Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala (46 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii fursa ya kutoa mchango wangu. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Nkenge kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kunirejesha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia, kupongeza hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais alipozindua Bunge hili. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa taarifa aliyowasilisha leo hii hapa Bungeni ambayo imezingatia pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais katika ukurasa wa 16, alibainisha kwamba matarajio yake ifikapo mwaka 2020 angalau viwanda viweze kutoa ajira 40% ya ajira zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa sasa na taarifa za Mheshimiwa Waziri alizowasilisha, inaonesha kwamba kwa mwaka 2014 viwanda vimetoa ajira kwa asilimia 3.1. Sasa lengo letu ni kuhakikisha sasa viwanda vitoe ajira ifikapo mwaka 2020 kwa 40%. Sasa kutoka asilimia 3.1 kwenda 40% kuna kazi kubwa ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa leo, nitabainisha masuala muhimu ambayo yakizingatiwa tutaweza kufikia 40% ya ajira kutolewa na viwanda. Jambo la kwanza, ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amebainisha kwamba, kwa vyovyote vile itakavyowezekana lazima tutekeleze utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo au wanasema flat projects.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepitia ile orodha ya ile miradi, nikagundua kuna mradi mkubwa umesahaulika kwa bahati mbaya na mradi wenyewe ni ujenzi wa Kajunguti International Airport. Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye kampeni, jambo mojawapo aliloahidi wana Misenyi, alisema akiingia Ikulu, fedha zote atakazozikuta atazileta Misenyi kulipa fidia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Kajunguti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwakumbusha wasaidizi wake, wahakikishe katika Mipango ijayo, wahakikishe wanazingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, lakini pia Kajunguti International Airport ni muhimu siyo tu kwa Misenyi, lakini pia kwa Taifa. Tunazungumza kuanzisha masoko ya kimkakati kwa sababu uwanja huo wa Kajunguti, siyo tu tutajenga uwanja wa Kimataifa lakini utaendana na ujenzi wa viwanda, utaendana na kuendeleza maeneo maalum (Special Economic Zones), utaendana na kuweza kuzalisha bidhaa mbalimbali zilizo karibu na Soko la Afrika Mashariki ukizingatia ukweli kwamba tunapakana na Rwanda, Burundi na Uganda, lakini pia tunaweza kuuza maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia, tunaposema kwamba tunahitaji kuwa na uchumi wa viwanda, hatuwezi kusahau kilimo. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyowasilisha leo hii hapa, nimesoma yote, lakini sioni maneno ya kilimo kwanza yakijitokeza, nikafikiri labda tumeanza kusahau sahau kilimo kwanza. Nitoe ushauri, kilimo kwanza ni jambo la muhimu, hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda bila kuwa na kilimo kinachozalisha kwa ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimesoma hotuba hii, mara tatu, mara nne, sikuona maneno Big Results Now yakijitokeza. Nikaanza kufikiri kwamba labda sasa Big Results Now siyo msisitizo tena, lakini nikumbushe kwamba Big Results Now ni muhimu, zile sekta sita ni muhimu, zisipozingatiwa kwenye mipango yetu tutafika sehemu tuisahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwamba unapozungumza kwamba unataka uwe na uchumi wa viwanda lakini unapenda vilevile kuhakikisha una kilimo kinachozalisha kwa ziada, lazima tuhakikishe migogoro ya wafugaji na wakulima inakoma. Jimboni kwangu kuna mgogoro mkubwa wa Kakunyu. Mgogoro huu umechukua zaidi ya miaka 15. Sasa kuwa na mgogoro ambao haumaliziki. Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alishatoa maelekezo mgogoro huu uishe na Mheshimiwa Magufuli ametoa maelekezo mgogoro huu uishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi pia washirikiane kuhakikisha wanamaliza mgogoro huu kabla sijaanza kuchukua hatua nyingine ambazo nitaona zinafaa kama mwakilishi wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niseme naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba muhimu iliyowasilishwa leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kutekeleza kwa ufundi na ustadi mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, yako mambo mengi ya kuthibitisha hilo, mambo mawili yanathibitisha jinsi Ilani inavyotekelezwa vizuri, Serikali imeweza kuongeza mapato kutoka bilioni 870 Novemba, 2015 hadi trilioni 1.3 kwa mwezi ilipofika Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imeweza kuanza kutekeleza mkakati wa elimu bure hata kabla ya bajeti mpya ya 2016/17 haijawekwa, hiyo imewezekana tu kwa kubana matumizi, kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, yakaelekezwa kwenye utekelezaji wa elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa tunalojifunza baada ya kuanza kutekeleza elimu bure ni kwamba ukiangalia shule ya awali pamoja na darasa la kwanza uandikishaji wa wanafunzi wameongezeka zaidi ya asilimia 100. Kwa maneno mengine, wako Watanzania wengi walioshindwa kuanza shule ya awali, walioshindwa kuanza darasa la kwanza, kwa sababu ya gharama zisizokuwa na tija ambazo wazazi walikuwa wanalazimishwa kwamba lazima zilipwe hivyo kuna watoto walioshindwa kuendelea na shule, sasa baada ya kuanza kutekeleza elimu bure tunaona vijana wakiongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wako wengi tuliowapoteza. Ni matarajio yangu katika Wizara inayohusika itakuja na mpango wa kuonesha ni jinsi gani wale tuliowapoteza Watanzania wengi tu ni kwa jinsi gani tutaweza kuwapa elimu ya msingi kwa sababu wao tayari wameshaikosa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa ziara aliyoifanya katika Jimbo langu la Nkenge, na pia kuweza kutembelea Wilaya ya Misenyi, kwa kweli niseme amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza kutembelea kata ya Kakunyu katika Wilaya ya Misenyi, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika ziara ile alitoa maelekeza mbalimbali ambayo yatasaidia kumaliza mgogoro kati ya wakulima, wafugaji wazawa, na wawekezaji mbalimbali waliopewa blocks katika Ranchi ya Misenyi. Matarajio yangu ni kwamba maelekezo hayo yataweza kutusaidia kuondoa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 na ningependa kuchukua nafasi hii kushauri baadhi ya mambo yakizingatiwa yatatusaidia kumaliza mgogoro huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo lazima lizingatiwe ni dhana na maneno ya watu ambao wamekuwa wakisema vijiji vilivyo ndani ya Kata Kakunyu, Kilimilile, Nsunga na Mtukula viliingilia maeneo ya Ranchi za Mabale pamoja na Misenyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi vilikuwepo kabla ya Ranchi mbili za Mabale na Misenyi hazijaanzishwa. Kwa hiyo, wale wanaosema vijiji viliingilia maeneo ya ranchi kuanzia leo naomba waseme kwamba ni Ranchi za Mabale na Misenyi zilizoingilia maeneo ya vijiji kwa sababu vijiji vilikuwepo na vilishasajiliwa na vinatambulika Kiserikali na vina hati. Kwa kuwa vijiji ndivyo vilitangulia kuwepo kabla ya ranchi ni makosa na dharau kwa wananchi wa Misenyi kusema wameingilia ranchi wakati wao walikuwepo hata kabla ya ranchi haijakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nashauri lizingatiwe Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea kule na kutoa maelekezo, tunatarajia kwamba Mawaziri watayafanyia kazi na bado wanaendelea kuyafanyia kazi. Kabla hawajamaliza kuyafanyia kazi, wananchi wameshaanza kubugudhiwa, tarehe 17 mwezi uliopita na tarehe 18 mwezi huu, baadhi ya wananchi wamenyang’anywa majembe ili wasiendelee na kilimo. Kufanya hivyo ni kuchelewesha kutekeleza sera ya Hapa Kazi tu! pia ni kutoheshimu maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lazima lizingatiwe ili tupate ufumbuzi wa kudumu ni lazima Waziri wa Mifugo ashirikiane na Waziri wa Ardhi, ashirikiane na Waziri wa Ulinzi na Waziri wa TAMISEMI; nina uhakika hawa wote wakishirikiana kwa pamoja na siyo kila mmoja anakwenda kwa wakati wake na kufanya yanayomhusu eneo lake, tutaweza kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme na nisisitize kwamba kuna umuhimu ukiangalia mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ambao tunalenga kuutekeleza unabainisha kwamba tunahitaji trilioni 107 kuweza kuutekeleza, na kati ya hizo Serikali itatoa trilioni 59 na zilizobaki zitatolewa na private sector, hivyo, ukiangalia Mpango wa Pili tunaopanga kuutekeleza, sehemu kubwa ya fedha zitatokana na private sector. Sasa ili private sector waweze kufanya kazi lazima tuongeze nguvu za kujenga mazingira wezeshi kama ambavyo imebainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira wezeshi ni muhimu kwa sababu ndiyo yatawezesha private sector kuweza kuchangia vizuri katika utekelezaji wa Mpango wetu. Nitaeleza mambo matatu muhimu kama mfano wa mambo muhimu ambayo yakifanywa na ambayo hayahitaji fedha za kigeni kuyafanya, lakini ukiyafanya unaweza kusaidia kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa mfano, hivi sasa hapa Tanzania viwanda vinavyozalisha simenti vikitaka kuuza simenti yake ndani ya Afrika Mashariki vinalazimika kutafuta kibali kutoka kwa Mkemia Mkuu kabla hawajauza, lazima watoe asilimia 2.5 ya thamani ya simenti wanayouza. Ukifanya hivyo unakwamisha viwanda bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapotumia sukari na wengine wa Kanda ya Ziwa na Watanzania wengine kila kilo ya sukari inakatwa kodi ya reli. Sasa mtu unajiuliza, kuna uhusiano gani kati ya sukari na kodi ya reli? Utaratibu huu unaongeza gharama ambazo hazina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaambiwa waliopo kwenye kilimo cha alizeti kama wataanzishiwa utaratibu wa kupata mbegu mpya wataweza kuongeza ajira kutoka milioni moja ya Watanzania wanaopata ajira hivi sasa hadi Watanzania milioni kumi, lakini ili kupata mbegu mpya waliopo kwenye sekta ya alizeti kwa Tanzania unahitaji miaka saba ili kuweza kupata kibali cha kupata hiyo mbegu mpya, wakati Uganda wanahitaji miezi sita tu ya kuweza kupata hiyo mbegu mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba naunga mkono hoja na naomba nimalizie kwa kusisitiza kwamba ili tuweze kujenga Tanzania yenye viwanda, lazima tuhakikishe tunaunga mkono zoezi la Export Processing Zones na tutafanya hivyo kwa kutenga maeneo na kuhakikisha maeneo ya wawekezaji yanapatikana siyo ya kutafutwa. Vilevile kule Nkenge kuna mpango mkubwa wa kujenga uwanja wa Kimataifa wa Mkajunguti natarajia kwenye bajeti hii zitatengwa fedha za kulipa fidia kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kupitia Wizara ya Viwanda tunataka kuanzisha Export Processing Zone ya Kimataifa ili uwanja wa kimataifa wa Mkajunguti usiwe uwanja tu usiyokuwa na cha kusafirisha, vilevile tuwe na Export Processing Zone. Tukifanya hayo tunaweza kupiga hatua na kwenda kwa kasi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tuondoe utitiri wa ukiritimba katika kuratibu masuala mbalimbali. Kwa mfano, mwekezaji yeyote akitaka kuwekeza Tanzania lazima kabla hajaanza kufanya hivyo aende TBS kutafuta kibali, lazima aende TFDA kutafuta kibali cha kitu kile kile, akitoka huko lazima aende kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Sasa ukiangalia yote haya yanaongeza ukiritimba usio kuwa wa lazima na kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyosema Tanzania ni ya 139 sasa ili tuweze kuboresha mazingira ya wawekezaji, lazima hatua za makusudi zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono haja. Katika ukurasa wa 63 hadi 64 wa hotuba ya Waziri imeandikwa ifuatavyo:-
