Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Stella Simon Fiyao (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Jambo la kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniba neema na kibali cha kuwepo katika Bunge hili la Kumi na Mbili. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naishukuru familia yangu ambayo imekuwa bega kwa bega na mimi mpaka hatua ya mwisho hata kuipata hii nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende moja kwa moja kwenye kuchangia suala la hotuba ya Mheshimiwa Rais kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo kwenye Taifa hili limekuwa ni muhimu sana na linahitaji kuchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu sana. Endapo suala hili litachukuliwa kwa uzito huo itapelekea kutokutoa shilingi trilioni 1.3 kila mwaka kwa ajili ya kwenda kuagiza chakula nje ya nchi na fedha hii tuielekeze moja kwa moja kwenye pembejeo za kilimo ili wakulima waweze kupata pembejeo kwa bei ndogo na waweze kulima na kupata mazao ya kutosha ikiwa ni sambamba na kuwatafutia soko la mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba suala la kilimo limebeba ajira nyingi sana za vijana ndani ya Taifa letu na endapo tutalichukulia kipaumbele, tutapunguza changamoto kubwa ya vijana wetu kukosa ajira ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni la wafanyabiashara ndani ya Taifa letu la Tanzania. Suala hili limekuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara. Issue ya kodi imekuwa ni changamoto kubwa sana ambayo inapelekea wafanyabiashara wengi ndani ya Taifa kukimbia na kwenda kuwekeza katika mataifa mengine kwa sababu ya kukwepa kodi kubwa ambazo wameendelea kuzipata ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba kuna umuhimuwa kupitia upya Sheria za Kodi kwa wafanyabiashara, kwa sababu kodi hizi zimekuwa ni kandamizi. Huu utaratibu waTRA kuwakadiria kodi wafanyabiashara, unapaswa kupitiwa kwa upya. Wafanyabiashara wamekuwa wakikadiriwa kodi kubwa na wakati mwingine zinazozidi mitaji yao na hivyo kupelekeakukimbia kuwekeza ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Mheshimiwa Rais amesema wazi kabisa kwamba anahitaji kodi ziwe rafiki kwa wafanyabiashara, kuna umuhimu mkubwa wa kulichukulia jambo hili kwa uzito ili wafanyabiashara wengi na wa kutoka mataifa mengi waweze kuwekeza ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho kabisa, pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kusimamia uchaguzi, lakini ni suala lisilopingika kabisa na ni suala la wazi kabisa kwamba uchaguzi ulikuwa na dosari nyingi. Kutoka hatua ya kwanza kabisa ya zoezi la uchukuaji wa fomu, zoezi la urudishwaji liligubigwa na mambo mengi ya ovyo kabisa. Katika hatua ya kwanza ya uchukuaji wa fomu, wagombea wengi kutoka Vyama vya Upinzani walikamatwa na kupewa kesi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, siku zilivyokaribia za urudishaji wa fomu, hata wale waliokuwa wamebahatika kuchukua fomu, walikamatwa na kupewa kesi, hawakupata kabisa ile nafasi ya kurudisha fomu. Pamoja na hilo, hata wale ambao walipata nafasi ya kurudisha fomu, siku chache baadaye walikamatwa na kupewa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kabisa, hatuwezi kusema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki. Pamoja na hilo, hata tu mara baada ya uchaguzi wananchi walijitokeza kwenda kupiga kura. Watu walipiga kura kwa kujitoa na wengine walikuwa ni wazee, wengine walikuwa ni wanawake wajawazito, lakini watu walivamiwa kwenye vituo vya kupigia kura. Wengine walipigwa, wengine waliumizwa na wengine wameachiwa majeraha mpaka sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, hata mara tu baada ya wananchi kupiga kura, wagombea walitangazwa kabla ya majumuisho. Ni kitu ambacho kinaumiza sana.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, wakati natafuta amekaa wapi huyo mtoa taarifa, kengele imeshagonga.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha. Ahsante.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Muswada huu wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Pia niipongeze Wizara kwa kuleta Muswada huu muhimu sana kwa Taifa letu. Naamini Muswada huu utaenda kuwa mwarobaini wa changamoto ambayo wananchi wetu wamekuwa wakikutana nayo.

Ninavyosema changamoto hakuna asiyejua kwamba kukosekana kwa hii sheria kumepelekea wananchi kukumbana na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na kuingiliwa katika mambo yao binafsi. Sisi sote ni mashahidi wa miaka miwili, mitatu iliyopita kuna watu waliingiliwa mpaka kwenye akaunti zao, wakasachiwa na wakakutwa wana kiasi cha shilingi ngapi na wakafilisiwa, wote ni mashahidi.

Mheshimiwa Spika, naamini Muswada huu unakwenda kuwa mwarobaini kwa Taifa letu na pia unakwenda kusaidia kuongeza wawekezaji wa nje na ndani kwenye Taifa letu kwa sababu tunajua tumechelewa kuna maeneo tumekosa wawekezaji ni kwa sababu ya kukosa tu hii sheria. Sasa naamini Bunge hili likipitisha hii sheria, tutakwenda kupata wawekezaji wa nje na ndani wa kutosha kwa sababu wawekezaji wengi wanashindwa kuwekeza kwenye Taifa ambalo halina hii Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lakini sasa naamini tunakwenda kupata wawekezaji wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba niwe na mambo machache ya kushauri. Kwenye Muswada huu ni muhimu kukaongezwa neno faragha ili kuleta uzito wa hii sheria. Tukiongeza neno faragha, tunajua neno faragha limebeba tafsiri kubwa ili tulete uzito mkubwa wa hii sheria, tuliongeze hili neno kwenye hiki kichwa cha hii sheria na hii itaweza kusaidia.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna mambo mengi ambayo yamezungumzwa kwenye huu Muswada ikiwa kwenye kifungu cha 47 faini za kiutawala. Kwenye faini za kiutawala imezungumziwa kwamba faini ya mwisho itakuwa ni shilingi milioni 100, lakini hawajatoa ufafanuzi kwamba hiyo milioni 100 italenga makosa yapi. Jambo hili linaenda kuleta mwanya wa watu kuonewa hata kama leo hii watatuambia kwamba mambo haya yatakwenda kuonekana kwenye kanuni, amesema ndugu yangu Mtaturu pale. Mambo ya kanuni Wabunge tunakuwa hatuhusiki, tunatunga sheria salama na rafiki kwa wananchi, lakini hawa wananchi wetu wanakwenda kuumizwa na kanuni ambazo zinakuwa zimetungwa na Wabunge tunakuwa hatujazipitia. Kwa hiyo hapo tunakwenda kutengeneza tatizo.

Mheshimiwa Spika, ili twende sawa na sheria hizi zikawe salama ni zikawe rafiki kwa wananchi wetu, ni vyema kwenye utungaji wa kanuni wakaangalia maslahi mapana ya mwananchi ili mwananchi asiende kuumizwa huko. Naamini tukifanya hivyo hili linaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nisiwe na maneno mengi sana ya kusema kwenye hili jambo, lakini niombe tu niwashawishi Wabunge wenzangu kwenye Bunge hili kwamba tuipitishe sheria hii ili tuweze kwenda kunufaika kama Taifa na iweze kuwasaidia wananchi wetu wa chini na wa kawaida ambao wameendelea kuonewa kwa kukosekana sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Mpango wa Tatu wa Bajti ya Taifa letu. Nijikite moja kwa moja katika sekta ya kilimo, ni Dhahiri kuwa sekta ya kilimo imekuwa ikichangia kwa asilimia kubwa katika pato la Taifa. Lakini kwa bahati mbaya bajeti ya sekta ya kilimo imekuwa haitekelezeki. Imekuwa kilimo kikipewa bajeti ndogo sana na kusababisha mambo mengi kukwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sekta hii kuchangia katika pato la Taifa letu wakulima wetu wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi sana na kubwa katika suala zima la pembejeo za kilimo. Na changamoto hii inasababishwa na mlundikano mkubwa wa kodi uliopo kwa wafanyabiashara na umesbabisha wakulima wetu kuumia sana, lakini kwa kuwa ni jukumu letu sisi kama Waheshimiwa Wabunge, kuhakikisha tunaishauri Serikali ili tuweze kuzipitia sheria za kodi na kuzifanyia marekebisho. Tuna jukumu kubwa la kufanya maana sheria zilizopo zinawaumiza sana wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili pia liendane sambamba na kutafuta soko. Kumekuwa na changamoto kubwa ya masoko ya mazao, hususan katika Mkoa wa Songwe wananchi wetu wamekuwa wakijishughulisha sana na zao la kahawa, zao la mahindi, zao la mpunga na maharage na mambo mengine. Lakini kwa sasa ukienda Songwe mahindi gunia linauzwa kwa shilingi 30,000/= tu wakati huo mkulima nanunua mbolea kwa bei ya 65,000/= mpaka 70,000/= mbolea aina na DAP, kitu ambacho kinasababisha wakulima wetu kuumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linawatesa sana wakulima wetu na kuwakatisha tamaa sana katika suala zima la kilimo. Kwa nini nasema tuangalie masoko? Asilimia kubwa wananchi wa Mkoa wa Songwe na Rukwa walikuwa wanategemea sana kuwauzia Wakongo mahindi na Wakenya, lakini leo hii biashara imekufa, Wakongo hawawezi kununua tena mahindi kwasababu, watu wa Afrika Kusini wameliteka soko la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkulima wa Tanzania akibeba mahindi kwenda kuyapeleka Kongo kutoka Tanzania kwenda kufika Kongo ni kilometa zaidi ya 1,000 lakini mtu wa Afrika Kusini akitoka na mahindi kutoka Afrika Kusini kwenda kufika Kongo ni kilometa zaidi ya 2,000 lakini mtu wa Afrika Kusini anauza mahindi kwa kilo 250/= na Mtanzania anauza kwa 360/= lakini bado haimlipi. Jambo hili linawakatisha sana tamaa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sababu ya kuweka uhusiano mzuri na mataifa ambayo yanatusaidia katika suala zima la soko, ili tuweze kuwanufaisha pia wakulima wetu na kutokuwakatisha tamaa. Lakini pia Serikali ituambie ni kwa namna gani kilimo ambacho ndicho uti wa mgongo wa Taifa letu kinaweza kuinua pato la Taifa. Ikiwa tu bajeti inayotengwa haitekelezeki kwa mwaka 2019/2020 utaona bajeti iliyotekelezeka ni asilimia 15 tu. Sasa tutawezaje kuinua wakulima kama bajeti tunayopanga ndani ya Bunge hili haiwezi kutekelezeka kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo tuna haja kubwa ya kutunga sheria za kusimamia utekelezaji wa bajeti ambazo tunazipitisha ndani ya Bunge hili, ili ziweze kutekelezeka. Na kuwepo nidhamu katika kutekeleza bajeti ambazo tunakuwa tunazipitisha ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la umeme. Tumeendelea kuzungumzia suala la viwanda ndani ya Taifa letu. Ni dhahiri kabisa kwamba, viwanda asilimia kubwa vinategemea umeme. Lakini leo ukienda katika Mkoa wa Songwe limekuwa ni jambo la kawaida umeme kukatika siku mbili mpaka tatu bila sababu za msingi. Sasa hawa watu ambao tunataka wawekeze katika Taifa letu, wawekezaji wa ndani nan je tunawakatisha tamaa. Mtu hawezi kuweka kiwanda akitegemea kutegemea nguvu ya solar ama generator kuendesha kiwanda chake. Ni lazima ategemee umeme ili uweze kumsaidia kwenye kiwanda, sasa tusifike mahali kuwakatisha tamaa wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza katika Taifa letu kwa njia ya umeme tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii umeme Mkoa wa Songwe umekuwa ni kawaida kukatikakatika, lakini ukikaa Dodoma hapa unaweza ukajisahau kwamba, Songwe na Dodoma ni nchi mbili tofauti, lakini kumbe mikoa yote iko ndani ya Taifa moja. Umeme Dodoma mimi sijawahi kushuhudia umeme ukiwa umekatika ndani ya Jiji la Dodoma, lakini Songwe ni kawaida umeme kukatika. Tunawahamasisha vijana wetu kujiwekeza, tunahamasisha vijana wetu kujiajiri, hivi leo kijana amejiajiri katika kazi anachomelea, wengine wana saluni, umeme unakatika siku mbili-tatu maisha yake atayaendeshaje kwa namna hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawakatisha tamaa pia vijana wetu. Tuombe suala la umeme pia lichukuliwe ili tuweze kuwatia moyo wawekezaji na vijana wetu ambao wameamua kujiajiri ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa mpango huu uendane na kuzipa nguvu halmashauri zetu ikiwa ni pamoja na kurejesha baadhi ya vyanzo ambavyo vimechukuliwa na Serikali kuu. Mfano chanzo cha property tax, chanzo hiki tuliona tu kwenye vyombo vya Habari kwamba, Waziri ametangaza kwamba, halmashauri watakusanya, lakini uhalisia ni kwamba, fedha hizo zitakusanywa na halmashauri na zitapelekwa Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pengine tuone tunaona kwamba, inaonekana Serikali Kuu tumekosa watu wa kutukusanyia tunataka halmashauri sasa itusaidie halafu mwisho wa siku fedha hizi zinakuja kwenye Serikali kuu. Tunaomba kama Serikali kuu imedhamiria kukirudisha chanzo hiki kwenye halmashauri, halmashauri wakusanye wao na fedha hizo ziingie katika mfuko wa halmashauri, jambo hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote tunajua kwa asilimia kubwa ukiangalia kwenye masuala ya barabara leo hii tunazungumzia mambo ya barabara ambazo zinaendeshwa na TARURA. Tumekuwa tukifeli sana kwasababu, aslimia kubwa TARURA wanategemea chanzo cha ndani cha halmashauri na halmashauri tumekuwa tukipata fedha kidogo kwasababu ya vyanzo vingi kuchukuliwa na Serikali kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe sasa kama itawezekana vyanzo ambavyo vinawezekanika halmashauri kukusanya turidishe mikononi mwa halmashauri na halmashauri iendelee kukusanya, ili iweze kujiendesha pia. Kwasababu, kuna wakati tunapata hata hati zisizoridhisha kwenye halmashauri zetu kwasababu ya miradi kuchelewa kutekelezeka yote ni kwasababu ya Serikali kuu kutopeleka fedha kwa wakati na kutopeleka fedha za kutosha kulingana na bajeti inavyokuwa imetengwa na halmashauri. Tuweze kuzipa miguu halmashauri, ili ziweze kutembea na ziepukane na kupata hati chafu na hati zisizoridhisha. Vyanzo vingi ambavyo halmashauri inaweza kuvirejesha tuweze kuvirudisha halmashauri iweze kukusanya. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, najua wazi kabisa kwamba moja ya majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuwa kiunganishi baina ya Serikali na vyama vya siasa, lakini ajabu ni kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu haijatekeleza jukumu hili la kuhakikisha inaviunganisha vyama vya siasa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mahusiano kati ya Serikali na Vyama vya Siasa, hususan Vyama vya Upinzani yamekuwa na uhasama na uadui mkubwa kwa kipindi chote cha miaka mitano. Ndani ya miaka mitano tumeshuhudia mambo kadhaa yakiendelea kutokea ndani ya Taifa letu…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Stella, pokea Taarifa. Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
maneno yanayosemwa na Mheshimiwa Mbunge siyo sahihi. Kama Serikali na Vyama vya Siasa tungekuwa na uhasama mkubwa, usingeshuhudia Vyama vya Siasa vikienda kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vimekuwa vikitoka hadharani na kuthibitisha kwamba kwa kweli, katika kujenga demokrasia na ujenzi wa ustawi wa Watanzania, kazi ya Serikali inaungwa mkono na Vyama vya Siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa vimekuwa vikitoka hadharani katika maadhimisho ya shughuli mbalimbali za Kitaifa na kuthibitishia Watanzania kwa umoja wao kama vyama vya siasa vinakubali kwamba Serikali imesimama na inatekeleza majukumu yake sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo, ni mifano michache ya kuonesha kwamba Serikali na vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano ya karibu na mmekuwa mkishuhudia katika matukio mbalimbali Serikali iko na vyama vya siasa. (Makofi)

SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Stella Fiyao, Taarifa unayopewa ndiyo hiyo. Kwamba ushirikiano upo isipokuwa chama ambacho chenyewe hakitaki tu.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia mambo mengi katika Serikali yakiendelea, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa kuzuiliwa mikutano ya hadhara, jambo ambalo liko kikatiba na katika Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia viongozi wa vyama vya siasa na wanachama, hususan wa vyama vya upinzani, wakikamatwa, wakishitakiwa na Serikali na kupewa kesi mbalimbali zikiwemo kesi za uhujumu uchumi, kesi za uchochezi na wakati mwingine kupewa hata fine kubwa ambazo haziko kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya miaka mitano…

SPIKA: Niliona taarifa, wapi? (Kicheko)

Aah, endelea Mheshimiwa Stella Fiyao. Aah, Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Kicheko)

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu na nchi nyingi ambazo hazijaendelea, tunaongea sana siasa badala ya uchumi. Hata tukiwa hapa kwetu nchini tunawatoa Watanzania wetu ku-concentrate kwenye masuala ya uchumi na kulenga zaidi siasa.

Mheshimiwa Spika, rai yangu kwa Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Rais ametoa kauli ambayo ni njema sana kwamba kesi zote ambazo hazina base zifutwe. Kwa kauli ya aina hiyo, ni nia ya dhati sana ya kiongozi wa kisiasa kusema.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu, kwa sababu tunajadili masuala ya kibajeti na tumetoka kujadili mpango, Waheshimiwa Wabunge, hebu tuchukue mwelekeo huo. Hata viongozi wa kisiasa ambao wako nje ya nchi, warudi tujenge nchi yetu, tujenge uchumi. Hata viongozi wa kisiasa ambao wako hapa wanajadili vitu ambavyo vinawatoa wananchi wetu kwenye umoja, tufuate kauli ya Mheshimiwa Rais ambayo ameonesha nia ya dhati. Tusimtoe kwenye dira hiyo ili tujenge uchumi.

Mheshimiwa Spika, tuna dola 1,080 tu, bado tuna deni la karibu dola 2,090 kufikia dola 3,000 ambayo ni lengo la uchumi wa kati wa kiwango cha juu ili tuweze kutafuta uchumi wa juu zaidi. Nawasilisha.

SPIKA: Mheshimiwa Stella, taarifa hiyo unapewa kwamba siasa zote baada ya uchaguzi ni hapa mjengoni. Unapokea?

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, tunasubiri utekelezaji wa hicho alichokisema Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho pia tumeshuhudia Miswada Miswada ya Sheria za Vyama Vya Siasa ikiletwa ndani ya Bunge. Miswada hiyo ilikuwa na masharti magumu kwa vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na kuvidhibiti, lakini mbaya zaidi ni kuingilia chaguzi za ndani za vyama vya siasa. Vyama vya siasa vilipotoa wito kwa Serikali wa kufanya maridhiano ya kujenga umoja wa Kitaifa, Serikali ilinyamaza kimya, mpaka sasa haijasema chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo basi, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya vyama vingi, tumetengeneza hofu kubwa sana kwa wananchi. Tumezalisha hofu kubwa, hasa kwa wafuasi wa vyama vya upinzani kwani, wafuasi wengi wa vyama upinzani sasa hivi hawana amani kwa kuwa tu wako vyama vya upinzani. Mfano mzuri ni katika Mkoa wa Songwe, Jimbo la Tunduma…

SPIKA: Mheshimiwa Fiyao subiri. Mheshimiwa Katambi ulikuwa umesimama, taarifa. (Kicheko)

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kwa Mzungumzaji kwamba katika Katiba yetu, Ibara ya 107(a) inasema kwamba chombo pekee cha utoaji haki kitakuwa ni Mahakama. Kwa msingi huo, mpaka sasa ninavyozungumza, nimefanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, amethibitisha kwamba hakuna electoral petition yoyote ambayo imepelekwa kwa maana ya kwamba wakati wa uchaguzi kama kuna mtu aliumizwa angeweza kutumia avenue ya kisheria. Katika hilo nimpe Taarifa pia, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watu wote wana usawa, kwa mujibu wa Ibara ya 13. Usawa huu mbele ya sheria, haiangalii chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Taarifa ninayompa, katika kipindi chote, hata wakati fulani ambapo tulijaribu kwenda kuzurura hivi, kuna kesi ambazo wakishinda upande mwingine, wataona Mahakama imetenda haki; wakishindwa kesi hiyo, inaonekana kwamba Mahakama haziko huru. Vilevile kwenye uchaguzi, wakishinda uchaguzi kama alivyoshinda pale Nkasi, Tume ilikuwa huru, lakini wakishindwa uchaguzi, Tume haiko huru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jean-Jacques Rousseau na Montesqueus walitoa msingi wa separation of power kwamba kutakuwa na Bunge, Serikali na Mahakama. Katika hivi, kuna institutional separation na functionale separation na personale separation. Kwa msingi huo, maana yake vyombo hivi vinasimamiana na ndiyo maana leo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko huru, chaguzi zinafanyika kwa uhuru na hakuna kesi yoyote iliyopelekwa Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipenda nimpe Mheshimiwa Mbunge taarifa hiyo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Fiyao shule hiyo umeielewa kidogo?

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea. Mfano mzuri ni kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe, Jimbo la Tunduma ambao wanaishi mpakani. Leo hii wananchi asilimia kubwa wanakimbilia nchi jirani ya Zambia kutokana na hofu kubwa kwa kutishiwa na Madiwani ambao wamepita, wako madarakani, wameendelea kuwatisha wananchi wakiwapa kesi za kuwasingizia na zisizokuwa na dhamana. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, hata wakipewa kesi zenye dhamana Watendaji wa Kata na Mitaa wamekataa kutoa barua kwa kusingizia kwamba wanatishiwa na Wakuu wa Wilaya kutoa barua za dhamana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Stella dakika zako zimeisha. (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, muda wangu ulikuwa bado.

SPIKA: Dakika zako zimeisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ukiukwaji mkubwa sana wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa na Jeshi la Polisi na ukiukwaji huu umefanyika hasa pale Polisi wanapokuwa wakiwakamata watuhumiwa, wamekuwa wakikiuka hizi haki ikiwa na pamoja na kuwafanyia vitu vya hovyo ambavyo pia vinakiuka kabisa haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu iliyotolewa Aprili, 2021, imesema wazi kabisa, ripoti hiyo ilikuwa ni ya mwaka 2019/2020, imesema wazi kabisa kwamba matukio manne ya mauaji ya raia yamefanyika mikononi mwa polisi. Na matukio haya yalifanyika tu kutokana na polisi kuwakamata watuhumiwa kwa kutumia nguvu kubwa sana ambayo ilisababisha pia watuhumiwa kupoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, Ibara ya 13(6)(b), nitainukuu, inasema wazi kabisa kwamba; “Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo;”(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini haya mambo tumekuwa tukiyashuhudia wazi kabisa, raia wetu wakitendewa mambo ya ajabu, kana kwamba wameshakutwa na makosa wakati huo bado Mahakama inakuwa haijathibitisha makosa yao, jambo ambalo linakiuka haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, sheria hiyohiyo Ibara ya 13(6)(e), inasema; “Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili tumeliona likifanywa na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, lakini mbali na hayo, tunajua wazi kabisa, wakati mwingine watuhumiwa wanapokamatwa na kupelekwa katika vituo vya polisi kule hakuna bajeti ya chakula, lakini watu wamekuwa wakikamatwa, wakijazwa katika vituo vya polisi na sheria inasema mtu akikamatwa anatakiwa akae kwenye kituo cha polisi saa zisizozidi 48. Lakini watu wanakaa mpaka wiki mbili wako mikononi mwa polisi, jambo ambalo limekuwa likikiuka kabisa sheria za…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa; mwenye taarifa aendelee.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hata matendo ya kikatili kwa watoto wa kike na wanawake yanafanyika katika vituo vyetu vya polisi, wanavyokamatwa watu wanafanyiwa mpaka ubakaji kwenye vituo vyetu vya polisi.

Mheshimiwa Spika, nampa taarifa hiyo kwasababu vipo na kama utakuwa unatakiwa uthibitisho watu waende wakaulize mahabusu ambao wamekaa zaidi ya mwezi vituo vya polisi na wakapelekwa magerezani.


SPIKA: Pokea taarifa Mheshimiwa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, ninaipokea taarifa hiyo kwasababu hata mwaka jana, mwezi Agosti nilipokamatwa na Jeshi la Polisi, nilitishiwa kumwagiwa tindikali usoni. Kwa hiyo hivyo ni vitendo ambavyo vinafanywa na Jeshi la Polisi.

SPIKA: Mheshimiwa Stella, yaani kidogo nishtuke kwamba na wewe ilikuwa… endelea kuchangia Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, suala la wananchi wetu kukosa dhamana; leo hii suala la dhamana limekuwa kama tu ni zawadi ya polisi. Wananchi wamekuwa wakikosa dhamana kwa makosa ambayo yanadhaminika kisheria. Na jambo hili limesababisha magereza mengi kujaa sana. Jambo hili la wananchi wetu kunyimwa dhamana limesababisha wananchi wetu kujaa sana huko magereza bila sababu za msingi.

Mheshimiwa Spika, wakati huohuo, kumekuwa na matukio mengi sana ambayo yanasababisha kunyima uhuru wa watu wetu, ikiwa ni pamoja na watu kukaa muda mrefu gerezani, mtu anakaa mpaka miaka kumi, mitano, mitatu, kesi yake bado haijasikilizwa. Akiuliza anaambiwa upelelezi bado haujakamilika. Lakini mwisho wa siku huyu mtu inakuja kutolewa hukumu hajakutwa na hatia, amekaa gerezani miaka kumi, hiki tunawanyima wananchi wetu haki zao za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaishauri Serikali iweze kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Makosa ya Jinai, tufanye marekebisho ya sheria hizo ili kuwapa uhuru wananchi wetu. Kwasababu mwisho wa siku tunayajaza tu magereza bila kuwa na masuala ya msingi kabisa.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kabisa; ndani ya magereza kumekuwa na mambo mengi sana ambayo wengine wameyazungumzia lakini ntayazumgumzia hapa. Pamoja na changamoto ambayo ameizungumzia dada yangu, Mheshimiwa Esther, magerezani kiukweli kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, leo hii magereza wanachanganywa na watoto wa miaka 13, 14 hadi 15. Mwanamke wa miaka 60 anakaguliwa mbele ya mtoto wa miaka 14; hili jambo kiukweli linahuzunisha sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Stella, muda hauko upande wetu.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji, Mkoa wa Songwe pia umekuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo imekumbwa na changamoto kubwa sana ya maji. Mkoa wa Songwe ni mkoa wenye kata 94 lakini kati ya kata zote hizo hakuna kata ambayo ina uhakika wa kupata maji. Hivyo changamoto hiyo imepelekea wananchi wa Mkoa wa Songwe kutumia muda wao mwingi sana kuhakikisha wanapambana kutatua changamoto ya maji kwenye maeneo yao.

