Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kavejuru Eliadory Felix (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na namshukuru Mungu kwa mara ya kwanza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi ya pekee kwanza kuwashukuru wananchi wapiga kura wote walionipigia kura nyingi kule kwenye Jimbo la Buhigwe. Ninawashukuru sana na ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi ya pekee kutoka kwenye moyo wangu wa shukrani kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoka humu wakaja kunipambania. Ushindi wangu nilioupata ni wa sisi sote, ni wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Chama changu Cha Mapinduzi, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyoniteua na hatimaye nikapeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi na leo niko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, ninaomba sasa niende kwenye hoja mama. Kwenye wilaya yangu naenda kujikita kwenye suala la minada ya mifugo. Wizara ya Mifugo tunashukuru sana imetengeneza, imekarabati, imejenga mnada ambao unasimamiwa na wizara. Lakini huo mnada mpaka sasa hivi una zaidi ya miezi saba ulikwishakamilika, mkandarasi amekwishawaomba ili awakabidhi Wizara nao hawajafika. Ninaomba Wizara ije ifungue ili huo mnada ufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya ninayotoka iko mpakani, tunayo changamoto inayotokana na tozo ambalo inaonekana ni kubwa kwa wafanyabiashara wa mifugo. Ng’ombe mmoja anayesafirishwa nje na ni wafanyabiashara wadogo wadogo tu, tozo yake, ada yake ni 25,000. Hiyo imesababisha wafanyabiashara wa nchi jirani ambayo ni Burundi pale, hawaji kwenye minada yetu. Naomba Wizara ipunguze tozo hiyo ili waweze kuvuka na wanunue mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mnada wa halmashauri ambao uko mbali kwenye Tarafa ya Myama. Kwenye Tarafa ya Manyovu tuna ng’ombe wengi sana. Mifugo hio wanaenda kiholela, wanatoroshwa, hatuna mnada. Ninaomba tufungue mnada mwingine wa Halmashauri katika Kata ya Kibande ambayo ni karibu kabisa na iko mpakani mwa Burundi, ili Warundi waweze kuvuka wenyewe na wakishavuka wanunue wale ng’ombe na biashara nyingine zitaamka pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi hapo hapo kwenye Idara ya Mifugo ninayo Tarafa ya Myama, ina kata saba. Kuna kata moja inaitwa Kata ya Kajana, ina mifugo wengi; hatuna josho. Naomba josho lijengwe pale. Nikirudi kwenye minada, tulikuwa na Afisa Minada mmoja lakini mpaka ninaposimama na kuzungumza hapa mbele ya Bunge lako Tukufu amekwishahamishiwa Pugu. Naomba mtuletee Afisa Minada ili aendeshe huo mnada ambao mmetujengea ulete tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kuchangia hapo kwenye mifugo, tuna matatizo na tuna upungufu wa Maafisa Ugani. Hata wale waliopo hawana vitendea kazi. Tunaomba Wizara yako iwaone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara ya kwanza, naamini Wabunge wenzangu mtaendelea kunilea. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kumpongeza Waziri wa Nishati na Naibu wake na viongozi wote wanaoshirikiana kwa utumishi wao uliotukuka, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikushukuru wewe binafsi kwa kuniona lile la vinasaba kurudi kwenye TBS na Wabunge wote wakaamua litungiwe sheria. Hili ni jambo jema na la ukombozi kwa uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda ni mchache, naomba niende moja kwa moja kwenye changamoto za umeme katika Mkoa wa Kigoma. Umeme ndiyo ufunguo wa maendeleo ya viwanda na ni uhai wa maendeleo ya jamii. Mkoa wetu mpaka sasa haujaungwa na Gridi ya Taifa na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati amesema hapa kwamba ifikapo 2023, Mkoa wetu utakuwa umeungwa na Gridi ya Taifa na hilo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu. Kuna vituo viwili vya kupozea