Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Felista Deogratius Njau (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Moja kwa moja niende kwa upande wa TAMISEMI katika kipengele hiki hiki cha TARURA. TARURA imekuwa kama kibogoyo asiyekuwa na meno, lakini analazimishwa kula mifupa. Nasema maneno haya kwa sababu TARURA hawana shida. TARURA siyo tatizo, tatizo ni bajeti wanayopewa. TARURA wapo tayari kabisa kufanya kazi, lakini fikiria bajeti nzima ya barabara, TARURA wanapewa asilimia 30 badala ya kupewa asilimia 40 mpaka 50. Mimi napendekeza TARURA waongezewe fedha kwa sababu wanachezea nafasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimsikia Mheshimiwa Waziri akisoma hapa, anasema TARURA kwenye kilometa za mraba, wako 144,000. Sijui kama ni kweli, lakini pia ina wingi sana wa barabara. Kwa hiyo, TARURA watengewe fedha za kutosha ili kilio hiki cha Watanzania basi waweze kufutwa machozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda Dar es Salaam katika jiji ambalo ni kubwa, ambalo ni kitovu cha biashara na ni muunganiko wa Mikoa yote ya Tanzania. Dar es Salaam kumekuwa na msiba na kilio katika majimbo yote ya huko kuhusiana na barabara hasa zile za mitaa na barabara kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara za Dar es Salaam nyingi ambazo hazipitiki ni suluhisho la foleni za Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa mfano, Barabara inayotokea Kairuki kupitia Mikocheni, barabara ile inayopitia shoppers ilikuwa suluhisho kabisa la foleni za Dar es Salaam. Mtu anayesafiri Dar es Salaam kutoka Bunju kuelekea Posta ambapo ndipo kwenye Ofisi za Serikali, anachukua masaa matatu kama anatoka hapa kwenda Morogoro.

Mheshimiwa Spika, mtu huyu anafika ofisini anasinzia, akili imechoka, uwezo wake wa kufikiri umeshapotea. Tunaanza kusema watu wetu hawa-perform vizuri, hawa- perform kwa sababu hawapo active, wakifika pale kama mtu ametoka kulala kwenye msiba. Barabara nyingi ni kilio. Kuna barabara moja ipo Ununio; mwaka 2020, baada ya mvua hizi kunyesha nyumba 10, yaani familia 10 zilihama kabisa zikaondoka wakaenda TARURA wakaambiwa chimbeni mfereji. Hakuna miundombinu pale ya mfereji kuelekeza maji baharini. Wale watu wanapeleka wapi haya maji? Familia 10 zipo juu ya nyumba. Sasa hivi wanapiga simu wanasema Mheshimiwa Njau, tunaondoka sasa, wananiaga niwapeleke wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kitu kimoja. Barabara ni kwikwi Tanzania nzima. Nikisema za vijijini, Mikoa inayohusiana na Kilimo, inayohusiana na biashara na mazao, hakika tunadumaza pato la Taifa. Kwa sababu kama vijijini barabara ni mbovu, hawawezi kwenda kwenye Wilaya, hawawezi kwenda kwenye Mikoa kupeleka mazao yao, tunasema hatupati mapato. Barabara ni suluhisho la biashara na barabara ni suluhisho la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wengi wanaosimama hapa wanalia juu ya bajeti sehemu fulani. Twende tukatoe mzizi wa fitina kwenye miundombinu. Tukitoa hapa kwenye barabara, tunaweza kwenda vizuri. Pia niseme, hata wakijenga barabara hizi, kama Serikali hatujaweka nguvu kubwa katika kujenga mifereji, ni kazi bure. Barabara zinachongwa leo, baada ya siku tatu maji yanajaa na barabara zinakuwa vile vile. Kwa hiyo, lazima tuweke miundombinu ya mifereji. Kwa mfano, pale Mikocheni Shoppers, kuna adha ya mafuriko; pale ni mifereji tu ndiyo mchawi.

Mheshimiwa Spika, ikipatikana mifereji thabiti, barabara zikajengwa vizuri, barabara hizi zitakuwa imara. Barabara zinaharibika kwa sababu hakuna mifereji. Tuna wataalam wetu, wakandarasi; kuna msiba na kilio cha Makandarasi. Kwenye ripoti ya CAG ameainisha zaidi ya shilingi bilioni 81.52 hazijalipwa kwa Makandarasi, tunategemea kupata matokeo chanya kwa mtu ambaye anakudai na unampa kazi mpya! Hatuwezi kupata matokeo chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukalipe madeni haya ya Makandarasi ili tuweze kuanza nao vizuri na kumaliza vizuri. TARURA hawa hawa ambao wanatengewa asilimia 30, wanaidai Serikali shilingi 125,854,000/=. Hivi kweli hawa ambao fedha zao hazitoshi, bado wanadai; tukawalipe TARURA Ninaongea haya kwa sababu tuna barabara za kimkakati; wakati tunatenga bajeti, hebu tuweke kipaumbele kwenye barabara za kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kawe tuna barabara inatoka Mabwepande kuelekea Kibamba - Mbezi, ile barabara ni ya kimkakati kabisa kwenda kupunguza foleni, lakini barabara ile imekaa kama haina mwenyewe. Kuna barabara zimejengwa nusu; barabara ya Shoppers imejengwa kwa lami nusu, mwaka wa nne leo watu wanachungulia na kurudi, iko nusu. Twendeni tukamalize miradi baada ya kuianza, ndipo tuweke miradi mipya.

Mheshimiwa Spika, nashauri wakati tunaanza kupanga bajeti, tuangalie miaka ya nyuma: Je, tulikuwa tuna kiporo? Siyo kila siku tunaibua miradi mipya wakati ya zamani imesimama. Tutakuwa kila siku tunaelemewa na tunaonekana hatufanyi kazi, lakini watu wanachapa kazi.

Mheshimiwa Spika, ninakwenda kwenye ulipwaji wa motisha na madeni. Viongozi kama alivyosema msemaji aliyepita, Madiwani hawana thamani. Kwa sababu hawa ndio wanaosimamia mapato yetu, twendeni tukawape motisha, tusimame nao, tuwasemee. Madiwani ukikaa nao anakwambia posho yangu; ananung’unik! Tunakutana na Madiwani, anasubiri apate huruma ya Mkurugenzi wakati yeye ndiye anatakiwa kumwajibisha Mkurugenzi. Hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende tukapange upya. Nina imani na Serikali hii, sasa nina imani Mheshimiwa Mama Samia amesimama na viongozi wake, siwezi kuwakosoa kwa sababu ndiyo wameanza, nawaona wanaweza kufanya mabadiliko makubwa na nchi hii ikaenda kuona maisha mengine tofauti.

Mheshimiwa Spika, nasemea Jiji la Dar es Salaam kwa sababu mwisho wa siku Jiji la Dar es Salaam ndiyo jiji ambalo limekusanya mapato ya ndani makubwa kwa asilimia 104, limevuka asilimia 100. Kama Jiji hili ndivyo lilivyo, basi turudishe mapato kule chini, kwa maana ya miundimbinu. Miundombinu ikipatikana, wafanyabiashara watafanya biashara zao na wafanyakazi watafanya kazi vizuri wala hutasikia minong’ono.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ambayo kimsingi inagusa jamii kubwa ya Watanzania.

