Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Neema Gerald Mwandabila (4 total)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo imeweza kunijibu, lakini kiupekee kabisa nataka nitoe angalizo kwa Serikali kwamba Kituo cha Afya Tunduma asikichukulie kama vituo vingine ambavyo viko nje ya mpaka wa Tunduma kwa maana mahitaji yake yanakuwa ni makubwa zaidi, kwa hiyo anaposema kwamba ataweza kupunguza watumishi Tunduma tena awapeleke kwenye hospitali hiyo inayojengwa naona kama bado changamoto itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninapenda niulize maswali yangu mawili ya nyongeza; ni lini hasa Serikali itaweza kuanzisha huduma katika hii hospitali inayojengwa ambayo ameweza kutuonesha kwamba asilimia 82 ya ujenzi imeshafanikishwa. Kwa hiyo, ninatamani kujua ni lini hasa huduma zitaanza kutolewa pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ninapenda kufahamu mahitaji ya kituo cha afya kulinga na na nature ya watu wa pale tunahitaji madaktari, na madaktari aliyosema nina uhakika ni hao madaktari wawili ambao wanasubiria Hospitali ya Wilaya ianze kufaya kazi.

Sasa basi ninatamani kujua ni lini hasa Serikali itpeleka madaktari na wauguzi wakunga, siyo wahudumu wa afya kama walivyoweza kuanisha kwenye majibu yao, mahitaji yetu ni madaktari na wauguzi wakunga, specifically hapo ninapenda kupata majibu. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumhakikishia Mheshimiwa Mwandabila kwamba Serikali inakichukulia kwa umuhimu wa hali ya juu sana Kituo cha Afya cha Tunduma kwa sababu ya idadi ya wananchi wanaohudumiwa katika kituo kile na ndiyo maana katika maelezo yangu ya msingi nimeeleza namna ambavyo Serikali imepeleka watumishi wengi sana, watumishi 22 wa ziada ukilinganisha na ikama ya mahitaji ya kituo cha afya, na hiyo ni dalili kwamba Serikali inajali na kuthamini sana huduma za Kituo cha Afya cha Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba kwa sababu tunaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Tunduma, kwa vyovyote vile, idadi ya wagonjwa watakaotibiwa katika kituo cha afya itapungua na wengine watakwenda kutubiwa katika Hospitali ya Mji wa Tunduma itakapokamilika. Kwa hiyo, ile idadi ya wagonjwa ambayo itaondoka Kituo cha Afya cha Tunduma itakwenda kuhudumiwa katika hospitali ya mji na watumishi hawa waliopo. Lakini pia Serikali itakwenda kuajiri watumishi wengine kama ambavyo mpangio upo katika mwaka wa fedha ujao ili tuweze kuongeza watumishi katika hospitali ile ya mji lakini pia katika Kituo cha Afya cha Tundma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Hospitali hii ya Mji wa Tunduma inayojengwa inatarajia kuanza huduma za awali za OPD ifikapo tarehe 27 Aprili, 2021 ili wananchi wetu waanze kupata huduma za awali za OPD wakati shughuli za umaliziaji na ujenzi wa miundombinu mingine inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza japo majibu walionipa angalau yanaridisha.

Swali la kwanza, natamani kufahamu; kwa kuwa magereza wao wamekiri bado uwezo wa kulisha mahabusu na wafungwa ni mgumu, upo kwa asilimia 54. Je, hawaoni sasa ipo haja ya hawa mahabusu kuweza kushirikishwa kuzalisha chakula chao tu kwa sababu maandiko yanasema kila mtu atakula kwa jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili natamani kufahamu; tunafahamu kabisa Magereza changamoto ya magodoro ni kubwa sana. Katika changamoto hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha magodoro yanakuwepo kule, lakini hali bado ni ngumu; na tunafahamu kuna taasisi nyingi sana zinazokuwa zinahitaji magodoro kama shule na Serikali haiwapatii:-

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya mahabusu au wafungwa wote wanaokuwa wanafungwa wakawa na kigezo cha kwenda na magodoro yao ili kuweza kupunguza changamoto ile kwa sababu sio wote wanashindwa kuwa na godoro hilo kuliko kuiongezea Serikali mzigo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kanuni au Sheria, hakuna eneo ambalo linakataza kwamba watu kuingia na vitu wanavyovitaka katika Magereza, lakini sasa sababu mbili ndizo ambazo zinatufanya mpaka tufike hatua ya kusema kwamba haiwezekani kila mtu aingie na kitu chake Gerezani. Sababu ya kwanza, moja ni busara ya Jeshi la Magereza kama Jeshi la Magereza. La pili, ni sababu za kiusalama.