“Katika mwaka 2015/2016 Wizara imesambaza na kutoa elimu kwa wadau kuhusu Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 na Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo wa mwaka 2011. Jumla ya nakala 300 za Sera ya Taifa ya Mifugo na nakala 200 za Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo zimesambazwa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakala hizi ni kidogo ukizingatia umuhimu wa sekta ya mifugo. Nashauri nakala nyingi zaidi zichapwe na kusambazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu akifuatana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alitembelea Kata ya Kakunyu-Missenyi na kutoa maelekezo ya jinsi ya kumaliza mgogoro wa wafugaji wa Kakunyu na wawekezaji waliopewa blocks za kufuga katika Ranchi ya Missenyi. Nitashukuru Mheshimiwa Waziri akibainisha alivyotekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mgogoro wa Kakunyu umedumu muda mrefu. Wakati umefika tupate ufumbuzi wa kudumu. Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu itakuwa vyema kuzingatia yafuatayo:-
(i) Vijiji vyote vilivyo ndani Kata ya Kakunyu, Nsunga, Mutukula, Kilimilile na Mabale vilishasajiliwa, vina hati na vinatambulika kisheria;
(ii) Vijiji husika vilikuwepo hata kabla ya Ranchi ya Missenyi na Mabale kuanzishwa;
(iii) Mipaka ya asili kati ya Ranchi ya Missenyi na vijiji inatambulika ni vizuri izingatiwe; na
(iv) Mahitaji ya ardhi ya sasa na vizazi vijavyo lazima yazingatiwe kama alivyoelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua kwa haraka ili tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Nashauri pia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ashirikiane kwa karibu na wa TAMISEMI, Ulinzi na Ardhi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo ni muhimu sana katika maendeleo ya Chuo Kikuu chochote. Kwa muda mrefu Chuo Kikuu Mzumbe kinaendeshwa na kusimamiwa na Kaimu Makamu Mkuu (Acting Vice Chancellor), ninaomba Wizara iharakishe na ikamilishe taratibu za kupata Vice Chancellor wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba wa walimu wa awali kwa walimu wa awali ambao wamehitimu katika vyuo mbalimbali na wamekuwa wakijitolea kufundisha kwa muda mrefu ingekuwa vizuri waajiriwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya China ilibainishwa nia yake ya kushirikiana na Serikali yetu kujenga chuo cha Veta Mkoa wa Kagera. Naomba Wizara iongeze msukumo ili chuo cha VETA – Kagera kianze kujengwa. Eneo la kujega chuo hicho lipo na Balozi wa China Tanzania alishatembelea eneo hilo. Ninaomba pia Mheshimiwa Waziri akipata nafasi atembelee eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu wengi ambao wanapandishwa madaraja lakini mishahara yao haibadilishwi, naomba Wizara ijitahidi kuhakikisha walimu wote wanalipwa stahili zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utaratibu wa kufundisha unaitwa Montessori utaratibu huu ni mzuri na una manufaa mengi ukilinganisha na utaratibu wa kawaida tunaotumia. Aidha, hapa Tanzania kuna vyuo vinavyofundisha kwa kutumia mfumo huu. Ninaomba walimu waliofundishwa kutumia mfumo wa Montessori waajiriwe na Seikali. Aidha, kwa kuanzia, madarasa ya awali yanaanza kutumia mfumo wa Montessori kufundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti nilikuwa nimejipanga kwa ajili ya dakika kumi lakini nitajitahidi nitumie muda mfupi kadri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 22 Februari, 2016 wananchi wa maeneo ya Omukajunguti ambao walielekezwa wasiendelee na shughuli za maendeleo katika eneo hilo na tathmini ikafanyika kwa ajili ya kulipwa fidia kwa ajili ya uwanja wa Kimataifa wa Omukajunguti; na tarehe 22 Februari, 2016 wakapokea barua kutoka Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano iliyowekwa sahihi na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ndugu G. Migire kwamba fedha hizo zitatengwa katika bajeti hii. Sasa wananchi wakaniomba wakisema ukienda huko unga mkono bajeti ya Wizara ili tuweze kupata fedha yetu ya fidia. Lakini nimepitia kitabu hiki na vitabu vingine, sioni fedha hizo za kulipa fidia. Kwa hiyo nachelea kuunga mkono bajeti hewa inapokuja kwenye suala la kulipa fidia watu wa Omukajunguti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nataomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kunipa maelezo nielewe vizuri ili nitakapokuwa naunga mkono bajeti yake nikikutana na mpiga kura wangu akaniuliza niwe na majibu sahihi ya kumueleza kwanini niliunga mkono bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningependa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, tunayo ahadi thabiti ya Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni alituahidi akiingia Ikulu fedha zote atakazozikuta atazichukua azilete Omukajunguti kwa ajili ya kulipa fidia. Mheshimiwa Rais akishazungumza, Mheshimiwa Waziri natarajia asaidie katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. Vigezo vingine vyote vinathibitisha ule uwanja ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Kagera, kwa ajili ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo la pili kwa harakaharaka tunayo ahadi ya kilometa tatu za lami kwa ajili ya Mji wa Bunazi, nimeangalia kwenye kitabu hiki sizioni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa 40 za barabara kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Katoma hadi Kashenye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukiangalia hesabu kwa haraka haraka, barabara hii imekuwa ikijengwa kwa kiwango cha lami kwa mita 500 kila mwaka. Kwa mwendo huu itachukua miaka 80 ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo. Sasa miaka 80 kujenga kilometa 40, huo sio mwendo wa hapa kazi tu, ni mwendo wa konokono ambao nakuomba Mheshimiwa Waziri unisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu dakika zenyewe ni chache tuna ahadi inayotoka kwa Makamu wa Rais juu ya barabara ya lami kutoka Kaja hadi Mugana, Hospitali Teule ya Wilaya. Naomba Mheshimiwa Waziri akiwa anjibu atusaidie kufafanua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumza kwa sababu ya muda, naona figisufigisu katika ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria. Ahadi ilikuwa kujenga meli nne, mbili Ziwa Tanganyika, moja Ziwa Victoria na nyingine kule Ziwa Nyasa. Lakini ukisoma kitabu hiki, ahadi hiyo sasa taratibu inabadilika sasa tunaona fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 20 za kuanza kujenga meli katika Ziwa Victoria, sioni lini tutaanza kujenga kule Ziwa Tanganyika wala Ziwa Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukisoma kitabu hiki kwa haraka haraka kama una akili ya kufikiria kidogo unapata mashaka, kwa sababu inaonekana zimetengwa shilingi bilioni 20 za kujenga meli mpya katika Ziwa Victoria, lakini hatuelezwi, meli hiyo mpya itagharimu Shilingi ngapi. Lakini katika kitabu hiki hiki tunaambiwa itakarabatiwa MV Victoria kwa shilingi bilioni 20. Sasa kama shilingi bilioni 20 zinatumika tu kukarabati inakuwaje tena unatenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kujenga meli mpya? Mimi nadhani kama ni kweli shilingi bilioni 20 ndizo zinazotakiwa kwa ajili ya ukarabati basi zingetengwa fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kujenga meli mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri anafahamu Serikali ilitoa shilingi bilioni 600 kwa ajili ya ukarabati MV Victoria lakini fedha hizo hazikufanya kazi iliyokusudiwa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri alichukua hatua. Lakini napenda niseme kama siku chache zilizopita, shilingi bilioni 1.3 zilikuwa zinatosheleza kukarabatia MV Victoria, imekuwaje leo sasa inabadilika si shilingi bilioni 1.3 tena ni shilingi bilioni 20 zinazohitaji kufanya ukarabati. Ndiyo maana nakuwa na wasiwasi, ningependa Mheshimiwa Waziri, anieleze kwamba katika maamuzi haya hakuna figisufigisu bali kweli tunataka kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kuji-adress kwa yale tunayokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiit, kwa sababu ya muda naomba niishie hapo. Nachelea kuunga mkono hoja mpaka hapo nitakapokuwa nimepewa maelezo yatakayoniwezesha mimi kurudi kwa wananchi na kuwaeleza kwa nini nimeunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza Sekta ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jumuiya ya Ulaya inatekeleza sera ya malighafi (mkakati wa malighafi) kwa lengo la kukabiliana na upungufu wa madini muhimu kwa maendeleo ya nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo wa malighafi wa jumuiya kuna madini zaidi ya 26 ambayo Jumuiya ya Ulaya imeyawekea mkakati wa kuyatafuta na kuyapata kwa gharama yoyote, mahali popote yalipo. Nashauri Wizara itambue uwepo wa mkakati huo na ijipange vizuri kuwezesha Tanzania kunufaika na madini yaliyo katika kundi hilo la madini muhimu kwa kuzingatia mtazamo wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo wa Jumuiya ya Ulaya wa malighafi raw material strategy. Jumuiya ya Ulaya inaelekeza nia yake kusaidia Mataifa mbalimbali katika jitihada zake za kutafiti upatikanaji na madini mbalimbali na kuweka kumbukumbu za uwepo madini hayo hasa madini muhimu. Nashauri Serikali ijipange vizuri kunufaika na mpango huo wa Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tunajipanga kuwa nchi ya viwanda pamoja na jitihada nzuri zinazofanyika kusambaza umeme vijijini kuna changamoto ya umeme unaosambazwa maeneno mbalimbali kuwa wa low voltage. Nashauri jitihada ziongezwe za kuwekeza miundombinu ya kuongeza nguvu za umeme na hivyo kuondokana na tatizo la umeme wa low voltage. Kwa kufanya hivyo, itasaidia sana kupatikana umeme wa uhakika utakaosaidia mapinduzi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kielelezo namba nne katika ukurasa wa 83, kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini hadi Aprili, 2016 ni asilimia 1.9 iliyoendelezwa. Iinaonekana kama nchi tuna kazi kubwa ya kufanya hasa kuendeleza kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji na kuwahimiza kuendeleza visima vya gesi ambayo imeshagundulika. Kama nchi lazima tujiulize kwa nini inachukua muda mrefu kuendeleza visima vya gesi asilia na tunatakiwa kufanya nini kuendeleza kwa haraka visima vya gesi asilia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa hoja muhimu iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya kuisimamia sekta hii muhimu na kwa maana hiyo, sitamung’unya maneno, ninaunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 84 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna jedwali linaloonesha marejesho ya asilimia 30 kwa Halmashauri. Nimefuatilia pale nikagundua katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Misenyi hatujarejeshewa fedha. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wake watusaidie kwa sababu tulishawasilisha maombi yetu ya kurejeshewa asilimia 30 kama tunavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kusema kwamba katika kitabu cha utekelezaji wa miradi ya Wizara ya Ardhi pamoja na Shirika la Nyumba katika ukurasa wa 25 wamebainisha pale kwamba Mutukula Commercial Complex Center ule mradi umeshakamilika kama walivyoonyesha kwenye kitabu, lakini mimi kwa macho yangu hivi karibuni nilitembelea lile jengo, kwa kweli halijakamilka. Niliwauliza wenzangu baada ya kuona hapa leo hii kwamba imekamilika, lakini Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misenyi amenihakikishia akasema bado. Kwa hiyo, nadhani limekamilika tu kwenye vitabu, lakini kwa hali halisi, bado. Nawaomba wahusika walifanyie kazi ili jengo hilo likamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kupongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pale Mutukula wamenunua eneo na wamepima viwanja 22. Ni jambo jema kwamba sasa Mutukula itapendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakaribishe waungane nami na waungane na Wanamisenyi katika jitihada za kujenga mji wa kisasa wa Bunazi unaofanana na miji ya Ulaya. Mji huu tumejipanga kuujenga na niwakaribishe Shirika la Nyumba washirikiane na sisi. Mpango wetu tulionao, tutaanzia Mutukula, tutajenga Bunazi, tutaenda Kyaka na kwa kweli utaratibu tunaotaka kutumia, siyo kutoa ramani za kujenga nyumba tu, tutakupa kiwanja lakini pia tutakupa na ramani ya nyumba ya namna gani uijenge sehemu ipi. Tunataka tujenge mji wa kisasa unaofanana fanana na miji ya Ulaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawakaribisha Shirika la Nyumba waungane nami katika kutekeleza lengo hilo na kwa kweli Mheshimiwa Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, naomba nimwahidi kwamba ndani ya miaka mitano ijayo Mji wa Bunazi utafunika Mji wa Bukoba, siyo kwa nia mbaya ni kwa sababu ya masuala ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto ya upungufu wa wataalam wa ardhi, namwomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wake, watusaidie kutupa wataalam wa ardhi pale Halmashauri ya Misenyi ili tunapopanga mipango yetu, iweze kutekelezwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa tisa wa kitabu cha orodha ya migogoro alichotoa Mheshimiwa Waziri, naomba tu niongeze katika vijiji vilivyotajwa mle ni vijiji vya Kakunyu na Bugango pamoja na Byeju, lakini kijiji cha Nkerenge sijakiona pale, naomba kiongezwe. Pia katika Kata ya Mabale, hii ni Kata mpya, kuna mgogoro pia kati ya ranchi ya Mabale na vijiji vya Kenyana na Kibeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada ambazo amezifanya kumaliza mgogoro wa Kakunyu. Namuomba pia Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na yeye afuatilie kwa karibu mgogoro huu umalizike; na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Lukuvi utendaji wako mzuri unaouonyesha umechangiwa na kupata bahati ya kuwa DC wa Bukoba wakati fulani. Sasa Wanamisenyi tunatambua unaifahamu vizuri Misenyi, utusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mgogoro huu uweze kumalizika, jambo muhimu ni kuwa watu wote wanaohusika wafanye kazi kwa uadilifu kwa sababu bila kutanguliza uadilifu mbele, hakuna kitakachopatikana. Ipo migogoro mingine kwa mfano Hifadhi ya Msitu wa Miziro kuna mgogoro kati ya hifadhi na vijiji; vile vile katika Kata ya Buyango, Kijiji cha Kikono kuna mgogoro kati ya kijiji pamoja na Msitu wa Miziro na Kata ya Bugandika kuna mgogoro katika Kitongoji cha Ishozi na hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nianze kwa kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi walivyowasilisha vema bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017 ukurasa wa tisa mpaka wa kumi inabainisha kwamba kuna mikoa mitano ambayo inaongoza kwa umaskini. Nimesikia wenzangu walivyosema, sina sababu ya kukataa jinsi hiyo mikoa ilivyobainishwa kwa sababu nitaingia kwenye ubishi wa kiuchumi na wachumi siku zote huwa hawana jibu moja, kwa hiyo kwa sasa hilo naliacha. Nakubaliana na jinsi Mheshimiwa Waziri alivyowasilisha mikoa mitano lakini hoja yangu ni kwamba baada ya kuwa nimeiona hiyo mikoa mitano nikisoma kitabu cha bajeti sioni sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hiyo mikoa mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri baada ya kuibainisha basi bajeti hii ingekuja na mikakati maalum ya kusaidia hiyo mikoa mitano. Kwa kuwa sijaona, nitajaribu kubainisha baadhi ya maeneo ambayo tukitumia hoja hiyo hiyo kwamba tunayo mikoa mitano maskini sana, mambo yapi tusifanye ili kuendelea kuifanya hiyo mikoa kuwa maskini zaidi. Najua yapo mambo mengine ambayo yanaweza yakafanywa lakini nijikite kwenye bajeti yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, katika ahadi tulizotoa kwa wananchi, maana ukiangalia mikoa hii baadhi yake inalima kahawa na wengine wanalima pamba, lakini kahawa kwa mfano tuna aina ya kodi 26 ambazo tulibainisha kwamba kodi hizi zitapunguzwa au kufutwa kabisa. Bajeti hii mapendekezo pekee ya kodi inayopendekezwa kufutwa ni ada ya kukaanga kahawa kwa ajili ya kuuza soko la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile ada inayofutwa ni moja kati ya 26 zilizopendekezwa kupunguzwa au kufutwa. Kwa hesabu ya haraka haraka maana yake ni kwamba, hapo Mheshimiwa Waziri atakuwa ametekeleza asilimia tatu ya kile tulichoahidi. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba zile kodi 25 zilizobaki ingekuwa vizuri na zenyewe zikafutwa na zifutwe sasa katika bajeti hii kwa sababu hivyo ndivyo tulivyoahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia haraka haraka, je, wenzetu waliotuzunguka ndani ya Afrika Mashariki wanafanya nini? Uganda wao wana kodi ya asilimia moja tu katika zao la kahawa na ndiyo maana utakuta Watanzania wengi wanapenda kahawa yao wauze kupitia Uganda kwa sababu kule kuna unafuu wa kodi lakini sisi tuna kodi 26. Ukiangalia kwa nini tusifute kodi hizo hupati sababu. Vietnam kwa mfano wao wana asilimia moja tu kwenye zao la kahawa ambayo inakuwa charged kwenye point of exit, Uganda wana asilimia moja, sasa sioni sababu kwa nini na sisi tusifanye hivyo na tufanye hivyo katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wa uchumi wanatuambia mkulima wa Tanzania hasa wa kahawa yeye anatozwa wastani wa asilimia 70 ya fedha yote inakwenda kwenye kodi, lakini kwa Tanzania corporate tax ni asilimia 30 na akiwa amepata hasara halipi kodi hiyo, lakini kwetu sisi mkulima asilimia 70. Huyu mkulima apate faida, apate hasara, asilimia 70 ipo palepale. Kwa hiyo, nadhani hilo eneo tunaweza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia hii ada ya kukaanga kahawa inayopendekezwa kufutwa inamnufaisha nani? Ada hiyo inayanufaisha makampuni makubwa yanayofanya biashara ya kuuza kahawa nje na siyo wakulima wadogo wadogo. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kulitazama hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tulipopitisha sheria hapa ya kuruhusu haya makampuni makubwa kuingia kwenye ushindani wa kununua kahawa, tulitoa angalizo na sheria iko wazi kwamba hawa tuliowaruhusu kununua kahawa kushindana na Vyama vya Ushirika, wasishindane na Vyama vya Ushirika kwenye grass roots. Tuliwaambia wakitaka kununua kwenye grass root, basi kule Moshi wasiende kushindana, wasifanye mambo mawili. Huwezi ukawa unanunua kwa mkulima, halafu unakwenda Moshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotokea hadi sasa ninavyozungumza, wanunuaji hawa wakubwa, kina OLAM na wengine wananunua kwenye grass roots, wakienda mnadani wanakwenda kununua kahawa yao tu waliyonunua, kwa hiyo unaua ushindani na inaleta tatizo kubwa kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuizungumza haraka haraka, maana tuna mikoa mitano ambayo tunaambiwa ni maskini sana na sina ubishi lakini tufanye nini sasa. Kuna ugonjwa wa mnyauko fizari. Huu ugonjwa wa mnyauko fizari umeleta janga la kitaifa kwa sababu kwa muda mrefu Mikoa ya Kigoma, Kagera na mingineyo tumekuwa tukijitosheleza kwa chakula lakini baada ya huu mnyauko fizari kuanza hatuwezi kujitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nafikiri kutaja tu mikoa hii inaongoza kwa umaskini haitoshi, ningefurahia kama Mheshimiwa Waziri angetangaza kwamba kuna janga la kitaifa la kupoteza migomba, kwa hiyo tunakuja na mkakati maalum. Tunajua wataalam wetu wa kilimo wamejitahidi kutafuta ufumbuzi, ufumbuzi peke yake waliopata ni kufyeka, kwamba migomba ikipatwa na ugonjwa wa mnyauko fizari dawa ni kufyeka tu, kwa hiyo wanatembea na mapanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani dawa si kufyeka tu, hata kama ni kufyeka Mheshimiwa Waziri anaweza akaja na physical, bajeti inaweza ikasema tutakuja na panga la kufyeka lakini wakati huo huo tuna milioni moja, tunasema tukifyeka hapa kwa sababu umekumbwa na ugonjwa wa mnyauko fizari tunakupa fedha ya kukuwezesha kuishi kwa miezi sita, miezi saba, mwaka mmoja mpaka hapo utakapoanza kuvuna. Watakuita wenyewe wakulima kwamba njoo ufyeke hapa, lakini kama unatembea na panga tu na kama akili yetu inaishia kwenye kutembea na panga tu na kufyeka, basi tujue tutazidi kuongeza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi kuna Benki ya Maendeleo ya Wakulima. Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo yenyewe inasema kahawa si zao la food security. Napenda nitoe hoja hapa kwamba kahawa ni zao la food security kwa sababu mkulima akiweza kuvuna vizuri atauza atapata chakula. Kwa hiyo, ni uwezo mdogo wa kufikiri kusema kwamba zao la kahawa halihusiani na food security, si kweli. Kwa sababu ukishasema hivyo maana yake Vyama vya Ushirika vinalazimika kuendelea kukopa kutoka CRDB asilimia 18 ili viende kununua kahawa na vinakwenda kushindana na wanunuzi wengine wanaokopa nje kwa asilimia tatu na kuendelea, huwezi kushindana namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa harakaraka naomba nimtahadharishe Mheshimiwa Waziri, anafahamu kwamba alipokutana na wenzake katika Afrika Mashariki wamekubaliana kwa Kenya, vile viwanda vinavyozalisha ngozi na mambo mengine, wanapozalisha wa-offload kwenye soko la Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapo-offload bila kulipa italeta madhara makubwa kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, natarajia Mheshimiwa Waziri atanipa ufafanuzi akiwa anajibu hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami ningeungana na wenzangu kuzungumza kama walivyozungumza. Hata hivyo, kwa kuwa tetemeko lililoanzia jimboni kwangu bado linatetemesha na bado linamtetemesha na Mbunge mwenyewe kwa hiyo naomba nijikite kwenye tetemeko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu tarehe 10/9/2016 saa tisa na dakika 27 mchana katika eneo lililo kilometa 27 Kaskazini Mashariki mwa Nsunga kulitokea tetemeko kubwa la ardhi. Eneo hilo si pengine bali ni Wilaya ya Misenyi katika Kata ya Minziro, Kitongoji cha Murungu B. Tetemeko hilo lilileta madhara makubwa na madhara hayo yameelezwa na Waheshimiwa mbalimbali waliochangia katika Bunge hili na viongozi mbalimbali walitembelea eneo