Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bakar Hamad Bakar (1 total)

MUswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu kuweza kuchangia muswada huu wa sheria ambao tunaenda kuujadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa uwasilishaji wake mzuri wa mapendekezo haya ya muswada huu wa sheria, lakini kipekee sana naomba nimpongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati ya PAC, Mama Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, kwa uwasilishaji mzuri na wa fasaha sana kwenye hotuba yake ambayo ametoka kuiwasilisha. Mchango wangu mimi utakwenda kwenye maoni haya ya jumla ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwenye muswada huu wa sheria, Ibara ya 18 ambayo imefanyia marekebisho kwenye kifungu cha 30, inakwenda kuzifanya au kuzitaka biashara zote ambazo mitaji yake ni kuanzia milioni 700 ama turn over ya milioni 500 kwenda kuwasajili ama kuwaajiri wahasibu ambao wamesajiliwa wenye CPA, lakini tunazo taasisi ama mashirika ya umma makubwa yenye mitaji zaidi ya hizo milioni 700 na zaidi ya hizo milioni 500 ambazo zimetajwa ndani ya sheria hii ambazo zimefanya taasisi zisizokuwa za Serikali ziajiri wahasibu, lakini mashirika haya kwenye kurugenzi zao hayana wahasibu wenye CPA. Kwa hiyo, tumependekeza kwenye Bodi za Wakurugenzi kwenye mashirika haya ya umma angalao na wao wawe na mhasibu japo mmoja kwenye bodi zile ambaye atakwenda kusaidia kwenye masuala haya ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bodi nyingi za wakurugenzi kwenye mashirika na mashirika yetu haya ndio ambayo yanakwenda kuzalisha na ndio ambayo yanakwenda kuongeza mapato makubwa kwenye nchi yetu. Sasa kuziacha tu bodi hizi bila ya wenye taaluma hii na jambo hili kuwekwa kwenye sheria kwa kweli ni kuzipa mianya bodi hizi kukwepa wana-taaluma hii wenye CPA. Kwa hiyo, tunapendekeza sana kwamba jambo hili lina uzito mkubwa na liweze kuchukuliwa kuingizwa kwa wahasibu wenye taaluma ya uhasibu wenye CPA kwenye Bodi za Wakurugenzi kwenye mashirika mbalimbali ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, NBAA ni taasisi ya kitaifa, lakini sheria hii ambayo tunaenda kuipitisha/kuitunga leo, ni sheria ambayo inahusu Tanzania Bara peke yake. Tunatambua kwamba Zanzibar sasa hivi wapo kwenye mchakato wa kuanzisha bodi kama hii ambayo itahusiana na usajili wa wahasibu na wakaguzi kwa kule Zanzibar, lakini bado kuna ukakasi kwamba, kwa sababu hii ya NBAA ni Bodi ya Taifa, je, recognition ya wana-taaluma hawa itakuwaje? Wale ambao watasajiliwa na Bodi ya Zanzibar watakapokuja huku Bara watatambulikaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii bado ipo kimya sana, haijaeleza kwamba, tutawatambuaje wana-taaluma hii watakaotoka upande mmoja wa muungano kwenye sehemu nyingine, wale watakaotoka Tanzania Bara kwenda kufanya kazi Zanzibar Bodi ya Zanzibar itakuwaje, lakini wale ambao watasajiliwa na Bodi ya Zanzibar watakaokuja kufanya kazi huku Bara watatambulikaje na sheria hii? Kwa hiyo, tunaomba pia Mheshimiwa Waziri aje atueleze jambo hili kwenye sheria hii litakaaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa sababu, taasisi hii ni ya kitaifa, tayari ime-comply na imejiunga na taasisi mbalimbali za kimataifa, sasa siamini kwamba taasisi kama hii ambayo itaundwa kule Zanzibar itapata ruhusa wapi ya kuweza kujisajili na taasisi za kimataifa? Ziko taasisi mbalimbali kama IVAC, lakini iko PAFA, kuna INTROSAI na AFROSAI; taasisi zote hizi NBAA ni mwanachama kule, lakini je, Bodi ya Zanzibar ambayo itaenda kuundwa sasa hivi itakuwa mwanachama kule? Itaruhusiwa kuundwa kule?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, tunaona kwamba, kwa experience tunazo bodi au tunazo taasisi ambazo Zanzibar na Tanzania Bara zinakanganyana kwenye kujiunga ama kupata ushirikiano kwenye mashirika ya kimataifa, nikitoa mfano, tunayo TFF na ZFF kule mpaka leo Zanzibar si mwanachama wa mashirika yale au taasisi zile za kitaifa zinazohusiana na jambo hili. Kwa hiyo, na jambo hili tunaliona kwamba, huko mbele huenda, kuna wasiwasi, ikaja ikatokezea mkanganyiko kama huu na ikatokezea mtafaruku kwenye mambo yetu haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 4 kwenye muswada huu imetaja majukumu ya Bodi hii ya NBAA, lakini majukumu haya tunaona kwamba yamechukuliwa/ yamechanganywa majukumu ya udhibiti na usimamizi. Tumependekeza kwamba tuanzishe public oversight body ambayo itaenda kushughulikia baadhi ya majukumu kwamba, tusiipe mzigo mkubwa taasisi hii ya NBAA kufanya mambo yote ya udhibiti pamoja na usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)