Mheshimia Naibu Spika, naamini kabisa changamoto hii ya maji ikiweza kutatuliwa itaweza kuepusha migogoro mingi ya ndoa ambayo inatokea pasipo sababu za msingi. Pia changamoto hii ikitatuliwa endapo tutaweza kuondoa migogoro ya ndani ya ndoa tutaepusha pia changamoto kubwa ya watoto wa mitaani ambao ni zao kubwa la migogoro ya ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba utekelezaji wa miradi ya maji umekuwa na changamoto kubwa sana na utekelezaji huu bajeti yake imekuwa ikitekelezwa kwa kiwango kisichoridhisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika,katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, fedha ambazo zilikuwa zimetengwa katika utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika miradi ya maji ni bilioni 913.83, lakini fedha ambayo ilikuwa imetolewa ilikuwa ni bilioni 230.99 tu. Jambo hilo lilisababisha utekelezaji wa miradi ya maji kutekelezwa kwa asilimia 25 tu na kutotekelezwa kwa asilimia 75, jambo ambalo pia linawakwamisha sana wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara ilitengewa bilioni 623.6, lakini fedha ambazo zilikuwa zimetolewa zilikuwa ni bilioni 135.19, ambapo miradi iliweza kutekelezwa kwa asilimia 22 tu, hivyo tuliweza kufeli kwa asilimia 78, miradi ya maendeleo ya maji haikuweza kutekelezwa kwa asilimia 78 jambo ambalo tulifeli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2018/2019, bajeti iliweza kutekelezwa kwa asilimia 15 tu na kwa mwaka 2019/2020, bajeti iliweza kutekelezwa kwa asilimia 61, lakini kwa mwaka 2021 bajeti iliweza kutekelezwa kwa asilimia 40. Jambo hili linatupelekea kukwama sana kwa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto hiyo ya bajeti ndogo, kumekuwa na changamoto kubwa pia ambayo inapelekea kufeli sana hasa kwenye visima ambavyo tunachimba. Changamoto hiyo inasababishwa na upungufu wa wataalam wa kufanya tafiti kwenye maeneo yetu ili kujua ni wapi maji yanaweza kupatikana; kuna maeneo tumechimba visima maji hayajapatikana kabisa, hivyo ikapelekea kuonekana kama fedha tunatupa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, inaonyesha wazi kabisa kwamba kati ya visima 10,485 visima vilivyochimbwa visima 490 havikuweza kuwa na maji. Pia CAG alibaini wazi kwamba, kati ya fedha bilioni 768 zilizopelekwa kwa ajili ya uchimbaji wa visima ambazo pia baada ya visima hivyo kuchimbwa, visima hivyo havikuweza kuwa na maji, maana yake tukapelekea kuonekana kwamba tumetupa karibu ya kiasi cha Shilingi bilioni 764.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hizi zinasababishwa na kutokuwa na watafiti wa kutosha katika maeneo yetu. Hivyo naishauri Serikali, tuna sababu kubwa ya kuwa na wataalam wengi wa kufanya tafiti kabla ya kuchimba visima vya maji ili Serikali tusiweze kuingia hasara. Tukifanya hivyo naamini tutaweza kufanikiwa katika suala zima la maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa ambayo pia imebainishwa na CAG, suala zima la madai ya Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), imebaini kuwa karibu kiasi cha bilioni 12 wanaidai Serikali. Ili tuweze kufanikiwa katika miradi ya maji, tulipe haya madeni ambayo tunadaiwa na RUWASA ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kwa moyo kabisa. Tukifanya hivi naamini tutaweza kupunguza changamoto kubwa ya maji ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote naomba nizungumze wazi, nimesema hapo awali wananchi wa Mkoa wa Songwe ni wahanga wakubwa wa suala zima la maji safi na salama. Jambo hili limekuwa likipelekea wananchi wetu kuugua typhoid mara kwa mara kwa sababu maji wanayoyapata sio safi na salama, lakini bado hawapati maji ya kutosha maana yake hayohayo yasiyo na salama bado sio ya kutosha kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie ni lini atatekeleza mradi wa maji kutoka Ileje ili uweze kuwakomboa wananchi wa Mkoa wa Songwe, waweze kuondokana na changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili katika kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Muswada huu wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Pia niipongeze Wizara kwa kuleta Muswada huu muhimu sana kwa Taifa letu. Naamini Muswada huu utaenda kuwa mwarobaini wa changamoto ambayo wananchi wetu wamekuwa wakikutana nayo.

Ninavyosema changamoto hakuna asiyejua kwamba kukosekana kwa hii sheria kumepelekea wananchi kukumbana na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na kuingiliwa katika mambo yao binafsi. Sisi sote ni mashahidi wa miaka miwili, mitatu iliyopita kuna watu waliingiliwa mpaka kwenye akaunti zao, wakasachiwa na wakakutwa wana kiasi cha shilingi ngapi na wakafilisiwa, wote ni mashahidi.

Mheshimiwa Spika, naamini Muswada huu unakwenda kuwa mwarobaini kwa Taifa letu na pia unakwenda kusaidia kuongeza wawekezaji wa nje na ndani kwenye Taifa letu kwa sababu tunajua tumechelewa kuna maeneo tumekosa wawekezaji ni kwa sababu ya kukosa tu hii sheria. Sasa naamini Bunge hili likipitisha hii sheria, tutakwenda kupata wawekezaji wa nje na ndani wa kutosha kwa sababu wawekezaji wengi wanashindwa kuwekeza kwenye Taifa ambalo halina hii Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lakini sasa naamini tunakwenda kupata wawekezaji wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba niwe na mambo machache ya kushauri. Kwenye Muswada huu ni muhimu kukaongezwa neno faragha ili kuleta uzito wa hii sheria. Tukiongeza neno faragha, tunajua neno faragha limebeba tafsiri kubwa ili tulete uzito mkubwa wa hii sheria, tuliongeze hili neno kwenye hiki kichwa cha hii sheria na hii itaweza kusaidia.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna mambo mengi ambayo yamezungumzwa kwenye huu Muswada ikiwa kwenye kifungu cha 47 faini za kiutawala. Kwenye faini za kiutawala imezungumziwa kwamba faini ya mwisho itakuwa ni shilingi milioni 100, lakini hawajatoa ufafanuzi kwamba hiyo milioni 100 italenga makosa yapi. Jambo hili linaenda kuleta mwanya wa watu kuonewa hata kama leo hii watatuambia kwamba mambo haya yatakwenda kuonekana kwenye kanuni, amesema ndugu yangu Mtaturu pale. Mambo ya kanuni Wabunge tunakuwa hatuhusiki, tunatunga sheria salama na rafiki kwa wananchi, lakini hawa wananchi wetu wanakwenda kuumizwa na kanuni ambazo zinakuwa zimetungwa na Wabunge tunakuwa hatujazipitia. Kwa hiyo hapo tunakwenda kutengeneza tatizo.

Mheshimiwa Spika, ili twende sawa na sheria hizi zikawe salama ni zikawe rafiki kwa wananchi wetu, ni vyema kwenye utungaji wa kanuni wakaangalia maslahi mapana ya mwananchi ili mwananchi asiende kuumizwa huko. Naamini tukifanya hivyo hili linaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nisiwe na maneno mengi sana ya kusema kwenye hili jambo, lakini niombe tu niwashawishi Wabunge wenzangu kwenye Bunge hili kwamba tuipitishe sheria hii ili tuweze kwenda kunufaika kama Taifa na iweze kuwasaidia wananchi wetu wa chini na wa kawaida ambao wameendelea kuonewa kwa kukosekana sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonyesha wazi kabisa kuna changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara katika nchi yetu, na hii changamoto inaikabili nchi yetu kwa Kiswahili chepesi tunaweza tukasema hili ni Janga la Taifa kwa sasa, kwa sababu karibu kila Mbunge aliyesimama hapa ameweza kuzungumzia changamoto ambayo inamkabili kwenye Jimbo na kwenye Mkoa wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii inaonekana ni changamoto kubwa sana na tuseme tu wazi uchumi wa Taifa letu kwa asilimia kubwa pia unategemea miundombinu mizuri ya barabara. Ili uchumi uweze kukua ni lazima kuwe na miundombinu iliyo mizuri, wawekezaji hawawezi kuja kuwekeza mahali ambapo pana miundombinu mibovu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni katika Mkoa wetu wa Songwe, katika Mkoa wetu wa Songwe tuna ardhi nzuri yenye rutuba ya kutosha, lakini changamoto kubwa ambayo inasababisha wawekezaji washindwe kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wetu ni kutokuwa na miundombinu iliyo mizuri ya barabara. Muwekezaji kwa namna yoyote anapokuja kuwekeza eneo lolote lile kitu cha kwanza anaangalia miundombinu imekaaje, je, kama atalima mazao, atavuna atayafikishaje eneo la soko? Mwisho wa siku tumekosa wawekezaji kwa sababu kubwa tu ya miundombinu kuwa mibovu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Jimbo la Tunduma, ndani ya Jimbo la Tunduma tuna barabara ambazo wananchi walipisha kutoka mwaka 2016/17 walipisha kwa hiari yao wenyewe wakavunja zile nyumba ili kupisha barabara, lakini mpaka leo hili jambo la barabara limekuwa ni stori kwa wananchi wa mji wa Tunduma na badala yake wameishia kuambulia vumbi na kuugua mafua yasiotibika kila kunapoitwa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anasimama atuambie ni lini ataweza kukamilisha barabara hizi ambazo wananchi wamepisha kwa hiari yao wenyewe pia kulipwa fidia ya aina yoyote ile ni lini ataweza kuzijenga barabara hizi, ili mwisho wa siku wananchi wa Tunduma wasikatishwe tamaa kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la ucheleweshwaji wa malipo ya wakandarasi. Ucheleweshwaji wa malipo ya wakandarasi umekuwa ukilisababishia Taifa kupata hasara kubwa sana. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021, ripoti ya CAG imezungumza wazi kabisa katika ujenzi wa reli ya SGR hasara namna tulivyopata kwa sababu ya wakandarasi kucheleweshewa kupata fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti inasema kipande cha kwanza cha ujenzi wa Reli ya SGR wakandarasi walicheleweshewa kupata fedha zao ndani ya muda waliokubaliana ndani ya muda wa siku 56, lakini baada ya kuchelewesha Mhandisi Mshauri aliweza kupokea nyaraka za madai na vielelezo ambavyo wakandarasi walikuwa wakiidai Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mwisho wa siku riba iliyotozwa kwa ucheleweshwaji wa wakandarasi ilikuwa ni dola za kimarekani milioni moja na laki mbili na elfu themanini na sita na pointi tisini na moja ($1,286,000.91) ambazo kwa fedha za Kitanzania ilikuwa ni takribani bilioni mbili na milioni mia tisa themanini na tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii inaonyesha namna gani ambavyo Serikali tunapata hasara za kizembe na fedha hizi ziliidhinishiwa na hao wakandarasi wakalipwa fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapata wasiwasi ni hasara ngapi ambazo tunazipata kutokana na wakandarasi kucheleweshewa kulipwa fedha zao kwa wakati, wakati huo fedha zote hizi zingetusaidia kutekeleza miradi mingi ambayo wabunge wamekuwa wakiipigiwa kelele ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuepusha mianya ya ufujaji fedha za umma tunaomba Serikali ilisimamie jambo hili kuhakikisha wakandarasi wanalipwa fedha zao kwa wakati ili kuepukana na kuiletea Serikali hasara zisizokuwa na msingi. (Makofi)

MHE. RIDHIWANI J.M. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana muda wake umekwisha Mheshimiwa

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. RIDHIWAN J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tumsaidie tu Mheshimiwa Mbunge anafoka sana anatuumiza masikio.

MHE. STELLA S. FIYAO: Nakula vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nashukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika wizara muhimu ya Viwanda na Biashara na niseme tu wizara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa kuanza na Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa mwaka 2020 ambayo ripoti hiyo imeitaja Tanzania kuwa imeshika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 kwa urahisi wa kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka sita mfululizo sasa Tanzania imeweza kushika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo ambavyo nitakwenda kuzitaja. Kwa mwaka 2015 Tanzania iliweza kushika nafasi ya 131 kati ya nchi 190; lakini kwa mwaka 2016 Tanzania imeweza kushika nafasi ya 139 kati ya nchi 190; kwa mwaka 2017 Tanzania ilifika nafasi ya 132 kati ya nchi 190; kwa mwaka 2018 Tanzania imeweza kushika nafasi ya 137 kati ya nchi 190; kwa mwaka 2019 imeshika nafasi ya 144 kati ya nchi 190 na kwa mwaka 2020 Tanzania imeweza kushika nafasi ya 141 kati ya nchi 190. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja nafasi hizo ambazo Tanzania imeshika lakini bado hatujafikia lengo la Tanzania kushika nafasi ya tarakimu mbili. maana yake lengo letu tulikuwa tushike walau kutoka 99 kushuka chini mpaka moja, lakini hatujaweza kufikia lengo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini hatujaweza kufikia lengo hili? Hii yote inatokana na mazingira magumu yaliyojitokeza ndani ya miaka mitano ya wafanyabiashara wetu kufanya biashara. Ndani ya miaka mitano wafanyabiashara wamefanyabiashara kabika mazingira magumu sana na mazingira hayo yamepelekea wengi kufunga biashara zao. Lakini hata wengine waliotamani kufungua biashara wameshindwa kufungua bisahara kutokana na masharti magumu yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hiyo imeathiri sana, ninaweza kuzungumzia hasa wa mikoa iliyoko mpakani. Mimi ninatokea Mkoa wa Songwe ambao uko mpakani mwa Tanzania na Zambia. Ukifika pale Tunduma ni mpakani, sasa hivi asilimia kubwa wamefunga maduka yao kutokana na changamoto kubwa ya biashara. Na hii yote inatokana na mlundikano mkubwa wa kodi ambao wafanyabiashara wengi wameshindwa kuumudu badala yake wamekimbia na kwenda kuwekeza kwenye nchi jirani ya Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukienda upande wa Zambia, asilimia 60 ya wafanyabiashara wakubwa walioko Zambia ni Watanzania. Ukienda jioni pale Nakonde, Black maduka makubwa yote yanamilikiwa na Watanzania na Watanzania wamekwenda kuwekeza kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sababu ya kufanya mabadiliko sana na siku zote nimeendelea kusema kinachopelekea yote hayo ni mlundikano mkubwa wa kodi, tuna sababu kubwa sana na siku zote tumeendelea kusema kufanya marekebisho ya kodi, ya Sheria za Kodi. Marekebisho hayo tukiyafanya wafanya biashara wetu wataweza kufanya biashara kwa uhuru. Sasa hivi tunapata faida gani kama Watanzania wanakwenda kuwekeza nchi jirani, lakini huduma zote wanakuja kuzipata Tanzania. Tukizungumzia barabara wanakuja kunufaika Tanzania, tukizungumzia maji, afya wanakuja kunufaika Tanzania, lakini wakati huo wamekwenda kuwekeza katika nchi jirani ambapo Tanzania hatupati faida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Zambia kule mfanyabiashara ataulipia mzigo wake wakati wa kuujumua. Atafanya biashara kwa uhuru hata bughudhiwa na jambo lolote, lakini ukija Tanzania mlundikano wa kodi unawakimbiza wafanyabiashara wetu. Siwezi kutaja kodi moja moja, lakini nitasema tu kwa ufupi. Ukija Tanzania mfanyabiashara ili afanye biashara yake kwanza jambo la kwanza atatakiwa kuisajili biashara yake, na kwenye suala zima la kuisajili biashara sio bure, kunatakiwa fedha. Akishaisajili anatakiwa kulipia kodi TRA, huyo huyo mfanyabiashara mmoja. Lakini baada ya hapo kuna kodi ya zuio anatakiwa kuilipia huyu huyu mfanyabiashara. Baada ya hapo ya kodi ya zuio, kuna kodi nyingine nyingi ambazo zingine ni kodi yaani anatoa kodi kadri anavyopata wateja anatakiwa kulipia kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna gharama za OSHA huyu huyu mfanyabiashara anatakiwa kulipia; kuna leseni za biashara kwenye Manispaa na Halmashauri zetu huyu mfanyabisahara anatakiwa kulipia; kuna Zimamoto kuna mambo mengi ya kodi mlundikano umekuwa ni mkubwa wa kodi na mlundikano huu unasababisha wafanyabiashara wetu wanashindwa kuwekeza kwenye Taifa letu na badala yake wanakwenda kuwekeza kwenye mataifa jirani. Ni dhahiri kwamba hata mataifa yetu jirani na yenyewe kwenye ushindani wa kibiashara. Kwa hiyo, yanatafuta kila njia kuhakikisha kwamba yanawashawishi Watanzania kwenda kuwekeza huko kwao, tuna sababu ya kufanya marekebisho ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kununua tv ya shilingi 500,000 ukimuomba mwenye duka akupunguzie anakuambia wazi kabisa bei yangu halisi ni shilingi 425,000, ukitaka nikuuzie 425,000 sitakupa receipt. Maana yake hapo kodi katika hiyo tv moja ya shilingi 500,000 ni shilingi 75,000.

