Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe (33 total)

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Kavuu yanafanana kabisa na matatizo ya Jimbo la Magu na hivi karibuni kupitia mpango wa REA wameweza kuweka umeme katika Kata yangu ya Usevya katika Jimbo la Kavuu. Hivi karibuni umeme umeanza kuwaka takribani wiki tatu baada ya REA kukamilisha ujenzi wake pale lakini mpaka sasa hivi wananchi hao hawana umeme ikiwemo pamoja na mimi. Je, kwa kuwa wananchi wale walikuwa na hamu na umeme huo ambao haupatikani, Serikali inasema nini kuhakikisha kuanzia sasa umeme unapatikana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba yapo maeneo ambayo hayana umeme hadi sasa. Kwa ridhaa yako niombe kusema kwamba nitakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuyatambue kwa kina maeneo ambayo hayana umeme na tuyafanyie kazi ili wananchi wapate umeme.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nasikitika kwamba, pesa hizi ni za bajeti ambayo tunakwenda kumalizia, naomba nijue ni lini pesa hizi zitatoka ziende zikafanye kazi hiyo kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, kwa uzoefu unavyojionesha pesa hizi zinaweza zikatoka mwisho wa bajeti yaani Juni 30. Je, pesa hizi zinapotoka zinakwenda wapi?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, pesa hizi ni za bajeti ya mwaka huu 2015/2016, lakini kama nilivyojibu awali, miradi mingi sana ya maji katika kipindi hiki toka tunapotoka katika mwaka wa uchaguzi mpaka hivi sasa, ni miradi mingi sana siyo katika Jimbo la Kavuu peke yake, isipokuwa miradi mingi sana imekuwa ikisuasua kutokana na upelekaji wa fedha. Hata hivyo Serikali imefanya juhudi kubwa sana mara baada ya kukusanya mapato makubwa Serikalini kuhakikisha kwamba maeneo mbalimbali ambayo miradi ilikuwa imesimama sasa ianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba Wizara ya Maji kwa kupitia Wizara ya Fedha, maeneo mbalimbali ambayo miradi mingine ilikwama sasa hivi imeshaanza kufanya kazi. Imani yangu kubwa iliyoko ni kwamba Ndugu yangu Mbunge ambaye najua siku zote ulikuwa ukipambana Jimboni kwako katika maeneo haya, kwa kipindi hiki tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo, Serikali iweze kupeleka maeneo yote ambayo miradi ilisimama ilimradi, miradi ikamilike katika mwaka huu wa fedha,
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, hata katika ripoti za Mkaguzi wa Serikali kuna miradi mingine inakwama kwa sababu fedha zinafika mwishoni. Kwa hiyo, niwaombe hasa ma-engineer wetu kule site kwamba, wajipange vizuri kiasi kwamba pesa hii itakapofika wahakikishe usimamizi unakwenda kwa haraka ilimradi wananchi wa Jimbo la Kavuu waweze kupata huduma za maji katika maeneo yao.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa kutambua uwezo wa wajasiriamali wa Mkoa wa Katavi ambao bado wana viwanda vidogovidogo, lakini kwa kuwa, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inalenga uchumi wa kati, je, Serikali inasema nini kuwekeza sasa katika viwanda vikubwa kutokana na malighafi zinazopatikana Mkoa wa Katavi ili tuweze kufikia malengo ya uchumi wa kati?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kwa kuwa, Mkoa wa Katavi una wanyama wengi wafugwao hususan ng‟ombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kiwanda cha kusindika mazao ya ng‟ombe, hasa katika Jimbo la Kavuu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu haja ya kujenga Kiwanda cha Nyama Katavi na Sumbawanga kule, Mheshimiwa Mbunge Wataalam wa Wizara yangu leo wako hapa full team, unione na uwasiliane na Mheshimiwa Zungu kuna Mwekezaji anatafuta mahali pa kujenga viwanda vikubwa vya nyama, nikupe offer leo hii tuonane, huyo mwekezaji aende Katavi na Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kujenga viwanda vikubwa. Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe, ananishawishi kusoma hotuba yangu kabla ya wakati! Mkakati wetu ni kuhakikisha viwanda vidogo sana tunavipa nguvu viwe viwanda vidogo na viwanda vidogo viwe viwanda vya kati na viwanda vya kati viende viwe vikubwa, tunafanya business graduation. Kwa hiyo, tutawapeleka taratibu hasa wazawa, kusudi twende sambamba tufike kwenye viwanda vikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi kama kuna malighafi ambayo inatupa faida ya kiulinganisho niko tayari wakati wowote tusaidiane Wabunge na Serikali ya Katavi, mniambie nini kinawapa faida ya kiulinganisho ili kusudi nilete wawekezaji. Wawekezaji wote watakuwa hapa mpaka Jumatatu, kila mtu ajichukulie wa kwake pale nje.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi napenda kwanza kumshukuru ameweza kueleza kwamba kuna fedha ilitengwa kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 ambayo bajeti yake inakwisha mwezi wa Sita tarehe 30; na hizi fedha amesema Serikali imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 42 kwa kiwango cha changarawe ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo ni shilingi milioni 246. Swali langu, je, fedha hizo zitatoka kabla ya Juni 30 mwaka huu? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na kufahamu changamoto za barabara zilizoko katika Majimbo yetu hasa katika mikoa yetu hiyo ya pembezoni, tatizo siyo barabara anayoniambia ambayo imetengewa fedha ya kutoka Kibaoni kupitia Majimoto mpaka Kasansa na kwenda Inyonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la barabara nilizokuwa nikisema ni ambazo ziko chini ya Halmashauri na concern yangu na ya wananchi ni kwamba Halmashauri hizi mpya zikiwemo na mikoa mingine mipya ya Simiyu, Geita pamoja na Katavi kwamba hazina bado uwezo wa kuwa na hizo barabara. Swali langu la msingi hapa ni kwamba Serikali iangalie sasa namna ya kutafuta fungu la dharura kwenye barabara zilizoko ndani ya Halmashauri. Kwa mfano, kwangu, barabara ya kutoka Mamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kikwembe, naomba ufupishe tafadhali.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Kwa mfano, kule kwangu, barabara ya kutoka Mamba kwenda Kabunde, barabara ya kwenda mpaka Maimba, barabara ya kutoka Lunguya mpaka Majimoto; barabara hizi hazipo kabisa. Naomba Serikali iangalie namna ya kupata fungu la ziada kuweza kutoa hiyo kwa ajili ya kutengeneza. Naomba kupata majibu ya maswali hayo, lini fedha hizo zitapatikana na ningependa zitakapopatikana tupewe taarifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge anayezungumza hapa, ni Makamu Mwenyekiti wangu wa Kamati yetu ya TAMISEMI na Utawala Bora. Kwa hiyo, najua kwamba anajua wazi namshukuru sana, ameshiriki kwa kiwango kikubwa katika mchakato wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fedha kwamba lini zitakwenda? Hili hata jana nililisema; nikasema, miradi mingi sana kwa kipindi kilichopita ilisuasua. Jana nilifanya reference siyo kwa miradi ya barabara peke yake isipokuwa hata miradi ya maji na miradi mbalimbali ya elimu, miundombinu ya madarasa, yote ilikwama kwa sababu makusanyo ya fedha yalikuwa siyo mazuri. Nilisema pia kwamba kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga, ndiyo maana tunaona kila mwezi makusanyo ya mapato yameongezeka. Sasa hivi mradi mingi sana iliyokuwa imesimama, inaanza kutengewa fedha za kuanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kwamba katika kipindi hiki Mheshimiwa Kikwembe kabla hatujamaliza, basi mafungu hayo na wenzetu wa Hazina watatuhakikishia kwamba wanapeleka fedha zinazokusudiwa ili mradi wananchi waweze kupata huduma hii ya barabara. Kwa hiyo, nakiri kweli fedha hazijafika, lakini Ofisi ya Rais (TAMISEMI) inaendelea kufanya harakati na Ofisi ya Wizara ya Fedha ilimradi fedha zile kama zimetengwa katika bajeti ya fedha mwaka huu unaomalizika, iweze kupatikana na miradi iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Halmashauri mpya ni kweli; na kweli Jimbo lako ni Halmashauri mpya pale na siyo hilo isipokuwa ni Halmashauri mbalimbali. Ndiyo maana katika bajeti yetu ya mwaka huu mtaona tumetenga karibu shilingi bilioni 240 plus. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunazifikia Halmashauri katika miundombinu ya barabara. Bajeti zile tumetenga kwa sababu sehemu nyingine kuna barabara korofi na barabara zenye vikwazo, bajeti yake nayo tumeitenga hivyo hivyo karibu shilingi bilioni 45. Lengo letu kubwa ni kuangalia jinsi gani tutafanya kwenye Halmashauri ambazo ziko katika changamoto kubwa ili tuweze kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kusema kwamba hapa kuna fedha za dharura; kesho na kesho kutwa zitatoka, isipokuwa, kama Serikali, tunachukua ombi hili na lengo ni Mikoa ya Pembezoni yote, siyo Jimbo la Mheshimiwa Kikwembe peke yake bali Mikoa yote ya Pembezoni imekuwa na changamoto kubwa sana, lazima Serikali tuliangalie kwa jicho la karibu ili kuweza kutatua matatizo ya wananchi.
