Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Nusrat Shaaban Hanje (13 total)

MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu na kuingiza mbinu tete na stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kiushindani vijana wanaohitimu na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi kupata stadi mbalimbali zikiwemo stadi za maisha na mbinu tete ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ajira na kiteknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itafanya mapitio ya mitaala ya shule za msingi na sekondari ili kuingiza stadi mbalimbali kama vile stadi za maisha hususan stadi za karne ya 21 na mbinu tete. Stadi za karne ya 21 ni pamoja na fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia ya habari na mawasiliano. Stadi na mbinu hizi zitasaidia kuwajengea vijana uwezo wa kiushindani katika soko la ajira. Ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je Serikali ina mpango gani wa kutumia mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora hususani za alizeti ambayo ndio zao la uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa zao la alizeti katika kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula hapa nchini ambapo asilimia 68 ya mafuta ya kula yanatokana na zao hilo ikilinganishwa na mazao mengine ya yanayochangia asilimia 31.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mafuta nchini kwa kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni 40 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya uzalishaji wa mbegu ya Wakala wa Mbegu wa Serikali ili kuzalishaji mbegu za alizeti na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutawezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu za alizeti kutoka tani 538 katika msimu wa 2019/2020 hadi kufikia tani 10,000 za mbegu bora za alizeti mwaka wa fedha 2019/2030 ambazo zitatosha kutumika katika eneo la hekta milioni 1.2 zinazoweza kuzalisha tani 500,000 za mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, kwa kuthamini umuhimu wa zao la alizeti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kugundua na kuzalisha aina mpya ya mbegu bora za alizeti zenye sifa ya kutoa mavuno na mafuta mengi na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa kutoka aina 1 hadi 17 za zao la alizeti katika msimu wa 2019/2020.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

(a) Je, kwa nini kipande cha reli ya kati kutoka Manyoni hadi Singida hakipo kwenye mpango wa ukarabati?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati kipande hicho cha reli ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mpango wa ukarabati wa mtandao wa reli iliyopo na kufufua njia za reli zilizofungwa kwa awamu kwa kuanzia na njia kuu (main line). Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali inazingatia Mpango wa Miaka Mitano wa Taifa ambao unaanzia 2021/ 2022 – 2025/2026. Aidha, Serikali itaendelea na ukarabati wa matawi ya reli ikiwemo kipande cha reli kutoka Manyoni hadi Singida kulingana na mahitaji ya ukuajiwa uchumi na uwezo wa kifedha. Lengo la Serikali ni kuboresha miundombinu ya reli ili kurahisisha huduma za uchukuzi nchini.

Mheshimiwa Spika, sehemu (b); Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo na miundombinu ya reli imara katika kuchochea uchumi wa nchi. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi sehemu (a), Serikali itaendelea kufungua njia zote zilizokuwa zimefungwa ikiwa ni mkakati wake wa kurejesha huduma za usafiri wa reli wenye uhakika nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TRC imepanga kufanya tathmini kwa ajili ya ufunguaji wa njia zilizokuwa zimefungwa kwa lengo la kujua gharama za ukarabati. Maeneo ya reli yatakayohusika ni pamoja na Kilosa – Kidatu na Manyoni – Singida. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba Serikali inafanya kazi eneo la reli Manyoni – Singida, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha Mahabusu/Magereza ya Watoto na Watu wazima ili kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyoweza kujitokeza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kulinda haki ya mtoto, Serikali ilitunga Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 ambayo inakataza kifungo kwa watoto na kuweka mahabusu magerezani na iwapo italazimu kuwekwa mahabusu sharti awe chini ya uangalizi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii au mahabusu za nyumbani au chini ya uangalizi wa taasisi yeyote itakayotamkwa katika amri ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Jeshi la Magereza za Mwaka 2003 Toleo la 4, chini ya Kanuni 488 zimeweka utaratibu mzuri wa kuwatenga wafungwa na mahabusu katika sehemu maalum na vyumba maalum kwa kuzingatia umri ambapo wafungwa na mahabusu watoto hutengwa katika mabweni yao maalum pasipo kuchanganywa na wakubwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali inalo Gereza la Wami ambalo ni maalum kwa watoto ama vijana waliokatika ukinzani wa sheria na kuhukumiwa vifungo ambavyo huhamishiwa huko na kutumikia vifungo vyao wakiwa peke yao kama vijana bila ya kufungwa na watu wazima.