Kwanza kabisa kabla ya kwenda mbele ni lazima tuangalie huku nyuma tulifanya vizuri kiasi gani au vibaya kiasi gani ili tuweze kujisahihisha. Nikisema hivyo ninakwenda moja kwa moja kwenye mpango wa utekelezaji wa bajeti wa miaka ya fedha ya mwaka 2016/2017 ambayo bajeti ya Wizara hii ilikuwa ni asilimia 44; mwaka 2017/2018 ilikuwa ni asilimia 9.51 mwaka 2018/2019 ilikuwa ni asilimia 6.5; ukijumlisha kwa wastani wake miaka hii minne mfululizo unakuja kupata asilimia 20 tu ya bajeti katika sekta muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwendaje mbele katika kauli hii ya nchi ya viwanda huku tukiweka asilimia 20 miaka minne mfululizo. Hatuwezi kwenda kwa sababu mwisho wa siku mipango hii ni lazima itekelezwe, pesa ni lazima ziwepo ili maendeleo yawepo. Kwa tathmini hii ya mpango target yetu ni nini? Mpango wa Pili tulikwama wapi leo tunakwendaje mbele? N lazima tu-refer tulikotoka ili tuangalie tulikwama wapi twenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa sababu hapo nyuma wakati wa kauli mbiu ya nchi yetu ya viwanda ilivyopamba moto, kuna Waziri alisimama kwenye matamko yake akasema tutakwenda kujenga viwanda 100 kila mkoa; alikuwa ni Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo, akasema tutakwenda kujenga viwanda, hizi kauli hizi zisiwe mapambio zikawaponza Watanzania wakatuona huku tunapiga mapambio tu, haiwezekani. Hizi kauli ziende na vitendo, na alivyosema hivi nilikumbuka Kiwanda cha Tanganyika Packers nikasema kiwanda hiki kikifufuliwa wananchi wa Jimbo la Kawe na Dar es Salaam wanakwenda kupata ajira nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikasema kiwanda hiki kimebeba jina la Kawe maana ya Kawe ni njia ya kupita ngo’mbe (cow way) ni Kawe nikasema kiwanda hiki kikifufuliwa tutakwenda kupata ajira nyingi kwa sababu viwanda vingi vimekufa. Siweze kurejea haya kwa sababu viongozi na Wabunge wengi wameongea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kufikia malengo wakati sekta ya kilimo tumeiacha nyuma, hawa ni mapacha ni lazima tuangalie kilimo tunatengaje bajeti yake inatekelezwa vipi hili twende mbele kwa sababu kama hatuna raw material hatuwezi kwenda na viwanda. Na ukiangalia kwa miaka mitano mfulululizo sekta ya kilimo wametengewa asilimia 17 tu; tunakwendaje kwa namna hiyo? Hatuwezi kwenda kwa sababu hawa ni mapacha bila raw materials viwanda haviwezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hayo najielekeza kwenye nafasi yetu ya kidunia ambayo wengi wameiongelea ya 141 kati ya nchi 190; tunakwenda hivyo tulikuwa tumejiwekea malengo kama Tanzania twende kwenye double digit position, hatuwezi kwenda kama malengo yetu hatuwezi kuyatekeleza vizuri wakati tunapanga. Nikisema hayo ninaangalia mazingra ya biashara na viwanda kwa Tanzania ni rafiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwama kwa sababu mazingira si rafiki, Tanzania kuna utitiri mkubwa wa kodi, ukileta uwekezaji anaaanza kujiuliza wazawa wameshindwa kuwekeza kwa sababu ya utitiri wa kodi. Nikianza kutaja hatutamaliza, ukitaka kufungua kiwanda au kuanzisha biashara ni lazima uende ukasajili BRELA kule ni pesa, ni lazima ulipe kodi ya zuio, hiyo ni pesa; ni lazima ulipe kadiri unavyopata hiyo ni pesa; ni lazima ulipe gharama za OSHA hiyo ni pesa; ni lazima ulipe kodi ya ujuzi hiyo ni pesa; bado Manispaa wanakusubiri ulipe leseni hiyo ni pesa; gharama za Zimamoto, ada za Mamlaka ya Chakula; hiyo ni pesa na gharama lukuki ambazo ziko hapa. Mlundikano huu wa kodi, mwananchi wa kawaida mwenye mtaji wa kawaida hawezi kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda namna hiyo Mheshimiwa Waziri nikuombe wakati unakuja na mkakati wako, una-wind up hapa, utueleze ni mkakati gani ulionao ili kuwezesha Watanzania waweze kuwekeza. Tusiimbe tu nchi ya viwanda kwa mdomo, tukatekeleze kwa vitendo kwa sababu…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza anasema kwamba Serikali haijajenga viwanda kwa maana kauli ilipamba tu moto, lakini viwanda vingi havijaanzishwa. Nataka nimpe taarifa kwamba kutokana na Tanzania National Business Portal, ripoti inayozungumzia kwamba toka Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, viwanda 4,877 vimejengwa. Kati ya viwanda hivyo, viwanda 201 ni viwanda vikubwa, viwanda 460 ni viwanda vidogo, viwanda 3,406 na viwanda 4,401 ni viwanda vidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpe taarifa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba mazingira ya viwanda yanakuepo na viwanda vingi vimeshajengwa nchini. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu sizungumzii viwanda vinavyofichwa chumbani, nazungumzia viwanda vyenye tija kwa wananchi, nazungumzia viwanda ambavyo vilikuwepo na hatujaviona. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista, viwanda vipi vinafichwa chumbani? Naomba uondoe hilo neno.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema huwezi kuwa na blender useme una kiwanda; huwezi kuwa na cherehani moja unaajiri watu wangapi?

