingesaidia sana uzito wa hii hospitali ambayo imeelemewa. Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vituo vya afya ambavyo vipo katika Mkoa wa Katavi, hususani vile vya Karema, Mwese na Mishamu, napenda kujua hayo.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ameuliza ni lini hospitali hii ya Mkoa itakamilika kwa sababu hospitali ya Mpanda ambayo ni ya Wilaya sasa ndiyo inayotumika kwa ajili ya kutoa huduma hizo za Kimkoa. Je, ni hatua gani za dharura ambazo Serikali inaweza kuzichukua kwamba tutajaribu kuona na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda namna ambavyo tunaweza tukaiongezea uwezo wa dharura hiyo hospitali ya Wilaya ili kuweza kumudu majukumu ya Kimkoa. Hata hivyo, bado narudia kusema jibu la suluhu ya kudumu katika jambo hili ni kuhakikisha kwamba tunajenga hospitali hii na ndiyo maana Serikali inaendelea kutenga fedha kwaajili ya kujenga hospitali ya Mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza je, kama kuna vituo vya afya ambavyo vinaweza vikasaidia kupunguza uzito huu wa wagonjwa katika hospitali hii ya Wilaya ambayo sasa inatumika kama hospitali ya Mkoa. Ni kweli Serikali tumejipanga na tutajaribu kuona kwa vipaumbele na kwa maeneo
aliyoyasema kama tunaweza tukaanza na vituo hivyo kutokana na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Mpanda.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya mpya ambayo ina Jimbo moja tu la Uchaguzi la Mpanda Vijijini. Eneo hili la kiutawala ni kubwa mno, lina uwezo wa kutoa mgawanyo wa halmashauri mbili, kwa maana ya Ukanda wa Ziwa, Halmashauri ya Karema na ukanda wa huku juu eneo la makazi mapya ya Mishamo. Je, ni lini Serikali itafikiria kutoa mamlaka ya kugawa maeneo haya, ili yaweze kuwasaidia wananchi wa Mpanda kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, Wilaya ya Mpya ya Tanganyika, lakini pale awali nadhani tulikuwa katika mchakato ulikuwa hatuna Wilaya hii, lakini baadaye mchakato ukafanyika tukapata Wilaya, lakini bado changamoto ni kubwa sana ya Halmashauri hii. Kwa hiyo, naomba niseme tena vilevile Mheshimiwa Kakoso kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya awali kwamba mimi naomba Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua eneo lenu nalo limegawanyika sana hapa katikati, Halmashauri nyingi zimepatikana katika eneo hilo, lakini bado kijiografia eneo bado ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tena nitoe maelezo yaleyale kama niliyotoa mwanzo ni kwamba, andaeni tena ule mchakato upite katika vigezo vyote, katika vijiji, WDC, Halmashauri, RCC, halafu ikifika katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI kama nilivyosema ni kwamba, tutafanya maamuzi sahihi kutokana na vigezo vitakavyokuwa vimefikiwa katika eneo hilo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mpanda Vijijini lina miradi miwili ya umwagiliaji. Mradi wa kwanza ni ule wa Karema ambao Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo lakini bado haujakamilika na mradi wa pili ni ule wa Mwamapuli ambao unamwagilia vijiji vya Kabage. Miradi yote hiyo haijaweza kukamilika kwa wakati. Je, ni lini Serikali inaweza kukamilisha miradi hiyo ili iweze kuwasaidia wananchi ili kutopata hasara kwa fedha za Serikali ambazo zimeshatumika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia kuhusu miradi ya umwagiliaji, ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na miradi ya umwagiliaji katika eneo hilo lakini baadhi ya miradi hiyo ilipata matatizo kidogo na tumeagiza kuifanyia kazi. Kwa sababu ya masuala yaliyotokea siwezi kumjibu sasa hivi, ripoti ikija naweza kumfahamisha. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba yale matatizo yote yaliyojitokeza yanatatuliwa na tuhakikishe kwamba tunakamilisha ile miradi ili wananchi waweze kutumia miradi ile ya uwagiliaji wazalishe zaidi tuweze kupata chakula.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali ilitumia fedha nyingi sana kujenga gati la Karema, fedha hizo ambazo zilipotea na kilichojengwa pale ni nyumba moja ambayo haijakamilika na kuna choo ndicho ambacho kilikamilka; lakini fedha zilizotolewa na Serikali ni nyingi sana:-
Je, wale walioisababishia Serikali hasara kubwa sana ya fedha nyingi, mmewachukulia hatua gani ambazo ni za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Moshi Kakoso, naomba tuijadili kwa undani kama ambavyo tulianza na tuwashirikishe watu wengi zaidi ili hatimaye kama kweli kuna tatizo hili linaloongelewa tuanze kuwashughulikia wahusika kwa kutimia vyombo vyetu vya dola kuanza kufanya uchunguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ninachomwomba Mheshimiwa Mbunge, tupate taarifa kamili. Tunavyofahamu, bajeti ilitumika kama ilivyopangwa na kazi ilifanyika kama ilivyopangwa. Sasa kwa taarifa ya Mheshimiwa Moshi Kakoso, naye akiwa ni mmoja kati ya watu ambao tumedhamiria kwa pamoja kuwajengea miundombinu Watanzania, nina uhakika ana taarifa za ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuzipate hizo taarifa za ziada ili hatimaye tuzipeleke kwenye vyombo vya dola wazifanyie kazi na baadaye tuchukuwe maamuzi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, mradi wa ORIO ulikuwepo toka mradi wa umeme vijijini Phase II ambao ulihusisha vijiji vitano, vya Kabungu, Ifukutwa, Igalula na Majalila. Mradi huu ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha, Serikali ilishindwa kuwekeza fedha ambazo zinge-support kampuni ya ORIO. Je, Serikali ina majibu yapi sahihi ambayo yatawezesha miradi hii iweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nilikuwa nataka kufahamu uwiano wa miradi hii ya umeme vijijini. Yapo maeneo mengine ambayo sasa hivi yana asilimia mpaka 80, yamepata miradi hii, maeneo mangine bado hayajakuwa na fedha zinazopelekwa kwenye maeneo husika kama Jimbo la Mpanda Vijijini. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya mgawanyo wa fedha zinazofadhili Mradi wa Umeme Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge, kwamba mradi wa ORIO ni wa Uholanzi. Ni kweli kwamba sisi tulikuwa hatujalipa fedha, lakini sasa fedha zimelipwa na hiyo mitambo imetengenezewa Ubeligiji na itafungwa. Ndio maana engine nyingine ambazo zilikuwa Ngara na kwingine tutahamisha, kwa sababu engine zinakuja zimeshatoka na wanazifunga kule; kwa hiyo mradi huo utatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza juu ya uwiano, ni kweli napenda kukiri, kwanza Awamu ya Kwanza ya Umeme Vijijini, ilikuwa ni ya majaribio, ilifanyika ndani ya mkoa mmoja tu, Awamu ya Pili, tumejaribu kwenda nchi nzima. Lakini ukweli ni kwamba uwiano sio mzuri, na ndiyo maana Awamu ya Tatu tumekubaliana kwamba itabidi tufanye tathimini mkoa kwa mkoa, tuone mikoa ambayo imefaidika kwa kupata umeme Awamu ya Kwanza na ya Pili, safari hii watapata vijiji vichache kusudi vijiji ambavyo havijapata umeme vipewe kipaumbele.
Ninapenda kukiri kwamba mikoa ambayo kusema ukweli hawajapewa umeme sana ni mikoa ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na REA Awamu ya Tatu inaweka mkazo hapo
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi hasa ya WMA imekuwa ya muda mrefu katika nchi yetu. Jimboni kwangu vipo vijiji ambavyo vina migogoro ya WMA wakati vijiji hivyo ardhi hiyo ni mali yao, lakini kumekuwa na tatizo la wakulima kusumbuliwa, kufukuzwa, kuchomewa nyumba kwenye maeneo yao. Je, ni lini Serikali itakomesha tabia hii ya kuwachomea wananchi kwenye Vijiji husika vya Kabage, Sibwesa, Kapanga na eneo la Kagobole?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tukifanya rejea ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika majibu yake alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, alisema kwamba ni maeneo mbalimbali. Hata hivyo, katika suala la kutaka Wabunge kuuliza swali la nyongeza, Wajumbe wengi wamesimama kuonesha kwamba jambo hilo linagusa siyo sehemu ya Mheshimiwa Kakoso peke yake au sehemu ya Mheshimiwa Nkamia peke yake isipokuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tukifanya rejea, Waziri Mkuu alipokuwa akitembelea katika Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine katika Kanda ya Ziwa, alipofika kule Geita miongoni mwa matatizo yalikuwa ni ya wakulima na wafugaji hasa sehemu za hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu alitoa maelekezo katika Wizara ambazo kwa njia moja au nyingine zinashirikiana hasa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii hali kadhalika na TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, naomba, Mheshimiwa Kakoso, sitaki kuweka commitment hapa ambayo maelekezo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshayatoa ni kwamba, timu itaundwa kuangalia maeneo yote ya mgogoro na kuangalia mbinu gani ya kuweza kutatua case by case kutoka na hali halisi ya mgogoro husika.
Mheshimiwa Spika, jambo hili Mheshimiwa Kakoso tumelisikia kama Serikali, ni miongoni mwa maeneo ambayo yatajumuishwa kufanyiwa kazi kwa pamoja kuondoa migogoro hii katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naongezea majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni kweli kuna matatizo mengi sana katika WMAs nyingi, siyo hii tu anayotoka Mheshimiwa Kakoso. WMAs zimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria, ni maeneo ya hifadhi ambayo yanamilikiwa na wanavijiji, kandokando mwa hifadhi za Serikali, lakini WMAs hizi zimepewa mipaka na zimepewa majukumu na mamlaka ya kumiliki maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, nadhani Wilaya au kwa makusudi au kwa kutokujua wanaingilia mipaka hiyo. Kwa sababu wanaotakiwa kusimamia kuweka mipaka ya WMAs hizi ni Viongozi wa Wilaya. Sasa nitashangaa Viongozi wa Wilaya kuingia kuchoma! Hata hivyo, kinachotakiwa Mheshimiwa Kakoso hapa, kila WMA iweke matumizi bora ya ardhi katika eneo lake wanalomiliki ili ijulikane wazi sehemu ya kilimo ni ipi na sehemu ya mifugo ni ipi na mipaka hiyo na ramani hizo zinasajiliwa kwenye ngazi zote kuanzia Wilaya, Mikoa na Wizara ya Maliasili.
Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Kakoso arudi kule akaangalie je, mipaka hii ya WMAs imesajiliwa katika ngazi zote hizo na mipango ya matumizi bora ya ardhi imefanyika? Kwa sababu ikifanyika mipango ya matumizi bora ya ardhi na wanaofanya ni watalaam wa ardhi na viongozi wa Wilaya haitatokea hata siku moja kuwa na contradiction kati ya Viongozi wa Wilaya na WMAs.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, tumekusudia kama Serikali wote kwa pamoja, Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI, Maliasili na watumiaji wakubwa wa ardhi kilimo na mifugo, kukaa pamoja, kuainisha migogoro yote hii hata hiyo migogoro ambayo inasababishwa na hifadhi, wafugaji na wakulima ili kwa pamoja tukae tuweze kuitatua migogoro hii.
Mheshimiwa Spika, najua hapa wakisimama, kila mmoja ameguswa na migogoro kama hii. Kwa hiyo, ni kweli kwamba tumeamua kama Serikali tutakaa pamoja na nitaleta kwenye bajeti yangu sehemu ya migogoro kwa uchokozi, ambayo mmeshatuletea Waheshimiwa Wabunge, kama bado mingine ipo tutaendelea kujazilizia ili Wizara hizi zote zinazohusika tuweke utaratibu wa namna ya kupitia mgogoro mmoja baada ya mwingine ili tuweze kuitatua.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mpanda Vijijini ni jimbo ambalo lina kata 16, kati ya hizo tatu tu ndizo ambazo zina vituo vya afya. Napenda kumuuliza swali Naibu Waziri, ni lini itajenga vituo vya afya katika Kata ya Mnyagala, Kasekese, Mpanda Ndogo, Tongwe, Bulamata, Ilangu, Ipwaga na Katuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Jimbo la Mheshimiwa Kakoso lina tatizo kubwa sana na ukiangalia ni jimbo ambalo zamani lilikuwa likigawanyika na bahati mbaya resources zao zimekuwa ni changamoto kubwa. Siyo tatizo la zahanati tu lakini hata suala zima la ambulance wana tatizo, hilo nalifahamu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchakato wetu hivi sasa na Wabunge ni mashahidi, wafanye reference kutoka katika Halmashauri zao, tumetuma barua kutoka TAMISEMI kuwaelekeza wabainishe changamoto za miundombinu hasa katika zahanati na vituo vya afya na kuwapa maelekezo jinsi Serikali inavyojipanga katika mkakati mpana wa kutatua tatizo la afya hasa katika suala zima la ujenzi wa zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu kubwa ni kwamba Mkurugenzi wa Jimbo la Mheshimiwa Kakoso na Madiwani watakuwa wanafanya harakati hizo kubainisha ili Serikali iweze kujipanga kwa kuwa na mpango mpana wa kutatua tatizo la ukosefu wa vituo vya afya katika nchi yetu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso kwamba sasa hivi yuko Bungeni lakini waraka uko kule na watu wako site hivi sasa kubainisha changamoto hizo kwa ajili ya mpango mpana wa Serikali ili kutatua tatizo hilo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua barabara ya kutoka Mpanda kwenda Mkoa wa Kigoma ni barabara ambayo imeahidiwa na Serikali kujengwa kwa kiwango cha lami na tayari kuna kilomita 30 kutoka Mpanda Mjini mpaka eneo la Usimbili Vikonge, limeshafanyiwa upembuzi yakinifu. Swali kwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itaanza mchakato wa kuijenga barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie barabara hii tumeanza kuijenga kama ambavyo yeye ameisema na tutaendelea kuijenga hadi ikamilike kama viongozi wetu wa Kitaifa walivyoahidi na ilishaanza kujengwa. Kwa hiyo, suala itaanza lini sio sahihi, imeshaanza kujengwa na mwenyewe amezitaja kilomita ambazo tayari tumezijenga. Tutaendelea kujenga na tutaikamilisha kabla ya kipindi hiki cha miaka mitano haikijakwisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema ni kituo ambacho kimekamilishwa ujenzi na Serikali lakini tatizo kituo hicho hakina umeme ili kiweze kufanya kazi. Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kukamilisha kituo hicho ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Tarafa ya Karema?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Jimbo la Mpanda hadi sasa linapata umeme kwa kutumia mafuta kitu ambacho ni gharama kubwa sana. Hata hivyo, tumeshakaa na Mheshimiwa Kakoso, tumeainisha vijiji vyote vya Mpanda na Katavi, vijiji vyote vya eneo lake pamoja na hospitali na maeneo mengine yatapata umeme kuanzia Julai, 2016.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kuhudumia miradi ya maendeleo ya maji katika Kijiji cha Igagala na Kijiji cha Majalila ambacho ni Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Tanganyika. Serikali ilipotoa hizo fedha usimamizi wa mradi huu haukwenda sahihi. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia miradi ambayo tayari fedha ilikuwa imetengwa na wafanyakazi ambao ni wasimamizi wamesababisha hasara ya kutokukamilika kwa mradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya ziara Mkoa wa Katavi na mimi niliungana naye na hii miradi tuliitembelea na yale matatizo tukayakuta, kwamba miradi imeanza, miundombinu imejengwa lakini bado kuna matatizo madogo ya kuweka pump ili wananchi waendelee kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuta pia kweli kulikuwa na tatizo la kimikataba lakini tatizo hilo tayari nimeshaliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ili waweze kuwasiliana na Katibu Mkuu wa TAMISEMI kwa sababu Halmashauri ya Mji wa Mpanda ndiyo iliyosaini ule mkataba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili tayari tumeshalichukua tunalifanyia kazi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Namuuliza swali Naibu Waziri, alipokuja Mpanda alituhakikishia wananchi wanaoishi vijiji vya Kabungu, Mchakamchaka, Ifukutwa na Majalila ambako ni Makao Makuu ya Wilaya kwamba ataleta umeme ifikapo mwezi wa tisa. Je, ni lini Serikali itathibitisha kauli yake ambayo aliitoa yeye mwenyewe alipofika huko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nilitembelea maeneo mengi sana katika Jimbo la Mheshimiwa Kakoso na hasa kabla ya kutaja maeneo ya Majalila, Mheshimiwa Kakoso kwanza nikuhakikishie Gereza lako la Kakalankurukuru ambalo lina miaka 37 halina umeme litapatiwa umeme mwezi ujao kupitia Mradi wa REA unaoanza mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea pia Kata ya Majalila ambako kuna mitambo na miradi ya maji. Nikuhakikishie Mheshimiwa Kakoso, mradi wa REA utakapoanza kufikia mwezi Januari hadi Februari mwaka unaokuja mradi wako wa Majalila utafungiwa jenereta za umeme, lakini pia jenereta ya umeme itaunganishwa na umeme ambao sasa unapitia mradi wa REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Kabungu nilikitembelea pamoja na Mpanda Mji Mpya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kakoso nikuhakikishie, vijiji vyako vyote 32 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA kuanzia Disemba na Januari mwaka unaokuja.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na kwa kiwango kidogo kitakachozalishwa mwaka huu:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la ukosefu wa classifiers ambao wanafanya msimu wa zao kuwa mrefu sana? Ni lini Serikali itakuja na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuajiri classifiers ambao watasaidia kutatua tatizo la tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Wizara na Serikali inatambua changamoto iliyopo kwa sababu kuna upungufu wa classifiers. Bodi ya Tumbaku iko katika hatua za kuhakikisha kwamba, changamoto hiyo inaondoka na tunaamini kwamba, kwa kiasi kikubwa tunapoelekea kwenye msimu mwingine wa tumbaku tatizo la classifiers halitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wafahamu kwamba, ili kuweza kupata bei nzuri ya tumbaku na kuweza kuuza tumbaku nyingi zaidi ni lazima vile vile tumbaku yetu tufanye iweze kushindana. Kwa sasa tumbaku yetu inakabiliwa na changamoto kubwa. Imekuwa ni vigumu sana kuwapata wanunuzi kwa sababu hatutunzi mazingira na vile vile kwenye kilimo cha tumbaku tunatumia watoto kitu ambacho hakitakiwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiwa na tumbaku nzuri namna gani, ni lazima vilevile uangalie mazingira ambayo umezalisha. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba, tunapanda miti, tunafuata masharti yote, lakini vilevile watoto wasifanye kazi kwenye mashamba ya tumbaku.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wakati Jumuiya inaanzishwa maeneo haya yalikuwa na kijiji kimoja tu cha Sibwesa, lakini leo hii kuna vijiji zaidi ya sita na kata mbili zimeanzishwa kwenye maeneo hayo na Serikali inatambua maeneo hayo ya kiutawala. Je, ni lini Serikali kupitia Wizara wataenda ku-review mipaka hiyo ambayo ipo inayoleta migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo hayo ili kuondoa shida inayosababisha wananchi kupigwa mara kwa mara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati Jumuiya inaanzishwa ilikuwa na malengo mazuri ya kiuchumi ambayo kwa sasa hayapo na wananchi hawajanufaika na mradi wowote ule ulioanzisha Jumuiya hiyo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaachia hayo maeneo ili yaendelezwe na vijiji vyenyewe husika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza kimsingi anakubaliana na hoja ya jibu la msingi kwamba tangu wazo la kuanzishwa kwa WMA lilipotolewa hadi leo mabadiliko mengi yametokea ikiwemo kuongezeka na kubadilika kwa maeneo ya utawala. Ameuliza swali ni lini Serikali itaenda kushughulikia mabadiliko hayo na kuweza kupima umuhimu wa kuendelea na wazo la WMA?
Mheshimiwa Spika, jibu langu ni kwamba mara tu baada ya kukamilika kwa kikao hiki kinachoendelea cha wiki mbili mimi na Mheshimiwa Mbunge tutapanga ratiba vizuri kwa sababu nadhani tukienda pamoja mimi na yeye tutafanya jambo ambalo ni la tija zaidi.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anasema hapo zamani eneo hili ni kweli lilikuwa linaonekana lina faida za kiuchumi na kijamii lakini kwa maoni yake anasema kwamba hali hiyo imebadilika kwa hivyo hivi sasa anadhani kwamba kuna haja ya Serikali kupitia upya mawazo au maamuzi hayo.
Mheshimiwa Spika, jibu ni kama lilivyo kwenye majibu ya msingi aya ya mwisho kabisa kwamba sasa Serikali tutakwenda kwanza kutoa ushauri lakini pia kushirikisha wataalam wa eneo hili ili tuweze kwa pamoja sasa kupima hicho ambacho tunasema kwamba zamani kilikuwepo lakini sasa hakipo. Mimi naamini tukienda wote tukakaa pamoja na kukagua maeneo yanayohusika tunaweza tukafikia muafaka. Ahsante sana.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya maji ya Tabora ni sawa sawa na matatizo ya maji ya Mkoa wa Kagera hasa Bukoba Mjini. Kwa sasa hivi ukame umechukua muda mrefu mito mingi imekauka. Je, ni lini Serikali itatuweka kwenye Mpango wa Ziwa Victoria angalau hizi kata zilizoko karibu na Bukoba Mjini zipate maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anazungumza kuhusu maji ya Ziwa Victoria kupelekwa Kata za Mjini Bukoba. Hivi sasa Serikali imejenga mradi mkubwa sana wa kutoa maji Ziwa Victoria kusambaza katika Mji wa Bukoba. Tatizo lililopo tu ni kwamba baadhi ya maeneo yako juu. Kwa hiyo, Serikali itaweka pump za kuweza kupandisha maji zaidi kwenye yale maeneo ambayo yako juu kuliko yale ya chini ili tuweze kuona kwamba wananchi wetu wa Manispaa ya Bukoba watapata maji ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kazi ambayo inaendelea na kila mwaka tumeweka fedha kila Halmashauri na tumetoa mwongozo kwamba kwa kulingana na fedha ambazo zipo tumetenga kwenye Bajeti yetu kila halmashauri ianze kufanya manunuzi ili kusudi maeneo yale ambayo hayakuwa yamefikiwa maji yaweze kufikiwa maji kulingana na malengo ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunataka maeneo yote ya mijini tufikishe maji kwa 95% ikifika mwaka 2020; kwa hiyo Wabunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani, tuwe karibu sana katika mipango ya maendeleo ya sekta maji kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Ziwa Tanganyika ni eneo ambalo kumefanyika utafiti wa gesi na mafuta hasa kwenye Tarafa ya Karema. Eneo hilo kuna uhakika wa kupatikana mafuta na gesi, je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mkoa wa Katavi na ukanda mzima wa Ziwa
Tanganyika juu ya utafiti ambao umefanywa mpaka sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa utafiti umeshaanza kufanyika katika Ziwa Tanganyika ili kugundua gesi iliyopo na makampuni yaliyopita kufanya ni makampuni mawili ya Chuo Kikuu cha Ujerumani pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanajiolojia wa Tanzania pamoja na TPDC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa ni
kuanza kufanya appraisal ili kujiridhisha na gesi iliyopatikana. Zipo dalili za kugundua lakini kinachofanyika sasa niappraisal na shughuli ya kukamilisha appraisal itafanyika mwezi Agosti
mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo baada ya Agosti mwaka huu Mheshimiwa Kakoso wananchi wanaozunguka Ziwa Tanganyika wataanza kupata gesi asilia katika maeneo hayo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi kuna miradi ya umwagiliaji ambayo imeanzishwa na Serikali na imetumia fedha nyingi sana. Miradi hiyo ni mradi wa Karema, Kabage na Mwamkulu. Miradi hii ya Serikali imetolewa fedha nyingi, bahati mbaya sana Serikali inapoanzisha haiwezi kuikamilisha hiyo miradi. Nilikuwa nataka kujua ni lini Serikali itakamilisha hiyo miradi ya Karema, Kabage na Mwamkulu ili iweze kuwanufaisha wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ilianza, ni kweli ilichelewa kukamilishwa lakini sasa hivi tumeandaa timu ambayo inakwenda kupitia ili kuainisha changamoto ambazo zimefanya isikalimike ili tuweze kutoa fedha tuhakikishe kwamba miradi hiyo yote mitatu Karema, Kabage na Mwamkulu inakamilika.
Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tayari, na mimi mwenyewe nimeshakwenda kutembelea Mradi mmojawapo pale na huo mradi sasa hivi tayari kazi inaendelea mkandarasi amerudi site ili kuhakikisha kwamba miradi yote hii inakamilika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa taratibu zote za kuipandisha hadhi barabara hii zilishafanyika ikiwemo kupitia vikao halali vya Wilaya na Mkoa na kikao cha Road Board mimi mwenyewe nilishiriki tukaipitisha hii barabara. Nilikuwa nataka kuuliza ni sababu ipi inayokwamisha kutokupandishwa hadhi kwa barabara hii?
Pili, kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati anaanza safari ya ushindi ya kuomba ridhaa ya wananchi, ziara yake ya kwanza aliifanya Mkoa wa Katavi na kituo cha kwanza alianzia maeneo ya Mishamo aliwaahidi wananchi wa Mishamo kuwaboreshea barabara hiyo ya kutoka Mishamo mpaka Ziwa Tanganyika kwenye jimbo la Mheshimiwa Hasna Mwilima.
Je, hawaoni sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, ambayo aliwaahidi wananchi wa Mishamo ili kutekeleza ahadi iliyokuwa ameiahidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukurusana Mheshimiwa Moshi Kakoso kwa sababu itabidi nikapate ukweli ama mkoa haujawasilisha Wizarani ama pale Wizarani pana uzembe. Kwa hiyo, nitakwenda niangalie na nifuatilie hili suala kama kikao halali kilishakaa kwa nini Wizarani hatujapata hayo maombi.
Kwa hiyo, baada ya hapo nikishajua wether kuna tatizo Mkoani inawezekana walikaa lakini hawakuwasilisha au pengine pale Wizarani kuna tatizo.Nitakapopata jibu mtaona matokeo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Mishamo kwenda mpaka Baharini ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, wakati wa kampeni tumeipata tunayo katika orodha ya ahadi tulizonazo, nikuhakikishie kwamba tunakwenda awamu kwa awamu katika kutekeleza ahadi zote ambazo tuliziahidi katika kipindi hiki cha miaka mitano. Tutahakikisha ahadi hiyo nayo tutaitekeleza.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa magereza mengi nchini yamekuwa chakavu likiwemo Gereza la Kalilamkurukuru lililopo Wilaya ya Tanganyika. Nini mkakati wa Serikali kuimarisha magereza haya kwa kuyafanyia ukarabati sambasamba na nyumba za askari?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Kakoso kwa swali lake zuri la nyongeza. Niseme tu kwamba tuna mikakati ya aina mbili, kwa upande wa nyumba za askari kama nilivyoelezea wakati wa bajeti tunaenda hatua kwa hatua, tuna miradi midogo na mikubwa ambayo tunaitekeleza. Kwenye ukarabati sambasamba na upande wa ujenzi wa nyumba tumekubaliana kutumia bajeti inayotengwa lakini pamoja na nguvukazi tunayoipata kutokana na wajuzi tulionao kwa upande wa askari, lakini wajuzi tulionao kwa wale walioko magerezani ili tuunganishe nguvu zote hizo na bajeti inayopatikana tuweze kufanya marekebisho pamoja na ujenzi wa makazi mapya pamoja na mabweni kwa ajili ya wafungwa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza. Serikali iliazimia kufanya marekebisho ya kuziboresha bandari za Maziwa Makuu kwa maana ya Ziwa Victoria, Nyasa na Lake Tanganyika. Serikali iliazimia kujenga bandari ya Kalema ili iweze kuunganisha na nchi jirani ya DRC. Ni lini bandari ya Kalema itakamilika kama Serikali ilivyokuwa imetoa hoja ya kujenga bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kakos, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya bandari za Mwambao wa Ziwa Tanganyika. Amekuwa mstari wa mbele sana katika kulihangaikia hilo na sisi tunamuunga mkono katika hilo, tutahakikisha dhamira yake ya kuwatumikia watu wa Mwambao wa Ziwa Tanganyika inatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba kazi inayofanyika sasa ni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa reli na bandari, reli kutoka Kaliua mpaka Kalema pamoja na bandari yake ili hatimaye tujenge reli na bandari tuweze kuhudumia mizigo mingi kutoka Kalemie upande wenzetu wa DRC Kongo. Nimwombe akubali kwamba yale ambayo tunakubaliana katika Kamati ndiyo Serikali itakayoyatekeleza. Ahsanteni sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Wilaya mpya nyingi hazina Hospitali za Wilaya ikiwemo na Wilaya yangu ya Tanganyika; ni nini mkakati wa Serikali wa kuweza kujenga hospitali sambamba na kuimarisha vituo vya afya wakati inajipanga kujenga hospitali hizo za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Moshi pale kwake wanahudumiwa na Hospitali ya Halmashauri ya Mpanda iko Mpanda Mjini na Makao Makuu ya Wilaya ya Tanganyika Majarila na eneo lingine lote mpaka unaenda ziwani, wananchi wanapata shida kubwa sana. Mheshimiwa Mbunge unakumbuka tulivyokuwa Jimboni kwako tumeenda mpaka katika Makao Makuu ya Halmashauri yako ambayo inatarajiwa kujengwa hivi sasa na miongoni mwa jambo ulilolipendekeza ni kwamba tufanye utaratibu wa kuboresha kile kituo cha afya cha Majarila.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba, Serikali sasa imetenga takribani shilingi milioni 700 kupeleka katika eneo lako, lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi wako ambao wanachangamoto kubwa ya kiafya. Serikali imesikia sana kilio cha wananchi wa Tanganyika na Serikali iko tayari nadhani katika kipindi hiki kuanzia mwezi huu wa Mei mpaka tutakapofika mwezi wa Julai ni imani yangu kubwa tutapeleka nguvu kubwa sana kujenga theatre na kuweka vifaa vyote vya wazazi ili tupunguze vifo vya mama na watoto tuweze kuvipunguza katika eneo lako. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa wilaya mpya ambazo hazina huduma ya hospitali ya wilaya. Kwa nyakati tofauti, Serikali imekuwa ikiahidi Kituo cha Afya kijiji cha Majalila ambako ni Makao Makuu ya Wilaya. Nilikuwa nataka kujua kauli ya Serikali, je, Kituo kile cha Majalila, ni lini kitaanza kupewa fedha na hatimaye kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Wilaya ya Tanganyika imegawanyika kutoka Mpanda na mimi Mbunge nafahamu tulifika pale kwake ni kweli kuna tatizo kubwa sana. Kwa mfano wananchi wanaotoka Mwese wakija Mpanda Mjini ni tatizo na tulifika pale Majalila ambapo Makao Makuu ya Wilaya ile inataka ijengwe, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya Halmashauri yako ya Wilaya. Juzi nilikuwa naongea na Mkurugenzi wako wa Mpanda DC kuangalia jinsi gani tutafanya.
Kwa hiyo, kuna shilingi milioni 500 tunawaletea na hii sisi tunasema kama ni kingiambago tu, ni fedha ya kwanza tutatoa fedha nyingine kwa ajili ya kununua vifaa ambayo jumla yake itakuwa karibuni shilingi milioni 720. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie wananchi wa Tanganyika hili ni jukumu la Serikali kuwafikia watu wote hata ndugu yangu wa Kakonko tulifanya jambo hili kwa sababu siku ile tuliyofika shida ilikuwa kubwa. Hii ni kazi ya Serikali na itafanya kazi kila mahali kwa manufaa ya wananchi wake wa Tanzania.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali, kwa kuwa wananchi wa Bukene wamepata fursa nzuri ya kupata umeme na wananchi wa Bukene wamejipanga katika shughuli nzima ya ujasiriamali na tatizo kubwa wao wana ukosefu wa mitaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wananchi wa Bukene ili waweze kupata mitaji na waweze kuanza shughuli za ujasiriamali?