MHE.DKT. PUNDECIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali yetu ina lengo jema la kuunganisha barabara za mikoa ili kuharakisha maendeleo katika nchi yetu yote; na kwa kuwa ujenzi wa barabara nyingi umekuwa ukikumba nyumba nyingi zinazokuwa pembezoni mwa barabara ambazo zinawekewa „X’ kwa mfano, kutokea Ilalangulu kwangu kule mpaka Kasansa na fidia mara nyingi wanatathmini pale ambapo pesa zinakuwa hazijapatikana lakini pindi zinapopatikana wanakuja kuwalipa wananchi fidia ile ya mwanzo:-
Je, Serikali inasema nini kufikiria namna ya kutathimini upya fidia za wananchi mara ujenzi unapoanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Fidia ile ya zamani na hata ya sasa ya mwaka 1999 imeeleza wazi kwamba baada ya kufanyiwa tathmini na kama fidia itachelewa kulipwa kuna penalty zimewekwa. Kwa hiyo, malipo yanalipwa zaidi na kuna utaratibu, malipo yanaongezeka kwa kadri muda unavyoongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hiyo sheria tuliiweka kwa makusudi kabisa tukijua wakati mwingine uwezo wa Serikali wa kulipa kwa pamoja ni mdogo, maana miradi mingi inaihusu Serikali. Kwa hiyo, katika kuwafidia wale ambao wanacheleweshwa kulipa, kuna utaratibu huo wa kufanya mahesabu mapya kwa kuzingatia kipindi ambacho amecheleweshwa kulipwa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge hili litatekelezwa pindi tutakapoanza kupata nguvu ya kulipa fidia katika eneo husika.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, suala hili ni nyeti na linagubikwa na mambo mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo imani mbalimbali za kidini, mila na desturi. Je, ni lini sasa White Paper hiyo itapitishwa katika makundi mbalimbali ya jamii, ili iweze kupata maoni yake mbalimbali na kuweza kutungwa Sheria inayoweza kumlinda mtoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili; chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuwa, mpaka sasa hivi elimu yetu ya mpaka sekondari ni bure. Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kuongeza elimu ya kidato cha bure ikawa mpaka form six ambayo ni elimu ya lazima, ili tuweze kuvuka ule umri wa miaka 18 ukizingatia sasa hivi watoto wameanza kusoma wakiwa chini ya miaka minne mpaka mitano? Je, Serikali inasema nini kuhusiana na hilo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge, napenda kumjibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba, kila safari tunaanza kwa hatua kwa hiyo, Serikali imeanza kutoa elimu bure na hatua ya kwanza tumeanza na elimu msingi mpaka kidato cha nne. Kuna changamoto ambazo zinajitokeza katika kutekeleza hii, kwa hiyo, tupate nafasi tutatue changamoto, lakini mawazo na mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge ni jambo la msingi ambalo Serikali italiangalia baada ya kuwa tumeweka vizuri hii ambayo tumeanza nayo kwa awamu ya kwanza.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa napenda niishukuru Serikali kwa kukiri udhaifu mbalimbali ambao unaweza kuwa unasababishwa na ajali zinazoweza kuwa zinatokea ambazo zimeelekezwa kwenye swali la msingi ikiwemo ni pamoja na uzoefu na uchakavu wa miundombinu. Swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba wote tunafahamu Tanzania na China ni nchi marafiki na bidhaa nyingi za biashara karibu asilimia 95 zikiwemo pikipiki za bodaboda zimekuwa zikitoka China.
Swali langu, je, ni kwa nini Serikali sasa isione namna ambayo inaweza ikafanya mazungumzo na Serikali ya China kwa kuangalia bidhaa ambazo zinaingizwa zikiwemo za bodaboda na vitu vinginevyo ili Serikali ya China ama kupitia makampuni yanayoagiza hizi pikipiki kuweza kuchangia katika zahanati zetu kama vile ambavyo wawekezaji wengine wanavyofanya katika kutoa huduma za jamii? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, pamoja na kuanzishwa na kuletwa hiyo Sheria ya Bima, je, Serikali haioni pamoja na hayo yote, kuiomba na kufanya mazungumzo na Serikali ya China pia katika kusaidia kuongeza vifaa tiba? Kwa sababu bima peke yake haimsaidii mwananchi aliyekatika miguu miwili ama mmoja kuweza kutibiwa na bima, bado atahitaji kununua mguu wa bandia na vitu vinginevyo na hospitali za Serikali yetu bado hazina uwezo katika wa kuwa na vifaa kama hivyo. Je, hawewezi wakafanya mazungumzo ili kuweza kupatiwa huduma hasa za afya ambazo zinaweza zikaenda moja kwa moja vijijini kwa wananchi wetu? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Watengenezaji wa pikipiki na magari yao yanakidhi viwango na TBS inathibitisha. Tatizo kubwa la ajali za bodaboda au hizi gari aina ya Noah ni kwa ajili yetu sisi watumiaji. Watu wanaendesha bodaboda wakiwa wamelewa, wanapakiana watano mpaka sita, huwezi kumlaumu mtengenezaji. Hata chakula, ukila kilo 10 za pilau zitakudhuru. Kwa hiyo ni juu yetu sisi Watanzania tufuate masharti ya kutumia hivyo vifaa sio tatizo la Mchina.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kitaalamu ajali inaweza ikasababishwa na matatizo yanayoweza kujitokeza katika ngazi nne tofauti. Katika ngazi ya mtumiaji, katika ngazi ya chombo, lakini pia katika mazingira ambapo ajali imetokea kwa maana ya design of the road na vitu kama hivyo.
