Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nusrat Shaaban Hanje (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa muda nizungumze.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kabla sijazungumza kwa sababu na mimi ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili la Kumi na Mbili, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na kunijaalia kila kitu mpaka hapa nilipofika. Pia niwashukuru wazazi wangu na familia yangu na watu wangu wote ambao wako karibu na wananifahamu wanajua nini kinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kuzindua Bunge la Kumi na Mbili iliyotolewa Novemba 2020, niseme kabisa nimesikilizia hotuba hiyo nikitokea gereza la Isanga ambako nilikuwa mahabusu pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo mawili, eneo la kwanza nitachangia katika ukurasa 13 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2020 ambako amezungumza na nitaanzia na hilo kwa sababu amezungumza kwenye hotuba yake kwamba ndiyo jambo la kwanza na la umuhimu ambalo anafikiri katika Serikali yake kwa muda wa miaka mitano atashughulika nalo ambalo ni kulinda na kudumisha amani ya nchi umoja, uhuru na mshikamano pamoja na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kwa uzito wa hoja hiyo na mimi naomba nichangie kwenye hoja hiyo kwa yafuatayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nia ya dhati ya kulinda amani ya nchi, kwa sababu wote tunafahamu kwamba amani ni tunda la haki, kwa hiyo, kimsingi unapozungumza kwamba Serikali imejipanga kulinda amani ya nchi lakini pia kulinda mshikamano wa nchi huwezi ku-ignore vitu vidogo vidogo ambavyo vinaonekana kama tunazungumza vitu vingine na tunatenda vitu vingine. Ninasema hivi kwa sababu naona hapa kama vile hawa wanazungumza hawa wanajibu lakini kimsingi kuna mambo ya msingi ambayo wote tunakumbuka, mimi nitasema deep down kila mtu anajua kwamba there was something very wrong kwenye uchaguzi wa 2020.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Kuhusu Utaratibu.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anajua moyoni kwake kulikuwa kuna mambo ambayo si ya kawaida mpaka watu ambao si wanasiasa walikuwa wanajua, watu wanaofuatilia demokrasia ya nchi yetu, watu wanaofuatilia taratibu za uchaguzi kwenye nchi yetu walikuwa wanajua kuna shida kubwa imetokea kwenye uchaguzi wa 2020. That is the fact kwa sababu fact hazibishaniwi. Kwa hiyo, sitaenda into details nini kilitokea kwa sababu kila mtu anafahamu nini kilitokea Zanzibar, watu waliwekwa ndani, kesi zaidi ya 20 na kimsingi mpaka sasa kuna kesi mbili tu na sitaenda kwenye details kwa sababu najua kuna kanuni zinanizuia kuzungumza masuala ya kimahakama.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat, naomba ukae.

Mheshimiwa Ali King, kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 70 (1) mpaka 9 inaeleza kuhusu kusema ukweli au kuhusu kusema uongo. Mheshimiwa aliyekaa kitako, Mheshimiwa Nusrat Hanje anazungumza kwamba vyombo vyote ambavyo vilikuwa vinashughulikia uchaguzi huu vimethibitisha kwamba uchaguzi haukuwa mzuri au haukuwa huru na haki kwa mujibu wa maneno ambayo ameyatumia.

Mimi namthibitishia kwamba vyombo hivyo vyote vilivyoruhusiwa na kujihusisha na uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi na observers wote walithibitisha kwamba uchaguzi ulikuwa uko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Uchaguzi ndiyo iliyotoa matokeo ya uchaguzi kwa sababu uchaguzi ulikuwa huru. Ma-observers wa Umoja wa Afrika, EISA ya South Africa, Umoja wa Ulaya na East Africa wote hawa walisema uchaguzi ulikuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa afute kauli yake au athibitishe chombo gani ambacho kilikuwa kina authority ambacho kimethibitisha uchaguzi haukuwa sawa. Nashukuru. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, alikuwa anachangia Mheshimiwa Nusrat Hanje, kwa mchango wake akasimama Mheshimiwa Ali King kuonesha kwamba anachokizungumza au anachochangia Mheshimiwa Nusrat kinavunja Kanuni ya 70 ambayo inakataza Waheshimiwa Wabunge wanapotoa michango yao kusema uongo Bungeni.