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi una fursa nyingi za uwekezaji na vivutio vya kutosha hasa kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na eneo la maliasili. Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara wana mpango upi wa kusaidia Mkoa huu ili kuweza kupatiwa wawekezaji waje kuwekeza katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, la kwanza katika suala la mitaji, nipende tu kuwahamasisha wananchi wote wakiwemo wananchi wa Bukene kwamba mtaji wa kwanza ni mtu kuamua kufanya shughuli ya uzalishaji, mtaji wa pili ni huo wa kupata taarifa na mafunzo, lakini vilevile kufuatilia taasisi kama za benki na kwa upande wetu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia SIDO kama nilivyosema awali, tunao mfuko ambao unawezesha wajasiriamali pale ambapo wapo serious katika kufanya shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Katavi niwaombe kupitia Serikali ya Mkoa na Halmashauri na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhamasisha fursa zilizopo katika Mkoa wa Katavi ili wawekezaji wengi wa ndani na wan je waweze kupenda kuwekeza katika Mkoa huo. Kwa siku za nyuma mmekuwa mkifanya makongamano mbalimbali ya kukaribisha wawekezaji, nashauri muendelee kufanya hivyo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mkoa wa Katavi ni kimbilio la wananchi wengi ambao wamekosa ardhi ya kilimo na wakati huohuo ardhi iliyopo Mkoa wa Katavi asilimia themanini imemilikiwa na misitu ya Serikali kiasi kwamba wananchi walio wengi wamekosa kupata nafasi ya kufanya shughuli zao za kiuchumi kupitia sekta ya kilimo hasa katika kata za Sibwesa, Kasekese, Katuma, Bulamata ambako kuna migogoro mingi ya ardhi. Je, Serikali imejipanga vipi kutatua kero ya ukosefu wa ardhi ili wananchi waweze kuitumia ipasavyo kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyozungumza katika Mkoa wa Katavi sehemu kubwa ya ardhi ni misitu na maeneo ya hifadhi. Ni lengo la Serikali kuendeleza maeneo hayo katika msingi wa kuendeleza misitu na hifadhi kwa ajili ya ustawi wa mazingira lakini vilevile kwa ajili ya kuendeleza ile hali nzuri ya hewa ikiwemo mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba katika halmashauri na vijiji vyote tuendelee kuhakikisha kwamba kila kijiji kinakuwa na mpango ardhi wa eneo lake ambao unaainisha maeneo ya kulima, maeneo ya kuishi kama kijiji, maeneo ya mifugo na malisho ili kusudi tuwe na mipango endelevu ya maisha yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndilo jibu langu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto nyingi sana za Mikoa mipya na Wilaya mpya ambazo nyingi hazina Hospitali za Wilaya. Nini kauli ya Serikali ikiwemo wilaya ya kwangu ya Tanganyika ambayo haina Hospitali ya Wilaya. Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la ukosefu wa Hospitali za Wilaya katika maeneo yote nchini ambayo hayana Hospitali za Wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba afya kwa wananchi wa Tanzania kama ilivyo kipaumbele na ndiyo maana bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 269. Hii inaonesha jinsi ambavyo Serikali itahakikisha kwamba huduma hii inawafikia wananchi na kwa kuwepo Hospitali za Wilaya maeneo yote ambayo Hospitali za Wilaya hazipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizitake halmashauri zote zianze kwa kutenga maeneo lakini pia kwa kutumia own source na wao waanza ili Serikali iweze kuunga mkono jitihada hizo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao bado hauna chanzo kizuri cha maji; Mkoa wa Katavi umepakana na Ziwa Tanganyika. Je, Serikali ina mpango gani kuweza kuyatoa maji Ziwa Tanganyika na kuyaleta Makao Makuu ya Mkoa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kutumia maji ya Ziwa ya Tanganyika kupeleka Mkoa wa Katavi, tayari andiko limeshaandikwa na limeletwa. Wizara tunafanyia kazi na mwaka ujao wa fedha tutaweka mshauri ili aanze kufanya kazi na baadaye tuongeze fedha kwa ajili ya kuchukua maji kutoka Kalema kuyaleta Mji wa Mpanda kupitia Jimbo lake. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na vyumba na uhaba wa nyumba za walimu limekuwa tatizo kubwa sana na Jimbo langu ni miongoni mwa matatizo ambayo yanawakabili katika shule ya Busongola, Bulamata, Vikonge, Mchangani, Kapanga na Kafishe ambako kuna vyumba viwili tu vya madarasa lakini zipo darasa saba. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na uhaba wa nyumba za walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu wangu Mheshimiwa Kandege kwa clarification nzuri kwa maswali yote yaliotangulia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto kubwa sana ya vyumba vya madarasa na ndio maana kwa Serikali kipindi hiki cha sasa tulifanya tulitumia takribani shilingi bilioni 21 kuhakikisha tunaongeza vyumba vya madarasa katika shule za sekondari 85 na shule za msingi 19. Lakini hata hivyo kipindi cha muda mfupi uliopita tumetumia takribani shilingi bilioni 16 kufanya uwezeshaji mkubwa katika shule za sekondari 65 na shule za msingi 56 lakini hata hivyo naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika fedha tulizozitenga takribani shiling bilioni 246 kwa ajili ya kusaidia kwamba yale maboma yaliyojengwa kuhakikisha tunayakamilisha naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tushirikiane vya kutosha na wizara ya fedha, fedha ziweze kutoka ziende katika halmashauri zetu kwa lengo la kumalizia viporo na kujenga maeneo mengine lengo kubwa wanafunzi wetu wapate mahali pa zuri pa kusomea.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi hii, kwa kuwa Kituo cha Afya cha Mwese ni cha muda mrefu sana, kina zaidi ya miaka 40 hakijafanyiwa ukarabati wa aina yoyote na Serikali iliahidi kukikarabati kituo hicho. Je, Serikali ni lini itapeleka fedha kwa ajili ya kituo hicho ili kiweze kuwasaidia wananchi wa Kata hiyo ya Mwese?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya Mwese ambacho ni cha muda mrefu, je, ni lini Serikali itakuwa tayari kutenga pesa ili kufanya ukarabati?
Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana kwamba ni kiu ya Waheshimiwa Wabunge wengi wangependa vituo vya afya viweze kukarabatiwa, na ndiyo maana Serikali kwa kujua umuhimu huo tumeanza na vituo vya afya 205, si haba. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira awamu kwa awamu na kwa kasi tunayoenda nayo naamini muda si mrefu na kituo cha afya cha kwake kitapata fedha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Vituo vya Afya vya Mwese, Karema na Mishamo ni vituo ambavyo vinahudumia wananchi wengi kwenye Jimbo la Mpanda Vijijini. Vituo hivi havina huduma ya kimsingi ya wataalam na hasa suala zima la ambulance. Naomba kujua, Mheshimiwa Naibu Waziri atavisaidia vipi hivi vituo vya afya ambavyo vinahitaji huduma ya Serikali ili kuokoa maisha ya wananchi kwenye Jimbo hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba yako mahitaji ambayo hayatoshelezi katika vituo vyetu vya afya na hospitali zetu, lakini hospitali hizi zipo kwenye Halmashauri na Halmashauri ndizo hupanga bajeti zake za kila mwaka.
Sasa nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, sehemu ya kuanzia katika kukamilisha huduma mbalimbali katika Sekta ya Afya, iwe ya elimu, mipango yote inaanzia kwenye Halmashauri. Kama watakuwa waliweka kwenye bajeti zao, basi wanaweza wakapata hizo ambulance na vifaa ambavyo pengine vina upungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kwa sasa hatuna mpango mahsusi wa kununua magari ya ambulance kwa nchi nzima kwa sababu, upungufu ni mkubwa, isipokuwa tunaangalia kutokana na bajeti zao za Halmashauri na sisi Serikali kwa fedha iliyopitishwa tutakuwa tumewatengea na kuwapatia fedha hizo kwa kadiri walivyoomba katika bajeti zao.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa jitihada ambazo zimefanywa, barabara ile imeanza kujengwa, lakini Serikali iliahidi barabara hiyo inapojengwa ingejengwa sambamba na kilometa 60 za kutoka Uvinza kuja eneo la Mishamo ili ziweze kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais na vile vile Ilani ya Chama cha mapinduzi. Je, ni lini eneo hilo la kipande cha kilometa 60 kutoka Uvinza kuja Mishamo kitaanza kujengwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa ujenzi wa barabara ulishaanza, tayari Serikali imetathmini wale ambao wamefuatwa na barabara. Ni lini wale ambao walioathirika kwa kufuatwa na barabara wataanza kulipwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliahidi kwamba tungejenga kuanzia Uvinza na vile vile kuanzia huku ambako tumeanzia na nimuahidi tu kwamba, madam tumeanza kupata hizi fedha kwa ajili ya upande mmoja, tumeona tuanze hii wakati tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ule upande wa pili. Nimhakikishie mara tu tutakapozipata fedha tutatekeleza ahadi tuliyoitoa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu watu ambao wameifuata barabara; nimhakikishie tu Mheshimiwa Selemani Kakoso na wananchi husika kwamba watu wote walioifuata barabara hawatalipwa fidia na wale wote ambao barabara imewafuata watalipwa fidia; na taratibu za kuwatambua zilishafanyika na nimhakikishie kwamba hilo tutalitekeleza.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma ni Mikoa ambayo haijafaidika na miradi ya REA Awamu ya Tatu kwa sababu ya walioomba tenda kugombania tenda na kushtakiana Mahakamani. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ili wananchi wa Mikoa hiyo waweze kupata huduma ya REA awamu ya tatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Kakoso kwa swali lake zuri. Nichukue fursa hii kuwapa pole na kuwaomba radhi wananchi wa Mikoa ya Kigoma na Katavi, lakini ameuliza Serikali ina mpango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimtaarifu suala hili lipo Mahakamani. Kwa kuwa, Mahakama ni chombo pekee ambacho kinatoa haki, sisi kama Serikali ya Awamu ya Tano tutasikiliza maamuzi ya Mahakama, kwa hiyo mgogoro huu utatatuliwa na Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie kwa kuwa, Mamlaka ya Manunuzi (PPRA) hawakuwa na kipingamizi katika suala la mchakato, Wakala wetu wa Nishati Umeme Vijijini (REA) wameanza mchakato wa kumpata mkandarasi mpya, lakini kama yatatokea maamuzi mengine ya Mahakama tutaendelea kuyaheshimu, lakini kwa mpango ndani ya Wizara tunaamini kuanzia Machi 2018 Mkandarasi mpya atapatikana. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa majibu ya Serikali ambayo yana matumaini ya ujenzi ya Hospitali ya Wilaya.
Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali iliahidi na mipango yake inachukua muda mrefu, je, Serikali ina mpango gani wakati inajipanga kuweza kukiboresha kituo cha afya cha Hamai ili kiweze kutoa huduma nzuri sambamba na kuchimba kisima ambacho ni tatizo kwenye eneo la kituo hicho cha afya?
Swali la pili, kwa kuwa matatizo ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ni sawa na tatizo lililoko kwenye Wilaya ya Tanganyika na Naibu Waziri analifahamu hili. Serikali iliahidi kujenga kituo cha afya Majalila. Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kujenga kituo hicho cha Majalila?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Halmashauri ya Chemba tunao huu mpango wa kuhakikisha tunajenga Hospitali ya Wilaya. Kwa vile changamoto ya Jimbo la Chemba ni kubwa ndiyo maana Serikali katika mpango wake wa kuboresha vile vituo vya afya 100, kituo cha afya cha Hamai ni miongoni mwa vituo vya afya ambacho tunaenda kukiwekea ufanisi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ambapo imani yangu ni kwamba si muda mrefu mchakato huo utaanza.
Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba kwa wananchi wa Chemba na hili tumeshaongea na Mheshimiwa Nkamia kwamba tutafanya kila liwezekanalo katika kipindi kifupi kijacho tutaenda kukiboresha kile kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la Wilaya ya Tanganyika Mheshimiwa Mbunge unafahamu tulikuwa wote Tanganyika nilivyokuja Jimboni kwako. Tulitembelea Makao Makuu yako na Wilaya yako ya Tanganyika ambayo ni mpya, ndiyo maana tumepanga katika mpango wa kuboresha Wilaya hii katika eneo la Majalila kile kituo cha afya ambacho kinasuasua sana tutamekiingiza katika mpango wa vituo vya afya 100.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishe kwamba wananchi wa Tanganyika wawe na imani kwamba Serikali inaenda kufanya investment kubwa eneo lile ili wananchi wa Tanganyika wapate huduma nzuri za afya.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Niulize sasa maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa msimamizi wa mradi huu aliyejenga mradi wa maji wa Kijiji cha Ngomalusambo alijenga chini ya kiwango, ikiwa ni pamoja na kufunga pampu ya kusukuma maji ambayo haina uwezo na haikuwa stahili iliyokuwa imelengwa. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Mkandarasi na Msimamizi aliyejenga mradi huu chini ya kiwango na kuipotezea Serikali kiasi kikubwa cha fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi mingi ya maji imekuwa na tatizo ya usimamizi mbovu kiasi kwamba miradi inayoelekezwa haitengenezwi vizuri. Mfano pale Kijiji cha Majalila kulikuwa na mradi mkubwa wa maji ambao Serikali imetoa fedha nyingi lakini ilipangiwa kujengewa vituo vya maji 28 vikajengwa 12. Je, msimamizi wa mradi huu wanachukua hatua gani ili aweze kuwajibishwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi wa Ngomalusambo kwamba imefungwa mashine ambayo iko chini ya kiwango siwezi kulizungumza hapa sasa, lakini kwa taarifa nilizozipata ni kwamba ule mradi ulianza lakini charging capacity yake kile kisima imekuwa kidogo, kwamba pampu inafungwa lakini ikisukuma maji sasa hivi wanasukuma takribani masaa 18 wanavyotumia diesel maana yake gharama inakuwa kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni taarifa ambazo nilizipata kwa wataalam wangu. Hata hivyo, concern aliyozungumza Mheshimiwa Mbunge naomba tuifanyie kazi, kwenda kufanya uchunguzi je, ni kweli kisima kimepoteza uwezo au pampu iliyofungwa haina uwezo. Maana yake mpango uliopo sasa hivi katika Halmashauri ya Mpanda ni kwenda kuchimba kingine kuhamisha ile mitambo iendelee kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Mbunge anasema pampu iliyofungwa haina uwezo basi hili maana yake ni jambo kubwa sana lazima tukalifanyie kazi na ikiwezekana tuunde Tume maalum kwenda kuchunguza kwamba kipi kinachojili katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika katika mradi wa Majalila na Mbunge anakumbuka siku ile tulivyofika pale tulikuta ule mradi upo idle pale katika Wilaya Tanganyika haufanyi kazi. Nikatoa maelekezo na nimepata taarifa mradi ule umeshaanza kufanya kazi, lakini inaonekana kwamba kuna changa la macho, badala ya vituo vya maji 24 vimefungwa 12 maana yake hapo kuna tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa matatizo hayo yote, kama hali ipo hivyo, Ofisi ya TAMISEMI hatuwezi kuridhika na hali hiyo. Naomba nimhakikishie tutaunda Tume maalum kutoka ofisini kwangu kwenda kufanya uchunguzi wa miradi hiyo miwili, lakini siyo hiyo miradi miwili na ile miradi mingine minne inayoendelea, kuweza kubaini kwamba ni tatizo gani linaendelea lengo kubwa tuweze kulinda fedha za Serikali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilio cha Mheshimiwa Mbunge kimesikika, tunaenda kukifanyia kazi kama tulivyofanya kazi Mkoa wa Geita na maeneo mengine.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi na mikoa mingine ambayo imekuwa inapokea wakimbizi ni mikoa ambayo iliathirika sana kiuchumi kwa sababu nguvu yao kubwa sana ilipelekea kubeba mzigo wa wakimbizi kutoka nchi jirani na kupelekea kuwa na umasikini kwenye maeneo hayo.
Je, Serikali imejipanga vipi kusaidia maeneo ambayo yalitoa nguvu zao kubwa sana kusaidia ndugu zetu wa nchi za jirani na hali ya maisha sasa ya wananchi ambao walifanya kazi ya kuwapokea ndugu zetu wamekuwa na mazingira ya maisha duni?
Tunaomba Serikali itupe majibu, inatusaidia vipi katika mikoa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwa Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi nao ni hivyo hivyo. Tumeweka vipaumbele hasa kuhakikisha tunafungua mikoa hii kwa miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Mheshimiwa Mbunge ni shahidi kwamba miundombinu inafunguka ili wakulima wetu waweze kusafirisha mazao yao kwa haraka na nguvu zote kama Serikali tunaelekeza kwenye mikoa hii iliyoonyeshwa kwenye utafiti ule kwamba ni ya mwisho katika hali ya umasikini ndani ya Taifa letu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Katavi unazalisha mazao ya kilimo ya biashara na chakula, nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wakulima hawa ambao wamejitolea, wanafanya kazi kwa bidii lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa masoko kwa mazao wanayozalisha? Nataka kupata…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mazao ya chakula na mazao yale ya kimkakati ya biashara sisi tumesema kama Serikali hatufanyi biashara, kazi yetu ni ku-regulate na ku-control. Isipokuwa kama Serikali, sisi kuanzia sasa tunatoa vibali ili wakulima wote wawe na uhuru wa kuweza kuuza bidhaa zao zote au mazao yao yote nje ya nchi lakini kwa kuhakikisha kwamba pia kama Serikali tuna chakula cha kutosha ndani ya nchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi hii. Eneo la Mishamo ni eneo ambalo liliishi wakimbizi na sasa hivi ni Watanzania wapya ambao wamepewa uraia na Serikali. Eneo hili kupitia Shirika la UNHCR lilichimba visima karibu vijiji 16, vijiji hivyo kwa sasa havina maji kwani visima hivyo vilishaharibika. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kufufua visima hivyo ambavyo kimsingi vikifufuliwa na Serikali vitatatua kero ya maji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake lakini kwa namna bora ya kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Maji tumekuwa na taratibu ya kufufua visima vyote ambavyo vimekufa kwa kuvirudisha katika hali yake ili wananchi waweze kupata maji. Nipo tayari kuongozana naye kwenda kuona hali halisi ili mwisho wa siku tupange namna gani tunaweza tukavifufua visima vile ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya ambayo haina Mahakama ya Wilaya, sambamba na Mahakama za Mwanzo ni zile ambazo zimechakaa na hazina watumishi wa kuzifanyia kazi hizo Mahakama. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa Mahakama za Mwanzo sambamba na Mahakama ya Wilaya na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Tanganyika itajengwa mwaka 2019/2020 na kama nilivyosema fedha imepatikana kwa hiyo tuna uhakika kwamba Mahakama hiyo itajengwa kwa kipindi hicho huko Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi wa Mahakama, ningependa kusema kwamba upo upungufu wa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo 3,000 kwa sababu sasa hivi wako watumishi 6,000 na wanahitajika watumishi wengine 3,000. Wizara inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupata vibali vya ajira. Mara vibali hivyo vitakapopatikana miongoni mwa Mahakama ambazo zitapewa kipaumbele ni Mahakama za Mwanzo naamini pia zitagusa Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kunipa nafasi hii, nishukuru majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatia matumaini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijiji 16 ambavyo vipo katika eneo la Mishamo ni vya muda mrefu na miundombinu yake ilishakuwa chakavu. Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kupeleka miradi mikubwa ambayo itawasaidia hawa wananchi kupata maji yenye uhakika?
Swali la pili, ipo Miradi ya Maji ya Mwese, Kabungu, Kamjera yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4 na tayari wakandarasi walishafanya kazi kwa kuanza na fedha zao; je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizi ili waweze kukamilisha hiyo miradi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali kwanza ni kujenga miundombinu mikubwa kwa ajili ya maji ili yaweze kuwafikia wananchi mbalimbali na katika hivyo vijiji 16 vya Mishamo ambavyo amevisema Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha kwamba tunajenga miundombinu mikubwa ambayo itaweza kuwafikia wananchi wote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Mheshimiwa Kakoso tunazo takribani kandarasi tano. Tuna makandarasi watano ambao wanafanya kazi na kazi hiyo ina gharama takribani ya shilingi bilioni 2.78. Mpaka sasa hivi makandarasi wawili bado hawaja-rise certificate yoyote, mkandarasi mmoja tumeshamlipa advance payment na makandarasi wawili ambao ni Dar Huduma na DDSA tayari wameleta certificate na hivi sasa tunaendelea na kuzichambua ili tuweze kuwalipa makandarasi hao.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Tanganyika ni ziwa ambalo lina kina kirefu na kufanya wavuvi wanaovua kwenye ziwa hilo kuwa na uvuvi wa kubahatisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wavuvi wa eneo la ziwa Tanganyika wavuvi wa Kasanga, Kirando, Karema, Ikola na Kalia na eneo zima la Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwanza nimpongeze Mheshimiwa Moshi Kakoso kwa ufuatiliaji wake wa hali ya juu ya tasnia hii ya wavuvi na maendeleo ya wavuvi wa kule ziwa Tanganyika.
Kwa upande wa namna ambavyo Wizara tulivyojipanga kuwasaidia taasisi yetu ya TAFIRI imefanya utafiti ambao pamoja na kuwasaidia kuweza kufanya uvuvi wa tija. Lakini pia wavuvi wanakabiliwa na tatizo kubwa la upotevu wa rasilimali samaki kwa maana baada ya kuwavua post-harvest loss, tumewasaidia kwa kuwatengenezea majiko ambayo tunaita majiko bunifu. Haya majiko yanatumia jua na vilevile wakati wa masika wanatumia nishati kidogo sana ya kuni. Yameweza kuwasaidia sehemu kubwa ya Kigoma na tunakwenda katika mafanikio haya kuyapeleka vilevile katika sehemu za Mkoa wa Rukwa na Katavi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Moshi Kakoso ya kwamba tutawafikia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Jimbo la Mpanda Vijijini ni kubwa lenye kilometa za mraba 16,900. Jimbo hili limekuwa vigumu sana kurahisisha shughuli za kiutendaji kwa sababu ya ukubwa.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuligawa Jimbo hili ili kupeleka huduma kwa wananchi kuwa karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hapa nchini yako maeneo ambako Majimbo yake ni makubwa sana pamoja na hili Jimbo ambalo Mheshimiwa Kakoso amelitaja.
Sasa utaratibu wake hautofautiani sana na maelezo ambayo nimeyatoa hapo awali kwamba namuomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane, lakini hasa yeye kuwasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili waingize kwenye orodha ya maeneo ambayo watayataja kwamba yanahitajika kugawanywa kuwa Majimbo mawili. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane baada ya hapa pengine tuonane ili tupeane maelezo zaidi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Kapalamsenga sasa hivi iko kisiwani kwa kukosa miundombinu baada ya mvua zilizonyesha kuharibu kabisa miundombinu ya barabara. Serikali ina mpango gani wa kuharakisha kuifanyia matengenezo barabara hiyo ambayo kimsingi inawasaidia kwa ajili ya shughuli za maendeleo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba mvua za safari hii zimekuwa nyingi pamoja na neema ambayo inasababishwa na mvua lakini ni ukweli usiopingika kwamba barabara zetu nyingi zimeharibika. Naomba nitumie fursa hii nimuagize Meneja wa TARURA aende huko barabara ya Kapalamsenga ili akatizame uhalisia na nini ambacho tunaweza tukafanya ili wananchi waendelee kupata huduma. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naishukuru na kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya baada ya kutoa fedha za kupeleka Kituo cha Afya cha Mwese na Kituo cha Afya cha Mishamo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jiografia ya Jimbo la Mpanda Vijijini ambalo lipo katika Wilaya ya Tanganyika liko katika mazingira ya mtawanyiko; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ambulance ambayo itawasaidia kwenye hivyo vituo vya afya; Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Mwese na Kituo cha Afya cha Mishamo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kutokana na eneo mtawanyiko mkubwa wa Jimbo la Mpanda Vijijini lililopo katika Wilaya ya Tanganyika ambayo ni Wilaya mpya kunahitajika ambulance kutokana na kwamba maeneo yako mbalimbali sana; Mwese, Mishamo na kile kituo kingine ambacho amekitaja. Tutakapopata mgao wa ambaulance ambao utapatikana kabla ya mwezi wa kumi, basi naomba sana tuendelee na mawasiliano ya karibu ili tumpe kipaumbele.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kata ya Kapalamsenga iko jirani na Ziwa Tanganyika lakini haina maji kabisa. Ni lini Serikali itatatua tatizo la kata hiyo kwa kupeleka maji kwa kuyatoa Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunatambua kabisa unapokuwa karibu na waridi lazima unukie. Labda nimwombe Mheshimiwa Mbunge tukutane tushauriane na Mkurugenzi wa eneo husika, tuangalie ni kwa namna gani tunaweza tukabuni mradi katika kuhakikisha wananchi wake wa kata hiyo wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imejitahidi sana kuhamasisha wananchi kujenga vyumba vya madarasa na nyumba za walimu lakini bado kunahitajika nguvu ya Serikali kumalizia majengo yale ikiwemo Shule ya Msingi Busongola, Bulamata, Pandandogo na nyinginezo. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili ziweze kumalizia majengo hayo ambayo wananchi wamejitolea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi Selemani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kwa nchi nzima maeneo mengi kabisa wananchi wamejitahidi, wamejenga majengo na mengi ya majengo hayo yamefika kwenye lenta tayari kumaliziwa. Sasa hapo ni jukumu letu sisi Serikali, Halmashauri na wadau wengine kuunga mkono nguvu za wananchi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo tunalizingatia. Naomba sana tuwasiliane mwezi huu wa Julai na Agosti ili kusudi tuweze kuyatatua matatizo kama hayo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Katavi usikivu wa TBC sio mzuri kabisa na baadhi ya maeneo hawasikii matangazo ya aina yoyote na hutumia matangazo ya nchi jirani. Je, ni lini Serikali italeta mtambo kwenye Mkoa wa Katavi ili wananchi waweze kupata huduma ya TBC?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 ipo mikoa mitano ambayo ipo kwenye bajeti. Mikoa hiyo ni mikoa mipya ukiwemo Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Katavi, Zanzibar pamoja na Mkoa wa Njombe. Kwa hiyo nichukue nafasi hii kuweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, Mkoa wa Katavi upo kwenye mpango na tunamhakikishia kwamba usikivu wa TBC katika Mkoa wake utaboreshwa. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi. Zao la tumbaku linategemea sana kununuliwa kwake kuwa na wateuzi wa zao hilo, kwa maana ya ma-classifier; Serikali ina mpango gani wa kuongeza classifier ili waweze kuliteua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa najibu swali la Mheshimiwa Mbunge Almas Maige nilisema kama Serikali tumejipanga kutafuta Classifiers wengine, na nikasema zaidi kwamba mpaka sasa hivi tumeongea na nchi kama ya Vietnum na wameshaji-commit kwamba katika msimu huu watanunua tani 1,000 za tumbaku. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi hii na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuweza kuniwezesha kunipa fedha za Kituo cha Afya cha Mwese na fedha za Kituo cha Afya cha Mishamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali dogo la nyongeza ambalo nilitaka kujua, Mkoa wa Katavi kwa ujumla na Wilaya ya Tanganyika ambako kuna Kituo cha Afya cha Mwese, Kituo cha Afya cha Kalema, Kituo cha Afya cha Mishamo, sambamba na zahanati zilizomo kwenye Wilaya ya Tanganyika na Mkoa kwa ujumla wa Katavi kuna uhaba mkubwa sana wa madaktari kwenye sekta hiyo ya afya. Ni lini Serikali ina dhamira ya dhati kutoa tatizo la uhaba wa watumishi wa sekta ya afya katika Mkoa wa Katavi hasa Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya swali la msingi nimeelezea kwamba bado ni kweli tuna changamoto kubwa sana ya rasilimali watu katika sekta ya afya. Katika mwaka huu wa fedha Serikali ilitoa kibali cha ajira cha watumishi 3,152 ambao walisambazwa katika mikoa mbalimbali, lakini vilevile nimesema katika jibu langu la msingi tunatarajia kupata kibali kipya cha kuajiri watumishi katika Serikali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Mheshimiwa Mbunge pindi kibali hicho kitakapotoka Mkoa wa Katavi utakuwa ni mmoja wa mikoa ambayo tutazingatia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza naipongeze Serikali kwa jitihada ambazo walizifanya na kutoa ushirikiano kwangu na kuwawezesha wakulima hawa waweze kulima zao hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi, kwa kuwa wakulima wamelima pamba kwenye maeneo ya Wilaya ya Mpanda Tanganyika na wamelima kupitia mfumo usiokuwa na ushirika, je, hawaoni sasa ni wakati muafaka kwa wakulima hawa ambao wamelima zao hili waruhusiwe kununuliwa zao lao kupitia makampuni binafsi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Halmashari za Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika watanufaika vipi na zao hilo hasa kupitia cess ambayo Halmashauri wanatakiwa waipate? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza kabisa Mheshimiwa Kakoso kwa sababu amekuwa ni champion kwa uanzishwaji wa zao la pamba katika Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza; la kwanza ni kuhusu mazao yale ya cess. Naomba nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini, ushuru wa mazao wanatakiwa wajipange na kufanya mikakati thabiti kuhakikisha kwamba mazao ndiyo yanayoingizia Hamlashauri mapato. Kwa hiyo, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini zihakikishe kwamba zinatilia mkazo katika ushuru wa mazao ambao ni ule tunaita cess.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nitoe rai kwamba wakulima wote nchini wajiunge kwenye AMCOS (Vyama vya Msingi vya Ushirika) na ndivyo ambavyo sisi kama Serikali sasa hivi tunaimarisha katika kuleta mapinduzi ya vyama vya ushirika. Nashukuru.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza, naishukuru sana Serikali kwa kuweza kunipatia fedha za Kituo cha Afya cha Mwese na Kituo cha Afya cha Mishamo. Tatizo ambalo lipo kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika vituo vya afya havina Wahudumu na Madaktari kwa ujumla. Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari ili waweze kufanya kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kakoso anafahamu kabisa kwamba sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeshatangaza nafasi kwa ajili ya watu wa afya wakiwepo Madaktari, Wahudumu, Manesi. Naomba nimhakikishie katika hawa ambao watakuwa wameajiriwa na naamini kwamba na wengi watakuwa wameomba wakiwa wanatokea maeneo huko ili pale wanapopewa nafasi ya kwenda kufanya kazi wasije wakasema mazingira yale kwao ni mageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha Watumishi tunawasambaza ili wakatoe huduma kwa wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kusaidia wachimbaji wadogo wadogo. Jimboni kwangu wapo wachimbaji wadogo wadogo wa Kata ya Katuma ambao wanajishughulisha na uchimbaji wa dhahabu. Je, Serikali inachukua hatua ipi ya kusaidia wachimbaji wadogo waweze kufanya shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuwainua ili watoke kwenye uchimbaji mdogo waje kwenye uchimbaji wa kati, na walio kwenye uchimbaji wa kati waende kwenye uchimbaji mkubwa. Kazi ya Serikali, hatua ya kwanza ya kuwasaidia wachimbaji wadogo ni kuwarasimisha. Kila mahali ambapo tunakuta kuna wachimbaji wadogo ambao hawapo rasmi tunawarasimisha kwa kuwaweka kwenye vikundi na baadaye kuwapatia leseni wawe na uhalali wa kuweza kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kuwapatia mafunzo ya namna bora ya uchimbaji kwa kuzingatia sheria lakini vile vile utunzaji wa mazingira. Kazi hizi zote Mheshimiwa Mbunge ataziona baada ya bajeti hii kwa sababu hii ni Wizara mpya, tutakuwa na progamu maalum ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wake wa Kata ya Katama.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya kubwa na tarafa zake zimekaa kwa mtawanyiko. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuharakisha kujenga jengo la mahakama katika wilaya hiyo? Ili kuweza kuwasaidia wananchi ambao wanapata tabu sana kutoka eneo lingine kwenda lingine kwenda kutafuta huduma za mahakama?

