Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwantumu Mzamili Zodo (13 total)

MHE. MWANTUMU M. ZODO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na upungufu wa Watumishi wapatao 16,000 kwenye Sekta ya Afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa hivi sasa imetokana na mahitaji mapya yanayotokana na ujenzi na upanuzi wa hospitali za rufaa za kanda, mikoa, ujenzi wa hospitali za Halmashauri, ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi 2020 Serikali iliajiri watumishi wapatao 14,479 na zaidi ya watumishi 565 walipatiwa ajira za mkataba kwa kugharamiwa na makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za afya. Pia katika mwaka wa fedha 2020/2021 sekta ya afya inatarajia kuajiri jumla ya watumishi wapya 12,476.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO - K.n.y. MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:-

Usambazaji wa umeme vijijini unapaswa kukamilika ifikapo Mwaka 2021/2022:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa usambazaji wa umeme vijijini unakamilika kama ilivyopangwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme (TANESCO) inaendelea kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2022. Mradi huu unalenga kufikisha umeme katika vijiji 1,974 ambavyo havijafikiwa na miundo mbinu ya umeme. Aidha, mradi huu pia, utafikisha umeme katika vitongoji 1,474.

Mradi huu utakapokamilika utafanya vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara kufikiwa na miundo mbinu ya umeme na gharama ya mradi huu ni takribani shilingi 1,040,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika kwa wakati, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza usimamizi, kupunguza wigo wa kazi za wakandarasi ili kurahisisha usimamizi, wakandarasi kulipwa kwa wakati na kuhakikisha vifaa vyote vinavyohusika vinapatikana nchini.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza:-

Kada ya Elimu inakadiriwa kuwa na upungufu wa walimu takribani 60,000.

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri na kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa walimu waliokoma utumishi wao kwa sababu mbalimbali kama vile kufariki, kustaafu na walioachishwa kazi kwa mashauri mbalimbali ya kinidhamu. Aidha, Mwezi Mei 2021 Ofisi ya Rais- TAMISEMI imetangaza ajira 6,949 za walimu wa shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Sekta ya Afya nchini ina upungufu wa Watumishi wapatao 16,000:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Sekta ya Afya nchini ina upungufu wa watumishi ambapo hadi mwezi Mei 2021 watumishi waliokuwepo ni asilimia 41 ya mahitaji halisi. Upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu kazi, kufariki na kuongezeka kwa idadi ya Vituo vya kutolea huduma za afya nchini kutokana na utekelezaji wa Programu ya Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya kutolea huduma za Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 Serikali kwa kushirikiana na wadau imeajiri watumishi 12,868 wa Sekta ya Afya ambao wamepangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Adha, Serikali inakamilisha taratibu za ajira 2,726 za watumishi wa kada mbalimbali za afya zilizotangazwa Mwezi Mei 2021. Watumishi hao watapangwa kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya vyenye uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kukabiliana na changamoto hii, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi wa kada za afya kwa awamu, nashukuru.
MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya Wavuvi wa ukanda wa Pwani ili kuchochea uchumi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, Mbunge - Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya wavuvi wa Ukanda wa Pwani, Serikali inafanya yafuatayo: -

(i) Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wavuvi kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka taasisi mbalimbali za fedha;

(ii) Kupitia ufadhili wa Shirika la IFAD, Serikali inaboresha masoko ya mazao ya uvuvi pamoja na kuweka miundombinu wezeshi ya kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na;