Sasa Mtanzania yupi ambaye atakubali kutoa shilingi 500,000 asikubali kutoa shilingi 425,000 kwa hiyo watu wanakubali kununua vitu bila receipt ili kukwepa hiyo shilingi 75,000 kwasababu anajua itamsaidia katika masuala mengine. Na badala yake tumeendelea kuzikosa hizo kodi. Ni lazima tukubali kufanya marekebisho ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie wawekezaji, wawekezaji wanapokuja kuwekeza kwenye Taifa letu kumekuwa na mzunguko mkubwa sana na usumbufu mkubwa wao kupatiwa vibali vya uwekezaji na nafasi hiyo imepelekea wengine kukata tamaa, mwekezaji anafuatilia kibali mpaka miaka miwili, mitatu anaendelea kufuatilia kibali cha uwekezaji, mwisho wa siku anaamua kukata tamaa anakwenda kuwekeza kwenye mataifa mengine ambapo anaona kuna uwalau hakuna usumbufu. Lakini usumbufu huu umesababisha mianya ya rushwa, badala yake kumekuwa na mianya mikubwa ya rushwa mtu anajikuta mpaka anapatia hicho kibali lazima atoe rushwa. Sasa tunajitengenezea sisi wenyewe mianya ya rushwa kwa wawekezaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la viwanda. Katika suala zima la viwanda NSSSF waliamua sijui nizungumzieje hapa, yaani Mifuko ya Hifadhi ya Jamii waliamua kujiwekeza katika suala zima la ufufuaji wa viwanda. Na waliweza kutoa takribani shilingi bilioni 339 kwa ajili ya kufufua viwanda 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali ina mkakati gani ama imeweka malengo gani kuhakikisha fedha hizi zinarudi ili kutokuwatesa wastaafu wetu. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja atuambie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo mwisho ni suala la teknolojia. Ninaamini kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia maana yake kengele imeshapiga malizia sentensi yako.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, aaah, ni refu sana. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi niopate kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuzungumzia suala la ajira; wako wafanyakazi wengi ambao wanatoka nje ya nchi na wanakuja kuajiriwa katika nchi yetu ya Tanzania, lakini pamoja na kwamba wanaajiriwa, wanaajiriwa kwa kigezo cha kwamba ni wataalam, lakini pamoja na kuajriwa wamekuwa wakilipwa fedha nyingi sana ambazo fedha hizo wakati mwingine wamelipwa fedha dola za Kimarekani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo lakini bado katika nchi yetu tumekuwa na wataalamu ambao wakati mwingine wanazidi vigezo vya hao wageni ambao wamekuja kupata ajira katika nchi yetu, lakini wafanyakazi hao wengi wamekuja kwa namna ya kupitia makampuni mbalimbali ambayo yamekuwa yakipata tender katika nchi yetu, hususan katika masuala ya barabara, uchimbaji wa madini, katika masuala ya minara, na kadhalika. Wamekuwa wakipata tender hizo kupitia hao wataalam ambao wamekuwa wakija kupitia hizo kampuni ambazo zimekuwa zikija kupata tender katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote kumekuwa na changamoto kubwa na kumekuwa na utofauti mkubwa wa Watanzania wanapokwenda kuomba ajira ama kupata fursa nje ya nchi. Watanzania wengi wanapokuwa wakienda kupata fursa nje ya nchi za kupata ajira wamekuwa wakiambulia kupata mambo yasiyoridhisha kama vile kufanya usafi, kulinda, kufanya kazi za ndani, changamoto nyingi pia wamekuwa wakikumbana nazo ikiwa ni pamoja na kuteswa na kudhalilishwa wakati mwingine utu wao kwa sababu tu ni Watanzania.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo changamoto, naomba niiombe Serikali, ni wakati muafaka sasa Serikali kupitia balozi zetu kwenye nchi mbalimbali duniani kuhakikisha wanafanya njia mbalimbali kuhakikisha Watanzania wetu wanapata fursa stahiki wanapokuwa wamekwenda kuomba kazi huko nje ya nchi. Kinyume na hapo balozi zetu zisipofanya hivyo zitakuwa hazijatutendea haki kwa sababu sisi sote tunashuhudia namna ambavyo Watanzania wamekuwa wakati mwingine wakipitia mazingira magumu sana wanapokuwa huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tuombe Serikali sasa itumie fursa hii kupitia mabalozi wetu walioko nje ya nchi kuhakikisha wanazitafuta fursa maana yake pia ni sehemu ya wajibu wao, watafute fursa za ajira kwa ajili ya Watanzania wetu kwa sababu tumeona wakati mwingine hao wageni wanapokuja kupata ajira katika nchi zetu wamekuwa wakipewa ushirikiano wa kutosha na Serikali zao huko nje, jambo ambalo limesababisha wamefanya kazi kwa ufasaha na wamefanya kazi kwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kisawasawa. Ni wakati sasa na sisi tuombe balozi zetu zitusaidie huko nje kuhakikisha zinatafuta fursa stahiki kwa Watanzania ili waweze kupata ajira za kutosha huko nje na mwisho wa siku pia warudi kufanya maendeleo katika nchi yao.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote naomba nizungumzie suala la uwajibikaji wa mabalozi wanapokuwa huko nje. Ni wazi kabisa kwamba uwajibikaji wa mabalozi haujawa wazi. Uwajibikaji wa mabalozi wetu huko nje haujawa zai kabisa na tuseme wazi ili kuhakikisha kuwa mabalozi wetu wanakwenda kusimamia na kukuza diplomasia ya uchumi tunatakiwa tuweke mikakati, lakini pia tunatakiwa tufanye mabadiliko ya mfumo wa uwajibikaji wao, lakini mwisho wa siku mabalozi hawa waweze kuwajibika kwa hili Bunge. Wakiwajibika kwa hili Bunge ninaamini watafanya kazi kiufasaha na uwajibikaji wao utakuwa wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunahitaji hawa mabalozi wawe wanawasilisha mpango wao wa kazi kila mwaka. Wawasilishe mpango wao wa kazi kila mwaka katika Bunge hili kupitia Kamati ya Mambo ya Nje, wakifanya hivyo inaweza kusaidia wao kuwajibika ipasavyo wanapokuwa huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninaamini kwamba ikiwa taarifa zao za uwajibikaji zitaletwa katika hili Bunge, pia Bunge tupewe nafasi ya kutoa mapendekezo kwa nafasi zao za teuzi. Tunapoona wamepwaya katika suala zima la uwajibikaji Bunge tuna uwezo wa kutoa mapendekezo ni nini wafanye. Ninaamini tukifanya hivyo tunaweza tukasaidia uwajibikaji wa mabalozi wetu wanapokuwa huko nje.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Kuna Taarifa Mheshimiwa Stella Fiyao.

T A A R I F A

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Stella kwamba kwa mujibu wa utaratibu wa miongozo, taratibu, kanuni, sheria na miongozo mbalimbali zipo taratibu za kila makundi kuwa na sehemu ya uwajibikaji wake. Serikali itawajibika kwa utaratibu wake kwa maana ya watumishi wanajua jinsi ya kuwajibika, lakini vilevile tunayo Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Kamati hii imekuwa ikipata taarifa mbalimbali za uwajibikaji wa mabalozi, ikipata taarifa mbalimbali za masuala yote ambayo yanahusu Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa hiyo, haipo na wala haitakuja kutokea Bunge kuja kuanza kuwahoji mabalozi kuhusu uwajibikaji wao. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Stella Fiyao unapewa hiyo Taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza huo nilikuwa natoa ushauri wangu. Kwa ushauri una uwezo wa kupokelewa ama kutokupokelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini tukifanya hivyo hii itaondoa uzembe katika utendaji, pia itasababisha mabalozi kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao wanapokuwa nje ya nchi na itaondoa dhana iliyojengeka muda mrefu kwamba cheo cha ubalozi ni cheo cha starehe.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika mpango huu. Na kwa umuhimu mkubwa nitachangia katika sekta ya kilimo, hasa kwa kutambua umuhimu wake mkubwa katika kuongeza Pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua umuhimu mkubwa wa sekta hii katika kukuza uchumi wa Taifa letu, na hasa tunapozungumzia sekta ya kilimo, ni sekta ambayo imetanuka kwa upana wake. Leo hii tumeketi katika Bunge hili ni kwa sababu tumekula chakula vizuri na ndiyo maana tumekusanyika hapa, yote hii ni sekta ya kilimo tunaigusa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini umesimamia kikao vizuri hapo kwa sababu umekula chakula kizuri. Leo hii tunamuona Waziri wa Fedha amekaa pale kwa kutulia, ni kwa sababu amekula chakula vizuri; yote hii tunaigusa sekta ya kilimo. Hata mgonjwa anapokuwa hospitali, doctor anapompa dawa anasisitiza kwamba ale chakula kwa kutambua umuhimu wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunapozungumzia viwanda, ili viwanda viende sawasawa ni lazima kwanza mtu awe amepata chakula, ameshiba na ndiyo maana atafanya kazi katika viwanda. Kwa hiyo hii ni sekta muhimu sana katika Taifa letu na tunatakiwa tuichukulie kwa uzito wa hali ya juu sana kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tuamini kwamba hakuna uchumi unaoweza kukua katika Taifa lolote kama sekta ya kilimo itawekwa nyuma kwanza. Ni lazima tuitangulize sekta ya kilimo mbele ndipo tunaweza kufanikiwa katika mambo mengi ya kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema sekta ya kilimo ni muhimu sana; leo hii sekta ya kilimo inachangia kwa asilimia 26.7 katika kukuza uchumi wa Taifa letu, hivyo, tunapaswa kujua kwamba hii ni sekta muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu na la kusikitisha ni kuona kwamba sekta muhimu ya namna hii yenye kukuza uchumi wa Taifa letu inakua kwa asilimia 3 mpaka 4; hiki ni kitu cha kushangaza sana kwenye Taifa letu. Na ninashukuru jana Mheshimiwa Rais Samia alipokuwa akihutubia aliweza kuigusia sekta ya kilimo, kwamba ni sekta muhimu katika kukuza pato letu la ndani. Hata Mheshimiwa Rais anatambua umuhimu wa sekta hii katika kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninaona kwamba kwa namna sekta hii inavyokuwa kwa kusuasua inaonesha kwamba siyo kipaumbele katika Serikali yetu. Ninaweza nikazungumzia hali halisi, hasa kwa mikoa yetu ambayo kwa asilimia kubwa wanategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wananchi wa Mkoa wa Songwe wamekaa kusikiliza kauli ya Serikali inasema nini kuhusu pembejeo za kilimo maana hali ni mbaya sana ambayo inasababisha wananchi wengi na wakulima asilimia kubwa kukata tamaa kutokana na bei ya pembejeo za kilimo kuwa mara mbili ya ilivyokuwa awali. Na bei hizo zimesababisha wakulima wengi kushindwa kumudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu huu ukienda kwenye mikoa yetu ni mikoa ambayo wakulima wengi wanakuwa wameandaa mashamba lakini ni tofauti kabisa na miaka yote. Sasa hivi ukienda kila mkulima amekaa kwa hali ya kujisahau maana hana tumaini lingine. Watu wanawaza watapataje hizo pembejeo za kilimo kutokana na hali ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri tu Serikali, kama tunavyoweza kuweka kipaumbele katika miradi mingine, kama tunavyoweza kuhakikisha sekta ya ujenzi inakua kwa kasi, kama tunavyoweza kutumia nguvu kubwa kukuza sekta ya nishati, nguvu hiyo hiyo tuielekeze katika sekta ya kilimo ili kukomboa uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali siyo shwari kwa mikoa yetu. Sasa hivi hata tukienda huko kwenye mikoa yetu kuna hatari ya kupigwa mawe, maana mwananchi hana tumaini kabisa na hajui kesho yake itakuaje. Na kwa kujua kwamba mawazo huwa yanasababisha vidonda vya tumbo, ni hatari zaidi huko kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuugua vidonda vya tumbo maana hawana tumaini, wamejawa na msongo wa mawazo, kitu ambacho kinaweza kikawasababishia matatizo ya kiafya kwenye miili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali itumie njia ya dharura kutatua suala la pembejeo za kilimo kwenye mikoa yetu. Tuombe Serikali itoe ruzuku kwa dharura ili kupeleka katika pembejeo za kilimo na wananchi wetu waweze kupata pembejeo za kilimo kwa bei ndogo ambayo kila mkulima ataweza kumudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikuwa tunanunua mbolea kwa shilingi 65,000 lakini bado kilikuwa ni kilio kwa wananchi. Leo ukienda Mkoa wa Songwe, mfuko wa mbolea unaupata kwa shilingi 120,000, jambo ambalo hakuna mkulima anayeweza kumudu gharama hizi. Lakini wakati huohuo ukienda sokoni mkulima anauza gunia la mahindi kwa shilingi 30,000 na kwa kanuni, ili ulime eka moja na uweze kuvuna mahindi ya kutosha ni lazima uwe na mifuko sita ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mkulima gani ambaye anaweza kumudu shilingi 720,000 kwa ekari moja tu; mkulima yupi wa namna hiyo? Hiki kitu hakiwezekani, hebu tuombe Serikali jambo hili mlichukue kwa udharura. Kwa wakati mwingine tunasema mioyo yetu inavuja damu maana tunajua hali za wakulima wetu huko mikoani hali ni mbaya mno. Na kuna wakati sisi kama Taifa tunapaswa kujifunza hata kwa nchi jirani ambazo zimetuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda Zambia na Malawi bei za mbolea ziko chini kuliko Tanzania, lakini Malawi na Zambia wanajumua mizigo yao huko nje ambako ndiko na Watanzania tunakojumua na wanapitia katika Bandari ya Tanzania kwenda kwenye nchi zao lakini bei zao zipo chini. Hii inaonesha kwamba mrundikano wa kodi kwenye nchi yetu unawatesa na kuwaumiza wakulima wetu. Tuombe tuwanusuru wakulima wetu, lakini tunusuru uchumi wa Taifa letu; tuweke ruzuku katika pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninaomba kuishauri Serikali kama wengine walivyosema kwamba fedha zilitolewa zaidi ya bilioni mia moja ishirini na kwa ajili ya kununua mazao. Nataka kusema jambo hili kwa uchungu kabisa. Fedha hizi kwa asilimia kubwa hazijamgusa mkulima wa chini maana fedha hizi kwanza zimefika kwa kuchelewa lakini badala yake zimewagusa wafanyabiashara badala ya wakulima. Wakulima bado wana maumivu, bado wana kilio pamoja na Serikali kutoa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe kwa wakati mwingine fedha zitolewe kwa wakati ili ziweze kumlenga mkulima mdogo ambaye ndiye anayehangaika kule chini na anasota, fedha zitolewe kwa wakati. Na ninaamini tukifanya hivi tunaweza kumkomboa mkulima wa chini ambaye anataka kukwamuka kutoka hatua ya kwanza kwenda ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika mpango huu na hasa katika mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea mbele sana, kuna wakati ni vyema tukaenda sawa na Watanzania na tukatoa ufafanuzi mzuri ili Watanzania wakatuelewa, hasa tunaposema uchumi wa Tanzania umekua, tuwe tunawafafanulia wananchi, huo uchumi umekua kwa namna gani? Kwa sababu uhalisia wa kile tunachokisema na ukienda kwa hali za Watanzania huko uraiani, ni mbaya kila kunapoitwa leo, zinazidi kuwa mbaya. Kwa hiyo, Watanzania hawaelewi wanaposikia uchumi umekua, wanajiuliza huo uchumi unakua kwa namna gani? Kwenye makaratasi au mifukoni kwao? Kwa hiyo, kuna wakati tuwe tunawafafanulia Watanzania ili wawe wanaelewa maana halisi ya uchumi kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda huko uraiani, sasa hivi hata Mtanzania aliyekuwa ana uwezo wa kula milo mitatu, sasa hivi hata kula mlo mmoja ni shida. Hali ni mbaya, biashara haziendi, hali siyo nzuri kiukweli. Kama Taifa, lazima tufike mahali tuwafafanulie Watanzania huo uchumi tunaosema umekua, ni kwa namna gani, ili tuwe tunaenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la nishati, hasa katika mpango huu. Katika mpango huu nataka kujua Mpango hasa wa Taifa ni upi katika suala zima la kukabiliana na changamoto kubwa ya umeme ambayo ipo huko mikoani kwetu? Naweza nikasema hata wa Mikoa kama Dodoma na maeneo mengine wanaweza wasinielewe, lakini uhalisia sisi tunaujua wananchi wa Mikoa ya Mbeya na Songwe, hali ya nishati ya umeme ni mbaya sana na kwa wakati mwingine unaua mpaka uchumi wa Wana-Songwe. Sasa katika kufuatilia mpango sijaona kabisa kwamba Wizara ina mkakati gani wa kukabiliana na changamoto kubwa hii ya umeme ambayo imekuwa ni shida kwa wananchi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mpango, ni vyema tukaja na mikakati, lakini ukisoma katika ule ukurasa wa 122 kipengele (f), utaona wanasema, “kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali, kujenga na kukarabati miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme. Hizi ni sababu za kawaida ambazo hata mtoto mdogo huko Songwe anazijua. Sisi Wanasongwe tunataka mkakati, kwa sababu kiukweli umeme umechangia kuzorotesha uchumi wa Wanasongwe isivyokuwa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Songwe tulianza mgao kabla ya mgao. Suala la kukatika umeme Songwe ni hali ya kawaida mpaka masaa 24 umeme hakuna. Uchumi wa Wanasongwe unakufa. Wananchi wadogo wadogo ambao wamejiwekeza wanashindwa kuendeleza maisha yao kwa sababu tu yakukosa umeme. Hivi tunawaweka kwenye kundi gani hawa wananchi wa Mkoa wa Songwe? Tunaua uchumi wa Wanasongwe. Hasa ukizingatia tunavyozungumzia Mkoa wa Songwe, ule Mkoa ni langu kuu la SADC; Mataifa mengi yanaingia kwa kupitia Mkoa wa Songwe hasa Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria unaenda katika lango la SADC masaa 24 Mji ni giza. Hebu fikiria! Tunaposema Tunduma ama Songwe ni lango, tunamaanisha. Mwananchi yeyote au mgeni yeyote anapoingia kupitia mpaka wa Tunduma, anapofika Tunduma, tafsiri yake ile, ndiyo anaiona sura halisi ya Tanzania. Sasa kama sura halisi ya Tanzania ina uwezo wa kukaa giza masaa 24, tunaeneza picha gani kwa wageni ambao wanaingia katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haikai sawa. Kuna wakati najiuliza, hivi Serikali inapotuambia kwamba ina uwezo wakuzalisha umeme na kuuza nchi nyingine, inamaanisha nini? Au tunawadanganya Watanzania! Kwa sababu huwezi kuzalisha umeme ambao una uwezo wa kwenda kuuza kwenye Mataifa mengine ikiwa watoto wako ndani tu umeme hauwatoshi. Hii tunamaanisha nini? Tuache kuwadanganya Watanzania. Tuongelee uhalisia, tatizo ni nini ambalo linapelekea umeme kukosekana kila kunapoitwa leo? Vingine tujiulize, kwamba Dodoma na Songwe imekuwaje? Hii si ni Tanzania moja! Mbeya na Dodoma si ni Tanzania moja! Sasa inakuwaje? Kwamba tumewaweka wananchi kwenye mataba! (Makofi)