Swali la pili, kwa kuwa Mahakama za Mwanzo zimekuwa katika mazingira mabaya na hayana kivutio cha aina yoyote kwa watumishi wanaofanya kazi kwenye maeneo hayo. Serikali iko tayari kwenda kukarabati jengo la Mahakama ya Mwanzo eneo la Karema na maeneo ya Mishamo ili waweze kupata huduma iliyo sahihi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba huduma ya kimahakama ni huduma ambayo kila mwananchi anastahili. Ni kweli katika mazingira ambayo ameyasema ya Wilaya ya Tanganyika wananchi wanatembea umbali mrefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba katika mpango huu kama nilivyosema hapo awali katika jibu langu la msingi kwamba kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika ili wananchi wengi zaidi waweze kupata fursa ya kupata huduma za kimahakama.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Wizara yetu ya Katiba na Sheria tumeingia makubaliano na Chuo cha Ardhi pamoja na Taasisi ya masuala ya nyumba tunajenga mahakama hizi kwa teknolojia ya kisasa ya moladi ambayo inatumia muda mfupi sana. Kwa hiyo, imani yangu ni kwamba na zile Mahakama za Mwanzo alizozisema, kutokana na bajeti ilivyo basi tutaanza Mahakama ya Wilaya na hizi zingine pia na kutokana na mfuko wa bajeti ulivyo. Lakini nimhakikishie kwamba Serikali inatambua kilio hicho na tutayafanyia kazi kadri bajeti inavyoendelea kupatikana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kata ya Mnyagala ni kata ambayo ina idadi ya watu wengi na vijiji kadhaa ambavyo hakuna huduma ya kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi Sulemani Kakoso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wana hamu vituo vya vingi vijengwe na nimepata fursa ya kwenda jimboni kwa Mheshimiwa Kakoso tukaenda mpaka Mwese kule kuna kazi nzuri sana inafanyika ya ujenzi wa kituo cha afya kama ambavyo kazi nzuri imefanyika Kituo cha Afya Mwese, naomba nimtoe wasiwasi kwamba hata hicho kituo ambacho ana-propose kwa kadri nafasi itakavyoruhusu hatua kwa hatua tutahakikisha tunawasogezea wananchi huduma ya kupata matibabu ya afya kwa jirani.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Ikola – Kasangantongwe imeharibika sana na mvua zilizonyesha na kusababisha wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo na kuanza kutumia njia ya majini ambayo siyo salama.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha kuijenga barabara hiyo ya Kasangantongwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Mheshimiwa Spika, nimepata fursa ya kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Kakoso na katika maeneo ambayo barabara zinajengwa unaona thamani ya pesa ni pamoja na Jimboni kwake. Yeye mwenyewe anakiri kwamba barabara hii ambayo anaitaja imeharibika kutokana na mvua ambazo zinanyesha na ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo ambayo mvua ni za uhakika ni pamoja na Jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumwagiza Meneja wa TARURA ili akaangalie uharibifu wa hiyo barabara namna aone namna ambavyo anaweza angalau akafanya maboresho katika maeneo korofi sana ili barabara hii iweze kuendelea kupitika na wananchi waendelee kufaidi matunda ya CCM.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa RUBADA kwa muda mrefu imeshindwa kuyaendeleza haya mashamba, je, haioni sasa ni wakati muafaka Serikali iyachie maeneo haya kwa ajili ya matumizi ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Bonde la Mto Karema kuna mradi wa umwagiliaji ambapo Serikali imetoa fedha nyingi lakini mradi huo haujawahi kukamilika na una muda mrefu sana. Ni lini Serikali itakamilisha mradi wa irrigation uliopo pale Karema?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza amependekeza kwamba kwa sababu RUBADA imeshindwa kuendeleza mabonde haya basi yarudishwe mikononi mwa wakulima. Kwanza, nataka nimueleze Mheshimiwa Mbunge RUBADA haijawahi kumiliki ardhi kama jibu langu la msingi lilivyokuwa, muda wote wa uhai wa RUBADA ardhi hii ilikuwa inamilikiwa na Serikali za Vijiji na vijiji husika na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ni kwamba Bunge lako hili Tukufu mwaka 2017 lilipitisha sheria hapa tulishaifuta RUBADA sasa hivi haipo, mali zote za RUBADA zimerudi Serikalini na ziko chini ya Msajili wa Hazina. Sasa hivi tuko kwenye mchakato wa kuona nani apewe ardhi hiyo kwa ajili ya kuiendeleza. Hilo wazo lake tunalichukua kwamba kama itarudishwa tena kwa wananchi kwa sababu iko kwa wananchi basi itakuwa hivyo na wataendelea kuilima.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Bonde la Mto Karema, anataka kujua lini mradi huu utakamilika. Ni kweli kwamba miradi mingi ya umwagiliaji katika nchi hii ama ilitekelezwa chini ya kiwango au ilitekelezwa pasipo ufanisi uliokusudiwa. Kama Serikali baada ya kuliona hilo wataalam wanapitia kufanya tathmini ya kina tuone athari tuliyoipata ili kutumia tathmini ile tuweze kuyaendeleza mabonde haya. Kutegemea na upatikanaji wa fedha tutapanga jinsi ya kwenda kumalizia mradi huu.
MHE. SELEMANI M. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wamejitahidi sana kwa kushirikiana na wananchi, wamejenga shule za sekondari zipatavyo sita, lakini kwa bahati mbaya sana bado baadhi ya majengo hayajapata kuezekwa. Kwa hiyo, tulikuwa tunauliza, Serikali ina mchango gani wa kuwasaidia hao wananchi ambao wametumia nguvu kubwa ili waweze kukamilisha hayo majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mwezi wa Pili mwanzoni tumepeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 29.9 kumalizia majengo kwa maana ya maboma katika Shule za Sekondari. Ninaamini Halmashauri karibu zote, kuna baadhi ya maeneo tu hatukupeleka, lakini maeneo mengi tumepeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba vile vile mwaka huu wa fedha tuna miradi mingi na fedha ambazo zipo kwenda kumalizia maboma. Sasa kama kuna changamoto katika eneo hili kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, tutazingatia maombi yake ili tuweze kumalizia majengo haya na watoto wetu waweze kukaa sehemu salama na waweze kupata elimu kama ambavyo ndiyo makusudio na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii. Pamoja na jitihada kubwa za Serikali zilizofanywa za kupeleka fedha kwa ajili ya kumalizia maboma, bado Wilaya ya Tanganyika kuna uhitaji mkubwa wa kumalizia majengo ambayo yalianzishwa kwa nguvu za wananchi hasa ya shule za sekondari Ablulamatam, Kapalamsenga, Tongwe na Mnyagala kwenye kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itawaunga mkono wananchi ambao wamejitolea kwa kiwango kikubwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunatambua kuna uhitaji mkubwa na kuna majengo ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na wadau mbalimbali na Serikali yenyewe. Na ndiyo maana tuliekeza kwenye fedha ile ya maboma, kazi mojawapo ni kuchangia na kumalizia nguvu za wananchi. Na hata hizi ambazo zimepekwa sawa bilioni 68.48 ambayo ni wiki iliyopita tu, hizi fedha zina maelekezo, humu kuna fedha ambazo zinaenda kwenye ujenzi lakini pia kuna fedha za ku- balance ikama, kuna hoja ilikuwepo hapa kwamba kuna walimu wa kike shule moja hakuna walimu wa kiume, au walimu wa kiume hakuna walimu wa kike; wakurugenzi watumie fedha hii walimu walipwe ili waweze ku-balance kama kule halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo tumeomba, shule ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, fedha zimeenda kwenye halmashauri yake, ni wao sasa kuangalia je, hiyo fedha itumike namna gani. Lakini kadri tutakapopata uwezo tutakuwa tunazingatia maeneo ambayo yana changamoto kubwa ili kuweza kuondoa hiyo kero lakini hasa kuchangia na kushiriki katika nguvu za wananchi ili wasiendelee kulalamika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya umwagiliaji imetumia fedha nyingi sana hapa nchini na miradi hiyo haijakamilika ukiwemo mradi wa Skimu ya Karema. Nilikuwa nataka kujua Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Skimu hiyo ya Karema?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, huu mradi umechukua takribani miaka 10 haujakamilika na kusababisha hasara kwa wakulima baada ya mifumo ya maji iliyotengenezwa kusababisha mafuriko makubwa kwenye maeneo ya uzalishaji. Serikali kupitia kwa Waziri je, yuko tayari kwenda pamoja kushuhudia ile miradi na kubomoa ule mradi ili uweze kuwasaidia Wananchi ambao kimsingi wanakula hasara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anatambua kwamba, juhudi za Serikali ambazo tumezifanya tumetumia fedha nyingi sana katika miradi mingi ya umwagiliaji, ukiwepo huu wa Karema na fedha zote zilizohitajika tulipeleka, lakini tukiwa wakweli miongoni mwa miradi mingi ambayo pesa zake hazikutumika kwa mujibu wa malengo ya Serikali na kuwanufaisha wakulima ni pamoja na miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Serikali kulitambua hilo nduo maana kwamba, kabla ya kuanza kupeleka pesa nyingine wala kuomba hapa kwenye Bunge lako utuidhinishie pesa nyingine nyingi zaidi tuliona kwanza tufanya tathmini ya kina, ili tubaini kasoro na tubaini ufanisi na changamoto ambazo tumezipitia kwenye miradi ile kabla ya kutenga fedha hizo. Na nimuarifu Mheshimiwa Kakoso kwamba, tathmini hiyo tumeshaimaliza na tumebaini mapungufu yalikuwa wapi na ni namna gani kwamba, tulifanya vizuri na vibaya; sasa ndio maana nimemuahidi kwamba, tutatenga fedha katika bajeti ijayo ya mwaka 2020/2021 baada ya kumaliza tathmini hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema kwamba, kama Serikali niko tayari kuambatana naye kwenda katika mradi huu wa Karema, ili kwenda kuubomoa miundombinu, ili Wananchi hawa waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuko hapa kwa ajili ya kujenga, dhamira ya Serikali ilikuwa ni kusogeza na kuwaletea maendeleo Wananchi wale wa Karema, ili wawe na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji na kuweza kulima zaidi ya mara mbilil kwa mwaka. Kwa hiyo, hatuko tayari kwenda kuiobomoa, ila niko tayari kuambana naye kwenda hapo Karema na timu yangu ya wataalam ili kwenda kuangalia kasoro hizo ili tuweze kutafuta ufumbuzi wa kuziboresha zaidi tuwaletee maendeleo Wananchi wa Karema.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, maeneo yote ya mipakani mwa nchi, Mkoa wa Rukwa, Katavi, Kigoma ni Mikoa ambayo haina usikivu wa TBC redio a wananchi wengi wanasikia redio jirani mfano ukienda Kasanga wanasikiliza redio Zambia, ukija Kirando wanasikiliza redio ya kutoka nchi ya DRC na Kigoma wanasikiliza redio za nchi jirani ya Burundi.

Ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya karibu ya redio ili kuwafanya wananchi wasikie taarifa za kutoka kwenye Taifa lao?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa maswali yaliyotangulia, napenda kulijibu swali la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu swali hili limejitokeza mara nyingi sana hapa Bungeni naomba tu nisisitize kwamba nchi yetu imekuwa ikitegemea vituo vinane vya kurushia matangazo miaka yote hii vituo vya masafa ya kati mid-wave ambavyo vilikuwa Dar es Salam, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Songea, Nachingwea na Mbeya. Vituo vyote hivi vya midwave vimechakaa na vingi kwa kweli vimeharibika kabisa haviwezekaniki kutengenezwa kwa sababu vinatumia teknolojia ya kizamani. Ndiyo maana ni karibu miaka kumi ilioyopita tumeanzisha mradi wa kuweza kuboresha usikivu wa redio yetu hii ya Taifa kwa kutumia mitambo ya FM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Bunge hili linaanza tulianza na vituo vitano vya mpakani, tulianza na Longido, Rombo, Tarime, Kibondo na Nyasa, hali ni nzuri; tukafatia Lushoto na baadhi ya maeneo ya Mtwara. Sasa hivi katika bajeti ya mwaka huu tunahangaika na Pemba, Unguja, Simiyu, Songwe na Njombe. Vilevile tumeingia mkataba na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo tutashambulia maeneo ya Kilwa, Kilombero, Kyela, Itigi na Rungwa na kufanya ongezeko la Wilaya 33 katika kipindi hiki kuweza kusikika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea, tumefika Wilayani kwa Mheshimiwa Kakoso, tayari tumepeleka wataalamu wanaangalia ni maeneo yapi upande wa Ziwa Tanganyika tuweze kuyapelekea mitambo ya FM.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha karibu shilingi bilioni moja kwa ajili ya Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi inaenda kwa kusuasua sana na Mheshimiwa Waziri alituahidi kutupa fedha karibu shilingi bilioni nne ili ziweze kujenga hospitali hiyo: Je, ni lini Serikali italeta hizo fedha?

