Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nusrat Shaaban Hanje (13 total)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kwamba anatambua uhitaji wa kuweka life skills na soft skills kwenye elimu yetu Tanzania.

Je, Serikali iko tayari sasa kwa ajili ya kuendana na mabadiliko ya mfumo ya Sayansi na Teknolojia pamoja kizazi kipya kwa sababu generation inabadilika. Serikali sasa ipo tayari kulifanya, kuifanya topic ya soft skills ambayo inafundishwa kwenye somo la civic kwa form one topic ya kwanza form two topic ya kwanza na form three topic ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari sasa kufanya topic ya life skills iwe somo maalum sasa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inatengenezewa utaratibu mzuri wa upimaji wa uelewa na kuhakikisha kwamba vijana wanapata maarifa zaidi kuliko kusoma kwa ajili ya kujibu mtihani?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, je, lini sasa Serikali itaanza mchakato wa kushirikisha wadau wa elimu wakiwemo wanafunzi wenyewe na watu wa ku-develop mitaala ili kuhakikisha kwamba wanayoyasema yanatekelezwa kwa vitendo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2021/2022 tunakwenda kufanya maboresho na mapitio ya mitaala kama nilivyozungumza hapo awali. Kwa hiyo, suala la kuingiza life skills, suala la kuhuisha mitaala ni suala ambalo lina mchakato mrefu ukiwemo na huo Mheshimiwa Mbunge aliouzungumza.

Kwa hiyo, tutahakikisha tunaenda ku-absolve au kuhusisha na mawazo hayo ambayo ulikuwa nayo maadam tayari hili lilishakuwa ni topic kwenye masomo naweza vilevile tukaifanya kama somo kwa kadri utafiti utakavyotuelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala kwamba ni lini, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2021/2022 tutakwenda kuianza kazi hiyo kwa kadri itakavyowezekana. Ahsante.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mwaka ujao wa fedha tutafanya mapitio ya mitaala. Lakini swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Nusrat alikuwa ameomba kwamba wadau washirikishwe. Nilikuwa nataka kumtoa hofu kwamba Serikali inapoandaa mitaala huwa inawashirikisha wadau na hata sasa hivi tutawashirikisha. (Makofi)

Kwa hiyo, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kama kuna mambo yoyote ambayo wanadhani yanapaswa kuingia katika mitaala yetu Wizara ya Elimu tupo tayari kupokea maoni yenu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna umuhimu sana katika barabara ya Singida – Supuka – Ndago ambayo kimsingi inapita katika Jimbo la Waziri wa Fedha pia.

Je, ni lini sasa Serikali itaichimba angalau kwa kiwango cha changarawe barabara hii ambayo zaidi ya miaka kumi haijafanyiwa marekebisho yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza barabara ya Supuka – Ndago ambako ni Jimbo la Iramba Magharibi ambapo anatokea Waziri wa Fedha wa sasa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Niseme tu kabisa kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na upatikanaji wa mbegu ya alizeti kwa wananchi wa Mkoa wa Singida naomba nimuulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mkoa wa Singida wamekuwa wakilima kwa utaratibu wa kawaida kabisa ule ambao wanalima wakimaliza wanaweka mbegu baada ya kuuza wanabakiza kidogo kwa ajili ya kwenda kulima tena mwakani ndio utaratibu wanaoutumia mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri sasa yupo tayari kwa ajili ya kwenda kukutana na wakulima wa alizeti wa Mkoa wa Singida hususan jimbo la Singida Magharibi kwenye kata za Mwaru, Mgungia, Muhintiri, Minyukhe kwa ajili ya kwenda kuzungumza nao sasa kuona namna gani ambavyo ku-in cooperate mawazo yao na ya Wizara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa mbegu ya alizeti, zinapatikana zenye tija ili walime kilimo ambacho sio cha desturi? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hanje kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenda ku-visit tupo tayari na tutafanya hivyo na Mwenyezi Mungu akijaalia mwezi huu wa Juni tutakuwa na Mkutano mkubwa utakaoongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Mkoa wa Sindiga kwa ajili ya suala la zao la alizeti na kukutana na wazalishaji na wakulima wa alizeti. (Makofi)
MHE. NUSRAT SH. HANJE: Mheshimiwa Spika ahsante, pamoja na majibu Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mkoa wa Singida ni mkoa muhimu sana pamoja na Mkoa wa Dodoma na Simiyu katika uchumi wa nchi, kwa sababu inatambulika kwamba Singida sasa hivi ni pilot kwenye zao la alizeti mahususi kwa ajili ya nchi, kwa hiyo pamoja na jibu lake kwamba mwaka 2022/2023 kwamba ndio ataweka kwenye mpango.

