Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Florence George Samizi (7 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, asante sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yako mazuri nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuishukuru Serikali kwa kutupatia kituo hicho katika Kata ya Bunyambo ambayo ilikuwa hatuna kituo cha afya katika Tarafa hii ya Kibondo Mjini tangu tupate uhuru. Lakini hata hivyo Kata hii ya Murungu iko takribani kilometa 31 kutoka Kibondo Mjini ambapo kuna hospitali ya wilaya na ukizingatia kwamba sasa bado tuna kata 8 katika tarafa hii ambazo hazina kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi ni lini Serikali itatujengea kituo cha afya katika Kata hii ya Murungu kwa kuzingatia umbali huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninatambua na Serikali inatambua kwamba tunahitaji kupata kituo cha afya katika Kata ya Murungu na ni ahadi za viongozi wetu wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Serikali inaendelea kutafuta fedha na mara fedha zikipatikana tutapeleka fedha pale kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, asante sana. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga na kuboresha miundombinu ya maji katika Jimbo la Muhambwe, hususan Kata za Kibondo Mjini, Bunyambo na Kitahana ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji ulioko katika jimbo hilo?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe, nadhani mwezi mmoja ama miwili iliyopita, Mheshimiwa Mbunge wa Mihambwe ameingia katika Bunge hili. Amekuja ofisini, na jana tumekwisha mpa pesa, zaidi ya milioni 100 ili kuhakikisha kwamba wananchi wake wanakwenda kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana kuwasaidia wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi: -

Mheshimiwa Spika, soko hili la ujirani mwema ni soko kati ya nchi ya Tanzania na Burundi. Kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, mahali pale Serikali imeweka pesa kujenga yale mabanda kwa ajili ya biashara, lakini hakuna kituo cha polisi, hakuna TRA, wala hakuna uhamiaji, hivyo, kufanya utendaji wa soko lile kuwa hafifu kwa sababu ya hatarishi hii.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa mpaka uko kilometa tano ndani ya nchi ya Tanzania kwa hiyo, hata pale ambapo uhamiaji wanafanya shughuli zao za kawaida inasababisha usumbufu sana kwa wananchi. Hivyo, napenda kujua ni lini Serikali itaweka vile vipaumbele vya One Stop Centre kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, ikiwamo forodha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Florence kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwasemea wananchi wa Muhambwe, lakini nimhakikishie kwamba, hoja hizi zote ambazo amezileta Serikali imeanza kufanyia kazi, likiwemo suala hili la kupima maeneo ya viwanja 145 kuzunguka soko, ili tuweze kupata maeneo kwa ajili ya kujenga Vituo vya Polisi, Forodha, lakini pia nae neo la Uhamiaji. Kwa hiyo, mara baada ya ramani zile kukamilishwa ambazo tayari mchakato unatarajiwa kuanza wakati wowote, sasa tutaenda kuomba kwenye sekta husika waweze kujenga vituo hivi na kuwezesha soko kufanya kazi vizuri. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipatia nafasi.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibondo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kwamba nyaraka za zabuni kwa sasa ziko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya vetting ili kazi ya upanuzi wa uwanja huo zianze. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kizazi ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi wa Kata aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge wametoa nguvu zao, wameanza ujenzi wa kituo cha Afya na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia. Tumekubaliana kwamba tukipata fedha tutakwenda kuchangia nguvu za wananchi pale, kituo cha afya kikamilike tuanze kutoa huduma za afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, halmashauri hii makusanyo yake ya mwaka 2021 ilikuwa bilioni 5.3 kwa mwaka na Jimbo hili la Muhambwe liko mpakani ambapo tuna biashara za ujirani mwema kwenye Masoko ya Mkarazi na Kumshwabure. Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa kujenga TRA ya kudumu lakini pia na kujenda ushuru wa pamoja mpakani ili kudhibiti biashara holela za mpakani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, wananchi wa Muhambwe wanafuata huduma za leseni Mkoani Kigoma ambapo ni kilomita 240 kutoka Jimbo la Muhambwe. Je, ni lini Serikali itaanzisha huduma za leseni katika Jimbo la Muhambwe ili kuwaondolea adha wananchi hawa wa Muhambwe?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, Serikali imelichukua na tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba ikimpendeza Mheshimiwa Mbunge niambatane naye kwenda kuona hali halisi ya Wilaya ya Kibondo, tuone namna gani tunaweza tukatatua usumbufu huu ambao wanapata wananchi wetu wa Kibondo. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa skimu zilizojengwa katika Jimbo la Mhambwe, ikiwemo Nyendara, lumpungu, Kigina, Mgondogondo, Kahambwe, lili ziweze kuwasaidia wakulima wa jimbo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika moja ya mikakati tuliyonayo katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha tunakarabati na kukamilisha skimu ambazo tulizipitia na kuona zinahitaji marekebisho madogo ili wananchi waendelee kutumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika baadhi ya skimu katika Jimbo lake zitatekelezwa mwaka huu na nyingine katika mwaka ujao wa fedha. (Makofi)