Sasa matatizo yote haya imeonekana kwa kipindi kirefu yanasababisha ajali za barabarani ambazo zinasababisha maumivu kwa watumiaji ama muda mwingine zinasababisha vifo. Yote haya ambayo ni madhara yanayotokana na ajali za barabarani mwisho wa siku yanakwenda ku-impact mfumo wa afya, yanaenda kuongeza mzigo wa gharama kwenye kutoa huduma za afya. Ndiyo maana Serikali sasa inakuja na mkakati wa kufikiria namna ya ku-charge gharama fulani kwenye kila chombo cha moto ambacho kitaingia barabarani kabla hakijaingia barabarani. Tozo hiyo itakuwa inatozwa kila mwaka, lakini bado tuna mazungumzo ndani ya Serikali kuona kama jambo hili litakubalika ili tuweze kulileta sambamba na mapendekezo mengine kwenye Sheria ya Single National Health Insurance ambayo tunatarajia kuileta hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kwamba wote wanaopata ajali wawe na bima za afya ili waweze kupatiwa huduma pale ambapo inajitokeza wamepata matatizo yoyote ya kiafya. Lakini hatuwezi kuchukua mzigo wa magonjwa ya watu wetu tukaurundika kwa Wachina eti kwa sababu wanaunda vifaa vya moto, hapana. Jukumu la kutoa huduma za afya zilizo bora kwa Watanzania ni la Serikali yao na hatujalishindwa bado.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sitakuwa mbali sana na wanaohitaji miji ipandishwe hadhi. Kwa kuwa kata ya Majimoto sasa imekuwa kubwa kiasi ambacho inatakiwa kupandishwa hadhi na tumekwishaleta maombi katika Wizara inayohusika. Je, ni lini sasa maombi hayo yatashughulikiwa ili kata ya Majimoto iwe Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kupandisha hadhi na naomba nijibu na Wabunge wengine kwa sababu nimeona wengi wamesimama humu ndani na concern yao wote inafanana na ndiyo maana tuliunda kikosi kazi kwenda kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo kwako Majimoto Mheshimiwa Mbunge. Jambo lile sasa liko ofisini kwetu linafanyiwa uchambuzi wa kina, naomba nikutoe hofu kwamba uchambuzi ule wa kina ukishafanyika basi maamuzi sahihi yatafanyika kwa mujibu wa sheria ambapo Waziri mwenye dhamana amepewa mamlaka hayo. Naomba vuta subira tu wakati kazi hii inawekwa vizuri lakini siyo Majimoto peke yake nikifahamu Dongobesh kule na maeneo mengine wote concern yao ni hiyo hiyo, kwa hiyo kama Serikali inafanyia kazi kwa upana wake suala hili.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira yaliyopo Nsimbo yanafanana kabisa na mazingira yaliyopo katika katika Jimbo la Kavuu na kupitia initiative ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara katika Jimbo la Kavuu alituomba tuanzishe Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe kufuatia kuwepo na kadi za CHF kwa sababu za NHIF hazitumiki kule.
Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu, kutokana na juhudi za wananchi wa Jimbo la Kavuu kuwapatia gari la wagonjwa ambao wamekuwa wakitumia umbali mrefu kutoka Mpimbwe kwenda Mpanda na sasa tutumie katika Jimbo la Kavuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi sana huwa nazungumza hapa Bungeni kwamba, issue ya gari la wagonjwa ni vema kwanza tukai-allocate katika bajeti zetu za kila mwaka, hilo ni jambo la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu sana Mheshimiwa Dkt. Kikwembe anavyohangaika kwa Jimbo lake, ndiyo maana hapa juzi alikuwa anahangaika tupeleke huduma za afya pale na ndiyo maana tulimhakikishia pamoja na Waziri wa Afya, na Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda pale na akatoa ahadi, tutaenda kufanya ukarabati mkubwa wa kituo chake cha afya kwa kuingiza fedha nyingi ili akina mama na watoto sasa waweze kupata huduma nzuri, hasa huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Kikwembe mahitaji yako ambayo umeongea mbele ya Waziri Mkuu, Serikali imeyachukua kwa ujumla wake, hata hivyo, naomba nipendekeze, kwa Wabunge mbalimbali katika suala la ambulance lazima tuliainishe katika bajeti zetu, likishakuwepo katika bajeti tunapata msingi mzuri wa kulifanya jambo hilo katika utekelezaji wake.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, suala hili ni la kikatiba kwa maana ya kwamba linahusisha Serikali ya wananchi kwa maana ya Serikali za Vijiji. Kwa kuwa wananchi wamekuwa wakichangia takribani 20% ya maendeleo katika maeneo yao ya vijiji. Je, Serikali sasa inafikiria nini kupeleka pesa za maendeleo kwa wakati ili wananchi hawa waweze kujua sasa ile miradi ni mali yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli dhana hii inapeleka fursa kwa wananchi na ni kweli tumeshuhudia wananchi katika maeneo mbalimbali wakishiriki vyema katika kutekeleza dhana hii kwa kujitolea katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata hivyo, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kwa kipindi cha sasa na nina maana itakapofika mwezi wa Sita mtaona jinsi gani imepeleka nguvu kubwa sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika sekta ya afya mwaka huu peke yake fedha tulizopeleka katika mifuko mbalimbali ikiwepo Basket Fund ni zaidi ya shilingi bilioni 79 na sasa hivi tumeshapeleka fedha za quarter ya nne ambapo tunaenda kukamilisha shilingi bilioni 106, hii ni sekta ya afya peke yake. Tumefanya hivyo pia katika sekta ya elimu na maeneo mbalimbali na juzi juzi hapa tumenunua vifaa vya maabara katika maabara zote zaidi ya 1,000 ambapo vyote vilikuwa vinagharimu shilingi bilioni 16.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna fedha nyingine za LDGD ambazo zimeenda moja kwa moja ambazo hazina ukakasi katika kuzitoa kwake. Serikali imepeleka hela za kutosha na ni mara ya kwanza baada ya miaka minne iliyopita tulikuwa hatufanyi hivyo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuweka nguvu kubwa ya kutosha, lengo kubwa ikiwa ni kuwawezesha wananchi kutekeleza miradi yao.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, katika majibu yake ya msingi amesema kwamba watalipwa pale maeneo watakapoyahitaji, lakini tukiangalia kuna maendeleo yanayoenda kufanywa sasa hivi, kwa mfano katika barabara yangu ya Kibaoni, Usevya, Mbede, Majimoto, Mamba, Kasansa mpaka Mfinga ambako tutatekeleza REA III. Ni lini wananchi hawa wenye alama za ‘X’ za kijani mtawalipa pesa zao ili waweze kufaya marekebisho ya nyumba zao waweze kuweka umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Ulega, ni kwamba kila tunapotaka kuanza kujenga barabara fedha zinazotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinaunganishwa vile vile na fedha za kulipa fidia katika maeneo ambayo tunatarajia kuyajenga.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe na wananchi wa Kavuu kwamba tutawalipa fidia wale wanaostahili kulipwa fidia mara tutakapopata fedha za kuanza kujenga barabara husika.
MHE. DKT. PUDENSIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumweleza kwamba, pamoja na kwamba Serikali ina nia njema ya kuweka sekondari za wasichana kila tarafa na kwa sasa katika Jimbo langu ama Mkoa wa Katavi kila tarafa bado haijawa bado na Sekondari za form five na six.