(iii) Kupitia Taasisi ya Utafiti a Uvuvi (TAFIR), Serikali inatarajia kuweka vifaa vya kuvutia samaki katika Bahari ya Hindi kwa ajili ya kusaidia wavuvi kupata samaki kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea na programu ya kuainisha maeneo yenye uvuvi wenye tija kwa kutumia satellite ili kuwataarifu wavuvi maeneo ambayo samaki wanapatikana kwa wingi, ahsante.
MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Vuga - Mlembule katika Mji Mdogo wa Mombo Wilayani Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamilu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Vuga - Mlembule ulioanza kutekelezwa mwezi Julai, 2020 ambapo utekelezaji hadi sasa umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022. Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake), ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo 500, ujenzi wa matanki punguza mawili (2) na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji umbali wa Kilometa 10.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zinazoendelea ni ujenzi wa matanki punguza manne (4) na ulazaji wa mabomba ya usambazaji Kilometa 4.3. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wananchi wapatao 21,284 wa Vijiji vya Mlembule, Mwisho wa Shamba, Mombo na Jitengeni.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Hopsitali ya Wilaya ya Pangani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshemiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamilu Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 21 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa Hospitali kongwe 21 ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani. Aidha, kupitia mpango huo, kila hospitali kongwe imetengewa shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati hospitali za Halmashauri ambazo miundombinu yake imechakaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kote.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wakulima wa zao la Mwani ili kuongeza tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023 Serikali imetenga fedha za program maalum ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wa mwani pembejeo kwa mkopo wa masharti nafuu na usio na riba kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kwa awamu ya kwanza, Wizara itatoa pembejeo za mwani zenye thamani ya shilingi 447,251,244 kwa wakulima 343 waliokwenye vikundi katika wilaya saba za Muheza, Pangani, Mtama, Mkuranga, Kilwa, Lindi Mjini na Mtwara Vijijini, ahsante.
MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa miundombinu chakavu katika Vyuo Vikuu?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika Vyuo Vikuu vya Umma hapa nchini. Ili kutatua changamoto ya uchakavu wa miundombinu vyuoni Serikali imefanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Chuo Kikuu cha Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inaendelea na ukarabati wa miundombinu chakavu na ujenzi wa miundombinu mipya katika Vyuo Vikuu vyote vya Umma 14

na Taasisi tano (5) za Elimu ya Juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji vyuoni. Aidha, Taasisi hizi zimekwishapokea fedha kwa ajili ya kuendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu kupitia Mradi wa Mageuzi ya Uchumi katika Taasisi za Elimu ya Juu (HEET).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi za mabasi katika Halmashauri za Mkoa wa Tanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mpando wa uboreshaji wa Majiji na Manispaa Tanzania TSCP imejenga Stendi ya Kisasa katika Jiji la Tanga na Halmashauri ya Mji wa Korogwe zilizogharimu takribani kiasi cha Shilingi billioni 10.7, ujenzi wa stendi hizo umekamilika na zinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya shilingi billioni 10.312 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya stendi katika halmashauri nchini. Aidha, Serikali itaendelea kujenga stendi za mabasi katika halmashauri kwa awamu kupitia programu mbalimbali kama, TACTIC, TSCP na vyanzo vingine yakiwemo mapato ya ndani ya halmashauri, ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuviwezesha Vikundi vya Wanawake vya Ufugaji Mkoani Tanga ili viweze kuongeza tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamilu Zodo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 hadi mwezi Machi, Halmashauri za Mkoa wa Tanga zimetoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.56. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi Bilioni 1.82 zimekopeshwa kwenye vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na biashara ndogondogo pamoja na ufugaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchanganuo huo hapo juu, vikundi vya Wanawake 102 vyenye wanufaika 875 vinavyojishughulisha na kazi za ufugaji wa mifugo ya aina mbalimbali vimekopeshwa kiasi cha Shilingi Milioni 575 na kuweza kutengeneza ajira zipatazo 253.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Bweni Wilayani Pangani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tararibu za manunuzi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Pangani katika Mto Pangani litakalounganisha Vijiji vya Bweni na Pangani lenye urefu wa meta 525 ziko katika hatua za mwisho kwa ajili ya kusaini mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali vikiwemo vya ufugaji ambavyo wanawake wamehamasika ili wafuge kwa tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri za Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini, zimekuwa zikitoa mikopo ya uwezeshaji kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani. Mikopo hiyo imekuwa ikitumika kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo ufugaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023, Halmashauri za Mkoa wa Tanga zilitoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya shilingi bilioni 4.569 ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.827 zilikopeshwa kwa vikundi vya wanawake ambapo vikundi 102 vya wanawake vyenye wanufaika 875 vinavyojishughulisha na kazi za ufugaji vimekopeshwa kiasi cha shilingi milioni 575.39.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuviwezesha vikundi mbalimbali kwenye shughuli za uchumi na uzalishaji ikiwemo vikundi vya akina mama ili kutengeneza ajira, kipato na hivyo kupunguza umaskini.