Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Suleiman Haroub Suleiman (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kutoa mchango wangu katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2021 - 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nakushukuru wewe kwa kuongoza kikao hiki kwa uweledi na Ufanisi. Nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania kwa uongozi wake imara na wenye matokeo chanya kwa Taifa letu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu wa Wizara na Watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani na pongezi hizo, nina michango, ushauri na maswali yenye lengo la kujenga, siyo kubomoa. Naishauri Wizara kushirikiana na Serikali za Mikoa, Wilaya na Mitaa. Lengo kuu ni kushajiisha utalii wa ndani, kwani wananchi wengi hawana uelewa juu ya dhana nzima ya utalii. Hivyo basi, Serikali hizo zitasaidia kushajiisha, kuhamasisha na kuelimisha dhana nzima ya utalii. Pia Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio Wenyeviti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa sehemu zao. Amani na utulivu ndio kitu muhimu sana kwa ustawi wa utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii ni sekta mtambuka, hivyo basi, naishauri Wizara kuendelea kushirikiana na baadhi ya taasisi ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya TAMISEMI, Kilimo na Ardhi, kwani itasaidia kufikisha huduma stahiki kwa watalii wa ndani na wa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara kuboresha miundombinu tofauti ikiwemo mawasiliano ya simu, barabara kwa baadhi ya hifadhi sambamba na sehemu za vivutio vya utalii. Kwani ukosefu wa Mawasiliano kutazorotesha uongezekaji wa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na janga lililoikabili dunia, Covid 19, nashauri Serikali kuboresha utalii wa ndani kwa ushirikiano baina ya SMZ na SMT kwani kuna vivutio vipo Zanzibar ambavyo Tanzania Bara hakuna, pia vipo vivutio Tanzania Bara ambavyo Zanzibar havipo. Tubuni vivutio ziada vya Utalii, mfano ngoma za jadi ili kuhifadhi utamaduni, silka, mila na desturi, kuendeleza miradi kwa kiwango kizuri na kwa muda stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri nilioainisha hapo juu, napenda kutoa pongezi za dhati tena kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara. Nimefarajika kuona kunaanzishwa aina tofauti za utalii, ukiwemo utalii wa michezo, utalii wa fukwe na utalii wa meli. Swali langu ni: Je, meli kwa ajili ya utalii huo ipo wapi sasa hivi; na je, ina hadhi ya watalii wa kiwango gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hamwoni haja ya kuanzisha utalii wa tiba asili? Je, Wizara imejiandaa vipi kukuza utalii wa ndani kwa vitendo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawatakia kazi njema kwa maslahi ya uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na uzima.

Pili, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliongoza vizuri sana Taifa letu. Aidha, nakupongeza wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na wasaidizi wako wote kwa kuendesha vikao vya Bunge kwa umakini na umahiri kabisa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa wasilisho zuri na hotuba yenye kuleta matumaini kwa ustawi mzuri wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, naomba kuchangia sehemu mbili tu nazo ni ushirikiano kwa Taasisi za SMZ na Taasisi za SMT.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu ni kiungo muhimu sana katika kutatua changamoto mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Nazipongeza ofisi hizi kwa kazi nzuri wanazozifanya, lakini bado kuna haja kuendeleza ushirikiano kwa taasisi za zetu ambazo sio za Muungano Kikatiba. Mfano Afya, Maji, Uwekezaji, Utalii na kadhalika, kwani ushirikiano huo kasi yake ikiongezeka basi itakuwa na mafanikio kwa SMZ na SMT na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pili ni masuala ya mazima ya kupambana na masuala ya udhalilishaji na ukiukwaji wa maadili. Matendo ya kujamiiana ya jinsia moja au ndoa za jinsia moja sambamba na uharibifu wa vizazi vyetu kwa maana watoto wetu. Jambo hili ni hatarishi sana kwa ustawi mzuri wa Taifa letu. Hivyo naiomba Serikali na Watanzania kwa ujumla kukemea na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu na Katiba yetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naunga mkono hotuba hii kwa asilimia mia, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara yetu muhimu kwa ustawi wa Taifa letu. Aidha, naomba kuchukua fursa hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu kwa kutuongoza kwa umahiri na uweledi mkubwa, ninamuombea kwa Mwenyezi Mungu amjaalie afya njema na mafanikio mema zaidi.