Mheshimiwa Ali King ameeleza yeye kwa kuvitaja ama kwa kuzitaja taasisi alizoona kwamba zilionesha kwamba uchaguzi huo ni huru. Wakati wote tukimsikiliza Mheshimiwa Nusrat nilikuwa najaribu kusikiliza hoja yake ni ipi kwa sababu ameeleza mambo ambayo yako jumla hajasema mahsusi, kwa hiyo nilikuwa nasikiliza hoja yake nijue inaelekea wapi.

Kwa hiyo, pengine atakuwa pia na mifano kama ambavyo ziko taasisi, ama viko vyombo ambavyo vimesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Kwa hiyo, pengine viko vyombo vya habari, ama taarifa, ama taasisi zilizosema haukuwa! Kwa hiyo, mnipe fursa nisikilize mchango wake halafu nijue hoja yake inaishia wapi kwa sababu kwa sasa inanipa vigumu kidogo kutoa mwongozo mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Nusrat, ushauri wa jumla umesikiliza Waheshimiwa Wabunge wakichangia pande zote, hata wa huku umewasikiliza wakichangia hoja ambazo hauna uthibitisho mahususi zinatakiwa kusemwa kwa namna ambayo hutaambiwa ulete ushahidi, kwa hiyo, huo ni ushauri wa jumla, malizia ushauri wako.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi nilizungumza nikasema deep down ndani ya moyo wako kila mtu anajua kulikuwa kuna shida mahali kwenye uchaguzi wa 2020, kila mtu atajitafakari yeye na Mungu wake anajua hicho ndio nilichokizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia labda nishauri jambo moja ambalo ndio hoja ilikuwa hiyo, kama ni kweli umeshinda kihalali na umeshinda, kimsingi sitaki kwenda kwenye uchaguzi kwa sababu Taifa linasonga mbele na kimsingi Watanzania wana matumaini makubwa na pengine namba ndogo ambayo imepatikana na watu ambao wataleta chachu fulani kwenye Bunge hili. Kwa hiyo, wacha tu mwiba utokee ulipoingilia.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, wacha tu mwiba utokee ulipoingilia. Kwa hiyo, kimsingi, nashauri kama kuna kesi ambazo zilitokana na uchaguzi…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri, Mheshimiwa Rais kwa sababu ya hotuba yake…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge mniruhusu hapa mbele nina majina mengi kwa hiyo hapana! Mheshimiwa Halima tafadhali! Kuhusu taarifa sitaziruhusu ili majina yaweze kuisha hapa, isipokuwa kama mtu anavunja kanuni hilo halivumiliki na Bunge kwa sababu muda tulionao ni mfupi na majina ni mengi. Mheshimiwa Nusrat. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri ambao wanahusika na masuala ya kisheria na kimahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi uchaguzi umeisha tujenge Taifa si ndio hivyo tunazungumza hivyo, sasa twende ili tusonge mbele. Kuna watu mpaka leo bado wanasumbuliwa mahakamani na kesi za uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kama kuna watu wanahusika na hayo mambo waachieni watu wakafanye maisha yao, kwa nini bado wanaenda mahakamani mpaka Mheshimiwa Salome Makamba bado ana kesi ya uchaguzi, tuna kesi zipatazo 20 Mainland na Visiwani. Sasa watu wa ACT kule kuna vitu walifanya huko na nini kesi zimepunguzwa mpaka zimebaki mbili ya Nassoro Mazrui na mwenzake yule Ally Omar Shekha. Kwa hiyo, kimsingi nashauri hivyo hatuna haja waache basi watu waendelee na mambo yao unawashikilia watu kwenye kesi za uchaguzi ambao unajua uchaguzi wenyewe yaani mtu unamchukulia mkewe halafu unataka kumuua, come on! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo la pili ambalo nataka kumalizia ni kuhusiana na masuala ya mahakama. Kwenye hotuba ya mwaka 2015 ya kufungua Bunge kwa maana ya Bunge la Kumi na Moja na Bunge la Kumi na Mbili, Mheshimiwa Rais alizungumzia suala zima la mahakama na ni miongoni mwa watu ambao nimeishi kwa vitendo na ninashuhudia vitu ambavyo vinafanyika kwenye mahakama zetu na kwenye magereza zetu. Kimsingi kuna tatizo kubwa sana na yeye alizungumza na akashauri kwamba wajaribu kurekebisha mifumo ya uendeshaji kesi ili kusiwe na mrundikano wa watu wengi sana kwenye magereza zetu. Kimsingi huwezi kutenganisha magereza, wafungwa, mahabusu na mahakama. Kwa hiyo, tukizungumza mahakama maana yake haya mambo yote yanahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunapozungumza tishio la COVID na mrundikano wa watu ambao wana kesi za upelelezi za miaka zaidi ya kumi kwenye magereza ni jambo la hatari kiafya. Mheshimiwa Waziri wa Afya yupo anasikia, kule kuna changamoto kubwa na niseme, Bunge likiwa hapa watu wale wadada zetu wale wengine wanafanya shughuli zao nyingine wanakuja, wakija hapa kila siku wanakamatwa wanapelekwa hapo, mimi nimekaa hapo Isanga, wanakuja pale tunaitaga kontena jipya mpaka wanatenga cell maalum ya watu wanaoletwa ambao wanaondoka na kuja ambayo unajua huyu wiki ijayo atakuja tena kwa sababu atakamatwa tena uzururaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, labda nishauri kuna vitu vya kurekebisha, Mheshimiwa Rais sijui kama wale wanaomshauri au pia Waziri kuna jambo moja la digital platform ya kuendesha kesi, siyo lazima watu wahudhurie mahakamani, lakini pia itasaidia kupunguza mlolongo wa kesi, kwa sababu kulikuwa kuna malalamiko kwenye kipindi cha corona watu walikuwa hawaendi kabisa mahakamani kwa sababu kila mtu alikuwa anajua mikusanyiko ilikuwa haitakiwi. Walijaribu kidogo kuendesha kesi kwa kupitia digital platform zoom, Jaji huko aliko kesi zinaamuliwa, nafikiri waongezewe uwezo wafanye kazi ili tupunguze milolongo na mrundikano wa kesi kwenye magereza zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, huwezi kuanza na jambo jipya.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Naomba nianze kwa kutoa masikitiko yangu kwa Waheshimiwa Wabunge vijana ambao wako kwenye Bunge hili ambao kimsingi zaidi ya asilimia 60 ni vijana. Natoa masikitiko yangu kwa sababu kama vijana, tunao wajibu kama ambavyo kila kizazi kina wajibu wake, kama vijana tunao wajibu wa kulisaidia Taifa hili kwa sababu tuna Tanzania moja tu, sasa haiwezekani vijana tuko zaidi ya asilimia 60 kwenye Bunge hili lakini tunashindwa kutoa msaada kwa ajili ya kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa vijana ambao wengine wameshachangia, lakini najua wanaweza kuchangia tena kwa maandishi wakashauri yaliyo bora na mema kwa ajili ya Taifa hili. Ambao bado, nawashauri, hatuna Tanzania nyingine, tuna Tanzania hii moja, tutoe michango yenye tija kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat, nasikia kuna taarifa mahali. Hebu ngoja tuelewane kidogo. Subiri kwanza Mheshimiwa Saashisha.

