Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Husna Juma Sekiboko (17 total)

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fedha za matumizi mengineyo (OC) kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya kama inavyotoa kwa Wakuu wa vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mahali hapa, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ametujalia tumekutana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii niwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Uzini kwa uzalendo na mapenzi makubwa ya kunichagua kwa kura nyingi nikawa Mbunge. Maana wamenitoa kutoka kwenye mavumbi, wamenitoa kwenye majalala, wamenileta kwenye viti, nimekaa na wafalme. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, aidha, nichukue fursa hii nimshukuru na kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, maana baada ya Mungu kuweka baraka, naye ikampendeza akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

SPIKA: Sasa jibu swali Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kama Taasisi ya Serikali hupokea fedha za matumizi (OC) toka Wizara ya Fedha na huzigawa fedha hizo kupitia Kamati Maalumu ya Fedha (Tanzania Police Force Resources Committee), ambayo huzigawa fedha hizo kwenda kwa Makamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Mikoa na Vikosi; na hao ndiyo wenye mamlaka ya kupata OC kisheria.

Mheshimiwa Spika, jukumu la kugawa fedha kwenda kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya hufanywa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa husika kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila Wilaya, kama vile ukubwa wa wilaya, Idadi ya vyombo vya usafiri ilivyonavyo, ikama ya Askari na takwimu za matukio ya kihalifu yaliyopo. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaoshindwa mitihani kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwaendeleza vijana wakiwemo wale ambao hawakubahatika kuendelea na ngazi ya elimu inayofuata ya masomo baada ya kuhitimu. Hii ni kwa sababu vijana hawa ndiyo rasilimaliwatu ya Taifa inayotegemewa katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mipango mbalimbali ya kuwaendeleza vijana hao. Mipango hiyo ni pamoja na ujenzi wa Vyuo vya VETA katika ngazi za Mikoa na Wilaya pamoja na ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2020/ 2021, Serikali imeendelea na ujenzi wa vyuo vipya vya VETA 29 katika ngazi ya Wilaya ambavyo vinatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kwa lengo la kuwezesha wananchi na vijana kupata ujuzi mbalimbali. Aidha, vipo vyuo 34 vya Wilaya na 22 vya Mikoa ambavyo vinadahili wanafunzi katika fani mbalimbali na hivyo kutoa fursa kwa vijana hao kujiendeleza na kupata ujuzi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba wazazi na Watanzania kwa ujumla kutumia vyuo hivyo ili kuwawezesha vijana na wananchi wengine kujiendeleza na kupata ujuzi katika fani mbalimbali. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:-

Je, Serikali inatumia njia gani kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupata mafunzo ya ujasiriamali, uandaaji wa maandiko ya miradi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili wapate mikopo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini wa kipato katika jamii. Serikali imeweka kipaumbele katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kama mkakati wa kufikia usawa wa kijinsia katika nyanja zote.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuwezesha wanawake kiuchumi na kuwaunganisha na taasisi za mikopo inaratibu makongamano ya kiuchumi ya wanawake wajasiriamali ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/ 2020 hadi sasa Serikali imewezesha makongamano matano (moja katika kila mkoa) katika mikoa mitano (5) ya Arusha, Dodoma, Singida, Ruvuma na Mbeya kati ya makongamano 26 ya mikoa iliyopangwa.