MWENYEKITI: Basi tumia lugha nyingine, lakini siyo ya chumbani.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, blender hata ndani si unajua. Kwa hiyo…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Naomba nimpe Mheshimiwa dada yangu taarifa kwamba hivi tunavyozungumza bajeti iliyoko mezani kwake hapo zimeshatengwa shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufufua kiwanda kikubwa sana cha Kilimanjaro Machine Tools, kiwanda ambacho kilikufa miaka mingi, sasa kimeshatengewa hela. Kiwanda hiki kinatengeneza viwanda vingine vidogo vidogo, kazi yake ni kuunda vyuma na fedha imeshatengenezwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kumpa taarifa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inaendeleza kujenga viwanda vikubwa vikubwa kama hiki ambavyo havipatikani kwingine duniani. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kaka yangu Mheshimiwa Mafuwe, alikuwa anataka kuchangia kwa sababu hayuko kwenye list. Mimi niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba maneno haya siyasemi mimi; kupitia Ripoti ya CAG anasema kwamba kumekuwa na utekelezaji mdogo wa bajeti ya maendeleo kwa viwanda vidogo vidogo katika ngazi zote za Serikali; mfano, kwa miaka minne ya nyuma mfululizo, Wizara ya Viwanda na Biashara imetumia asilimia 16 tu ya fedha za maendeleo zilizopelekwa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogo vidogo. Maneno haya si ya kwangu, ni maneno ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo ninasema tujielekeze kwenye ukweli, tunavyopanga hapa tuweke bajeti na ile bajeti iende na ikatekelezwe. Sisemi mapambio ya kuweza kumfurahisha mtu. Watanzania huko nje wanalia, akina mama huko nje wanalia kwa sababu hata akiwa na biashara yake ule utitiri wa kodi kwa miaka mitano iliyopita hii Watanzania wengi biashara zao zimefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi mtakuwa ni mashahidi, hamuwezi kusema lakini mnajua kwenye majimbo yenu kilio cha Watanzania ni kikubwa kuliko tunavyofikiri. Twende tukarekebishe kwa sababu kazi ya Bunge ni kuielekeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuielekeza Serikali ikaangalie utitiri huu wa kodi, ipunguze ili wananchi wetu wapate nafuu na waweze kuwekeza. Nia yetu ni njema kwa sababu Tanzania yetu ni moja, tunahitaji maendeleo, hatuhitaji malumbano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa hatuhitaji ahadi, tunahitaji utekelezaji. Utekelezaji ni jambo la msingi kwa sababu baada ya kutoka hapa tutakuwa na dhambi ya kujibu kwa Mwenyezi Mungu. Wale watu wenye imani kila siku unamwambia mtoto wako utanyonya kesho kama mtoto wa kuku halafu mwisho wa siku Watanzania wanakosa imani na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukatekeleze vile tulivyovipangilia ili tuweze kufikia azma ya Serikali ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa pumzi alizoweza kunipa siku ya leo lakini nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwa leo, nishukuru kwa kidogo, wanasema usiposhukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa huwezi kushukuru. Niweze kushukuru kwa mawazo haya yaliyochukuliwa kwa sababu nimekuwa ni mdau wa barabara nimekuwa nikichangia kwenye barabara katika TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi nimejikita sana kwenye barabara. Kwa hiyo, nimeona hapa mrejesho uliokuja umekwenda kuleta suluhu kama tutakwenda ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza jinsi Serikali inavyopoteza wawekezaji, nikaeleza jinsi inavyoweza kufikia kukosa pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja kama hatutatengeneza miundombinu thabiti ya barabara. Lakini nikaeleza ni jinsi gani tutashindwa kwenda kufikia kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda kama hatutatengeneza miundombinu; nikaeleza ni jinsi gani hatutafanya kilimo chenye tija kama hatutatengeneza miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoongea hivi narejea kwenye hotuba ya bajeti kwenye ile para ya 39. Nimeona pale kwamba Serikali inakwenda kuomba mikopo ya bei nafuu kwenye Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeainisha pale kiasi cha dola za Kimarekani milioni 120 imeelekezwa itakwenda Dar es Salaam. Ikaelekezwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 300 zitakwenda mikoani kwa lengo la kukuza uchumi. Lakini pale ikaelekezwa milioni 50 dola za Marekani Serikali itakwenda kuweka pale; lakini mwisho wa siku tunapata jumla ya dola za Kimarekani milioni 470. Tukienda kubadilisha kwa fedha zetu za Kitanzania kwa rate ya leo ni shilingi 2,300 tunapata trilioni 1.081. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukihama twende ile para ya 88 ambapo kuna tozo ya mafuta. Serikali inaendelea kutafuta fedha mbadala ili tuweze kupata suluhu ya kero ya barabara. Kwenye tozo ya mafuta ya petrol na diesel tumesema pale kila lita moja itatozwa shilingi 100. Serikali ikadadavua ikapata 322,158,000.20, ukijumlisha unapata trilioni 1.403 fedha hizi ni nyingi sana na zote zinatakiwa zielekee TARURA ndio lengo la Serikali. Na ukiangalia asilimia ya barabara zetu za vumbi ni asilimia 72.4 Nchi nzima kwenye mtandao wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ni nyingi naomba nishauri jambo. Kwa sababu fedha hizi ni nyingi na zikiwekezwa kweli kwenye TARURA zitaleta tija, ninaomba fedha hizi ziwekwe kwenye ring-fence ili zisitumike kwenye matumizi mengine lakini jinsi zilivyotengwa ziende eneo husika. Namba mbili, fedha hizi jinsi Mheshimiwa Waziri alikuja hapa akadadavua vizuri aje hapa wakati wa kuhitimisha fedha hizi zianishe barabara zinazokwenda kujengwa. Lakini pia zianishwe zinakwenda kujengwa kwa kiwango kipi cha lami, cha changarawe au kiwango kipi ili tuangalie thamani ya fedha zetu zinakwenda kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikifanya hivyo ninarejea pale ambapo Serikali iliona inakwenda kukuza fursa ya kiuchumi ndio maana fedha hizi zikaelekezwa zile dola milioni 300 zikaenda mikoani. Kuna mfano wa barabara ambazo ni kwikwi tutakuwa tunaimba mapambio hapa kila siku kama hatutekelezi wajibu wetu na kutenda kile ambacho tunachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara za mikoani ambayo mikoa inalima, inalima mazao ya biashara, inalima mazao ya mbogamboga, kwa mfano; kama Morogoro kuna barabara ile ya Bigwa – Kisaki ile barabara ni kwikwi lakini wakulima walioko kule ni wengi na barabara ile ikijengwa inaweza kuleta tija ni kwa Mheshimiwa Babu Tale. Lakini ipo barabara ile ya Iringa ambayo inapita Lujewa, Madibila mpaka Mafinga ile barabara ni ya kibiashara kule wapo wakulima, wapo watu ambao wako pale wanalima mahindi ikitengenezwa vizuri inaweza kuimarisha pato la mtu mmoja mmoja lakini kuimarisha pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya Njombe – Kibena kuelekea Lupembe mpaka Madeke kule kuna wakulima wa parachichi. Tunaachaje kutengeneza barabara hizi za kimkakati. Kama lengo letu ni kukuza fursa za kiuchumi na kibiashara twende tukaangalie hizi barabara za kimkakati. (Makofi)