Mheshimiwa Nusrat, takwimu za kuwatuhumu vijana wote humu ndani, unamaanisha hakuna kijana aliyesimama akatoa mchango! Yaani wataanzia kutoa mchango baada ya wewe kutoa mchango? Maana umeisema kwa namna kana kwamba vijana wote waliochangia, hakuna wazo walilotoa kabisa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Afute kauli.

MWENYEKITI: Hiyo haikai sawasawa. Nanyi mnakumbuka takwimu alizozitoa Mheshimiwa Spika humu ndani. Mimi nilisikiliza michango yote, nami huhudhuria Bunge kila siku, Wabunge vijana wanafanya kazi nzuri.

MBUNGE FULANI: Alikuwa gerezani, arudishwe ndani.

MWENYEKITI: Wanaishauri Serikali, wametoa mawazo ya kuboresha maisha ya vijana. Wameeleza kuhusu mikopo, kuwekeza kwenye mitandao, kilimo na kuhusu Benki ya Vijana. Tunataka nini jamani? Mheshimiwa Nusrat, ongezea pale ambapo wenzako wamechangia. Lile ambalo wenzako hawajaliona, changia wewe, lakini usioneshe kana kwamba hakuna kijana anayetoa mchango humu ndani isipokuwa wewe. Hapana, hiyo haikai sawasawa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Anawaza kufukuzwa kwenye chama.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat endelea. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Labda ningefika mpaka mwisho ndiyo mngejua namaanisha nini.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-recognize kwa waliyozungumza, kwa sababu kimsingi hakuna tupu iliyo tupu kabisa. Kwa hiyo, kuna waliyoyazungumza.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hanje, ngoja kwanza. Hebu tutulie kidogo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimesimama.

MBUNGE FULANI: Kutachafuka humu ndani! Vijana tumeongea, tumefanya kazi kubwa! Kutachafuka humu!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimesimama, kwa hiyo, mkae. (Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge, tuelewane jambo moja. Nimeeleza hapa kwa kirefu nikiwa nimekaa. Nimelazimika kusimama kwa sababu Bunge hili watu wanaotakiwa kusimamia utaratibu ni wale wanaosimamia vikao. Na mimi nimeeleza vizuri; michango ya vijana waliopita, wa vyama vyote ambao wameshachangia, wamefanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)

Hiyo michango waliyoitoa ni ya muhimu yote. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sana!

MWENYEKITI: Hakuna kijana aliyesimama hapa ambaye hajatoa mchango wa muhimu kwenye mapendekezo haya ya Mpango. Kwa muktadha huo, ndiyo maana nimemwambia Mheshimiwa Nusrat, naye ni kijana, aanzie pale ambapo wenzake wameishia, achangie mchango wake. Yale ambayo wanaona…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mtulie kidogo, mkitajwa majina, mnakuwa wa kwanza. Mtulie msikilize. Nikiwa nimesimama hakuna mtu anaruhusiwa kuzungumza. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kweli! (Makofi)

MWENYEKITI: Tuelewane vizuri; na tuheshimiane. Nikiwa nimesimama, Bunge linatakiwa kutulia.

MBUNGE FULANI: Sawa.

MWENYEKITI: It is only me who should be speaking because I have the right to speak. (Makofi/Kicheko)

Kwa hiyo, nikiwa nazungumza, kila mtu anapaswa kunyamaza. Ndiyo kanuni zetu zinavyosema. Tusome Kanuni, tuzielewe ili humu ndani tuheshimiane kama tunavyoitana Waheshimiwa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, hoja ya kwamba hakuna tupu, tupu kabisa, hakuna Mbunge yeyote aliyemtupu humu ndani. Kila Mbunge analo jambo ambalo wale waliomtuma wanaamini atalifanya humu ndani. Ndiyo maana kanuni zinamlinda kila Mbunge anapopata fursa ya kuchangia. Nami ni kazi yangu kumlinda kila Mbunge kwa mujibu wa kanuni zetu. (Makofi)

Bunge letu hili, alishasema Mheshimiwa Spika wakati linaanza, tukiamua kuliletea dharau, tunajidharau wenyewe. Tukiamua kuliheshimu, tunalitafutia heshima sisi wenyewe. Kwa hiyo, humu ndani tuheshimiane kama ambavyo sisi tumeamua kuheshimiana na wale waliotutuma wanatuita Waheshimiwa. Kila Mbunge anao mchango wake, hakuna Mbunge aliye tupu humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nizungumze, kwa sababu mipango ilikuwa imepangwa kwa miaka 15 kwa miaka mitano mitano, for the last ten years, ripoti za CAG zinaonyesha kuna failure kubwa sana katika utekelezaji wa mipango. Bajeti zinapangwa, mambo hayaendi kwa sababu…

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea Mbunge akaweka mapendekezo au akazungumza…

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat kuna taarifa. Mheshimiwa Jaqueline Msongozi.

