Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwantumu Mzamili Zodo (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Kwanza kabisa kama utamaduni wetu Watanzania kushukuru na mimi naomba nishukuru kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili tukufu, naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kikiongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Mwenyekiti wa chama chetu, Wajumbe wa Kamati Kuu, lakini pia nawashukuru akinamama wa Mkoa wa Tanga kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naishukuru Kamati yangu ya Utekelezaji Mkoa wa Tanga na Taifa pamoja na familia yangu kwa kuni-support. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais kwenye kipengele cha elimu. Kutokana na muda sasa hivi ni mchache, dakika tano, nitakwenda moja kwa moja kwenye elimu, sitaweza kugusa vitu vyote na kwa kuwa mambo mengi yameshaongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi toka tumeanza mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la elimu, Serikali ya Chama chetu cha Mapinduzi ikiongozwa na Jemadari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa; kutoa elimu bure ndani ya kipindi cha miaka mitano. Kuanzia 2016 mpaka leo tumetoa shilingi trilioni
1.01 ambayo imesababisha ongezeko la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na elimu bure, pia Rais John Pombe Magufuli chini ya uongozi wake ameongeza idadi ya madarasa katika shule za msingi kutoka madarasa 16,899 tuliyokuwa nayo hapo awali mpaka kufikia madarasa 17,804. Pia tumeongea shule za sekondari kutoka shule 4,708 mpaka shule 5,330. Pia tumekarabati shule kongwe na wengi tunaotoka huko mikoani ni mashahidi kati ya shule 89, shule 73 zimekarabatiwa na zimebaki shule 16 na ni Imani yangu kwa Serikali hii na kasi hii ya Awamu ya Tano tutakwenda kumalizia shule hizi 16 kwa kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia mabweni 253 yamejengwa, kwa hiyo, ni mafanikio makubwa. Vyumba 227 vya maabara vimejengwa na maabara 2,956 zimepatiwa vifaa. Tumeona ongezeko la madawati la asilimia 200. Hayo ni mafanikio makubwa kwa Rais huyu mtetea wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, idadi ya wanafunzi nimesema kutoka 1,648,359 mpaka 2,185,037 kwa shule za sekondari. Kupitia kipengele hicho cha elimu na mafanikio hayo makubwa na kazi kubwa naomba nishauri kitu. Naomba nishauri upande wa mtaala. Tumeona mambo ni makubwa yaliyofanywa lakini kwenye kipengele cha mtaala iko haja ya ku-review mtaala wetu, malengo ya mtaala.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru, naomba niunge mkono hoja kwa mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana kwenye elimu na Wizara nyingine zote. Ahsante nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MWANTUM M. ZODO: Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri TAMISEMI kuwapatia watendaji wa kata mafunzo ya muda mfupi kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma. Watendaji wa kata na vijiji ndio wasimamizi wakuu wa shughuli za Serikali kwenye maeneo yetu, watendaji wa kata na vijiji ndio wasimamizi wakubwa wa kila siku wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu, watendaji hawa ndio wakusanyaji wakuu wa ukusanyaji mapato ya halmashauri zetu, watendaji wa kata na vijiji ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi kwa ngazi za kata na vijiji. Mkurugenzi, Mkuu wa Idara wala DC hawawezi kuwa site kila siku, badala yake wanatekeleza majukumu yao ya kiofisi ya kila siku. Watendaji hawa ndio Serikali ya kwanza mwananchi wa kawaida anayokutana nayo kila siku, lakini pia ndio wanaoishi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, tuendelee kukuomba Mheshimiwa Waziri kutafuta fungu kwa ajili ya mafunzo haya ya watendaji kama Kamati ilivyopendekeza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nikushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Elimu. Naomba nianzie kwenye sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002. Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, tulikuwa tupo watu milioni 34 Tanzania. Lakini baada ya miaka kumi sensa ya 2012 tulitoka milioni 34 mpaka milioni 45. Ni nini tafsiri yake. Tafsiri yake ni kuwa kila mwaka kutoka 2002 mpaka 2012 tulikuwa tunaongeza kwa wastani wa watu milioni moja kila mwaka. Kwa maana hiyo pia kila mwaka tuna wajibu wa kuongeza madawati, madarasa, Walimu, vifaa mashuleni kwa sababu idadi ya watu haishuki bali inaongezeka na itaendelea kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye ajira za Serikali. Serikali imeajiri watu 480,000 tu mpaka sasa. Kutoka kwenye watu milioni 45 ni sawa na asilimia moja, lakini wengine wameajiriwa kwenye sekta binafsi na wengine wamejiajiri kwenye kilimo na biashara nyingine kama ujasiriamali na vitu vingine kama hivyo. Sasa tukiangalia takwimu hizo, ipo haja sasa ya kufanya maboresho makubwa kwenye mtaala, kwa sababu ni kiwango kidogo sana kinaajiriwa, asilimia 99 ya watu wanatakiwa wajiajiri wenyewe ndio tafsiri yake. Kwa maana hiyo sasa tunatakiwa tuboreshe mitaala na tuongeze yale masomo ambayo mwanzo tulikuwa tumeyafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani wakati mimi nasoma, kulikuwa na masomo ya sayansikimu, kulikuwa na masomo kama sayansi kilimo, kulikuwa kuna masomo kama maarifa ya nyumbani. Masomo yale yalikuwa yanafundisha vitu mbalimbali, mkiwa kule shuleni mnafundishwa kilimo, upishi, mnapika keki na nini, lakini sasa hivi tunawekeza fedha nyingi sana kwenye elimu bure, tukishamaliza hapo mwanafunzi anamaliza darasa la saba, anakwenda kutoa 350,000 tena kufundishwa kupika keki. Sasa sijui tunamsaidiaje? Tumewekeza fedha nyingi kwenye kumsomesha, halafu bado akatafute tena ujuzi mdogo tu wa kupika keki kwa 350,000. Anakwenda kujifundisha ushonaji ambao mwanzo yalikuwepo hayo masomo, lakini sasa anakwenda kujifundisha kwa 200,000, anakwenda kujifundisha ujasiriamali kwa 500,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali ya Tanzania inawekeza fedha nyingi sana kwenye elimu bure. Kama tunawekeza fedha nyingi kwenye elimu bure, ipo haja ya kufanya maboresho kwenye mtaala wetu umwezeshe mwanafunzi baada ya elimu kujitegemea, lakini sasa wanafunzi hawa pia bado ni ngumu sana kujitegemea moja kwa moja kwa sababu; elimu ya msingi umri wa mwanafunzi kuanza shule ni miaka saba na miaka sita. Mwanafunzi anamaliza elimu ya msingi akiwa na miaka aidha 12 au 13, ni uongo hata kama tutampa hizi stadi mwanafunzi wa miaka kumi mbili atakayemaliza darasa la saba na mfumo ukamuacha akawa amefeli yupo nyumbani, bado hawezi kufanya chochote huyu bado ni mtoto mdogo mnoo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa, niishauri Serikali elimu msingi iwe ni kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, angalau sasa huyu mwanafunzi wa darasa la kwanza mpaka kidato cha nne; tukimpa sasa hizo skills anaweza baada ya hapo akitoka akaenda kukaanga chips, anaweza akawa bodaboda, anaweza akaenda kwenye ufugaji, anaweza kwenda kwenye kilimo, lakini sio mwanafunzi wa miaka 12 au 13 ambaye mfumo umemwacha, hataweza kufanya chochote. Matokeo yeke ndio hizo ajira za watoto wanachukuliwa kwenda kufanya kazi za ndani, kuuza karanga, tunaona watoto wengi stendi, majumbani, wapo watoto wadogo sana wamemaliza darasa la saba hawakupata bahati ya kuendelea, aidha anafanya kazi za ndani au anauza karanga stendi au anauza mayai ni watoto wadogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa, naona ipo haja ya kufanya maboresho kwenye mtaala, lakini pia kuangalia elimu msingi iwe ni kuanzia shule ya msingi mpaka form four, angalau mtoto huyu atamaliza form four akiwa aidha na miaka 16 au 17 angalau tutakuwa tumemvuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii nyeti ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, wakati wa bajeti ya Wizara ya Elimu nilitoa mchango kuhusu ajira. Serikali yetu imekuwa na changamoto kubwa ya ajira hata Waziri wa TAMISEMI asubuhi alilithibitisha hilo. Kati ya nafasi za walimu 6,000 zilizotangazwa mpaka sasa watu 89,000 wameomba ajira hizo, kwa hiyo, tunaweza tukapata picha hapo.

Mheshimiwa Spika, mbadala wa hilo ambalo litaenda kutatua changamoto hiyo ya ajira kwa vijana wetu na Watanzania ni kupitia sekta hii ya kilimo. Hata hivyo, mkazo kwenye sekta hii ya kilimo ni mdogo mno na Watanzania wengi tunalima bila tija, tija yetu ni ndogo sana kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri tu, mimi natokea Mkoa wa Tanga, miaka miwili, mitatu iliyopita tulihamasishwa sana kulima mihogo na wewe mwenyewe nafikiri utakuwa ni shahidi, tukaambiwa kuna Wachina wanakuja kununua mihogo lakini watajenga viwanda vikubwa. Niko na jirani yangu hapa Mzee Mwijage nafikiri alikuwepo wakati huo Mzee wa Viwanda na yeye atakuwa ni shahidi na watu walihamasika sana walikwenda kuchukua mikopo mikubwa sana kwenye mabenki. Ilikuwa ukifika pale kwa Msisi Wilayani Handeni, kuna mashamba ambayo labda uzunguke kwa bodaboda au upande juu ya mlima ndiyo hilo shamba lote unaweza kuliona.

SPIKA: Mheshimiwa Mwantumu, Kanuni zetu zinaruhusu kumuuliza Mbunge swali. Kwa hiyo, unaweza kumuuliza Mheshimiwa Mwijage vile viwanda ulivyoahidi viko wapi na mimi kwa kweli nitatoa nafasi ajibu. (Makofi/Kicheko)

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nitafanya hivyo.