Je, Wizara haioni umuhimu wa kutafakari upya jambo hili kulinganisha na umuhimu wa Mkoa wa Singida kwa sasa kwenye bajeti ya mwaka huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mkoa wa Singida kwenye miundombinu ya barabara bado kuna changamoto sana. Je, Wizara ina mpago gani wa kuhakikisha kwamba inaunganisha Mkoa wa Singida kwa barabara za lami ili kuhakikisha kwamba wakulima wa alizeti na vitunguu wanafikiwa mpaka kwenye vijiji vyao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba nijibu mswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Nusrat kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nifanye marekebisho huu mwaka unasomeka 2021/2022; maana yake kuanzia Julai tathmini inafanyika tuweze kupata gharama ili tulipishe eneo la kipande cha reli ambacho kimetajwa.

Sehemu ya pili; Mheshimiwa Mbunge amesema kuunganisha barabara hizi za lami kwenye eneo lake Mkoa wake wa Singida, ni kweli kwamba tunao utaratibu mzuri wa kila Mkoa, kwa maana Meneja wa TANROADS Mkoa anapaswa kuratibu zoezi la barabara katika Mkoa wake husika. Sasa tupokee hoja yako kama kuna eneo ambalo halipitiki kabisa kwa sasa, nielekeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Singida afanyie kazi kama kuna sehemu ya kuchukua dharura tufanye hivyo ili kufanya maboresho kwa wakulima wa alizeti, vitunguu na maeneo mengine wapate huduma nzuri ya usafiri, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo, tayari wameshaanza kuzichukua kwa kuona umuhimu wa kufanya mapitio ya mitaala yetu ya elimu.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nikufahamu kwa sababu kimsingi wameshafanya makongamano kadhaa ya wadau na marafiki wa elimu kwa ajili ya kukusanya maoni. Lakini wamepitia elimu ya awali, msingi na sekondari kimsingi vyuo na vyuo vikuu bado. Kwa hiyo, niulize sasa Wizara ama Serikali ina mpango gani wa kutuletea pia kufanya mapitio ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kuna maoni ya watanzania wametoa mbalimbali kuna masuala ya kilimo, kuna masuala ya ujasiriamali pamoja na stadi za kimaisha na mambo mengine mengi yote yamejadiliwa. Lakini vyuo na vyuo vikuu ambavyo ndio kimsingi vinatoa watu ambao ndio watenda kazi kwenye nchi. Ni lini sasa Serikali italeta kufanya marekebisho pia ya mtaala na masuala ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo hivyo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nitoe ufafanuzi na kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Hanje. Utaratibu wa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu wana taratibu zao za kuanzisha mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano katika vyuo vikuu seneti ndio chombo kikuu ambacho kina mamlaka ya kuangalia mitaala katika vyuo vikuu na vyuo vya kati vina nyanja tofauti, vyuo vya kilimo viko chini ya Wizara ya Kilimo, vyuo vya utalii viko chini ya Wizara ya Utalii, vyuo vya afya viko chini ya Wizara ya Afya na wote wana taratibu zao. Wizara husika ndio zinakuwa na mabaraza kwa mfano Wizara ya Afya, Baraza la Madaktari ndio linaangalia mitaala ya madaktari, Baraza la Wauguzi linaangalia mitaala ya manesi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kiasi fulani hili jambo labda nilipokee kama Serikali tuangalie namna ya kuliratibu. Kwa sababu, kwa sasa hivi sio vyuo vyote vya kati vinasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Elimu na wala Wizara haihusiki moja kwa moja na kuidhinisha mitaala. Ila imekasimisha mamlaka kwa seneti za vyuo vikuu pamoja na vyombo ambavyo vimewekwa, kwa mujibu wa sheria katika vyuo husika kushughulika na mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu tuangalie namna gani labda kwa kuongezea kabla sijamalizia. Ni kwamba nako pia tumeelekeza wafanye mapitio ya mitaala na katika huu Mradi wa Higher Education tuna fedha ambazo tumetenga, kwa ajili ya kufanya mapitio makubwa na ndio maana mradi unaitwa mageuzi ya kiuchumi na yanajikita katika kuimarisha uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, mapitio ya mitaala yanafanyika kwa hiyo tutaangalia utaratibu mzuri wa kuratibu tupate mapitio yanayofanyika. Ili tuweze kuja kutoa taarifa kwenye chombo muhimu, ambacho ndio kinasimamia sheria na kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kimsingi suala la uraia pacha na Diasporas limefanyiwa mjadala mpana sana kwa muda mrefu sana. Sasa kwa sababu Serikali na niipongeze kwa kufanya jitihada ya kutambua mchango wa Diasporas na tunaamini kwamba wakifungua wakipewa hati maalum ama uraia pacha pamoja