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza, kwanza afute kauli yake aliyoongea kwanza, halafu ndiyo aendelee na mchango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Kicheko/Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walzungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimeshatoa maelezo ya namna ya kwenda kuanzia hapa tulipo. Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nazungumza kwamba, tunafeli kwa sababu hatuna sheria. Ibara ya 63(3)(c) inaruhusu Bunge kutunga sheria ya kusimamia mipango kwa ajili ya kusaidia uwajibikaji na kusaidia mipango kufanya kazi. Mpaka sasa for the last ten years hatujawahi kuletewa Muswada. By then mimi nimekuja lakini hakuna Muswada uliowahi kuletwa hapa Bungeni (If I am not right, kuna wakongwe watasema) kwa ajili ya kusaidia ufanikishaji na usimamiaji wa mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kila siku tunapanga, tunarudi hapa kwenye kilimo. Tunaona kabisa tumetoka hatua moja, tumeenda hatua mbili mbele, tumerudi nane nyuma. Tunarudi tunasema tunapanga tena. Bajeti haiendi mathalan…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: … bajeti ya maendeleo imetekelezwa kwa asilimia 17.55.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat kuna taarifa. Mheshimiwa Ndaisaba.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumpatia taarifa Mheshimiwa Nusrat. Katika maelezo yake amesema kwamba tunafeli kwa sababu hatuna sheria ya kusimamia mipango. Naomba nimfahamishe kwamba kila jambo linalotungwa; bajeti ya Serikali, lina sheria mama na lina-fall kwenye specific category ambayo ina sheria zake. Ukienda kwenye kilimo kuna sheria, kwenye maji kuna sheria, kwenye barabara kuna sheria. Sheria zile ndizo zinazoratibu utekelezaji wa mipango ya Serikali