Mheshimiwa Spika, katika makongamano haya elimu ya matumizi ya teknolojia rahisi na sahihi katika uzalishaji, kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi pamoja na umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora wa bidhaa zinazozalishwa ili kukidhi matakwa ya kisheria na masoko inatolewa. Aidha, makongamano haya yamewafikia takribani jumla ya wanawake 2,768 kati ya 1,500 waliolengwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na SIDO, TBS, TMDA, BRELA na Halmashauri imeendelea kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali hapa nchini katika stadi mbalimbali za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na namna ya uboreshaji wa huduma na bidhaa zinazozalishwa na wanawake na uandaaji wa maandiko ya miradi. Katika kipindi cha mwaka 2019/2020 jumla wanawake 3,424 walifikiwa kati ya 5,000 waliolengwa.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya malengo ya Mtaala wa Elimu ya Msingi na Sekondari nchini ili kuendana na uhitaji wa sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufanyia marekebisho mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ili kuwawezesha wanafunzi kupata stadi mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya wakati. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikiboresha mitaala hiyo kila kunapokuwa na hitaji la kisayansi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imepanga kufanya mjadala mpana kuhusu mfumo wa Elimu nchini ambao utahusisha Sera ya Elimu na Mitaala kwa ujumla ili iendane na wakati na ikidhi mahitaji ya sasa na baadaye. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuhamisha Dawati la Kijinsia kutoka Jeshi la Polisi na kwenda kwenye Vituo vya kutolea Huduma za Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria mbalimbali za Nchi. Jeshi la Polisi limepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, Fungu Na. 5, Kifungu kidogo cha (322) ya mwaka 1965 na kuboreshwa mwaka 2002 ya kulinda raia na mali zake na kupeleleza makosa mbalimbali. Hivyo, Dawati hilo ni vyema likaendelea kukaa lilipo sasa badala ya kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanapatiwa huduma rafiki na za haraka, Dawati hili hushirikiana na Vituo vya Mkono kwa Mkono ambavyo viko kwenye Vituo vya Afya vikiwa na Wataalam wa Afya, Maafisa wa Jeshi la Polisi, Ustawi wa Jamii na Wanasheria kwa ajili ya utoaji wa huduma stahiki.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Wanawake na Watoto wanapata shida Baba wa familia anapofariki; pamoja na Sheria ya Mirathi;

Je Serikali ina mpango gani zaidi wa kumsaidia mjane katika masuala ya mirathi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia na kusemea kwa nguvu kuhusu dhuluma wanazofanyiwa wanawake na watoto mara baada ya baba wa familia kufariki.

Mheshimiwa Spika, sheria zinazohusiana na mirathi, zinatamka wazi kuwa wanufaika wa mirathi ni mke wa marehemu, watoto wa marehemu na wazazi wa marehemu. Vilevile inaelekeza kuwa msimamizi wa mirathi si mrithi wa mali za marehemu labda atokane na makundi tuliyoyataja hapo juu. Uteuzi wa msimamizi wa mirathi hufanywa na kikao cha familia na baadaye kuthibitishwa na Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kuendelea kwa vitendo vya dhuluma, udhalilishaji wa familia ya marehemu akiwemo mke na watoto, Serikali imeanza kupitia upya Sheria ya Usimamizi wa Mirathi hiyo katika kubaini mapungufu ili iweze kurekebishwa. Kwa kuwa mchakato huo uhusisha taasisi za dini, mchakato umeanza wa kukutana nao na pia kukutana na viongozi wa makabila mbalimbali ili kupitia mila zao ambazo nyingi ni za udhalilishaji.