na kwamba kuna restriction ya katiba hawaoni sana ifike hatua lifike tamati suala la kujadili masuala la uraia pacha na Diaspora tulifanyie kazi sasa kwa sababu tumeona impact yake ni kubwa zaidi kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo imetuambia sasa hiyo ni ndogo tu tukifungua tutapata faida nyingi Zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni kama imefika hatua tulifanye sasa kwa vitendo suala la kutambua kuwapa hadhi maalum ama kutambua mchango wa Diaspora kiuhalali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa watanzania wanaoishi nje ya Nchi na kama nilivyojibu hapo awali ni kwamba tayari saa hivi Serikali inafanya tafiti ya kuangalia vipi tunaweza tukaangalia uwezekano wa watanzania hawa kupewa hadhi maalum. Hivyo namuomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda kidogo ili kumaliza tafiti na taratibu hizo ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nitauliza maswali pamoja na majibu hayo, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba amezungumiza suala la Kanuni za Magereza ambazo zinataka watoto watengwe tofauti na watu wazima wanapokuwepo Mahabusu. Mlundikano wa Mahabusu kwenye magereza zetu hauruhusu jambo hilo ni kwa nini sasa Serikali isiongeze au isipeleke Maafisa Ustawi wa Jamii ambao watakuwa wanashughulika na Watoto wanapokuwa kule kwa sababu ni vigumu sana ku-monitor. Kwa mfano, Gereza la Segerea kuna mahabusu si chini ya mia moja watoto na Maafisa wapo wawili tu ME na KE. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; kwa nini sasa Serikali isipitie upya kujua idadi ya watoto ambao wana kesi kwenye Mahakama zetu na kwenye Mahabusu zetu yaani kwa maana ya Magereza ili sasa ile sheria kwa jinsi ilivyowekwa na ni nzuri, lakini utekelezaji wake ni mgumu ni kwa nini sasa wasipitie upya ili kuhakikisha kwamba watoto hawa wanasaidiwa kwa sababu hali za watoto wetu kwenye Magereza zetu ni mbaya mno. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum, nayo nayajibu kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa atarejea kwenye jibu langu la msingi atagundua kwamba kuna sehemu nimesema kutakuwa kuna Maafisa wa Ustawi ambao watakuwepo maalum katika magereza kwa ajili ya kusimamia haki na maslahi na kuwalinda watoto hawa. Kwa hiyo, kama changamoto ni Maafisa hawa kuwa kidogo basi nimhakikishie tutajitahidi Serikali kupitia Jeshi la Magereza ili kuona kwamba tunaongeza Maafisa hawa ili watoto wetu waweze kupata huduma nzuri za kuweza kusaidiwa na Maafisa hawa pamoja na kwamba kuna nafasi nyingine ya kushughulikiwa na wazee wao na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa amegusia suala la kwa nini isipitiwe upya sheria au tuone namna, nimwambie kwamba sheria hii kwamba ipo vizuri, lakini kwa kuwa na yeye ameshauri tuipitie upya basi tutakaa tutaipitia sheria hii ili kama kutakuwa kuna mapungufu basi tutajua namna ya kuifanyia marekebisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge pia aliuliza umuhimu wa kujua idadi ya kesi za watoto. Kesi zote zinazokwenda Mahakamani zinasajiliwa kwa namba, kwa hiyo kama atauliza swali mahsusi kwa Mahakama maalumu au kwa Gereza maalum idadi hiyo itapatikana kwa namba na kwa majina ya wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili; Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaweka misingi ya kulinda maslahi ya mtoto. Kwa hiyo, kwa mtu aliyechini ya kizuizi cha magereza anapopelekwa mahakamani kama hapati huduma inayostahili akiwa magereza anayohaki ya kutoa hiyo hoja kwa Hakimu ambapo shauri hilo lipo mbele yake na maelezo ya kisheria kwenda kwa wanaosimamia hizo selo yakatolewa. Nninakushukuru. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa kuwa mifuko hii imeonekana haina tija ya kutosha kwa sababu zinatolewa fedha taslim, ni kwa nini sasa Serikali isije na mpango mbadala wa kutoa facilities (vitendea kazi) na kuwawezesha vijana badala ya kuwapa fedha taslimu ambazo pia zimekuwa hazirudi kwenye Serikali lakini pia haziwafikii vijana wa kutosha. Ni kwa nini sasa wasilete utaratibu wa kuwapa vitendea kazi ili waweze kufanya kazi na tuone kitu kinafanyika?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Hanje Mbunge kama ifuatavyo. Ni kweli kumekuwa na changamoto nyingi kama ambavyo nimesema kwa maana ya kutokuwa na fedha za kutosha mahitaji ya wananchi ambao wanataka kukopeshwa au kupata fedha kutoka kwenye mifuko hii. Lakini lengo la Serikali ni lile lile kuimarisha na kuwasaidia kwa ukaribu zaidi wananchi katika kuwawezesha.