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, TAARIFA.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa kwamba barabara ile ya Kibena stop Lupembe, Madeke barabara ambayo inaunganisha mkoa na mkoa. Kweli kuna umuhimu sana wa barabara hizi kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali ipo hatua nzuri ya kutengeneza barabara hizi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa hiyo.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hii kwa sababu ni kati ya wadau ambao wanalalamika juu ya barabara hizo. Niendelee, naendelea kuainisha barabara za kimkakati kwenye mkoa ule wa Kagera kuna barabara ya Mulushaka, Ukwenda, Mrongo, barabara hii inaelekea mpaka mpakani mwa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya sehemu hizo tumefika sisi wanasiasa tumetembea mtaa kwa mtaa, mkoa kwa mkoa, kwa hiyo tunafahamu kero za nchi hii. Barabara hii ukifika kule mpakani kuna wakulima wa ndizi, kuna wakulima wa kahawa, barabara hii ikitengenezwa tunakwenda kukuza pato la Taifa lakini pato la mtu mmoja mmoja ambayo ndio dhamira yetu ambayo Wabunge tuko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema pia bajeti hii iainishe madaraja. Kuna madaraja ambayo ni sugu watu wanaongea huku kipindi hicho cha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na TAMISEMI watu wengi wanaongea juu ya madaraja, vilio kwa kina mama wajawazito wanajifungulia barabarani. Tuainishiwe na madaraja haya ili tuweze kujua fedha zetu inakwenda kutumika vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sasa naelekea Dar es Salaam. Katika Mkoa wangu wa Dar es Salaam, Dar es Salaam ni mkoa wa kimkakati na ni mkoa wa biashara na ni kitovu cha biashara Nchi nzima. Dar es Salaam huwezi kusikia mtu anasimama hapa anaomba viatilifu, anaomba mbolea, anaomba pembejeo. Dar es Salaam tunaomba miundombinu thabiti. Tunaomba miundombinu kwa sababu mpaka Dar es Salaam inaibuka katika Majiji yote kwamba ndio Jiji ambalo linakusanya ushuru mwingi kila siku na kimkoa inashika namba moja ni kwa sababu Dar es Salaam ndio mkoa wa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam kuna tatizo la miundombinu, nikipita kwako kwenye mitaa ile ya Ilala, ninaona barabara za mitaa bado haziko sawa. Pia maji taka Dar es Salaam ni asilimia 14 tu tumeunganishwa katika mfumo wa maji taka, asilimia 86 ule mfumo wa maji taka umeingiliana na maji masafi huko huko tunakutana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu na magonjwa ya homa ya matumbo. Kila mwaka kipindupindu kinaazia Dar es Salaam, siyo kwa sababu nyingine bali ni mfumo wa maji taka ambayo siyo rafiki. Niombe wakati Waziri anakuja, aje na utaratibu mzuri kwa jinsi gani maji taka yataelekezwa baharini au sehemu nyingine kuliko ilivyo hivi sasa. Dar es Salaam mvua ikinyesha ndiyo wakati wa wananchi wa kupumua na kuanza kucheulisha vyoo vyao na yale mambo yanatapaa barabarani, kwa hiyo siyo salama sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa sababu Dar es Salaam ndio Jiji la kimkakati, wawekezaji wanapokuja kitu cha kwanza wanaangalia miundombinu, kama miundombinu siyo rafiki wawekezaji wanatukimbia. Na Dar es Salaam ndipo wawekezaji wanaanza kushukia pale, kwa hiyo wanaangalia mandhari, pia wafanyakazi wa Dar es Salaam ni uchovu kwa sababu mvua ikinyesha inakuwa ni jam kunakuwa na foleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe wakati Mheshimiwa Waziri unakuja kuhitimisha, uje na mkakati wa miferiji Dar es Salaam, mifereji ambayo inasababisha barabara zetu za lami zinakatika, hakuna miundombinu thabiti ya mifereji, mvua ikinyesha mafuriko watu hawapiti mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye wizara hii muhimu. Ninapozungumzia kwenye ujenzi na uchukuzi moja kwa moja tunaelekeza kwenye mambo ya miundombinu kama barabara, reli na vitu vinginevyo. Katika sekta hii, imeonesha kukua mfululizo ndani ya miaka minne, imekuwa ikikuwa kwa asilimia 14.4 tangu 2016/2017, 2020/2021. Hii sekta inakua bila kigugumizi pamoja na janga la corona lakini imeiongezea Nchi pato la Taifa asilimia 14.8. Hii ni sekta ya pili kwa kuongezea Nchi pato la Taifa ukitoka kilimo lakini kwa kukua imeibuka kinara sekta hii ni muhimu inahitaji jicho la tatu kwa mustakabali wa Taifa na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema hivi ninaona kuna changamoto chache ambazo tunaweza tukizimaliza hii sekta inayoenda kukua na kuwa kinara na pato la Taifa litakuwa zaidi na mwananchi mmoja mmoja ataweza kumiliki uchumi. Nikisema hivyo, ninaweza kusema wakandarasi walioingia mkataba, wakandarasi waliosajiriwa kwenye nchi yetu asilimia 10 tu ndio wageni kwa nchi za nje, asilimia 10. Asilimia nyingine ni wazawa lakini ukifanya upembuzi pale unakuta asilimia 60 ya miradi mikubwa inashikiliwa na asilimia 10 ya wakandarasi wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashindwa kuwa wazalendo kwasababu Wakandarasi wetu hawakidhi vigezo, kigezo cha kwanza hawana mitaji, hawana mitaji mizuri kwahiyo hawawezi ku-afford kuweza kushika hii miradi mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine hawana ujuzi wa kutosha, hawana ujuzi wa kutosha kwa hiyo mwisho wa siku tunatakiwa tukae chini tuweze kuwawezesha wakandarasi wetu wawe na ujuzi wa kutosha ili kuweza ku- afford ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni vifaa vya ujenzi havikai kwenye level moja bei zake zinapanda na kushuka na sometimes hazipo kabisa. Kwa hiyo, mwisho wa siku hawa wataalam wetu wanashindwa kwenda kwenye ushindani wa wakandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongea haya ninasema kwasababu Wakandarasi wetu wakiweza kushika hizi tenda uchumi wa mtu mmoja mmoja ndani ya nchi yetu utakua, lakini pato la Taifa litaongeza kwa sababu watu wetu watakkuwa na fedha mfukoni. Niishauri Serikali katika hili, tunavyoona namna hii tuweze kuwawezesha Wakandarasi wetu waweze kumiliki hii miradi mikubwa ili tuweze kuona matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninapotoka mahali hapo, ninaona kabisa barabara nyingi, vilio vingi vya Wabunge humu ndani wanalia juu ya barabara, hawatoki kwenye reli wanaingia kwenye reli ya barabara kwa sababu ndio kero inayomgusa mwananchi wa kawaida kule chini vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zinazounganisha mikoa kwa mfano barabara zinazounganisha mikoa kuja Dar es Salaam, barabara hizi ni mbovu za mikoa ya kimkakati mikoa ya kilimo. Mikoa ya Njombe, ya Iringa, Mikoa ya Singida barabara hii si salama kwa hiyo wananchi wa kawaida hawawezi kuleta mazao yao Dar es Salaam. Wakifika Dar es Salaam wanakutana na adha nyingine ya mafuriko, Dar es Salaam miundombinu ya mafuriko hakuna mifereji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wanatengeneza mkakati huo wa barabara waangalie mifereji kwasababu maji haya ya mifereji yamekuwa ndio chanzo cha kukata barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini mafuriko ukifika Jangwani eneo lile la mkutano kuelekea Kariakoo pale hapapitiki wakati wa mvua ni kwa sababu hakuna miundombinu ya mifereji ambayo ni imara. Ukija barabara ya Tegeta kuelekea Bunju, Boko, Basihaya mifereji hakuna barabara zimejengwa zipo vizuri lakini unakuta magari yame- stuck hayawezi kutembea kwa sababu maji yanajaa barabarani, barabara zinakatika kuisababishia Serikali kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuone namna gani bora wakati tunapokwenda kuweka miundombinu ya barabara tuona namna bora ya kutengeneza mifereji. Jiji la Dar es Salaam halina miundombinu rafiki, ukiangalia Jiji la Dar es Salaam watu wanasema kuna lami lakini ni asilimia 14 tu ya Jiji la Dar es Salaam wananchi wake wameunganishwa kwenye maji machafu, maji taka asilimia 14. Asilimia nyingine tunachanganyika na maji hayo hayo tunakunywa, magonjwa ya mlipuko Dar es Salaam, wanaotoka mikoani wanakutana nayo, basi ni vurugu tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, wanajua Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mnajua, miundombinu ya Dar es Salaam si rafiki kila siku watu wanaugua vipindupindu, wanaugua UTI, wanaugua magonjwa kadha wa kadha kwasababu tu ya miundombinu, lakini sio adha nyingine. Niombe kwa sababu ni kitovu cha biashara, twende tukaitengeneze Dar es Salaam na mikoa yake inayounganishwa kuja Dar es Salaam ili tuweze kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoongea hapa kuna wananchi wangu wa Ununio hawana pa kukaa, barabara hazina mifereji, watu wapo pembezoni wamekaa wametulia hawana pa kwenda mbele wala kurudi nyuma, nyuma zinaelea. Ni Dar es Salaam hapo sio mikoani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikiangalia kiini naona ni mitaro niiombe Serikali chonde chonde kipindi kilichopita niliongelea juu ya mitaro pale Nyamachabisi alikuja waziri kipindi kile nafikiri waziri wangu anafahamu. Alikuja kipindi kile Nyamachabisi miundombinu ya mitaro hakuna watu wanaelea. Niombe, niombe Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Serikali Sikivu na Mawaziri wake waweze kuweka mikakati mizuri ili wananchi waweze kufanya biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoongelea miundombinu, ninaongelea viwanda huwezi kuwa na viwanda imara kama huna miundombinu. Ninavyoongelea mbiundombinu ninaongelea kilimo, huwezi kuuza mazao yako ya kilimo kama huna miundombinu. ninapoongelea hiyo miundombinu naongelea uwekezaji, wawekezaji wanaanglia miundombinu ndio wanakuja kwenye nchi yetu. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenisaidia kufika mahali hapa hii leo. Naishukuru pia familia yangu ambayo kimsingi imekuwa nyuma yangu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kwenye hotuba ya Rais ambayo imeeleza kwenye ile page ya 21 namna gani wanawake na vijanawanakwenda kupata mikopo ya asilimia 10. Nimesema kuhusiana na hili linatakiwa jicho la tatu kwa sababu wanawake wengi ndiyo wanaoonekana kwenda mbele kwenye hii mikopo na wanawake hawa wamepata changamoto lukuki. Changamoto hizi hazitatuliwi kwa muda mrefu, kwa sababu wanawake hawa wanaenda kupewa vigezo ambavyo haviko kwenye utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wanadaiwa kadi za Chama Cha Mapinduzi, kama hauna kadi ya Chama Cha Mapinduzi hupati mkopo. Lakini wanawake hawa hawa baada ya kupata mikopo hawana mtu wa kuwafundisha ni namna gani watakwenda kufanya biashara kwa kiwango kidogo wanachopewa ili kuleta tija kwenye jamii. Kikubwa zaidi hawa wanawake wanaopata mikopo au wengine wanaokosa wanakimbilia kwenye microfinance...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Njau, kuna Kanuni inavunjwa. Mheshimiws Jenista Mhagama Kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye utaratibu. Kanuni ya 71 mambo yanayokatazwa Bungeni lakini 71(1) ambacho Mbunge haruhusiwi kusema taarifa ambazo hazina ukweli, lakini kiambatane na Kifungu cha 70(4) ambacho kinamtaka kuthibitisha ni kwa kiasi gani jambo linalosemwa kwamba si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu, kwa mujibu wa miongozo tuliyojiwekea inayosimamia utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri zetu, kigezo cha uanachama wa mwombaji wa mikopo hakipo na hakijawahi kutumika. Halmashauri zote zimekuwa zikitoa mikopo hiyo kwa uwiano ulio sahihi kabisa. Kinachozingatiwa ni taratibu zile za kimiongozo ambazo zinatakiwa kila mwombaji mkopo aweze kuzifuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Bunge hili lisitumike kuzungumza mambo ambayo hayana uasili na uhalisia. Mara nyingi tumekuwa tukimsikia Mheshimiwa Rais akisema maendeleo ya taifa hili hayatazingatia chama, dini, ukabila wala jambo lolote ni maendeleo huru kwa Watanzania wote kwa mambo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge alikuwa anachangia Mheshimiwa Felister Njau, ameeleza maelezo kuhusu mikopo inayotolewa na vigezo vinavyozingatiwa. Akasimama Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa mujibu wa Kanuni ya 71 na 70, ametoa maelezo ambayo sote tumeyasikia, sitayarejea lakini hoja ya msingi iliyotolewa hapo ni kwamba, Mheshimiwa Felister Njau wakati anachangia amezungumza taarifa kuhusu mikopo ambazo hazina ukweli kwa mujibu wa Mheshimiwa Jenista. Kanuni yetu ya 70 inatuongoza namna ya kwenda na jambo ambalo limezungumzwa hapa, lakini Mbunge ataamua sasa kusimama kama alivyofanya Mheshimiwa Jenista kuonesha kwamba jambo hilo linalosemwa halina ukweli na ametoa ufafanuzi kwa nini anasema halina ukweli.

