Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwantatu Mbarak Khamis (1 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii kwa mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nami kuweza kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu Muumba Mbingu na Ardhi ambaye amenijalia pumzi na wakati huu nikaweza kusimama hapa kuelezea mchango wangu juu ya bajeti yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na walionitangulia kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri kwa namna ambavyo wameanza kutelekeza majukumu/kazi yao na kuwajengea matumaini zaidi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wake Mheshimiwa Masauni pamoja na Watendaji wa Wizara ya Fedha kwa kuandaa pamoja na kutuwasilishia bajeti hii ambayo leo tuko hapa katika kuijadili; bajeti iliyojaa matumaini na bajeti iliyobeba dhamira ya kuwaendeleza Watanzania. Hii ni ishara njema ya namna ambavyo Serikali yetu ya Awamu ya Sita inavyokwenda kutatua shida za wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa suala zima la uimarishaji wa elimu. Nichukue nafasi hii pia kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa namna ilivyojipanga katika suala zima la kuimarisha elimu Tanzania kwa kujenga Shule za Sekondari nyingi, Shule za Msingi pamoja na kukarabati shule za zamani na isitoshe kuajiri walimu wengi kwa lengo la kuimarisha elimu na kuona watoto wetu wanapata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili zaidi nitazungumzia wanafunzi wenye ulemavu. Nachukua nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa namna walivyojali wanafunzi wenye ulemavu na wakaweza kuwajengea mazingira mazuri. Ukiangalia uhitimu wa wanafunzi wenye ulemavu kipindi cha nyuma na sasa hivi ni tofauti. Kwa sasa kila mwaka ufaulu wa wanafunzi wenye ulemavu umekuwa ukiongezeka kwenda sekondari na hata vyuo, na wewe mwenyewe nadhani utakuwa shahidi. Hii yote inatokana na juhudi za Serikali kusomesha walimu wa kutosha ambao wanasomea kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum. Pia hii inatokana na jitihada za walimu hawa. Bila ya jitihada hii, hawa wanafunzi wasingefika hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali kuangalia walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu kwa sababu walimu hawa wana kazi kubwa. Kumfundisha mwanafunzi mwenye ulemavu ni tofauti na kumfundisha mwanafunzi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu anayefundisha mwanafunzi mwenye ulemavu anatumia masaa mengi zaidi. Kwa hiyo, tunahitaji kuwajengea uwezo lakini pia kuwapa motisha ili waweze kuwasaidia watoto wetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa, nataka kuzungumzia suala la tozo. Naunga mkono mapendekezo ya Waziri kuhusu kufanyia marekebisho Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa bidhaa zinazonunuliwa Tanzania Bara kwenda Zanzibar na zinazonunuliwa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Napongeza marekebisho haya kwa sababu yatakwenda kuondoa kero ya muda mrefu ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wafanyabiashara. Siyo tu kwa wafanyabiashara, hata kwa wananchi wa kawaida ambao walikuwa wakinunua bidhaa zao kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande wa pili wa Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala hilo pia litaondoa zile hoja kwa wale wasioutakia mema Muungano wetu waliokuwa wakilitumia sana suala hili. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa tunatengeneza sheria nyingi na nzuri na pale ambapo tunahisi zinahitaji marekebisho tunafanya hivyo, lakini tunatengeneza sheria, tunafanyia marekebisho, lakini shida inakuja katika utekelezaji wa sheria kutokana na baadhi ya Watendaji wetu kutokuwa na uaminifu na hii usababisha mambo yasiende kama yalivyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika hili, namwomba Mheshimiwa Waziri baada ya kufanya marekebisho haya, awe mfuatiliaji mzuri na timu yake hili kuona malengo ya Serikali yameweza kufikiwa. Pamoja na hayo, pia namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atupe ufafanuzi wa kina juu ya tozo hizi: Je, sitahusika mpaka kusafirisha magari? Kwa sababu unapotoa gari Zanzibar kule Bara ni shughuli; au unapotoa gari Bara kuleta Zanzibar ni shughuli. Aje atufafanulie, tozo hizi ni vipi zitagusa masuala ya magari unapotaka kusafirisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine nitajikita katika suala zima la tozo katika kufanya miamala ya matumizi ya simu. Hili suala ni jema sana, Serikali yetu ipo katika kuona inatengeneza mazingira kwa maslahi ya wananchi wake. Kuna miradi mingi imepangwa, kuna shughuli nyingi zimepangwa katekelezwa na zote hizi zinategemea mapato. Kwa hiyo, naunga mkono suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mheshimiwa Waziri kuwasilisha hotuba yake hapa, kumekuwa na uelewa tofauti tofauti na watu wanazungumza maneno tofauti juu ya tozo hizi. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho basi aje atoe ufafanuzi wa kina juu ya tozo hizi kwa lengo la kuleta uelewa mzuri kwa wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika mchango wangu mwingine ambao unazungumzia miradi ya kimkakati inayoibuliwa na Halmashauri zetu. Kuna miradi ambayo huwa inaibuliwa na Halmashauri. Miradi hii inaibuliwa lakini kuna vigezo maalum. Kigezo cha kwanza, Halmashauri iwe na uwezo wa kuongeza mapato, iwe na uwezo na mpango wa kujitegemea na pia iwe na uwezo wa kuandika andiko la mradi. Hata hivyo, kuna Halmashauri zetu nyingine tunaona hazitaweza kukidhi hivi vigezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetunga sheria ya kuzitaka Halmashauri kuchangia asilimia 10 ya mapato yake. Tumeona katika ripoti, inaeleza kwamba kuna Halmashauri zimetimiza asilimia 100, kuna Halmashauri asilimia 30, na nyingine asilimia 50. Hata hivyo, kuna Halmashauri zimewezesha vikundi vingi, lakini kuna Halmashauri zimewezesha vikundi kidogo. Hii inatokana na uwezo wa Halmashauri zenyewe.

Kwa hiyo, kutokana na vigezo hivi, nahisi bado hazijatendewa haki zile Halmashauri zenye uwezo mdogo; na lengo letu ni kuziwezesha Halmashauri kukusanya mapato na kuhudumia wananchi pamoja na kuleta maendeleo katika Halmashauri zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naomba sana iundwe timu ya wataalam iende kwenye Halmashauri, tuziangalie Halmashauri ambazo hazina uwezo, zijengewe uwezo hili waweze kuzitambua fursa zinazowazunguka ili nao waingie katika ushindani wa makusanyo. Kwa hiyo, Halmashauri hizi nazo zitaongeza uwezo wake na wataweza kutimiza matakwa ya sheria ya kukamilisha kwa asilimia 100 yale makusanyo ya asilimia 10 ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi/Vigelegele)