Je, haoni sasa kuna umuhimu na ulazima wa hii Shule ya Sekondari ya Mpanda kuanza sasa kwa kidato cha kwanza mpaka cha sita ili tuweze kuzuia mimba za utotoni kama sera na Serikali inavyosema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama Serikali, tunaona umuhimu hasa wa kupunguza mimba za utotoni na kwa wasichana ambao Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiwapigania hapa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kama ikiwezekana basi mchakato huo utaanza katika vikao husika kuanzia Baraza la Madiwani then itaenda katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa, then itafika kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya sekta ya elimu na hapo akiridhia jambo hilo basi litaanza. Kwa hiyo, hili jambo halina mashaka, ni suala zima la kuangalia ni jinsi gani tutafanya.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunasisitiza na Serikali inaweka nguvu ya kutosha na kama kuna changamoto kubwa, tutaona jinsi gani tutafanya ikiwa hata kuanzisha shule nyingine mpya zenye ubora unaofanana na ule. Lengo kubwa ni kuhakikisha watoto wetu hasa wasichana waweze kusoma katika mazingira rafiki tupate viongozi na wataalamu wa baadaye.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Wakati tunapitisha bajeti tuliongelea suala la kodi ya majengo kwamba nyumba za kawaida zitaanzia shilingi 10,000 na nyumba ambazo zinakuwa kwenye level ya maghorofa zitaanzia shilingi 50,000. Lakini cha kushangaza mpaka sasa hivi tunaona kodi hizi hazina uwiano, unakuta kati ya nyumba na nyumba mwingine anapelekewa kodi ya shilingi 10,000 mwingine shilingi 30,000, mwingine shilingi 40,000.
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu hizi kodi na uwiano ambao si sawa kati ya Halmashauri ama Manispaa ndani ya Manispaa moja unakuta kata nyingine bei ni tofauti na kata nyingine bei ni tofauti, ama Halmashauri moja ni bei tofauti na Halmashauri nyingine ni bei tofauti.
Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kodi ambayo tuliipitisha sisi wenyewe Wabunge wakati wa bajeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kodi aliyoiongelea ya majengo inayokusanywa tofauti kutoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine ni kodi iliyopitishwa na Bunge lako tukufu kwa ajili ya mwaka 2016/2017, ndiyo hiyo ambayo inakuswanywa na inaonekana kuna utofauti kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, kodi ambayo Bunge lako tukufu imeipitisha mwaka huu wa 2017/2018 ni kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Kikwembe; kwa nyumba za kawaida ni shilingi 10,000 na nyumba za ghorofa kama ambavyo ilielezewa kwenye Finance Act ni shilingi 50,000. Kwa hiyo, utofauti unaoonekana ni ile tu wananchi wetu walichelewa kulipa kodi ya majengo ya mwaka 2016/2017 lakini kwa mwaka 2017/2018 kodi itakayotozwa ni kama ambavyo Bunge lako Tukufu limepitisha.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na swali la Mheshimiwa Kapufi kuhusiana na hizi kodi za zimamoto, ninachojiuliza na wananchi wanachojiuliza hasa wa Jimbo la Kavuu wanataka kujua, kwa nini hizi tozo zimeanza kutozwa sasa, na watu gani wameshirikishwa? Kwa sababu zinaoneka zimeibuka, hata kama zilikuwepo kwa ujibu wa Sheria, zimeibuka kiasi kwamba hata wale wenye guest houses sasa hivi zimamoto wamekuwa wakiwavamia na kuwa-charge hizi kodi. Kwa hiyo, tunaomba ufafanuzi ni gazeti namba ngapi zilizoruhusu hizi kodi zianze kutumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya awali kabisa ni kwamba tozo hizi zinatokana kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ambazo tumejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu Mheshimiwa Mbunge ameonyesha interest ya kufahamu namba ya GN ambayo siponayo hapa hiyo namba nitampatia, lakini ni kwamba tozo hizi zinafanyika kwa mujibu wa regulations ambayo niliisema pale awali ya The fire and rescue force fire precaution in buildings regulations ya mwaka 2015. Hivyo kinachofanyika hapa hata ilikuwa ifanyike hapo awali lakini utekelezaji wa Sheria unaendelea kuwa ni halali kwa sababu ilikuwepo Kanuni hii na sasa ndiyo utekelezaji wake unafanyika.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa kwa sababu mengi ni ya ukweli. Ni kweli nyumba nyingi hazijafanyiwa uthamini lakini zinatozwa hizo kodi na kodi zinazotozwa ni kwamba siyo zile tulizopitisha za shilingi 10,000 wala shilingi 50,000 ni zaidi ya shilingi 300,000 kwa nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini. Kwa hiyo, nashukuru kwa jibu lake ambalo amelisema ni la ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye swali langu, kwa kuwa nyumba nyingi za watu binafsi hazina BoQ kwa sababu wanajenga kwa kujidunduliza, leo mwananchi akipata shilingi 50,000 anasema ananunua cement, kesho kutwa akipata shilingi 100,000 atanunua bati, haweki kwenye kumbukumbu kwamba mwisho wa siku ametumia shilingi ngapi; na hiyo nyumba Serikali haifanyii uthamini, lakini kesho inampelekea bili ambayo wao uthamini wao aidha ni wa macho ama ni wa nini, bila kuangalia kumbukumbu za yule mtu binafsi.