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Mwantumu.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, nachotaka kusema baada ya yale maagizo na sisi viongozi kuhamasisha wananchi hakuna kiwanda hata kimoja kimejengwa na hata wanunuzi wenyewe hawapo. Watu wale wamechukua mikopo mikubwa mabenki na mpaka sasa hivi watu wengine wana presha. Kwa hiyo, niiombe Wizara tuwe tuna taarifa za kutosha, tukisema tunapeleka viwanda na kuhamasisha wananchi kweli viwanda vije.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo sasa hivi tumeibua tena zao lingine la kimkakati, zao la mkonge kwa Mkoa wa Tanga. Namshukuru sana Waziri Mkuu ameshakuja karibu mara tatu na ukisoma mikakati ya Serikali wana mikakati mizuri sana. Kuna Bodi ya Mkonge pale na nafikiri Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge toka jana yuko hapa, anafanya kazi nzuri sana. Waziri Mkuu aliagiza wakati wa ziara yake kwanza yale mashamba matano yagawanywe na wale watu wa Bodi ya Mkonge waanze kugawanya yale mashamba kwa wale wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo yale na baadaye ndiyo wajaribu kuangalia watu wengine. Kweli Bodi ya Mkonge inafanya hivyo wameanza kugawa kwa shamba lile la Hale, Mwelia, Magoma, Mgombezi na mashamba mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasa watendaji wetu wa Serikali, huku juu mipango ni mizuri sana lakini sisi tuko kule chini tuna deal sana na watu wa kule chini wa ngazi za mashina, matawi, huku chini hakuna taarifa kabisa yaani ukiacha wale wananchi wanaoishi kuzunguka mashamba yale ya mikonge, wale ambao hawaishi kwenye yale mashamba ya mikonge hawana taarifa kabisa. Wanakwambia tunasikia mkonge unalipa, tunasikia sasa hivi mkonge hekta moja ni shilingi 3,600,000, kwa hiyo na wao wenyewe wanasikia. Wakati hapo kuna Afisa Kilimo Mkoa ameajiriwa, kuna Afisa Kilimo Wilaya yuko pale kaajiriwa na anafanya kazi, kuna Maafisa Ugani japokuwa ni wachache lakini wapo, huyu Mkurugenzi peke yake wa Bodi ya Mkonge kama hatasaidiwa na hawa watendaji wengine wa Serikali hataweza kufanya kazi hiyo mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa Wizara iwaelekeze watendaji wao kushuka chini kwenye mikutano ya vijiji, mikutano ya kata na hata kwenye mikutano ya Majimbo; Wabunge wanajitahidi sana mara nyingi kuzungumzia suala hili, lakini watendaji wale wa Serikali hawazunguki kutoa hamasa. Wala huwezi ukajua kama kuna Afisa Ugani pale kwenye ngazi ya kata na hata ukimuuliza mwananchi hamjui kabisa. Wale watu wapo tu hawatoi elimu, kilimo kinaporomoka lakini wameajiriwa wanalipwa mishahara. Kwa hiyo, niiombe Wizara isimamie watu wake ili kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwenye kilimo niipongeze Wizara ya Kilimo nimeona kilimo kinaendelea kukua. Kwa mfano, mwaka 2019 kimekuwa kwa 4.4% na 2021 ukuaji wa kilimo ni 4.9%. Pia kwenye ajira kinaendelea kutoa ajira kutoka kwenye 58.1% mwaka 2019 mpaka 65%.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja lakini naomba Wizara sasa ihakikishe inafanya kazi kweli kweli kuleta tija kwani kwenye kilimo tija bado ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami naomba nishukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia Wizara hii muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kujikita kwenye habari baadaye nitakwenda kwenye michezo na kama muda utaniruhusu, nitamalizia kwenye utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa habari naomba niongelee hili Shirika letu la Utangazaji la Taifa - TBC. Maeneo mengi ya Mkoa wetu wa Tanga hayana usikivu, kwa mfano kwa maeneo kama vile ya Mkinga, Mlalo na Bumbuli wanasikiliza sana redio za Kenya kuliko za Tanzania. Kwa hiyo hali hii ni ya hatari sana, wale watu wanakosa mawasiliano kabisa na kama tunavyojua, mawasiliano ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la TBC kwa maeneo hayo walifunga minara yao kwa Kata za Mnyuzi na Kwemshai maeneo ya Korogwe na Lushoto. Lakini sasa maeneo ya Mlalo na Bumbuli yako nyuma ya mlima, kwa hiyo hayapati mawimbi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri waliopita walikwenda mara kadhaa wakaahidi kushughulikia suala hilo lakini mpaka sasa halijashughulikiwa. Kwa hiyo, niiombe Wizara itukumbuke watu wa Mkoa wa Tanga kwa maeneo hayo ambayo hatuna usikivu waende wakarekebishe mitambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia cha kushangaza ni kwamba hapo awali maeneo hayo yalikuwa yanakamata lakini baada ya kutoka kwenye mfumo ule wa analogue kwenda kwenye mfumo wa digital wa fm ndiyo yamepoteza usikivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo nashindwa kuelewa, kwa nchi nyingine wakitoka kwenye mifumo ya zamani wakiwa wanaboresha mifumo yao kwenda kwenye mifumo mipya ndiyo wanafanya vizuri zaidi. Lakini sasa ni tofauti sisi kwa nchi yetu, yaani tulivyokuwa kwenye analogue maeneo yale yalikuwa yana usikivu na tulikuwa tunakamata vizuri hizo redio. Lakini baada ya kufanya marekebisho yale kutoka kwenye hizo short waves kwenda kwenye fm, maeneo yale yamepoteza usikivu. Kwa hiyo niiombe Wizara iende katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kwenye Shirika letu hili la Utangazaji la TBC, naona kama bado vifaa vyao vingi si vya kisasa; naomba wapatiwe vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waandishi wetu wa habari naona maslahi yao bado ni madogo mno, tuangalie namna ya kuongeza