Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Felista Deogratius Njau (35 total)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ifahamike kwamba kuhusu upimaji wa ardhi ndani ya nchi yetu mlolongo huu umekuwa na kigugumizi kikubwa na kupelekea Serikali kupoteza mapato, migogoro ya ardhi isiyokuwa na lazima na tatu wananchi kukosa dhamana ya kwenda kuchukua mikopo maana yake wananchi kupata umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la kwanza; Ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa kwa sababu Waziri alisimama kwenye vyombo vya habari akajinasibu akasema ndani ya mwezi mmoja mtu akishapimiwa atapata hati. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi wa Basihaya wako tayari baada ya kukaa na Mwekezaji, Serikali na wananchi wa Basihaya wako tayari kulipa premium, kiwango ambacho kilikuwa ni makubaliano kati yao na premium ni kati ya 1% mpaka 1.5%. Ni lini sasa Serikali itakwenda kutoa hati katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itapima maeneo yote ili kuweza kuondoa pengine adha ambayo watu wanaipata. Naomba niseme tu bajeti ambayo tunaendelea nayo imeainisha namna ambavyo Wizara imejipanga katika kuhakikisha kwamba maeneo yote nchini yanapimwa. Katika kufanya hilo pia tumeweza kushirikisha makampuni binafsi katika kufanya ule urasimishaji kwenye yale maeneo ambayo tayari yalikuwa yameshakaguliwa. Suala la kupima nchi nzima liko katika utaratibu wa bajeti ya Serikali na inategemea pia na upatikanaji wa fedha, lakini mpango upo ambao tutakwenda kukamilisha upimaji. Hili pia linahitaji ushirikiano na taasisi binafsi ambazo tumekuwa tukizishirikisha ambapo nyingi zimeonekana pia hazina uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo kama Wizara tunatafakari namna bora ya kuweza kukamilisha zoezi hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo amezungumzia habari ya umilikishaji katika maeneo yale, kwanza nataka tu niseme kwamba Mheshimiwa Felista anatakiwa kuishukuru sana Serikali kwa sababu maeneo yale ambayo anaombea watu kumilikishwa kisheria ilikuwa waondolewe, kwa sababu walikuwa wamevamia, lakini busara ya Wizara au ya Serikali ilipelekea kufanya mazungumzo ili wale watu waweze kumilikishwa na zoezi hilo linaendelea. Katika urasimishaji ile premium ambayo anaizungumza ni asilimia moja ambayo ni ya chini kabisa ukilinganisha na maeneo mengine ambayo wanalipa almost 2.5% na kabla ya hapo ilikuwa 15%, ikashuka ikawa 7.5%, ikaja 2.5% kwenye urasimishaji ni 1%. Kwa hiyo wanachajiwa kiasi cha chini kabisa kuweza kuwawezesha kupata umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la Hati, nadhani ninyi wenyewe ni mashahidi, Mheshimiwa Waziri pia ameweza kukaa ofisini na kuweza kuwapigia watu mmoja mmoja kuja kuchukua hati zao. Nimezunguka almost nchi nzima nikienda kugawa hati katika maeneo mbalimbali. Kuna hati ziko tayari lakini Watanzania hawaji kuchukua hati zao, lakini ukija nje wanasema hati hazitoki. Kasi ya utoaji hati kama tulivyosema ni ile ile ndani ya mwezi mmoja kama halmashauri imekamilisha taarifa zote, hati yako unaipata na zoezi hilo linafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wale wote wanaohitaji kupata umiliki wa ardhi kama ambavyo ameongelea Mheshimiwa basi wawe tayari, pia ukishapeleka maombi yako uhakikishe umekwenda mpaka mwisho na umechukua hati yako. Wizara ndiyo custodian wa hati.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mpaka sasa kuna kaya kumi ambazo maji yameingia ndani na hawana pa kuishi katika Mtaa wa Ununio, Serikali ina mkakati gani wa dharura kabla ya kutekeleza mradi huu alioutaja ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata mahali pa kuishi na sehemu zile nilizoainisha zinapata majibu mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilio hiki ni cha nchi nzima kwa maana matatizo haya yamekuwa yanajirudia kila eneo la nchi; ni lini basi Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kujenga mifereji imara ili basi maeneo haya maji yaweze kuelekezwa kwenda kwenye maziwa, mito hata bahari ili kuepuka adha ya magonjwa ya milipuko pia na adha kwa wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza alikuwa anaomba kujua upi ni mkakati wa dharura katika eneo la Ununio ambao Serikali imeuweka kuhakikisha tunatatua tatizo hilo la mafuriko. Nimuambie tu kabisa kwamba Serikali iko kazini na baada ya janga hili inafanya tathmini ya mwisho kuhakikisha kwamba tunasaidia maeneo hayo hususan maeneo ya Ununio katika Kata hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza ni lini Serikali itaweka mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba tunaondoa majanga haya hususan kwa kujenga mifereji. Nimhakikishie kabisa kwamba sasa hivi moja ya mkakati mkubwa ambao Serikali unao katika kila barabara tunayoijenga tunaambatanisha na ujenzi wa miundombinu hususan mifereji. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu ya mikakati ambayo ipo na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutajenga mifereji mikubwa pamoja na midogo kuhakikisha janga la mafuriko nchi nzima katika maeneo yote ambayo tunayasimamia hayapatwi na hii adha ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha. Ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Shirika la Nyumba la Taifa lengo lake kisheria ni kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi wa kima cha chini na hii inasababisha wananchi wale kununua kwa bei rahisi. Hata hivyo, Shirika linashindwa kutekeleza jukumu hili kutokana na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo inakuwa kwenye vifaa vya ujenzi. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuondoa hii kodi katika vifaa vya ujenzi kwa shirika la nyumba la Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Ripoti ya CAG ya 2019/2020 ilionesha kwamba mradi huu usipokamilika mapema basi Serikali itaingia hasara kwa kulipa Shirika la Nyumba shilingi bilioni 100 na mpaka sasa wakandarasi wanalipwa. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza mradi huu ili kuepuka hasara hii ya Taifa ambayo inaenda kuingia?