Mheshimiwa Spika, aidha Serikali inaendelea kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kingono na ukatili mwingine na kusimamia ipasavyo Sheria ya Watoto na Sheria zingine nchini zinazotoa ulinzi kwa watoto. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, ni yapi yalikuwa malengo ya Serikali kuanzisha Chuo cha Diplomasia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia hapo awali kilikuwa ni chuo cha kimkakati ambacho kilianzishwa kwa ushirikiano kati Tanzania na Msumbiji kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali katika nyanja za kidiplomasia na uongozi katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutoka katika hizo nchi mbili. Kutokana na ubora cha chuo hiki Serikali ilifanya maboresho kwa kuongeza mitaala na kilianzisha kozi katika ngazi ya cheti, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na shahada ya uzamili ambazo zilianza kujumuisha wanafunzi kutoka nje ya mfumo wa watumishi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa chuo kimezalisha wanadiplomasia wengi ambao wameweza kuajiliwa katika Serikali yetu, sekta binafsi pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa. Hivyo, chuo kimefikia lengo lake baada ya kufanyika kwa maboresho husika na kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa letu na wananchi kwa ujumla.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani kuiwezesha GST kufanya utafiti wa kisayansi na teknolojia kuhusu Critical Minerals ili kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeielekeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuandaa taarifa kuhusiana na madini mkakati (Strategic/Critical Minerals) hasa madini teknolojia ikiwemo madini muhimu kwa ajili ya nishati ya kijani (green energy minerals). GST imeanza kuandaa andiko kuhusiana na madini haya na kuainisha ni madini yapi ndiyo ya kimkakati kwa mtizamo wa dunia na nchi, matumizi ya madini hayo na mahala yanapopatikana.

Aidha, GST imebaini maeneo ya kufanya tafiti za jiofizikia katika maeneo sita (blocks) kwa nishati ya kijani (green energy) na matumizi ya magari ya umeme. Serikali inaendelea kutafuta wadau wa maendeleo ambao watashirikiana katika kufanya tafiti za jiosayansi. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je? Serikali ina mkakati gani wa kuzuia ukatali wa kijinsia na utumikishwaji wa watoto katika makambi yanayotarajiwa kujengwa ili kuwezesha ujenzi wa Bomba la Mafuta Hoima Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia na utumikishaji wa watoto vinakomeshwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mradi wa bomba la mafuta Hoima Tanga, kupitia MTAKUWWA Wizara yangu imejipanga kuimarisha na kuzijengea uwezo Kamati za Ulinzi na Usalama kwa watoto kwa vile Serikali itaendelea kutumia vyombo vya dola kuhakikisha wale wote wanaotumikisha watoto na kufanya vitendo vya ukatili wanachukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je ni lini Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya Kati nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu Swali la Mheshiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa elimu ya kati katika maendeleo ya nchi, Serikali imeendelea kugharamia uendeshaji wa vyuo vya kati kupitia ruzuku ambapo kwa mwaka 2022/2023, imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 41.47 kwa wanafunzi 2,435 waliopo katika vyuo vya kati wanaosoma fani za sayansi na ufundi. Aidha, Serikali inakamilisha taratibu za kuwezesha mikopo kutolewa kwa ajili ya elimu ya kati.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, kwa namna gani Serikali inatekeleza Kanuni ya Kimtandao ya Network Neutrality katika utoaji na upatikanaji wa huduma za jamii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya Network Neutrality ni hali ya kuweka usawa katika huduma zote zinazopatikana kwenye mtandao wa intaneti bila kuathiri kasi, gharama wala upendeleo wa tovuti fulani au maudhui ya aina fulani mtandaoni. Serikali inasimamia Sekta ya Mawasiliano kwa kuzingatia kikamilifu Kanuni ya Kimtandao ya Network Neutrality ambapo mtoa huduma yeyote wa mtandao wa intaneti anaruhusiwa kutoa huduma ya mtandao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeweka utaratibu wa kuwezesha watoa huduma kutoza gharama za data bila kujali ni ya matumizi ya mitandao gani ya kijamii, tovuti au programu tumizi mbalimbali.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, ni fursa gani za uwekezaji zinapatikana Tanzania?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba uniruhusu nitumie dakika moja tu kutoa shukurani. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyonipa kumsaidia katika ofisi yake katika eneo la mipango na uwekezaji. Nimuahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa bidii na utii wa hali ya juu kwake, kwa Serikali yake, kwa nchi yetu na kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa ushirikiano ambao ulinipa nikiwa Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati yako, nakushukuru sana lakini niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano na niwaombe wanipe ushirikiano katika hatua hii ambayo ninayo kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naomba sasa nijibu swali namba tano la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali. Naomba nitaje sekta tano tu kwanza, katika sekta ya kilimo tunazo fursa za uwekezaji katika kuongeza thamani ya mazao. Tunayo pia fursa ya kilimo katika mazao ya kipaumbele kama vile mafuta ya kula, sukari na ngano. Tunazo pia fursa katika eneo la utalii hasa katika ujenzi wa hoteli na makazi, tunazo fursa katika eneo la viwanda hasa katika viwanda vinavyolenga uzalishaji wa mbolea, dawa za mifugo na binadamu, nguo na mavazi na bidhaa za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati na gesi tunazo fursa za uwekezaji katika kuzalishaji nishati, katika uvunaji wa gesi na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi. Tunazo pia fursa katika eneo la madini hasa katika maeneo ya utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani ya madini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, lini Serikali itapitia Mtaala wa Vyuo Vikuu ili kufungamanisha elimu sambamba na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu. Katika ngazi ya Vyuo Vikuu, kikanuni, mitaala huandaliwa na Vyuo Vikuu vyenyewe kisha kuidhinishwa na Seneti na kuwasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu kwa ajili ya uhakiki na ithibati. Hata hivyo, tayari Wizara yangu imeshatoa maelekezo kwa Vyuo Vikuu kuhuisha na kufanya maboresho ya mitaala yote ili iendane na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa ambayo kwa sasa inalenga kutoa Elimu itakayompa kijana wa Kitanzania elimu na ujuzi kwa mujibu wa mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Spika, Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) vimepata mafunzo mbalimbali ya kuandaa programu zinazoendana na vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira. Aidha, Vyuo vimeunda Kamati za Ushauri wa Insia (Industrial Advisory Committees) zenye Wajumbe kutoka Sekta za Waajiri kwa ajili ya kuzishauri Taasisi za Elimu ya Juu kutoa programu zinazoendana na soko la ajira. Kupitia utaratibu huu, zaidi ya programu 300 zitaanzishwa au kuhuishwa ili kuendana na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa sambamba na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira, ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, Serikali inatumia utaratibu gani kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mipango na Bajeti zinazopitishwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali husimamia na kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti zinazopitishwa na Bunge kwa utaratibu ufuatao: -