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo sheria nyingine anayotaka iibuke sheria juu ya sheria ni ya namna gani? Naomba apokee taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu nimezungumza kitu kingine na amezungumza kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wabunge sasa hicho nilichokizungumza kama vijana tungeweza kusimama pamoja tukashauri Serikali ilete Muswada kwa ajili ya kuhakikisha mipango tunayoipanga, itekelezwe ili tuepuke budget reallocation, tuepuke kutokupeleka bajeti kama zinavyopangwa kwenye Bunge la Bajeti, wanapanga bajeti hazipelekwi, Mpango wa Maendeleo…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: … bajeti ya maendeleo kwenye kilimo imepelekwa asilimia 17.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: …asilimia 82 haijapelekwa…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, kwa Mheshimiwa Nusrat hii itakuwa taarifa ya mwisho. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anayeongea ni kana kwamba sisi wazee ama wenye umri mkubwa, hatustahiki kuchangia Mpango wa Maendeleo. Tumeletwa na wananchi na wametuamini pamoja na umri wetu kuja kuchangia maendeleo na kufikisha mipango yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa, vijana wanataka kuleta ubaguzi wakati tumeongoza kwenye kura kwa asilimia nyingi pamoja na umri wetu mkubwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tumsikilize. Mheshimiwa Nusrat, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mzee wangu shikamoo! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaheshimu wazee wote, lakini tunafahamu hata Wamasai wapo humu ndani, morani; huwezi kufananisha age. Yaani hiyo age conflict. Ila nawaheshimu sana wazee wangu. Mpo! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza kwamba bajeti ya maendeleo kwenye kilimo haijaenda kwa asilimia 82. Tuna shida ya mbegu kwenye Taifa, tuna tatizo la mbegu kwenye Taifa, lakini Serikali imetenga mashamba tisa ya kuzalisha mbegu. Ni shamba moja tu ambalo linazalisha mbegu, linafanya kazi mwaka mzima. Mashamba mengine yote nane yanategemea kilimo kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwenye jambo moja. Mheshimiwa Spika juzi alivyokuwa kwenye kiti alitoa mfano akasema anatamani tupate kitu cha ziada kuwasaidia vijana wetu, anachukia kuwaona wako kwenye pool table. Naomba ku-declare interest, mimi ni Mwalimu. Kama nchi, tuna tatizo kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu, watoto wetu wanakosa vitu vitatu vya msingi na Waziri wa Elimu yupo asikilize. Elimu yetu haina career guidance, haina personal development. Leo tunazungumza soft skills, wasomi wengi wanaotoka vyuo vikuu, inawezekana nikiwemo mimi na wengi wetu humu na wengine wako nje, tunakosa vitu vya msingi. Tunafundishwa kwenye Civics Communication Skills, tunafundishwa self-esteem, self-confidence na nini, lakini tunashindwa ku-connect na maisha halisi. Ndiyo maana kuna motivation speakers. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Eric Shigongo yule pale anaelewa, ndiyo maana leo kuna motivation speakers wengi kwa sababu tunashindwa, yaani hatuwezi ku-connect maisha ya shule na nini kipo mtaani, ndiyo maana watu hawawezi kujiongeza. Falsafa ya Kuanzia sokoni, watu walitakiwa wajifunze shule, siyo wanamaliza shule, ndiyo wanatoka wanakuja kuambiwa kwenye biashara tuanzie sokoni. No!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kitu kingine cha msingi tunakosa. Leo Waheshimiwa Wabunge wanakalishwa chini wanafundishwa investment, shule wanasoma pesa, lakini hawasomi financial management; elimu yetu inakosa financial management; tunasoma Book Keeping na Commerce (makabati), haina reality kwenye ukweli. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatoa mchango wangu pia kwenye maandishi kuhusiana na elimu; nishauri kwa sababu kila mtu ana akili (everybody is genius), lakini if you judge a fish by its ability to climb a tree, anaishi maisha yake yote hajui kama yeye ana akili. Kwa hiyo, naweza nikashauri hiyo kwa sababu natamani kuona tunafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naishia hapo. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza kwasababu ni mara yangu ya kwanza tangu tumepata janga kubwa la Taifa kuzungumza hapa nitoe pole kwa Watanzania wote kwa msiba mkubwa tulioupata wa kuondokewa na Mheshimiwa Rais, lakini pia nitoe pole kwa Mheshimiwa Rais mteule Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rais ambaye yeye alikuwa msaidizi wake wa kwanza na wa karibu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais mteule Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kwa kuwa Rais.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Philip Mpango kwa kuteuliwa kwa mujibu wa Katiba kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, lakini pia niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa kuendelea kuwa pamoja na nchi yetu kutokana na kipindi ambacho tumepitia cha mpito na mambo magumu ambayo tumepitia.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie na nitachangia kwenye Sekta za uzalishaji na nitajikita katika sekta ya kilimo, kwasababu Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na tunajua tumekuwa tukitumia kauli hiyo tangu tunasoma; lakini pia practicability yaani utekelezaji wa maendeleo ya Taifa tunategemea sana kilimo kwa sababu kama tunazungumza Tanzania ya Viwanda na kama mwelekeo wa Serikali maana yake hatuwezi kuzungumza viwanda bila kilimo.

Mheshimiwa Spika, na kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamekuwa wana champion hoja ya kilimo, kwabababu utakumbuka hata mzungumzaji aliyepita amezungumza pia kilimo, na ninajua Waheshimiwa Wabunge wengi sisi kama nchi wengi tunajua tunalima kwa namna tofauti tofauti, lakini pia tunajua umuhimu; wake, kama ambavyo Mwenyekiti wa Kamati ametoka kuzungumza. Kwamba tunahitaji malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu kwasababu tunategemea malighafi za ndani sasa hauwezi kuzungumza malighafi za ndani bila kuzungumza kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa pekee sana kwa mujibu wa ripoti ya CAG na mambo ambayo amechambua kwenye ripoti yake, ukiangalia mpango wa kwanza na wa pili kwasababu tunazungumza Mpango wa Tatu lakini wakati tuko sasa hivi lazima tukumbuke tulikotoka kwa hiyo, kwenye suala zima la kilimo kuna mambo kadhaa ambayo CAG katika ukaguzi wake ameyaona.