maslahi ya waandishi wa habari. Wanafanya kazi kubwa na ni kazi ngumu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona hata tunapokuwa kwenye misafara ya viongozi, wakati viongozi wanakimbia na zile V8 nao wanakimbia na magari yao na wanatakiwa kuwahi pale tukio likitokea, kila kituo mnachohama yaani unaona wanavyopata taabu na wanavyoomba lift kwenye magari ya viongozi. Kwa hiyo, naomba sana pia waandishi wa habari waangaliwe kwa upande wa maslahi na upande wa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye michezo. Michezo ni ajira, michezo ni afya na michezo ni uwekezaji pia. Lakini nimesikiliza vizuri hotuba ya Wizara hapo asubuhi, hoja yao moja kubwa, walisema mkakati mmoja wapo wa Wizara ni kuongeza ushiriki wa michezo kwenye ngazi za shule na jamii. Nafikiri ndiyo mkakati wao mmoja mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa kuongeza ushiriki tu peke yake haitatosha kama Wizara haitashirikiana na Wizara nyingine kama vile TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Kwa sababu samaki mkunje angalia mbichi; vipaji vinaandaliwa watoto wakiwa bado wadogo na watoto wetu hawa kwa muda mwingi huwa tunawakabidhi shuleni, tunawakabidhi kwenye Wizara ya Elimu. Mpaka mtoto yule anaporudi kwako, kama mara nyingi anavyosema Mheshimiwa Jumanne Kishimba ambaye leo nafikiri hayuko hapa anasema tunakukabidhi mtoto yule akiwa mdogo unakuja kunirudishia mtoto akiwa mkubwa na hajui chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sasa huku shuleni kuna michezo na kwenye shule zote za Serikali huwa kuna pesa zile za capitation. Pesa zile zinaingizwa kila mwezi na ni pesa nyingi sana ambazo kama tungezisimamia vizuri, Wizara ya Michezo nayo ingekuwa inafuatilia, wakashirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI, nafikiri tungeibua vipaji vingi vya watoto wakiwa kuanzia wadogo mpaka tukawaendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo tu, tuchukulie tuna shule za msingi na za sekondari 20,000 zote jumla, na ziko zaidi ya hizo, na kila shule kwa mfano mimi nilikuwa mwalimu, kwa mwezi shule yangu ilikuwa inapokea shilingi 243,000 pesa za michezo kila mwezi kwenye kila shule ya Serikali ni asilimia kumi, unatenga pembeni, pesa ile ya capitation ambayo ilikuwa ni kama elfu ishirini na kitu hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukichukua tu ile 20,000 mara shule 20,000 ni pesa nyingi sana, ni millions of money na huo ni mwezi mmoja, sikwambii mwaka mzima, sikwambii miaka mitano. Ni billions of money tunapeleka pesa za michezo kwenye kifungu kile cha capitation lakini hakuna vipaji vinavyozalishwa huko kwa sababu kwanza hakuna vifaa, hakuna viwanja na wale wanafunzi hawana lishe, hawawezi wakashiriki michezo wakiwa na njaa, tutakuwa tunajidanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapohapo kila mwaka tuna mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA. Yale mashindano yapo toka enzi kwa hiyo sasa hivi yamekuwa tu ni kama mazoea. Tulitarajia pia kupitia mashindano yale ya michezo shuleni kila mwaka, pale ndiyo tungekuwa tunaibua wanafunzi ambao wanapenda michezo, ni rahisi sana kuwasoma pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mashindano yale huwa yanaanza ngazi za shule Tanzania nzima, yanakwenda ngazi ya Wilaya Tanzania nzima, ngazi za Kata, ngazi ya Kkoa na baadaye wanafunzi wanapelekwa Taifani. Na maeneo yote humo inakopita kwenye hiyo michakato wanafunzi huwa wanalala kambini na wanachangiwa chakula na baadaye wanafunzi wanafika mpaka mwisho Taifani tunapata washindi wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kupata wale washindi wa Kitaifa kila mwaka, hawaendelezwi na wala Serikali haitambui chochote. Na ukimuona kama kuna mchezaji ambaye ameibuka yaani ni yeye mwenyewe juhudi zake mwenyewe, usifikiri kwamba kuna jitihada za Wizara pale, hapana. Kwa asilimia kubwa wanaoibuka; si wasanii, si wachezaji, si kwenye vikundi vya ngoma, ni jitihada zake mwenyewe. Ni mwanafunzi tu alikuwa na interest ya michezo, akitoka shule anakwenda kwenye viwanja vya vumbi, anacheza na baadaye anakuwa mchezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni wakati sasa wa Wizara hizi tatu kushirikiana, hizo pesa zisipotee. Tunaweza kuibua wachezaji wengi sana kupitia pesa zile na Wizara yenyewe ikifanya jitihada. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Wizara, tunaweza tukajenga shule za kanda; ni ngumu sana kujenga shule za michezo katika kila mkoa, lakini tunaweza angalau tukaanza na kanda. Kwa hiyo, wale wanafunzi tukishakuwa tumewachagua kwenye zile UMITASHUMTA na UMISETA, ni vizuri sasa wale wakawa historia yao vizuri, ndiyo mana nasema hizi Wizara zishirikiane.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Wizara ya Elimu ndiyo yenye watoto, Wizara ya TAMISEMI ndiyo yenye miundombinu ambayo ndiyo tunaweza tukawaomba baadaye wakatusaidia kujenga shule hizo. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali tunaweza tukafikiria kujenga shule hizo za kikanda lakini pia tunaweza tukaboresha viwanja vyetu shuleni pamoja na kuboresha lishe ku-promote michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii nyeti, Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa kabla sijaanza kuchangia naomba niwapongeze Mawaziri wote wa TAMISEMI wanafanya kazi nzuri, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Dugange na Mheshimiwa Silinde.