Mheshimniwa Mwenyekiti, ukienda leo Mkoa wa Songwe kilio kikubwa cha wananchi ni umeme. Hawana amani, wananchi wanashindwa kuzalisha, wanashindwa kuendeleza biashara zao, wanashindwa kuendeleza viwanda kwa sababu ya umeme. Kwenye mpango huu nilitarajia Wizara, ituambie...

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji, kwamba huu mgao wa umeme ni nchi nzima, hata Nyang’hwale huwa tunakosa. Asiseme kwamba kuna ubaguzi na matabaka. Umeme mgao upo kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa taarifa, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella, taarifa hiyo.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taarifa ninaipokea kwa mikono miwili. Shida wanayokutana nayo wananchi wa huko Nyang’hwale, ndiyo wanayokutana nayo wananchi wa Mkoa wa Songwe kwenye lango kuu la SADC, ni ajabu. Tufike mahali tuambiane ukweli hapa. Wananchi huko hawatuelewi. Tuambieni kwa nini mnatuletea taarifa tofauti, kama tuna uwezo wa kuzalisha umeme wa kuuza nje ya nchi, kwanini ndani usitutoshe? Hii ina maana gani? Ina maana gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali za wananchi wetu ni mbaya, mbaya sana, tunaua uchumi wa Wanasongwe. Hatuwezi kuvumilia kuona hiki kitu kinaeandelea, lakini wakati huo kwenye mpango hatuoni ukija na mikakati madhubuti ya kukabiliana na hili tatizo la umeme. Ili tuende sawa, ni vyema Wizara ya Fedha ikatuletea mpango madhubuti wa wa kukabiliana na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia viwanda. Hivi kiwanda kipi kinaweza kuendeshwa bila umeme? Kipi hicho kiwanda? Kiwanda kipi? Labda kama tutatumia generator na solar tuambiane hapa, lakini kama tunategemea huu umeme; ndiyo maana kuna wakati wananchi wanahoji kwamba hata hiyo reli ya SGR, hivi itategemea huu huu umeme uu kuna umeme mwingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali tuambiane ukweli, na tuombe Wizara ya Fedha ije na mpango madhubuti ni namna gani imejipanga kukabiliana na changamoto kubwa ya umeme ndani ya Taifa letu? Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa ajili ya usalama wa Taifa letu. Nasema Wizara hii ni muhimu kwa sababu kwanza ndiyo Wizara pekee ambayo inahakikisha usalama wa raia na mali zao, lakini ndiyo wizara pekee ambayo inahakikisha usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza baadhi ya watendaji wa Jeshi la Polisi ambao wanajitahidi kufanya kazi kwa uaminifu na kutekeleza majukumu yao kisheria; japokuwa wana mishahara midogo sana ambayo haitoshelezi, lakini pamoja na hayo wamekubali kufanya kazi kwa uaminifu kwa kulitumikia Taifa letu. Niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo kuna baadhi ya watendaji ndani ya Jeshi la Polisi ambao hawafanyi kazi kwa uaminifu na badala yake wamekubali kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kwa kutekeleza tu matakwa yao. Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo polisi haoni aibu kwenda kumkata mwananchi eti kwa sababu tu ametangaza kiasi cha rambirambi kilichopatikana msibani. Hili ni jambo la ajabu sana.

Mheshimiwa Spika, tuna baadhi ya polisi ambaye mpaka anakwenda kumkamata raia nyumbani kwake hamwambii ana mkamata kwa kosa gani? Anamchukua anamfikisha kituoni hamwambii amemkamata kwa kosa gani, anakaa naye siku ya kwanza, siku ya pili, siku ya tatu, mwananchi anauliza umenikamata kwa kosa gani? Anamwambia kosa utalikuta mahakamani, hili ni jambo la ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwingine akibananishwa sana kwamba aambiwe umenikamata kwa kosa gani? Anachukua simu anapiga anasema huyu niliyemkamata nimpe kosa gani? Hili ni jambo la ajabu sana! Hii inaonesha tuna baadhi ya Askari Polisi ambao hawatambui majukumu yao na ni hatari sana kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine; katika maeneo yetu na ndani ya Taifa letu kuna baadhi ya uhalifu ambao unaendelea, lakini kuna biashara nyingi ambazo zinafanyika zisizokuwa halali. Wananchi siyo kwamba hawajui, wanajua isipokuwa kuna wakati wanaogopa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa sababu ya kuhofia usalama wao. Mwananchi anakwenda kutoa taarifa polisi kuonesha kwamba kwenye eneo fulani kuna mhalifu fulani aidha anafanya biashara haramu au anafanya biashara zisizokuwa sahihi, lakini baada ya yule mtuhumiwa kukamatwa jioni anaachiwa na ana ambiwa kabisa unajua aliyekuchongea ni nani? Ni mtu fulani. Mwisho wa siku wananchi wanashindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa sababu ya kuhofia usalama wao, kwa sababu mwisho wa siku yule mtu anapoachiwa anakwenda ku-deal na yule mtoa taarifa. Hii siyo haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka mtoa taarifa alindwe. Matokeo yake, mwisho wa siku tumeendelea kufuga wahalifu ndani ya Taifa letu kwa sababu tu ya kushindwa kuwalinda watoa taarifa; hili ni jambo la hatari sana kwa Taifa letu. Tunapaswa kuwa na askari ambao wanakuwa ni waaminifu ili tulijenge Taifa lililo salama zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia katika suala zima la magereza. Magereza za ndani ya Taifa letu zimekuwa na hali mbaya, mbaya, mbaya sana. Nasema hali mbaya sana kwa sababu hata mimi kuna baadhi ya magereza nimekaa. Magereza zetu zina hali mbaya isiyokuwa kawaida, miundombinu ni mibovu, hairidhishi kabisa yaani hata kwamba mtu analala humo ndani ukioneshwa cell ambayo watu wanalala wakati mwingine ni hatari kabisa hata kwa afya za wananchi wetu. Hali ni mbaya, lakini ukifuatilia katika Ripoti ya CAG iliyotolewa Machi, 2022, imeonesha wazi kabisa baadhi ya magereza ambazo zina mrundikano mkubwa wa wafungwa na mahabusu.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni katika Gereza la Keko, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG inaonesha wazi kabisa gereza lile lina uwezo wa kupokea mahabusu na wafungwa 340, lakini badala yake lilikutwa likiwa na wafungwa na mahabusu 999; ni zaidi ya asilimia 194, jambo ambalo ni hatari sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ukienda katika Gereza la Kingurungwa huko Lindi, kwa mujibu wa Ripoti ya CAG inaonesha wazi kabisa gereza lile lina uwezo wa kutunza mahabusu na wafungwa 39 lakini badala yake lilikutwa likiwa na wafungwa na mahabusu 88 zaidi ya asilimia 126. Hii ni hatari.

Mheshimiwa Spika, ukienda katika gereza la Kiomboi lililoko Mkoani Singida, Ripoti ya CAG inaonesha wazi kabisa kwamba gereza hili lilikuwa na uwezo wa kutunza wafungwa na mahabusu 58 lakini badala yake lilikutwa lina wafungwa na mahabusu 132 zaidi ya asilimia 128, hii ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, badala yake wafungwa na mahabusu wamekuwa wakiambukizana magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, magonjwa ya vifua, upele na mambo mengine ambayo ni hatari kwa afya zao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. STELLA S. FIYAO: Kengele ya kwanza.

SPIKA: Kengele ni moja tu, sekunde 30 malizia.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali, kuna umuhimu mkubwa wa kuziondoa kesi ambazo upelelezi wake umechukua muda mrefu kukamilika, ikiwa ni pamoja na kesi za kisiasa ambazo wameendelea kuwashikilia watu kutoka Uchaguzi Mkuu, 2020 mpaka leo watu wanaendelea kushikiliwa katika kuta za gereza. Kuna haja ya kuziondoa kesi hizi ili kupunguza msongamano wa watu huko magerezani.