Mheshimiwa Spika, mathalani nitayazungumzia hayo huwezi kuzungumza kilimo bila kuzungumza mbegu, sasa kama Taifa tulikubaliana kwamba tutakuwa na mashamba tisa ya kuzalisha mbegu lakini ukweli ni kwamba kwa mujibu wa ripoti ya CAG mpaka sasa ni shamba moja tu ambalo linafanyakazi mwaka mzima lakini mashamba mengine nane yanategemea msimu wa mvua kwa hiyo yako kwa mujibu wa msimu. Sasa hatuwezi tukazungumza kwamba tunataka tufanye kilimo kiwe sekta ambayo ni stable wakati hatuzungumzi tunapataje mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji mashamba yote tisa ambayo yametengwa kwaajili ya kuzalisha mbegu nchini yafanye kazi yote mwaka mzima bila kusubiri msimu wa mvua kwasababu ripoti ya CAG inasema tunategemea shamba moja ambalo linafanyakazi mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye nchi ambayo asilimia kubwa tuna water bodies tuna maji kwa asilimia kubwa sana kwenye nchi yetu ardhi ya Tanzania hatuwezi tukawa tunategemea mvua watu wanatushangaa kwasababu kuna vitu tu haviko sawa kwenye scheme za umwagiliaji kwasababu ili uweze kufanya uzalishaji kwa kutumia umwagiliaji lazima utengeneze scheme za umwagiliaji zifanye kazi ili uweze kufanya kilimo especially cha kuzalisha mbegu kwasababu mashamba tisa kama nchi ni mashamba machache sana ambayo tunaweza tukatengeneza utaratibu mzuri na tukayahudumia mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kama nchi ripoti ya CAG inatuambia ni 39% tu ya pembejeo za kilimo zimegawiwa yaani ugavi kwenye pembejeo za kilimo ni 39% tu. Sasa unategemea Taifa lizalishe malighafi kwaajili ya viwanda vyake kwa Tanzania ya viwanda halafu unafanya ugavi wa pembejeo za kilimo kwa 39% tu. Kuna jambo Wizara na Waheshimiwa Wabunge kuna jambo lazima tukubaliane kwamba kama tumeamua kwamba tunatengeneza Tanzania ya viwanda ni lazima tukubaliane suala zima la kilimo ndiyo msingi na ni lazima wote ikiwezekana tuzungumze kuhusu kilimo. Kwasababu ndiyo tutapata malighafi kwaajili ya viwanda vyetu lakini ndiyo sehemu ambayo itatusaidia sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwasababu sasa hivi mwenyekiti wa kamati amezungumza kwamba sasa hivi tunalima kilimo cha kujikimu yaani watu wanalima sana ni kwaajili ya kuendeleza maisha kwamba wapate chakula waishi lakini kwa ardhi ukubwa wa ardhi ambao tunao kwenye Taifa letu lakini water bodies ambazo tunazo kwenye Taifa letu, resourcefully ya wasomi na watu ambao wana profession za mambo ya agriculture Taifa letu limebarikiwa sana tunatakiwa tutoke huku tuende sehemu nyingine zaidi kwenye kuboresha kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ripoti ya CAG inatuambia ni 1% tu ya wakulima wamepatiwa mafunzo na mbinu bora za kilimo sasa asilimia moja tu wamepatiwa mafunzo ya mbinu bora za kilimo. Kuna jambo hapa haliko sawa, na hii ni kwa mujibu wa ripoti ya CAG na wapo maana yake watu wanaelewa nini tunachokizungumza. Bahati nzuri nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Naibu Waziri pale kwasababu mara nyingi ndiyo tumekuwa tunamuuliza hata yeye maswali na yeye anajibu na anafuatilia Mheshimiwa Hussein Bashe. Kwa hiyo, kwasababu lengo letu ni kujenga na hii nchi ni ya kwetu maana yake hakuna mtu atatoka huku aje kutuambia tunajengaje nchi yetu hapa ni sehemu ambayo ni lazima tuweke nguvu Mheshimiwa Waziri yupo na Mheshimiwa Naibu Waziri pia yupo na Mheshimiwa Naibu Waziri pia yupo tuangalie tunafanyaje kwenye suala zima la kilimo na kimsingi mimi ni wa Singida kwetu tunalima alizeti, na tunalima kweli kweli alizeti kwa hiyo, ni declare interest kwamba mimi pia ni mkulima Pamoja na kwamba tunalima kwa simu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye upande wa pili nitoe mapendekezo labda nini kifanyike kwaajili ya kuhakikisha kwamba pengine utekelezaji wetu wa mipango ukiangalia mpango wa kwanza na mpango wa pili ni lazima tukubali kwamba kuna sehemu inawezekana haiko sawa ndiyo maana unakuta tunapanga bajeti za sekta za uzalishaji halafu hazitekelezwi kama tunavyopanga kama Bunge linavyopanga.