Mheshimiwa Spika, moja ya mifuko ambayo inatoa mikopo hii ni NEDF kupitia SIDO pia tumekuwa tukiwapa ujuzi lakini na wengine vitendea kazi. Lakini sasa baada ya kuwa na lengo hili la kuona namna gani kuunganisha mifuko hii naamini taarifa hiyo ndiyo itakuja na utafiti rasmi wa namna gani ya kuboresha ikiwemo kama ni kuwasaidia vitendea kazi hasa vijana ambao wanakuwa wanakopa fedha hizo au wengine na kutokutimisha lengo la mikopo hiyo nakushukuru.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa lengo ni kuboresha elimu yetu nchini. Ni kwa nini sasa Serikali isipandishe hadhi Shule ya Sekondari Sepuka ambayo ipo Jimbo la Singida Magharibi ambayo kwa sasa ndiyo shule kongwe kuliko shule zote katika Tarafa ya Sepuka ambayo imebeba nusu ya Kata za Jimbo la Singida Magharibi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba ombi la Mheshimiwa Mbunge ni Shule ya Sepuka sijajua ni sekondari ama msingi, lakini naamini ni Sekondari kwenda Kidato cha Tano na cha Sita ambao wanataka tupandishe hadhi na kuwa kidato cha tano na cha sita kwa sababu inapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali. Moja ya mpango wa Serikali ni kufanya upanuzi wa shule za sekondari za Kata 100 katika mwaka 2022 ili tuongeze wigo wa kuongeza wanafunzi wa kwenda kujiunga na kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Spika, naamini kama lipo katika mpango, basi maana yake tutalifanyia kazi katika mwaka huu fedha 2022/2023, lakini kama halipo maana yake tutalifanyia kazi katika mwaka wa fedha unaokuja 2023/2024. Kwa hiyo, nitayapitia ili niweze kujiridhisha nione kama halipo katika mwaka huu, kama litakuwepo mwakani maana yake tutaliingiza, kwa hiyo ni hilo tu. Ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

(a) Je, wanafunzi wanaosoma Chuo cha Diplomasia wanafanya wapi mafunzo kwa vitendo ili sasa lengo la kuanzisha Chuo cha Diplomasia liwe limetimia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imekubali kwamba yaliyokuwa malengo ya msingi kuanzia Chuo cha Diplomasia kwa sasa yamebadilika kutokana na mahitaji ya nchi na pia kutokana na masuala mengine ambayo Serikali wanajua kwanini walipadilisha.