SPIKA: Haya. Ahsante sana.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Nitaanza kwanza kwa kuugusa Mkoa wa Songwe kwa sababu Mkoa wa Songwe tuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. Mkoa wetu una kata zaidi ya 90 lakini hakuna kata yenye uhakika wa kupata maji safi na salama. Changamoto hii imepelekea baadhi ya maeneo kujikuta wana-share maji pamoja na mifugo; hasa ukienda katika Wilaya za Ileje, Momba na maeneo mengine changamoto kubwa ya maji wananchi wamejikuta wana-share maji pamoja na mifugo jambo ambalo ni hatari sana kwa afya za wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nitazungumzia sana changamoto kubwa pia iliyopo katika Jimbo la Tunduma iliyo ya muda mrefu. Changamoto ya maji imekuwa ni kubwa sana ndani ya Jimbo la Tunduma na changamoto hii imepelekea wananchi watumie muda mwingi sana kwenda kuyatafuta maji, badala ya kufanya masuala mengine yanayohusiana na maendeleo ya Taifa letu. Lakini pia ndani ya mji wa Tunduma kuna mradi mkubwa wa maji ambao ulikuwa umeshafanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2013 na Kampuni ya Networkers ya Marekani.

Mheshimiwa Spika, upembuzi huu ulifanyika kutoka Mto Songwe Ileje na kuja kuyaleta maji katika Jimbo la Tunduma, jambo ambalo mpaka leo halijatekelezeka na bado wananchi wa Tunduma wana kilio kikubwa cha changamoto ya maji.

Mheshimiwa Spika, nitaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja hapo atuambie ni lini mradi huu utaanza kutekelezeka ili wananchi wa Mji wa Tunduma waepukane na changamoto ambayo wamekuwa wakiipata kwa muda mrefu zaidi?

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna mradi mwingine wa maji kutoka katika Wilaya ya Mbozi. Mradi huu unatoka katika Kijiji cha Ukwile na ulikuwa ukiwahudumia wananchi wa Kata ya Mpemba na Kata ya Katete. Mradi huu kutokana na ubovu na uchakavu wa ile miundombinu, kwasababu miundombinu iliyopo kwenye ule mradi ni ya mwaka 1971, hivyo miundombinu hiyo imechakaa sana, na kupelekea wananchi kushindwa kupata maji. Lakini nitaomba pia Waziri atakapokuwa anakuja atuambie ni lini watafanya mabadiliko wa ile miundombinu ili wananchi wa Kata ya Mpemba na wananchi wa Kata ya Katete waweze kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama kutoka katika mto Ukwile. hii inaweza ikatusaidia sana kutokana na changamoto kubwa ambayo inawakuta wananchi wa mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lakini changamoto nyingine kubwa ni kwa wananchi kusomewa bills zisizo sahihi. Hiki ni kilio cha maeneo mengi sana ndani ya Mji wa Tunduma na ndani ya Mkoa wa Songwe kwa ujumla. Changamoto hii imekuwa ikiwakabili wananchi wanapewa bills kubwa ambazo ni tofauti na uhalisia wa maji ambayo wanakuwa wameyatumia kwa wakati huo; jambo ambalo limekuwa likiwaumiza sana wananchi wetu,

Mheshimiwa Spika, ningeomba kuishauri Wizara. Wana sababu ya kuhakikisha kila mwananchi wanae mhudumia kwenye suala zima la maji wafunge mita ili waweze kupata uhalisia wa gharama ambazo wanakuwa wanawatoza wananchi wetu. Kwasababu hatimaye wananchi wetu wamebaki wakiumia, wanatoa kodi kubwa tofauti kabisa na ule uhalisia wa matumizi yao yam aji. Tunaomba hili lizingatiwe kwasababu linawaumiza sana wananchi wetu (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala zima la upotevu wa maji. Katika ripoti ya CAG ya Machi, 2022 inaonesha kabisa kwamba kuna tatizo kubwa ambalo linaikabili Wizara la upotevu wa maji; changamoto ambayo imesababisha Wizara kupata hasara kubwa. Ukisoma katika ripoti ya CAG inaonesha kwamba kwa mwaka 2020/2021 upotevu wa maji uliigharimu mamlaka kiasi cha Shilingi bilioni 175. Hii ni gharama kubwa sana ambayo pengine ingeweza kutusaidi hata kuendeleza miradi katika maeneo mengine ambako haiwezekani kabisa, kumekwama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo hii nazungumzia mradi wa kutoka Ileje kwenda Tunduma pengine kusingekuwa na hizi changamoto fedha hizi zingeweza kutusaidia hata sisi wananchi wa mji wa Tunduma kuweza kutatua changamoto ya maji. Kwasababu ukirudi kule Tunduma huu mradi ninaouzungumzia unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni tatu tu. Sasa kama tunaweza kupoteza fedha Shilingi bilioni 175 Shilingi bilioni tatu inawezaje kutushinda. Hili tunaomba Wizara pia ilizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini changamoto kubwa ninayoiona, Wizara ina sababu ya kuongeza watumishi katika eneo la maji ili waweze kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo ambayo wanawahudumia wateja. Kwasababu sababu wanazozitoa hapa zilizosababisha kupata hasara hii kubwa ni kama vile wateja kujiunganishia maji kinyume na utaratibu. Jambo hilo limepelekea Wizara kupata hasara kubwa sana. Jambo la pili ambalo wanalisema ni kuvuja kwa mabomba.

Mheshimiwa Spika, sasa, Wizara ikipata watumishi wengi katika maeneo ambayo wanawahudumia wateja hizi changamoto zinaweza kupungua na hatimaye hatuwezi kuwa na idadi kubwa ya upotevu wa maji kiasi ambacho tunapata hasara kubwa. Tuombe hili lizingatiwe. Wizara ione umuhimu wa kuongeza watumishi katika sekta ya maji ili waweze kufanya ziara na kutembelea yale maeneo ambayo wanatoa huduma kwa wateja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Niungane na wenzangu waliotangulia, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua siku ya jana katika mikopo ya asilimia 10 ya kuhakikisha wanabadili utaratibu, namna ya utoaji wa hiyo mikopo. Ukweli ni kwamba sasa Mfuko huu ulikuwa unakwenda kufa, kwa nini ulikuwa unakwenda kufa? Ni kutokana na utaratibu ambao ulikuwa unatumika katika suala zima la utoaji wa mikopo. Jambo la pili, mikopo hii ilikuwa haiwafikii walengwa na badala yake ilikuwa inawanufaisha watu chache kwa ajili ya maslahi yao binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ukweli sisi sote tunajua utaratibu wa mikopo hii inavyotolewa kwenye halmashauri zetu, lakini ukisoma Ripoti ya CAG ya mwaka huu 2022/2023, ni masikitiko makubwa sana kuona kwamba bilioni 88 zimepotea na hazijulikani ziliko na hata vikundu vilivyopewa mikopo hii ya bilioni 88 havijulikani vilipo. Hili ni jambo la aibu kwa watu waliopewa dhamana ya kusimamia mikopo hii ili iweze kuwafikia welangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kauli ya Serikali naomba nishauri mambo machache: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza tunaomba waliohusika katika suala zima la utoaji wa mikopo hiyo ambayo haijulikani ilipo wachukuliwe hatua ili liwe fundisho huko mbele tuendako, mambo yako wazi kabisa. Ukisoma katika Ripoti ya CAG, ukienda katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, vikundi 34 vimepewa mikopo zaidi ya milioni 600 na pointi lakini vikundi hivyo havijulikani, havijulikani kwa maendeleo hawavijui kabisa. Hili ni jambo la ajabu, kikundi ili kipewe mkopo kwanza jambo la kwanza ni lazima Afisa Maendeleo wa eneo husika akajiridhishe kwamba kikundi kipo na kina mradi kinaouendesha ndipo kikundi kinapata sifa ya kukopa mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunaliona kwenye halmashauri zetu, ili kikundi kipewe mkopo ni lazima kiwe na mdhamini mwenye mali zisizohamishika. Kikundi hiki ndipo kinapewa mkopo, sasa hivi vikundi vilipewaje mkopo wakati Maafisa Maendeleo wa maeneo husika hawavijui na wala hawavitambui kwenye maeneo yao. Utaona hiki ni kitu cha ajabu sana. Tuna watu wachache ambao wanakwamisha juhudi za Serikali, hawa wanatakiwa kuchukuliwa hatua ili huko mbele tuendako hayo mambo yasijirudie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nizungumzie kwenye Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Sisi sote tutakuwa ni mashahidi na hata Waziri inawezekana anajua, ndani ya miezi sita wananchi wa Mji wa Tunduma wamekuwa wakikutana na adha kubwa ya stendi na hili liko wazi na hili limekuwa ni janga ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Stendi ilikojengwa hatukatai kujengwa stendi ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma na hilo ni hitaji la kila mmoja kuona maendeleo yanafanyika kwenye eneo lake na hili jambo sisi Wabunge tunashukuru, lakini changamoto ambayo wananchi wamekuwa wakikutana nayo ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tunduma wamekuwa wakikutana na adha na mateso makubwa sana ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Stendi iko ndani ya Kata ya Mpemba, Kata ya Mpemba ni Kata ambayo iko mwanzoni unapoingia ndani ya Mji wa Tunduma, Kata ya Mpemba imepakana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi lakini kushoto imepakana na Halmashauri ya Wilaya ya Ileje. Kutoka katika Kata ya Mpemba kwenda kufika ndani ya Mji wa Tunduma Mjini ni kilomita 12, mwananchi anatoka Wilaya ya Mbeya amepanda gari analipia nauli Sh.4,000, lakini akishashushwa ndani ya Stendi ya Mpemba kutoka pale kuja kufika Mjini anatumia zaidi ya nauli aliyotumia kutoka Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi wananchi wamekuwa wakikutana na changamoto kwa sababu jambo la kwanza daladala hazitoshelezi za kuwatoa katika eneo la Mpemba kwenda kuwafikisha Tunduma Mjini hazitoshi. Jambo la pili, wananchi mpaka wamekuwa wakifikia hatua ya kuibiwa, wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi wengine wametembea kwa mguu umbali mrefu kiasi kwamba wamekutana na changamoto mbalimbali ambazo zinahatarisha usalama wa maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, alichukue hili aende akapitie Halmashauri ya Mji wa Tunduma aone namna wananchi wanavyokutana na changamoto kubwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma na najua kwa nafasi yake ana uwezo wa kushauri kwa sababu kama Baraza tumeshauri lakini mawazo yetu kama Baraza hayajafanyiwa kazi. Badala yake watu wachache ambao wanaona jambo hili linaweza kufaa ama kwa maslahi yao, wanalichukua jambo hili kana kwamba sasa imekuwa ni siasa, lakini siasa hii inawaumiza wananchi wa Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivi tusisubiri wananchi wa Mji wa Tunduma waje waandamane kwa sababu tumeona migomo ya waendesha daladala imefanyika, migomo ya waendesha mabasi yaendayo mikoani imefanyika. Sasa tusisubiri migomo ya wananchi wa kawaida ndipo tuje Mji wa Tunduma kwa ajili ya kutatua changamoto hii. Niombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni eneo lake alichukue jambo hili, aone ni namna gani anaweza kutusaidia kukabiliana na changamoto hii ambayo imekuwa ni mateso na changamoto kubwa kwa wananchi wa Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, jambo la tatu naomba nizungumzie suala zima la elimu. Sisi sote tunajua na wananchi wetu wanajua kwamba elimu ya sasa ni elimu bila ada, lakini changamoto ambayo wananchi wamekuwa wakiikuta ni afadhali ya ada. Tuseme ukweli kabisa, changamoto ambayo wananchi wamekuwa wakikutana nayo ni afadhali ya kulipa ada, lakini si changamoto hii ambayo wananchi wanakutana nayo sasa, ni afadhali Serikali ikawa wazi na ikasema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hela hizi ambazo zinatolewa kwa ajili ya kusapoti elimu ya bila ada hazipelekwi ipasavyo mashuleni. Badala yake Walimu na wanafunzi wamekuwa wakikutana na mazingira magumu sana huko mashuleni kwa sababu bajeti yao haitekelezwi ipasavyo na badala yake ile bajeti inapelekwa kidogo jambo ambalo linashindwa kukidhi mahitaji ya wanafunzi na Walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la vitabu vya kufundisha na kufundishia. Ukisoma katika Ripoti ya CAG iliyotolewa Februari, mwaka huu 2023 inasema wazi kabisa, kulikuwa na bajeti ambayo ilikuwa imetengwa katika Mradi wa Fungu 4393. Mradi huu ulikuwa umetengewa kiasi cha bilioni 22.850 kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya wanafunzi milioni 2.25, lakini badala yake mpaka kufikia Februari mwaka huu 2023 hakuna hata shilingi mia ambayo imetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya wanafunzi, ni nini tunafanya kwa wanafunzi wetu? Tumewaweka Walimu katika mazingira magumu, lakini tumewaweka wanafunzi katika mazingira magumu ya kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenda miundombinu na madawati hali ni mbaya, mtoto anakalia jiwe kutoka darasa la kwanza mpaka darasa la saba halafu mnategemea akiwa Dokta akutibu vizuri?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. STELLA S. FIYAO: …Haiwezekani! Hatuwezi kufika kwa utaratibu wa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara ya Maji. Hii ni Wizara muhimu sana kama walivyotangulia kusema, uhai wa Taifa letu unategemea Wizara hii pia ya Maji kwa sababu ni muhimu katika kila sekta. Tukisema Ujenzi unagusa maji, tukisema nini kila kitu kinagusa maji, tukisema usafi, afya kila kitu kinagusa maji. Kwa hiyo ni Wizara muhimu sana kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara kwa namna ambavyo bajeti yake inatekelezeka. Tukiangalia katika suala zima la bajeti ya miradi ya maendeleo katika fedha zilizokuwa zimetengwa shilingi bilioni 657.899 fedha zilizotoka kufikia Aprili 2023 zilikuwa ni shilingi bilioni mia sita ishirini na tatu na milioni saba Hamsini na tatu na point. Kiukweli hii inatia moyo hata Wabunge tunapokaa hapa kupitisha bajeti kiuhalisia inatia moyo mpaka kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutia moyo huku bado kuna changamoto kubwa kwenye suala zima la usimamizi na ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa, hili ni tatizo kubwa sana kwenye maeneo yetu. Bajeti inapita huku inatekelezeka lakini ukienda kwenye suala la usimamizi na ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa kumekuwa kunasuasua sana. Hii imepelekea miradi mingi kutokamilika kwa wakati na wakati mwingine kutokwenda kwenye lengo sawa sawa na vile inavyokuwa imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Mji wa Tunduma pale sasa hivi utakuta kuna ma-tank ambayo yamepakwa rangi za kila aina, lakini hakuna maji. Utaona kuna miundombinu kila maeneo, ukifika utasema Mji wa Tunduma una maji, lakini ukienda kwenye uhalisia, wananchi wa Mji wa Tunduma asilimia kubwa hawapati maji safi na salama. Hii ni hatari sana. Wananchi wetu wanataka wanapoona yale ma- tank, wanavyoona miundombinu ya maji imetembea kila mahali, kitu kikubwa wanachokitaka siyo yale matenki, siyo mabomba yaliyopitishwa kila maeneo, wanachotaka ni uhalisia wa maji. Sasa tunataka tuone maji, tusione tu yale matenki ambayo yanabadilishwa rangi. Tunataka tuone uhalisia wa maji kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia kama walivyosema Wabunge wengine wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Waziri kuna hatari ya sisi Mkoa wa Songwe kukimbia na Shilingi yako. Kiukweli. Kwa sababu uhalisia hakuna kata hata moja ndani ya Mkoa wa Songwe ambayo ina uhakika wa kupata maji safi na salama kwa uhakika, hakuna. Katika taarifa yako unasema kwamba hali ya upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 77, lakini ukienda Wilaya ya Momba, ukienda Halmashauri ya Mji wa Momba kuna vijiji 72. Kati ya vijiji 72, vijiji 28 tu ndiyo vyenye uhakika wa kupata maji. Kwa hiyo, napata shaka na hii asilimia 77, ni wapi? Ni wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata shida. Karne hii ya leo watu wana-share maji na mifugo. Ukienda Momba…

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wana-share maji na mifugo, ni kitu cha hatari sana.