hilo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda niseme machache kwamba katika Mpango wa maendeleo tunaoupanga niungane na wale ambao wameshauri ingekuwa vizuri basi katika mpango huo tujipange pia jinsi ya kukabiliana na madhara hayo. Kwa mfano, katika Kitongoji cha Murungu pale tetemeko la ardhi lilipoanzia karibu nyumba zote zilienda chini. Kwa hiyo, matarajio ya wananchi makubwa waliyonayo ni kwamba, Serikali itaweka utaratibu mzuri na kuchukua hatua za kibajeti za kuwawezesha kuweza kujenga nyumba zao upya. Sasa linaweza kufanyika vipi, Waziri wa Fedha anafahamu Serikali inaweza ikatumia mbinu mbalimbali lakini hayo ndiyo matarajio ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya tetemeko la ardhi kutokea lazima tujifunze. Jambo la kwanza ambalo ni muhimu tujifunze, tujipange kwa changamoto kama hizo zitakazotokea baadaye. Kwa sababu kubwa lililojitokeza ni kwamba tulikuwa hatujajipanga vizuri kwa sababu hakuna aliyejua kwamba tunaweza kupata tetemeko la ardhi, sasa limejitokea ni vizuri tujipange kwa siku zijazo likitokea tuwe tumejipanga vizuri. Inapochukua zaidi ya wiki tatu kufanya tathmini ya tetemeko la ardhi inakuwa ni majanga ndani ya majanga. Kwa sababu hata yule ambaye angependa kukusaidia haji kukusaidia kwa sababu wewe mwenyewe hujui tatizo lililokukuta ni lipi na hujui unatakiwa kufanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tetemeko la ardhi kutokea ilitolewa taarifa kwamba utaratibu wa kukusanya michango utaratibiwa, ni jambo jema. Pia utaratibu wa kutoa matamko baada ya kutokea tetemeko la ardhi na wenyewe unahitaji kuratibiwa kwa sababu kila mtu anapokuwa anasema analofikiri linaenda kwa wananchi walewale, tunapeleka taarifa za kuchanganya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi mmoja mzito baada ya tetemeko kutokea alisema kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi watawezeshwa kupata vifaa kama cement pamoja na mabati ili waweze kujenga, wakafurahia. Baadaye likatoka tamko lingine zito kwamba hakuna atakayetoa
vifaa vya ujenzi bali wenye uwezo waanze kujenga na wananchi wakaanza kutuuliza Mheshimiwa Mbunge mnasema wenye uwezo tuanze na je, wasiokuwa na uwezo mnawafanyaje, sikuwa na majibu kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na mtaalam mmoja kiongozi akatoa kauli akasema tetemeko hili ni kubwa, tunafanya uchunguzi wa miamba, kwa hiyo msianze kujenga msubiri mpaka tukishajua miamba imekaaje huko chini ya ardhi. Mpaka leo nazungumza taarifa ya miamba ikoje chini ya ardhi haijatoka. Nayasema mambo haya kwa sababu tusipojipanga vizuri mbele ya safari yatatuletea matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hata jinsi tulivyokuwa tukijitahidi kusaidia wananchi, nilienda kwa mfano upande wa Minziro kule nikakuta wananchi wengi walikuwa wanasaidiwa na wataalam wetu wa maafa kwa kupewa kitu kinaitwa sheeting. Wanasema nimefika pale nimekuta watu hawana nyumba, wataalam wanaeleza, tumetoa sheeting, sheeting ni turubai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye kutembeatembea nikakuta maeneo mengine wana tents zimetengenezwa vizuri, nikawauliza nyie hizi mmetoa wapi? Wakasema jirani zetu hapa ambao ni ndugu zetu wametutolea hapa wanatusaidia kujenga na kila tent linajengwa kwa Sh. 70,000 na linakuwa limejengwa vizuri. Nikagundua kwamba wataalam wa maafa wa Tanzania wao wanachojua inapotokea maafa ni kugawa sheeting tu lakini hawachukui hatua kuangalia kidogo kwa wenzao wanafanya nini inapotokea matatizo kama yale. Si lengo langu kumlaumu mtu yeyote, lakini ni vizuri kujifunza ili siku zijazo tusirudie katika matatizo yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia humu kwenye kitabu cha mapendekezo ya Mipango tunafikiri kwamba hali ya hewa itakuwa nzuri Afrika Mashariki lakini ukweli hali ya hewa si nzuri hata huko Kagera kwenyewe ninakozungumzia, kila mahali unapopita agenda kubwa ni ukame, kule Karagwe ni ukame, Misenye ni ukame na kila sehemu ni ukame. Kwa hiyo, matarajio yetu katika Mpango huu basi changamoto hizi za ukame zizingatiwe ili tuone tunaweza kufanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango yote mingi tuliyonayo katika kitabu hiki yako mambo mengi, wengi wetu huwa tunazungumzia fedha lakini tunalo tatizo lingine. Miradi mingi haitelezeki si kwa sababu ya fedha kutokuwepo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha alielewe hili, wakati mwingine fedha za kutosha zinakuwepo, lakini uwezo mdogo wa wale wataalam wetu tuliowapa majukumu kushindwa kusimamia hii miradi ni tatizo kubwa kuliko hata tatizo la ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili nitatumia mifano miwili, kwa mfano tunao mpango wa SEDP unaeleweka Wizara husika ilitoa zaidi ya shilingi milioni 790 za kuweza kujenga nyumba za Walimu katika shule za Sekondari za Kashenye, Bwanja, Nsunga na Kakunyu. Wakandarasi wamefanya kazi yao vizuri, shilingi milioni 709 zilishatolewa, lakini juzijuzi nilikuwa kwenye ziara nimefuatilia kwenye Halmashauri yangu wakandarasi waliojenga nyumba katika sekondari nilizotaja wamelipwa tu shilingi milioni 600 zaidi ya shilingi milioni 200 hazijulikani ziko wapi, viongozi wote hawajui lakini kazi imefanyika, sasa hilo ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna tatizo la mradi wa maji katika Wilaya yangu. Kwa mfano, tuna miradi ya maji mikubwa, kule Ruzinga tuna mradi mmoja wa maji wa shilingi milioni 567, Rukurungo, Igurugati shilingi milioni 400, Bugango, Kenyana, Kakunyu ni mabilioni ya fedha lakini miradi yote hii ukiitembelea unachokiona ni mabomba ambayo yanatoa hewa badala ya kutoa maji. Mabilioni ya fedha yametumika lakini hakuna maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkutano mmoja wa hadhara mtaalam mmoja akaniambia Mheshimiwa tumepata maji mpaka mabomba yamepasuka. Nikamwambia hongera nitakuja unioneshe mabomba yalivyopasuka. Nikamuuliza mabomba mliyotumia yakapasuka yako wapi? Akasema Mheshimiwa ni haya hapa. Nikamwambia bomba hili haliwezi kupasuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkutano tukachimba pale nikakuta bomba lililo ndani ya ardhi siyo kama lile alilonionyesha kwamba walitumia. Nikamwambia mbona bomba ni tofauti, akasema Mheshimiwa unajua sikuelewa swali ulilouliza. Kwa hiyo, umefanyaje? Akasema tumetumia mabomba yaleyale ya zamani yaliyokuwepo. Kwa maneno mengine wale wana Ruzinga hadi leo hawajapata maji na zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimetumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Waziri wa Fedha na kwa Serikali ni kwamba, tatizo siyo fedha tu, tatizo pia ni kuwa na wataalam ambao uwezo wao ni mdogo. Lazima jambo hili tuliangalie, Serikali itupe wataalam wenye uwezo, kama hawajaenda shule sawasawa wapelekwe shuleni, hata kama ni kuazima popote pale tuazime tunachotaka ni utekelezaji wa yale mambo tuliyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nilijibiwa hapa kwamba siku za karibuni kule Kajunguti International Airport wananchi wataanza kulipwa fidia na niliambiwa hapa kwamba kabla ya mwezi Oktoba watakuwa wamelipwa. Naomba nieleze masikitiko yangu kwamba hadi leo hii hakuna aliyelipwa hata shilingi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuzingatia kuwa ninazo dakika tano tu nitaongelea hoja mbili. Naomba nibainishe kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati, sote kwa pamoja tuna nia ya kujenga Tanzania ya viwanda; lakini kwa masikitiko makubwa baadhi ya wawekezaji tunaowakabidhi viwanda hivi ili watusaidie kuviboresha kwa kuleta teknolojia za kisasa, wao badala ya kufikiria kujenga Tanzania ya viwanda wanafikiria kujenga Tanzania ya ma-godown. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni kiwanda chetu cha nguo cha Urafiki. Tulipotemebelea sehemu ile tulishangazwa na tulishtuka kuona Mkurugenzi Mkuu hajui mission kwa nini wapo pale na hajui vision kwa nini wapo pale, jambo hili lilitusikitisha sana. Lakini baadaye tukabaini kwamba wakati fulani zilitolewa fedha kwa ajili ya kununua mitambo, fedha zilitumia lakini hakuna mtambo hata mmoja ulioletwa, kwa hiyo ulinunuliwa mtambo hewa. Wakati Serikali inahangaika na watumishi hewa wakati umefika pia kubaini mitambo hewa inayonunuliwa, badala ya kuendesha kiwanda, inanunuliwa mitambo hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tulibaini kuna mpango wa makusudi wa kuhakikisha spare ambazo zinatakiwa kutumika kwenye kile kiwanda hazinunuliwi na wala haziagizwi, mashine inapoharibika inabidi sasa ing‟olewe kwa sababu hakuna spare, huo ni mkakati wa kubadilisha kile kiwanda kuwa godown. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukabaini kwamba pamoja na kung‟oa ile mitambo pale kuna menejimenti mbili; kuna menejimenti inayoongozwa na wazawa na kuna menejimenti inayoongozwa na wawekezaji. Wawekezaji wanajua ya kwao na wazawa wenzetu wanajua ya kwao. Kwa hiyo, ni menejimenti mbili katika kiwanda kimoja, matokeo yake hakuna kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ambayo ningependa niimalizie na nyingine niziache, tumeona tatizo la kutotenga fedha za kulipa fidia, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage anajitahidi kuhangaika lakini kwa mfano pale Omkajunguti tunataka kuweka Export Processing Zone, zinatakiwa fedha za kulipa fidia, lakini hadi sasa tumeendelea kuzungumza tu hakuna fedha iliyotolewa. Labda tu nimshauri waziri muhusika kwa kuwa alishaniaidi kulipa fidia hizo, alisema ifikapo mwezi wa kumi atakuwa amelipa na sasa hajalipa, ikifika wakati wa bajeti tusigombane, nitafuata taratibu za Kibunge zinazotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia hii fursa ya kuwa mchangiaji katika hoja muhimu iliyo mbele yetu. Naomba niseme awali kabisa kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukurasa wa 26 kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; huduma za kiuchumi; amebainisha kwamba Serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha mfumo unganishi; mfumo wa kuweka kumbukumbu za ardhi, mfumo funganishi wa kuhifadhi
kumbukumbu za ardhi na tayari wameshaanza kujenga.
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni zuri na nitaomba liharakishwe na liweze kukamilika kwa wakati kwa sababu litatusaidia sana katika kuondoa migogoro ya mara kwa mara ya ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa ukiangalia inachangiwa na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuweka kumbukumbu za ardhi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nyote mnafahamu kuna mgogoro mkubwa kule Misenye uliochukua muda mrefu, lakini ukiuangalia ule mgogoro kwa nini umechukua muda mrefu, sababu kubwa ni kutokuwepo kwa mfumo wa kuweka kumbukumbu za ardhi; na hasa kutokuwa na kumbukumbu
za kielektroniki. Nitaeleza hoja tano kwa nini nasema kutokuwa na mfumo huu kumechangia sana kuleta migogoro ambayo ingeweza kuepukika?
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ramani inayotumiwa na NARCO kwa mfano, ramani inayotumiwa na NARCO na iliyotumika katika kugawa blocks kule Misenyi. Ramani hiyo kwanza inatumika kwa siri kubwa, lakini ramani yenyewe ukiwauliza NARCO wenyewe kwamba iko wapi hawawezi kukupa ramani ambayo inatumika; kila mtu anatumia ramani yake kulingana na anavyoona inafaa.