Mkoa wa Katavi una Chuo cha Uuguzi ambacho ni cha muda mrefu sana yapata miaka 10 hakijaendelezwa: Je, ni lini Serikali itamalizia hiki Chuo cha Uunguzi ili watu weweze kupata huduma za kimsingi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Serikali imetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.4, tumeshatanguliza shilingi bilioni 1.5 na fedha hizi zipo, kadri Mkandarasi anapokuwa anaendelea na kazi na ana-raise certificate, sisi Serikali tutaendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Spika, lengo na kusudio la Serikali ni kuhakikisha hospitali hii inakamilika na kwamba baada ya hapo, ile Hospitali ya Mpanda ambayo ilianza kama Kituo cha Afya na sasa hivi imekuwa ndiyo Hospitali ya Mkoa, tuweze kuirejesha katika Halmashauri na kuweza kuhudumu kama Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameulizia kuhusiana na Chuo cha Afya cha Uuguzi kilichopo pale. Ni kweli, nami nimewahi kufika pale Mpanda tumekiona. Wizara ilituma timu kwenda kufanya mapitio na kuangalia hali ya majengo na uhitaji. Sasa hivi tupo katika mkakati wa kuangalia matumizi bora ya kile chuo. Pindi taratibu zitakapokamilika tutawapa taarifa Mkoa wa Mpanda, jinsi gani ya kuweza kukitumia kile Chuo kwa malengo ambayo tulikuwa tumekusidia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuwanusuru wakulima wa tumbaku waliokosa mikataba ya tumbaku baada ya kampuni ya TLTC kufunga shughuli zake hapa nchini na wakulima wanakosa majawabu. Tulikuwa tunaomba Serikali itoe majibu ya msingi wakiwemo wakulima wa Mishamo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kwanza wa Serikali ni kuendelea kutoa elimu kwa wakulima. Kilimo, mauzo ya soko la tumbaku ni soko la kimkataba, unatakiwa kuzalisha baada ya kuuza. Kwa hiyo, lazima kwamba, tuendelee wakulima wakaheshimu makubaliano hayo wasiendelee kuzalisha kabla hawajajua mnunuzi ni nani na watauza kwa bei gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati wa pili, tuko kwenye majadiliano tunaongea na kampuni ya BAT ambayo imekubali kununua tumbaku yetu zaidi ya tani 8,000 ambao tukishamaliza majadiliano hayo tutawaleta huko kuja kununua hiyo tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu tunaendelea na mazungumzo na kampuni ya TLPC ili ambayo ile iliyojitoa ili waendelee kununua tumbaku ya wakulima wetu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, wakandarasi wengi wanaofanya shughuli za miradi ya maji kwenye Wilaya ya Tanganyika, Mradi wa Kamjela, Kabungu, Ifukutwa na Mhese, asilimia kubwa hawajalipwa fedha zao. Je, ni lini Serikali itawalipa fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha hiyo miradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, nikubaliane naye kwanza, ni kweli tulikuwa na madeni takribani zaidi ya bilioni 88, lakini kama unavyotambua, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha, umepata fedha hizo zaidi ya bilioni 88 katika kuhakikisha tunawalipa wakandarasi, na hata hivyo pia tumepata bilioni 12.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie hata wewe katika Jimbo lako la Kongwa wakandarasi wako sasa tumekwishawalipa. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya saa saba tukutane ili tuweze ku-crosscheck ile taarifa na yeye katika wakandarsi wake katika kuhakikisha tunawalipa. Ahsante sana.
MHE. SELEMANI M. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao hauna hospitali ya mkoa na unategemea sana Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya kutoa huduma kiasi kwamba wagonjwa wamekuwa wengi na kuifanya ile hospitali kuzidiwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka fedha kwa ajili ujenzi wa hospitali ya mkoa ili iweze kuendana na muda kwa wakati?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Moshi Kakoso kwa swali lake la nyongeza kuhusu ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi. Na kama nilivyojibu katika swali la msingi kipaumbele chetu kama Serikali ni kukamilisha ujenzi wa Hospitali za Rufaa za mikoa katika mikoa mipya ikiwemo Mkoa wa Katavi. Mheshimiwa Kakoso tayari timu yangu ilishafika Katavi mwezi uliopita na hivi leo nikitoka hapa naenda ofisini kwa ajili ya kusaini mikataba ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Katavi. Lakini tutaanza na majengo manne ya kipaumbele, tutaanza jengo la wagonjwa wa nje OPD tumelitengea takribani shilingi bilioni 3 tutajenga jengo kwa ajili ya huduma ya uzazi na watoto wachanga martenity block tumetenga 3.3 bilion, tutaweka jengo la ICU na Theatre na jengo la nne la kipaumbele ni jengo kwa ajili ya huduma za radiolojia na mionzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwatoe hofu wananchi wa Katavi kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mheshimiwa Kakoso usiwe na shaka 2020 utasimama kifua mbele baada ya kuwa tumetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi. Kwa hiyo, takribani kuna kama bilioni 9 tumezitenga kwa ajili ya Katavi mwaka huu wa fedha 2019/ 2020.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na tatizo kubwa la walimu katika nchi nzima, na kuna walimu ambao wanajitolea kufanya kazi za kufundisha katika maeneo mbalimbali nchini, zinapojitokeza ajira walimu hawa hawapewi nafasi; je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha walimu wanaojitolea wanapewa kipaumbele pale nafasi zinapotoka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vigezo ambavyo sasa hivi Serikali imekuwa ikitumia katika kuajiri walimu ni pamoja na kuzingatia walimu wote ambao wamejitolea kwa muda mrefu katika shule wanazofundisha. Kwa hiyo, hata katika hizi nafasi 6,000 ambazo tunakwenda kuzijaza zitazingatia vigezo hivyo. Na tumetoa maelekezo kwa maafisa elimu wote ngazi za wilaya kuleta taarifa za walimu wote wanaojitolea katika shule zao ili tuweze kuwazingatia katika ajira mpya. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana Mheshimiwa Rais alipokuja Mkoa wa Katavi aliagiza Wizara ya Maliasili na Wizara ya Ardhi kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi kati ya mapori ya akiba na hifadhi ya Taifa ya Katavi. Lakini utekelezaji mpaka sasa bado haujafanyika ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja Mkoa wa Katavi ili asimamie zoezi hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Katavi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge hili Tukufu tutaongozana naye kwenda kutatua taizo hili kwa hiyo nimuondoe wasiwasi tutaondoka naye, ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI M. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wakati tunasubiri mradi wa kuyatoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka Mpanda Mjini, Serikali iliahidi kutupatia shilingi milioni 240 kwa ajili ya kukarabati vyanzo vya maji na kuhakikisha vijiji vile ambavyo vilitakiwa vipate maji, vinapatiwa maji:-