(b) Je, ni kwanini sasa Serikali isione haja ya kupitia upya mfumo wa utoaji elimu kwenye chuo hiki ambacho lengo lake lilikuwa ni kutoa viongozi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hata wanaotolewa katika chuo hiki wahitimu wengi hawatumiwi kama ambavyo lengo la kuanzisha chuo hicho lilivyokuwa. Sasa ni kwanini wasipitie upya ili wanaohitimu katika chuo hicho wawe na tija kwa taifa na Serikali ifikie malengo yake inayosema kwamba inazalisha viongozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kuhusu mafunzo kwa vitendo. Chuo hiki kimsingi kinapowatoa wale wanafunzi wanakwenda kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya field zao, moja ya eneo ambalo wanapewa nafasi ni Wizara ya Mambo ya Nje yenyewe ambako wanafunzi wachache huwa wanapewa nafasi kutokana na ukweli wa uwezo wa Wizara yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maeneo mengine ni kwenye taasisi mbalimbali zenye sura ya Kimataifa, vile vile kule kwenye NGO na maeneo ambayo utendaji wake upo katika sura ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tija, ni kwamba chuo hiki kina tija kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa sasa kimezalisha wanadiplomasia wengi sana ambao wanatumika katika maeneo mbalimbali. Na ukizingatia kwamba tuna hiki chuo kiliboreshwa na kufanyiwa maboresho ya uhakika kimekuwa na sura ya chuo kikuu, na sasa hivi kinatoa hadi shahada ya juu, kama nilivyoieleza hapo, wanatoa hadi masters pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba mafunzo wka vitendo wanapatiwa lakini vile vile tija inaonekana kwenye Nyanja za kimataifa na wasomi wengi sana tumekuwa tukiwatumia katika maeneo mbalimbali, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ni kwa nini sasa Serikali isione haja ya kushirikisha taasisi binafsi za fedha ili ziweze kutanua wigo wa kupata fedha zaidi kwa ajili ya kutoa mikopo na yenyewe ibaki ku-regulate tu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hivi sasa tunaendelea na mazungumzo na taasisi mbalimbali za fedha, lakini katika bajeti yetu ya mwaka 2022/2023 tayari wenzetu wa NMB wameweza kuongeza bajeti yetu ya mikopo kwa ajili ya vijana wetu wa elimu ya juu pamoja na elimu ya kati zaidi ya shilingi bilioni 200. Kwa hiyo kama Serikali tunalifanya hilo na tutaendelea kulifanya.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali kuhusiana na utayari wao kwenye suala la madini muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumeona thamani ya fedha kwenye ongezeko la asilimia 9.4 kwenye bajeti ya GST mwaka wa fedha huu unaoendelea ambapo mapato yame-shoot mpaka asilimia 141.
Ni kwa nini sasa Serikali isilete mkakati wa dharura kwa ajili ya ku-fund GST ili iweze kufanya tafiti za kisayansi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; sasa hivi tunapozungumza GST imefikia wapi na Serikali imefikia wapi kwenye masuala ya critical minerals kwenye utafiti na uchimbaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza; ili kuboresha teknolojia ya kutafuta madini na hasa tafiti ya madini haya ya kisasa, GST kupitia Wizara yetu ya Madini imeanza mkakati rasmi wa kuanzisha mashirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje na kuandika maandiko mahsusi ambayo yatatusaidia kupata fedha za kuwekeza katika utafiti wa madini ya kimkakati. Tuna Kampuni ya Noble Helium ambayo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na GST, tuna Kampuni ya Rocket Tanzania Limited.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kuhusu hatua ambazo tumeshafikia katika kutafiti na kuzalisha madini ya kimkakati; ni kwamba sisi kupitia Tume yetu ya Madini kama Wizara, tayari tunatoa leseni za utafiti wa madini ya kimkakati kwa ajili ya utafutaji wa madini na uchimbaji wa madini. Na Serikali imekuwa na ubia na baadhi ya kampuni hizo na kwa ruhusa yako naomba nitaje chache.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, tuna kampuni inayoitwa Lindi Jumbo Limited wenye leseni ya uchimbaji wa kati na wanaendelea na utafiti na sasa hivi wamefikia hatua ya kuendeleza ujenzi wa eneo la mradi.

Mheshimiwa Spika, hapo hapo Mkoani Lindi tuna Kampuni inaitwa Ngwena Tanzania Limited, wana leseni za utafiti wa madini ya kinywe na sasa hivi wako katika hatua ya uthamini kwa ajili ya ulipaji wa fidia. Na pia wale wa Jumbo nao wanafanya utafiti wa madini ya kinywe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hizi chache nipende tu kumhakikishia kwamba sasa hivi Tanzania imeamka na wawekezaji wakubwa wa ndani na nje wanajihusisha na utafutaji wa madini ya kimkakati. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri alisema kuna ngazi mbalimbali ambazo zinashughulika na hayo, lakini wanaonaje sasa wakati huu wasianzishe jeshi la jamii kama lilivyo Jeshi USU kwa upande wa Maliasili, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jamii inalinda watoto wetu dhidi ya ukatili pamoja na wanawake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Ni kwa nini sasa Serikali isiende kwenye shule zetu kwa ajili ya kuanzisha klabu za stadi za maisha na majukwaa ya stadi za maisha kwa ajili ya kuwajengea watoto wetu uwezo wa kujilinda wenyewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nusrat kama ifuatavyo. Swali lake la kwanza kuhusu Jeshi Jamii; Wizara imejipanga na mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na usalama. Mpango huu umejielekeza kuanzia ngazi ya vijiji hadi mkoa na kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kila eneo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu jukwaa la watoto; Wizara yetu ina majukwaa ya watoto ambayo yanahimiza ulinzi na usalama. Pia yapo mabaraza na clubs za watoto kuanzia shule za msingi, sekondari hadi Vyuo. Klabu hizi zinawafunza watoto na kuwaelimisha waweze kujitambua, kujielewa, kujiamini na kujieleza wakati wowote katika kujikinga na ukatili dhidi ya watoto. (Makofi)