Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Stergomena Lawrence Tax (1 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu, nianze kwa kuzipongeza Kamati zote kwa taarifa nzuri walizowasilisha. Pia kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Vita Kawawa, Mwenyekiti wa Kamati ya NUU na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia, ushauri wanaotupatia ambao unatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea michango mingi kutoka kwenye Kamati na Wajumbe mbalimbali waliochangia. Naomba niwashukuru na niwahakikishie kwamba michango hii yote ni muhimu na tutaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa mambo yaliyojadiliwa na kwa uchache wa muda, nitajaribu kuongea machache na kwa ufupi sana. Mtanisamehe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, napenda niweze kuongelea mengi kadiri nitakavyoweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa mojawapo lililoongelewa kwa umuhimu na kuchangiwa na watu wengi ni kuhusu diplomasia ya uchumi, kufunganishwa na uchumi, ushirikishwaji wa sekta, limekwenda mpaka Halmashauri na kupanua uelewa wa diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema kwamba diplomasia ya uchumi ni kitu muhimu sana na imekuwa na mafanikio makubwa sana kibiashara, kiuwekezaji, kiutalii na hata miradi. Pengine Waheshimiwa Wabunge hamfahamu kwamba baadhi ya miradi mikubwa mnayoona ikitekelezwa hapa nchini imeibuliwa na Balozi zetu ikiwa ni sehmu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kipindi hiki au katika awamu hii ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, diplomasia ya uchumi imeshika kasi kubwa sana. Tumemwona yeye mwenyewe akitangaza fursa mbalimbali katika mataifa mbalimbali, tumemwona jinsi ambavyo amekuwa akitangaza utalii, tumemwona ambavyo amevutia wawekezaji mbalimbali, na hii yote imechangia katika kukuza diplomasia ya uchumi. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, diplomasia ya uchumi imekuwa na mafanikio makubwa, lakini hata hivyo siyo kwamba, hakuna changamoto. Tumefanya tathmini kama Wizara na kubaini kwamba zipo changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na masuala ambayo yameainishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, tunaandaa Mpango wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Madhumuni ni kuhakikisha kwamba tunaibua maeneo ya kimkakati, tunaainisha watekelezaji wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na tunapanga utaratibu wa kutekeleza ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya umma kama ilivyoelezewa na kuwaleta wadau wote pamoja. Kama nilivyosema, matarajio yetu ni kwamba, tutakamilisha kazi hii mwezi Desemba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mchango kwamba pengine tuangalie kuajiri kutoka sekta binafsi. Katika kuandaa mkakati huu, tutaona kama kuna haja ya kuajiri au tunaweza kuishirikisha sekta binafsi kwa utaratibu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, katika Taarifa ya Kamati, aya ya 3.2.1, sijui ni ibara au section (b) na (c), Kamati ilipendekeza tuandae mikakati miwili na mpango mmoja; Mkakati wa kuainisha fursa za kiuchumi, mkakati wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, na mpango wa ushirikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa ninaomba tuandae mkakati mmoja ambao tunaendelea kuuandaa na utajumuisha yote haya. Hii itakuwa na ufanisi zaidi. Kwa muktadha huo, naomba azimio hilo lisomeke namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nitapenda kuliongelea ni uratibu maalum wa kuwaandikisha diaspora. Hili ni jambo kubwa, na ni kweli, kama ilivyosemwa, limesimamiwa sana na Mheshimiwa Rais. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, siyo kweli kwamba hatuyajali maagizo ya Mheshimiwa Rais, la hasha, tunafanya kazi kubwa na tumefika pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaanza kuandaa mfumo wa kidijitali ambao mpaka sasa hivi umefika mbali na tunatarajia kufika mwezi Juni mwaka huu utakuwa umekamilika. Mpaka sasahivi prototype iko tayari, tumeshaandaa design na kilichobaki sasa ni kukamilisha mfumo huu. Kwa hiyo, hili limekwishakamilika, ni muda mchache tu mtaweza kuona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine muhimu ambacho kilijitokeza katika mazungumzo, mijadala au michango ni hadhi maalum kwa diaspora. Hapa ndipo tulipoambiwa tunamkwamisha Mheshimiwa Rais. La hasha, hatumkwamishi, na hatuwezi kufanya hivyo. Sisi ni jeshi lake, tuko nyuma yake, tunafanya kazi kuhakikisha yale yote aliyotuagiza