Pia naomba niwapongeze watendaji wote wa TAMISEMI wakiongozwa na Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Prof. Shemdoe wanafanya kazi nzuri na ni wa sikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintomshukuru Mheshimiwa Rais. Kama sintamshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kutupatia fedha za UVIKO na kujenga madarasa ya kisasa Tanzania nzima, na kwa muda mfupi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintomshukuru Rais kwa kutupatia fedha za tozo kuhakikisha tunajenga vituo vya afya; kuna baadhi ya vituo vya afya tulipata Milioni 250 za awali kwa ajili ya vituo vya tozo kwa Mkoa wetu wa Tanga, pia ni juzi tu zimeingizwa Milioni 250 tena kwa ajili ya umaliziaji wa vituo hivi vya tozo, tunamshukuru sana Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu sasa kwa TAMISEMI ni kuhakikisha wanatoa maelekezo kwa Wakurugenzi, vituo hivi vya tozo vinakwenda kukamilika kwa wakati kwa sababu fedha zake zote Milioni 500 baadhi ya maeneo imekamilika na imeshapelekwa. Kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI muongeze nguvu muendelee kuwa-puSh Wakurugenzi ili vituo hivi vikamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo mtoe maelekezo kwa Wakurugenzi. Baadhi ya Wakurugenzi wanafanya kazi nzuri sana, lakini baadhi ya Wakurugenzi kwa kweli ni tatizo na wanawaangusha sana TAMISEMI. Sasa hivi tupo safarini tupo baharini kwa hiyo tukiona mtu yeyote ana dalili ya kutoboa mtumbwi ni vizuri Mheshimiwa Waziri mapema tukamtosa yeye baharini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, zipo baadhi ya Halmashauri ambazo hazikutekeleza kabisa miradi ambayo tuliwapitishia mwaka jana kwa ajili ya bajeti na badala yake wamejificha kwenye madarasa ya UVIKO na vituo vya afya vya tozo. Kwa hiyo, kila unapokwenda kwenye ukaguzi kwenye Halmashauri wanakuonesha miradi ya UVIKO na miradi ya tozo lakini wao hawakutekeleza miradi yao kwa mapato yao ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zipo baadhi ya Halmashauri ambazo zimeishaingiziwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, zipo nazifahamu, naomba Mheshimiwa Waziri baada ya wachangiaji utakapokuja kukamilisha hotuba yako utoe tamko kuhusiana na Wakurugenzi ambao wamepelekewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi, fedha zipo kwenye akaunti lakini mpaka sasa wengine wapo kwenye hatua za msingi, wengine wanamwaga jamvi! Wakurugenzi hawa wanawaangusha Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Wizara yako, madarasa yamejengwa ni mazuri na ni mwaka jana tu baadhi ya shule wameongezewa shule za Kidato cha Tano na cha Sita, lakini shule hizi hazina uzio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano shule ya Tanga Tech pale Tanga Mjini ni shule kubwa na ni shule kongwe. Zamani ile shule ilikuwa ipo mbali sana na makazi ya watu lakini kadri mji unavyokua makazi ya watu yamekuwa yapo karibu sana na ile shule na shule ile haina uzio ni hatari sana kwa vijana wetu lakini hata shule ya Galanosi, Maramba High School na baadhi ya shule nyingine nyingi za Tanzania. Kwa hiyo, naombeni pia mje na mkakati wa kuzijengea uzio hasa shule zetu za bweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo fadhila kama sintaungana na wenzangu kuhusu posho za Madiwani. Mheshimiwa Waziri Madiwani wanafanya kazi kubwa ya kusimamia miradi yetu lakini pia Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Watendaji Kata, Watendaji wa Mitaa na Watendaji wa Vijiji. Kwa hiyo, naomba nao pia waangaliwe kwa jicho la huruma. Madiwani wajaribu kuongezewa posho lakini Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Watendaji…

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hawa Mchafu taarifa.