Mheshimiwa Spika, lakini pili, kuweza…

SPIKA: Aahaa, tayari maswali mawili. (Kicheko)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda hautoshi, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu sheria ilipitishwa Bungeni humu aangalie malengo mazima ya uanzishwaji wa Shirika la Nyumba. Mbali na hilo alilolisema, lakini kwa sasa Shirika la Nyumba halipati ruzuku yoyote kutoka Serikalini na hivyo ni shirika linalojiendesha kibiashara. Kwa hiyo, katika miradi linayofanya kuna kujenga zile nyumba za gharama nafuu ambazo watu wananunua na wengine wanapanga, lakini pia linakuwa na miradi ya kibiashara ambayo inaliongezea pato Shirika ili kuweza kupanua miradi na kuweza kuongeza wigo wa kupata pesa kwa ajili ya kuendelea kujenga. Kama sasa hivi hapa Dodoma wana mradi wa nyumba 1,000 ambao wanaendelea kujenga nazo ziko katika viwango tofautitofauti.

Mheshimiwa Spika, ameongelea suala la kuondolewa kwa VAT kwa Shirika la Nyumba. Naomba niseme tu, katika suala zima la ujenzi ni mashirika mengi ambayo yanafanya kazi hizi za ujenzi ikiwemo Watumishi Housing. Kwa hiyo, unapozungumzia suala la kuondoa VAT, Watumishi Housing nao wanajenga nyumba kwa ajili ya wafanyakazi, sasa huwezi ukasema unaondoa VAT wakati haya mashirika yote yanafanya huduma ileile ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuboresha makazi kwa watu wetu. Kwa hiyo, hili kama linaonekana kwamba ni tatizo basi nadhani ni jambo la kuangaliwa upya, lakini kwa sasa bado VAT itaendelea kutozwa kama ambavyo inaendelea, japokuwa kama Wizara tulikuwa na mpango awali wa kuangalia namna bora ya kuweza kuliwezesha Shirika kwa kuangalia pia katika suala hilo la VAT, lakini bado mchakato haujafikia mwisho wake kwa sababu ya hali halisi ya ushindani na mashirika yanavyofanya kazi kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, anaongelea suala la utekelezaji wa mradi ule kwamba unapata hasara na CAG ameonesha. Kwenye jibu langu la msingi nimesema ya kwamba kwa sasa tumepanga mradi huo utaendelea na ujenzi katika mwaka wa fedha huu 2020/2021 kwa sababu kubwa tu kwamba mradi wa Morocco Square ambao unaendelea mpaka sasa na tayari umefikia kwenye asilimia 92 ukikamilika ule tayari unaongeza vyanzo vya pesa kwa ajili ya ku-subsidize matumizi katika ujenzi ule. Pia tunayo Victoria Palace ambayo ina unit 88 lakini pale tayari 86 zimeshanunuliwa. Kwa maana hiyo ni pesa inayoingia kuliwezesha Shirika mbali na kutegemea mikopo basi pia kutoka katika vyanzo vya ndani vya miradi yake ya uwekezaji vitaenda kusaidia kuweza kukamilisha mradi ule ili kuweza kuboresha mji ule ambao uko katika eneo ambalo ni very prime.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niseme kwamba katika Jimbo la Kawe kuna barabara kama hizo ambazo ni sugu kama Barabara ya Ununio – Malindi, Mbweni – Teta mpaka Mpiji. Barabara hii inajengwa lakini inasuasua kwa muda mrefu: Ni lini sasa Serikali itamalizia barabara hii ili wananchi hawa waweze kupata nafuu?

