Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Felista Deogratius Njau (10 total)

MHE. FELISTA D. NJAU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa hati kwa Wananchi wa Meko na Basihaya baada ya maeneo hayo kupimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Meko liko katika Kata ya Kunduchi Manispaa ya Kinondoni awali eneo hilo lilitengwa kwaajili ya machimbo ya kokoto. Baada ya machimbo kufungwa Manispaa ilidhamiria kupima viwanja kwa ajili ya Kituo cha Biashara. Hata hivyo upimaji haukufanyika kutokana na eneo hilo kuwa limevamiwa na wananchi. Mwaka 2017 Manispaa ya Kinondoni ilimaliza mgogoro na wavamizi kwa kuruhusu wananchi wapimiwe viwanja katika eneo hilo kupitia mpango wa urasimishaji wa makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ilikubalika kuwa wananchi watapimiwa viwanja katika maeneo yale waliyoyaendeleza na maeneo yaliyo wazi yatapangwa na kupimwa viwanja vya matumizi ya umma. Kazi ya upimaji ilianza tarehe Mosi Januari, 2019 na kukamilika tarehe 20 Januari, 2021 na jumla ya viwanja 840 vimepimwa na hatua ya umilikishaji zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Basihaya lipo katika Kata ya Bunju, Mtaa wa Basihaya ambako kuna Vitongoji vya Chasimba, Chatembo, Chachui ambavyo kwa sehemu kubwa uendelezaji wake umefanywa ndani ya ardhi inayomilikiwa na Kiwanda cha Saruji cha Wazo. Wamiliki wa Kiwanda cha Wazo walipeleka malalamiko Mahakamani baada ya kuona eneo lao limevamiwa. Mahakama kupitia Shauri Na. 129 la mwaka 2008 kati ya Haruna Mpangao na wenzake 932 dhidi ya Tanzania Portland Cement ilitoa uamuzi kuwa wananchi waliovamia katika eneo hilo waondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ardhi ilichukua jitihada za kufanya majadiliano na mwekezaji ili kuangalia namna bora ya kutatua mgogoro huo ambapo iliamua wananchi walioendeleza katika maeneo hayo wasiondolewe bali walipe gharama ambazo atapewa mwekezaji ili akanunue eneo lingine kwa ajili ya kupata malighafi za kutengeneza saruji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshawapimia viwanja waendelezaji wote katika eneo hilo ambapo jumla ya viwanja 4,000 vimepatikana na kila mwendelezaji atatakiwa kulipia gharama zitakazotumika kumlipa mmiliki wa kiwanda. Wizara inaendelea kufanya majadiliano na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo kuhusu gharama na fidia ya eneo lililoendelezwa na wananchi.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la mafuriko katika maeneo ya Mbweni Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya mafuriko katika maeneo ya Mbweni Teta, Bunju Basihaya, Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni katika Jimbo la kawe. Serikali kupitia Mradi wa kuboresha Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP) imetenga shilingi bilioni 8.4 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua wenye urefu wa kilomita 8.89 katika Kata ya Mbweni. Awamu ya pili ya mradi huu itajumuisha mifereji ya maji ya mvua katika maeneo ya Kunduchi, Nyamachabes, Ununio na Mikocheni.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji ya mvua ili kuondoa kero ya mafuriko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam ikiwemo Jimbo la Kawe.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kairuki hadi Mikocheni Shoppers ambayo hadi sasa imejengwa kipande kidogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratias Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kairuki hadi Mikocheni Shoppers inayojulikana kwa jina la Barabara ya Warioba - Chakwu yenye urefu wa kilomita 1.73 ilijengwa kwa kiwango cha lami kipande cha kilometa 1.13 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.017 katika mwaka wa fedha 2014/2015. Hivyo, kipande chenye urefu wa kilomita 0.6 hakikujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii yote inahitaji matengenezo makubwa kikiwemo kipande cha kilometa 0.6 ambacho hakina lami. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepanga kufanya tathmini ya barabara hii na Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kujenga na kuifanyia matengenezo barabara hii kwa mujibu wa matokeo ya tathmini.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha kifedha JKT ili iweze kutekeleza kwa ufanisi mradi mkubwa wa kilimo cha mpunga Chita JKT – Morogoro na Shamba la Mngeta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kifedha kila mwaka ili liweze kutekeleza kwa ufanisi shughuli zake, ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo, ikiwemo mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika shamba la mpunga lililopo Chita mkoani Morogoro na Shamba la Mngeta. Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ilitoa Shilingi 4,000,000,000 ambazo zimetumika kununulia zana na vifaa vya kilimo kwa ajili ya shamba la Chita. Aidha, katika Mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi 4,000,000,000 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya kumalizia awamu ya kwanza ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa ekari 2,500 huko Chita.