T A A R I F A

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nasimama kwa Kanuni ya 77(1). Napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mzungumzaji aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema hapa kwamba taratibu au mchakato kuhusiana na posho za Madiwani tayari ulishaanza. Kwa hiyo, Wizara ni ileile, Naibu Mawaziri ni wale wale pengine aliyebadilika ni Waziri. Tulikuwa tunaomba sasa waanzie pale alipoishia Mheshimiwa Ummy Mwalimu na kuendelea mbele kuhusiana na hii posho ya Madiwani. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji. Ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Hawa kwa taarifa ambayo inaboresha mchango wake. Taarifa inatakiwa iwe uelekeo kama huo, kuna kitu kina-miss unakiongezea. Ahsante endelea Mheshimiwa unaipokea taarifa?

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru sana kwa taarifa naipokea. Naomba Watendaji Kata, Vijiji na Mitaa hasa ukizingatia mwaka huu tunakwenda kwenye Sensa ya Watu na Makazi wapewe mafunzo. Tunacho Chuo chetu cha Utumishi ambacho kazi yake hasa ni kuendelea kuwajengea uwezo Watumishi wetu wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji hawa wanafanya kazi kubwa na mwananchi wa kawaida kabisa Serikali yake ya kwanza anayokutana nao ni hii. Tulishuhudia baadhi ya miradi tukiwa tunakwenda kukagua miradi, wananchi wanamsikiliza Mtendaji wa Kijiji kuliko Mkurugenzi. Wananchi wanamsikiliza Mtendaji wa Kijiji kuliko hata Mkuu wa Wilaya (DC), kwa hiyo watu hawa ni muhimu sana tusiwaache wapewe mafunzo ya muda mfupi wakiwa kazini kupitia Chuo chetu cha Utumishi ambacho kina matawi yake kila Kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna chuo hiki Tabora kwa ajili ya Kanda Ziwa na Kanda ya Magharibi, lakini kipo Chuo hiki Dar es Salaam kwa ajili ya Kanda ya Mashariki, pia kuna branch nyingine ipo Tanga kwa Kanda ya Kaskazini, kipo Chuo hiki Singida kwa ajili ya Kanda ya Kati, pia kipo Mtwara kwa ajili ya Kanda ya Kusini na kipo Mbeya kwa ajili ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana TAMISEMI na Katibu Mkuu najua atalibeba hili, Naomba Katibu Mkuu hangaika nalo hili kutafuta fedha kwa ajili ya hawa watu kupatiwa mafunzo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, nisije nikasahau maana ya Wizara hii kidogo ni mazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi nashindwa nianzie wapi. Changamoto ya ajira ni kubwa sana, na wote tunashuhudia kila Mbunge sasa hivi ana kimemo cha kuombwa ajira na wananchi wake, lakini sasa matarajio yetu kuna baadhi ya Wizara ambazo zingeenda kutatua changamoto hii ya soko la ajira, ikiwemo Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Michezo pamoja na Wizara ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa nasikitika sana sijui kama Wizara hii itaweza kutatua changamoto hii ya soko la ajira. Kwa sababu nikisoma hizi Taarifa za Waziri na Kamati, Wizara hii hata makusanyo yao tu yenyewe hawawezi kukusanya ambayo wenyewe wamekadiria ili wakusanye, hawawezi kukusanya na hawafiki lengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka 2022/2023 Wizara hii ililenga kukusanya bilioni 80.1 ambayo mifugo ikusanye bilioni 40.1 na uvuvi bilioni 40 lakini mpaka wanafikia mwezi Februari quarter tatu zimepita Wizara ya Mifugo imekusanya bilioni 16.6 na Wizara ya Uvuvi bilioni 13.3 kati ya bilioni 40 sawa na asilimia 33. Tumebakiza robo moja ya mwaka; na kwa makusanyo yote jumla wamekusanya kwa asilimia 37.5.
Kwa muundo huu hawawezi kufikia lengo; na sijui kwa nini hawafikii lengo na makadirio haya wameweka wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko Kamati ya TAMISEMI, kule kuna halmashauri zinakusanya makusanyo yake zinavuka lengo, zinakwenda asilimia 104, 110, yaani wanakusanya mpaka wanavuka lengo. Hata wale ambao hawavuki lengo basi angalau wanakuwa juu ya asilimia 50, lakini kwa Wizara hii sidhani kama watafika hata asilimia 50 mpaka kufika mwezi wa saba; kwa hiyo napata wasiwasi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini makadirio ya bajeti ya kipindi kinachokuja cha mwaka 2023/2024 wameongeza tena bilioni mbili wakisema wataongeza makusanyo. Sasa napata wasiwasi; kama huu mwaka uliopita hata sidhani kama watafika nusu ya makusanyo lakini mwaka huu unaokuja wanasema wataongeza kidogo watakusanya bilioni 82.