Mheshimiwa Spika, siku moja nilisikitika sana nilipoelezwa na mtaalam mmoja kwamba ramani waliyonayo iliyoanzisha Misenyi Ranch, mpaka ukishavuka Mto Kagera kwenda mpaka Uganda yote ni Misenyi Ranch. Sasa maana yake, mwenye ramani ile na anayetumia ramani
ile anakuwa hatambui na anapuuza ukweli kwamba katika eneo hilo kuna Vijiji, Kata na watu wanaishi. Pia ukiangalia hata blocks zenyewe zilizotengwa katika Misenye Ranch, migogoro iliyopo kati ya blocks na vijiji inasahau ukweli kwamba vijiji vilikuwepo kabla Ranch haijaanzishwa. Kwa hiyo, hii imekuwa ikileta mgogoro.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nasema tukiwa na kumbukumbu za vijiji, maana vijiji vinapimwa, vinakuwa na hati, ziwe kwenye mfumo mmoja ili mtu asitoe hati juu ya hati. Maana kwa kufanya hivyo, matokeo yake inakuwa ni kuleta vurugu.
Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia ni kwamba mipaka ya blocks zile zilizotengwa inabadilishwa kila kukicha na tuliowapa hizi blocks wana mamlaka siku hizi wanabadilisha blocks kadiri wanavyoona inafaa. Akiamka asubuhi anaanza kutembea anaweka mipaka na leo kwa mfano nimeletewa taarifa zaidi ya kaya 3,000, sasa ni displaced persons ni watu ambao wapo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
lakini hawana sehemu ya kuishi, wameondolewa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ambayo inatokana na kutokuwepo na mfumo wa kuweka kumbukumbu, sote tunafahamu kwamba vijiji katika Misenye Ranch vilikuwepo kabla ya ranch na mipaka inajulikana kwamba ni Mto Kyaka, Kuru na Kigoroga lakini historia hii imepotoshwa, hakuna anayejua historia hii na kumbukumbu hazipo.
Mheshimiwa Spika, tuna tatizo lingine kubwa ambalo sote tunalijua ni kati ya misitu. Kwa mfano kule Minziro ukiangalia migogoro inayojitokeza kule Kata ya Minziro ni mipaka kati ya Minziro kama Kata na Vijiji vilivyo ndani ya Kata ile na Msitu wa Minziro.
Mheshimiwa Spika, sasa nasema ndiyo maana nimefurahia sana huu utaratibu wa kuanzisha mfumo unganishi wa kuweka kumbukumbu za kieletroniki ukianzishwa na taarifa zinaonesha unaanza itatusaidia sana. Hilo ni jambo la kwanza, ndiyo maana nimesema naunga mkono hoja hii kwa sababu inakuja na utaratibu ambao unaweza kutusaidia.
Mheshimiwa Spika, pia migogoro mingi ya ardhi tuliyonayo; iliundwa tume hapa ya kusaidia kutafuta ufumbuzi hadidu za rejea na akasema jambo moja kubwa kwamba tuwe na subira. Akatuomba viongozi tuwe na subira, tusubiri hiyo tume imalize kazi yake.
Mheshimiwa Spika, matarajio yangu tume hiyo ikimaliza kazi yake Wabunge watapewa fursa ya kupokea ripoti hiyo na kushirikishwa kama tulivyoahidiwa; lakini subira hii naona Mheshimiwa Waziri Mkuu iko kwa wanasiasa tu, lakini kwa viongozi wengine kule Kagera, wao hawana
subira yoyote. Hawasubiri cha tume, wala nini, wanaendelea kila mtu anafanya anavyoona anataka.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninapozungumza imetolewa ultimatum ya miezi minne watu wote kuondoka na kwenda kule watakapoona inafaa; jambo ambalo mimi kama mwakilishi wao silikubali, kwa sababu limetolewa kabla hata Tume yenyewe iliyoundwa kufuatilia suala hili
haijatoa taarifa yake.
Mheshimiwa Spika, ni vizuri wakati wanasiasa tunaombwa kuwa na subira, basi hawa Waheshimiwa wengine nao niombe pia na wao wawe na subira. Subira ikiombwa kwa upande mmoja tu, hiyo siyo subira; sote ni viongozi lengo letu ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi waliniomba kule wakasema Mheshimiwa inaonekana sasa ng’ombe wanapendwa kuliko watu, nikawaambia hapana watu kwanza, ng’ombe baadaye. Wakaniomba wakasema Mheshimiwa sasa uturuhusu tushike fimbo tuweze kupambana; nikasema hapana, siwezi kuwaruhusu kwa sasa kwa sababu tuliombwa tuwe na subira. Kama ukifika wakati huo, basi mimi nitakuwa wa kwanza kuongoza mapambano hayo lakini kwa sasa tuwe na subira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kuongoza Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua kama alivyoeleza kaka yangu Mheshimiwa Lwakatare, tetemeko lililotukumba Mkoa wa Kagera, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri alipofika pale Jimboni kwangu Misenyi kuna eneo moja linaitwa Kabyaile akakuta zahanati imeenda chini yote kwa sababu ya tetemeko, akanipigia simu akaniuliza Mheshimiwa Kamala hapa zahanati yako imekwenda bado unahitaji zahanati au unahitaji kituo cha afya. Nikamwambia Mheshimiwa mimi ni nani kuombwa na Waziri nipewe kituo cha afya nikaendelea kung’ang’ania jambo dogo! Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu kituo cha afya hicho kimejengwa na kinafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ziko changamoto zinaendelea, lakini nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri wa Nishati na Madini kwa kuhakikisha umeme unafika pale kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais, umeme umefika pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais alituahidi kutupa access road ya lami ya kwenda pale Kabyaire na lami hiyo sasa itajengwa kwenda pale Kabyaire ili wagonjwa waweze kufika pale bila matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kuwa tunayo na ahadi ya Makamu wa Rais ya kuhakikisha tunapata barabara nzuri ya kwenda Mgana basi tuunganishe hii access road ya Kabyaire na access road ya kwenda Hospitali Teule ya Mgana ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Pia nichukue nafasi hii kushukuru kwa kweli kwa mambo yote hayo ambayo yamefanyika ndani ya kipindi kifupi na wenzetu wa Bukoba Vijijini walipoona Kabyaire sasa inapata kituo cha afya na wao wakatuomba wakasema tunaomba nasi tupate huduma kutoka kwenye kituo hicho na hatuna sababu ya kuwabagua wenzetu, niombe basi Serikali ifanye utaratibu iunganishe barabaa ya Kabyaire pamoja na ile inayokwenda Bukoba Vijijini kwa kaka yangu Mheshimiwa Rweikiza ili wananchi wote waweze kupata huduma safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa siyo mkweli kama nitamaliza kuzungumza hapa bila kueleza ukweli kwamba Hospitali Teule ya Mgana (DDH) pamoja na taarifa nzuri zilizopo ya fedha tunazooneshwa kwamba tumepokea kwa ajili ya kutoa huduma, lakini ukweli pale huduma ya mama na mtoto hakuna, hakuna huduma ya bure kama inavyotarajiwa itolewe, hili limekuwa tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Baraza la Madiwani walikuwa na kikao na wakazungumza, Mwenyekiti wa Halmashauri akaniambia wanakaa na mimi nikamwambia nilishamueleza Mwenyekiti wangu wa Halmashauri wakiona jambo lolote wakae na wakiona hawaoni siendi wajue bado naamini wanafanya kazi.

Kwa hiyo, wamekaa na wamezungumza walipomaliza akanipigia akasema Mheshimiwa mambo hayaendi, nikasema sasa kama mambo hayaendi, basi kabla mimi mwenyewe sijaja nitamuomba kwanza Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa sababu leo atawasilisha hoja yake basi nitamuomba atusaidie na yeye kuja hapo Mgana aweze kuangalia na kujifunza nini kimetokea, Hospitali ya Mgana ambayo ilikuwa inatoa huduma nzuri kwa watoto sasa haitoi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumuomba Mheshimiwa Waziri aungane nami tuende tutembelee hiyo hospitali ya Mgana tuweze kuondoa hii pandora’s box inayojitokeza ya maajabu ambayo yameanza kujitokeza ya hospitali kushindwa kutoa huduma….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu. Hoja ya kwanza niliyonayo leo ni kuhusu Wakala wa Huduma za Misitu. Wakala huyu anajitahidi kufanya kazi yake na kwa kweli tatizo kubwa linalojitokeza ni kwamba kwa muda mrefu alikuwa likizo lakini baada ya kuhimizwa na baada ya Wakala huyu kwenye mipango yake kuona kwamba ni muhimu sasa waanze kuweka mipaka ya kuonyesha eneo lao lakini kubwa linalojitokeza hapa ni mabadiliko ya tabianchi, lazima sote tukubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilayani Misenyi kwa muda mrefu sana hali ya hewa ilikuwa nzuri. Hakuna mtu aliyefikiria kuna sababu ya kwenda kulima kwenye maeneo ya matingatinga, hata hawa wenzetu wa huduma za misitu hawakuona umuhimu wa kubainisha mipaka kwa sababu kila mtu alikuwa na eneo la kutosha, kwa hiyo kulikuwa hakuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na mahitaji ya maeneo kuongezeka, sasa kila mmoja anajitahidi kuweka mipaka yake. Watu wa hifadhi wanajitahidi kubainisha mipaka ya maeneo yao kuonesha wanaanzia wapi na wanaishia wapi lakini na wananchi pia wangependa wawe na maeneo ya kutosha ya kuchungia mifugo yao. Wananchi wanafuata maelekezo ya viongozi ambapo tumezoea inapokuja wakati wa ukame wanawahimiza waende kulima kwenye maeneo ya matingatinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia pale Wilayani Misenyi, kuna hifadhi inaitwa Lusina; hii inagusa Kata za Bugandika na Bugorora; kuna hifadhi inaitwa Kikuru; hii inagusa Kata za Buyango na Ruzinga, lakini pia kuna hifadhi nyingine kubwa tu inaitwa Minziro. Hifadhi zote hizi zina changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na changamoto ya hawa wenzetu wa hifadhi kuanza kubainisha maeneo ya hifadhi zao na kwa kufanya hivyo unakuta wananchi wanaona wameingiliwa maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri utagundua kuna kipengele kinasema kuna vijiji 228, hii ni kwa nchi nzima na maeneo mengine, vipo ndani ya hifadhi na vijiji 157 vimeshasajiliwa. Sasa kama kwenye kitabu chake cha hotuba Mheshimiwa Waziri anatambua vipo vijiji 228 ndani ya hifadhi katika maeneo mbalimbali Tanzania na anabainisha kwamba vijiji 157 vimeshasajiliwa maana yake alichokuwa anajaribu kutueleza Mheshimiwa Waziri ni kwamba kuna migogoro hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ikishatokea kinachotakiwa ni kuitafutia ufumbuzi. Hatuwezi kuacha migogoro hii ikaendelea kwa sababu ukiacha na wewe unakuwa sehemu ya mgogoro. Kwa hiyo, nimwombe Profesa najua amebobea katika masuala haya, najua ana nia nzuri, najua wataalam wake kupitia hizi hifadhi za misitu wana nia nzuri pia basi tushirikiane kuhakikisha kwamba migogoro hii tunaipatia ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nishukuru wenzetu wa TANAPA kwa sababu nilipoteuliwa mara ya kwanza kuwa Balozi, maana kazi nyingine hizi hujasomea, nakumbuka baada ya kuteuliwa Mheshimiwa Rais akatuambia Ubalozi husomei nenda tu mtafanya kazi. Nikauliza wenzangu pale tunaanzia wapi? Tutakubaliana kwamba hebu tuwaombe TANAPA ambao wanasimamia hizi hifadhi watupe angalau mafunzo kidogo, tukienda nje huko basi tuweze kuitangaza Tanzania kwa sababu huwezi ukatangaza kitu usichokijua. TANAPA wakatupangia safari nzuri, tukaenda Northern circuit lakini pia wakatupeleka Southern circuit, tukatembelea Ruaha ni nzuri kweli kweli, tukaenda Katavi