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwongezee taarifa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wetu wa Songwe, kwamba katika Jimbo la Momba kati ya vijiji 72, ni vijiji 22 tu ndiyo vinapata maji safi na salama ya kwenye bomba. Vijiji 50 havina maji. Kwa upatikanaji wa Jimbo la Momba ni sawasawa na asilimia 30 tu, lakini vijiji vilivyobaki 50 tunakunywa maji na nguruwe, punda, mbuzi na ng’ombe. Vijiji 50, na jambo hili linaendelea kushamiri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Fiyao unaipokea taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza taarifa naipokea kwa mikono miwili kwa sababu huo ndiyo uhalisia wa Jimbo la Momba. Ni hatari! Kwa karne hii, leo wananchi wana-share maji na mifugo! Ni jambo la hatari. Ndiyo maana typhoid kwenye Mkoa wa Songwe haziishi, maana ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atakapokuja hapa, atuambie mkakati wake katika Mkoa wa Songwe ni upi, kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunataka tujue, tumeendelea kusema hapa, kila inapofika Wizara ya Maji tunachangia na tunasema. Mmeendelea kutuahidi kipindi kirefu kwamba maji yatatoka kwenye Mto Songwe huko Ileje, yatakuja Tunduma, yataenda Vwawa, yataenda Mbozi, leo hii mmetubadilishia mpango, mnasema maji yanakwenda kutoka Momba. Tunataka mtuambie, kwa sababu tangu mwaka 2019 mlisema tayari mmeshafuatilia na mmejua gharama za mradi, mradi utagharimu kiasi gani. Leo hii mmetubalishia mpango, mnasema maji yanakwenda kutoka Momba, yanaenda Tunduma, yanaenda Vwawa, yanaenda Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waziri atakapokuwa anakuja hapa atuambie, ni lini mradi huo utatekelezeka? Ni lini mradi huo utatekelezwa? Kwa sababu tumechoka kuimba humu, tumechoka kusema, tumechoka kuzungumza. Tuambieni ni lini mradi huo mkubwa utatekelezeka kwa ajili ya kukomesha tatizo la maji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Mbozi na Vwawa? Lini mradi utatekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, bado tumeendelea kuimba, kuna mradi ambao unahudumia Kata ya Mpemba na Kata ya Katete. Mradi huu unatoka Ukwire Wilaya ya Mbozi kuja Halmashauri ya Mji wa Tunduma na unahudumia Kata hizo mbili, miundombinu yake ni mibovu. Miundombinu ilitengenezwa tangu mwaka 1971, mpaka leo kuna tatizo kubwa. Mradi huu ulikuwa unawakomboa sana wananchi wa Kata ya Mpemba na Kata ya Katete. Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unakuja hapa, utuambie ni lini mtafanya ukarabati mkubwa kwenye mradi huo ili wananchi wa Kata ya Mpemba na Kata ya Katete waweze kunufaika na maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, sisi watu wa Songwe tuangaliwe kwa jicho lingine. Tunachangia asilimia kubwa sana kwenye pato la Taifa, hebu tuangalieni kwenye suala la maji, tuondoleeni hizi changamoto. Ninaamini changamoto hizi zinatibika kama Mheshimiwa Waziri utaamua. Tusaidie wananchi wa Mkoa wa Songwe tuepushieni changamoto kubwa ya maji ambayo inaleta athari mpaka kwenye ndoa. Tusaidieni! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kuishukuru Wizara kwa sababu nimepitia na nimeona asilimia kubwa naona Mkoa wa Songwe kwa sehemu tumeguswa kwenye bajeti hii. Kwa hiyo niwapongeze kwa kweli na sisi Wanasongwe tunaona bajeti hii imetugusa kwa sehemu, kwa sababu ukiona kutoka Barabara ya Mbarizi mpaka Mkwajuni tumetengewa kilometa 86, siyo kidogo; japo bado lakini naamini wataendelea kutufikiria zaidi na zaidi.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye Barabara ya Mlowo mpaka Kamsamba kilometa 50 wametutengea. Ukiangalia Barabara ya Mpemba mpaka Ileje, kilometa 50 na maeneo mengine wametugusa. Niombe tu kwamba bajeti hii tunaomba iwe inatekelezeka na itekelezeke kweli kwa sababu Wanasongwe tumetegemea hasa kwa sababu asilimia kubwa barabara hizi ni barabara za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo bado tuna changamoto kwenye maeneo mengine kwenye barabara hasa ukizingatia Barabara ya kutoka Mlowo inayopita Isansa – Magamba mpaka Mkwajuni. Tunaomba Wizara waliangalie hili. Barabara hii tumekuwa tuna changamoto kubwa sana hasa kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe. Tumeendelea kulizungumza mara nyingi, wananchi wa Wilaya ya Songwe hapo wanapohitaji huduma za mkoa inawalazimu kwenda kupitia Mkoa wa Mbeya. Wakitoka Mkoa wa Mbeya ndiyo wanapata usafiri mwingine kuelekea Mkoani Songwe. Kwa hiyo tuombe Serikali waliangalie jambo hili kuweza kututengenezea barabara ya kutoka Mlowo itakayopita Isansa – Magamba mpaka Mkwajuni ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe.

Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara nyingine ambayo pia imekuwa ni changamoto ni Barabara ya kutoka Chapwa inayopita Chindi mpaka Chitete. Tunaomba barabara hii Wizara iiangalie. Tunajua jinsi wananchi wa Momba ambavyo wanajishughulisha na shughuli za kilimo, ufugaji na mambo mengine. Tunaomba barabara hii waikumbuke kwenye bajeti zao ili tuweze kuwakomboa na kuwarahisishia huduma wananchi wa Wilaya ya Momba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba nizungumzie, ni kweli tunatenga bajeti sana kwenye Wizara hii, lakini tunaona changamoto kubwa miradi mingi inachelewa kutekelezeka na kuchelewa kutekelezeka kwa miradi kunapelekea miradi mingi kuongezeka gharama. Gharama za miradi zinaongezeka kutokana na miradi mingi kuchelewa kutekelezeka. Tunaomba Wizara iliangalie hili ili mwisho wa siku tusiwe tunatumia fedha nyingi kwa ajili ya mradi ambao pengine unaweza kutekelezeka kwa fedha kidogo na fedha zingine zinaweza kusaidia kwenda kwenye maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine la wakandarasi kuchelewa kulipwa malipo yao. Tumeona sisi sote kwenye taarifa hata zilizopita wakandarasi wanavyocheleweshwa kulipwa malipo yao mara nyingi imetokea faini kwa Serikali, tunalipa fedha nyingi kwa sababu ya kuchelewesha malipo ya wakandarasi. Tunaomba Wizara iliangalie, tumeona maeneo mengi wakandarasi wanachelewa kukabidhi miradi, lakini hatuoni wao wakilipa zile asilimia ambazo wanatakiwa kukatwa pale wanapokuwa wamechelewesha mradi. Kwa hiyo tunaomba Wizara pia iliangalie hili ili tuende kwa usawa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba nizungumzie suala la bandari kavu ndani Mji wa Tunduma. Sisi sote tunajua 70% ya mizigo yote inayoshuka katika Bandari ya Dar es Salaam inapita ndani ya Mji wa Tunduma na tumeendelea kusema, tumezungumza sana, tunaomba Serikali waangalie umuhimu wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma ili kurahisisha huduma.

Mheshimiwa Spika, wote tunajua ya kwamba Tunduma ni lango kuu la SADC. Mkoa wa Songwe ni lango kuu la SADC, Wizara iangalie umuhimu wa kujenga bandari kavu. Sisi sote tunajua nchi yetu na maeneo mengine tuko katika ushindani wa kibiashara. Wizara izingatie na iangalie umuhimu wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma ili kurahisisha huduma na wakifanya hivi na wote wanajua kabisa Halmashauri ya Mji wa Tunduma tayari imejitahidi kwa sehemu yake kuhakikisha inapambana kupata zaidi ya ekari 2,000 kwa ajili ya kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma. Tunaomba Serikali waliangalie hili kwa umuhimu wake ili kuhakikisha Halmashauri ya Mji wa Tunduma inajengwa bandari kavu kama eneo la lango kuu la SADC na hiyo itakuwa imerahisisha huduma sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie jambo lingine ambalo ni suala la Uwanja wa Kagera, Uwanja wa Ndege. Wote tunajua changamoto ambazo zimeendelea kutokea Kagera. Tumeona maafa, tumeona wananchi wamepoteza maisha, tumeona na changamoto hizi zinasababishwa na hali ya hewa.

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali ione umuhimu wa kujenga uwanja mwingine mpya ndani ya Mkoa wa Kagera, kwa sababu sisi sote tunajua kuna uhitaji mkubwa wa usafiri wa anga kwenye Mkoa wa Kagera. Hebu Wizara waliangalie hili na waone umuhimu wa kujenga uwanja mpya ili kuepusha maafa zaidi yanayoweza kutokea kwenye Mkoa wa Kagera. Wananchi wetu tunawahitaji na huduma tunahitaji zitolewe, tena huduma zilizo sahihi zaidi. Wizara ione umuhimu wa kujenga uwanja mpya ndani ya Mkoa wa Kagera ili tuweze kurahisisha huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie suala la ATCL. Wamezungumza wengi sana, naomba niishauri Wizara, naomba niishauri Serikali, ni kweli watu wamezungumza sana ATCL, lakini Serikali ione namna gani ya kulisaidia Shirika la ATCL ili lisiweze kuingia hasara kama tunavyoiona sasa. Kwa asilimia kubwa naona hata Serikali wanasababisha shirika hili kuendelea kudidimia. Nasema hivyo kwa sababu Serikali wameikodishia ndege ATCL, ndege zinakamatwa lakini ATCL bado inaendelea kuwalipa Serikali. Serikali ikae chini ijitafakari na wao watakuwa ni sehemu ya kulididimiza hili shirika. Serikali iangalie namna ya kuisaidia ATCL ili iweze kuinuka kutoka mahali ilipo kwenda eneo lingine.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante. (Makofi)
Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Katiba ya Usafiri wa Anga Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kusema naunga mkono azimio hili kutokana na umuhimu wake. Pamoja na kuunga mkono nina mambo machache ya kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukubaliana kwa azimio hili ni kwamba tumekubali kuingia katika ushirikiano na ushindani wa kibiashara. Hata hivyo, kama tumekubali kuingia katika suala zima la ushindani wa kibiashara ni lazima tuangalie shirika letu. Je, lina uwezo wa kukabiliana na huo ushindani ambao tunakwenda kuingia?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirudi kwenye hali halisi ya shirika letu la usafirishaji limekuwa likikabiliana na changamoto nyngi sana. Vile vile, tumeona katika taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya CAG namna ambavyo shirika hili limekuwa likikabiliana na matatizo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa tunakwenda kuingia kwenye ushindani wa kibiashara ni lazima Serikali ikubali kufanya mabadiliko kwenye suala zima la ushindani wa kibiashara ili twende tukafaulu kwenye suala zima la ushindani wa kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa kwenye taarifa ya CAG namna ambavyo shirika limepata hasara kwa miaka mitano mfululizo. Sasa kama tunakwenda kuingia kwenye ushindani wa kibiashara na tunaona kuna maeneo ambayo shirika letu linakwama, ni lazima tuwe na mambo ya kushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia taarifa ya CAG hiyo hiyo ya mwaka 2022, inasema wazi kabisa kwenye suala la ukaguzi wa mashirika ya umma namna ambavyo shirika lina madeni makubwa kuliko mtaji lilionao. Sasa, kama tunakwenda kuingia kwenye ushindani wa kibiashara ni lazima Serikali ikubali kuyatazama haya ili tusiende kuaibika huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya CAG inasema wazi kabisa kwamba mtaji ambao shirika lilikuwa nao ni bilioni 295.2, wakati huo madeni ambayo shirika linadaiwa ni bilioni 535. Tafsiri yake shirika lina mtaji hasi…. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Stella, changia hoja ambayo iko mbele yako. Changia mjadala wa kuridhia kuingia katika huu Mkataba wa Civil Aviation.

MHE. STELLA S. FIYAO: (Hapa alizungumza bila kutumia kipaza sauti).

