Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Neema Gerald Mwandabila (14 total)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi na vifaa muhimu kwenye hospitali inayojengwa katika Mji wa Tunduma ili ianze kufanya kazi mapema?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza madaktari na wakunga pamoja na kuongeza bajeti katika Kituo cha Afya cha Tunduma ili kukidhi mahitaji ya kituo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa tangu Mheshimiwa Rais aliponipa dhamana ya kumsaidia kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nimuahidi kwamba nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Tunduma ambayo ilianza kujengwa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Ujenzi wa awamu ya kwanza unahusisha jengo la ghorofa moja lenye sehemu tisa za huduma mbalimbali za OPD ambalo limetumia shilingi bilioni nne ambalo hadi Machi, 2021 ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Baada ya kukamilisha ujenzi huo Serikali itapeleka watumishi na huduma za OPD zitaanza kutolewa. Serikali imeshawapanga madaktari wawili katika hospitali hii ambao kwa sasa wanaendelea kutoa huduma kwenye Kituo cha Afya Tunduma wakisubiri kukamilika kwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Tunduma kina jumla ya watumishi 74 kati ya watumishi 52 wanaohitajika katika ngazi ya kituo cha afya na hivyo kuwa na ziada ya watumishi 22. Idadi ya watumishi waliozidi inatokana na kituo hiki kutumika kama Hospitali ya Mji wa Tunduma. Hivyo, watumishi hawa watahamishiwa katika hospitali mpya ya mji mara itakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itaomba kuindhinishiwa shilingi milioni 409 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Tunduma ambalo ni ongezeko la shilingi milioni 84 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi milioni 325 iliyoidhinishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza:-

(a) Je, ni lini mahabusu wataruhusiwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali wakiwa Gerezani?

(b) Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwezesha Magereza kwa chakula kwa kuwa mkakati wa kila Gereza kujitegemea kwa chakula umeshindwa kutekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Songwe, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 78(1) cha Sheria ya Magereza, Sura 58 iliyorejewa Mwaka 2002, kimeeleza kuwa, pamoja na mahabusu kulazimika kufanya kazi za usafi kwenye bweni analoishi na usafi wa mwili wake, vyombo anavyotumia, nguo na samani anazotumia, pia anaweza kufanya kazi za uzalishaji kwa ridhaa yake. Kifungu hiki kinasomwa sambamba na Kanuni Na. 421 ya Kanuni za Kudumu za Magereza, Toleo la Nne la Mwaka 2003.

(b) Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango wa kujitosheleza kwa chakula Magerezani umeanza kwa magereza nane (8) ya Songwe, Kitai, Kitengule, Mollo, Pawaga, Arusha, Ushora na Ubena kwa lengo la kuzalisha kwa wingi na kusambaza chakula katika magereza mengine ambayo hayapo kwenye mpango. Uwezo wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa umeongezeka na kufikia 54% kwa mwaka 2020/2021 ikilinganishwa na 23% kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni sita kwa ajili ya kuongeza mashamba na kuimarisha miundombinu na zana za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuyafikia malengo ya kujitosheleza kwa chakula.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Vyuo Vikuu katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huanzisha Vyuo Vikuu na kutoa vibali kwa watu na taasisi binafsi kuanzisha Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa ya kusoma Elimu ya Juu. Vyuo Vikuu vilivyopo hupokea wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara, Visiwani pamoja na wanafunzi kutoka nje ya nchi. Huo ndiyo utamaduni wa Vyuo Vikuu duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Songwe kuna Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kilichopo katika Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe. Pia, kuna Kampasi ya Myunga ambayo ni Tawi la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) iliyopo katika Wilaya ya Momba. Hivyo, wananchi wanashauriwa kuendelea kuvitumia Vyuo hivyo na vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kuongeza nafasi za udahili na ubora wa Elimu ili kukidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Mahakama kutoa hukumu ya pande mbili hasa mtuhumiwa anaposhinda kesi kuepuka usumbufu kufungua kesi mpya ya kulipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni na taratibu za madai ya fidia, kuachiwa huru kwa mshtakiwa katika shitaka la jinai hakumpi haki ya moja kwa moja ya kulipwa fidia. Ili mshtakiwa aweze kulipwa fidia kutokana na kushinda shauri la jinai, ni lazima athibitishe Mahakamani kwamba mashitaka dhidi yake yalikuwa ya hila; na kwamba hakukuwa na sababu za msingi za kumshtaki. Kuachiwa pekee kwa mshtakiwa katika shitaka la jinai hakumaanishi mashtaka dhidi yake yalikuwa ya hila na waliomshitaki hawakuwa na sababu ya kuamini alitenda kosa.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 345(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaipa mamlaka Mahakama kutoa amri ya mtuhumiwa aliyeshinda shauri lake la jinai kulipwa gharama za shauri iwapo shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Kujitegemea (Private Prosecutor).
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanawake wanakuwa wachimbaji wa madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia STAMICO ina jukumu la kuwasadia wachimbaji wadogo wa madini wa makundi mbalimbali nchini wakiwemo wanawake. Aidha, STAMICO imeandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha wanawake pia wanakuwa wachimbaji madini nchini.

Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo inahusisha, pamoja na mambo mengine, kutoa mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake kupitia vituo vya mfano tulivyonavyo katika maeneo ya Katente (Bukombe), Lwamgasa (Geita) na Itumbi (Mbeya); kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi za mashapo kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambapo kwa sasa STAMICO imeagiza mitambo mitano ya uchorongaji maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini ili kuwasaidia kufanya utafiti.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni kuwaunganisha wachimbaji na taasisi za Kifedha zikiwemo Benki za CRDB, NMB na KCB kwa lengo la taasisi hizo kuweza kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wanawake. Ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mchepuko kwa kiwango cha lami kutoka Mpemba kupitia Chapwa Mwakakati katika Mji wa Tunduma kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mji wa Tunduma umekuwa ukikumbwa na msongamano mkubwa wa magari kuanzia Mpemba hadi Forodhani (Boarder) hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara ya ndani ya Tunduma na wanaokwenda uelekeo wa barabara ya Tunduma - Sumbawanga.

Mheshimiwa Spika, ili kupunguza adha hiyo, Serikali itatenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Sogea - Transformer yenye urefu wa kilometa 2.0 kwa kiwango cha lami ili iwe njia mbadala kwa watumiaji wa barabara za Mji wa Tunduma.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara ya mchepuko inayoanzia Mpemba – Chapwa - Makambini kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuondoa msongamano mkubwa wa magari. Ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanza kutoa Posho kwa Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kila Halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa kuwalipa posho, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, ni miradi mingapi ya kimkakati imejengwa katika Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ikiwemo ya uwekezaji wa madini, kilimo, biashara na uvuvi ambayo ina mchango mkubwa katika mapato ya Wilaya hiyo. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na:-

(i) Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira.

(ii) Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Bwelui wa megawati 4.7 wenye thamani ya shilingi 19,675,520,200.

