Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (22 total)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka 2017/2018 Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anazindua Siku ya Ushiriki wa Afya Duniani katika Jimbo la Ushetu katika Halmashauri ya Ushetu, Kata ya Ulowa, aliwaaahidi wananchi kuwajengea kituo cha afya, lakini hadi leo ni miaka mitano kituo hicho hakijaanza kujengwa.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Kituo Cha Afya kwa wananchi wa Ulowa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote za viongozi wetu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji, kikiwepo Kituo cha Afya katika Kata ya Ulowa. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali imechukua mahitaji na ahadi hii, na tunatafuta fedha, wakati wowote kupitia fedha za tozo tutaleta pale milioni 250 ili Kituo cha Afya cha Ulowa kianze kujengwa. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, hizi zimekuwa ni namba tu ambazo zikisomwa kila mwaka; lakini ukienda kwenye uhalisia kabisa huwezi kukuta mkulima mfano wa pamba ana kitambulisho cha usajili, hata kwenye korosho huwezi kukuta mkulima kwenye korosho ana kitambulisho cha usajili. Ukiangalia hata Chama chetu cha Mapinduzi juzi tu kimesajili wanachama wake, lakini tayari wamepewa kadi. Sasa mimi nataka nijue kauli ya Serikali ni lini sasa hawa wakulima wa mazao ya kimkakati watapewa kadi za usajili ambazo zitakuwa kama vitambulisho kwao?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; tumekuwa zikiagizwa pembejeo nyingi ambazo zinakuja kwa wakulima lakini madhara yake zinakuwa zinabaki kwa sababu uhalisia kamili wa wakulima waliosajiliwa bado haujajulikana. Nataka nipate majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali tunaendelea na zoezi la usajili wa wakulima nchi nzima ambapo mfumo unaotumika hivi sasa ni mfumo ambao unampa kila mkulima utambulisho maalum kwa maana atakakuwa na namba yake maalum ambayo ndiyo utakuwa utambuzi wake. Zoezi hili linaendelea katika maeneo mengi kwa ukamilifu mzuri na uratibu unaendelea vizuri na tunaamini kabisa likikamilika litatibu changamoto zote ambazo wakulima wanazipata hasa katika utambuzi wao kwa sababu kila mkulima atapata namba yake maalum ya utambuzi; na tunaamini kupitia hapo sasa hata zile huduma muhimu watazipata kwa rahisi zaidi.

Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili linaendelea na linaendelea vizuri na mwisho wa siku tutakuwa na kanzidata ya wakulima wote nchini kila mtu kwa maeneo yake alipo pamoja na maeneo ambayo anayamiliki na mazao anayalima na yields anazipata.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Serikali itapeleka lini mawasilino ya uhakika ya simu kwa wananchi wa Ushetu hasa katika Kata ya Ulewe, Igwamanoni, Igunda pamoja na Bukomela ambapo wananchi hao bado wanapanda juu ya mti na milimani kutafuta mawasiliano ambayo ni hatari sana kwenye maisha yao.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ambazo Mheshimiwa Cherehani amezitaja tayari katika bajeti ya Serikali ambayo ililetwa Bungeni hapa Kata hizo ziliwekwa katika bajeti. Bajeti hii ambayo inaunganisha minara 763 na kama ambavyo nimesema hapo mwanzoni tayari tumeshatangaza tenda tarehe 20 Oktoba na tarehe 2 Disemba itafunguliwa na baada ya hapo ujenzi wa minara hii utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa nini sasa Serikali isipeleke mbegu bure kabisa kwa wakulima wa alizeti ili waweze kuzalisha alizeti kwa wingi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mafuta hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona tunaongeza uzalishaji wa zao la alizeti, kila jambo linakwenda kwa hatua. Hatua ya kwanza tumeanza na ruzuku ya kuuza mbegu ya kilo moja kwa Sh.5,000 ambayo katika hali ya kawaida mkulima angepata kwa Sh.35,000 mpaka Sh.40,000. Kwa hiyo kwa hatua hii, ni hatua nzuri ambayo Serikali imeianza na huko mbeleni tutalifikiria ombi la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2020, wakati anafunga kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Ushetu, alipokea simu kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. Magufuli na akawaahidi maelefu ya wananchi pale kwamba atawajengea kilometa 54 za lami kutoka Kahama – Nyandekwa - Iboja mpaka Iyogo kilometa 54 za lami: je, ahadi hii itaanza kutekelezwa lini kwa wananchi wa Ushetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tukisema, ahadi zote za viongozi wa Kitaifa ni ahadi ambazo zinatekelezwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeahidiwa tunazo lakini tunaendelea kuzitekeleza kadri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na hii barabara ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii pia itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliagiza. Ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ahadi hii sasa ina miaka Sita na inaenda mwaka wa Saba, ahadi zote zinazotolewa na Viongozi wetu wa Kitaifa wanatoa kwa sababu ya hali ilivyo ngumu kwenye Majimbo yetu yaliyo mengi. Ninavyojua kwa Viongozi wa Kitaifa ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, ahadi hii hata hayati marehemu John Kwandikwa aliifuatilia sana lakini utekelezaji wake mpaka leo haujafanyika.