NAIBU SPIKA: Wewe hebu kaa kimya. Mimi naongea na wewe unasema, kama nani? Kuna shirika gani katika dunia sasa hivi linatengeneza faida kwenye ndege? Nitajie moja tu. Changia hoja iliyokuwepo mbele, kama umemaliza kaa chini. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika ni lazima tutoe angalizo kama Bunge. Ni vema Serikali ikajidhatiti katika kuwekeza kwenye shirika hili ili tupate matokeo yaliyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, naomba kuishauri Serikali iwekeze kwenye shirika hili ili liweze kujiendesha kibiashara. Jambo la pili, Serikali iwekeze kwenye shirika hili ili tuweze kuinuka kidedea katika suala zima la ushindani wa kibiashara. Hatuwezi kuingia kwenye ushindani wa kibiasharra kama Serikali haijakubali kuwekeza kwa asilimia mia moja kwenye shirika hili, tuta-fail na tutaaibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kushauri, kumekuwa na changamoto nyingi za ukamataji wa ndege. Ni vema Serikali ipitie kesi za madai za kitaifa ili kuepusha changamoto ya ukamataji wa ndege na kuziingiza ndege zetu kwenye hatari ya kukamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo naunga mkono Azimio, lakini naomba Serikali iyazingatie niliyoshauri. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Naendelea kusema na nitatizidi kusema Wizara hii ni muhimu sana na ukiangalia michango mingi ya Wabunge utaona kuwa suala la barabara ni janga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara limekuwa ni janga na ndiyo maana unaona kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia kwa habari ya barabara kwenye eneo lake kwa sababu hali ya barabara kwenye maeneo tunayotoka kiuhalisia hairidhishi, hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitaanza kwa kuzungumzia barabara ya kutoka Mloo kwenda Chitete mpaka Kamsamba na niombe Wizara iangalie barabara hii kwa jicho la pili, kwa sababu barabara hii kwanza ina mchango mkubwa kwa uchumi wa Mkoa wa Songwe, lakini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Mloo - Chitete kwenda Kamsamba inatumiwa na wakulima wengi sana na wavuvi ambao wanatoka huko Kamsamba na maeneo mengine. Sasa hatuwezi kusema barabara hii haina mchango katika pato la Taifa letu. Hebu tuona Wizara iangalie barabara hii kwa umuhimu wake kwa sababu barabara hii imekuwa na changamoto kubwa, wananchi wanapata shida kweli kweli lakini wakati huo wanachangia kwa asilimia kubwa katika pato la Taifa letu. Tuombe Wizara iangalie barabara hii kwa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kuzungumzia kwa suala la Mji wa Tunduma. Sisi sote tunajua kwamba Mji wa Tunduma ni lango kuu, ni mji ambao upo mpakani kwanza, lakini ni lango kuu la SADC. Nchi nyingi zinatumia mpaka huu wa Tunduma na ukiangalia asilimia 70 mizigo inayoshushwa katika bandari yetu inakwenda kupitia katika Mji wa Tunduma. Lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa sana ya barabara kutokana na ule mrundikano wa magari makubwa wananchi wetu wamekuwa wakikutana na adha kubwa sana, jambo ambalo kwanza linawacheleweshea katika masuala ya uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa barabara hii hebu tuombe, wizara ione umuhimu na ilichukulie jambo hili kwa dharura kuhakikisha inafanya upanuzi wa haraka wa barabara ili kuweza kuwanusuru wananchi wa Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi mmoja uliopita kulikuwa kuna maandamano na mgomo wa madereva wa magari makubwa ambao wanavuka katika huu mpaka wa Tunduma, jambo ambalo liliwapelekea wananchi wa Mji wa Tunduma kupata adha kubwa sana. Hebu fikiria mwananchi anatoka Tunduma kwenda kupata huduma ya kiafya kwenye Hospitali ya Mkoa anachukua siku tatu kufika Vwawa, hili ni jambo la ajabu sana. Hebu tuombe Wizara ichukulie jambo hili kwa dharura na barabara hii iweze kupanuliwa kwa udharura wake kwa sababu tunajua sisi sote mpaka huu namna gani ambavyo unachangia katika pato la Taifa letu. Hebu tuombe jambo hili wizara ilichukulie jambo hili kwa udharura.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ambalo nataka kuishauri Wizara, niombe Wizara ione umuhimu wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma. Kwa sababu sisi sote tunajua ili kurahisisha huduma kwa nchi jirani ambazo zinapata huduma katika mpaka wa Tunduma, Wizara ione umuhimu wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma ili tuweze kuepuka changamoto zingine ambazo hazina ulazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la kibajeti katika Wizara hii ya Ujenzi hasa katika bajeti ya barabara. Kwa mwaka huu wa fedha katika miradi ya maendeleo ya barabara kiasi ambacho kilikuwa kimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya barabara ni shilingi trilioni 1.588. Lakini kiasi ambacho kilikuwa kimetolewa ni shilingi trilioni 1.093; fedha hizi hakuna fedha yoyote iliyoelekezwa katika miradi ambayo tuliipangia ndani ya Bunge hili. Hakuna fedha yoyote iliyokwenda kutekeleza mradi hata mmoja, badala yake fedha hizi zimekwenda kulipa madeni ya nyuma na kilio cha barabara kimebaki palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana leo hii ukiona kila Mbunge anainuka na kulia kwa habari ya barabara kwenye eneo lake kwa sababu katika bajeti tuliyokuwa tumepitisha hakuna mradi wowote uliotekelezwa hili ni ajabu sana. Leo hii msione Wabunge wanataka kuruka sarakasi mezani wana uchungu ni namna ya kuhakikisha ujumbe wao unafika na Wizara hii iweze kuwaelewa. Tunafanya mambo gani, ikiwa tunapoteza muda tunakaa ndani ya Bunge hili, tunachangia tunashauri kwa habari ya barabara katika maeneo yetu, tunaelezea changamoto zilizopo huko kwenye maeneo yetu na barabara nyingi zinagusa uchumi wa Taifa letu, halafu tunatenga bajeti, bajeti inakwenda kulipa madeni yote, ni jambo la ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukaa kupoteza muda kwenye Bunge hili tukiwa tunajadili bajeti ya kulipa madeni ya nyuma, haiwezekani. Hebu tuombe Wizara inavyotuletea bajeti zake humu wawe wanatuambia katika kiasi cha maendeleo tunachotenga ni kiasi gani kitakwenda kulipa madeni na kiasi gani kitakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo ili tutoke tukiwa wamoja. Nje na hapo hatuwezi kueleweka kwa wananchi wetu kwa sababu mwisho wa siku wananchi wetu hawawezi kutuelewa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nizungumzie suala la wakandarasi; kuna hasara kubwa ambayo tunaipata Serikali imekuwa ikiingia hasara ya shilingi 2,900,000,000 kila mwaka na hasara hii inatokana na wazabuni kucheleweshewa kulipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii fedha tunayoisema leo hii kama naweza kuzungumzia barabara ya Mloo – Chitete kwenda Kamsamba hivi hii fedha si ingeweza kutusaidia hata watu wa Mkoa wa Songwe jamani. Fedha hii ingeweza kutusaidia, lakini wewe fikiria kila mwaka Serikali inaingia hasara ya shilingi bilioni 2.9; hii haikai sawa. Hebu tuombe Wizara hii ijitahidi ikae na iangalie ni namna gani inayakwepa haya hatuwezi kila siku tukawa tunapiga kelele tunapigia haya haya. Mwaka jana nimesema hapa hasara ambazo tunazipata kutokana na kuchelewesha malipo ya wakandarasi, lakini leo hii bado tunaingia kwenye Bunge hili tunajadili haya haya mambo hii haikai sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uhitaji mkubwa sana kwenye maeneo yetu wananchi huko hawatuelewi kwa sababu hali ni mbaya na kodi wanatoa hii haikai sawa. Hebu tuombe Wizara iangalie namna bora ya kutatua hizi changamoto ili tutoke tukiwa wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika mpango huu. Kwanza naanza kwa kuzungumzia suala la Bandari Kavu ya Tunduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua hata Serikali inajua umuhimu wa mpaka wa Tunduma hasa kwa kuzingatia kwamba mpaka wa Tunduma ni lango kuu la SADC. Mpaka wa Tunduma unapitisha mizigo zaidi ya asilimia 73 inayoshuka katika Bandari ya Tanzania. Mizigo yote hii inapita katika mpaka wa Tunduma ambalo ni lango kuu la SADC. Katika michango yetu mbalimbali tumeendelea kuisisitiza Serikali na kuiomba, ione umuhimu mkubwa wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma ili kurahisisha huduma za usafirishaji wa mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajabu ni kwamba, tangu nimeanza kuusoma Mpango huu, sijaona mahali ambapo Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha inajenga bandari kavu katika Mji wa Tunduma ili kurahisisha huduma kwa watu ambao wanatumia mpaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike wazi kabisa kwamba sasa hivi mataifa yapo katika ushindani wa kibiashara ikiwemo Tanzania. Tunaona mataifa mengi ambayo yanaandaa mipango ya kujenga bandari kavu katika mataifa yao. Ni lazima Serikali ione umuhimu wa kujenga bandari kavu katika Mji wa Tunduma hasa ukizingatia kuwa ni lango kuu la SADC ili kurahisha huduma na kuendelea kuwashawishi watu ambao wanatumia mpaka huu wa Tunduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua umuhimu wa bandari kavu na sisi sote tunaona namna Halmashauri ilivyolichukua jambo hili kama kipaumbele. Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetenga zaidi ya ekari 2,000 kwa ajili ya kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma. Tumeomba miundombinu, tumeona reli imepita katika lile eneo, tunaona hospitali kubwa imejengwa katika yale maeneo, tunaona stendi imejengwa katika yale maeneo. Tunaiomba Serikali ione umuhimu wa kujenga bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma ili kuleta ushindani wa kibiashara na mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia suala la kilimo. Nazungumzia upatikanaji wa mitaji katika Sekta ya Kilimo. Mimi ninatokea Mkoa wa Songwe, Mkoa ambao asilimia kubwa ya wananchi wake wanaishi vijijini na ni wakulima wakubwa, na ni wakulima wazuri kabisa ambao wanategemewa na Taifa hili. Tunaona katika pato la Taifa namna kilimo ambavyo kimekuwa na mchango mkubwa, zaidi ya asilimia 26 kilimo kinachangia katika pato la Taifa. Hivyo, kilimo ni kipaumbele kikubwa ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona katika upatikanaji wa mitaji ya sekta ya kilimo kwa mwaka 2022/2023, taarifa inasema zaidi ya shilingi trilioni 2.622 zilitengwa na benki kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10, lakini katika fedha hii shilingi trilioni 2.622 ambayo ilitengwa na hizo benki, 7% tu ndiyo ilikwenda katika uzalishaji wa mazao, asilimia 93 ilikwenda katika biashara ya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatari kwa Taifa letu. Tunaona namna watu ambavyo wamezama kwenye biashara na wamesahau kwenye suala zima la uzalishaji wa mazao ndani ya Taifa letu. Ndiyo maana tunatumia fedha nyingi kuagiza baadhi ya mazao nje kwa kuwa huku ndani tumeshindwa kuwekeza. Tuna wakulima wengi sana ambao wamejitoa kwenye suala zima la kilimo, lakini wengine wanashindwa tu kwa sababu ya mitaji. Tuna ardhi ya kutosha ambayo hata nusu, hata robo bado hatujaifikia, lakini bado tuna changamoto kubwa ya kuagiza baadhi ya vyakula nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, ione umuhimu wa kuwekeza fedha nyingi ambazo zinatengwa na benki, ziende kwenye uzalishaji wa mazao na siyo biashara. Ni lazima tuzalishe mazao ya kutosha, ni lazima tuzalishe mazao ya aina mbalimbali ya kutosha ndani ya Taifa letu na ikiwezekana tuuze nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona kuna changamoto. Ukisoma katika taarifa utaona ya kwamba Magereza yetu yanatumia zaidi ya shilingi bilioni 10 kila mwaka kwa ajili ya chakula. Wakati huo tunaona namna ambavyo Magereza yana ardhi kubwa na nzuri ya kutosha ambayo inaweza kutusaidia katika uzalishaji wa mazao. Changamoto kubwa ambayo Magereza wanashindwa ni kukosa mtaji na fedha za kuendeshea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ione umuhimu wa kuwekeza fedha na kuwakopesha watu wa Magereza ili waweze kuzalisha chakula kingi na ikiwezekana wajiendeshe, wajikwamue kiuchumi na waweze kutusaidia katika suala zima la uzalishaji wa chakula ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumza jambo moja. Kumekuwa kuna changamoto, kwamba wakulima wetu wanatumia muda mwingi kupambana na kuhakikisha wanajikwamua katika suala zima la kiuchumi kupitia kilimo. Nasema wazi, tumeona katika mkoa wetu na maeneo mengine, Serikali imewatangazia wakulima kwamba iko tayari kununua mazao na wakulima bila kusita wamejitoa kwa moyo wote kuiuzia Serikali mazao. Ajabu ni kwamba, NFRA Wakala wa Chakula, inaeleweka hiyo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajabu ni kwamba, tangu mwezi wa Tisa, wa Nane, wa Kumi, watu wamechukua mazao lakini wakulima hawajalipwa fedha zao, pamoja na Serikali kuchukua haya mazao. Tunaomba, watu wamelipwa wachache na wengine bado hawajalipwa na ukizingatia katika mikoa yetu, tumeingia katika msimu wa kilimo. Huyu mkulima mnamweka kwenye eneo gani? Mimi ninachojua wakulima wanalima mazao wakiwa na malengo.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella, kuna Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilinunua mazao yenye thamani ya shilingi bilioni 194. Mpaka kufika siku ya jana, Serikali imemaliza madeni yote ambayo ilikuwa inadaiwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella, Taarifa rasmi hiyo unaipokea?

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei Taarifa.

MWENYEKITI: Aaah!

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa kwa sababu, sisi mwezi huu na mwezi uliopita tayari tumeingia kwenye maandalizi ya kilimo. Mnawaletea wakulima wetu vidonda vya tumbo! Nina uhakika hata Momba huko Isanga hawajalipwa. Labda kama mmelipa jana, ndiyo mtuambie. Kama watu wamepimiwa mazao kutoka mwezi wa Nane wamelipwa jana, hii inakaa sawa? Kwamba hawa wakulima hawana malengo? Hakuna anayefanya kazi bila malengo. Acheni kuwasababishia wakulima umaskini usio na lazima. Ni lazima tuseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala zima la barabara. Sisi wote tunajua zaidi ya asilimia 80 mpaka 90 ya mizigo na abiria wanatumia barabara. Hivyo, ni wazi kwamba barabara ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu na maendeleo ya kijamii. Hata hivyo kumekuwa na changamoto, na ndiyo maana kila Mheshimiwa Mbunge anayesimama hapa, anazungumzia suala la barabara. Barabara imekuwa ni changamoto kwenye nchi yetu. Maeneo mengi barabara zinakufa, zina hali mbaya kabisa. Kuna maeneo hata barabara za kuunganisha mikoa na mikoa zina hali mbaya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, kengele ya pili.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, lakini muda wangu mwingine ulichukuliwa na Mheshimiwa Waziri. Nashukuru.