Swali la pili, ni mkakati gani endelevu wa Serikali ambao sasa baada ya barabara hizi kujengwa wataweka mitaro ambayo haitaathiri barabara hizi kwa sababu imeonekana barabara nyingi zinaharibika kwa sababu ya mitaro? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuainisha baraba nyingine katika Jimbo la Kawe ambazo ni mbovu ikiwemo barabara ya Ununio – Malindi, Mbweni – Teta mpaka Mpiji na akaiomba Serikali izitengeneze. Najua Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi nzuri na mimi nimwahidi kabisa kwamba kama tulivyozungumza katika swali letu la msingi, tutaendelea kufanya tathmini na kadri tutakavyopata fedha hizo barabara zitatengenezwa. Hiyo ndiyo nia ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili amejaribu kuainisha kwamba ni mkakati gani ambao unaweza kusaidia zile barabara zetu zisiharibike ikiwemo kujenga mitaro itakayopitisha maji nyakati za mvua? Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge anatambua kabisa kwamba kuna mpango mkubwa wa DMDP wa ujenzi wa barabara kwa maana ya miundombinu yote katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya fedha ambazo zipo ni pamoja na kujenga mitaro ili kuhakikisha barabara zetu zote zinakuwa na ubora katika muda wote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie mkakati wa Serikali ni pamoja na kuendelea kujenga mitaro, madaraja na kuziboresha barabara zetu kwa kipindi chote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nilikuwa nataka niiulize Serikali ni lini itamaliza kero ya maji ambayo imekuwa ni sugu katika Kata ya Wazo, Mitaa ya Nyakasangwe, Mitaa ya Salasala na Mivumoni Kata ya Mbezi Mtoni, Sakuveda na Mabwepande Mtaa wa Mbopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia DAWASA wanafanya kazi nzuri sana maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Na tayari mikakati kabambe inaendelea na kufikia mwaka ujao wa fedha maeneo mengi sana ya maeneo hayo yote uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge yatakuwa yamefikiwa na maji bombani.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni lini Serikali itajenga barabara inayoanzia Bunju A kupitia Mabwepande ikiunganisha na Jimbo la Kibamba ambayo barabara hiyo imekaa muda mrefu na ikitolewa ahadi bila utekelezaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yalikuwa pia ni ahadi ya Mheshimiwa Hayati Rais na pia yalikuwa ni maagizo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hizo barabara, TANROADS kwa maana ya Mkoa wa Dar es Salaam kusaidiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) tutahakikisha kwamba hizi barabara zinatekelezwa kuanzia kipindi hiki cha mwaka wakati wa utekelezaji wa bajeti ya kuanzia mwaka huu 2021. Ahsante.
MHE. FELISTER D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, wavuvi wengi wadogowadogo katika ukanda wa Pwani Jimbo la Kawe hasa katika Kata za Msasani, Kawe, Mbweni na Kunduchi wanachangamoto kubwa ya mtaji wa kununua vifaa vya kisasa stahiki ambavyo vinaweza kuwasaidia kupata samaki kulingana na taratibu za kisheria. Ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wavuvi hawa wanapata vifaa hivyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Njau kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mtaji kwa wavuvi ni moja ya Sera yetu ya Serikali na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imesisitiza katika kuweka mazingira rafiki ili kusudi wavuvi wetu waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, katika hili, kwa kutumia dirisha lililopo Benki yetu ya Kilimo, iko mikopo kwa ajili ya wavuvi na wadau wanaoshughulika na masuala ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote wanaotoka katika maeneo ya wavuvi kuhakikisha kwamba wavuvi wanakaa katika vikundi. Na sisi tupo tayari kwenda kuwaunganisha na mabenki na hata kuwapa elimu na mpango mkakati wa namna ya kuandika kuweza ku-access fursa ile ya kupata mikopo, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, katika jimbo la kawe Kata ya Mbweni kuna wavuvi wengi wadogo wadogo na upatikanaji wa samaki ni mwingi sana lakini wavuvi wele hawana soko la uhakika pale, hawana sehemu maalum ya kuuzia. Ni lini Serikali itajenga soko la uhakika katika Kata ya Mbweni ili kuinua uchumi wa wavuvi wadogo wadogo na kuinua pato la Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felisha Njau kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika maeneo ambayo yana wavuvi wengi kwenye Jimbo la Kawe wako wavuvi pia. Hapa karibuni nilikwenda kwenye Beach ya Kawe kwa maana ya Kawe Beach, ambako pale lipo Soko la Wavuvi, tayari tumetoa maelekezo kwa wataalam wetu kwenda kuzungumza na viongozi wa eneo lile wakiongozwa na Mheshimiwa Diwani kijana Mheshimiwa Lwakatare, kwa ajili ya kukaa na wavuvi wale na kupanga mpango tuweze kushirikiana na Hamnashauri ya Wilaya ya Kinondoni ambayo ina mapato mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tutashirikiana nayo kuhakikisha kwamba tunatengeneza soko zuri ni mahali pazuri ambako tunaweza kuvua kutengeneza samaki na watu waweze kwenda pale weekends ku-enjoy samaki wa baharini, ni samaki wazuri sana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Katika Kata ya Wazo, Jimbo la Kawe tayari zahanati imekamilika, lakini hakuna Jengo la Mama na Mtoto. Ni lini Serikali itajenga jengo hilo ili kunusuru uhai wa akinamama hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Kata ya Wazo zahanati imekwishajengwa lakini hakuna Jengo la Mama na Mtoto, lakini nafahamu Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni haiwezi kushindwa kujenga Jengo la Mama na Mtoto. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutenga fedha kwa ajili ya kujenga Jengo la Mama na Mtoto katika zahanati hii kwenye Kata ya Wazo.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwenye taasisi nyingi za Serikali na zisizo za Serikali kuna mkanganyiko mkubwa kwamba wananchi wengi wenye namba za NIDA hawapati huduma. Naomba kauli ya Serikali leo kuhusiana na wananchi wenye Namba za NIDA ambao hawana vitambulisho na wanakosa huduma hasa kwenye mikopo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli ya Serikali ni kwamba huduma za Serikali popote zilipo zinatakiwa zitolewe kwa kutambua uhalali wa namba za vitambulisho. Kwa sababu hatuwezi kumhukumu mwananchi kutokupata huduma kwa kosa ambalo siyo lake. Kama amechukua hatua zote za kisheria kuweza kujisajili, amepatiwa namba ya kitambulisho na kadi hatujampa kwa kosa ambalo siyo lake, lazima huduma yake ya msingi apate.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kauli ya Serikali ni kwamba taasisi zote zinazohusika za Serikali, kama kuna changamoto basi tutakaa tuzungumze ndani tuone, inawezekana pengine kuna baadhi ya Taasisi kulingana na masuala ya kisheria au masuala ya kimiundombinu zinashindwa kutekeleza hayo. Tutalichukua kama Serikali kwa pamoja tuzungumze tuone tunalitatua vipi maeneo ambayo bado kuna tatizo katika kukibali ama kuzipokea namba hizo za utambulisho wa wananchi. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwakuwa eneo hili kuna baadhi ya maeneo tayari yana miundombinu ya umwagijiaji na miundombinu hii ipo ardhini na ikikaa kwa muda mrefu inaweza kuharibika nataka kujua: -