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ahadi hii na kwa nini Serikali isitafute fedha za ziada kuhakikisha kituo cha afya hiki kinajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoeleza ni kwamba hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nieleze tu Bunge lako tukufu kwamba moja ya mpango mkubwa wa Serikali ambao ulikuwepo awali ni kuhakikisha kwamba zile Tarafa zote nchini ambazo hazikuwa na vituo vya afya tulikuwa tunapeleka vituo vya afya, ndiyo maana katika mwaka wa fedha huu unaokwenda kuisha Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya 233 ikiwemo katika Jimbo la Ushetu ambapo tumepeleka fedha awamu ya kwanza, fedha za tozo Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho wao wamepeleka katika eneo lingine.

Meshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika eneo hili ambalo liko katika ahadi baada ya kumaliza huu mkakati ambao tumeuainisha kumaliza Tarafa zote nchini basi na eneo lako tutaliweka katika kipaumbele kuhakikisha kwamba hii ahadi haichukui muda mrefu ili kuwasaidia wananchi wa Kata ya Ulowa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwenye Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kupeleka fedha kwenye ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichopo katika Halmashauri ya Ushetu; na wananchi wale walishajichanga pamoja na wadau mbalimbali wakajenga msingi. Sasa nataka nijue, ni lini Serikali inapeleka fedha hizi ili kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu maeneo ya Wilaya mpya kama ilivyo ya Ushetu wanahitaji kuwa na vituo vya polisi ili kusogeza huduma za usalama wa raia karibu zaidi na wananchi. Ni ahadi yetu kwamba kwa vyovyote vile kwa sababu wananchi wameshajitokeza, wamechangia nguvu zao na jitihada wakafikia mpaka kiwango cha msingi, nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge, kwamba pale ambapo tutapata fedha kwa ajili ya ujenzi, Wilaya ya Ushetu itazingatiwa pia. Nashukuru.
MHE: EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, Serikali itaanza lini ujenzi wa kilometa 30 kwa kiwango cha changarawe kutoka Uyogo kupita Iberansua, Mbika mpaka Urowa, ambapo barabara hii imekuwa kiungo kikubwa sana kwa wananchi na uchumi wa halmashauri wa Ushetu na mpaka tunavyoongea sa hizi magari yanadondoka ya wakulima wanaosafirisha mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Nyongeza la Mheshimwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii kama alivyosema inahitaji kujengwa kwa changarawe. Sehemu ya barabara hii ilikuwa chini ya barabara ya TARURA na sasa ndo imepangiwa bajeti. Nataka nimuhakikishie

Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka huu tutakwenda kuikarabati barabara hiyo. Nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa Mkoa wa Shinyanga aende aitembelee hii barabara na kuifanyia ukarabati wa haraka ili kuokoa maisha na mali na hayo magari ya wananchi. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Halmashauri ya Ushetu imekamilika ujenzi wake, lakini wananchi bado wanatembea zaidi ya kilometa 80 kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama.

Je, ni lini Serikali italeta vifaa tiba katika hospitali hiyo ili wananchi hawa waanze kupata matibu karibu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza priority ambayo Mheshimiwa Waziri wa Afya ameelekeza sasa hivi ni kuhakikisha hospitali zote zile ambazo zimeshajengwa vituo vya afya, zahanati na hospitali za Wilaya na majenzi yote, kuhakikisha sasa vifaa tiba vinaenda kununuliwa. Kama ambavyo nilisema jana sasa hivi shida siyo fedha kwa sababu Rais wetu kama nilivyosema tayari alishapeleka shilingi bilioni 333.8 na tayari kila mwezi kuna utaratibu wa kupeleka shilingi bilioni 15 MSD. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwanza nitumie fursa hii kwa kushirikiana na wenzangu wa TAMISEMI kwamba RMO asimamie kwanza OPD kwenye hiyo hospitali ianze, kwa sababu inawezekana kuanza OPD mapema na kujipanga kwa ajili ya kuanza wakati tunangojea vifaa vya kuhakikisha hospitali hii inaenda kufanya kazi kama full flagged kama hospitali ya Wilaya. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuondoka kwa kampuni ya TLTC hapa nchini kumechangia kudorora kwa soko la Tumbaku.