umeme, Kituo cha Nguruka na Kidahwe. Nilikuwa nawasiliana mchana huu, je, ile site ambayo ilipendekezwa kijengwe kituo cha kupozea umeme kuna shughuli yoyote inayofanyika, jawabu ni kwamba hakuna chochote kinachoendelea na muda unaendelea kusonga mbele. Watu wa Kigoma tumekaa kwenye giza kwa muda mrefu, watu wa Kigoma wanaasili ya kufanya kazi sana, tuna mazao ya kimkakati ya michikichi ambapo mwaka kesho tunahitaji tuwe na viwanda, tunaomba tuungwe kwenye Gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jimbo langu la Buhingwe, namshukuru Waziri na mkandarasi ambaye alitupa amesonga mbele, lakini naomba kasi iendelee kwa kuweka umeme kwenye Vijiji vya Janda, Murungu, Changwe, Kilelema na vingine vyote vilivyobaki ili na sisi pale pafunguke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri ustawi wa Taifa lolote ule utategemea maendeleo yaliyopo lakini ukiwa unaongezwa na kukuzwa na tafiti. Nimshauri Waziri wa Nishati awekeze kwenye utafiti kwa kuwa kule Uganda pamekwishagunduliwa mafuta kwenye Ziwa Albert na wataalam wa miamba wanasema kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu ambapo sisi Tanzania ni matajiri yawezekana tuna hazina kubwa ya mafuta na gesi basi utafiti uendelezwe na kuwepo mtaji wa kuweka kwenye tafiti ili tafiti ziendelee na tuendelee kubaini utajiri ambao Mwenyezi Mungu ametujalia.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii adhimu kwanza kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia kwa kutuletea bajeti nzuri. Nampongeza na Makamu wake Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Nampongeza Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu na watumishi wote wa Wizara ya Fedha. Bajeti waliyoiandaa hakika inatibu kiu ya Watanzania. Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kwa namna ya pekee Waziri Mkuu kwa Mkoa wetu wa Kigoma jinsi anavyosimamia zao la kimkakati la Mchikichi, Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye hoja ya bajeti. Nimeipitia bajeti, nikaangalia Tanzania sasa hivi inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 60. Katika milioni 60, ni 5% tu ndio ambao ni direct tax payer, wanaolipa kodi moja kwa moja. Asilimia tano katika milioni 60 ni sawa na milioni tatu. Ukitoa kwenye milioni 60 unabakiza milioni 57 ambao sio walipaji wa kodi wa moja kwa moja. Nikajiuliza swali: Je, upo uwezekano wa watu milioni tatu kulipa kodi ambazo zitatosheleza Serikali itoe huduma kwa watu milioni 57? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri wa Fedha anisikilize kwa makini tuna kila haja ya kutafuta na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza tukapanua wigo wa kodi. Wigo wa kodi ni lazima utokane na kupanua wingi wa shughuli za kiuchumi ndani ya nchi yetu, naomba nishauri, Tanzania tumejaliwa vyanzo vingi. Mungu ametujalia, lakini hatujavifanyia kazi. Mathalani Mkoa wetu wa Kigoma, Mungu ametupa ardhi nzuri, inastawi kila aina ya mazao, lakini ndani ya ardhi hiyo Mungu ametupa madini ya Dolomite ambayo ndiyo malighafi haswa ya mbolea ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atambue kwamba katika Mkoa wa Kigoma tuna madini ya Dolomite ambayo mimi mwenyewe niliwahi kuhusika kwenye kampuni iliyokuwa ya Kimarekani wakapita wa Anglo American walikuwa kwenye utafiti wa madini, walisema maeneo yafuatayo; Ilagara, Kazuramimba, Basanza, Makere na Kitagata ni maeneo ambayo yana malighafi ya kutengeneza mbolea ya kusaidia nchi hii na tunaweza tukafanya mapinduzi ya kilimo kwa kupata mbolea ambayo inaweza ikatengenezwa ndani ya nchi yetu. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa jicho la pekee. Wakati wale wa Ngara wanasaidiwa kile kiwanda cha Nikeli na Liganga tuangalie uwezekano wa kuwa na kiwanda cha kutengeneza mbolea katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijiuliza, kwa nini tunaagiza chumvi kutoka nje wakati sisi kwenye ukanda wa ziwa wa bahari tuna vyanzo vingi vya kutengeneza chumvi? Ukienda kule kwenye Ziwa Eyasi upande Meatu Mkoa wa Simiyu, tuna deposit kubwa ya chumvi. Ukija Kigoma, ile miamba yote ya Uvinza ni chumvi. Kwa nini tusiweke uwekezaji mkubwa na tukazalisha ya kutosheleza na ile fedha ambayo tunaagiza bidhaa ya chumvi nje tukaitumia kwa mahitaji mengine na badala yake tukauza sisi wenyewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie mahali hapo kama sehemu mpya ambapo itakuwa ni chanzo cha mapato ya fedha ya Serikali na chanzo cha ajira kwa waliokosa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuendelea, ni lazima tufunge mkanda kwa kufanya mapinduzi katika kilimo chetu. Hata Ulaya waliendelea baada ya kufanya mapinduzi katika kilimo. Tunahitaji sekta ya umwagiliaji ipewe fedha. Zaidi ya hapo kwenye tafiti papewe kipaumbele. Hatuwezi tukasonga mbele kama hatuna tafiti. Tunaomba tafiti kwenye kilimo zipewe kipaumbele, kwenye madini zipewe kipaumbele na kwenye uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye uvuvi nayo ni sehemu ambapo tunaweza tukapata fedha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, mengine unaweza ukamwandikia Waziri, umechangia vizuri sana.

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa upekee kabisa kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia hoja kwenye Azimio la uanzishwaji wa Soko Huru katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, azimio hili ni azimio zuri sana, linafaida nyingi sana, ningeomba kila Mbunge aweze kuridhia mkataba huu, una faida nyingi sana. Kwanza ukiangalia nchi yetu kijiografia Tanzania mahali ilipo tumebahatika kuwa sehemu nzuri kijiografia, tuna maliasili, tuna ardhi nzuri. Kwa hiyo ni suala tu la kujipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhia mkataba huu utafungua masoko mapya kwa mazao yetu ya kilimo. Tunachangamoto ya mazao kama tulivyoona kwenye mahindi, lakini litafungua masoko mapya kwa mazao mengine madogo madogo kama alizeti na choroko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mkataba huu utaimarisha mnyororo wa thamani utakuwepo na nini na ushindani, ushindani wa uzalishaji ambao tunaenda kushindana katika soko hilo huru utaboresha ubora wa mazao yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo mimi ninashauri sana, ninashauri Serikali ijipange kwa kuelimisha kwa kutoa elimu kwa mapana na kwa marefu kwa wazalishaji wetu. Kama ni kilimo sasa twende kwenye kilimo cha biashara, tulime kilimo cha kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile taasisi za kifedha zijipange kupunguza riba na ziwe tayari kusaidia wazalishaji kwa maana ya wakulima na wajasiriamali wapate mitaji ili tuweze kusogea kwenda kwenye masoko ya mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu ambazo zipo sasa hivi nchi ambayo ina uchumi mzuri kwenye hili soko ambalo tunaenda kwenye wale wanachama ambao wamekwisha saini ambao ni 42. Nchi ambayo ina uchumi mzuri sasa hivi ni Nigeria ikifuatiwa na Egypt, ikifuatiwa na Afrika Kusini, sisi hatupo mbali sana tupo kama namba 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tuna nafasi nzuri kama Serikali ikijipanga ikahakikisha, ikaboresha miundo mbinu ili wakulima wetu huko wanako zalisha barabara zikafika, kukawepo na gharama ndogo za usafirishaji wa mazao yetu tutafaidika zaidi, zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo azimio hili ni zuri, litatusogeza mbele, litaenda kuzalisha mabilionea wengi katika Tanzania yetu na litaenda kuleta mabadiliko makubwa sana katika sekta mbalimbali; sekta ya kilimo na biashara pia kutokana na ushindani utakaotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga hoja Azimio hili la Mkataba wa Uundwaji wa Soko Huru la Afrika. (Makofi)