kuyafanya, tunayatekeleza kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mbali sana. Mpaka sasa hivi tulishakusanya maoni ya wadau, tulishakusanya mapendekezo kutoka diaspora, tumeshayachambua, tumeshashirikisha wadau wote na tumeshaainisha maeneo ambayo tuna imani kwamba yanakwenda na matarajio na matakwa ya diaspora ambayo sasa mfumo umeshawekwa na utaratibu umeandaliwa, lakini kilichobaki sasa hivi tunapeleka kwenye Baraza la Mawaziri. Kitakachofuata baada ya hapo, kwa sababu yapo maeneo ya kisheria ambayo yatatakiwa kufanyiwa kazi, kwa hiyo, baada ya Baraza kupitisha waraka huu, tutaendelea na mabadiliko ya sheria ili hadhi hii maalum iweze kufanyiwa kazi. Tumefika mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa ruhusa yako, ni uendelezaji wa balozi na vitega uchumi, limeongelewa sana na ninawashukuru sana kwa kuliongelea hili. Hili ni jambo kubwa sana na ni kweli kabisa kwamba taswira ya nchi yetu inaonekana pia kupitia balozi zetu tulizonazo nchi mbalimbali, lakini ni suala kubwa linalohitaji rasilimali nyingi. Mjumbe mmoja ameeleza kwamba, kati ya majengo 110, majengo 67 yanahitaji aidha kujengwa upya, kukarabatiwa au kubomolewa kabisa na kujengwa upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kwamba hatuwezi kufanya kazi hii peke yetu, na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tunafanya kazi hii kwa kushirikiana na sekta binafsi. Tayari nimeshaunda Kamati ya Kitaasisi inayojumuisha sekta binafsi na sisi wenyewe. Kwanza kuainisha nini tunaweza kufanya kwa haraka? Mahitaji tunayoyahitaji sasa hivi ni nini? Wizara ya Fedha inaweza ikatenga kiasi gani? Tuko katika mchakato wa bajeti ili iweze kuingia katika bajeti inayofuata, lakini sekta binafsi na yenyewe inaweza ikashiriki namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la sheria ambalo pia lilikuwa linatusumbua, lakini sasa hivi tayari PPP inafanyiwa maboresho na tuna imani kwamba sekta binafsi itaweza kushirikiana nasi na mtaona matokeo baada ya muda siyo mrefu. Ni kazi kubwa kwa sababu inahitaji uandae concept note, uwe na feasibility study, uwe na design; yote haya yanaandaliwa na Kamati ili hata pale tukapopata fedha tuweze sasa kwenda na kuanza kutekeleza kazi hii. Hata ukipata fedha sasa hivi Waheshimiwa Wabunge unaweza usifanye kazi hii kama haya maandalizi hayajawa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kama utaniruhusu, ni suala la kujitoa katika COMESA. Naomba tu kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, hatujapata hasara yoyote. Sisi tulikuwa wanachama wa jumuiya tatu, na tukiwa pekee wanachama wa jumuiya tatu. Tumebaki tukiwa Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC. Baada ya kuwa tumejitoa, tuliona kwamba hatuwezi kuwapoteza wale wachache ambao hatukonao ambao walibaki katika COMESA na nchi zote zilikuwa zikihangaika wakati huo, kwamba tuko katika configurations nyingi. Inatusumbua, tunalipa michango mingi, lakini pia kuna obligations ambazo zinapandana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukakubaliana kuanzisha utatu unaoleta pamoja COMESA, EAC na SADC na tunashirikiana katika mihimili yote mitatu; uendelezaji wa viwanda, uendelezaji wa miundombinu, na pia uendelezaji wa masoko na biashara. Pia ipo miradi ambayo tunatekeleza pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 ulizinduliwa ukanda huru wa biashara (FTA), kilichobaki sasa hivi ni kufanya ratification. Katika hii tripartite inatuwezesha sasa kufanya biashara kwa pamoja kama ambavyo tungefanya na COMESA peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ilikuja hoja kwamba, tunapoteza biashara kubwa na DRC. Kuna utoafauti kati ya ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa nchi na nchi. Vinapotokea vikwazo ambavyo ni baina ya nchi na nchi tunavitatua baina ya nchi na nchi. Tumeendelea kutatua vikwazo mbalimbali kama ilivyoelezewa kati ya Kenya na Tanzania na hata kati ya DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuthibitisha kwamba hatujapoteza biashara katika DRC, biashara hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2012 biashara yetu ilikuwa ni Shilingi bilioni 50.2 lakini miaka minane baadaye kufikia mwaka 2020 biashara yetu ilikua kufikia Shilingi bilioni 334 kutoka Shilingi bilioni 50. Kwa hiyo, biashara inaendelea na hatujapoteza kitu chochote na urari wetu kati ya DRC na Tanzania ni chanya. Hivyo hakuna tulichopoteza, bali tumenedelea kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umenivumilia, umeniongezea muda. Nakushukuru sana, naomba niishie hapo. (Makofi)