Pia pongezi kwa Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia nampongeza Waziri Mheshimiwa Engineer Hamad Yusuf Masauni na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia IGP, Makanda, RPC, OCD na maafande wetu wote walio chini ya Wizara hii. Nchi ipo salama na kwa mipango na mikakati ya Wizara hii nina imani thabiti kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama na Watanzania tutaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba kuchangia na kushauri machache kama ifuatavyo; kwanza kutoa mafunzo ya ukarimu na matumizi ya lugha nzuri kwa wananchi. Kuna baadhi ya askari hasa Zanzibar unapokwenda kutafuta huduma za usalama na ulinzi baadhi ya askari wanawajibu raia lugha zisizoridhisha na zinazovunja moyo, haziendani na heshima ya Jeshi letu

Pili, utoaji wa huduma nzuri hasa katika sehemu za kuingia nchini kwa mfano uwanja wa ndege na bandarini, mfano Zanzibar uchumi wake unategemea zaidi sekta ya utalii hivyo basi askari wa Uhamiaji wa maeneo hayo ni vizuri watoe huduma nzuri na stahiki kwa Watanzania na wasio Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu Vitambulisho vya Mtanzania kwa wenye sifa za kupatiwa. Kuna ukakasi kwa baadhi ya maeneo katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo.

Nne ni kuhusu doria; ni jambo zuri sana kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yetu sehemu tofauti za nchi yetu hivyo ninashauri Jeshi la Polisi liendelee na doria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho, naipongeza Serikali inayoongozwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na wasaidizi wao wote. Aidha nikutakie kheri na mafanikio mema zaidi Waziri - Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni na Naibu Waziri - Mheshimiwa Jumanne Sagini katika kutimiza majukumu mliokabidhiwa na Mheshimiwa Rais kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na amani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake uliotukuka kheri na baraka ziwe kwake.

Mheshimiwa Spika, aidha natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii wakiongozwa na Dkt. Francis.
Mheshimiwa Spika, binafsi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, nimejionea na kupata taarifa za utekelezaji wa Wizara katika kipindi cha Kamati hivyo basi nina ushauri tu kwa maslahi ya Taifa letu.

Kwanza, Wizara hii sio Wizara inayoshughulikia masuala ya Muungano wa Tanzania, lakini ushirikiano kati ya baadhi ya taasisi za SMZ na SMT zitasaidia kuengeza idadi ya watalii wa ndani na wakimataifa. Mfano, Mamlaka ya Hifadhi na Urithi wa Mji Mkongwe Zanzibar, Idara ya Mambo ya Kale, Idara ya Utamaduni na Sanaa, Mamlaka ya Mazingira na kadhalika, hivyo basi nashauri Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Zanzibar kwa lengo la kuongeza idadi na namba ya watalii.

Mheshimiwa Spika, pili, Wizara kuongeza kasi ya utangazaji wa vivutio sambamba na kubuni activities tofauti katika vivutio vyetu. Mfano, kuweka michezo ndani ya maeneo wanayozuru/sehemu za utalii. Hii itasaidia wageni kushawishika kuja mara kwa mara nchini.
Tatu, kuboresha miundombinu katika maeneo yanayotumika kwa wageni kutembelea, mfano barabara; nne kuboresha huduma ya mawasiliano katika hifadhi zetu. Kukosa mawasiliano ni changamoto kwa watalii kwani zipo sehemu bado mawasiliano ya simu hakuna.
Tano, kufikisha huduma za kifedha kwa baadhi ya maeneo yanayotumika kwa kazi za kitalii. Mfano ATM, WAKALA na kadhalika ili mtalii aweze kutumia akiwa ndani ya hifadhi kununua huduma tofauti na hii zaidi inawalenga watalii wa ndani; sita, kumaliza miradi yenye kuongeza idadi ya watalii lakini pia yenye kuongeza fursa za ujio wa watalii nchini, mfano, meli kwa ajili ya utalii wa majini, malango katika hifadhi zetu, Mradi wa REGROW, Mradi wa Nyuki na kadhalika.

Saba, kuitumia filamu ya Royal Tour katika matamasha ya kimataifa. kwani filamu ya royal tour imeitangaza sana nchi yetu; nane, Wizara kutumia historia na uasilia wa maeneo yanayotumika kwa shughuli za kitalii. mfano; Mikindani (biashara ya Utumwa), machifu na historia zao (Chifu Mkwawa Nyika wa Iringa) na kadhalika; tisa kuipa nguvu Idara ya Malikale na Makumbusho na kumi, kuboresha mahusiano mema na Mataifa tofauti.

Mheshimiwa Spika, kumi na moja, Wizara ifikirie kuweka kumbukumbu ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa nguvu ya kifedha na maarifa Wizara hii na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, hitimisho, nampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia na kuisaidia sekta ya utalii kifedha kwa kuamini kuwa sekta hii ina mchango mkubwa sana kuinua uchumi wa Tanzania. Ninawatakia kila la kheri katika kutimiza majukumu mliokabidhiwa na Mheshimiwa Rais. Mimi Mjumbe wa Kamati naunga mkono hoja asilimia mia. Ahsante sana.