Je, Serikali inatupatia majibu yapi kupeleka hizo fedha shilingi milioni 240?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Wizara tuliahidi hizi fedha ziweze kwenda kusaidia kukarabati miundombinu muhimu ili vile vijiji viweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mbunge hizi fedha mapema tunavyoanza mwaka wa fedha 2021/2022 zote zinatumwa katika Wilaya yako, lengo ni kuona kwamba ule mradi unakarabatiwa na wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambazo zilichelewa sana kupata umeme wa REA. Kwa bahati nzuri kwa sasa Serikali inatekeleza mradi huo. Kwenye Mradi wa REA phase II vipo vijiji vilisahaulika kuingizwa kwenye mradi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha vijiji vilivyosahaulika katika mradi wa phase II?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi na swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Mbogo. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Kakoso pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote wa Katavi pamoja na Mpanda wanavyofuatilia masuala ya umeme vijijini katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo maeneo nchi nzima ambayo yalisahaulika na yalikuwa yanafikia takriban maeneo ama vijiji 610.

Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mheshimiwa Kakoso vijiji vyote 610 ambavyo vilisahaulika tumefanya marejeo na vijiji vyote vimeingia kwenye mpango na vimekabidhiwa wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Kakoso kwa sababu ni kweli hata kata kubwa ya Mishamo pamoja na Mwese pamoja na Utamata vilisahaulika lakini vyote vimeingia kwenye mpango na wananchi wote watapata umeme kwa uhakika ndani ya miezi 18 kutoka sasa. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Zipo skimu zilizoanzishwa na Serikali ikiwemo skimu ya Karema ambayo ilianzishwa toka miaka iliyopita kama saba hivi. Skimu hiyo haijafanya kazi na zipo nyingi nchini zinazofanana na ile skimu: -

Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha miradi iliyoanzishwa huko nyuma ukiwemo mradi wa skimu ya Karema?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo ameshatoa maelekezo kwa Tume ya Umwagiliaji Nchini kwa kuhakikisha ina take stock ya scheme zote nchini kwa zile zinazofanya kazi na ambazo zinahitaji ukarabati na zile ambazo zinahitajika kujengwa mpya. Hivi sasa kazi hiyo inaendelea na katika maeneo hayo pia tutaigusa skimu hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema ya Karema; na tutatoa pia maelezo ndani ya Bunge letu hatua ambazo tumezifikia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii mikubwa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kupata nafasi ya kuuliza swali, lakini niishukuru sana Wizara ya Maji kupitia kwa Waziri mwenye dhamana wamefanya kazi kubwa sana ya kupeleka huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa ya Mkoa wa Katavi tunahitaji kupata chanzo cha uhakika cha maji na chanzo hicho kipo Ziwa Tanganyika ambalo linaweza likatatua tatizo la maji kwa kupeleka huduma kwa Wilaya zote tatu kwa maana ya Wilaya Tanganyika, Wilaya ya Mlele na Wilaya ya Mpanda.

Ni lini Serikali itakuja kutatua tatizo la kupeleka huduma ya maji kuliko kutumia fedha nyingi wanazozitumia kuandaa miradi midogo midogo ambayo haina tija?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoendelea kufuatilia suala la matumizi ya vyanzo vya uhakika kama Ziwa Tanzanyika. Wizara tumejipanga kuona kwamba maziwa yote tunakwenda kuyatumia tukiamini tunakwenda kutatua tatizo hili la maji na tutamtua ndoo mwanamama kichwani kama ambavyo Mheshimiwa Rais anatutaka na tumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kutupa fedha Wizara ya Maji. Hivyo, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi tuko katika kufanya usanifu ili kuona mwaka 2022/2023 matumizi ya maji makuu kama vyanzo vya maji vya uhakika yaweze kufanyika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nishukuru sana Serikali kwa kuleta fedha za TARURA zinazojenga Barabara ya kutoka Kambanga kwenda Ifinsi na kutoka Majalila kwenda Ifinsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani zote hizo barabara ile haitakuwa na umuhimu wa aina yoyote kama hakutakuwa na bajeti ya Daraja la Mto Mnyamasi eneo la Ifinsi.

Je, ni lini Serikali itajenga daraja hilo ili iweze kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Bugu ambao hawana mawasiliano kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naye ameomba daraja, na kiukweli madaraja mengi ndiyo hayo ambayo sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tuliahidi kwamba tunayafanyia tathmini ili kuhakikisha kwamba tunarahisisha usafiri katika maeneo mbalimbali nchini. Na ahadi hiyo tuliitoa ndani ya Bunge kwa sababu maeneo mengi nchi hii yanasumbuliwa zaidi na madaraja, kwa sababu, moja, ya kuharibika, lakini pili, maeneo mengine yana madaraja ambayo wakati wa misimu ya mvua yanakuwa hayafikiki kabisa kwa sababu ni mabovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatakiwa tukajenge madaraja ya kudumu ili kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanapata huduma hiyo ya usafiri na usafirishaji wa wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Kakoso lipo katika mipango yetu, na asubiri tu kwamba baada ya mwaka huu wa fedha, naamini yale yako ndani ya bajeti tutayatekeleza. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Msitu wa Mpanda North East ulishapoteza hadhi ya uhifadhi kutokana na shughuli za kibinadamu, pamoja na Serikali yenyewe kuchangia kwa kugawa maeneo kuyafanyia shughuli za maendeleo ukiwemo Mji wa Mpanda pale Mpanda Mjini ni eneo la TFS, makazi ya Katumba na vijiji vilivyotajwa.

Je, ni lini Serikali itakuja kutatua huo mgogoro kumaliza mgogoro huo kwa kupitia timu ya Mawaziri wanane ambao Serikali ilielekeza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa TFS imekuwa na tabia ya kuwapiga wananchi, kuwaibia mali zao kila wanapozalisha mali, kipindi cha uzalishaji mali hawaendi kuwapiga na kipindi cha uvunaji wanakwenda kuwanyang’anya mali zao. Ni lini tabia hii itakomeshwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pamoja na majibu ya msingi maeneo haya yaliingizwa kwenye timu ya Mawaziri wa kisekta nane ambao walikwenda kuchakata na pia wameweza kufika katika mikoa 13 kutoa maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hizi za migogoro. Hivi ninavyoongea sasa kuna wataalam wako katika maeneo hayo ikiwemo Mpanda Vijijini ambako wataalam wamekwenda kufanya tathmini hiyo. Maeneo haya kama kweli yanakosa sifa ya kuwa hifadhi basi yataingizwa kwenye utatuzi wa migogoro ya Mawaziri nane na kisha yataingizwa kwenye ufutaji wa GN ambazo zipo tangu mwaka 1947.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa TFS kunyang’anya mazao, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kuna changamoto ya namna hii ambayo imejitokeza, basi naomba nilichukue, twende kulifanyia kazi na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imejipanga kupanua bandari za Mwanza na Bandari zile za Nansio; je, Serikali imechukua hatua gani za haraka kuhakikisha wanakamilisha hizo bandari ili ziweze kuwasaidia wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema na tayari ilishaanza kufanya kazi; je, ni lini Serikali itaanza kuleta meli kwenye eneo la Bandari ya Karema, meli za kimataifa na meli za ndani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikipanga fedha katika bajeti mbalimbali hususan kupitia TPA kwa bandari hizi za Mwanza, Nansio, Mwanza Kusini na Mwanza Kaskazini. Na hivi navyosema Bandari ya Nansio tayari tumeshafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja a Bandari za Bukoba pamoja na Kemondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusiana na meli za Kwenda kwenye bandari yetu ambayo imezinduliwa hivi karibuni na hususan katika Ziwa Tanganyika, tunataraji hivi karibuni tutafanya mkutano na washirika ambao ni wadau muhimu katika usafirishaji wa bandari za Ziwa Tanganyika kutoka Congo, Zambia, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo hivi karibuni utaanza kuona meli zikienda katika bandari hiyo mpya ya Kalema. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi nimeomba kupatiwa vifaa kingaradi kwenye eneo la Mwese.

Je, Serikali ni lini itapeleka hivyo vifaa kwa kuwa, eneo hilo lina radi za mara kwa mara na wananchi wengi wamekuwa wakipoteza maisha yao na mali zao, hasa mifugo?

Mheshimiwa Spika, napenda kupata majibu ya msingi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri atueleze vifaa hivyo vitafika lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 bado unaendelea na sasa tuko katika robo ya pili, namhakikishia Mheshimiwa mbunge kwamba tutahakikisha hii pesa imeenda na kwenye maeneo hayo ya Mwese pia, vifaa hivi vitafika kwa kukamilisha na hiyo miundombinu ya umeme ambayo inahitajika katika maeneo hayo kwa haraka iwezekanavyo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi na Wilaya zake kumekuwa na wimbi la mauaji ya mara kwa mara hii ni kwa sababu hakuna vituo vingi vya polisi.

Je, ni lini mtatujengea kituo cha Polisi katika Kata ya Kasekese Wilaya ya Tanganyika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba nilichukue hili tulifanyie kazi ili tuone hatua ya kuchukua.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mkoa wa Katavi una miradi mingi midogomidogo ambayo imeletwa na Serikali na tunaipongeza, lakini mwarobaini wa Mkoa wa Katavi kuepukana na miradi hiyo midogomidogo ni kuleta Mradi wa Maji wa kutoka Ziwa Tanganyika kuleta makao makuu, je, ni lini mradi huu utaanza kufanyiwa kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Katavi ni moja ya eneo ambalo litakwenda kunufaika na maji kutoka Ziwa Tanganyika kama nilivyojibu kwa Mbunge wa Nkasi, tutakapopata fedha hii ni miradi yetu ya kimkakati tutakwenda kutekeleza.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kujenga Soko la Kimataifa katika Kijiji cha Itetemya, Kata ya Karema ambacho kingewasaidia kuunganisha kati ya nchi ya DRC Congo na wananchi hao: Je, ni lini huu mradi ambao iliahidi takribani miaka mitano iliyopita utatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilishatoa ahadi juu ya ujenzi wa soko katika eneo hilo. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa kati ya maeneo ambayo tunayapa kipaumbele ni ujenzi huu wa masoko. Nimwondoe hofu kwamba katika mikakati yetu inayokuja tutaunganisha masuala ya miundombinu ya masoko tunayoyafanya na ujenzi wa masoko hayo, pamoja na kumkumbuka katika eneo lake. Hivyo Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi katika bajeti inayokuja pia tutaikumbuka katika eneo lake hilo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Wilaya ya Tanganyika imekamilika kila kitu, tatizo lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba ambavyo vinapelekea huduma ya upasuaji kukosekana katika hospitali hiyo.

Je, ni lini itakamilisha kuleta vifaa tiba ambavyo vimebaki katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza hospitali hiyo tuliitembelea na nilitegemea Mheshimiwa Mbunge kwanza angeshukuru kwa Digital X-Ray ambayo tayari tuliikabidhi pale siku ile, yeye hakuwepo lakini Mkuu wa Wilaya alipokea kwa niaba yake.