(a) Wizara ya Fedha na Mipango kila mwaka huandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi na Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali;

(b) Kutoa Waraka Na.1 wa Mwaka wa Fedha wa utekelezaji wa bajeti unaoelekeza na kusisitiza utekelezaji wa vipaumbele;

(c) Kuandaa mwongozo wa maombi na utoaji fedha kwa lengo la kuhakikisha fedha inatolewa wakati wa uhitaji na inatumika kwa wakati;

(d) Kusimamia uwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti na ambazo huchambuliwa ili kutathmini utekelezaji wa mipango kwa kuoanisha na malengo tarajiwa na bajeti zilizotengwa; na

(e) Kubainisha viashiria hatarishi vya utekelezaji wa bajeti na kufanya ufuatiliaji na tathmini ili kujiridhisha na uhalisia na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, Serikali imetekeleza kwa kiwango gani Mkakati wa Afrika wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STISA – 2024) kufuatia maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na ubunifu duniani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Mkakati wa Afrika wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu uitwao STISA 2024 mwaka 2015 kwa kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati husika. Utekelezaji umejikita katika maeneo yafuatayo; eneo la kwanza ni kuweka mazingira wezeshi ya watafiti na wabunifu kwa ujumla kwa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya utafiti na ubunifu kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia yaani MTUSATE; eneo la pili ni kuimarisha miundombinu ya utafiti na ubunifu kwa kuongeza idadi na kuwajengea uwezo watafiti na wabunifu kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Vituo vya Umahiri yaani ACE-II; Mradi wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi (ESPJ); Mradi wa Afrika Mashariki wa Kuboresha Mafunzo ya Ufundi (EASTRIP) na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Uchumi (HEET); na eneo la tatu ni kuimarisha mahusiano kati ya Taasisi za ubunifu /utafiti na sekta za viwanda, nakushukuru sana.