Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Florence George Samizi (3 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Hayati Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais wa sasa na Waziri Mkuu ya kujenga Kituo cha Afya Kata ya Murungu katika Wilaya ya Kibondo ili kusogeza huduma na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Jimbo la Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati Vituo vya Kutolea huduma za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa Huduma za Afya ya Msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati wa huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza mkakati huu, Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 25.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa 90 zisizo na Vituo vya Afya ikiwemo Tarafa ya Kibondo Mjini inayoundwa na Kata tisa za Murungu, Bunyambo, Kibondo Mjini, Biturana, Kumwambu, Kitahana, Rusohoko, Misezero na Bitare ambapo kiasi cha shilingi milioni 250 kimepelekwa kwa jili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Bunyambo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mkakati huu, Serikali, itaendelea kutoa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi zote za Viongozi.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa soko la ujirani mwema katika Kijiji cha Mukarazi ikiwemo miundombinu na ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Pamoja katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Folrence George Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Soko la Mukarazi ulianza kutekelezwa Juni, 2018 na kukamilika Oktoba, 2020. Ujenzi wa Soko hilo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 442.61 na kwa sasa soko limekamilika kwa asilimia 100 na linatumika mara mbili kwa wiki.

Mheshimiwa Spika, ili kufanya soko hilo kutumika kikamilifu Halmashauri imetoa kiasi cha Shilingi milioni 5.6 kwa ajili ya kupima viwanja 145 katika eneo la soko kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo biashara, huduma za polisi na forodha. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -

Je, ni lini Ofisi ya TRA itajengwa katika Halmashauri ya Kibondo ili kuzuia biashara holela katika masoko ya ujirani mwema kati ya Tanzania na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, TRA ilifanya utafiti katika maeneo yote nchini yenye uhitaji wa ofisi za kudumu za usimamizi wa kodi ikiwemo Halmashauri ya Kibondo na kubaini kuwa gharama za usimamizi wa kodi katika Wilaya ya Kibondo zitakuwa kubwa ikilinganishwa na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa. Kwa muktadha huo, TRA itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ukusanyaji wa kodi katika wilaya hiyo ili mara tu itakapokidhi vigezo, TRA itafungua ofisi za kudumu. Aidha, TRA itaendelea kuimarisha mfumo wa sasa wa kuhudumia walipakodi wa Wilaya ya Kibondo ili kuwawezesha kulipa kodi bila usumbufu wowote. Ahsante.