Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Neema Gerald Mwandabila (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kipekee kuweza kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali kuingia mahali hapa, hakika nimeona ni kwa namna gani jinsi Bungeni kulivyo pazuri kiasi kwamba kweli ukiwa umeingia humu kutoka lazima utamani kutoa roho ya mtu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikishukuru Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu kipenzi kwa kuweza kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa haki, lakini pia kusimamia wanyonge wote wa nchi hii waweze pia kushiriki katika maamuzi ya kutunga sheria katika nchi hii. Niweze kushukuru familia, wadau, rafiki, jamaa, viongozi wa dini na marafiki zangu wote wana maombi wote walioweza kunisaidia kuweza kufika mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu nishukuru Wanasongwe, niwashukuru wanawake wa mkoa wa Songwe kwa kuweza kuwa wazalendo na kunipa nafasi ya kuweza kuingia mahali hapa, bila kura zao haikuwa rahisi, lakini waliweza kusimama imara na kunipa kura na leo niko ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza katika hotuba hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kipekee niseme hii ni hotuba ambayo imejaa matumaini mengi kwa Watanzania. Watanzania tunayo imani kubwa na Mheshimiwa Rais kulingana na namna ambavyo ameweza kufanya kazi kubwa ndani ya miaka mitano iliyopita, aliyofanya ni mengi kila mtanzania anajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika kipembele cha elimu ya ufundi, nikirejea vyuo vya VETA na DIT ambavyo viko katika Mkoa wangu wa Songwe. Serikali imeweka pesa nyingi sana katika hivi vyuo vya VETA na DIT, ni vizuri vinavutia na vina mazingira mazuri sana kwa watoto wetu kuweza kupata mafunzo ya ufundi pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo ni kwamba, hivi vyuo havitumiki ipasavyo, havitumiki kwa kiwango kinachostahili. Ukienda katika maeneo yale idadi ya wanafunzi waliopo katika vyuo ni wachache. Kama Serikali imeweka pesa basi tutafute namna ambayo itakuwa nyepesi kwa vyuo hivi kuweza kupata wanafunzi na mchango wangu kwa Serikali, ningependa kushauri mambo yafuatayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kungekuwa na direct enrolment ambayo wale wanafunzi ambao wanakuwa hawajapata nafasi ya kuingia Sekondari, wapewe nafasi, wachaguliwe kama wanavyochaguliwa wale walioenda sekondari, waweze kupangiwa vyuo vya ufundi. Hii itasaidia wale wazazi wa wale watoto waone kama watoto wao nao pia wamepata opportunity na wakawajibika kuwapeleka watoto katika hivyo vyuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe kwa halmashauri kwa sababu tayari tunayo 10% ambayo tunatoa kama mkopo, tungetumia pesa hii kuweza kusababisha mafunzo kwa vile vikundi ambavyo vimekuwa vimeanzishwa. Kumekuwa na changamoto ya utoaji wa pesa nyingi kwa vikundi lakini wanavikundi wanashindwa kubuni miradi yenye tija, wanaishia kubuni pikipiki, wanaishia kubuni bajaji, lakini pia wanaishia kubuni kubuni miradi ya ufugaji kuku, kitu ambacho kinasababisha washindwe kufanya marejesho mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea na kumalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Mpango huu wa Mwaka Mmoja, lakini pia wa Miaka Mitano inayokuja. Kipekee kabisa nikupongeze kwa namna unavyoendesha Bunge hili, kikao hiki. Hakika unatutendea haki kama Wabunge na tunafurahia uendeshaji wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu dakika tano ni chache, lakini namuomba Mungu aniongoze ili niweze kuongea vyema kwenye suala la TANESCO, suala la nishati kwa ujumla, lakini pia, suala la TRA. Hakuna changamoto kubwa ninayoipata katika Mkoa wangu wa Songwe kama kusikia umeme umekatika, umeme hauna nguvu, umeme hautoshi, hakika wanavyokuwa wanaelezea wananchi kule huwa inasikitisha sana. Unakuta mwananchi ana ofisi, ofisi yake inategemea umeme. Analipa pango, analipa gharama nyingine zote, lakini mwisho wa siku anachokipata anakuta ni kichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika kusema hayo nasema gharama za uendeshaji wa umeme katika nchi yetu bado ni za juu. Ukiangalia kwa upande wa TANESCO, ni base katika suala la domestic electricity, gharama inayolipwa kwa kila watt below 75 ni shilingi 100. Gharama inayoenda kulipwa above 75 kilowatts ni 350, hapa sijazungumzia suala la industrial electricity. Tunapoongelea ushindani wa soko na Mheshimiwa wetu Rais amejitanabahisha kuwa sera yake kubwa ni kuifanya nchi ya Tanzania iwe nchi ya viwanda na tunajua viwanda haviwezi kuendelea pasipokuwa na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwa namna gharama hizi za umeme zinavyokuwa na nikiangalia soko la bidhaa zetu tunakotaka kuzipeleka, unakuta wakati mwingine tunawapa wakati mgumu wajasiriamali wetu na wawekezaji kwenye ushindani wa soko katika mataifa mengine. Nitarejea katika mfano mdogo tu wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kwetu sisi Tunduma hatuna shida sana na sukari kwa sababu, tuko mpakani tunatumia sukari ya Zambia. Wakati mwingine nawaza kwamba, inakuwaje nchi ndogo kama Zambia inatushinda sisi Tanzania kwenye uwekezaji wa sukari mpaka inaanza inafanya supply kwetu katika kanda zetu za mpakani kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari Zambia inauzwa Sh.2,000 ukija huku kwetu sukari inaenda hadi Sh.3,000. Sasa unapoongelea shilingi 3,000 na sidhani kama kuna Mtanzania yeyote humu ndani asiyependa kitu cha bei rahisi, hata kama tunasema ni uzalendo hauwezi ukaenda kwa style hiyo kwamba, nafanya uzalendo huku naumia. Kwa hiyo, niombe, niiombe kwanza Bodi ya Sukari itafute namna ya kuifanya biashara ya sukari kama fursa ya kuipatia Serikali pesa. Kama watawekeza vizuri na kama pia watu wa nishati watatuonea huruma kupunguza ghrama za uendeshaji wa viwanda naamini nchi yetu inakoenda itakuwa ni nchi ambayo ina mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Zambia nchi ambayo ni ndogo walipe umeme kwa gharama za shilingi 77 kwa domestic, lakini pia kwa business wanalipa shilingi
108.99 wakati hapa Tanzania domestic tu ni shilingi 100 na tena ni shilingi 350 yani kwa wale ambao wanatumia above 75 kilowatts. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie na itathmini vizuri kwenye suala la nishati ili viwanda vyetu viweze kukua, lakini pia iweze kufanya tathmini vizuri kwa kutafuta mazao ambayo yataweza kupunguza adha kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nirudi kwenye suala la TRA ambalo pia yamekuwa ni malalamiko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba niishie hapo. (Makofi)