Je, Serikali inasema nini na inatoa mwongozo gani thabiti kwa kutoa majawabu ili wananchi hawa ambao ni kama mimi binafsi, ambaye siweki kumbukumbu, nimejenga nyumba na leo nakuja kufanyiwa uthamini ambao ni zaidi ya pesa ambayo nakuwa nimeweka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la pili, tangu utaratibu huu umeanza, je, Halmashauri zimefaidika kwa kiasi gani? Kwa sababu sehemu ya Halmashauri sasa hawakusanyi mapato, mapato yanakusanywa na TRA na pia majengo mengi, maboma yako kwenye Halmashauri huko ambayo ni zahanati na mashule. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Kavuu kuna maboma ya shule 69 hayana mabati mpaka kesho, Halmashauri zimefaidikaje na hizi pesa zinazokusanywa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwenza kuhusu uthamini wa nyumba, uthamini wa nyumba unafanywa na wathamini wenye weledi mkubwa na hivyo thamani inayoelezwa ya kila nyumba imefanyiwa na wathamini hawa wenye weledi kwenye kazi yao na wenye uzoevu wa kutosha. Hivyo kila jengo linapewa thamani yake kulingana na bei ya soko la jengo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu Halmashauri zimefaidikaje? Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba madhumuni ya kodi hii ya majengo kuhamishiwa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa ni kuleta ufanisi katika ukusanyaji, lakini pia katika matumizi ya kodi hii ya majengo. Lengo la Serikali ni jema na kwenye ufanisi tunafanya vizuri. Kuanzia Julai mpaka Desemba tumeshakusanya zaidi ya shilingi bilioni 16.7 na kulingana na sheria yetu ya fedha ilivyoletwa na kupitishwa na Bunge lako Tukufu, ni kwamba pesa hizi zitarejeshwa kulingana na bajeti za Halmashauri husika zilizopitishwa na Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu kwa nia njema inafanya hayo yote.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilitaka kufahamu kutokana na maswali yaliyokuwa yanaulizwa, Mheshimiwa Mbunge aliyeketi muda siyo mrefu ameongea kuhusu Waheshimiwa Wabunge kutelekeza watoto. Sasa nilitaka kuuliza, Waheshimiwa Wabunge hawa wanatelekeza watoto kwa Waheshimiwa Wabunge wenzao ama nje ya Wabunge? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana suala la kutelekeza watoto katika Bunge limekuwa ni kubwa sana. Hili nalirudisha katika kiti chako sasa uweze kuangalia utaratibu mzuri wa kuweza kulishighulikia. (Kicheko)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa kuwa benki hii ukiitazama na kwa namna ambavyo anaongea kwamba inaelekea kupata hasara ni kwamba benki hii inaweza ikafa na Serikali ilikwishaahidi kuinusuru kwa kuipatia mtaji. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya kuipatia mtaji ili benki hiyo iweze kufanya kazi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sharti ambalo tulipewa na Serikali, nikiimanisha Waziri wa Fedha ni kwamba tufanye forensic audit ambayo tuliifanya mwaka jana na hiyo actually ndiyo imetusaidia tukabaini upungufu ambao ulionekana, kwa hiyo na Waziri wa Fedha anatusikiliza. Naamini kwa sababu tumeshafanya forensic audit, tumeteua Bodi mpya ya Benki lakini pia tumeweka Menejimenti mpya, kwa hiyo naamini Waziri wa Fedha atatimiza ahadi ya Serikali ya kuipatia mtaji benki kama walivyoahidi mwaka 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie tu Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwamba licha ya kuwa tunategemea kupata fedha kutoka Serikalini, lakini tayari tumeanza mazungumzo na Benki nyingine ambazo sitaki kuzitaja ziko tayari kufanya partnership na Benki ya Wanawake ili tuhakikishe kwamba huduma za Tanzania Women Bank zinatolewa pia katika Benki hiyo, kwa hiyo, tunakwenda vizuri na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pia iko tayari kuhakikisha inawezekeza katika Benki ya Wanawake, kwa sababu hii ni Benki ya wote na wanufaika wakubwa wa benki hii ni wanawake. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE.DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameongea kuhusu maeneo ya hifadhi ambayo yamekuwa yakihifadhiwa na Serikali lakini pia vyanzo vya maji. Kwa kuwa, wananchi wangu kwa kupitia Halmashauri ya Mpimbwe, Jimbo la Kavuu, wananchi wangu wa Kata ya Itobanilo; vijiji vya Senta Unyenye, Amani na Lunguya wamekuwa wakitumia maji ya Mto Kavuu ambao unapakana na mbuga ya Katavi na askari wa Katavi wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi wakati vijiji hivyo hawana maji na tumekuwa na ujirani mwema wa kutumia.
Je, Serikali inasema nini kuhusu hawa watu wa National Park kupiga wananchi hovyo wakiwa wanaenda kutafuta huduma za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wananchi wa kata hizo alizozitaja pamoja na hivyo vijiji vimekuwa vikitegemea sana maji ya eneo lile ambalo amelisema karibu na mbuga yetu ile ya Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Sheria zetu za Wanyamapori Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 hairuhusu wananchi kuingia katika maeneo ya hifadhi bila kibali. Kwa hiyo, hivi sasa ambacho kinaweza kufanyika ili kunusuru matatizo hayo, kwa sababu tuna sera ile ya ujirani mwema nitaomba tukae na Mheshimiwa Mbunge, tukakae na wananchi wenyewe ili tuweze kuangalia ni namna gani tunawapelekea maji katika maeneo ya vijiji vinavyohusika badala ya kuingia kwenye hifadhi ambapo wanakuwa wanahatarisha maisha yao na pia hali wataharibu hifadhi kitu ambacho ni kinyume na sheria. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane katika kutatua tatizo hili.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Kavuu na Mkoa mzima wa Katavi, kutokana na jiografia yake imekaa kama umbo la pweza. Je, Serikali inafikiria nini katika Jimbo la Kavuu, Halmashauri ya Mpingwe kuanzisha Mahakama yenye hadhi ya Wilaya kutoka kwenye hadhi ya Mahakama ya Mwanzo ili kuwanusuru wananchi kwenda katika makao makuu ya Nyonga ambayo wanapita katikati ya mbuga na kuhatarisha maisha yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yake nimeyasikia tutayafanyia kazi, na baada ya hapa namuomba tuonane katika ukumbi wa Bunge ili tuweze kuongea na nielewe hasa nini kifanyike kwa ajili ya eneo hilo. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nipate kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ina nia njema ya kupeleka nishati mbadala katika maeneo mbalimbali ya Tanzania; na kwa kuwa, Jimbo la Kavuu lina idadi kubwa ya wafugaji na kinyesi cha wanyama kinapatikana kwa wingi hasa ng’ombe, nguruwe na mbuzi. Pia, kwa kuwa, bado hatuna mtandao mzuri wa majitaka katika miji mingi ya vijijini ikiwemo Jimbo langu la Kavuu. Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kupitia taasisi za TADETO na UN Habitat katika kuanzisha miradi ya biolatrine ambayo inatumia kinyesi cha binadamu katika maeneo ya mashule, ili tuweze kupata gesi ya uhakika kutokana na kwamba sasa uharibifu wa mazingira katika Jimbo la Kavuu umekuwa mkubwa especially katika kukata miti hovyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba niulize si kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla, je, matumizi ya mkaa na gesi yapi ni bora zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba, Serikali inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa tufanye utafiti wa kutosha ili tuweze kutumia human waste kutoka kwenye pitlatrin na ku-convert kuwa energy ambayo inaweza ikasaidia matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba, Serikali iko tayari kutumia hii taasisi ya TADETO ambayo tayari imeshafanikisha miradi miwili Dar es Salaam kwa kujenga bioelectric ambayo sasa hivi inatumika kwenye sekondari mbili pale Dar es Salaam ikiwemo Sekondari ya Manzese. Teknolojia hii inatumiwa zaidi na Uganda kwenye shule za sekondari na shule za misingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake pili kuhusu yapi matumizi bora, tutumie gesi au tutumie mkaa. Ni bora kutumia gesi kwa sababu kwanza gesi bei yake ni nafuu ukilinganisha na bei ya mkaa. Kwa mfano, Dar es Salaam gunia moja la mkaa la kipimo cha kawaida ni Sh.75,000/= lakini ukienda kwenye teknolojia ya nguvu gani inapatikana katika mkaa, wataalam wameshafanya vipimo wakaona kwamba, tunapata unit 2.645 kwenye gunia la mkaa ni energy ambayo inayojulikana kwa kwa jina la Gigajoule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, unit moja ya gunia la mkaa inauzwa kwa Sh. 28,000/=, lakini ukienda kwenye gesi unit moja inauzwa kwa shilingi 18,000. Pia, ukitumia gesi tayari unakuwa umeshaokoa mazingira yetu, watu wa mazingira ukikata miti unaleta uharibifu wa mazingira ambao unaweza ukatuathiri kwenye mambo mengine kama kutopatikana kwa mvua inayostahili kwa masuala ya kilimo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maswali ya Shule za Sekondari za Wasichana katika eneo la Masasi linafanana kabisa na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mpanda iliyoko Mpanda Mjini na tumeshaleta maoni kwa Waziri wa Elimu pamoja na Waziri wa TAMISEMI kwamba shule ile ilikuwa inachukua kuanzia Form One mpaka Form Four na ikabadilishwa ikawa Form Five mpaka Form Six. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuhakikisha shule ile inachukua wasichana kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita kwa kuwa tuna shule moja tu Mkoa wa Katavi ya boarding? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwa sababu ni miongoni mwa Wabunge wachache ambao huwa wakiwa katika maeneo yao ya Jimbo ambao ni Walimu huwa wanaenda kushika chaki kwa ajili ya kusaidia watoto wetu. Naye ni Mwalimu mzuri wa masomo ya Sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba ni wajibu kuhakikisha kwamba miundombinu yote inayohusika katika uanzishaji wa ‘A’ Level inakamilika, lakini pia ithibati iweze kupatikana na Kamishna wa Elimu aweze kutoa kibali, hapo ndipo tunaposajili shule yetu kwa ajili ya kuanzisha Form Five. Kwa hiyo, naamini na shule anayoitaja Mheshimiwa Mbunge, pindi miundombinu itakavyokuwa imekamilika, Serikali haitasita kwa sababu uhitaji wa ‘A’ Level ni suala ambalo hatuna ubishi katika hilo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa tatizo kwenye swali la msingi la 323 la usafiri wa patrol kwa vituo vya polisi lipo karibu nchi nzima. Je, Serikali sasa inajipangaje kwenda kutatua tatizo hili la usafiri wa patrol katika vituo vya polisi hasa katika Jimbo langu la Kavuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama ambavyo nimesema mwanzo kwamba tuna mpango wa kuweza kuona jinsi gani tutapunguza changamoto ya vitendea kazi ikiwemo magari katika kutoa huduma za Jeshi la Polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndiyo maana sasa hivi tupo katika jitihada za kuweza kukamilisha na kurekebisha mapungufu ambayo yalijitokeza ili tuweze kusambaza magari hayo ambayo yanategemewa kusaidia kupunguza changamoto hiyo ikiwemo katika Jimbo lake, kulingana na vigezo ambavyo nimevieleza katika swali langu la msingi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Kibaoni – Majimoto - Mamba – Kasansa – Mfinga – Muze – Kilyamatundu - Mbozi imekuwa ikiandikwa sana katika vitabu vya bajeti kwa takriban miaka 10 sasa. Ni lini barabara hii ya kutoka Kibaoni - Kilyamatundu - Mbozi itafanyiwa upembuzi yakinifu na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu pia iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka 15 mfululizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwa sababu kuna wakati nimeahidi hapa kwamba baada ya Bunge hili nitakwenda eneo hili la Kavuu tuweze kuona eneo hili. Kwenye mpango mkakati wa ujenzi wa barabara, barabara hii imetajwa lakini tunajua umuhimu wa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi. Baada ya dhiki ni faraja, kweli ni miaka mingi tumesubiri barabara hii na pia kwenye bajeti yetu tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea sasa kufanya usanifu wa barabara hii na itakuwa ndiyo mwanzo wa kutengeneza barabara hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba Mkoa wa Katavi ulikuwa ni mkoa ambao ulikuwa unahitaji kuunganishwa sana. Utaona kwenye barabara ukitoka Tabora tunakuja Mpanda, ukitoka Mpanda pia tunakwenda katika Mkoa wa Kigoma, wakandarasi katika hatua mbalimbali wanaendelea ili kuonesha msisitizo kwamba Serikali imetambua umuhimu wa maeneo haya kuweza kuyaunganisha na mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimueleze tu Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwamba tumejipanga vizuri, kati ya mikoa ambayo ilikuwa bado ina shida ya kuunganishwa, huu ni mkoa mmojawapo. Nimshukuru kwa juhudi hizo, tutaendelea kuhakikisha kwamba barabara hii inapata tiba, inakuwa ni huduma kwa ajili ya kusaidia maeneo haya ambayo pia ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mazao na shughuli zingine za kuongeza uchumi wa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kurekebisha na kuvitibu visima viporo ambavyo mpaka leo havijatengenezwa.
Je, Serikali inasema nini sasa kuhusu visima vyangu virefu ambavyo vimetengenezwa miaka sita iliyopita mpaka leo havijarekebishwa, ambavyo ni, Kisima cha Tupindo, kilichopo Kata ya Mbede na Kisima cha Kibaoni ambavyo mashine zake zimedumbukia ndani na vimetumia kutengezwa takribani pesa za Serikali milioni 800?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi kubwa inayofanywa na mama yangu Kikwembe. Nimuombe tu kwa kuwa Wahandisi wote wapo bado Dodoma, labla baada ya saa saba afike na Mwandisi wake ili tuangalie namna gani tunaweza tukamsadi katika kutatua tatizo la maji.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa kweli leo nimefurahi kidogo. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri amenijibu vizuri. Naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, sera hii inalenga kutatua changamoto inayowapata wananchi kuhusu mitazamo mbalimbali lakini umesema pia sera hii inalenga kuwakopesha wanavikundi na mtu mmoja mmoja, swali langu ni kwamba; ni kwa nini sasa Halmashauri nyingi zimekuwa zikiwalazimisha wananchi wakope wakiwa kwenye vikundi vya watu watano na kuendelea, jambo ambalo kimsingi linamnyima mkopaji mmoja mmoja mwenye uwezo wa kukopa ambaye anaweza akajidhamini ili aweze kujiendeleza katika maisha yake?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, naishukuru Serikali yangu kwa sababu imeweza kuondoa riba katika hii mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri asilimia kumi, lakini, ni kwa nini sasa, bado tunasema kwamba, kwa mfano kwenye Mifuko ya Akinamama na Vijana, wazee na wanaume hawapati mikopo hii, jambo ambalo tunaweza tukawakopesha na wakaweza kuendeleza mifuko hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza kipengele cha kwanza alichouliza Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika swali lake anapendekeza ingefaa tukaanza kum-address mtu mmoja mmoja badala ya vikundi ambalo kimsingi na yeye mwenyewe atakubaliana na mimi na hata ukienda kule kwake, vikundi kwa maana ya ushirika ndiyo hasa njia ya kuweza kututoa sisi wanyonge. Naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge kuwa vyovyote, yule ambaye ana uwezo wa kuweza ku-access mabenki, window hiyo ipo, lakini katika hii pesa ambayo inatolewa na Serikali ni vizuri kwanza tukajikita katika vikundi maana tukisaidia vikundi tunasaidia watu walio wengi zaidi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, Serikali inachokifanya ni kuona namna ya kuweza kuyagusa makundi yote kwa wakati mmoja. Ndiyo maana pamoja na kwamba tunayo Mifuko ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi lakini pia tunayo mifuko maalum kwa ajili ya akinamama na vijana, lakini kundi la wazee na watu wengine ambao hawadondokei katika sifa hizo, wenyewe pia kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wanayo fursa ya kwenda kukopeshwa mtu mmoja mmoja au kupitia vikundi pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba bado hata kama kuna mzee na mtu mwingine yeyote ambaye anahitaji kupata mikopo hii, hata kama hadondokei katika kundi la vijana na akinamama lakini fursa hiyo ipo kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo ipo 19 na imekuwa ikifanya kazi hiyo kuwawezesha wananchi kiuchumi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Jimbo la Serengeti yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Kavuu hasa katika Kata za Chamalendi, Mwamapuli, Majimoto na vitongoji vyake; kumekuwa na matatizo ambayo wananchi hasa wafugaji wamekuwa wakisukumizwa na askari wa wanyamapori ndani ya Mbuga ya Katavi na wamekuwa wakipotea na mara nyingi wakiwa wakitafutwa na ndugu zao ni nguo tu zinapatikana:-
Je, Serikali inasema nini sasa kwa ujumla kuhusu askari wote wa wanyamapori wanaofanya kazi katika mbuga zote za National Park katika kuhakikisha usalama wa wale wanaowaita majangili wakati sio majangili? Kwa sababu tu wanakuwa wameingia kwenye mbuga, kwa hiyo, wataitwa majangili.