Je, ni lini hasa Serikali itatenga kiasi hichi cha Shilingi bilioni 11.5 ili kunusuru miundombinu hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwakuwa maeneo mengi nchini katika mikoa yetu yana madhari yanayofanana na Mngeta na maeneo ya Chita.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati sasa wa kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji kwa pamoja ili kupambana na uhaba wa chakula pamoja na kuendeleza usalama wa chakula nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Dar es Salaam. Kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana kwa kazi nzuri anayoifanya katika mkoa wake, lakini pia kwa hamu aliyonayo ya kuona kwamba siku moja jeshi hili linazidi kusonga mbele hasa katika shughuli za sekta hizi za kilimo. Hongera sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza mchakato na ukweli huu unapatikana katika jibu langu la msingi; ukiangalia kwenye mstari wa mwisho, utaratibu wa ndani unaendelea ili kuwasilisha maombi ya fedha Wizara ya Fedha na Mipango. Kwa hiyo, suala hilo la upatikanaji wa hizi Shilingi bilioni 11 tayari utaratibu tumeshauanza na muda wowote tunategemea kupata hizi fedha na tukizipata tutakwenda kufanya kile ambacho Mheshimiwa ameshauri.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kweli tumegundua na utafiti unaonesha kwamba shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na nyingine, kwa kweli zimekuwa zinaathiri sana vyanzo vya maji, athari ambazo mwisho wa siku zinakwenda kuharibu shughuli za kilimo na kufanya shughuli hizi zisiende vizuri.

Mheshimiwa Spioka, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba tumeshakaa na tutaendelea kukaa kufanya stadi mbalimbali kwa kushirikiana na wenzetu wa Tawala za Mikoa kwa maana ya wa Halmashauri, Vijiji na wale wa Mamlaka ya Mabonde ili kuona namna ambavyo tunahuisha vyanzo vya maji kwa ajili ya kuboresha shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Zahanati ya Mabwepande imechakaa na kusababisha wananchi na watumishi kuhudumiwa nje ya kituo chini ya mti: Je, ni lini Serikali itaenda kukarabati zahanati hiyo au kujenga kituo cha afya ili wananchi wa Mabwepande waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya mpango ambao sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tulikaa na Halmashauri zenye mapato makubwa ikiwemo Halmashauri ya Kinondoni, Jiji la Dar es Salaam pamoja na Ilala na Temeke. Tuliwaambia kwamba, kwa sababu maeneo yenu yana fedha kubwa, basi mhakikishe mnatenga fedha kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, kupitia swali hili ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa, nimwagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kuhakikisha kwamba anapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya cha Mabwepande. Ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Balozi nyingi nje ya nchi hazifanyi vizuri kwa ufanisi katika kutangaza fursa za nchi yetu vivutio pamoja na utalii. Nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha Balozi hizi zinafanya vizuri?

Swali la pili, kwa kuwa balozi zetu nyingi nje ya nchi hazina watumishi wa kutosha hasa balozi za kimkakati kama Congo na kwingineko, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama nilivyoelezea katika swali la msingi, kwamba utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ni kipaumbele muhimu cha Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba sera hiyo inatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ambayo inafanya kwanza ni Wizara ni kukiimarisha Kitengo chetu cha Mawasiliano ya Serikali ili kuhakikisha kwamba kinatoa taarifa zote muhimu kwa wadau kuhusu fursa zinazopatikana nje ya nchi na pia fursa ambazo zipo katika nchi yetu na hiyo imefanyika kwa ufanisi sana kwa sababu mfano Ubalozi wetu wa China ni ushahidi kwamba kitengo chetu kinafanya kazi vizuri kwa sababu ni taarifa nyingi ambazo Ubalozi wetu wa China zinapatikana kule na pia Serikali hapa na wananchi kwa ujumla wanapata taarifa nyingi za Ubalozi wetu na China na Balozi nyingine pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la watumishi, ni kweli kwamba ninaungana na Mheshimiwa Mbunge kwamba hapo nyuma kidogo hilo tatizo la ukosefu wa wafanyakazi lilikuwepo na lilikuwa ni kubwa, hata hivyo kwa hivi sasa tayari Serikali imechukua juhudi maalum za kuhakikisha kwamba suala hili halipo. Mfano, katika mwaka uliosha wa 2021/2022 jumla ya wafanyakazi 140 walipelekwa kwenye Balozi zetu mbalimbali nje ya nchi na suala hili ni endelevu, na tayari hivi sasa Wizara yetu imepata kibali cha kuajiri Maafisa wengi tu ambao watakuwepo Makao Makuu kwa ajili baadaye miaka ya mbele huko waweze kwenda kutumikia katika Balozi zetu.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Katika Kata ya Mbezi Juu, Mtaa wa Mbezi Mtoni na Sakuveda kuna changamoto kubwa ya maji. Ni lini Serikali itapeleka miundombinu hii ili wananchi waweze kupata huduma hii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi lengo letu ni kuona tunatua akinamama ndoo kichwani na Mheshimiwa Felista amefuatilia hili, ameshaongea nami. Kama tulivyozungumza, mantahofu, haya maeneo yote maji yatapelekwa na tunataka kuhakikisha ukifika mwaka 2025 maeneo yote ya vijijini yatapata maji kwa asilimia 85 na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Kata ya Wazo, Mkoa wa Dar es Salaam, kuna Kiwanda cha Twiga Cement ambacho kinatiririsha vumbi jingi kuelekea kwa makazi ya wananchi: Nini mkakati wa Serikali kuwanusuru wananchi hawa kuhakikisha hawapati athari za kiafya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la moja la nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hili jambo tumekuwa tunalipigia kelele sana na hasa hivi viwanda ambavyo vipo karibu na makazi ya wananchi. Tumekuwa tunalisemea sana na tumeshachukua hatua nyingi za kinidhamu lakini pamoja na hayo. tumeshakuwa tunakaa na wamaliki wa viwanda hivi na pia tumekuwa tunawapa taaluma.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba jambo hili tunaendelea kulifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba wananchi wanaendelea kuwa salama kutokana na hizi adha na changamoto za viwanda ambazo zinaweza zikawaathiri wananchi kwa njia moja ama nyingine, nakushukuru.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa upandaji wa chakula unategemea gharama kubwa wanazozitumia wananchi katika kulima kwa maana ya kuchelewa kupeleka mbolea. Je, ni nini mkakati wa muda mrefu wa Serikali katika kuhakikisha wanapeleka mbolea kwa wakati ili wananchi waweze kulima kwa faida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumepata changamoto katika msimu huu wa upatikanaji wa mapema wa mbolea hasa ile ya kupandia, kukuzia na kunenepeshea. Nataka nimwondoe hofu kwa mfumo ambao tumeuweka kwenye msimu ujao, tutahakikisha wakulima wanapata pembejeo hizo kwa wakati ili waendane na msimu.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi kwa wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa wa dhana hii ikilinganishwa na sasa inafahamika Kitaifa zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tumeona vyombo vingi vya habari na waandishi wa habari wakiwa nje ya nchi wakiripoti matukio hasi tofauti na fursa zilizoko Tanzania na zinazopatikana nje.

Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha waandishi wa habari walioko nje ya nchi wanatangaza nchi yetu na fursa zilizopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imeweka msisitizo zaidi katika dhana ya diplomasia ya uchumi, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kuelezea fursa mbalimbali zinazopatikana nje ya nchi kupitia makongamano na vyombo vya habari, lakini pia na mitandao ya kijamii. Pia katika maonesho mbalimbali Wizara imekuwa ikitoa hiyo elimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Wizara yetu au Serikali inachukua mkakati gani kwa ujumla kwa waandishi wa habari ambao wanapotosha hizi habari nje ya nchi. Kwanza ni kwamba balozi zetu zimekuwa very active mara zinapotokea taarifa hasi, basi mara moja wanashirikiana na vyombo vya habari vya nje katika kuhakikisha kwamba habari zinazotolewa ni za uhakika, ahsante sana.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niongezee kidogo kwamba kuhusu mkakati wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu jana wakati Kamati yetu ikitoa taarifa na kama ilivyoelekezwa pia na Kamati, tulieleza kwamba tunaandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kutekeleza diplomasia ya uchumi na katika mpango huo, moja ya kitu kitakachojumuishwa ni mpango wa kutoa elimu kwa umma. Kwa hiyo, tutatumia mbinu mbalimbali kuboresha utoaji wa elimu ya umma pamoja na yale tunayoyafanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ni kuhusu tunafanya nini kushirikisha hivi vyombo vinavyotoa elimu hasi kuhusu Tanzania. Tunalifahamu hilo pamoja na hayo yanayofanyika, tayari tumeanza mazungumzo na vile vyombo vya nje hususani vile vinavyoongea Kiswahili kwa sababu sasa hivi tunakuza pia Kiswahili kuwaomba pia wadau wetu.

Mheshimiwa Spika, juzi nimekutana na Idhaa ya Kiswahili ya Uturuki ambao wamefungua idhaa ya kiswahili na moja ya kitu nilichowaomba na mtaona ni kwamba sasa watusaidie kutoa elimu chanya na taarifa chanya kuhusu Taifa letu hususan vivutio tulivyonavyo, fursa tulizonazo na waachane na kutoa elimu hasi. Wao wamekubali kwamba watatusaidia kushirikiana na idhaa nyingine, ahsante. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Kawe Kata ya Wazo, mitaa ya Nyakasangwe, Mivumoni na Salala, miundombinu ya maji kwa maana matenki tayari imeshajengwa. Ni lini sasa Serikali itahakikisha maji yanatoka katika mitaa hiyo ili kuwaletea wananchi wale nafuu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maeneo yote ya Kawe miradi iko mwishoni. Hata jana tu nimemwona Mkuu wa Mkoa akiwa na watendaji wetu wa DAWASA wakifuatilia kule, hivyo miradi iko mwishoni. Muda siyo mrefu maji ya kutosha safi na salama yataanza kutoka.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi wa afya nchi nzima ni 336,453; waliopo ni 114,582 sawa na asilimia 34 tu na pungufu ni 221,946 upungufu huu ni mkubwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuajiri watumishi hawa ili kunusuru afya za Watanzania?

Swali la pili, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza database ili kutambua wahudumu wote wanaojitolea ili wakati wa ajira waweze kupewa kipaumbele? Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Swali la pili: Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza database ili kutambua wahudumu wote wanaojitolea ili wakati wa ajira waweze kupewa kipaumbele? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni upungufu. Ni kweli tuna upungufu kwenye Sekta ya Afya na unachangiwa na mambo mengi. Wakati mwingine katika Hospitali ya Wilaya tumeweka idadi ya watumishi, Hospitali ya Mkoa tumeweka idadi ya watumishi, na Hospitali ya Kanda hivyo hivyo. Pamoja na hivyo, utakuta kwa mfano Hospitali ya Mawenzi wana watumishi 400 lakini pale Mwananyamala hospitali, wanaona wagonjwa 500 kwa siku; ukienda pale Mnazi Mmoja Dar es Salaam ambayo ni ya Wilaya wana watumishi 170 wanaona wagonjwa 700 mpaka 800 kwa siku. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye eneo la kuangalia ni watu wangapi hospitali husika inaona wagonjwa kwa siku na tukaweza kupeleka watumishi kulingana na mzigo ulioko kwenye eneo, hata huo upungufu anaousema Mheshimiwa Mbunge haupo.