Mheshimiwa Spika, labda nitoe mapendekezo yafuatayo, pendekezo langu la kwanza napendekeza kuwe kuna sheria maalum kwasababu ni miaka 10 imepita mpango wa kwanza na Mpango wa Pili tunajadili Mpango wa Tatu phase ya mwisho ya miaka mitano ili itimie 15 tunaianza. Kwa hiyo, na nikiangalia hata nikisoma documentation na nini na Waheshimiwa Wabunge ambao ni wazoefu nyinyi mtalizungumza hili vizuri hatuna sheria mpaka sasa hivi ya kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama tunakaa tunajadili na tumekuwa tunajadili kuhusu mpango sisi wengine tumekuja juzi siyo wenyeji sana lakini kama tunapanga vitu ambavyo hatuvitungii sheria ya utekelezaji maana yake baadaye tunashindwa kujibana yaani tunashindwa kwamba tutabanana wapi kwasababu kama kutafanyika bajeti reallocation hakuna sheria ya kutu-guide kwamba sasa tumepanga mpango huu tunatumia sheria gani kusimamia utekelezaji wa mipango hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nishauri uletwe muswada wa sheria Bungeni tutunge sheria ya kusimamia utekelezaji wa mipango tunayoipanga kama Wabunge, kwasababu sisi ni watu wazima tuna akili zetu na kuna watu ni wasomi sana hapa na kuna watu wana mawazo mazuri sana lakini hatuna sheria ya kutu-guide kwamba sasa tunatekelezaje mipango tuliyojiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naweza kushauri ni kwamba sisi kama Wabunge sasa hivi tuko kwenye Bunge la Bajeti tunapanga bajeti na kuna bajeti ambazo tunajua kabisa kwamba Bunge hili ndiyo linatoa muelekeo wa Taifa kwenye masuala la bajeti. Lakini kama tunapanga bajeti za miradi ya maendeleo halafu hazitekelezwi katika kiwango ambacho Bunge limepanga maana yake ni kama vile kuna kukosekana nguvu kwa upande mmoja. Kwa hiyo, nishauri tunapokaa kama bunge tukapanga bajeti zinazokwenda kwenye miradi ya maendeleo tunaomba bajeti zitekelezwe kadri ambavyo Bunge hili limepanga kwasababu hiki ni chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni chombo ambacho kinakaa na tunatumia fedha na tunatumia muda kupanga kwa hiyo hatuwezekani tukiwa tunapanga halafu bajeti hazitekelezwi kama ilivyo na kimsingi sheria ndiyo itatusaidia kwasababu hata bajeti reallocation haitakuwa sana kwasababu kama sheria itatulazimisha kwamba kusifanyike bajeti reallocation especially kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ambayo tutajiwekea kufanya kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia jambo la mwisho naweza kushauri kuwe na uwajibikaji na kimsingi watu wanajitahidi katika kufanya wajibu wao lakini kwenye masuala la fedha kuwe kuna uwajibikaji endapo tunapanga tunapangiana program za kufanya na project za kufanya basi watu kuwe kuna uwajibikaji mkubwa kwenye masuala ya fedha ili kuwe kuna accountability kuwe kuna patriotism ule uzalendo mtu anauona kwamba sasa mimi hili ni jukumu langu kufanya jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwasasa nimechangia hapo. (Makofi)