Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwantumu Mzamii Zodo (9 total)

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi wengi zaidi katika Mkoa wa Tanga, hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Tanga ndio mkoa wenye halmashauri nyingi zaidi nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; utoaji wa huduma za afya kwa vituo vya Serikali unakabiliwa na changamoto nyingi tukilinganisha na vituo binafsi. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha huduma zinaboreshwa kwenye vituo vya Serikali ili kuongeza mapato ya Serikali? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajira 12,476, Serikali inaenda kuelekeza kwenye maeneo kama aliyoyataja ndio kipaumbele kitakuwa, ukiangalia Mikoa kama Kigoma, Mtwara, Songwe na mingine ambayo kwa kweli ni mikubwa, lakini kuna upungufu mkubwa zaidi, itakuwa ndio priority ya Serikali. Kwa hiyo, tunachukua ushauri wake na utaenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile swali lake la pili ameuliza kwamba, alitumia neno mapato kwenye eneo upande wa Serikali. Ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba, ukiangalia kwenye vituo vyetu vya Serikali, hasa ukiangalia kwenye eneo la bima tu, ukiangalia kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge utaona. Tukichukua hata zahanati tu, tuliwahi kuchukua moja, kwenye zahanati tu ya kawaida ambayo wanalipwa bima kidogo ukilinganisha na mkoani, unakuta wanaingiza milioni 84 kwa mwaka, lakini Serikalini wanaingiza 420, lakini ukigawa kwa idadi ya watumishi Serikalini tulijua walikuwa 187 huku kwenye private walikuwa 17, lakini utakuta kwa mwaka wanaingiza shilingi 5,300,000/=, lakini huku serikalini tena mkoani wanaolipwa zaidi wanaingiza shilingi 2,000,000/=

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunafikiri kuna umuhimu wa kwenda kufanya kazi kuhakikisha productivity ya watu wetu inaongezeka. Tukiongeza kwenye eneo la productivity maana yake hata kuna mahali ambapo prpductivity ndio inasababisha ionekane kwamba kuna upungufu, lakini upungufu sio halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna eneo la watumishi; tutaenda kuchukua modal ya Wizara ya elimu. Wizara ya elimu wameshirikiana vizuri sana na private sector kwamba, private sector wana shule, lakini na Serikali ina shule, lakini wamekuwa wanashirikiana vizuri sana bila kuwepo anayenyonya upande huu. Hivyo, kwenye afya tutaenda kudhibiti hasa kwenye eneo la kwamba, unakuta kuna watumishi wakati wa kufanya kazi Serikalini wako eneo la private sector wakati wameajiriwa ndani ya Serikali. Nalo hilo litaenda kufanyiwa kazi kwa nguvu na litatusaidia sana kuweka mambo sawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali la moja la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Tanga unazungukwa na milima ya Usambara; na kwa kuwa milima hii inatiririsha maji mwaka mzima hasa wakati wa mvua. Je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga mabwawa kuzunguka milima hiyo ili kuchochea kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zodo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikiri mbele ya Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba hatuwezi kutoka katika matatizo ya kilimo bila kuwekeza katika umwagiliaji. Huo ndiyo muelekeo wa Serikali na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Jambo la msingi ambalo tunalifanya sasa hivi kama Wizara kwanza ni kubadilisha modal ya Tume ya Umwagiliaji namna ambavyo inafanya kazi yake; mbili tunachokifanya kama Serikali ili kuweza ku-take advantage ya maeneo kama Milima ya Usambara lakini na maeneo mengine ya nchi yetu kwa ajili ya kujenga mabwawa katika bajeti mwaka kesho mtaona tumeweka chanzo kipya cha fedha kitakachokuwa cha Tume ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutawekeza kununua vifaa wenyewe ili Tume ya Umwagiliaji iwe na uwezo wa kupeleka vifaa kwa ajili ya kuchimba mabwawa na kujenga miradi ya umwagiliaji yenyewe kwa mfumo wa force account ili kupunguza gharama kubwa tunayotumia katika maeneo ambayo tunajenga skimu za umwagiliaji, kwa sababu gharama tunazotumia ni kubwa na hatuoni value for money. Kwa hiyo tunabadilisha mfumo tutatengeneza mfumo wa force account na tutanunua vifaa wenyewe ambavyo vitakuwa chini ya Tume ya Umwagiliaji kama tulivyofanya katika Skimu ya Pawaga na Ruaha ambako tumetumia vifaa vyetu wenyewe kurekebisha skimu hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wasubiri bajeti ya Wizara, wataona mwelekeo wa Wizara katika Sekta ya Umwagiliaji.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. naomba niulize maswali mawilinya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Jasini kwa Kata ya Moa na Mayomboni, Wilaya ya Mkinga wanapata usumbufu sana wa kukamatwa na askari wa Kenya na kwenda kushitakiwa Kenya na wakati mwingine mali zao kutaifishwa.

Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha hali hii inakoma? Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili,...

SPIKA: Wanakamatwa kwa sababu gani?

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, wanaonekana wameingia Kenya, wakivua Kenya, ni eneo la bahari.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, askari wa Kenya mara kadhaa wanaingia Jasini, hali ambayo ni hatari sana kwa nchi zetu hizi mbili.

Je, ni lini sasa Serikali itachukua hatua za haraka za kuhakikisha inaweka mipaka ili kuhakikisha Serikali ya Kenya na Tanzania zisije zikaingia kwenye migogoro? Asante nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA
MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nikiri ni kweli katika eneo la Jasini kwenye Kata ya Moa na Mayombo mara nyingi kumekuwa kukitokea ukamataji wa wananchi wa eneo hilo na hili pia liliwahi kutokea wakati pia tuko ziara kule, nilishafika mpaka Jasini.

Mheshimiwa Spika, lakini kinachotokea hapa ni kutokana na kwamba katika uimarishaji wa mpaka tumesema tunaimarisha kwanza maeneo ya nchi kavu kwa sababu majini katika kuweka maboya tayari mpaka nchi zote mbili ziridhie wapi maboya yawekwe, pamoja na kwamba, tunajua kuna ule mbali wa nautical miles 200 ambazo ziko kwetu, lakini hii haijaweza kufanyika kutokana na hali halisi ambayo kila ukitaka kuweka alama lazima mkubaliane wote.

Mheshimiwa Spika, lakini napenda kushukuru sana Balozi zetu, Ubalozi wetu wa Kenya pamoja na ule mdogo wa Mombasa. Nimshukuru sana Mheshimiwa Pindi Chana wakati yuko pale wametatua matatizo mengi kutokana na kesi hizi na sasa hivi balozi aliyeko pale, Consular Athumani Haji aliyeko Mombasa, ni juzi toka miezi sita iliyopita wameweza kutatua pia changamoto hiyo ya kuweza kukamatwa.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo kutokuwekwa kwa maboya pale ni kutokana na makubaliano ya nchi mbili, lazima mkubaliane ndio muweke alama hizo. Bila kukubaliana hakuna nchi itakayoweza kuweka.