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulega lazima waje na mikakati Madhubuti ya kuhakikisha wanaongeza makusanyo, vingenevyo hata mama mwenyewe hataona haja ya kuongeza bajeti kwenye hii Wizara. Kwa sababu hata kile ambacho wanakikadiria, yaani wao wenyewe hawajiwezi, kwa hiyo hataona sababu ya kuwawekeza sehemu ya watu ambao hawajiwezi, anaona akiweka huko fedha itaendelea kupotea. Fedha itakwenda, miradi itatekelezwa lakini hawatakusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulega yeye ndiyo umeingia juzi, wao ni wachapakazi, Mheshimiwa Silinde tumefanya wote kazi akiwa TAMISEMI, lakini Mheshimiwa Ulega mtani wangu yeye mwenyewe anajua; tangu mimi nimeingia Bunge hili kati ya Wizara ambazo nazifatilia kwa karibu sana ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wewe mwenyewe ni shahidi. Kwa hiyo nimuombe, sina wasiwasi na uchapakazi wake, aenende akaweke mikakati pamoja na watendaji wake wa kuhakikisha anaongea makusanyo. Atatupa nguvu sana hata sisi Waheshimwa Wabunge wampiganie ili waendelee kuongezewa bajeti ya Wizara yao. Lakini sasa kama hawawezi kukusanya tutashindwa kupiga kelele wao waongezewe bajeti, kwa sababu hata kile kiasi wanachopewa kitakwenda kupotea. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aje atueleze mikakati yake hasa ya kuhakikisha anakwenda kufikia lengo la makusanyo kwanza malengo ambayo wao wameyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya miradi hii ya maendeleo walipewa bilioni 182 ya miradi ya maendeleo, lakini sasa hizi fedha za maendeleo zinatengwa, ambazo kwa mifugo walipewa bilioni 46.7 na uvuvi bilioni 135; lakini hizi fedha hazipelekwi, yaani ni hela walizotengewa lakini hazipelekwi, kwa hiyo hawawezi kufanya kazi. Kwa mfano kwenye uvuvi kati ya bilioni 135.6 imepelekwa bilioni sita pekee kwa ajili ya miradi ya maendeleo, wakati sisi TAMISEMI mradi mmoja tu wa soko la Nyamagana ni bilioni 20. Kwa hiyo sasa unaweza ukaona hapo, Wizara nzima ni mradi mmoja wa soko kwenye halmashauri moja, ndio wanapewa kama fedha za maendeleo kwa Wizara nzima ya Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Ulega hawawezi kutoboa, mradi mmoja wa maendeleo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mzamili, muda wako umeisha, malizia.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha ahsante sana nashukuru. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri; Wizara hii ina migogoro mingi, na kati ya vitu vinavyosababisha migogoro pia ni malisho. Jana nilimsikia alikuja na mkakati wa malisho akasema atazalisha malisho ya kwenda kuuza mpaka nchi za Asia. Nishauri aachane na hii habari ya kuuza nchi za Asia kwanza …

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: … tutosheleze malisho ya hapa Tanzania kila mwaka ng’ombe wanakufa na wewe mwenyewe ni shahidi hauwezi kuuza Asia ilhali sisi wenyewe bado hatujajitosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa mimi naomba nisiipongeze Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wetu wa Ukanda wa Pwani hali zao ni duni sana kiuchumi na wote ni mashahidi. Mkoa wetu wa Tanga tuna bahari Wilaya ya Mkinga, Tanga, Muheza na Pangani katika Mkoa wetu wa Tanga. Mkakati waliokujanao mwaka jana ambao ndiyo mwaka wa fedha huu tunamalizia, walikuja na mikakati mizuri sana na mipango mizuri. Ukisikiliza mikakati yao ya mwaka jana mwaka wa fedha 2021/2022 na mipango yao ya mwaka 2021/2022 unasema basi hawa Wavuvi sasa hawaendi kutafuta kazi nyingine ya kufanya. Lakini cha kusikitisha mikakati ile ya mwaka jana ambayo walikuja nayo hakuna mkakati hata mmoja ambao wameutekeleza. Sasa Napata wasiwasi kama mikakati ile yam waka wa fedha 2021/2022 haikutekelezwa, sasa hivi tunakwenda kupitisha bajeti ya 2022/2023, sasa sijui hiyo watatekeleza vipi napata wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukiangalia mikakati yao ya mwaka jana walituambia kwenye Bunge hili wataweka miamba ya kuvutia Samaki ili kuongeza uzalishaji kwenye ukanda wetu ule wa pwani kwa Mikoa ya Tanga, Pwani, Dar-es-Salaam, Lindi na Mtwara. Hiyo miamba siyo kuiona tu hata kuisikia huko Pwani mimi ninakotoka sijaisikia! Sijaisikia na haipo. Hata Waziri wakati anasoma hotuba yake hakutaja kabisa pia hakutaja kwenye mwaka wa fedha huu anaohama nao kuwa labda tulishindwa mwaka huu, lakini mwaka unaokuja tutafanya, hawakusema! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye bajeti yao ya mwaka 2021/2022 walituahidi hapa watatengeneza vichanja kwa ajili ya kukaushia samaki na dagaa ili kuhakikisha wanapunguza upotevu wa mazao haya ya samaki. Baada ya kutuahidi yale kwa sababu niliuliza mpaka swali mwaka jana na nilijibiwa hapa nikaambiwa vichanja vile vinapelekwa, mimi nikaenda kule nikawaambia wanawake wenzangu wa Mkoa wa Tanga jamani jipangeni vichanja vinakuja na watu wamejiandaa vikundi viko kule wanasubiria vichanja. Vichanja mpaka leo havijaenda, imebakia miezi miwili tunamaliza hii bajeti hakuna kichanja kimekwenda. Sijasikia tena kwenye mpango wao hata kwenye hotuba sijasikia kuwa mwaka jana tuliahidi hivi lakini tumeshindwa na mwaka huu tutaendelea. Sijasikia na haipo na vichanja havipo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwaka jana hapa walituahidi wakasema wataongeza uzalishaji wa barafu na kujenga cold rooms kwa ukanda, tena walisema siyo cold rooms tu cold rooms za kutosha kwa Ukanda mzima wa Pwani kuanzia Tanga mpaka Mtwara. Mpaka leo hivi ninavyosema sijaona cold rooms hata moja hata tu ya mfano huko ninakotoka haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walituahidi hapa watakuja kuweka hizi cold rooms kwa sababu kama tunavyofahamu mazao ya samaki huwa yanaharibika kwa muda mfupi sana, sisi tunaotoka Ukanda ule wa Pwani samaki huwa hawavuliwi siku zote ndani ya mwaka mzima, kuna siku samaki wanapatikana kwa wingi na kuna siku samaki hawapatikani kabisa, kwa hiyo lengo lao lilikuwa ni zuri kuwasaidia hawa wavuvi kwamba, zile siku wanazopata samaki kwa wingi wangeweza kuhifadhi hata zile siku ambazo hawapati samaki bado wangeweza kuendelea kufanya biashara, lakini haipo, haijatekelezwa, sijaisikia kwenye mpango uliopita na sijaisikia kwenye mpango huu tunaokwendanao, sasa sijui imepotelea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walituahidi hapa mwaka jana watakuja kujenga soko la kisasa la samaki, baadhi ya maeneo likiwepo soko la samaki la Kipumbwi, Wilayani Pangani. Nalo nimesikia wamelisema, mwaka jana walisema watajenga kwa bajeti ile ya 2021/2022, hakuna msingi uliojengwa, hakuna hata soko lililoanza kujengwa. Kwenye bajeti hii wamesema tena tutajenga soko, wameliweka tena kwenye bajeti ya 2022/2023. Kwa hiyo, mwaka jana hata msingi tu, labda wangesema tumeanza tutaendelea, hata msingi tu haupo! Kwa hiyo, sasa napata wasiwasi sana na bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti yao pia ya 2021/2022 walituahidi hapa watanunua boti ya uvuvi kusaidia kule wavuvi wetu, sasa safari hii sijalisikia, badala yake sasa wamekuja kutuambia watanunua meli kubwa za uvuvi. Sasa kama yale boti hazikununuliwa hivi wataweza kweli kununua meli? Hapo napata wasiwasi? Badala yake sasa wametuambia walinunua boti za doria, siyo ya uvuvi tena. Wamesema tumenunua boti za doria, sasa nikawa sielewi nachanganyikiwa kabisa! Kwa hiyo, boti zilishindikana safari hii tutanunua meli kubwa za uvuvi, sijui ni meli tatu, sijui tano? Sasa napata mashaka kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara kwa sababu mambo mengi hawajayatekeleza yale waliyotuahidi mwaka jana, naomba sasa watueleze mikakati yao hasa madhubuti ya mwaka huu 2022/2023 watakwenda kufanya nini ili kuongeza uzalishaji wa wavuvi hawa kwa maeneo yetu yale ya Pwani na maeneo mengine hata ambayo siyo ya Pwani lakini kwa wavuvi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watatuhakikishia vipi, ni upi mkakati wao wa kuhakikisha wanawaunganisha wavuvi hawa na masoko? Waje hapa tuwe na mkakati wa uhakika, wavuvi wanahangaika sana, wanavua samaki wanazunguka nao kutwa nzima, mara wameoza, anakwenda anamwaga samaki. Sasa sielewi wakati kuna nchi kibao za jirani hazina kabisa bahari na wangependa wapate samaki kutoka kwetu, sasa sijui, Waziri aje na mkakati. Ni mkakati gani wa kuhakikisha wanawaunganisha wavuvi wetu na masoko ya uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia waje watumabie hapa ni mkakati gani wanaokuja nao wa kuhakikisha wanawawezesha wavuvi wetu kuongeza thamani mazao yao haya ya bahari? Waje hapa na mkakati wa uhakika watuambie ni mkakati gani wameuweka wa kuhakikisha watawaunganisha hawa wavuvi wetu na taasisi hizi za kifedha ili waweze kupata fedha za kuendelea kufanya shughuli zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wetu wale wa Ukanda wa Pwani pia wamehamasika sana kulima zao hili la mwani. Kwenye hotuba ya Waziri sijasikia kabisa akiongelea, hajagusa kabisa! Lakini ninawashukuru Wizara walikuja kama mara mbili, mara tatu, kupitia Naibu Waziri wa Uvuvi kwa wakulima wetu wale wa mwani waliwaletea vifaa kama vile viatu na kamba. Waliwawezesha, lakini changamoto bado ni kubwa sana, zao hili la mwani kwa Wabunge wasiofahamu ni zao muhimu sana, linatengeneza vitu vingi sana. Kwa mfano tunaweza kutengeneza sabuni ya unga…

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako Mheshimiwa.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hili zao la mwani tunaweza kutengeneza sabuni ya unga, sabuni ya maji, sabuni ya kipande, mafuta ya mgando, mafuta ya maji na juice pia, Mheshimiwa Ulega anafahamu. Kwa hiyo, ninaomba sasa Wizara waje watuambie watawasaidiaje hawa wakulima wa mwani kupata masoko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niunge mkono hoja. (Makofi)