kule tukajifunza mambo mengi. Nakumbuka tulikuwa na Mabalozi mbalimbali, Mheshimiwa Balozi Batilda, Mheshimiwa Balozi Marmo, Balozi aliyeenda Msumbiji, Misri na Mabalozi wengine, kwa kweli tulijifunza vitu vingi kutokana na ziara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoenda kwenye vituo vya kazi tukajikuta kumbe kazi yetu kubwa ni kuitangaza Tanzania lakini huwezi kuitangaza Tanzania usiyoijua, ziara ile kwa kweli ilitusaidia sana. Nachukua nafasi hii kuwashukuru TANAPA na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Kijazi kwa sababu nilikuwa sijapata nafasi ya kurudi katika Bunge hili kushukuru. Kwa hiyo, nilienda, nilifanya kazi, nilijifunza na nimerudi na nawashukuru sana kwa kutupeleka maeneo hayo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jedwali Na.3 la kitabu cha Mheshimiwa Waziri linaonyesha estimates za maduhuli kwa mwaka 2015/2016 ni shilingi bilioni 25 lakini ukiangalia estimates za mwaka uliofuata ni sifuri. Sasa sijui ni makosa ya uchapaji, huwezi ukawa na makisio sifuri sijui nini kilitokea. Pia ukiangalia hata maduhuli upande wa wanyamapori ni shilingi bilioni 13 kwa 2015/2016, lakini ukiangalia mwaka unaofuata estimate ni sifuri. Nimwombe Mheshimiwa Waziri na watalam wapitie ili waweke rekodi vizuri ili vitabu viweze kueleweka isije ikaonekana kwamba mwaka huu unapata shilingi bilioni 25 mwaka unaofuata unapata sifuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi ambayo wanaifanya najua kutangaza utalii ni kazi ngumu. Niseme jambo moja, nimesikiliza kwa makini hotuba ya wenzetu wa upinzani, hili suala la Loliondo limechukua muda mrefu na naomba niseme tusipoangalia, hatutapata ufumbuzi kwa sababu kuna wadau wengi wanaoshiriki kwenye changamoto ile lakini nzuri na mbaya zaidi kuna na hela nyingi pia. Sehemu yoyote ikishakuwa na hela nyingi zinazunguka, usipokuwa makini huwezi kupata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia OBC inaongelewa sana lakini nyuma ya OBC kuna wadau wengine pia ambao na wao wanachochea mgogoro huu. Ukitumia nguvu nyingi kuzungumzia OBC ukasahau wengine kama Wamarekani na watu wengine, ndugu zangu ule mgogoro wa Loliondo utaendelea miaka mingi kwa sababu kuna hela zinazunguka na watu hela wanazihitaji na hakuna anayependa kusema kwamba kuna hela. Kwa hiyo, ule mgogoro tusipokuwa makini utaendelea miaka nenda miaka rudi, watakuja Mawaziri hapa, tutawawajibisha, tutasema Waziri hapa umechukua mlungura ondoka, tutafanya kile na kile lakini Loliondo itaendelea kuwa Loliondo miaka nenda, miaka rudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa pale Brussels, ndani ya Bunge la Jumuiya ya Ulaya ilitolewa hoja nzito na Tanzania wakatuazimia pia, hoja ile ilikuwa inahusu land grabbing. Land grabbing ni hoja mpya na ya kisasa ambayo wanasema unamnyang’anya mtu ardhi unaenda kutumia kwa maslahi yako au kwa vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ile ya land grabbing ilipokuja, Bunge la Jumuiya ya Ulaya likaiazimia, likaleta hoja, likasema Mheshimiwa Balozi jibu. Balozi kazi yako ya kwanza lazima utetee nchi yako, kwa hiyo, unapoambiwa jibu, majibu unayotakiwa kutoa ni yale ya kutetea nchi yako siyo jibu lingine. Nilipopitia zile hoja zilizotolewa ambazo ni nyingi sana kuzipitia kwa sababu hapa Tanzania tuna zaidi ya mashirika 70 yote yako Loliondo na kila shirika lina taarifa na kila shirika linaongelea kivyake kuhusu masuala ya land grabbing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiacha tatizo tunaloliona Loliondo ndiyo wanasema kuna Loliondo nyingine kubwa inatengenezwa na Bunge la Ulaya limeshapitisha azimio. Tusipojipanga sasa, siku azimio likirindima ndani ya Bunge hili, ndugu zangu hatutaweza kupata majibu, tutaanza kutafutana mchawi ni nani, ndiyo maana nasema mapema ili tujipange. Yale majibu niliyotoa nikiwa Balozi, ukiwa Balozi unazungumza kama Balozi, nikija humu siwezi kuzungumza kama Balozi, nitazungumza kama Mbunge na hiyo itakuwa lugha tofauti kabisa, ndiyo maana nawaombeni ndugu zangu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo la kwanza, mpaka wa Tanzania na Uganda uko Mtukula, Minziro, Kakunyu na hauko Bunazi. Kwa hiyo, wale wote wenye mawazo ya kufikiri kwamba ukifika Bunazi umemaliza Tanzania na hivyo wanazuia mchele, mahindi na sukari kufika Mtukula. Naomba kuanzia leo ninapozungumza hapa wakome mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inaeleza na kubainisha kwamba kuna nia ya dhati ya kuanzisha masoko ya mpakani, masoko ya kimkakati. Huwezi ukaanzisha masoko haya na huwezi ukatekeleza mkakati huu kama una watu ambao wanafikiria mpaka wa Tanzania ni Bunazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuondoa tozo kama tulivyoziondoa ni jambo jema, lakini itakuwa na maana tu kama faida itamfikia mkulima moja kwa moja. Lengo pia liwe kuhakikisha sasa tunaongeza fedha anazozipata mwananchi kutoka asilimia 88 ya sasa walau tupandishe hadi asilimia 90 ya bei ya soko la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, makato ya 0.75% yaliyopunguzwa mpaka 0.375% ni jambo jema. Hata hivyo, lengo na best practice ni kufuta kabisa mwisho wa siku.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, kinachoitwa mifuko ya mazao ambapo kuna fedha zinakatwa na kupelekwa kusaidia mifuko hiyo ni makosa kwa sababu tulipoamua kuondoa gharama za kuendesha bodi mbalimbali hatukumaanisha kuleta makato mengine tukayaita makato ya mifuko ya mazao. Jambo hilo likome mara moja kwa sababu ni kumbebesha mkulima gharama ambazo tulishaziondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, cess 5% ambayo tunamtoza mkulima wa kahawa kupitia kwenye vyama vya msingi si jambo jema. Nchi zilizoendelea duniani kama vile Vietnam, Mexico na India, hivi sasa hutoza 1% tu kwenye border na si vinginevyo. Huu utaratibu tunaweza kuufuata na ukatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, kumkata mkulima wa kahawa kilo mbili kila gunia kwamba hiyo ndiyo gharama ya gunia si jambo jema na ni wizi wa mchana. Ukienda maeneo mengi vijijini unakuta mizani haikaguliwi na matokeo yake unaweza ukapeleka kilo 50 ukaambiwa hizo ni kilo 45, huo ni wizi wa mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Kigarama, kuna mtawala mmoja anaitwa Pastory Kabeba, mtawala huyu amekuwa akisababisha hasara kubwa kwa kupima mwenyewe kwa kufikiria anachoona kinafaa na kumbebesha hasara mkulima. Jambo hilo likome. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, soko la kahawa katika Afrika Mashariki tulikuwa tukifikiria sehemu tatu, tunazungumzia Jumuiya ya Ulaya, Sudan na Honduras lakini sasa South Sudan imeshajiunga na Afrika Mashariki. Kwa hiyo, badala ya kuzungumzia soko la Ulaya ambalo kwa maamuzi yetu tumeanza kujiondoa na kwa kuwa hatuwezi kuzungumzia Honduras, basi Mheshimiwa Tizeba peleka tume ya wataalam hapo South Sudan na tujiunge na Sudan tukauze kahawa yetu kwa sababu kuna soko kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kyakakera Wizara ilitumia shilingi milioni 497 kwa ajili ya maji ya umwagiliaji, maji hayo hata ukitaka kikombe kimoja hauwezi kukipata. Naomba hilo jambo ahangaike nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Labda nianze kutoa tu masuala machache ya utangulizi na hii ni kwa faida tu ya wachumi na wale ambao siyo wachumi wanaweza kujifunza. Jambo la kwanza ambalo ni neutral, tunaposema Serikali inatekeleza D by D, jambo muhimu siyo nani anakusanya fedha hizi, ni kwamba fedha hizi zikishakusanywa nani anazitumia? Nani anafanya maamuzi ya kuzitumia? Hilo ndilo jambo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia unapoamua kwamba unaongeza Sh.40/= kwa lita, sasa wachumi hata tungekusanya Maprofesa wa Uchumi humu kwenye ukumbi huu, wote wanaweza wakabishana; kuna wengine watasema labda bei zitaongezeka, kuna wengine watakwambia bei hazitaongezeka. Inategemea wachumi hawa walisomea Vyuo vipi na waliwaelewa vipi Walimu wao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmoja aliyefundishwa vizuri atakwambia kulingana na taarifa zilizowasilishwa Bungeni, Kitabu cha Mpango wa Maendeleo 2017/2018, ukikiangalia na taarifa iliyotolewa na World Bank iliyoko kwenye kitabu kile, kinakuonesha kwamba bei ya petroli mwaka 2014 kwa ujazo wa lita 1,000 ilipungua kutoka dola 905 kwa wastani mwaka 2014 mpaka dola 462. Kwa hiyo, atakwambia trend ya bei ya mafuta katika Soko la Dunia imekuwa ikipungua kutoka dola 905 kwa wastani mpaka dola 462.

Mheshimiwa Spika, mwingine atakuambia kuhusu diesel. Utauliza, je, diesel? Atakujibu kulingana na takwimu ambazo zimetolewa na World Bank kwamba nayo ilipungua bei kutoka dola 809 mwaka 2014 mpaka dola 380; na mwingine atakwambia kuhusu mafuta ya taa nayo pia yalipungua kutoka dola 407 mpaka dola 406 kwa ujazo. Kwa hiyo, atakwambia kwa kuwa trend inaonesha bei hizi zimekuwa zikipungua, hivyo, ongezeko lolote litalotokea katika masuala mengine ita-offset kile kinachotokea kwa sababu bei katika Soko la Dunia mwenendo ni kupungua sana kuliko chochote kile unachofanya kuongeza. (Makofi)

Kwa hiyo, itategemea huyo mtu alisomea wapi na anaelewa vipi kutafsiri hizi takwimu. Ukikutana na mwanafunzi wangu niliyemfundisha darasani ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Fedha, yeye atakwambia alipofundishwa na Mwalimu mmoja aliyebobea kwenye uchumi, alimwambia unapoangalia haya masuala ya bei kuongezeka na kupungua, kuna kitu kinaitwa surplus demand na kuna kitu kingine kinaitwa consumer surplus na producer surplus.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, atakwambia siku zote unapoongeza bei most likely, consumer surplus inaweza ikabadilika, lakini katika hili inaonekana ambaye atalazimika kupunguza bei ni yule consumer surplus kwa sababu kuna ushindani katika soko hili na kama mtu hatataka kushindana, ataondoka. Sasa huu ni uchumi mwepesi ambao nisingependa kuendelea na nawakaribisha wengine wasome vitabu vya Economics Made Simple. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme haraka haraka kabla sijasahau kwamba bajeti hii ni nzuri na naiunga mkono kwa asilimia mia moja. Naunga mkono kwa kuzingatia bajeti nyingi ambazo nimeziona nikiwa katika Bunge hili, lakini pia na bajeti zinazotokea maeneo mengine; na ukiangalia malengo yetu manne ni kwamba bajeti hii itatusaidia kuweza kuyafikia. Malengo yetu siyo mengi, ni machache. Tunasema tunataka kujenga uchumi wa viwanda, tunasema bajeti hii itatusaidia; tunasema tunataka kujenga uchumi wezeshi, bajeti itatusaidia; tunasema tunataka bajeti hii itusaidie kuunganisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu, bajeti hii itatusaidia.