Mheshimiwa Spika, na kingine ambacho ni changamoto kule sasahivi wameanzisha sheria ya uvuvi ambayo chombo kinapoingia ziwani lazima ulipe dola 500 na ukikamatwa pale fine ni dola 300. Sasa mara nyingi wavuvi wetu wanakuwa hawana, lakini diplomasia imekuwa ikitumika wanajadiliana kati ya ubalozi n akule na watu wanatoka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba katika swali lake la pili analosema ni lini hii itakomeshwa? Niwaombe tu muwe na Subira kwa sababu mchakato unaendelea katika suala zima la kuimarisha mipaka kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi. Tukiimarisha mipaka hiyo ya nchi kavu ikikamilika suala la kuweka maboya ndilo limebaki kwa sababu tayari mpaka ulishabainishwa isipokuwa ni kuweka alama tu. Tutaweka mara tutakapokuwa tumekubaliana na wenzetu wa Kenya.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na vyama vya ushirika walivonavyo wavuvi lakini bado wavuvi wetu wana hali duni sana kiuchumi katika ukanda wetu wa Pwani. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuwakwamua wavuvi wa pembezoni mwa Bahari ya Hindi kwa Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara katika kushiriki kwenye uchumi wa blue.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Zodo; kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan inao mkakati madhubuti au inayo mikakati madhubuti ya kuhakikisha inawasaidia wavuvi wa ukanda wa Pwani hasa kuendana na uchumi wa blue kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti tunayoitarajia ya mwaka 2021/2022, yako mambo ya msingi yatakayofanywa. La kwanza ni kuhakikisha tunaongeza uzalishaji katika miamba ya kuvutia Samaki, tutatengeneza katika Ukanda wote wa Pwani. Vile vile kama haitoshi tutahakikisha kwamba tunatengeneza vichanja vya kukaushia samaki, sababu moja kubwa inayowasumbua wavuvi ni upotevu wa mazao ambao wanayazalisha kwa kuoza na kwa kuharibika. Tunataka tuhakikishe kwamba samaki wote wanaozalishwa na wavuvi wa ukanda wa pwani hawaharibiki kwa sababu tutawaongezea thamani kwa kuwakausha, lakini vile vile tutakwenda kuongeza uzalishaji wa barafu na kuwa na cold rooms za kutosha katika ukanda mzima wa pwani, ili kuweza kuitumia vyema uchumi wa blue na kuongeza kipato cha mvuvi mmoja mmoja na hatimaye kuongeza kipato cha Serikali yetu. Naomba wavuvi watuunge mkono ili kuweza kufikia lengo hilo.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuwa kati ya vikwazo vya zao la alizeti ni upatikanaji mdogo kwenye Mbegu ya alizeti wa mafuta. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuja na utafiti wa kina wa kuhakikisha tunapata mbegu bora zinazotoa mafuta kwa wingi ili kuchochea wasindikaji na wakulima wa zao hili la alizeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza utafiti ni jambo ongoing tunaendelea kufanya utafiti lakini tumeshafanya utafiti wa kutambua aina gani za mbegu, tunazo mbegu aina mbili tuna high hybrid na tuna mbegu za OPV ambazo zinatumika kwenye uzalishaji wa alizeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya sasa hivi kama mlivyosikia kwenye jibu letu la msingi kwamba mwaka ujao wa fedha tutawekeza kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuzalisha mbegu za kutosha na malengo yetu ni kuzalisha metric tons 5,000 za Mbegu ambazo zitakwenda shambani ambazo zitatupatia metric tons 625,000 za mbegu za kwenda kukamuliwa ambazo zitatupatia metric tons 170,000 za mafuta kupunguza gape yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala la uzalishaji wa mbegu tayari tunashirikiana na sekta binafsi tutazalisha mbegu za kutosha katika mwaka ujao wa fedha na hii itatufanya kwamba tutakuwa tumepunguza 50% ya gape yetu, na mwaka unaofuatia nadhani kwamba tutakuwa tumemaliza. Kwasababu mahitaji yetu ni kupata mbegu za kwenda kiwandani kukamuliwa metric tons 1,226,000 ambazo zitatupatia wastani wa tani 400,000 za mafuta ili tuweze kupunguza kabisa tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sisi tunaamini kwamba kutoka upande wa Serikali ni kwamba ndani ya miaka miwili au miaka miwili ya fedha tutakuwa tumelipunguza tatizo hili la mafuta kwa kiwango kikubwa na priority ni zao la Alizeti yakifuatiwa na mazao mengine, kwa hiyo, utafiti umeshafanyika na mwakani tunaanza uzalishaji. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa changamoto iliyopo Jimbo la Mtwara Mjini la kukosa Hospitali ya Wilaya linafanana sana na changamoto ya Jimbo la Kilindi: Je, ni lini sasa Serikali itapeleka pesa kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ili kuokoa maisha ya akina mama wa Kilindi na Mkoa wa Tanga kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajenga Hospitali za Wilaya na Halmashauri katika Halmashauri zote ambazo hazina Hospitali hizo nchini kote. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya Halmashauri zote ambazo hazina Hospitali za Halmashauri na fedha hizo zitapelekwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali hizo. Kwa hiyo, pamoja na Jimbo hili la Kilindi kwa maana ya Halmashauri ya Kilindi itatengewa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi huo. Nakushukuru.
MHE. MWAMTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa moja ya changamoto ambazo zinasababisha kukosekana kwa watumishi kwenye sekta yetu ya afya ni pamoja na vifo, kustaafu na ujenzi wa vituo vya afya pamoja na zahanati. Na kwa kwakuwa bado tunaendelea na ujenzi wa vituo vya afya, je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kasi ya ujenzi wa vituo vya afya inaendana na kasi ya kuajiri watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mwaka 2017/2020 wameajiri watumishi 12,868 na wadau hao ni kama Benjamin Mkapa, AMREF na MDH. Je, ni upi mchango wa wadau hao katika ajira kwa sekta hii ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi ni kweli kwamba Serikali kwa kujali na kuthamini afya za wananchi imeendelea kujenga, kukarabati na kutanua vituo vya huduma za afya ili kusogeza huduma bora za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuzingatia hilo, Serikali pia imeweka mkakati wa kuhakikisha kasi ya ujenzi wa vituo vya huduma za afya kote nchini inaendana na kasi ya ajira za watumishi ili kuviwezesha vituo hivyo kuanza kutoa huduma za afya katika vituo vyote vinavyojengwa na kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 jumla ya watumishi takribani 12,868, wastani ya watumishi 4,200 kila mwaka wameajiriwa lakini hivi sasa Serikali inaendelea na ajira za watumishi 2,726 ambazo pia zitakwenda kupunguza upungufu wa watumishi katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba tunaajiri watumishi katika vituo hivyo, ahsante sana.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga soko kuu la kuuzia samaki kwa Mkoa wetu wa Tanga na ni lini ujenzi utaanza?