Mheshimiwa Spika, unapochukua kitu ukakiingiza kwenye Magereza, maana yake kinaweza kikachomekwa kitu kingine ndani yake ambacho kinaweza kikaja kuwadhuru wengine. Ndiyo maana hata ukifika wakati ukitaka kuleta chakula au dawa au kitu kingine, lazima tukithibitishe tukihakikishe na tujue kwamba hiki kina usalama kwako, kwetu tunaokipokea na kwa yule ambaye anakwenda kukitumia. Kwa hiyo, suala la kila mtu aingie na godoro lake, pazito kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine tunaweza tukajikuta tunatengeza tabaka kwamba kuna mtu anaweza kuingia na godoro lake na mwingine akashindwa. Kwa nini sasa na mahabusu nao wasishiriki katika shughuli za uzalishaji? Mahabusu na wafungwa wote ni binadamu, lakini hata akiitwa mfungwa, maana yake kesi yake imeshakuwa held, kwa maana ya kwamba imeshahukumiwa aende jela miaka mingapi? Kwa hiyo, yule tunayo sababu ya kumwambia sasa nenda kalime, nenda kazalishe kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya gereza. Sasa huyu mahabusu bado kesi yake haijahukumiwa kwa hiyo, yupo pale. Kusema tumchukue tukamfanyishe kazi, tukamlimishe bado kidogo busara hiyo hatujafikia. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali langu la nyongeza. Tunafahamu kabisa mradi wa STAMICO ni mradi ambao una maslahi kwa wananchi wa Kyela, Rungwe na Ileje. Ileje iko Mkoa wa Songwe. Ningependa kuona mradi huu unafanya kazi mapema sana.

Swali langu liko hapa, majengo yaliyojengwa eneo lile ni majengo mazuri ambayo ni kwa ajili ya ofisi na makazi ya watumishi. Makazi yale, siku hadi siku yameendelea kuharibika. Sasa natamani kujua, je, ni nini dhamira ya Serikali katika kuendeleza haya majengo yasiendelee kuharibika na kufanyika magofu huku wakati tukiendelea kusubiri huo mradi kufanya kazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge, kuhusu ukarabati wa majengo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema STAMICO imeanza ukarabati wa mgodi wa chini kama sehemu ya maandalizi na ili tuweze kuanza mgodi ni pamoja na maandalizi ya nyumba za staff. Kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mbunge tu kwamba jambo hili pia la ukarabati wa nyumba kama maandalizi ya mahali ambapo staff watakaoingia katika mgodi pia litakwenda kutekelezwa na tutawaagiza STAMICO kwamba wafanye mambo haya kwa pamoja ili pia tusiendelee kupata hasara ya nyumba ambazo hatimaye tunaweza tukahitaji kujenga nyumba mpya kumbe tungeweza kuzihifadhi hizi kwa ajili ya mkakati wa baadaye.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni sehemu mojawapo ambayo tunapata changamoto sana ya kuwa na idadi kubwa ya watoto waliotelekezwa na mara nyingi watoto hawa waliotelekezwa huwa wanakimbilia Ofisi ya Ustawi wa Jamii. Wanapofikiwa kule, Afisa wa Ustawi wa Jamii anapaswa kuwahudumia kwa huduma zote yule mtoto anazokuwa anahitaji mpaka atakapopata kituo cha kumpeleka. Lakini changamoto wanayoipata ni kwamba hawana fedha za kuwahudumia watoto hawa.

Je, ni lini Serikali itakuja na fungu maalum kwa ajili ya Maafisa wa Ustawi wa Jamii kuweza kuwahudumia watoto wao. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila; ni kweli, Serikali inatambua kwamba bado hatujawekeza vya kutosha kwenye eneo hilo kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii wetu waweze kufanya kazi hizi. Naomba niahidi kwamba tutafanya tathmini tuone ili kwenye kipindi kijacho cha bajeti tuweze kuanzisha namna gani ya kuwawezesha hawa Maafisa Ustawi wa Jamii. (Makofi)