Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kavejuru Eliadory Felix (1 total)

MHE. KAVEJURU A. FELIX: Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma na ujenzi mzima wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ni wa muhimu kweli, kwa kuzingatia kwamba nchi ya Congo DRC inaitegemea reli hiyo kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake, ambacho ni chanzo kikubwa sana cha uchumi wa nchi yetu. Naomba kujua ni upi mkakati wa Serikali wa kuharakisha ujenzi wa reli hiyo baada ya upembuzi huu ambao unakamilika mwezi huu wa Septemba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kavejuru Aliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kwamba kazi ya upembuzi yakinifu inafanyika na inakamilika mwaka huu, Septemba, 2021. Pia nimesema kwenye majibu ya swali la msingi kwamba tunatafuta mkopo wa gharama nafuu usio na masharti magumu ili ujenzi uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge naomba atupe nafasi tulifanyie kazi jambo hili. Limepewa uzito mkubwa na Mheshimiwa Rais ameshaelekeza kwamba miradi yote ya kimkakati ikiwepo hii SGR, kama nilivyotaja kwenye majibu yangu ya msingi, ni lazima ijengwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mbunge naomba awe na amani, eneo hili reli itajengwa na watu wa eneo hili watapata huduma ya usafiri. Ahsante sana.