Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Emmanuel Peter Cherehani (1 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa nafasi ya pekee aliyonijalia kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, pia nimshukuru sana Rais wetu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwa hekima na busara ya pekee kabisa ya kuweza kupeleka jina langu mbele ya wapiga kura wa Ushetu na niwashukuru sana wapiga kura wa Ushetu kwa kutupa kura nyingi za kishindo kwa kuweza kushinda kwa asilimia 96.69. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana Kamati kwa mapendekezo haya nilikuwa nayapitia pitia pamoja na ugeni wangu, lakini mimi ni mkulima nina-declare interest yangu na niwashukuru Wabunge wengi kwenye eneo la wakulima wamelijadili kwa mapana na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa dira na mwanga kwenye ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikumbuka jinsi Waziri Mkuu alivyopambana kuhakikisha ushirika unasimama, ameweza kurudisha mali nyingi za ushirika, amerudisha majengo mengi ya ushirika, amerudisha ginnery nyingi za ushirika, lakini kwenye mpango huu sijaona suala la ushirika linaguswa. Niseme tu kwamba pamoja na Wizara ya Fedha kufanya mambo mazuri, lakini wajikite sana katika kuhakikisha vyama hivi ambavyo vimerudishiwa mali za ushirika viweze kusimama na ginnery zote ziweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mali zilizorudishwa nikisema upande KNCU mali zote zilirudishwa nimefanya ziara kwenye maeneo hayo nikiwa kama kiongozi wa ushirika, mali nyingi zimerejeshwa lakini zinachakaa kwa sababu zinashindwa kuendelezwa na zinatakiwa ziendelezwe hasa viwanda zipewe fedha, vifufuliwe mazao ya wakulima yanunuliwe. Nimetembelea kiwanda cha KNCU ni kikubwa sana lakini ukienda wakulima wanalia hali ya kahawa yao hainunuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, katika mapendekezo haya, kwa upande wa Wizara ya Fedha waweze kupeleka fedha kwenye viwanda. Wapeleke fedha kwenye viwanda vya SHIRECU; SHIRECU wanunue pamba; wapeleke fedha Nyanza. Kuna ginnery ambazo ukizikuta ni nzima, zinachohitaji ni kuwa boosted kidogo tu. Mfano, kuna ginnery ya Kasamwa iko vizuri sana, inahitaji ipelekewe fedha, iingizwe kwenye Mpango iweze kufufuliwa, wananchi wa eneo la Kasamwa watauza pamba yao kwa bei nzuri kupitia ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano na niipongeze Wizara ya Kilimo mwaka 2019 na mwaka 2020 wameweza kufufua viwanda vitatu; kiwanda cha Chato, Kiwanda cha Mbongwe na Kiwanda cha KOM lilichopo Kahama. Tumeweza kuingia sokoni na Wizara ya Fedha kupitia Benki ya TADB ya Kilimo wamepeleka fedha. Tumeingiza ushindani na tumeweza kununua pamba kwa bei ya shlingi 1,050 hadi shilingi 1,750 kwa wakulima. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba ginnery ya Kasamwa, Manawa, Sola, Funze, Luguru, hizi ginnery ziangaliwe kwa jicho la karibu sana, zifufuliwe na wanaushirika waweze kupata faida kubwa, ushindani uongezeke. Ushindani unapoongezeka na watu wakapata bei nzuri, wakulima hawa wataenda kununua cement, mabati, nondo na wataendelea kuchangia mapato ya Serikali kupitia bidhaa hizo na watajenga nyumba nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa zao la Tumbaku, nataka nichangie kidogo kwa sababu nami pia ni mkulima wa Tumbaku. Mwaka 2012/2013 zao hili liliweza kuingiza fedha za kigeni zaidi ya Dola milioni 320 kwenye nchi hii; lakini wataalamu wetu hawa ambao wamesoma na wamesomeshwa na Serikali wameshindwa kulisimamia hili zao na mpaka leo limeshuka hadi kilo milioni 37. Shilingi milioni 420 ukizi-convert kwa leo tulikuwa tunaenda kwenye zaidi shilingi bilioni 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa, nikwambie tu, tozo zimekuwa nyingi mpaka zimewakatisha tamaa wanunuzi wetu. Nikikumbuka hata kampuni ya TOTC ilikuwa inanunua kwa zaidi ya vyama 70, ambapo imeondoka na imeacha hawa