SPIKA: Ngoja Mheshimiwa Naibu Waziri subiri kidogo, Waheshimiwa Wabunge nilishatoa maelekezo hapa kwa hiyo usimuweke Mbunge mazingira kwamba yeye hatambui huo mchango uliotolewa, anatambua mchango ni kwa sababu maswali lazima yawe mafupi, kwa hivyo anaenda moja kwa moja kwenye swali na wewe nenda moja kwa moja kwenye jibu la swali alilouliza. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni ukweli anachokisema Mbunge kulikuwa na vifaa vya Shilingi Milioni 507 vilitakiwa zipelekwe vimepelekwa vifaa vya Shilingi Milioni
203 vitaenda kumaliziwa mwaka huu kuhakikisha vimepelekwa vilivyobakia.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Kituo cha Polisi, wanatumia Kituo cha Polisi kwenye jengo la Ofisi ya Kata. Halmashauri ya Wilaya la Tanganyika kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wameomba wadau kuchangia, nami nikiwa miongoni mwa wadau kujenga Kituo cha Polisi. Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi ambao wamejitolea ili waweze kukamilisha hicho Kituo cha Polisi ambacho kipo katika hatua ya awali ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tumpongeze kwa kazi nzuri aliyofanya kama mmoja wa wadau na wadau wengine walioanza ujenzi wa Kituo hiki cha Polisi pale Tanganyika. Kwa niaba ya Waziri wangu, niahidi tu kwamba, tunamwelekeza IGP kupitia Makamanda wake waweze kufanya tathmini ya kiwango kilichofikiwa na kiasi gani kinatakiwa kama pungufu ili waweze kuingiza kituo hiki cha Tanganyika kwenye mpango wao wa ujenzi, nashukuru.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kwanza niipongeze Serikali kwa kujenga vituo vya afya na hospitali ya Wilaya. Kwa bahati mbaya sana idadi ya watumishi ambao ndio wanaokuja kufanya kazi kwenye maeneo husika kwenye vituo vya afya na hospitali ya wilaya bado ni wachache, Halmashauri yangu ya Wilaya kwenye hospitali ya wilaya mahitaji ya watumishi ni 608 waliopo ni 40 tu, kitu ambacho wanashindwa kufanya kazi na wanashindwa kutoa huduma ile iliyokusudiwa.

Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itapeleka wahudumu hasa kada ya wauguzi ili waweze kufanya kazi na hospitali ya wilaya ianze kufanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali imeleta X- ray kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika, kinachokwamisha sasa hivi ni Bodi ile ya Mionzi kutokwenda kuthibitisha. Je, ni lini watawapeleka wataalam hao na hiyo X-ray ilishafungwa kama miezi minne iliyopita? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imejenga Hospitali ya Halmashauri ya Tanganyika na hospitali ile imeanza kutoa huduma za afya kwa awamu ya kwanza na watumishi waliopo 40 kwa sasa ni wale ambao wanatoa huduma za awali. Serikali imeweka utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba majengo mengine yanapoanza kutoa huduma, watumishi pia wanapelekwa, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hawa watumishi 608 wanahitajika pale hospitali itakapoanza kutoa huduma katika majengo yote, lakini kwa sasa watumishi 40 wanatoa huduma zile za awali na Serikali itaendelea kupeleka watumishi ili waweze kutoa huduma zote katika wodi ambazo zinaendelea na ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la x-ray ni kweli Serikali imepeleka digital x-ray katika Halmashauri ya Tanganyika kama ambavyo imepeleka katika Hospitali za Halmashauri nyingi kote nchini na wataalam wa mionzi kutoka Arusha tutawasiliana nao wafike Tanganyika ili waweze kufanya ukaguzi na kutupa kibali cha kuendelea na huduma za x-ray, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vijiji vya Ngomalusambo na kijiji cha Vikonge ni miongoni mwa vijiji ambavyo Serikali ilitoa maelekezo kupitia kwa Mheshimiwa Rais Hayati Dokta John Pombe Magufuli viachiwe vibaki kuwa kwa matumizi ya wananchi, lakini mpaka sasa bado vijiji hivyo vina mgogoro kati ya TFS na vijiji hivyo.

Ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuahidi tuu Mheshimiwa Kakoso kwamba tutafika katika maeneo hayo nakuyaangalia kama yana umuhimu wa kuyaachia tutaendelea kuyaachia. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, Wilaya ya Tanganyika ina tarafa tatu na umbali wa tarafa moja hadi nyingine ni zaidi ya kilomita 130, na jiografia yake ni mbaya. Nilikuwa naomba kuuliza Serikali ni lini itaongeza gari la wagonjwa kwenye tarafa ya Kalema, Kabungu na Mwesi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni wilaya kubwa lakini hizi tarafa ambazo amezitaja na nyingine zinahitaji kupata upendeleo wa makusudi kupata gari la wagonjwa. Niseme kwa ujumla, Waheshimiwa Wabunge wote tutafanya tathmini, tunafahamu jiografia ya halmashauri zetu na majimbo zinatofautiana, tutafanya tathmini kwa maeneo ambayo ni makubwa yanahitaji magari zaidi ya moja. Hivyo, kati ya yale magari yanayoongezeka tutapeleka ikiwemo tathmini ya Tanganyika. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa halmashauri zilizopata fedha nyingi za Serikali kwaajili ya ujenzi wa madarasa; je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kuongeza mabweni kwenye Shule za Sekondari za Bulamata, Kakoso na Kabungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, katika maeneo ya Tanganyika ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha nimhakikishie tu kwamba Serikali ni kuhakikisha na yenyewe tunayafikia; na ndiyo maana sasa hivi tuna programu mbalimbali kuwafikia katika maeneo ambayo hayafikiki. Kwa hiyo, nimuondoe hofu kwenye hili analolizungumza. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kukamilisha miradi ya umwagiliaji ya skimu ya Karema na skimu ya Kabaki. Kupitia kwa Waziri aliyekuwpepo aliahidi kuwa atakamilisha hiyo miradi.

Je ni lini itakuja kukamilisha hiyo miradi miwili ndani ya Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi Seleman Kakoso Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, mimi nimefika na nilitoa pia ahadi hii mbele ya wananchi wake katika mkutano wa adhara ambao tuliufanya pale kijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja ya mwaka 2022/23 miradi wa skimu hizi imeainishwa na itatekelezwa kupitia bajeti hiyo inayokuja. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuliipokea na tunaendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi; kwanza ninaipongeza Serikali imejenga vituo vya afya vingi sana ndani ya Halmashauri ya Tanganyika, tuna tatizo la ukosefu wa vitendea kazi kwenye vituo vya afya pamoja na watumishi.

Je, ni lini Serikali itapeleka vitendea kazi na watumishi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vituo vingi vya afya vimejengwa lakini katika mwaka wa fedha huu Serikali imetenga zaidi ya bilioni 193 kwa ajili ya kupeleka vifaatiba katika vituo vilivyojengwa. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba kwa kiasi kikubwa vituo vyetu vimeanza kupokea fedha na vifaatiba kwa ajili ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili litaendelea katika vituo vya afya vya Halmashauri ya Tanganyika. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa kumekuwa na mkanganyiko wa kutoa huduma za kijamii kwenye eneo ambalo lina utawala wa aina mbili, Ofisi ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya TAMISEMI na wanaotoa fedha ni TAMISEMI. Je, mkanganyiko huu ni lini Serikali itakwenda kuuondoa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Umoja wa Mataifa ulijitoa kuhudumia kambi za wakimbizi na kukabidhi Serikali na Serikali ikatoa uraia. Tunavyozungumza leo hii eneo la utawala kata tayari kuna madiwani ambao wanafanya shughuli za kiutawala lakini eneo la Serikali za vijiji hakuna utawala wa aina yoyote. Ni lini mtakaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ili muondoe sintofahamu ambayo ipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkanganyiko ambao umetokana na vijiji hivi kuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais TAMISEMI kimsingi tunaendelea kuiweka sawa; na ndiyo maana siku za nyuma hatukuwa na madiwani katika zile kata nne lakini mwaka 2020 madiwani walichaguliwa. Pia kuna watendaji wa vijiji ambao siku za nyuma hawakuwepo; na linaloendelea sasa ni utaratibu tu wa ndani ya Serikali kuongea kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili tuweze kukubaliana mfumo mzuri zaidi wa kuendesha vijiji hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuondoa changamoto ambayo ipo kwa sasa, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi. Mradi wa REA wa vijiji 26 Wilaya ya Tanganyika ambao Mheshimiwa Naibu Waziri, alikuja akauzindia mpaka sasa haujakamilika. Je, ni lini Serikali itakamilisha ule mradi ili uweze kuleta tija kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilienda kuzindua Mradi huo mimi mwenyewe na Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo Mkandarasi wa ITIBIKO bado anaendelea na kazi site na makubaliano tuliyokuwanayo ni kufikia Desemba mwaka huu mradi huu pamoja na miradi mingine yote ya kupeleka umeme vijijini iwe imekamilika. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso kwamba jambo hili tunalifuatilia na kabla ya mwaka huu kwisha tutahakikisha ya kwamba kazi hiyo inakamilika katika eneo lake la Wilaya ya Tanganyika lakini na maeneo mengine.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa watumishi wengi wanaojitolea wamefanya kazi ya ziada, na kila mara ajira zinapotoka hawa wanaojitolea huwa hawapewi nafasi ya kupewa ajira: Je, Serikali mna mpango gani wa kuwasaidia wale wanaojitolea katika nafasi za Ualimu na Unesi waweze kupewa nafasi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Tanganyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyasema kwamba kumekuwa na watu wanaojitolea lakini wakati mwingine inapotokea ajira zimefunguliwa wanapata matatizo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwongozo wa ajira katika nchi yetu unataka ajira zote ziwe katika ushindani. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama watafuata taratibu zilizowekwa, hatuna tatizo katika jambo hilo.

Mheshimwia Mwenyekiti, ni kweli kwamba tatizo la upungufu wa walimu na kada nyinginezo katika utumishi wa umma ni jambo ambalo tunalijua na Serikali imeendelea kulishughulikia jambo hilo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeahidi na katika bajeti yetu tunakuja kusoma hapa hivi karibuni ya mwaka 2023/2024, majibu yote atayapata.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti nishukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kipindi hicho Ummy Mwalimu aliahidi shilingi bilioni 1.5 kuunganisha Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Uvinza kupitia Kata ya Kalia na Kata ya Mwese.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutakaa na wenzetu wa TARURA kuona mpango wao juu ya kutenga fedha hii ya bilioni 1.5 ya kuunganisha barabara kati ya Tanganyika hadi Uvinza. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika inazo shule za Kalema, Kabungu pamoja na Bulamata, ambazo zina tatizo kubwa sana la ukosefu wa mabweni.

Je, ni lini Serikali watapeleka fedha ili waweze kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti,ni kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta fedha, na sehemu ya fedha ambayo imeshapatikana katika awali tayari kuna maeneo ambayo tayari imeshaelekeza kuhakikisha kwamba zinafunguliwa shule za kidato cha tano na sita na zianze kufanya kazi. Kwa hiyo hata haya maombi yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa yatawekwa katika mpango ili Serikali iweze kuyatekeleza kwa kutafuta fedha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la kwanza; kwa kuwa wadau wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya na kumshirikisha RPC na OCD wamefikia hatua ya kutenga fedha na kuanza kujenga kituo hicho na Wizara mpaka sasa hawajatoa shilingi ya aina yoyote. Je, ni lini Serikali watapeleka fedha kwa kuwaunga mkono wananchi ambao wamejitolea kuhakikisha wanafanya kazi hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; halmashauri ya wilaya imetoa eneo na Serikali inatakiwa itoe shilingi milioni 20 kwa ajili ya kupata hati miliki. Je, ni lini sasa mchakato huo wa kupeleka hizo fedha utafanyika ili jitihada za kuejnga kituo hicho zianze kufanyika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, lini fedha zitapelekwa? Hatua ya kwanza kama alivyomaliza swali lake la pili ni kulipa hii fedha ya fidia na upimaji ya milioni 20 na nimuahidi katika bajeti ijayo fedha zimetengwa zitapelekwa. Baada ya kulipa fidia na kupata hati Wizara itaji-commit kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ku-support nguvu za wananchi kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wananchi wa Wilaya ya Tanganyika wanapakana na Wilaya ya Nkasi Kusini na upande wa Kaskazini wanapakana na Wilaya ya Uvinza. Maeneo haya kwa wananchi wanaoishi mwambao wa Ziwa hawana njia mbadala tofauti na njia ya majini.

Je, ni lini Serikali wataongeza bajeti kwa upande wa TARURA ili tuzifungue hizi njia tuepushe maafa kwa wananchi na mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni lengo la Serikali kuiongezea TARURA fedha. Kama mlivyo mashahidi, mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti ya TARURA nchi nzima ilikuwa shilingi bilioni 228, lakini baada ya bajeti ya 2021/2022 chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, TARURA imeongezewa fedha zaidi ya mara tatu kwenda shilingi bilioni 772. Tutaangalia hizi barabara zinazounganisha Tanganyika, Nkasi na Uvinza ili ziweze kupata fedha na kutengenezwa, kadri ya fedha itakavyopatikana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ina upungufu wa watumishi wa kada ya ualimu wapatao 1000 na kada ya afya wapatao zaidi ya 200.

Je, ni lini Serikali itaenda kutatua kero ya watumishi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, utatuzi wa changamoto ya upungufu wa wataalam wa sekta ya elimu na afya ni mchakato, safari ni hatua, tumeanza. Katika Halmashauri ya Tanganyika nafahamu ni moja ya halmashauri ambazo zilipata watumishi wengi sana katika ajira mbili zilizopita ukilinganisha na halmashauri nyingine kwa sababu ya vigezo vya kuwa ipo mbali zaidi lakini ilikuwa na upungufu mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba zoezi ambalo limeanza la kupeleka watumishi kwa wingi Tanganyika, litaendelea kadri tutakavyokuwa tunaendelea kuajiri watumishi wa sekta hizo. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa kufanya jitihada za kupeleka mradi hasa wa ujenzi wa Daraja la Mto Mnyamansi. Kwa kuwa eneo la Ifinsi kwenda Kijiji cha Bugwe hakuna mawasiliano ya aina yoyote. Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hiyo ili iweze kuwasaidia wananchi kwenye eneo hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili tunatambua jitihada za Serikali zilizofanywa, mmefungua barabara ya Kamibanga hadi Ifinsi, Majalila hadi Ifinsi lakini barabara zote hizo zilizofunguliwa hazijawekewa molamu na madaraja. Ni lini Serikali itaanza kujenga na kuboresha barabara hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakoso. La kwanza juu ya mpango wa ujenzi wa barabara hii ya Ifinsi – Bugwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba barabara hii haikuwepo na ilikuwa wananchi hawa wanakaa kwenye kisiwa kipindi ambapo mvua zinanyesha. Tayari baada ya utengaji huu wa bajeti ya 1.5 billioni, Serikali pia katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 475 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha changarawe kwenye vipande korofi na kuweka mifereji katika maeneo mbalimbali ya barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili lla Barabara za Kambanga – Ifinsi na maeneo mengine aliyoyataja Mheshimiwa Kakoso tutakaa naye Mheshimiwa Mbunge na kuona ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya ukarabati na kuweka kifusi katika barabara hizi.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Serikali imeboresha, imejenga shule nyingi za msingi na sekondari na kuna uhaba wa Walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kukidhi mahitaji ya Walimu ambao ni takribani Walimu 1,000 ni pungufu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mipango yake ya kuhakikisha hakuna upungufu wa Walimu katika Wilaya ya Tanganyika na wilaya zingine hapa nchini, ndio maana imeendelea kuajiri na hivi karibuni ajira 13,130 zimetolewa za Walimu kwa ajili ya kwenda kuziba mapengo na uhitaji uliopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kule Tanganyika.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi, Mkoa wa Katavi kwa ujumla una shida kubwa ya umeme kwa ujumla kwa sababu majenereta yaliyopo yameshindwa kuhimili idadi ya watu wanaotumia umeme. Serikali ina mpango gani wa dharura wa kupeleka jenereta litakaloenda ku-support umeme kwenye Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali katika mpango wa muda mrefu tunajenga sasa line ya kutoka Tabora – Ipole – Inyonga mpaka Mpanda Mjini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba gridi imeufikia Mkoa wa Katavi, lakini katika njia za muda mfupi kama alivyouliza naomba baada ya hapa tutashauriana naye ili tuone tatizo ni kubwa kiasi gani na tuone ni wapi tunakoweza kupata mashine ya dharura ya kwenda kuongeza nguvu katika Mkoa wetu wa Katavi ili kipindi ambacho tunakamilisha upelekaji wa gridi basi wananchi waendelee kupata huduma ya umeme.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, mradi huu wa skimu ya umwagiliaji ya Karema umechukua muda mrefu zaidi ya miaka kumi na swali kama hili nimeliuliza hapa Bungeni zaidi ya mara tano.

Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kwenda kubomoa ile miundombinu ambayo waliiweka ambayo haiwasaidii wananchi na kabla ya kuweka mradi ule wananchi walikuwa wakinufaika wanapata mazao yao. Lini Serikali wataenda kubomoa ule mradi?

Swali la pili, kwa kuwa ndani ya miaka kumi wananchi wamekuwa wakilima wakipata hasara kwa sababu ya miundombinu iliyowekwa mibovu. Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa fidia wakulima hao ambao wamelima kwa miaka kumi wakiteseka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu juu ya ujenzi wa mradi wa Karema wa umwagiliaji, lakini nimuondoe shaka kwamba ndiyo maana ukiona katika jibu la msingi tumeandika hapa kwamba mradi huu wa Karema ambao sasa hivi uko katika hatua za mwisho za usanifu wa bwawa pamoja na miundombinu ya umwagiliaji na tumeahidi kabisa hapa kwamba utakamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Kwa hiyo, nimuondoe shaka kwa sababu Serikali imeona hiyo kero ya wananchi na katika mwaka wa fedha unaokuja litatekelezeka kama ambavyo Wizara ya kilimo imeahidi na itafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu hasara ambayo wananchi wameipata kutokana na kushindwa kulima vizuri katika eneo lao, nimwambie tu kwamba ukweli ni kwamba hatuwezi kulipa fidia kwa hasara ambazo zilitokana na wao kulima eneo lile, lakini Serikali imekuwa ikizingatia umuhimu wa wakulima nchini na ndiyo maana umeona Serikali katika ku-boost kilimo ikawa imekuja na mradi wa kutoa ruzuku za pembejeo, yote hii ni kutaka kuwanufaisha wananchi ambao wanapata faida kutokana na ruzuku hizo. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha kilimo nchini ili kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata faida. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza: Mradi wa Kata ya Katuma ulipata Mkandarasi HEMATEC ambaye aliingia mkataba wa kufanya kazi tarehe 14 Desemba, 2021, mpaka sasa Mkandarasi huyo hajawahi kufika kwenye eneo husika:-

Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuchukua hatua za dharura ku-terminate huo mkataba ambapo kimsingi mradi huo unatakiwa ukamilike tarehe 20 mwezi wa Sita?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Tunapongeza jitihada zinazofanywa na Serikali na kuleta miradi mingi kwenye eneo la kwetu. Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Tanganyika hana gari la kumsaidia kufanya kazi:-

Je, ni lini Serikali italeta fedha au kuleta gari ili liweze kusaidia kutoa huduma kwenye eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu, maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpa pole Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifuatilia sana huyu Mkandarasi, lakini sisi kama Wizara hatutafumbia macho Mkandarasi yoyote mzembe, hata kama tumesaini mkataba, lakini ukienda kinyume na mkataba, tutakuweka pembeni kwa sababu hatuko tayari kufanya kazi na mtu anayetuchelewesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kwa kutumia Bunge lako Tukufu, naomba nitoe wito kwa ma-RM wote ambao Wakandarasi wao wanalalamikiwa kama huyu HEMATEC, RM wa eneo hili. Nitapenda ulete taarifa yako kesho asubuhi ili kujua ukweli wa suala la huyu Mkandarasi na endapo itabainika ni mzembe, tutamchukulia hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na DM wa Tanganyika kupatiwa gari, utaratibu unaendelea. Tunashukuru sana utendaji mzuri wa Director General wa RUWASA, Eng. Clement Kivegalo, ameendelea kufanya taratibu za kuona ma-DM wote wanapata vyombo vya usafiri. Hivyo katika magari yatakayokuja, naamini DG ataweka pia msisitizo kwa eneo la Tanganyika kwa umuhimu wake.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Wafanyakazi wa TAZARA wamekuwa wakiidai Serikali mafao yao na wamechangia michango yao yote katika kipindi cha utumishi wao, TAZARA ilikuwa haipeleki michango kwa wahusika.

Je, Serikali inawasaidia vipi hao wafanyakazi ambao wengi wao wamefariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama alivyokwisha kuuliza kuhusiana na wafanyakazi wa TAZARA ambao wamekuwa na changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari jambo hili linaendelea kushughulika nalo lakini kwa nia njema ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ilitokana na ile mifuko minne ambayo iliunganishwa. Katika ile mifuko minne ilirithi deni la Shilingi Trilioni 1.02 ya wanachama hawa ambao walikuwa wanadai katika maeneo mbalimbali. Nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba nina furaha kwamba fedha hizo zimelipwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza pia fedha zaidi ya Trilioni 2.17.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Bulamata AMCOS wa eneo la Mishamo walilima tumbaku zao na kuwauzia Kampuni ya Naile Leaf Limited wanaidai kampuni hiyo dola za Kimarekani 600,000. Ni lini Serikali itawasaidia hawa wakulima wadogo ambao wamedhulumiwa haki zao za kimsingi na walipewa leseni na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Moshi Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna madai ya wakulima dhidi ya hii kampuni, Mheshimiwa Waziri aliwaita makampuni yote yanayodaiwa na akatoa mwongozo wa malipo; moja kati ya kazi ambayo Mkurugenzi wa Bodi anaendelea kuifuatilia ni kuhakikisha kwamba wakulima hao wanalipwa lakini pia tumewapa sharti kwamba hatuta-renew leseni yao mpaka pale watakapokamilisha malipo ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Kilimo tunahakikisha kwamba tunasimamia kwa dhati ili wakulima hawa waweze kulipwa na jambo hili lipo ndani ya meza ya Mheshimiwa Waziri, kazi inaendelea kuhakikisha kwamba malipo haya yanafanyika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi; Wilaya ya Tanganyika ni wilaya ambayo ipo pembezoni mwa mipakani, ni wilaya ambayo haina kabisa kituo cha polisi na wananchi wamejiotolea kupitia hamasa ya Mkuu wa Wilaya wameanza kutoa michango ya kujenga kituo cha polisi.

Je, ni lini Serikali itawapelekea fedha ili wananchi hao waweze kupata kituo cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishajibu kwenye suala la Kyerwa, Wilaya zote za mpakani ni kipaumbele cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuona kwamba zinapata vituo vya polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, pale ambapo tutapata fedha Wilaya ya Tanganyika itajengewa kituo cha polisi kama ambavyo tumeahidi katika bajeti yetu iliyosomwa na Waziri wangu hapa mwezi mmoja uliopita.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kunipa nafasi.

Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni mikoa ambayo inamiliki Ziwa Tanganyika, kwa bahati mbaya sana mikoa hii yote hakuna sehemu Serikali imewekeza viwanda vya kuchakata samaki.

Ni lini Serikali itapeleka viwanda kwenye maeneo ya mikoa hiyo ili kuepukana na wizi unaofanywa na nchi jirani kwenye maeneo ya kwetu? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa sasa imefaulu kumpata mwekezaji ambaye amejenga kiwanda cha kuchakata mazao ya uvuvi kwenye Mji wa Sumbawanga. Kiwanda hiki hivi karibuni kitaanza uchakataji wa mazao ya uvuvi, lakini pia Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili pia kuwekeza kwenye maeneo ya ukanda mzima wa Ziwa Tanganyika kuanzia Kigoma kuja Mkoa wa Katavi mpaka Rukwa.

Kwa hiyo, Serikali tunaendelea na uhamasishaji na wawekezaji wakipatikana tutawapeleka kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ili waweze kuwekeza zaidi. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imejenga kwa mapato yake ya ndani kituo cha afya chenye hadhi ya hospitali eneo la Kalema, Kata ya Ikola, kituo hicho kimekamilika, tatizo lililopo ni ukosefu wa wataalamu na vifaa tiba.

Je, ni lini Serikali itawaunga mkono kwa kuwapelekea vifaa tiba na wataalamu ili kile kituo kianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze sana halmashauri hii kwa kujenga kituo cha afya kwa mapato ya ndani, lakini nimwakikishie kwamba katika ajira ambazo zinaendelea hivi sasa ambazo kufikapo Julai Mosi watumishi watapelekwa katika vituo vyetu tutahakikisha kituo hiki pia kinapelekewa watumishi ili kianze kutoa huduma. Lakini katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambavyo vitapelekwa ili kituo hiki kiendelee kutoa huduma za afya, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa idadi ya walimu wanaojitolea ni wengi na ajira zinapotoka huwa hawapati nafasi ya kuajiriwa hawa ambao wamejitolea. Halmashauri yangu ina zaidi ya walimu 60 ambao wamejitolea na waliopata ajira wamepata walimu watatu tu.

Je, Serikali haioni kwamba inavunja moyo wale walimu wanaojitolea na wanaopata ajira ni wale ambao wapo mitaani? Tunataka tupate mwongozo sahihi wa Serikali na majibu stahiki kwa wale ambao wanajitolea. (Makofi)

Swali la pili, kuna tabia ambayo imejengeka ajira zinapotolewa Halmashauri ambazo ziko vijijini zinapokea watumishi ndani ya miezi mitatu wale watumishi wote wanarudi maeneo ya mijini; Serikali haioni hii tabia ambayo imejengeka ni tabia ambayo inakuja kuua mfumo wa elimu au utumishi wa umma kwenye maeneo ya vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kuajiri watumishi wote bila kujali wanaojitolea na ambao hawajitolei. Changamoto ya kuajiri walimu wanaojitolea ilitokana na utaratibu ambao haukuwa rasmi wa kuwasilisha majina ya walimu wanaojitolea. Kwa sababu baadhi ya Wakuu wa Shule wasio waaminifu walikuwa wanatumia fursa hiyo kuingiza majina ya walimu ambao hawajitolei na mara nyingine wanaachwa walimu wale ambao wanajitolea.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo Serikali imeandaa mwongozo mahsusi na imeandaa mfumo ambao walimu wenyewe wataingia online kuji-register, kujiandikisha kwamba ni walimu wanaojitolea katika shule fulani na Serikali itafanya uhakiki na kuthibitisha kwamba walimu wale wanajitolea katika maeneo hayo. Hii itasaidia mara ajira zinapojitokeza kuona nani amejitolea kwa muda mrefu apate kipaumbele cha kupata ajira hizo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili jambo linafanyiwa kazi seriously na Serikali itahakikisha kwamba linakamilika mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili kuhusiana na walimu pia watumishi wa sekta nyingine ambao wanapangiwa katika Halmashauri za Vijijini na kuhama, kwenye utaratibu wa ajira kwa mfumo wa kieletroniki kwa sasa, tumeshaelekeza kwamba watumishi wote wa elimu au wa afya wakishaajiriwa kwenye Halmashauri hawatakiwi kuhama ndani ya angalau ya miaka mitatu tangu kuajiriwa. Unless kuna sababu ya msingi sana ya kulazimisha watumishi hao kuhama. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wale maeneo ambayo kuna watumishi ambao waliajiriwa maeneo ya vijijini na wamehamishwa kabla ya umri huo tupate taarifa hizo. Tumeshapata Ludewa tumeshapata maeneo mengine, tumeanza kushughulikia na watarejeshwa katika Halmashauri zilezile ili waendelee kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili tunalifanyia kazi, ahsante. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Niipongeze Serikali kwa kuleta ruzuku ya pembejeo. Wakulima wa zao la tumbaku mwaka jana hawakunufaika na ruzuku iliyotolewa na Serikali. Naomba kujua kwa msimu huu wa kilimo Serikali imejipangaje kuwapa ruzuku wakulima wa zao la Tumbaku?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso na wakulima wote wa tumbaku. Serikali inafanya mkokotoo wa namna gani wakulima wa tumbaku na wenyewe waweze kupata kuwa sehemu ya skimu ya ruzuku na tutatoa mawasiliano kupitia muunganiko wao wa TCJE ili waweze kuelewa namna gani na wao watafaidika katika msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana na mwaka huu wakulima wa tumbaku hatukuwaingiza kwenye mfumo wa ruzuku kwa sababu mfumo wetu wa ruzuku ulitazama zaidi mazao ya chakula kuliko mazao ambayo sio ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunatoa ruzuku kwenye pamba, tunatoa ruzuku kwenye korosho hatutoacha kuwapa ruzuku wakulima wa tumbaku kama wakulima wengine katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Niipongeze Serikali kwa kuleta ruzuku ya pembejeo. Wakulima wa zao la tumbaku mwaka jana hawakunufaika na ruzuku iliyotolewa na Serikali. Naomba kujua kwa msimu huu wa kilimo Serikali imejipangaje kuwapa ruzuku wakulima wa zao la Tumbaku?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso na wakulima wote wa tumbaku. Serikali inafanya mkokotoo wa namna gani wakulima wa tumbaku na wenyewe waweze kupata kuwa sehemu ya skimu ya ruzuku na tutatoa mawasiliano kupitia muunganiko wao wa TCJE ili waweze kuelewa namna gani na wao watafaidika katika msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana na mwaka huu wakulima wa tumbaku hatukuwaingiza kwenye mfumo wa ruzuku kwa sababu mfumo wetu wa ruzuku ulitazama zaidi mazao ya chakula kuliko mazao ambayo sio ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunatoa ruzuku kwenye pamba, tunatoa ruzuku kwenye korosho hatutoacha kuwapa ruzuku wakulima wa tumbaku kama wakulima wengine katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ilishatenga shilingi milioni 50 na wananchi wamejitolea kwa nguvu zao, wamefyatua tofali takriban milioni moja kwa kata nzima.

Je, Serikali imejipanga vipi kuwasaidia, kuwaunga mkono ili waweze kukamilisha mabweni hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Shule ya Bulamata watoto wanaosoma wanasoma takriban kilometa tano mpaka zaidi ya kilometa tano kuifikia shule hiyo.

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba ni wakati muafaka wa kuwasaidia hawa vijana kupeleka fedha na kuwasaidia gari ambalo litakuwepo pale kwenye hiyo shule ili liweze kusaidia huduma kwenye emeo la shule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwaunga mkono wananchi katika jimbo lake, ni kwamba jambo hilo Serikali tunalifanya. Moja katika hatia ya kwanza ni tuliwaagiza Halmashauri kutenga fedha za ndani, lakini na sisi, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutatafuta fedha kwenye vyanzo vingine ili tuweze kuongeza na kuwasaidia wananchi hao ambao wamejitahidi kwenye ujenzi wa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo ni sawasawa tu na swali lake la pili la msingi, kwamba tutatafuta fedha ili tuweze kuongeza na kumalizia shule yao na hayo mabweni, ili sasa watoto waanze kusoma kutokana na umbali huo. Ahsante sana.