Mheshimiwa Spika, tulikwenda Wilaya moja kule Shinyanga wakasema wana upungufu katika Hospitali ya Wilaya. Nilipowauliza, wakasema tuko 37. Ni kweli ukiwasikia Hospitali ya Wilaya wako 37, utasema kwamba ni wachache sana, lakini nikawauliza mnaona wagonjwa wangapi kwa siku? Wakaniambia tunaona wagonjwa 13. Unaweza ukaona kwamba kuna umuhimu wa kufikiria. Hilo moja, ni kwamba linatakiwa lifanyiwe kazi, kuangalia hali halisi na kupeleka watumishi kulingana na mzigo.

Mheshimiwa Spika, la pili, lile la kuweka database, ndicho nilichokisema hapa, tutashirikiana na wenzetu wa Utumishi kuona namna nzuri tutakayofanya na kuweka database kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuwatambua wakati wa ajira wapewe kipaumbele. Hilo ni wazo zuri sana, tunalichukua na tunakupongeza Mheshimiwa Mbunge.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Mwenge kuelekea Bagamoyo imekuwa na msongamano mkubwa na kusababisha Shughuli za kiuchumi Mkoa wa Dar es Salaam kusimama. Ni lini sasa Serikali itajenga barabara ya Mabwepande kuelekea Mbezi Jimbo la kibamba ili kuweza kupunguza foleni hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara ya kutoka Mwenge kwenda Mabwepande ni BRT number Four ambayo iko katika hatua za manunuzi, lakini barabara aliyoitaja itakuwa ni moja ya barabara za kupunguza msongamano lakini pia kwenda kwenye hii stendi mpya na iko kwenye mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali la nyongeza. Kumekuwa na hasara kubwa kwa wakulima wa migomba kwa sababu ya ugonjwa wa mnyauko. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa huu ili wakulima wa migomba wapate faida? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mkakati wa Serikali ndiyo pamoja na hizi tafiti ambazo zinafanyika za kuja na aina mpya ya mbegu ambayo itakuwa na uwezo wa kukabiliana na magonjwa mnyauko na huo ndiyo mkakati sahihi kwa sasa, kwa hiyo tuwahakikishie tu wananchi kwamba Serikali ipo kazini ili kuondoa hii adha ya wakulima ususani katika zao la mgomba.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na popo katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuna tatizo kubwa la kunguru ambao wamekuwa wakitapakaa kila mahali, wanajerui watoto; na hasa katika fukwe, ambako wamekithiri, na hivyo kuharibu utalii wetu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanadhibiti kunguru hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la nyongezala la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na tatizo la kunguru katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali kupitia Wizara imekuwa ikifanya jitihada ya kuja na mipango mbalimbali ya kuweza kuondokana na tatizo hili. Changamoto tunayoiona ni kwamba wenzetu kwenye maeneo ya halmashauri zetu wameliacha jambo hili kuwa ni jambo la Wizara peke yake. Tunawaomba sana wadau wenzetu katika maeneo ya halmashauri, kwa kutumia teknolojia iliyoandaliwa na Wizara tushirikiane ili kupambana na tatizo hilo. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga soko la kisasa la samaki katika Kata ya Mbweni ili wananchi waweze kujipatia kipato lakini kuiletea Serikali mapato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mheshimiwa Mbunge ameeleza jambo jema kuhusu soko la kisasa la uvuvi katika Kata ya Mbweni ambalo lipo katika sehemu ya mipango yetu kama Wizara, kikubwa tu sasa hivi ni kwamba tunatafuta fedha na tukishapata fedha katika maeneo yote ya kimkakati tutajenga kama ambavyo tunataka kutekeleza. Ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini na maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fire hydrants zinazotakiwa nchini ni 285,000 na zilizopo ni 2,348 sawa na asilimia 8.2 tu;

Je, Serikali haioni haja ya kujenga miundombinu hiyo ili kuzuia majanga makubwa ya moto yanatokea ili kuzuia pia Serikali kupata hasara na wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto hii inatokea katika miji na majiji makubwa;