Mheshimiwa Felista Njau, ili twende vizuri na kwa sababu sisi wengi hapa ndani ni wageni tutaelekezana tu vizuri hizi Kanuni taratibu, lakini Kanuni ya 70, Mheshimiwa Jenista ametumia fasili ya (4) na (7) inakupa fursa ya aidha kufuta kauli yako kama hilo jambo lililosemwa huna uthibitisho nalo, ama kama hutafuta hiyo kauli hapo nitatoa mimi maelekezo ya nini kifuate baada ya hapo.

Kwa hiyo, nakupa fursa kama huna uthibitisho ufute hiyo kauli, kama utakuwa hufuti kauli nitasimama tena kutoa maelekezo. Nakupa fursa ya kufuta kauli. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sifuti kauli kwa sababu nina uthibitisho na kimsingi nilikuwa nashauri kwa sababu watu wengi wanaweza wakatumia hiyo lakini ngazi za juu hawajui. Kwa hiyo, natoa ushauri mamlaka husika ifuatilie, hilo tu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sawa, sasa ukae Mheshimiwa Njau. Waheshimiwa Wabunge, naenda taratibu kwa sababu sisi wengi humu ndani ni wageni.

Mheshimiwa Felista Njau matakwa ya Kanuni ya 70, ukikataa kufuta kauli maana yake mimi naweza kukuelekeza uniletee ushahidi. Ushahidi utakaoniletea si wa maneno wa kuniambia kuna watu waliambiwa, hapana; utatakiwa ulete ushahidi wa kulithibitishia Bunge hili kwamba hicho ni kigezo cha mikopo mahali fulani na mahali fulani. Kwa hiyo, tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Kwa hivyo, unavyopewa hii fursa ni fursa ya muhimu sana lakini kama unao uhakika Bunge hili kwa sasa hivi haliwezi kukulazimisha kufuta kauli kwa sababu, wewe umesema unao uthibitisho. Sasa kwa sababu ya ugeni nakupa tena fursa ya pili, kama unao uthibitisho nitatoa maelekezo. Karibu, sekunde 30, unao uthibitisho?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuondoa mlolongo nafuta lakini naomba… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, kaa niiweke vizuri, kaa niiweke vizuri, eeh.

Waheshimiwa Wabunge, Kanuni zetu namna zinavyotutaka kuenenda niwashauri sana sote tuzipitie, Wabunge wageni lakini sisi sote kwa sababu hili ni Bunge jipya. Kanuni hizi ni toleo jipya kwa hiyo, ziko Kanuni ambazo zimebadilika hapa na pale niwasihi sana tukazipitie.