(iii) Mradi wa Ujenzi wa Soko la Kimataifa la Isongoole.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ya Kimkakati kuilingana na fursa zinazopatikana nchini kwa lengo la kukuza uchumi, nakushukuru.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, ni lini Muswada wa Ukomo wa Upelelezi wa Kesi utaletwa ili kupunguza msongamano wa kesi unaotokana na upelelezi kutokamilika?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 225(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, ukomo wa upelelezi katika baadhi ya makosa ni siku 60 na kwa mujibu wa kifungu 225(5), Mahakama imepewa mamlaka kuifuta kesi ambayo upelelezi wake haujakamilika baada ya siku 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.1) ya 2022 kwa kuongeza kifungu cha 131A kilichoweka masharti kuwa isipokuwa kwa makosa mazito na makosa yote yanayosikilizwa na Mahakama Kuu watuhumiwa wasifikishwe Mahakamani hadi upelelezi uwe umekalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashataka imetoa Waraka Na. 1 wa mwaka 2022, kuhusu Ufunguaji wa Mashtaka na Ukamilishaji wa Upelelezi wa Kesi za jinai uliotolewa tarehe 30 Septemba, 2022 na ulishaanza kutumika tarehe Mosi Oktoba, 2022. Waraka huo unataka upelelezi wa kesi za mauaji, kesi za makosa mazito na kesi zote zinazosikilizwa na Mahakama Kuu ambazo hazihitaji utaalam kutoka taasisi nyingine usichukue zaidi ya siku sitini (60) na zile zinazohitaji utaalam kutoka taasisi nyingine upelelezi usichukue zaidi ya siku tisini (90).
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Ikana – Chitete pamoja na kujenga kwa kiwango cha lami barabara za milimani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.03 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ambapo miamba ilipasuliwa kwenye kipande chenye urefu wa kilometa mbili ambacho kilikuwa na mwinuko mkali uliokuwa unafanya magari yashindwe kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi milioni 460 kwa ajili ya kuweka tabaka la zege la mita 200, ujenzi wa mifereji na kuongeza upana wa barabara kwa kujaza kifusi kwenye eneo la kona kali.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, ni faida gani ambayo Wafanyakazi wanapata kupitia uwekezaji wa fedha wanazokatwa na Vyama vya Wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ambayo wafanyakazi wanapata kupitia uwekezaji wa fedha wanazokatwa na Vyama vya Wafanyakazi ni pamoja na; Vyama vya Wafanyakazi kusuluhisha migogoro ya kikazi kwa niaba ya wanachama wake, kutoa huduma kwa wanachama kama vile ya utetezi katika Mahakama ya Kazi, na kutoa elimu kuhusu Sera na Sheria za kazi kwa ajili ya maslahi mapana ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama vya Wafanyakazi kupitia fedha wanazokusanya kutokana na ada za wanachama wao huzitumia kutekeleza majukumu ya vyama yaliyowekwa kikatiba na kisheria yanayotokana na uwepo wa vyama mahali pa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo baadhi ya Vyama vya Wafanyakazi ambavyo hutumia ada za uanachama kujenga majengo kwa ajili ya matumizi ya ofisi za vyama, kuwapangisha watu mbalimbali na kutoa huduma kwa wanachama wao. Fedha inayopatikana kutokana na uwekezaji hutumika kuongeza bajeti za Vyama vya Wafanyakazi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na kisheria kikamilifu, ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati Shule za Msingi za zamani katika Wilaya za Ileje na Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule 2,147 shule za msingi kongwe nchini ambazo zilianzishwa kabla ya kupata Uhuru mwaka 1961. Hali ya miundombinu ya shule hizo ni mseto zikiwemo zenye hali nzuri na nyingine zenye miundombinu chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeanza kufanya tathmini ya hali ya miundombinu ya shule zote za msingi kupitia mradi wa BOOST ili kubaini mahitaji ya ujenzi wa miundombinu mipya ya shule na hali ya uchakavu wa miundombinu iliyopo. Tathmini hiyo imeanza mwezi Aprili, 2022 na itakamilika mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya tathmini hiyo yatatumika kuandaa mpango wa uendelezaji na ukarabati wa miundomibinu ya Shule za Msingi kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba na lini huduma za Mahakama za Mwanzo zitaanza kutolewa katika Tarafa ya Msangano?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA aliibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Momba ni moja ya Wilaya ambazo zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wa ujenzi wa Mahakama katika mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na majengo yake yenyewe na mazuri.

Mheshimiwa Spika, vilevile, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Tarafa ya Msangano umepangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2022/2023 ikiwa ni pamoja na kufanya maandalizi ya mahitaji kama watumishi ili huduma zitolewe mara baada ya ujenzi kukamilika.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, Serikali ina Mkakati gani wa kufanya utafiti maalum katika Mji wa Tunduma ili kubaini ni namna gani unaweza kuchangia kukuza uchumi wa nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango, hususan kifungu cha 6, pamoja na majukumu mengine, Tume ya Mipango ina jukumu la kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo Tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia hili, Tume ya Mipango imejipanga kufanya tafiti mbalimbali na kuratibu tafiti zitakazofanywa na taasisi nyingine za umma na binafsi kwa lengo la kubaini fursa za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, hivyo, Serikali, kupitia Tume ya Mipango, itafanya tafiti mbalimbali kubaini fursa za maendeleo katika miji ikiwemo Mji wa Tunduma kwa lengo kubaini ni jinsi gani mji huu na miji mingine nchini inaweza kuongeza kasi ya maendeleo na kuchangia kukuza uchumi wa nchi, ahsante.