Je, Serikali inasema nini kuhusu Askari hao ambao wamekuwa wakiwateka wananchi na kuwapora ng’ombe zao na mali…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niseme tu kwamba sina taarifa kamili kwamba askari wetu wamekuwa wakiwakamata watu na kuwaingiza kwenye hifadhi halafu wanapotea moja kwa moja. Hizo taarifa hatunazo kama Serikali na kama Mheshimiwa Mbunge anazo na anao ushahidi wa namna hiyo, basi nitaomba nikae naye ili aweze kunipa hayo majina ya watu ambao wamepotea kusudi Serikali iweze kuchukua hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu namna ya kuboresha yale maeneo, naomba nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wote wanaopakana na hifadhi zetu kuhakikisha kwamba wanazingatia taratibu, sheria, kanuni na miongozo iliyopo. Hawaruhusiwi kuingia bila kibali kwenye hifadhi. Kwa kawaida ukiingia kwenye hifadhi bila kibali, ni vigumu sana kujua yupi ni jangili, yupi sio jangili. Kwa hiyo, ili kuweza kuondokana na hilo, ni kuwaomba wananchi kutoingia katika maeneo ya hifadhi ili kusudi tuondokane na hilo tatizo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Kata ya Maji Moto wameanza kuwekeza kuitikia kauli mbiu ya viwanda; na kwa kuwa hawana umeme wa uhakika; na kwa kuwa, REA Awamu ya Tatu, round ya kwanza haijulikani itaanza kutekelezwa lini katika Jimbo la Kavuu, je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuharakisha hizi tafiti zao za geothermal kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Maji Moto umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Kibaoni, Usevya, Ilalangulu na Manga vimefikiwa na umeme unaotoka Sumbawanga, lakini kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme katika maeneo hayo na kufanya wananchi katika Kata ya Kibaoni kupata hasara sana kutokana na kukatikakatika kwa umeme. Je, Serikali inawaeleza nini wananchi waliopata umeme huu ambao ni wa Kata ya Kibaoni kupata umeme wa uhakika ambao hauwatii hasara? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kushukuru maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kikwembe, lakini kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Mkoa mzima wa Katavi na hasa Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe lina shida na kero za umeme. Katika maswali yake ya msingi mawili, la kwanza ni geothermal. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, kati ya maeneo ambayo kwa kweli yanafanyiwa tafiti za kutosha katika upande wa geothermal ni pamoja na eneo la Maji Moto katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo 50 ambayo tunatarajia kuyafanyia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujua mashapo ya geothermal ni pamoja na Jimbo lake. Hivi sasa TGDC wanaendelea na kazi hiyo na mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kikwembe nampongeza sana kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na umeme wa uhakika katika maeneo ya Mheshimiwa Mbunge, Katavi pamoja na Sumbawanga, Serikali imeanza utaratibu wa kujenga njia kuu ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400. Katika maeneo ambayo tutayapatia kipaumbele sana ni pamoja na Jimbo la Kavuu ambapo maeneo ya Maji Moto ni maeneo ya kibiashara, kwa hiyo, njia kuu za kusafirisha umeme zitakamilika. na tumetenga shilingi bilioni 664 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kikwembe nampongeza sana, lakini Serikali inalifanyia kazi. Ni matarajio yetu kuanzia Januari miundombinu inaanza kujengwa.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri ametamka mradi ambao uko katika Bonde la Ziwa Rukwa lakini uko katika Jimbo langu mradi wa umwagiliaji wa Kirida ambao nilikwishaleta maombi pamoja na mradi wa Mwamapuli. Je, Serikali inakuja na kauli gani sasa kuhusiana na hii miradi ambayo tayari tulikwishawekeza pesa isipokuwa iliharibika kwa ajili ya mvua ili iweze kuendelezwa na kuleta tija kwa wananchi ambao tayari miundombinu ipo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamo wa Serikali ama kauli ya Serikali ni kuhakikisha miradi ya maji ambayo haijakamilika ni kuikamilisha na ile ambayo inahitaji ukarabati tuifanyie ukarabati katika kuhakikisha inaleta tija katika uzalishaji. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake yenye matumaini kwa sababu barabara ya kutoka majimoto Inyonga zabuni imeshatangazwa. Swali langu ni kwamba kwa kuwa barabara hii iko chini ya TANROADS na TANROADS wamesema kwamba wanatangaza zabuni ya kumpata mpembuzi na msanifu ili waweze kuianza barabara hiyo na kwa kuwa zoezi la kutangaza zabuni na mpaka kumpata mkandarasi ni la muda mrefu. Je, ni lini sasa katika maombi yangu maalum ya kilomita 2.0 katika Mji wa Usevya yatapatiwa majibu na barabara hiyo ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mkandarasi alipatikana ambaye ameweza kujenga kilomita
1.7 katika Mji wa Inyonga, lakini katika mwaka wa fedha 2018/2019 mkandarasi wa kujenga kilomita 2.5 amepatikana na yupo katika eneo la mradi. Je, ni eneo gani la mradi ambapo mkandarasi huyo yupo?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nazipokea shukurani alizozitoa, nazipokea kwa dhati, lakini pia kwa furaha nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ya usanifu kama nilivyojibu katika jibu la msingi tarehe 11 ambayo ni Jumatatu ijayo zabuni itafunguliwa na hii hakuna namna kwa sababu, harakati za ujenzi zinazingatia pia Kanuni na Sheria za Manunuzi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tupo kwenye hatua nzuri, mzabuni atakapokuwa amepatikana na sisi tutasimamia kwa umahiri ili hii kazi hii iweze kukamilika kwa wakati. Kwa hiyo, nimtoe hofu pamoja na wananchi wa Kavuu kwa ujumla kwamba sasa ujenzi wa barabara hii utakuwa umeanza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo la kilomita 2.0; eneo hili ni mwendelezo katika Mji wa Inyonga, lakini Mheshimiwa Mbunge nafahamu kwamba iko haja ya kuweka msukumo wa kujenga kipande cha barabara kutoka Kibaoni kuja kwenye Mji wa Usevya ambao ni Makao Makuu ya Halmashauri. Kwa hiyo nimtoe hofu tu kwamba, usanifu utakapokamilika na sisi tutaweka kipaumbele ili wananchi hawa wanaokwenda makao makuu waweze kuunganika vizuri na barabara ambayo sasa ukitoka Kizi kuja Kibaoni, hatimaye tuunganishe kipande hiki cha kuja Makao Makuu ya Wilaya, lakini pia sehemu ya Majimoto ambayo ina wafanyabiashara wengi na kuna sehemu kubwa ya uchumi. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi, tutazingatia haya maeneo ambayo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanaunganishwa vizuri.