Masharti yaliyoko humu huwa yanafuatiliwa nukta kwa koma, kwa hivyo, ukifuta kauli unafuta bila masharti. Hakuna neno lakini ama nafanya hivi, aahh-aa, isipokuwa yale uliyokuwa unayasema maelezo yako ya pili, sasa hii natoa Mwongozo; ungeweza kusema naishauri Serikali wakati wa kutoa mikopo wajaribu kuangalia hiki na hiki na hiki, lakini ukionesha kwamba kuna shida mahali ni lazima hiyo shida iletewe uthibitisho.

Waheshimiwa Wabunge, kwa muktadha huu na ili tuweze kwenda mbele, Mheshimiwa Felister Njau amefuta kauli yake. Kwa muktadha huo Mwongozo wa Kiti kuhusu huo utaratibu aliokuwa ameomba Mheshimiwa Jenista Mhagama ni kwamba taarifa hiyo haitakuwepo kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Njau endelea na mchango wako.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakwenda kwenye kipengele kingine page number 72 ambapo kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais kumeeleza kulinda demokrasia, uhuru, haki za wananchi na vyombo vya Habari. Mpaka sasa navyoongea mimi nilikuwa meneja kampeni wa Jimbo la Kawe, Mheshimiwa Halima James mwana wa Mdee, haki, demokrasia, usawa havikulindwa na havikulindwa toka uchaguzi mdogo wa mwaka 2014 uliofutwa, 2019 uliofutwa, lakini 2020 kulikuwa kuna mambo ya ajabu. Mimi ni kati ya watu niliyekamata kura fake mabegi matano kwenye vyombo vingi, lakini nikasema kwa sababu tunakuja kwenye Bunge hili ni lazima tuseme ukweli, demokrasia tunayoiimba tuifuate kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anajua kwenye Bunge hili amekuja vipi, ameshinda vipi, kwa njia zipi, lakini demokrasia ikaseme na mioyo yetu. Haki ya vyombo vya habari, kuna kipindi sisi tulikuwa tukisimama kwenye majukwaa mwandishi akaonekana amepiga picha, humuoni hata siku tatu, nne, ukimpigia simu anakimbia anasema nina kigugumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kama ni haki tunaitangaza, kama ni demokrasia tunaisema, tuiishi kwa vitendo kwa sababu hapa kila mtu ana imani yake. Kila mtu ana imani kwenye Bunge hili kwa hiyo, tuiishi kwa vitendo tusiimbe kwenye makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa minajili hiyo kuna watu lukuki, kuna wananchi waliokamatwa kipindi cha uchaguzi…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gwajima, Kanuni inayovunjwa?

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwa Kanuni ya 71(1)(a). Inasema: “Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge aliyekuwa anazungumza, bahati nzuri mimi ndiye Mbunge halali wa Jimbo la Kawe niliyeshinda kwa kura 194,000 dhidi ya mpinzani wangu aliyepata 30,000 peke yake. Naomba alithibitishie Bunge lako kwamba alikamata kura maboksi 50 kama alivyosema. (Makofi/kicheko)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, bahati nzuri hizi kanuni tutazifahamu tu, Bunge hili ni la miaka mitano, Mwenyezi Mungu atujalie uhai na uzima. Kanuni ya 71 inampa fursa Mbunge kusimama ukisoma fasili nyingine zinazofuata baada ya hapo na kusema kuhusu utaratibu, kwa maana ya fasili ya (2) inampa fursa Mbunge kusimama kusema Kuhusu Utaratibu ili kueleza mambo haya yasiyoruhusiwa Bungeni kwa lile ambalo linakuwa linazungumzwa.

Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe, amesimama kueleza kwamba taarifa zilizokuwa zinatolewa na Mheshimiwa Felista Njau za kuhusu vitu vilivyokamatwa huko Jimboni Kawe kipindi cha uchaguzi ama siku ya uchaguzi hazina ukweli. Sasa mimi siwezi kufahamu ukweli, anayeufahamu ni Mheshimiwa Felister Njau. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kabla hamjapiga makofi, hili jengo letu hili kuna muda kuna maneno fulani hivi yanaweza kusemwa pamoja na mambo mengine kwamba hili jumba ni jumba la kisiasa, lakini hili ni jumba ambalo ndiyo maana wanasema Mheshimiwa Spika Bunge lako Tukufu. Haiyumkiniki kwamba mtu anayesimama kuchangia humu ndani atazungumza mambo ambayo yanazungumzwa bila ushahidi, bila uhakika kwa sababu kila mmoja wetu anaitwa Mheshimiwa kwa maana ya ni kiongozi anaweza kusimamia kile anachokisema, anaweza kuthibitisha kile anachokisema.

Mheshimiwa Felister Njau huu ni utaratibu wa pili kwamba Kanuni inavunjwa. Humu ndani huwa ni kawaida watu wanaweza kusimama hata mara nyingi, lakini tazama michango yako isikupeleke mahali ambapo kuna Kanuni humu ndani zinakupeleka nje ya hili Bunge. Isitokee kwamba kila unachokisema tutafika mahali pa kwenda hapo, siyo kwa maana ya utoke nje, aah-aa, kwa maana ya uende huko Kamati ikajiridhishe, ulete huo ushahidi na mambo kama hayo. (Makofi)

Kwa hivyo, kwa muktadha wa Kanuni hizi kwa sababu, sasa husemi ukweli maana yake unarudi tena kwenye 70. Kama unao uthibitisho utasema hivyo, mimi nitaagiza utoe huo uthibitisho. Kama huna uthibitisho futa kauli yako kwa mujibu wa Kanuni ya 70 kama nilivyokusomea Fasili ya (7).

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Uthibitisho ninao na nikiambiwa nilete nitaleta uthibitisho. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Kanuni hii ya 70 inakataza Mbunge kusema uwongo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Tusikilizane Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane. Kanuni ya 70 inakataza kusema uongo Bungeni na fasili ya (4) ya (5) na ya (6) ukizisoma zote kwa pamoja utapata picha kwamba Kiti kitaagiza Mbunge ambaye amekataa kufuta kauli kuleta ushahidi kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge na siyo kumridhisha mtu mmoja.

Kwa muktadha huo fasili ya (6) inanitaka mimi nitoe muda wa kufanya hivyo. Mimi sitataka nimwambie alete ushahidi hapa kwa sababu naweza kumwambia alete sasa hivi ama alete baadae, kwa sababu alikamata maboksi na mabegi hataweza kuwa nayo humu ndani maana yatakuwa hayakupita pale nje kuingia humu ndani. Kwa muktadha huo, hayo mabegi, hayo masanduku yaliyokamatwa naiagiza Kamati yetu ya Maadili, itamsikiliza yeye halafu mimi nitaletewa huo ushahidi. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Njau utapeleka ushahidi wako kwenye hiyo Kamati yetu. Muda ninaoutoa kwa sababu leo ni siku ya Jumatano ndiyo kwanza tumeanza Bunge jana, kufikia Jumatano ijayo huo ushahidi uwe umeshauleta na Kamati yetu ya Maadili ikae wakati huo na kabla Bunge hili halijaisha tutatoa maamuzi kuhusu jambo hilo. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba dakika zangu zilindwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niombe mamlaka ambayo inaweza kushughulika, kuna vijana wengi katika kanda mbalimbali na mikoa wako ndani kwa kesi za kisiasa za uchaguzi na zinapigwa tarehe, ushahidi unakosekana. Katika kanda mbalimbali, Kanda ya Kusini 34, Kanda ya Nyasa 36, Viktoria 16, Serengeti 34, Pwani nane, wale vijana ni wa CCM na CHADEMA. Kwa hiyo, naomba mamlaka husika iwaondoe vijana hawa ndani kwa sababu shughuli au mtanange umekwisha. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njau, hao washauri wako wa hapo karibu wanatakiwa wakushauri mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na mambo yaliyoko mahakamani. Mambo yaliyoko mahakamani hayatolewi maamuzi hapa ndani.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, sorry, wako mahabusu.