Je, ni lini Serikali itakamilisha mazungumzo na kampuni hii ili iweze kurudi Tanzania kununua Tumbaku za wakulima na kuongeza tija na ushindani? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niwaambie wakulima wa Tumbaku na niwaambie Watanzania, kiwanda kilichokuwa cha TLTC na kampuni ya TLTC imenunuliwa na sasa hivi amepatikana mwekezaji mwingine na mwekezaji huyu yupo kwenye hatua za mwisho na mwaka huu kiwanda kile kitafunguliwa. Serikali tunawasaidia wawekezaji wapya kuweza kupata minimum quantity ya tumbaku ili kiwanda kile kifunguliwe, kwa hiyo nataka niwaambie tu wakulima wa tumbaku kilichokuwa kiwanda cha TLTC amerudi sokoni kupitia kampuni nyingine ambayo imeweza kununua kiwanda kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie tu kwamba kiwanda kile kinafunguliwa na ninaamini msimu ujao wa 2022/2023 uzalishaji na makisio yataongezeka tofauti na tulivyokuwa sasa hivi. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro uliopo katika Halmashauri ya Ushetu pamoja na Kariwa ambao unazidi kuchukua sura mpya na sasa mpaka wananchi wangu zaidi ya 17 wamekamatwa na kuwekwa ndani bila sababu zozote za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampa pole Mheshimiwa Mbunge, na pia nawaomba wananchi wa Ushetu wawe na subira. Tulipanga kwenda kufanya mazungumzo na wananchi, lakini ratiba zikaingiliana. Nawaomba wananchi wa Ushetu wawe wavumilivu, baada ya Bunge hili, tutaondoka na Mbunge wao kwenda kuzungumza na kutatua changamoto hii, ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Zao la pamba ni kati ya mazao ya kimkakati hapa nchini lakini wakulima wake bado wanazalisha kilo 300 mpaka 400 kwa heka moja.

Je, ni nini mkakati wa Serikali sasa kwa wakulima hawa waweze kuzalisha kilo 500 mpaka 1,000 kwa heka moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, anachokizungumzia Mbunge hapa ni tija na sisi tumejipanga katika Wizara kuhakikisha wakulima wetu wanalima kwa tija. Kwanza, kabisa kuwasaidia kupata viuatilifu sahihi; pili, kuwasaidia kupata teknolojia za kisasa za kilimo cha pamba; na tatu, ni kuhakikisha kwamba wanajifunza kanuni bora za kilimo kama ambavyo hivi sasa tumeona kule kupitia TARI na Balozi wa Pamba juu ya mfumo mpya wa spacing ambao umesaidia sana kuongeza uzalishaji katika zao la pamba.

Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba, tunatambua changamoto hizo na tumejipanga kuhakikisha kwamba mkulima wa pamba anazalisha kwa tija.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwulize Naibu Waziri wa Ardhi, Serikali inapeleka lini fedha za upimaji wa ardhi katika Halmashauri ya Ushetu hasa katika kata zinazokua kwa kasi; Kata ya Igwamanoni, Kata ya Idahina, Nyankende pamoja na Burungwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maombi ya wananchi wa Ushetu juu ya kupimiwa eneo lao yalishawalishwa kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, tutakapokuwa tumeshapata fedha hizo, tutaleta fedha Ushetu ili sasa maeneo yale yaweze kupimwa, kupangwa na kumilikisha wananchi wetu ili maendeleo yaweze kupatikana kama ambavyo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pengine nitoe ufafanuzi kuhusiana na hizi pesa ambazo halmashauri zinaomba kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha. Naomba watambue, fedha aliyotoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ile Shilingi bilioni 50 inakwenda kwenye Halmashauri kulingana na maandiko wanayotoa. Fedha ile inakwenda kusaidia kwenye Halmashauri ambazo ndiyo zenye mamlaka ya Upangaji. Kwa hiyo, tunategemea ile pesa isihesabike kama ndiyo fedha inayokwenda kukamilisha kazi, isipokuwa Halmashauri zinatakiwa kutenga fedha ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya ardhi. Kwa hiyo ile isihesabiwe kama ndiyo fedha ambayo inategemewa sana katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mamlaka za Upangaji, sisi tuna-support kuongeza kile ambacho ninyi mmetenga kwa ajili ya maendeleo ya Ardhi na siyo kwamba tunatoa bajeti kwa ajili ya ku-fulfill mpango mzima wa kupanga katika maeneo yenu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niwapongeze Wizara niwapongeze Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanazofanya. Kwa kuwa Manispaa ya Kahama ina chuo cha FDC ambacho kinafanya kazi kama ile ile ya Chuo cha VETA: Kwa nini sasa chuo hiki cha VETA kisijengwe katika Halmashauri ya Ushetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili: Kwa kuwa uhitaji wa Chuo cha VETA kwa wananchi wa Ushetu mkubwa sana kulingana na ongezeko kubwa la vijana ambao wanamaliza vyuo vikuu lakini hawaendelei na masomo ya juu: Kwa nini sasa Serikali isione hili kwa umuhimu kulingana na umbali wa kilometea zaidi ya 113 kutoka Ushetu kuja Manispaa ya Kahama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara haipangi maeneo ya kujenga vyuo hivi vya VETA, ni jukumu la Serikali za Mikoa pamoja na Wilaya kupanga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivi vya VETA. Naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakuu wa Mikoa washirikishe Waheshimiwa Wabunge wa maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba wanakwenda kupanga maeneo sahihi ya kuweza kufanya ujenzi wa vyuo hivi vya VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lakwe la pili, tunajua umuhimu wa vyuo hivi na hivi sasa tumeanza katika ngazi ya Wilaya pamoja na Mikoa; baada ya kukamilika zoezi hili katika ngazi za wilaya pamoja na mikoa, tutafanya tathmini ya kina ili kuweza kuona namna gani tunaweza kuzifikia zile Halmashauri ambazo labda ziko mbali na maeneo ambayo yamejengwa katika VETA zile za Wilaya pamoja na Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Mifugo imekuwa ikitoa ahadi kwa wananchi wa Ushetu kwa ajili ya kuwajengea majosho. Hata Mheshimiwa Mpina wakati akiwa Waziri alishafika Kaya za Nyankende, Ulewe na Ubagwe akaahidi lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi hakuna. Nataka nipate kauli ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imefanikiwa kupeleka jumla ya fedha shilingi milioni 540 kwa ajili ya ujenzi wa majosho katika halmashauri mbalimbali nchini, na bado kiasi cha shilingi takribani milioni 100 zipelekwe pia. Ninaamini Wilaya ya Ushetu ni miongoni mwa Wilaya ambazo ni wanufaika. Naomba mara baada ya hatua hii ya Bunge nikutane na Mheshimiwa Mbunge Cherehani aweze kunipatia orodha ya vile vijiji vyake ili niweze ku-cross check kwa ajili ya ufuatiliaji wa ujenzi wa majosho haya ya wananchi wa Ushetu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ushetu lina changamoto kubwa sana ya umeme, hasa maeneo ya vijijini, maeneo ya shuleni, hospitalini na hata maeneo ambapo umeme upo unakatika katika sana.

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa uhakika kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imetenga takribani Shilingi Bilioni 400 ili kuboresha na kuimarisha gridi yetu ya Taifa na hivyo tunaamini baada ya kupata hizo pesa na mradi wa kuboresha gridi ya Taifa kutekelezwa, tatizo la kukatika katika kwa umeme litaendelea kupungua kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Spika, pia katika eneo hilo umeme vijijini bado unaendelea kupelekwa kwa mikataba ambayo ipo na eneo la Shinyanga kwenye Jimbo lake ni eneo ambalo tayari lina Mkandarasi na anaendelea na kazi.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, changamoto ya maji katika Jimbo la Ushetu ni kubwa sana, lakini pia hata miradi iliyoanzishwa toka mwaka 2019 hasa katika Kata za Saba Sabini, Mkunze na Chambo haijakamilika.

Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha miradi hii ili wananchi hawa wa Ushetu waweze kupata maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kaka yangu Cherehani kwa kweli ameingia muda mfupi, lakini amekuwa anawapigania watu wake na si mara moja ameshafika ofisini. Kubwa utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, tutatoa fedha kwa Jimbo la Ushetu kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na wananchi wa Ushetu waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunatumia sasa maji ya Ziwa Victoria kuhakikisha wananchi wa Ushetu wanaenda kupata maji ya uhakika. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa vile utaratibu unaotumika sasa ni wa mkataba wa mwaka mmoja mmoja. Swali la kwanza; je, Serikali ina mkakati gani sasa ya kuwafanya wakulima hawa waweze kutambua ni kampuni ipi nzuri ili waweze kuingia nayo mkataba?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Bodi ya Tumbaku na ndiyo msimamizi mzuri wa zao hili, lakini haina fedha kabisa haina magari hata ya kwenda kwenye masoko, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweza kuiopatia fedha Bodi ya Tumbaku ili iweze kusimamia vizuri masoko ya tumbaku hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa sababu Bodi ya Tumbaku ina ofisi katika mikoa yote ya tumbaku na Bodi ndiyo custodian wa taarifa zote za makampuni ya ununuzi wa tumbaku tumekuwa tukitumia nafasi hiyo kuendelea kuwapa taarifa sahihi wakulima kupitia ofisi zetu hizo ili watambue mnunuzi mzuri wa kuingia naye kwenye mkataba. Sambamba na hilo, pia tunayo taarifa za wanunuzi wote katika tovuti ya Bodi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la bajeti kilifanyika kikao cha wadau wote wakakubaliana kwamba ili kuijengea Bodi uwezo kuanzia msimu unaokuja tutaanza kuchaja shilingi thelathini katika kila tumbaku mbichi kwa ajili ya kuiboresha Bodi yetu ya Tumbaku ili iweze kufanya ufatiliaji na kuendeleza zao hili la tumbaku.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Mgogoro kati ya Pori la Usumbwa Forest Reserve na Pori la Hifadhi ya Taifa Kigosi Moyowosi umedumu kwa muda mrefu sana. Sasa je, ni lini Serikali itaushughulikia mgogoro huu ili kuwapa nafasi wananchi wa Jimbo la Ushetu hasa wanaozunguka Kata za Idahina, Nyankende, Ulewe pamoja na Ubago waendelee na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niendelee kuwaomba wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo haya waendelee kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuangalia namna iliyo bora ya kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, tuna Kamati ya Mawaziri Nane ambayo ina maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais kwamba tuzunguke nchi nzima kuhakikisha kwamba tunatatua migogoro hiyo. Sambamba na hilo tumezielekeza taasisi, endapo kuna migogoro mipya ambayo haimo ndani ya hii migogoro inayotatuliwa na Kamati ya Mawaziri Nane basi tuanze pia kuangalia mchakato mpya kuangalia namna iliyo bora ili tuweze kutatua migogoro hiyo. Kwa hiyo, niwaombe wananchi wote ambao wana migogoro mipya katika maeneo yao Serikali inaendelea kuyafanyia kazi ili tuone njia iliyo bora ya kutatua migogoro hiyo.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali ina mkakati gani wa kuongeza Mkandarasi katika Wilaya ya Kahama yenye Halmashauri mbili Ushetu pamoja na Msalala kutokana na aliyepo kupeleka umeme kwa kusuasua sana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi anaepeleka umeme katika Wilaya ya Kahama ni Mkandarasi anayeitwa Tontan ambaye tunakiri ana mapungufu na hasa katika kazi yake anayoifanya Tanga na tumewekeana masharti ya kutimiza, akishindwa kuyatimiza mwezi huu wa Nne hautaisha ataondoka site zetu ili tuweze kupata Mkandarasi mwingine wa kupeleka umeme katika maeneo hayo. Kwa hiyo wananchi wa Kahama ninawaahidi kabisa kwamba umeme katika maeneo yao utapelekwa na utakamilika kwa wakati kwa sababu ni jambo linalotakiwa kukamilika kwa wakati.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakulima wa tumbaku wamekatwa makato makubwa sana ya upandaji wa miche ya miti ambapo ni zaidi ya shilingi 813 kwa kila mche mmoja.

Sasa kwa nini, Serikali isiondoe kabisa makato haya kwa wakulima wa tumbaku ili waweze kupanda miti kwa hiari yao bila makato yoyote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tuna kikao cha wadau ambacho tutajadili mambo haya na kuweza kukubaliana kwa pamoja. Kwa hiyo tumeuchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; Barabara ya Mpunze-sabasabini ipo Nyagholo mpaka Igwamanoni imekatikakatika haipitiki kabisa na imepandishwa kutoka TARURA kwenda TANROADS. Ni nini mkakati wa Serikali kwa ajili ya kuijenga barabara hii angalau hata kujua maeneo yaliyokatika ili wananchi waweze kupita kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja ilikuwa inahudumiwa na wenzetu wa TARURA, na ndiyo kwanza imekuja sasa TANROADS. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa wa Ushetu pamoja na wananchi wa Ushetu, kwamba tumesikia, na ninamwagiza Meneja wa Mkoa wa Shinyanga, cha kwanza aende akahakikishe kwamba yale maeneo yote ambayo yamekatika anayarejesha ili kuwe na mawasiliano. Pia aweze kufanya tathmini ili maeneo yote yale korofi tuweze kuangalia namna ya kuyarakabati vizuri ili yaweze kupitika muda wote hata kipindi cha masika, ahsante.