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili; ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wavuvi wa maeneo ya pembezoni kwa maeneo ya Moa, Chongoleani, Kipumbwi na Mkoaja kuuza samaki wao kwenye soko la pamoja kukwepa wachuuzi kuwachuuza kwa bei ndogo? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu ya msingi nimeeleza kwamba kwenye bajeti ya mwaka huu na kupitia ufadhili wa Shirika la IFAD, upo mpango wa Serikali wa kujenga masoko ya samaki. Na soko hili litajengwa katika Wilaya ya Pangani katika Kijiji cha Kipumbwi litakuwa ni soko zuri kubwa na la Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameuliza je watauzia wapi wavuvi wa Chongeleani, Mkinga, Kipumbwi na kwingineko. Naomba nimhakikishie kwamba soko hili litakapokuwa tayari, wavuvi wa maeneo yote aliyoyataja watafaidika kwa ajili ya kuuza bidhaa zao, ahsante sana.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa Serikali inajenga Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya nchi nzima na kwa kuwa baadhi ya hospitali za Wilaya ni kongwe.

Je, Serikali haioni haja ya kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati hospitali za wilaya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Pangani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa na Hospitali za Halmashauri kongwe ambazo zilijengwa miaka mingi. Zipo ambazo zimejengwa baada ya uhuru mapema, lakini zipo ambazo, zilijengwa hata kabla ya uhuru na kwa kweli miundombinu yake sasa ni chakavu. Lakini pia haziendani na kiwango cha hospitali za halmashauri ambazo sasa tunazihitaji. Kwa kutambua hilo Serikali tumefanya tathmini ya hospitali zote za Halmashauri kongwe na tumekwisha ziainisha. Tunaweka mpango, baada ya kukamilisha hospitali za Halmashauri 28, sasa tutakwenda kukarabati na kupanua hospitali zile kongwe ikiwepo Hospitali hii ya Pangani. Ahsante sana. (Makofi)