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa napenda niishukuru na niipongeze Serikali yangu kwa namna ambavyo imekuwa ikiwajali wananchi hasa wanaoishi vijijini na pia kuangalia namna gani ya kutatua matatizo ya wananchi. Pamoja na pongezi hizo za kupongeza Serikali yangu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; ni kwa kiwango gani Taarifa ya Wizara hizi ambazo zilikaa kama Kamati ambazo zimeweza kuja na ushauri namna gani ya kutatua matatizo ambayo hasa katika vijiji mfano katika Jimbo langu la Kavuu, vijiji vyangu ambavyo ni vijiji vya Ikopa, Itura, Luchima, Sentaunyenye, Iziwasungu, Kabunde na kwingineko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa tuna migogoro mikubwa katika kijiji cha Luchima na mpaka wa TANAPA kwa ajili ya mto wa Kavuu na nilikwishaleta maombi mwaka jana na TANAPA walikwishaanza kujenga kisima kwa ajili ya kupunguza mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kijiji cha Luchima pamoja na mpaka wao. Je, ni lini sasa hawa ndugu zangu wa TANAPA wataweza kumalizia kile kisima ili wananchi wangu wa kijiji cha Luchima waweze kuwa huru katika kufanya shughuli zao za kilimo na uvu vi bila kuingiliwa na askari wa TANAPA.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa karibu sana suala la migogoro baina ya maeneo ya uhifadhi na vijiji ambavyo amevitaja. Naomba nichukue nafasi hii kuwajulisha Wabunge wote ni kwamba taarifa hii ambayo Wizara yetu pamoja na Wizara zingine imeshiriki, itakapokuwa tayari kutumika sasa baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais tutashirikisha Wabunge na viongozi katika Serikali za vijiji vyote na Halmashauri kuangalaia mipaka mipya ambayo tutaiweka ambayo itaondoa migogoro hii ambayo imekuwepo kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu TANAPA kukamilisha mradi wa kisima cha maji, nawaelekeza TANAPA kwa sababu mradi huo walikwishaanza kukamilisha kisima hicho haraka katika mwaka huu wa fedha.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ya kutoka Kibaoni mpaka Mlowo imekuwa ikitajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia imekuwa ikitajwa kwenye kila bajeti inayopitishwa na Bunge hili. Je, kutokana na majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, barabara imekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu? Hivyo basi wanatafuta fedha ili kuja kuiwekea lami.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni hasara kuifanyia barabara upembuzi yakinifu na baadaye kuja kuitafutia fedha kwa ajili ya kuweka lami jambo ambalo utasababisha tena kuja kufanya upembuzi yakinifu mwingine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kabisa Serikali ikishafanya upembuzi yakinifu na ikafanya usanifu wa kina huwa hakuna gharama tena ya kurudia zoezi hilo kwa miaka ijayo hata miaka sita, lakini baada ya hapo ndiyo unaweza kufanya tena feasibility study upya baada ya kujiridhisha kwamba kuna mazingira ya kijiografia yaliyosababisha eneo hilo kubadilika, lakini ni ndani ya miaka mitano tunakuwa tumeshaanza kufanya utekelezaji wa miradi mbalimbali baada ya upembuzi yakinifu.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nzuri za Serikali kutaka kuhakikisha wananchi wanapata mazao yao pindi wanapokuwa wamelima vizuri lakini napenda kujua, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inafanya utafiti wa kutosha kuhusiana na aina ya mbegu na aina ya mbolea pamoja na aina ya udongo wa sehemu husika ili wananchi waweze kulima vizuri na wasiweze kupata hasara? Katika Mkoa wangu wa Katavi, Jimbo la Kavuu mahindi yameenda vizuri na mvua hizi lakini bado kuna mdudu ambaye amekuwa akishambulia mahindi na hivyo kusababisha hasara.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingi ya Kusini Magharibi imekuwa ikitajwa kama ni mikoa ya uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mpunga na maharagwe.

Je, Serikali ina mkakati gani hususan katika Mkoa wa Katavi kuhakikisha kwamba inafanya utafiti na ku-introduce zao la biashara kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi ili waweze nao kutoka kwenye masuala ya mazao ya chakula waende sasa kufanya biashara katika mkoa huo? Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba watu wao wanapata mazao ya kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali kwanza tuna Kituo chetu cha Utafiti cha Mlingano Tanga ambacho tumekipa jukumu mahsusi kwa ajili ya utafiti wa udongo kuangalia afya ya udongo na tabaka la udongo ili kufahamu kwamba udongo wa sehemu husika unakubali mazao gani, una upungufu wa virutubisho vya ardhi vya mbolea kiasi gani ili sasa kumwelekeza mkulima kulima kulingana na ikolojia ya eneo lake na mazao yanayokubali kutokana na ardhi ile.

Mheshimiwa Spika, kazi hiyo ya awali tumeshamaliza kwenye mikoa zaidi ya 16 na sasa hizi pia tumetambulisha maabara yetu kama pale SUA na Chuo cha Kibaha (TARI) kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, niwahamasishe wakulima wote kuchukua nafasi hasa kwenye kilimo cha biashara ni vizuri kufanya utafiti wa udongo kabla ya kulima kwa sababu ardhi imeshachakaa sana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mkakati wa Serikali tuliokuwa nao kwa ajili ya kutambulisha mazao ya biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu hususan katika Mkoa huu wa Katavi. Kwanza hili ni swali zuri sana na ni mkakati wa Serikali sasa hivi kuwatengenezea wakulima kuwa na kiiunua mgongo wakati wanapofikisha miaka zaidi ya 60 kwa sababu kuendelea kulima mazao muda mfupi mahindi na mpunga maana yake ni kuwalazimisha wakulima kulima mpaka kufa. Katika mipango hii ya Serikali katika Mkoa wake wa Katavi, mwaka huu tumeshaanza kuzalisha miche zaidi ya 600,000 ya korosho na tumeshagawa sasa hivi katika Wilaya ya Tanganyika miche zaidi ya 250,000 na tarehe 8 mwezi huu tunakwenda kugawa miche iliyobaki ya korosho zaidi ya 350,000 katika Wilaya zote za Mkoa wa Katavi ili sasa kutambulisha na kuhamasisha wakulima hawa wakalima mazao muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwaka huu temegawa zaidi ya miche 800,000 ya kahawa katika Mkoa huo huo wa Katavi na mwaka huu unaokuja katika bajeti tumepanga kuzalisha miche 1,000,000 ya kahawa, miche 1,000,000 ya korosho na miche 1,000,000 ya maparachichi ili kwenda kuipanda katika Mkoa huo wa Katavi. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo yaliyopo Jimbo la Mlimba yanafanana na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Kavuu na kwa kuwa nilikwisha omba maombi maalumu kwa ajili ya matengenezo ya daraja linalounganisha Kata ya Chamalemu D na Mwamwamapuli. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kupeleka pesa kwa ajili ya kutengeneza daraja hilo hili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za afya katika Kata ya Kibaoni badala ya kuzunguka Kata ya Mbede?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaondolea adha wananchi ili wasilazimike kuzunguka umbali mrefu wakati ingewezekana kujenga daraja ili wananchi wasitembee umbali mrefu. Naomba nimhaikikishie Mheshimiwa Mbunge ni vizuri baada ya Bunge hili, baada ya kipindi hiki tuwasiliane na coordinator wa Mkoa tujue uwalisia na uhitaji kwa ajili ya daraja hilo ambalo linaweza likajenga ili wananchi wasilazimike kutembea umbali mrefu wakiwa wanafuata huduma ya afya ambayo na yeye mwenyewe anaridhika jinsi ambavyo huduma hii inatolewa kwa karibu, lakini adha imekuwa ni hilo daraja.