Supplementary Questions from Hon. Minza Simon Mjika (15 total)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu tuna machine ya X-Ray tuliletewa toka mwaka 2002. Swali langu ni hili, katika hospitali hiyo hatuna mtaalam wa X-Ray:-
Je, ni lini Serikali italeta mtaalam wa X-Ray katika Wilaya hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu wana mashine ya X-Ray ambayo kwa kipindi kirefu imekosa mtumishi kwa maana ya mtalaam wa X-Ray. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeendelea kuwasiliana kwa karibu na Wizara ya Afya, lakini pia na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuona namna gani tunapata watumishi hawa ili tuweze kupata mtumishi mmoja na kumhamishia katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu. Wataalam hawa bado ni wachache lakini jitihada za Serikali ni kuendelea kuwasomesha ili tuweze kupata wataalam wengi ili waendane na kasi ya ujenzi wa vituo vya afya ambavyo kimsingi vitahitaji kupata watalaam hawa wa X-Ray.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshalifanyia kazi na tulishaainisha mtumishi kwa ajili ya kumpeleka Meatu na wakati wowote atakwenda kuanza kutoa huduma ya X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru sana.
Kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Meatu sasa napenda niulize kwamba ni lini sasa zoezi hili litaanza kwa sababu yapata wiki mbili hivi sasa hatujapata maji katika Wilaya ya Meatu na kuna vijiji ambavyo vinaukame sana kwa mfano Bukale, Mwambegwa na Chambara ni vijiji vingi sana hatuna maji kabisa leo yapata wiki mbili wakazi wa kule tunahangaika, tunapata taabu. Serikali ituambie sasa ni lini itatuletea maji huko kwetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama jibu langu la msingi nilivyosema mwezi Agosti, 2021 mradi huu unakwenda kuanzwa na suala hili ni jana tu jopo kamili la wizara liliweza kukaa na hawa wenzetu wa KfW na Mheshimiwa Waziri aliwahitaji watoe commitment yao namna ya kuweza kutekeleza mradi huu kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge nafahamu namna ambavyo unafuatilia suala hili ninakupongeza sana. Nikutoe hofu nitaongozana na wewe tutaenda kuhakikisha kwamba kila namna ambavyo ilikuwa imepangwa inakwenda kutekelezwa kwa wakati.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru sana kwa majibu ya Waziri, lakini sasa napenda nijue ni lini zoezi hili litaanza la ujenzi wa hiyo barabara? Naomba kupatiwa majibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimeainisha kwamba tayari tumeshaanza ujenzi kwenye baadhi ya maeneo na katika bajeti tutakayoanza kuitekeleza ambayo Bunge lako limepitisha, tumetenga fedha, kwa hiyo, mara tu bajeti itakapoanza kutumika barabara hiyo itaanza kujengwa, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina penda kushukuru sana kwa majibu mazuri ya Waziri. Lakini nina maswali mawili tu ya nyongeza. Katika Mkoa wa Simiyu kuna Wilaya tano lakini Wilaya ya Meatu ndio ina ukame sana kuliko Wilaya zote hizo tano. Nilipenda kujua ni lini sasa Serikali itachimba visima virefu vya maji na kusambaza katika vijiji hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana pamoja nami twende naye katika Wilaya ya Meatu aone wakina mama wanavyopata adha ya maji katika Wilaya ya Meatu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende kupokea pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Lakini vile vile nipende kumpongeza na yeye, kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ushirikiano mkubwa ndani ya Wizara ya Maji. Amekuwa mfuatiliaji mzuri sana akisaidiana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kaka yangu Simon wanafanya kazi nzuri kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 ni kuchimba visima virefu katika Wilaya ya Meatu. Tunatambua namna gani wakinamama wanapata shida ya maji katika Mji ule. Hivyo, tumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ameliona hili na ameshatupatia fedha tutaenda sasa kifua mbele kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuambatana kwangu ni kawaida. Hivyo, niseme Mheshimiwa Minza usiwe na wasiwasi baada ya Bunge hili, baada ya kumaliza ratiba ya Mikoa niliyoipanga nitakuja kwako Simiyu hususani Meatu. Lengo ni kuona hali halisi na kuongeza chachu na ufanisi wa miradi yetu ya maji. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, napenda kushukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu yenye matumaini. Lakini nina swali moja tu la nyongeza.
Je, ni lini Serikali sasa itajenga chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Busega? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Minza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, kwamba ujenzi wa vyuo hivi unalingana sawa au unaendana sawa na upatikanaji wa bajeti na upatikanaji wa fedha. Lakini naomba nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu, hatuishii tu kwenye ujenzi wa vyuo hivi tunakwenda mbali zaidi kwa sababu tukishajenga ni lazima tuweze kuangania namna gani ya upatikanaji wa vifaa lakini vile vile upatikanaji wa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali imejikita katika umaliziaji wa vyuo hivi 25 na baadae sasa tutakwenda kwenye mkakati wa kuweka bajeti kwa ajili ya kufikia Wilaya hii ya Meatu, Busega na Wilaya nyingine nchini zilizobaki kwa sababu Wilaya bado ziko nyingi, nakushukuru sana.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Ninapenda kutaka kujua jibu la uhakika leo, ni lini barabara ya kutoka Kolandoto-Kishapu-Lalagwa hadi Meatu itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza la Mheshimiwa Minza, Mbunge wa Viti Maalum Simiyu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tumetenga fedha kuanza ujenzi wa Kolandoto hadi Lalago, bababara hii ambayo ni barabara kuu na tutaanza kwa kilometa 10 kwa sababu fedha tumetenga katika bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali langu ni moja tu la nyogeza. Je, ni lini malipo hayo yataanza kwa sababu yamechukua muda mrefu sana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maombi tayari tumeshayapata na Serikali imeanza kuyahakiki na kabla ya kuisha mwaka huu wa fedha 2022 wananchi hawa watakuwa tayari wameshalipwa.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Napenda kuuliza swali moja.