wakulima hawana mahali pa kuuzia. Sasa naiomba Wizara ya Fedha, kiwanda hiki kipo Morogoro, ni kikubwa sana, kinazalisha na kusaga zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka. Toka mwaka juzi, 2019 kimeachwa, kampuni imeshaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kiwanda kama kingeweza kufanya kazi, Serikali ikaongea na kampuni hii ikaweza kurudi, wakulima hawa wakauza tumbaku zao, soko likapanda, kiwanda kikafanya kazi, ajira zikaongezeka, nina imani hata mazao yetu ya wakulima yanaweza yakanunuliwa vizuri na bei ikaongezeka kwa wakulima wetu. Kwa hiyo, naomba kushauri kwamba tozo zipungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata leo, pamoja na tozo nyingine ambazo zipo, bado upande wa wakulima tumeletewa Withholding Tax ya 2%. Wabunge wote wameongelea suala la pembejeo kwamba lipewe ruzuku na 2% ukiziunganisha kwenye makampuni ambazo zimekatwa, wakulima hawa wamekatwa zaidi ya dola 700 na kitu na hii ndiyo ilikuwa faida ya wakulima. Sasa leo hii bei ya mbolea imepanda. Fedha hizi ambazo wakulima walitakiwa waende kununua mbolea zimekatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikueleza, sisi kwenye upande wa wakulima huwa gharama za uendeshaji na gharama za uzalishaji. Sasa haya makato yamekuja katikati ya msimu ambao mkulima anatakiwa achukue fedha yake, haijaingizwa kwenye gharama ya uendeshaji. Mkulima ambaye amefanya kazi miezi kumi na mbili, kilimo kinaanza mwezi wa Saba, halafu soko anakuja kuanza mwezi wa Tano msimu unaokuja; anajiandaa sasa fedha yake na yeye angalau hata shilingi 500,000 aipate kwa mwaka, imekuja kukatwa. Sasa fedha ya kununua mbolea hana na bei imepanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri maeneo haya, wakulima wetu wanateseka sana, hali ni ngumu sana. Fedha hizi zirejeshwe kwa wakulima kwa msimu huu. Hata kama ni makato sasa yanakuja, yaingizwe kwenye utaratibu ambao hata wakulima tutaziingiza kwenye gharama za uzalishaji, tutaziingiza kwenye gharama za uendeshaji, lakini leo hii hazipo kabisa kwenye mjengeko wa bei. Tunaweza tukalalamikia ruzuku lakini matatizo mengine yanasababishwa na wataalamu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Fedha wakae karibu, wapeane taarifa, watembee njia moja ili kupunguza adha kwa wakulima wetu. Tunahitaji mkulima naye afufuke, alime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna jambo alilisema na nilimpongeza sana kwamba tuna matajiri wasiopungua 5,000. Sasa hao matajiri tunahitaji pia wawemo humu.

MWENYEKITI: Mabilionea.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabilionea 5,000. Sasa tunahitaji mabilionea hawa na wakulima wawemo; wapunguziwe tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi kwenye suala la pembejeo, ni kweli zimepanda kwa kiasi kikubwa sana. Sasa pembejeo imepanda, lakini bado tunaenda kuwanyang’anya na kile kidogo walichokusanya wakulima. Dola 708,000 ni zaidi ya shilingi bilioni moja ambazo zimechukuliwa kwa wakulima wetu ambao walitakiwa wanunue cash na msimu umeshaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu, fedha hizi ningerudia kwamba zirejeshwe kwa wakulima, kama ni tozo, basi tujipange kwa msimu ujao tuweze kuwapelekea na tuweze kuwafundisha wakulima wetu na tuwape elimu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekititi, la mwisho, mfumo. Wakulima hawa hatujawaingiza kwenye mfumo wa usajili. Tunalalamika lakini wataalamu wetu wako kule. Wakulima wetu nchi hii wasajiliwe, waingie kwenye mfumo, tuwatambue mmoja mmoja, tujue namna ya kuwahudumia. Tukifanya hivyo hatutateseka. Bila hivyo, tutaendelea kusema kuna Bwana Shamba na Maafisa Kilimo; watambulike kwenye mfumo. Tukifanya hivyo, hata namna ya kuwafikia na kuwajua walipo na wataalamu wetu ambao watalipwa mshahara na Serikali, tutajua kwamba huyu leo amehudumia wakulima wangapi na wako maeneo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)