NAIBU SPIKA: Mambo yaliyoko mahakamani hayatolewi maamuzi hapa ndani. Mheshimiwa Esther Matiko na Ester Bulaya msimpoteze Mheshimiwa Felister Njau.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njau malizia mchango wako.

MHE. ESTHER N. MATIKO: No, please, sasa mimi umeniingizaje hapo, I did not say anything.

MHE. ESTER A. BULAYA: Sijawasha microphone hapa, kichwa yake yeye mwenyewe iko vizuri.

MHE. FELISTER D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko na Ester Bulaya, muacheni mchangiaji amalize mchango wake. Muacheni mchangiaji amalize mchango wake, Mheshimiwa Felista Njau.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa, niko huku.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Naomba tu nimpe Taarifa mchangiaji Mheshimiwa Njau kwamba watu anaowazungumzia ni pamoja na wakazi wa Wilaya ya Mpwapwa ambao wako 18 walikamatwa, kesi haijaenda mahakamani…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane vizuri. Bunge hili siyo kazi yake kuingilia michakato ya taasisi zilizoko huko nje, labda kama hapa mbele kuna hoja hiyo, tuelewane vizuri na ninyi mnazifahamu kanuni, tuelewane vizuri. Mheshimiwa Njau malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nishukuru lakini niombe, wako Mawaziri wenye mamlaka hayo wasimame kidete kwa ajili ya kutetea haki za raia na tusiende kwa sababu ya itikadi au chochote. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nakushukuru kwa ajili ya kunipa nafasi hii. Pia nitoe pole kwa Watanzania wote kwa msiba mkubwa uliotufika. Kimsingi nimesimama mbele yako niweze kuchangia kidogo, lakini niweke msisitizo; naingia moja kwa moja kwenye Sekta ya Kilimo. Natamani kila mtu akisimama aweze kuona upana na ukubwa wa sekta hii ili tuweze kuweka nguvu inayohusika katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme sekta ya kilimo inaweza kuchukua asilimia 56.5 ya ajira zote za Watanzania. Nikienda kwenye asilimia; nakwenda kwenye asilimia 20 ya mauzo yote ya nje. Unaona hapa kidogo kuna ufinyu, kwa sababu sekta hii haijachukuliwa kwa uzito wake. Ikichukuliwa kwa uzito wake, hatutalia ajali za boda boda barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Nairobi wameweza kutenga SACCOSS maalum, wakakusanya vijana katika makundi na wanatengeneza mfumo wa kununua daladala kule wanaziita matatuu ili waweze kuwekeza. Sisi tuna ardhi kubwa ambayo ina rutuba, tuna maji. Kwa mfumo wa umwagiliaji, kama hatuna ile miundombinu, lakini tuangalie hizi mvua zinazonyesha, tunalia mafuriko; haya maji yanayotokana na mvua tungeweza kuweka pale miundombinu ya umwagiliaji tukavuna yale maji yakatusaidia kwenye kumwagilia, tusingelia leo mambo ya mafuta, tungewekeza kwenye alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa hawa vijana wanaokufa kwa boda boda hawajapata Plan B za ajira. Wakipata Plan B hatutalia vifo hivi, kwa sababu kila kijana anafikiria ajira ni boda boda. Pia tungeweza kuwapa elimu, wakaweza kuwekeza kwenye kilimo ambao ni asilimia kubwa sana, hawa vijana wangetoka na wangekwenda kusimama na utaona uchumi unakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuomba, kuna benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima, benki hizi hazijaona vijana. Vijana hawawezi kuwekeza kule kwa sababu wanaonekana hawana thamani fulani hivi. Labda wawekwe kwenye vikundi ili waweze kwenda kwenye benki hizi waweze kukopeshwa au waundiwe SACCOSS zao maalum waweze kukopa maana hawana dhamana, ndiyo maana hawakopesheki.

Mheshimiwa Spika, kijana wa Tanzania hata akienda mahali anaonekana muhuni tu, lakini ni Mtanzania ambaye kimsingi tukimpa mbinu, tukampa elimu, tukawekeza kwenye kilimo, hawa vijana wasingelia leo. Kingine, akina mama wengi wanalima kwa jembe la mkono, hawalimi kilimo chenye tija. Hata wakilima hiki kilimo chenye tija, hawajui zao ambalo wanaweza kulima liweze kwenda nje. Tuwekeze kwenye tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza kwenye tafiti, tukalima kilimo chenye tija, tutamkomboa mkulima mdogo na mkubwa na wote tutasimama. Niweze kusema hili suala kwa sababu tuna akina mama wengi wanalima kila siku ni kilio. Analima anaambiwa tu kwa maneno, kwa nadharia kwamba kilimo kitakukomboa, lakini haoni ukombozi wa kilimo hiki.