Mheshimiwa Spika, ikibainika kutokea vitendo vya dhuluma kwa wanafamilia waliopoteza baba wa familia inaelekezwa kwenda Mahakamani kutafuta haki zao. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge kutoa ushirikiano wa familia hizo ambazo nyingi hazina uelewa mkubwa wa masuala ya kisheria kufikia ili huduma hii na waweze kupata haki zao. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Lushoto – Magamba – Lukozi – Mlalo hadi Umba Junction kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Lushoto – Magamba – Lukozi – Mlalo hadi Umba Junction ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 66.23 na inasimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Hadi sasa jumla ya kilometa 9.1 kati ya Lushoto na Mazinde Juu zimejengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka huu wa fedha 2021/2022, jumla ya Shilingi milioni 420 zimetengwa ili kuendeleza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa kipande chenye urefu wa mita 400. Kazi za ujenzi zilianza mwezi Januari, 2022 na kazi zinategemewa kukamilika mwezi Juni, 2022. Hadi tarehe 10 Februari, 2022 kazi zilikuwa zimefikia asilimia 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa awamu kulingana na upatikana wa Fedha. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaifanya elimu ya sekondari kuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa lengo la kuiboresha elimu yetu ili iweze kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kupokea na kuchambua maoni ya wadau kuhusu Sera ya Elimu, hivyo suala la elimu ya sekondari kuwa ya lazima itategemea maoni ya wadau na mahitaji ya wakati. Rasimu ya kwanza ya Sera ya Elimu inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2022. Nakushukuru.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y. MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, kuna athari gani za kijamii kwa watumishi wenza kuishi mbali na watoto wao?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, familia ni taasisi muhimu sana katika kuleta ustawi kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Ni kweli kuwa yapo madhara ya kijamii kwa watumishi wenza kuishi mbali na watoto wao madhara hayo ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa watoto majumbani; kukosa malezi chanya inayopelekea watoto kuathirika kisaikolojia; watoto kutokupata lishe bora inayopelekea udumavu na mmomonyoko wa maadili na kuvunjika kwa ndoa kunakosababisha watoto wa mtaani. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa Serikali katika kuziendeleza timu za michezo za watoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini michezo ya watoto kwa kuwa umahiri wa timu mbalimbali unatokana na ushiriki mzuri wa watoto katika ngazi za chini ambazo hupelekea urahisi wa kuibua na kuendeleza vipaji. Serikali ina mkakati wa kuziendeleza timu za watoto kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mashindano mengi yanayohusisha watoto ili kuwajengea uzoefu.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya mikakati hiyo ni pamoja na uendeshaji wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA, ukarabati wa miundombinu ya michezo katika shule 56 teule za michezo, pamoja na usajili wa vituo vya michezo ya watoto (sports academies). Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuandaa mashindano ya timu za watoto na kuwajengea mazingira wezeshi ya kuendeleza vituo hivyo. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa lengo la kukomesha tabia ya udanganyifu katika mitihani ya Taifa ikiwemo mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo. Hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa walimu, wasimamizi wa mitihani na wadau wote wa elimu kuhusu athari za udanganyifu katika mitihani ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza jukumu la usimamizi wa mitihani hiyo kwa uadilifu na kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa kwa ajili ya uendeshaji wa mitihani.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa kutokana na udanganyifu katika mitihani ni hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za nchi. Hatua hizi zimekuwa zikichukuliwa kwa Walimu, wasimamizi na wadau wote wanaohusika katika kusimamia mitihani pale ambapo ilibainika pasina shaka kuwa walishiriki katika kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria wahusika wote wanaojihusisha na udanganyifu wa mitihani ili kuhakikisha kuwa nchi inapata wataalam wenye sifa stahiki. Nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti matumizi holela ya Dawa za Binadamu nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti matumizi holela ya dawa za binadamu nchini Serikali inatekeleza mambo yafuatayo: -

(i) Kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ikiwemo vipindi vya elimu kwa umma kwa kutumia wataalamu wa dawa.

(ii) Kusimamia muongozo wa matibabu nchini unaobainisha matibabu kwa kila ugonjwa ikiwemo dawa zinazohitajika kutibu magonjwa hayo.