Mheshimiwa Spika, Katika kuliendeleza shamba la Mngeta lenye ekari 12,000, kiasi cha Shilingi 11.5 zinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa zana, matengenezo na maboresho ya miundombinu ya uzalishaji, na gharama za uendeshaji. Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na Wizara ya kilimo ili kuona uwezekano wa shamba hili la Mngeta, kuwa sehemu ya mpango wa skimu za umwagiliaji. Taratibu za ndani zinaendelea ili kuwasilisha maombi ya fedha Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri Maafisa Habari katika Balozi zetu ili kuutangaza nchi na vivutio mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Maofisa wanaopelekwa Ubalozini, moja ya majukumu yao ya msingi ni kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imeweka msisitizo katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Miongoni mwa majukumu ya kila Ofisa na kila Ubalozi ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii wetu, kubidhaisha Kiswahili, kuvutia wawekezaji na kutafuta fursa za masoko kwa bidhaa zetu. Aidha, Wizara ina utaratibu wa kuwajengea Watumishi uwezo kupitia mafunzo ili waweze kufanya kazi zaidi ya moja ikiwemo kuwa na uwezo wa kutoa habari muhimu kwa wadau.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuainisha nchi ambazo fursa za biashara na uwekezaji zinaweza kuiletea nchi yetu mapato na kupandisha pato la Taifa zinapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza dhana ya diplomasia ya uchumi ambayo pamoja na mambo mengine ni kukuza biashara na uwekezaji toka nchi mbalimbali. Dhana hii inahusisha Sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi zetu imeendelea kutangaza fursa za kibiashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa letu. Ili kuzitumia fursa hizi kwa tija zaidi, Wizara imeendelea na maandalizi ya Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Mpango huo utajumuisha sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya kisekta yatakayochangia katika kukuza uchumi na Pato la Taifa. Mpango huu utajumuisha pia sekta binafsi na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba, 2023.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaajiri Wataalam wanaojitolea kwa muda mrefu kufanya kazi katika Hospitali mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwenye hospitali zetu kumekuwa na watumishi wanaojitolea. Wizara imetoa Mwongozo wa kuwalipa nusu mshahara kwa mapato ya ndani. Hata hivyo hospitali zetu za Mikoa, Kanda na Taifa zimeweza kuwalipa hadi asilimia 40 ya watumishi wote wanaojitolea mshahara kamili kwa kutumia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, Wizara itashirikiana na Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuona namna bora ya kuwapa kipaumbele kwenye ajira watumishi ambao wamekuwa wakijitolea kwenye vituo vya huduma za Afya kuliko walioko nje wakisubiri ajira.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SALOME W. MAKAMBA K.n.y. MHE. FELISTA D. NJAU
aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika magereza yetu upo msongamano mkubwa unaosabishwa na idadi kubwa ya mahabusu kuliko wafungwa hususani katika magereza ya mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, ni pamoja na kuhimiza matumizi ya vifungo vya nje kama vile Parole, Extra Mural Labour, huduma kwa jamii na huduma za uangalizi kwa wafungwa wenye viashiria vya kujirekebisha, msamaha unaotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maadhimisho ya sherehe za Muungano wa Tanzania na Uhuru wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkakati wa Serikali ni kuendelea kuelimisha na kuhimiza wananchi waishi kwa maadili bora na waepuke kuvunja sheria ili waepuke kufikishwa mahakamani na kufungwa. Aidha, Serikali itaendeleza mpango wa kujenga magereza mapya na kufanya upanuzi kwa magereza ya zamani ili kuongeza nafasi ya kuwahifadhi wafungwa na mahabusu kulingana na mahitaji na kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kutambua fire hydrants nchini na kuziwekea alama ili kusaidia wakati wa majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshirikiana na Mamlaka za Miji na Maji kukagua na kutambua fire hydrants 2,348 ambazo zipo Nchi nzima. Jeshi limeanza kutekeleza utaratibu maalum wa kimataifa wa utambuzi wa fire hydrants ambao ni kuziwekea alama ya FH. Jeshi pia linaziweka fire hydrants hizo katika mfumo wa utambuzi Kijiografia (Geographical Information System – GIS) na kuzijengea mifuniko migumu itakayozuia uharibifu wake. Aidha, Jeshi linawasiliana na mamlaka zinazohusika na ujenzi wa barabara na uendelezaji wa miji kudhibiti ujenzi holela wa makazi na upanuzi wa barabara za mitaa unaohusisha kuzifukia fire hydrants. Lengo ni kuzitunza fire hydrants zilizopo ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji wakati wa kutelekeza majukumu ya kuzima moto yanapotokea majanga, nakushukuru.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha fedha za ujenzi wa Balozi za Tanzania zinapelekwa ili kupunguza gharama kubwa ya kodi?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inatekeleza mpango mkakati wa miaka 15 wa kujenga, kununua na kukarabati majengo balozini kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 hadi 2031/2032.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Mwaka 2017/2018 na 2022/2023 Serikali imeweza kupeleka kiasi cha shilingi 10,357,785,067kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo katika Balozi zetu nje ya nchi ili kuyaweka katika hali nzuri na hivyo kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kupanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imekamilisha uchambuzi na utekelezaji wa mpango huo na kuandaa mkakati wa utekelezaji ambapo jumla ya miradi 14 ya kipaumbele imeainishwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano cha mwaka 2022/2023 hadi 2026/2027 kupitia fedha za Serikali pamoja na ubia na sekta binafsi. Aidha, Serikali itaendelea kupeleka fedha za ujenzi na ukarabati wa majengo katika Balozi zetu kwa kadri hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu, ahsante sana.