Ni lini barabara ya kutoka Kolandoto mpaka Meatu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kolandoto kwenda Meatu ni kati ya barabara ambazo zimeainishwa kwenye Ilani, na pia zipo kwenye mpango wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kuanzia na kilometa 92. Kwa hiyo, sasa hivi kinachosubiriwa ni Serikali kupata fedha ili ujenzi wa barabara hii uanze. Ahsante. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuishukuru Serikali kwamba katika Mkoa wa Simiyu tuna madarasa mengi sana, lakini kuna upungufu wa Ofisi za Walimu. Walimu wetu hawafanyi kazi kwa furaha kwa sababu hawana ofisi wengi wanakaa kwenye miti. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa Ofisi za Walimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tumeziagiza halmashauri kujenga ofisi kwa kila halmashauri kutenga mapato yao ya ndani kwa sababu moja ya jukumu letu sasa ni kujenga madarasa, mabweni, mabwalo ya chakula ambayo ndio kazi kubwa tunayoifanya sasa ikiwemo na majengo ya utawala kwa baadhi ya shule. Kwa hiyo kwa kadri tutakavyokuwa tunatafuta fedha tutakuwa tunapeleka, lakini tumeziagiza halmashauri kutumia mapato yao ya ndani kufanya hivyo. Kwa hiyo tunafanya hivyo kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa yote nchini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kuuliza, katika Wilaya ya Meatu tuna shida sana ya maji. Kwa Mkoa mzima wa Simiyu Wilaya ya Meatu inaongoza: Je, ni lini Serikali italeta maji safi na salama katika Wilaya Meatu ili wananchi wa kule wanufaike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu una bahati sana. Una mradi mkubwa ambao unaenda kutekelezwa kwa kutumia kigezo cha mabadiliko ya tabia ya nchi. Mradi ule utafikisha maji maeneo ya Meatu, Maswa na maeneo yote yaliyo karibu kuhakikisha wananchi wanapelekewa maji safi na salama. Nafahamu Mheshimiwa Minza nawe pia umefuatilia sana suala hili, na nilifika Meatu na tunaendelea na kazi. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kuuliza swali.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Simiyu tuna Wilaya Tatu ambazo zina upungufu wa watumishi wa afya. Wilaya ya Meatu, Bariadi na Maswa.
Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika Halmashauri hizi za Mkoa wa Simiyu kuna upungufu wa watumishi kama ilivyo kwenye Halmashauri nyingine zote hapa nchini, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi kwa awamu na ndiyo maana ajira 7,612 zimetangazwa na Halmashauri hizi pia zitapewa kipaumbele katika kuwapelekea watumishi hao. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mhesimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, naomba niulize swali la nyongeza, je, ni lini Serikali itaongeza watumishi wa afya katika Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba Halmashauri ya Meatu ina upungufu wa watumishi na itapewa kipaumbele kwenye ajira hizi ambazo zimekwishatangazwa.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Katika Mkoa wa Simiyu tuna Wilaya Tano, lakini Wilaya ya Meatu inaongoza kwa ukame wa maji.
Je, ni lini sasa tutapata maji ya kutoka Ziwa Victoria maana juzi tu Naibu Waziri amefika pale tumepata maji lakini maji yenyewe yameshakuwa ni ya mgao mtatusaidiaje katika Wilaya ya Meatu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Meatu ni kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, niliweza kufika mimi mwenyewe na ninakushukuru sana Mheshimiwa Minza kwa ushirikiano wako kwa namna ambavyo tumeweza kupunguza ile changamoto ya maji machafu na sasa hivi angalau mnapata maji kwa zamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria tayari unaendelea kufanyiwa kazi, kama unavyofahamu tayari watu wameshaanza kulipwa fidia zao na ule ni mradi maalum kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo tutarajie mwaka huu ujao wa fedha shughuli zote zitakwenda kufanyika vizuri.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itakarabati majengo ya Kituo cha Polisi Maswa ili yaweze kuendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kutoka Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Maswa kweli ni cha siku nyingi na kimechakaa. Maelekezo yetu kwa IGP na wasaidizi wake kule mikoani wafanye tathmini ya kiwango cha uchakavu na kubaini gharama zinazohitajika ni kiasi gani ili kiweze kupangiwa matengenezo kadiri tutakavyopata fedha.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kumshukuru sana Waziri kwa majibu yake mazuri. Nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Busega na Wilaya Itirima tuna hospitali nzuri sana za wilaya, tatizo ni moja majengo ni mazuri na yanapenda hatuna watumishi wa kutosha. Kwa hiyo hospitali zile hazina hadhi ya kuitwa hospitali ya wilaya kwa sababu watumishi hawatoshi;
Je ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha ili na wananchi wa kule wafaidike?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge jinsi anavyofuatilia masuala ya afya kwenye mkoa wake kwa kushirikiana na Wabunge wa majimbo. Kama ambavyo nimesema kwamba kwa mwaka huu tunategemea kupata watumishi takribani 12,000 hivi. Tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kupeleka watumishi maeneo hayo ili wananchi waweze kupata huduma kulingana na ukubwa wa hospitali yenyewe.