Je, Serikali haiona sasa kuna haja ya kuweka miundombinu hiyo katika miji na majiji makubwa, kwenye masoko na shule ili pia kuzuia majanga hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba fire hydrants zilizopo ni chache hazilingani na zile zinazohitajika, na ndiyo maana Jeshi letu la Zimamoto na Uokozi linawasiliana na mamlaka zote za ujenzi za miji pamoja na mamlaka za maji kila wanapotekeleza miradi hiyo wazingatie uwekeji wa hizi fire hydrants.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili ninakubaliana naye, kwamba miji mikubwa ndiyo iko kwenye changamoto kubwa zaidi ya kukumbana na majanga ya moto na kwa msingi huo mkazo zaidi utawekezwa kwenye miji mikubwa kadiri tunavyoendelea kuimarisha huduma za fire na uokozi.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa balozi zetu nje ya nchi inachukua gharama kubwa ukilinganisha na hapa kwetu, lakini kikubwa kabisa bajeti ambayo tunaiweka kila mwaka haiwezi kuakisi ujenzi wa majengo hayo kutokana na kwamba itachukua muda mrefu na hatuwezi kuona tija: Serikali haioni sasa ni bora kuchukua mkopo katika taasisi za fedha nje au ndani ya nchi ili kujenga majengo hayo kwa mara moja ili kuleta tija? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ujenzi wa balozi zetu unaleta tija kwenye Sekta ya Utalii, Biashara na Uwekezaji na huweza kuiletea Serikali pato la Taifa: Serikali haioni sasa ni bora kuainisha balozi za kimkakati ambazo zitaanza kujengwa mara moja ili kuletea Serikali yetu tija? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuanza na suala la kwanza, haya pia ni maelekezo mahususi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya Benki ya CRDB mwaka 2022 kwa jinsi ni namna gani itumie taasisi binafsi na taasisi za fedha katika kuendeleza majengo yetu ubalozini. Hivi sasa tayari Serikali imeanza mazungumzo na Benki za CRDB na NMB pia na mifuko ya hifadhi ya jamii kama vile PSSSF, WCF na ICCF ili kuona vipi tunaweza kushirikiana katika suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili la kuainisha balozi za kimkakati. Huu ni ushauri mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge na tayari Serikali imeshaanza kutekeleza mkakati huo na kwa kuanzia tutaanzia na Ubalozi wa Nairobi, New York, Washington pamoja na Ubalozi wetu wa London, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na ucheleweshaji wa mbegu kwa wakulima na hivyo wakulima kukosa tija kwenye kilimo chao. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mbegu zinapelekwa kwa wakati ili waweze kulima kwa tija? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, changamoto kubwa ya upatikanji wa mbegu kwa wakati ilikuwa ni kwamba mzalishaji mkubwa wa mbegu ASA alikuwa na yeye alikuwa anategemea mvua kama ambavyo mkulima kuzalisha mbegu. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan tumetenga fedha kuhakikisha kwamba tunaanza kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yetu ya mbegu ili tuwe tuna uwezo wa kuzalisha mbegu mwaka mzima na wakulima wazipate kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia katika mashamba yetu makubwa nane ya awali tumeweka miundombinu center na lateral pivot kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunamwagilia mashamba haya na mbegu zinapatikana kwa mwaka mzima na zitawafikia wakulima kwa wakati na msimu ukianza watakuwa nazo.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Manunuzi ya Umma inaelekeza asilimia 30 kwenda kwenye makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini Sheria hii inaonekana kuto tekelezeka.

Je, ni lini Serikali itatilia mkazo Sheria hii ili iweze kuleta tija kwa jamii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Njau kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ipo na inatekelezwa. Tuna toa maelekezo kwa maafisa masuhuli wote ambao hawajatekeleza hili watuletee ripoti na tuwaambie kabisa watekeleze sheria hii kama ilivyowekwa.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna sheria inayo guide mama wajawazito na wagonjwa kwaajili ya kutibiwa. Je, nini upande wa pili wa Serikali kuhusiana na vituo vya afya ambavyo hakuna jengo la mama na mtoto mfano Kata ya Wazo ambapo kunatokea vifo vingi kutokana na kukosekana kwa jengo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge ni shahidi hapa kwamba kwa mwaka huu katika historia ya Tanzania kuliko wakati wote fedha nyingi zimepelekwa kwenye eneo la afya naniukweli kwamba hatutaweza kumaliza vyote kwa wakati mmoja lakini kwakweli hoja yako Mheshimiwa Mbunge niyamsingi, kimsingi basi shirikiana na halmashauri yako na hata leo tuandike vizuri tuhakikishe tunashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI iingie kwenye utaratibu na kama haijawahi kuingia kwenye utaratibu tuanze sasa mchakato litekelezeke lakini kwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan wala usipate wasiwasi na hilo.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Katika Mkoa wa Morogoro eneo la Chita kuna hekari 12,000 zenye miundombinu ya umwagiliaji ambapo sasa hivi zinamilikiwa na JKT, lakini kwa uwezo wao wameweza kulima ekari 2,500. Je, ni lini Serikali itawekeza nguvu yake pale ili kuweza kusaidia usalama wa chakula na kuongeza pato la Taifa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Fungu Namba 05 la Tume ya Umwagiliaji katika Randama ukiangalia Jedwali la Nne limeainisha moja kati ya miradi ambayo tutakwenda kuitekeleza katika mwaka ujao wa fedha ni mradi wa JKT – Chita. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge mradi upo katika mpango na utatekelezwa katika bajeti inayokuja.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kero kubwa ya msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani imekithiri. Je, Serikali inaonaje ikaleta utaratibu wa vifungo vya nje kwa makosa madogo madogo ili kupunguza msongamano huo? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria mwaka huu, tulisema moja kati ya vipaumbele ni kwenda kuangalia upya, kuufumua na kuupanga upya mfumo wa jinai hapa nchini. Katika mpango huo moja kati ya jambo ni hili kuangalia adhabu mbadala ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Miongoni mwa kanuni ambazo zinalalamikwa na wavuvi ni ile kanuni ambayo inamlazimisha mvuvi kutokuvua chini ya mita 50 kwenda chini.

Je, wakati Serikali inaendelea na mikakati ya kurekebisha kanuni haioni haja ya kupeleka mitungi ya oxygen kwa wavuvi wadogo wadogo ili kuweza kuwaokoa na athari ya kuzama maji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Njau, kumradhi Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wavuvi wapo wanaofanya shughuli za uzamiaji kwa ajili ya kuweza kupata rasilimali na hii ni katika zile kanuni tunazokwenda kuzifanyia kazi ya maboresho; na baadhi yao wanataka watumie zaidi ya mitungi 10, sisi tunadhani tunao uwezo wa kuruhusu lakini kwa uchache kwa sababu tunaamini matumizi ya mitungi mingi ni kinyume cha uhalisia wa kwenda kile anachokikusudia isipokuwa tu kama ana lengo lingine ambalo kinyume na uvuvi. Kwa hivyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, wawe na subira ni katika kama jibu la msingi la mwanzo kwamba ni sehemu ya majibu tukakayoyatoa kwenye marekebisho ya Kanuni zetu. Ahsante.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka miwili sasa bandari ya Kalema ipo tayari lakini hakuna tija iliyopatikana licha ya Serikali kuwekeza zaidi ya bilioni 47. Hii inaleta shida kwa sababu fedha za wananchi zimekaa pale na hakuna pesa inayopatikana kwa sababu tu ya ubovu wa miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali ni lini exactly barabara hii ya kutokea Kigwira kuelekea Karema, itatengenezwa ili kuokoa fedha za walipakodi? (Makofi)