Mheshimiwa Spika, tukienda vijijini tukakusanya akina mama tukawapa elimu, wakalima kilimo ambacho kitakidhi vigezo kule nje, kwa sababu akina mama wengi wanalima, wanaweka mbolea ya chumvi chumvi, wakija kupima wanaona zao hili halifai. Tuwape elimu. Tuna mifugo; tuchukue mbolea za mifugo, tuweke kwa akina mama wale tuwekeze kwenye tafiti, leo kina mama tutawainua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa ninachoweza kusema kwenye sehemu ya pili ni mambo ya demokrasia. Mheshimiwa ameongea juu ya kuimarisha demokrasia, usawa na amani. Kuna watu wenye makovu, wana makovu yaliyopita huko nyuma. Tuna mategemeo; Tanzania, Taifa hili sasa hivi lina mategemeo makubwa na Rais wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. Lina mategemeo makubwa kutokana na kauli zake, wanasema kimjazacho mtu moyoni ndicho kinachotoka kwenye kinywa chake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu ameonyesha kunyesha suluhu kwa Watanzania. Kwa hiyo, Watanzania waliokata tamaa wamekuja kivingine. Niwaambie, kuna watu walikuwa wanagugumia, wanalia, wanashika matumbo, leo wanatembea vifua mbele, hata hawajaona kitu, kwa kauli ya kiongozi wetu mkuu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. Nampongeza lakini tumwombee kama Watanzania mama huyu asimame kwa hizi kauli anazosema azisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi kilichopita, watu walipata makovu. Kuna Watanzania wanaogopa kuja kwenye nchi yao, kuna Watanzania wana kesi za kubambikiwa, za kisiasa zisizoisha, kesi hazina ushahidi zinapigwa tarehe, hatuwezi kuzizungumzia. Mheshimiwa Mama Samia Suluhu amesema kesi zile zifutwe. Niweze kusema jambo moja, kwenye demokrasia wanasema, bila haki kuonekana inatendeka, demokrasia itakuwa inambwela mbwela. Najua kwa kipindi hiki cha mama yetu, demokrasia itakwenda ku-take place na haki za watu zinaenda kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba mamlaka husika na viongozi ambao wako hapa wenye dhamana waweze kuangalia hii michango ya Wabunge. Wabunge wanachangia kutokana na mambo yanayowakuta huko na wananchi wao, tuweze kuyachukua kwa u-serious ili tuyatekeleze ku-reflect kule nje ambapo tunapotoka. Vinginevyo tutakuwa tunaimba mapambio na mambo hayachukuliwi, yakibaki pale pale tunaonekana huku tunakuja kula bata, lakini huku tumesimama kwa ajili ya wananchi wetu. Tunaomba yachukuliwe kwa u-serious ili yaweze kutekelezwa na wananchi waweze kuona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye sekta hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ninaweza kuzungumzia kwa wavuvi wadogo wadogo. Kwenye Jimbo la Kawe ninapotoka wavuvi wadogo wadogo wapo kwenye kata ya Kunduchi na Kata ya Mbweni, lakini wanachangamoto, changamoto yao kubwa ni Sheria ya Uvuvi ambayo inawabana. Wavuvi hawa wanatakiwa wakiingia majini waingie mita 50, mita 50 kwenye kina ni unatoka Kunduchi una fika Unguja ndiyo unakuta hichi kina. Kwa hiyo, wanapata hii changamoto, lakini wana miundombinu hafifu, wanakuwa na bodi, zile boti engine yake ndiyo unashikia mkononi. Kwa hiyo, mawimbi yakimkuta katika ya bahari anazama na kupoteza maisha tuiangalie hii.

Mheshimiwa Spika, lakini pia ushirikishwaji katika utungaji wa sheria tunaomba wavuvi hawa wadogo wadogo washirikishwe kwa sababu kwenye taarifa zetu, wavuvi wadogo wadogo wanachangia asilimia 98 ya pato la sekta hii, kwa hiyo, tuwaangalie kwa uwangalifu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, changamoto zote wavuvi hawa wameweza kuvuna wastani wa tani 350 za samaki kwa mwaka hichi ni kiwango kidogo ukilinganisha na jinsi gani tulivyo na maeneo yetu, hiki ni kiwango kidogo na kwa sababu ni kiwango kidogo samaki hawatoshelezi kwa soko la ndani. Imelazimisha Serikali kuagiza samaki kutoka nje, samaki zinaagizwa tani 24 kutoka nje ambapo ni sawa na dola za Kimarekani milioni 25 uki-calculate kwa pesa ya Tanzania ni shilingi bilioni 690,000 kwa mwaka. Pesa hii ni nyingi na inakwenda nje kwa sababu sisi hatuna nyenzo za kutosha kusaidia wavuvi wetu wadogo wadogo.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali yangu kwa sababu naona Waheshimiwa Mawaziri ni wasikivu na wanachukua kwa sababu tunapokwenda ni kuzuri, walikuwa wanalalamika nyavu zinachomwa lakini sasa hivi elimu naona inafika na nyavu hazichomwi na sasa hizi milimita 16 imeshaeleweka kwa wavuvi. Kwa hilo, nawapongeza.

Mheshimiwa Spika, lakini nishauri pia tujue idadi halisi ya wavuvi wetu hili tuweze kuwasaidia wavuvi, wanalalamika hawasaidiki kwa sababu hawakopesheki, hatujui hata idadi yao, hatuna jinsi ya kuwasaidia kuweza kupata nyenzo nzuri na thabiti za kuweza kuingia majini.

Niombe Mheshimiwa Waziri unapokuja ku-wind up uweke vitu muhimu na facilities ambazo zitasaidia hawa wavuvi waweze kuingia kwenye deep sea bila ya kupoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, lakini niombe kwa sababu sekta hii ni muhimu sana, tunaweza kutanua wigo, tutanue wigo wa wawekezaji; wenzangu wamesema tutanue wigo kama tunaona tunafika hapa tunaweza kupiga hatua 100 mbele, tutanue wigo, tutafute wawekezaji waweze kuwekeza kwenye hii sekta, tuna utajirisho wa kutosha. Tukiweza kuweza vya kutosha sekta hii inaweza kuwa ya kwanza kwa kuingiza pato la Taifa. Inaweza kuwa ya kwanza kuajiri vijana wetu. Niki-refer kule nyuma kwenye Mpango wetu wa Pili wa maendelea tuli-target mpaka mwaka 2020 asilimia 4.6 ichangie pato la Taifa sekta hii kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, lakini hatukufika kwa sababu hatuna nyezo kwa hiyo hatuna nyenzo, mafunzo na hatuna vifaa muhimu, lakini mpaka 2019/2020 ni asilimia 24 tu ilitengwa katika sekta hii ya uvuvi. Kwa hiyo twende tukapitishe bajeti na itekelezwe ili tuweze kwenda kusaidia watu wetu sekta hii imeajiri vijana, vijana wengi wamekwenda hawana elimu, wapate elimu ya kutosha, lakini tutapata pato la Taifa, tutapata ajira za kutosha, tutapata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa sababu muda ni mchache, nashukuru sana. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyekiti wa Kamati ambaye ametusimamia kwa weledi mkubwa katika Kamati yetu na kuhakikisha mambo haya yanakwenda vizuri. Naenda kwenye kile kipengele cha 9 amendment ya section 22 (a) ambacho kinaonesha moja kwa moja kwamba, kuna vigezo maalum ambavyo vinawekwa ili mtu aweze kufungiwa fire hydrants.

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri aende mbali zaidi kwa sababu tumeona majanga ya moto yakienda kwenye mabweni ya watoto wetu, masoko makubwa, mabenki na kusababisha athari kubwa sana, lakini ukiangalia kwenye level hizo wanaweza wasifikie kwenye vigezo hivi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri itolewe elimu maalum na wale watu waweze kujilinda ili kuepukana na hasara itakayoweza kutokea; mali au watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia katika kipengele hiki ambapo Jeshi la Zimamoto limekuwa jeshi kamili kwa mujibu wa sheria. Tumeshuhudia uhalifu mkubwa wa kiwango kikubwa. Hata juzi tu Karikoo pale wakati soko linaungua huku vibaka wanaingia kwenye ATM Machines wanavunja wanachukua. Kwa hiyo, kitendo cha Jeshi la Zimamoto kupata silaha na kuweza kujilinda na kulinda mali za watu, ni kitendo ambacho kinatakiwa kiungwe mkono kwa sababu jeshi hili kuitwa jeshi bila silaha ni sawa na kibogoyo kupewa mfupa atafune. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Bunge lako Tukufu liridhie jeshi hili kupewa instruments zake zote ili liweze kusimama kama jeshi. Kwa sababu, sometimes wanawaona kama wako legelege, lakini nafikiri utaratibu utafuatwa ili jeshi hili likasimame imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mpaka hapo sitakuwa na mengi ya kusema zaidi ya kushukuru kwa nafasi hii. Nashukuru sana. (Makofi)