Primary Questions from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (4 total)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa wakulima wote nchini hasa wa mazao ya kimkakati ikiwemo pamba, korosho, kahawa, chai na michikichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikisajili wakulima kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Bodi za Mazao, Sensa ya Kilimo na Vyama vya Ushirika. Hadi Agosti, 2022 jumla ya wakulima 1,499,989 wa mazao ya kimkakati ya chai wakulima 31,093, pamba wakulima 556,384, kahawa 305,261, korosho 483,034, miwa 6,746, mkonge 2,369, pareto 10,846, tumbaku 53,758 na mazao mengine 50,498, wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili wa Wakulima (Farmers Registration System) na vyama vitatu vya ushirika wa michikichi wamesajiliwa. Serikali imeanza kupitia upya mifumo ya usajili wa wakulima kwa lengo la kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha usajili wa wakulima wa mazao yote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani na masoko.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa Kitaifa kote nchini ikiwemo ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika jimbo la Ushetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 inaendelea na mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati yenye uhitaji mkubwa nchini kote ikiwemo Kituo cha Afya cha Ulowa.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama ni miongoni mwa Wilaya zitakazojengewa Vyuo vya VETA ambapo kwa sasa Serikali ipo katika hatua za maandalizi ya ujenzi. Hivyo wananchi wa Jimbo la Ushetu watanufaika na Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kahama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaruhusu kampuni zinazonunua tumbaku kwenda kwenye AMCOS kujinadi ili kuongeza ushindani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hapo awali Serikali iliruhusu kampuni za ununuzi wa tumbaku kujinadi kwa wakulima na kuingia mikataba kwa misimu mitatu ya kilimo. Kilimo cha mikataba kwa misimu mitatu kiliathiri bei ya Tumbaku kwa mkulima kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji kampuni na uzalishaji. Jambo hilo lilisababisha Serikali kubadili mfumo huo na kwenda mfumo wa msimu mmoja ili kuongeza ushindani na ufanisi.
Mheshimiwa Spika, Kilimo cha mkataba kwa msimu ni mbadala mzuri kwa wakulima na kampuni kwasababu kinapunguza gharama zinazotokana na kampuni kujinadi. Vilevile, kilimo hicho kinatoa fursa kwa pande zote mbili kujitathmini kabla ya kuingia mkataba kwa msimu unaofuata.