Swali la pili, tuna barabara za kimikakati kuzunguka nchi za SADC. Ni lini, Serikali itaainisha barabara hizi, ili kuweza kuweka soko pamoja lakini kuokoa fedha zinazopotea na kikubwa zaidi kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na la Taifa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi barabara ambayo Mheshimiwa Felista ameitaja ya Kigwira kwenda Karema, tumeshasaini mkataba, kwa hiyo, baada ya kusaini ina maana Mkandarasi anaanza ku-mobilize mitambo ili ujenzi wa kiwango cha lami uweze kuanza. Vilevile Serikali ya Awamu ya Sita hatujaishia hapo, dhamira ya Serikali Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya SADC pia kuna African Union 2063 (The Africa We Want).

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha position ya Tanzania katika mikakati ya kiuchumi kwenye jumuiya hizi nilizozitaja, EAC, SADC na AU - Vision ya 2063 (The Africa we want). Tanzania tunataka tujipange tuwe vinara wa kiuchumi. Kwa hiyo, ujenzi wa barabara hizi na nchi za jirani siyo kwamba tunajenga tu kwa sababu tunawapenda sana, ndiyo ni mahusiano mazuri pia kimkakati lazima tuji-position ili kuweza kujenga uchumi imara, kutengeneza ajira kwa wananchi wetu na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo nikuhakikishie mikakati yote tunayo na tunaendelea kuitekeleza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya utafiti gani ili kujua makabila yaliyoko nchini, kuweza kuyasaidia na kuyaendeleza kuwa kivutio ili kuweza kuiingiza Serikali Pato la Taifa na watalii zaidi ya Wamasai? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, mpaka sasa tafiti 286 zimeshafanyika, tunachofanya ni mwendelezo wa tafiti hizo na kuona namna ambavyo tunaweza kutumia ufahamu tulioupata kupitia tafiti hizo ili kuyaenzi na kuhifadhi tamaduni za makabila mbalimbali zaidi ya Wamasai hapa nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka miwili sasa bandari ya Kalema ipo tayari lakini hakuna tija iliyopatikana licha ya Serikali kuwekeza zaidi ya bilioni 47. Hii inaleta shida kwa sababu fedha za wananchi zimekaa pale na hakuna pesa inayopatikana kwa sababu tu ya ubovu wa miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali ni lini exactly barabara hii ya kutokea Kigwira kuelekea Karema, itatengenezwa ili kuokoa fedha za walipakodi? (Makofi)

Swali la pili, tuna barabara za kimikakati kuzunguka nchi za SADC. Ni lini, Serikali itaainisha barabara hizi, ili kuweza kuweka soko pamoja lakini kuokoa fedha zinazopotea na kikubwa zaidi kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na la Taifa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi barabara ambayo Mheshimiwa Felista ameitaja ya Kigwira kwenda Karema, tumeshasaini mkataba, kwa hiyo, baada ya kusaini ina maana Mkandarasi anaanza ku-mobilize mitambo ili ujenzi wa kiwango cha lami uweze kuanza. Vilevile Serikali ya Awamu ya Sita hatujaishia hapo, dhamira ya Serikali Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya SADC pia kuna African Union 2063 (The Africa We Want).

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha position ya Tanzania katika mikakati ya kiuchumi kwenye jumuiya hizi nilizozitaja, EAC, SADC na AU - Vision ya 2063 (The Africa we want). Tanzania tunataka tujipange tuwe vinara wa kiuchumi. Kwa hiyo, ujenzi wa barabara hizi na nchi za jirani siyo kwamba tunajenga tu kwa sababu tunawapenda sana, ndiyo ni mahusiano mazuri pia kimkakati lazima tuji-position ili kuweza kujenga uchumi imara, kutengeneza ajira kwa wananchi wetu na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo nikuhakikishie mikakati yote tunayo na tunaendelea kuitekeleza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kilimo cha mbogamboga pembezoni mwa mito na mifereji inayotiririsha maji machafu kutoka viwandani katika majiji makubwa hasa Dar es Salaam.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi hawa ili waweze kukiuka athari ambazo zinaweza kutokea kiafya?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanatoa elimu kwa njia ya nadharia na vitendo. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa mwaka huu wametoa elimu mara ngapi na maeneo gani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ni kweli nikianza na swali la pili, takwimu kwa hapa siwezi kuwa nazo niwe mkweli nitalifanyia kazi.

NAIBU SPIKA: Jibu la kwanza.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo suala la pili, ni kwamba tutaendelea kutoa elimu. Vilevile, katika maeneo ambayo yana athari, kuna kanuni ziko katika ngazi za halmashauri ambazo zinapaswa kusimamiwa ili kuondoa kero hii ambayo Mheshimiwa Mbunge umeiainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu kwamba, sisi kama Wizara ya Kilimo tutaendelea kuelimisha wananchi wetu na vile vile tutazihamasisha halmashauri ziweze kutekeleza sheria na kanuni za halmashauri kwenye kusimamia yale maeneo ambayo yako katika mito na vile viwanda vinavyotiririsha majitaka katika maeneo ya wananchi, ahsante sana.