(iii) Kusimamia weledi wa watoa dawa katika maeneo yote yanayohusika na utoaji wa dawa kama vile maduka ya dawa na vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je Serikali inachukua hatua gani za kimkakati kufikia usawa wa kijinsia 50/50 ifikapo 2025?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuundwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kama chombo maalum cha kuratibu ajenda ya kufikia usawa wa kijinsia. Aidha, hatua nyingine ni Serikali kuendelea kutoa fursa na nafasi za uongozi na maamuzi kwa wanawake mathalani, kipengele cha 12(4) cha Kanuni za Utumishi wa Umma mwaka 2013, kinasema, “Inapotokea mwanamke na mwanaume wametimiza vigezo sawa kwa kulingana, basi kipaumbele atapewa mwanamke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji na Wilaya ya Mwaka 1982, inasema kuwe na asilimia 25 ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi. Aidha, katika uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005 asilimia hizo zilipandishwa hadi kufikia asilimia 31 ambayo ni moja ya tatu ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali inatambua gunia kuwa kipimo au kifungashio kwa mujibu wa Sheria?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo, The Weights and Measures Act (Amendment) Order, G.N. No. 725 of 2018, jedwali la 10 chini ya kifungu cha 2(b) cha Jedwali hilo ambacho kinasema mazao ya mashambani yatafungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu 100. Pamoja na kuelekeza wauzaji au wanunuzi wa mazao kutumia mizani, Serikali haitambui gunia kuwa kipimo bali ni kifungashio.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nitoe wito kwa wadau wote kuepuka matumizi ya gunia kama kipimo kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Vipimo, nakushukuru.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza huduma za afya na dawa zinazotolewa na Bima katika zahanati na vituo vya afya?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuongeza huduma za afya na dawa zinazotolewa na bima katika Zahanati na Vituo vya Afya imefanya yafuatayo:-

(i) Kuongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya zahanati kutoka aina 254 mwaka 2015 hadi kufikia aina 451 mwaka 2023.

(ii) Kuongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya kituo cha afya kutoka aina 414 mwaka 2015 hadi kufikia aina 828 mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa zilizoongezeka zipo katika miongozo ya Serikali na hivyo zinalipiwa na Bima ya Afya kwa wanufaika wa mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuongeza dawa Serikali imeboresha miundombinu, uwepo wa vifaatiba, huduma za maabara pamoja na rasilimali watu. Hata hivyo, Serikali inatambua kwamba kuna maeneo ya nchi ambayo uboreshaji huu haujafikia, hivyo ipo katika mikakati wa kuyafikia maeneo hayo.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:-

Je, ni kwa namna gani Serikali inalinda afya ya mama mjamzito na mtoto mchanga?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulinda afya ya mama mjamzito na mtoto mchanga, Wizara inafanya yafuatayo:-

(1) Kila mama mjamzito anayehudhuria kliniki anapata vipimo muhimu ikiwemo vipimo vya wingi wa damu, shinikizo la damu na kipimo cha protini kwenye mkojo ili kubaini mapema matatizo ya ujauzito;

(2) Matibabu na huduma ya mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano yanatolewa bila malipo katika vituo vyote vya Serikali;

(3) Serikali imeimarisha upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya kutibu matatizo yatokanayo na uzazi kwa kufikia asilimia 50 kwa vituo vyote vya kutolea huduma; na

(4) Watoa huduma za afya ya uzazi wamejengewa uwezo ili waweze kutoa huduma stahiki kwa akina mama wanaopata changamoto za uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wananchi wote hasa akina mama wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki na pia kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya kuvuja kwa mitihani inayosimamiwa na vyuo vya afya mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kutokea kwa changamoto ya kuvuja kwa mitihani inayosimamiwa na vyuo vya afya mwezi Agosti, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua zifuatazo ili kuhakikisha kuwa tatizo hili halijitokezi tena kwa kufanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza; ni kuboresha mfumo wa utungaji, uchapishaji na ufungaji wa mitihani kwa kushirikiana na Mpiga Chapa wa Serikali.

Jambo la pili ni kufanya mapitio ya Mwongozo wa Mitihani iliyo chini ya Wizara ya Afya ili kuendana na mahitaji ya kiulinzi na kiusalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kuongeza kasi ya kuanzishwa Mamlaka itakayosimamia mafunzo ya vyuo vya afya ngazi ya kati pamoja na uendeshaji wa mitihani.

Jambo la nne ni kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwenye ulinzi wa mitihani katika hatua zote kuanzia utungaji, usambazaji hadi utoaji wa matokeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.