Mheshimiwa Spika, kubwa tunasema ili bajeti hii iweze kutekelezeka, tunahitaji watu wenye uwezo wa kuisimamia vizuri na tunaona sasa tunaye Rais ambaye anaonesha yuko tayari kusimamia na ameanza na makinikia. Kwa hiyo, tusiwe na wasi wasi na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ya kuzingatia ili tuweze kufanikiwa vizuri. Siwezi kuyataja yote, nitataja machache. La kwanza ambalo lazima tulizingatie, chakula ni uchumi, chakula ni ushindani. Lazima tuongeze nguvu zetu za kuhakikisha tunasimamia vizuri Sekta ya chakula. Ukiangalia takwimu tulizonazo, taarifa iliyotolewa na Benki Kuu inaonesha mwaka 2014 wastani katika Wakala wa Hifadhi ya Chakula, zilipanda mpaka wastani wa tani 455,000. Ilipofika mwaka 2017 zimepungua mpaka wastani wa tani 86,000 kwa mwezi, Januari, 2017 zilipungua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutoka tani 455,000 wastani wa hifadhi ya chakula ndani ya ghala kwenda mpaka tani 86,000 lazima zote tukubali kwamba kuna tatizo. Kwa hiyo, lazima tuelekeze nguvu zetu za kuongeza wastani, kwa sababu tunapozungumza uhaba wa chakula kwenye nchi au chakula kilicho kwenye nchi tunaangalia chakula kilichoko kwenye ghala la Taifa na maghala mengine ya watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unapoona kwenye ghala la Taifa inapungua kutoka wastani wa 455,000 kwa mwezi hadi 86,000 kwa mwezi, maana yake kuna tatizo ambalo hatuwezi kulifumbia macho, lazima tulishughulikie. Lengo letu kwa kuwa sitaki kusema mengi, tulenge kuongeza wastani wa chakula kwenye ghala letu la Taifa kutoka tani 86 kwa mwezi hadi kuelekea tani 500,000 kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mpango wa Maendeleo kimeeleza vizuri kwamba chakula ni muhimu na lazima tujielekeze katika kuongeza hiyo hifadhi. Ili tuweze kufanya hivyo yapo mambo mengi ya kufanya. Moja, ni lazima tutoe uhuru kwa wakulima wetu kuwa na uhuru wa kulima na kuamua wapi wauze mazao yao bila kuwekewa masharti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, South Sudan sasa ni mwanachama wa Afrika Mashariki, wana soko kubwa la kupenda kununua mazao yetu, lakini mara nyingi tumekuwa tukizuia wakulima wetu kwenda kuuza mazao popote wanapotaka wakati inatolewa bei kubwa. Kwa kufanya hivyo, tunawaondolea uhuru wa kuuza popote na tunawazuia kwenda kwenye mabenki kukopa ili kuongeza uzalishaji. Ndiyo maana nasema, lazima tuongeze uhuru kwa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia lazima tuachane na kutoa vibali vya upendeleo. Kule Mtukula ukienda unakuta kuna baadhi ya watu, wengine tunao Bungeni humu, sitapenda kuwasema, wengine wanapata vibali vya kupeleka mazao nje cha nchi, wengine hawapewi vibali.

Mheshimiwa Spika, nilijaribu kufuatilia hili, nikagundua inahusisha Waheshimiwa wazito tu. Ni uchafu gani huu? Sasa sitawataja majina yao humu, lakini niwaombe tu waache kwa sababu wale wakulima wadogo wadogo na wao wanayo haki ya kuuza mazao yao kokote kule. Kwa hiyo, jambo hili liangaliwe.

Mheshimiwa Spika, napenda kwa haraka haraka kuzungumzia hoja nyingine ambayo inahusu suala la kuondoa ugonjwa wa mnyauko wa migomba. Kule Kagera tunao ugonjwa unaosumbua sana, tumejitahidi kupambana nao lakini wataalam wetu wa MARUKU wakubali kwamba wameshindwa. Serikali iongeze fedha ili tuweze kuondoa ugonjwa huu kabisa kuliko kudhibiti tatizo la uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kwamba ukiangalia taarifa ya hali halisi ya uchumi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama muda umekwisha, mengine nitachangia kwa maandishi, lakini naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. BALOZI DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii muhimu ya kuchangia mjadala unaoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kukiri kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati, hainiondolei haki ya kutoa maoni yangu pale ambapo kuna jambo naliamini, nalielewa vizuri na kuna jambo ambalo nilishawahi kulisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kwamba asilimia 10 kwenye mafuta ya michikichi, ile ambayo wanaita crude palm oil kutoka nje iondolewe. Kama unavyokumbuka jambo hili tulishalifanyia kazi kwa muda mrefu, tunalielewa, kwamba ukitaka kuendeleza viwanda vidogo vidogo vinavyosindika mafuta, kwa mfano vya alizeti na vinginevyo lazima udhibiti haya mafuta yanayotoka nje yanayoitwa crude wakati si crude. Nisingependa kuingia kwenye mjadala huo, Wizara ya fedha wanaelewa na walishafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa maoni yangu nafikiri asilimia 10 iendelee kuwepo ili kuweza kusaidia viwanda vidogo vidogo vinavyosindika alizeti na vinginevyo. Nilisimamia hili nikiwa Naibu wako, unakumbuka, jambo hili nililisimamia nikiwa Waziri, nilisimamia pia nikiwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki na naendelea kuamini hivyo nikiwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa vyovyote vile sitakuwa sehemu ya maoni tofauti na hayo ingawa huwezi ukazuia watu wengine kutoa maoni yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niseme suala la kongano la ngozi kule Zuzu…

(Hapa kulitokea hitilafu ya umeme)

MWENYEKITI: Hebu subiri kidogo Mheshimiwa Balozi. Jamani kuna shoti huko juu. Wataalam! Imeungua pale juu. Imeungua tu, hakuna kitu cha kuhatarisha hapo. Tuendelee.

MHE. BALOZI. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye hilo. Kama nilivyosema, nadhani licha ya hiyo changamoto, hoja yangu ibaki pale pale na Hansard wachukue kama nilivyosema kwa sababu siku zijazo watu watasoma hiyo Hansard na naomba msimamo wangu ubaki vile vile kwa sababu ndivyo ninavyoamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ukienda mbele ya Kamati ukaeleza changamoto zako tutazipokea changamoto hizo, lakini kupokea changamoto zako si kwamba tumepokea ziwe zetu, changamoto zako zitaendelea kuwa changamoto zako hadi pale tutakapoona uamuzi wa maana unaotakiwa kufanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Zuzu, kongano la ngozi la Zuzu ni jambo jema, limeelezwa vizuri na Wizara inafanya kazi nzuri, Wizara yetu ya Biashara na Viwanda na kwenye taarifa yetu tumeshauri ni jambo jema. Hata hivyo napenda nishauri, kama wenzetu wa Ethiopia walivyofanya; Ethiopia walivyofanya ili kusaidia Sekta ya Ngozi, wao walitoa temporary Government guarantee, ni temporary. Maana changamoto kubwa hata pale Zuzu tukiwatengea eneo tukasema sasa wanaotaka kuwekeza kwenye ngozi waje wawekeze hatimaye hawa wawekezaji wadogo wadogo tatizo kubwa ni mtaji. Mtaji wa kununua mitambo na mashine na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Ethiopia walivyofanya wao wana ngozi kama tulivyo na ngozi sisi huku, wanatoa temporary guarantee; kwa maana ya kwamba kama wewe ni mfanyabiashara wa ngozi unataka kuwekeza kwenye viwanda vidogo vinavyozalisha bidhaa za ngozi basi Serikali inaku-guarantee unapata hizo mashine, unajenga jengo zuri, unaweka mitambo yako, ukimaliza kuweka hivyo basi ile guarantee ya Serikali inaondolewa kwa sababu unakuwa sasa unaweza kusimama kwa miguu yako sasa Seriakli inasema tembea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia wamefanya hivyo na sisi kuna sababu ya kujifunza kutoka Ethiopia, tukifanya hivyo, nina uhakika hii Zuzu, tunasema kongano la ngozi la Zuzu litakuwa la manufaa lakini tusipofanya hivyo tutakuwa na kongano la ngozi la Zuzu na litaendelea kuwa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kidogo kwenye Wizara ya Mazingira. Tulienda kule Kihansi, kule kuna Maprofesa wazuri kutoka SUA. Walitufundisha mambo mengi, wanafanya kazi nzuri kuhusu masuala ya mazingira, ni wataalam wa kuhakikisha vyura wa Kihansi wanaendelea kuwepo. Hata hivyo mtaalam kutoka Wizara ya Mazingira moja alilotuambia kwamba wale vyura wa Kihansi wanapoendelea kuwepo; hoja sio vyura kuwepo, hoja ni kwamba wanapokuwepo wanasema mazingira mnayatunza vizuri. Wakipotea maana yake wanakwambia sasa mmeanza kuharibu mazingira. Kwa hiyo tusije tukaangalia vyura wa Kihansi kama vyura bali tuangalie wale vyura kama kielelezo kinachotueleza tunafanya kazi gani kutunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Profesa mmoja pale alituambia akisema ukiwa msafi sana unaishia kuugua sana. Sasa sitaki kuingia huko lakini na hilo somo tumejifunza pia kwamba ukiwa msafi sana basi wewe unaugua sana kuliko wasiokuwa wasafi. Kwa hiyo alitoa theory yake pale, wale maprofesa ni wazuri kwa theory lakini alituzindua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa tuliyoiona pale wale watalam Maprofesa kutoka SUA wanatumia fedha za wafadhili na fedha za wafadhili zinafikia mwisho wakati wowote. Sasa inabidi tuangalie tunasaidiaje tafiti kama hizo ziweze kuendelea. Kama fedha ya wafadhili zikimalizika na zile tafiti zikafungwa basi tutakuwa hatuyatendei haki mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Wizara ya Mazingira inabidi tuiangalie katika siku zijazo kuhakikisha tunaitengea fedha za kutosha kwa sababu mazingira yanapoleta changamoto kila mtu analalamika. Sasa tusiwe wazuri wa kulalamika tu bila kuchukua hatua; na hatua ya kwanza ni kuhakikisha tunatenga fedha za kutosha ili tuweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni hii dhana ya Tanzania ya viwanda. Nimesoma na sote tumesoma hapa, ule mpango wa miaka mitano na zile taarifa mbalimbali kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda. Tunaposema Tanzania ya Viwanda hatumaanishi na sidhani kama kuna mtu alishafikiria kumaanisha hivyo; hatumaanishi kwamba sasa Serikali itaanza kujenga viwanda, hapana! Tunaposema Tanzania ya viwanda ni kwamba tungependa kuweka mazingira mazuri ya wawekezaji katika viwanda, watu waje wawekeze katika viwanda, Watanzania wawekeze katika viwanda, hatumaanishi sasa kwamba Serikali itaanza kujenga viwanda.
Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia mada hii muhimu iliyo mbele yetu. Naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja iliyo mbele yetu na naunga mkono hoja hii kwa kutumia hoja ndogo saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza kwanini naunga mkono hoja hii, naunga mkono hoja hii kwa sababu itatuwezesha Tanzania kunufaika na shilingi trilioni 195 ambazo tutaweza kuzipata kwa sababu tu ya kuridhia mkataba huu. Kwa nini nasema tutanufaika na sehemu ya fedha hizi? Fedha hizi trilioni 195 zimetengwa kupitia makubaliano ya Nchi za ACP pamoja na Jumuiya ya Ulaya ni bilioni 70 sasa ukiziweka kwa fedha za Kitanzania zinakuja kwenye trilioni 195 na fedha hizi zinaelekezwa kwa nchi 78 kimsingi kwa sababu nchi wanachama wa ACP ni 79, lakini Cuba yeye ni mwanachama mtazamaji, kwa hiyo, yeye hatanufaika hata na shilingi moja.

Kwa hiyo, ukigawa fedha hizi kwa nchi zote za ACP ni fedha nyingi sana na fedha hizi zinalenga kuelekezwa kwenye Global Climate Change Alliance ambayo inalenga katika kutekeleza huo mkataba wa Paris. Lakini pia ni fedha ambazo zitatusaidia sana katika kupambana na mazingira ukizingatia ukweli kwamba rasilimali siku zote huwa hazitoshelezi, kwa hiyo, kila fursa inayojitokeza ya kukuwezesha kupata rasilimali lazima tuichangamkie kwa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa sababu najua kwamba tutaweza kunufaika na fedha hizi lakini nina uhakika kabisa kwamba Wizara imejipanga, wameanzisha mfuko wa kutafuta fedha za kupambaa na mazingira na najua mipango ambayo tayari wameshaiweka ya kuhakikisha wanapata fedha na ndiyo maana nalishawishi hata Bunge hili katika bajeti ijayo basi tutenge fedha za kuweka kwenye huo mfuko wa mazingira ili waweze kuandaa miradi mizuri ya kuweza kunufaika na fedha hizi na fedha nyinginezo. Kwa hiyo, hiyo ni hoja ya kwanza kwa nini naunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hoja ya pili, ukiangalia mazungumzo yaliyokuwepo kuhusiana na masuala ya mazingira nakumbuka pale Brussels tulikuwa na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mkataba huu maana mkataba huu ulizungumzwa maeneo mbalimbali duniani. Ulizungumzwa New York, ulizungumzwa Brussels, ulizungumzwa Beijing hata Tanzania mlizungumza wakati huo sikuwepo nilikuwa Brussels lakini tulipokuwa Brussels tulizungumza pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja kubwa ambalo lilichukua muda mrefu kuzungumza na kukubaliana ni kukubaliana kwamba ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kila nchi itabidi ichangie kulingana inavyoharibu mazingira lakini pia kwa kuzingatia uwezo wake wa kiuchumi. Hoja hii nchi zilizoendelea hazikuitaka sana lakini kwa mara ya kwanza katika dunia hii, nchi za ACP zikaungana na nchi za Ulaya ili kuwa na msimamo wa pamoja wa kwamba katika uharibifu wa mazingira basi kama wewe unaharibu zaidi utatakiwa uchangie zaidi katika kupambana na tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni hoja iliyotuchukua muda mrefu lakini nashukuru hatimaye hoja hiyo ilipita na ilipoenda UN mataifa yote yakakubaliana na ndio maana tunaita kifungu namba mbili katika mkataba huu kinachosema mataifa yote duniani yatawajibika kupambana na mazingira kulingana na jinsi anavyochangia, ukichangia kuchafua zaidi basi uchangie zaidi katika kupambana na hayo mazingira kwa hiyo, ndio maana nasema naunga mkono hoja hii kwa sababu ni hoja muhimu inatoa fursa hata kwa mataifa ambayo yanachafua zaidi yaweze kuchangia zaidi katika kupambana na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni kwanini naunga mkono haja hii ukiangalia kifungu namba tano kinasema nchi zinazoendelea zitaendelea kusaidiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Sasa ukisema nchi zinazoendelea na nchi nyingine zenye uchumi kama wa sisi ni kwamba sisi tunachangia kidogo katika kuharibu mazingira, lakini kifungu hiki kinatuhakikishia kwamba tutaendelea kusaidiwa katika kupambana na mazingira.

Lakini sababu nyingine kwa nini naunga mkono hoja hii ukiangalia sehemu ya pili, kifungu cha 4(2) kinasema nchi zinazoendelea ziendelee kukabiliana na hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mabadiliko ambayo hakuna mkataba ambao utasaini tu usiokupa wajibu, ni kwamba makubaliano haya tuna wajibu wa kufanya ni upi. Wajibu wa kufanya ni kuendelea kuwa na mikakati na kuonyesha dhamira ya kuendelea kupambana na mazingira ndiyo maana tunapopitisha tunatoa ridhaa maana yake tunakubali kama Bunge kwamba tutaendelea kusaidia Wizara yetu ya Mazingira na Masuala ya Muungano kuiwezesha kuendelea kupambana na mazingira hiyo ndio maana yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiangalia mwenendo wa bajeti Wizara imekuwa ikpatiwa kila mwaka unaona kwamba ilikuwa si fedha zinazotosheleza mahitaji yao yote basi kwa kupitisha kifungu hiki ninakuwa nina uhakika kwamba sasa tunaenda kutenga fedha za kutosha kwa Wizara ya muungano na masuala ya mazingira ili kuweza kusaidia masuala mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja iliyo mbele yetu kwa sababu hata mataifa makubwa kama Marekani na Japan sitawataja baadhi ya viongozi kwa sababu kidiplomasia si vizuri kumtaja mtu, wapo waliosema hawatakubaliana na masuala ya Paris Agreement, lakini naomba kulithibitishia Bunge hili kwamba mataifa yote makubwa mnayoyajua yaliyokuwa yanaonesha hayatakubaliana na kupambana na mazingira tayari yameweka sahihi na tayari yameridhia, sasa wale waliokuwa na wasiwasi waliojaribu kuonesha kwamba hawatakubali, wameshakubali sioni sababu kwa nini sisi tusiridhie kwa sababu sisi ni wanuifaika wakubwa wa makubaliano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuridhia maana yake tutaweza kunufaika na Global Environmental Facility, Adaptation Fund, pamoja na Green Climate Fund na mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho hoja ya saba kwa nini hoja iliyo mbele yetu ni muhimu tukiridhia maana yake tunaiambia dunia kwamba tutaendelea kupambana na mazingira, miradi mizuri kama ya Kihansi tutaendelea nayo kuna mradi mzuri sana unaendelea kutekelezwa chini ya ofisi ya Makamu wa Rais mradi kama Ruaha Mkuu, kutunza Ruaha Mkuu kwa sababu tunazungumzia Green Stiegler’s Gorge huwezi ukazungumzia Stiegler’s Gorge wakati unaendelea kuharibu mazingira, lakini tunaposema tunasaini, tunaiambia dunia kwamba tutatunza hata mazingira, lakini tutaendelea kutoa elimu, tutaendelea kutunza vyanzo vya maji, pale Ocean Road kuna mradi mkubwa wa kutunza mazingira na zaidi ya nchi 10 kutoka dunia nzima zinakuja pale kuangalia Tanzania tunafanyaje kutunza mazingira kwa hiyo, ni mfano wa kuigwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hizo saba naunga mkono hoja iliyo mbele yetu kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii muhimu ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu. Naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi kwa Serikali yetu na kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika na inafanyika kwa speed ambayo ni kubwa na walio wengi hawakutarajia kama tunaweza kufanya mambo haya kwa speed tunayoenda nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulipoweka mtaalam mshauri ili ashauri nchi za Afrika Mashariki ni kwa namna gani tuendeleze mfumo wetu wa reli, yule mtaalam alitushauri nchi za Afrika Mashariki akasema hizi reli zenu mlizonazo ni vizuri muendelee nazo kwa sababu nyie ni nchi maskini, nyie hamhitaji zinazoenda kwa kasi na hamna fedha za kufanya hayo mambo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tuliokuwepo wakati ule pale Arusha tulikataa na tukamwambia huyo mtaalam mshauri kwamba ni kweli uchumi wetu haujakaa vizuri nchi za Afrika Mashariki, labda hatuhitaji treni zinazokimbia sana kama unavyosema labda bado sisi ni nchi maskini, lakini hatuwezi kukaa hivyo milele, tunabadilika kila siku. Kwa hiyo, tukakubaliana kwamba tutajenga sasa standard gauge kwa nchi zote za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali yetu kwamba tumeonesha njia, nchi zote za Afrika Mashariki tulikubaliana kwamba sasa tujenge standard gauge lakini Tanzania tumeanza sio tu tunajenga standard gauge lakini pia tunajenga standard gauge ambayo tutatumia nishati ya umeme. Hilo ni jambo kubwa nawapongeza sana wanaohusika na tuendelee kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea mambo machache, la kwanza, kuna malalamiko ya wananchi Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, jukumu mojawapo ni kushughulikia malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi. Malalamiko yao mengi lakini kwa leo nitazungumzia malalamiko ya wananchi wa Kata ya Kakunyu ambayo yamechukua zaidi ya miaka 18 bila kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mgogoro mkubwa na umechukua muda mrefu, mgogoro wa Ranchi ya Misenyi pamoja na vijiji vinavyozunguka Ranchi ya Misenyi. Mgogoro huo umechukua muda mrefu, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu sasa wakati umefika tuweze kupata ufumbuzi na ukiangalia kwa umakini. Mgogoro huo umechangiwa na mambo matatu ambayo tukiamua tunaweza tukayapatia ufumbuzi kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza lililochangia sana mgogoro huo ni kwamba, tulipoamua mwaka 2002 kwamba Ranch ya Misenyi na Ranch nyingine ambazo kuna maeneo makubwa yasiyotumiwa vizuri yawekwe kwenye blocks ndogo ndogo na wagawiwe wafugaji wadogo wadogo, lakini utekelezaji ulivyoanza haikufanyika hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia uamuzi uliofanyika ni mzuri, lakini utekelezaji ulipoanza haikufanyika hivyo, hawakugawiwa wafugaji wadogo wadogo badala yake waligawiwa watu wala hawajawahi kuona ng’ombe na wengine wala sio wafugaji na wengine wala hawapo ni marehemu lakini waligawiwa Ranch. Sasa mgogoro ukaanzia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kukatokea uamuzi, ulikuwa mzuri tu kwamba ile Ranchi ya Misenyi kwa maeneo ambayo ranchi ilikuwa haiyatumii, basi lazima NARCO iyagawe katika blocks ndogo kama nilivyosema haikufanyika hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ilikuwa ni kwamba ukiangalia ile ramani ambayo NARCO walikuwa wanaitumia na ambayo bado wanaitumia ingawa hawataki kuionesha, ramani ile wanayoitumia wao unapofika Mto Kagera unapovuka tu ramani wanayoitumia NARCO inaonesha kuanzia Mto Kagera mpaka kwenye mpaka wa Uganda hakuna mtu anayeishi na hakuna kijiji wala kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanapokaa kwenye meza yao wanagawa wanavyotaka, jambo ambalo sio sahihi. Maana unapovuka Mto Kagera unakutana na Makao Makuu ya Wilaya, unakutana na Kata nyingi tu na vijiji vingi tu lakini ramani wanayoitumia kugawa blocks zinazotuletea matatizo, yenyewe inaonesha unapokatiza tu Mto Kagera hakuna vijiji, kata wala mtu. Sasa kwa utaratibu huo lazima migogoro ya namna hii iendelee kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi, leo hii nimeona nishauri ufumbuzi. Nitashauri mambo manne; jambo la kwanza, ni kwamba mipaka ya Ranchi ya Misenyi na Vijiji vinavyozunguka ranchi hiyo ni Mto Kiboroga na Mto Kyaka Kuru, hii ndio mipaka inayoeleweka kwa mtu yeyote yule. Kwa hiyo, ufumbuzi wowote ule ambao hautabainisha kwamba mipaka ya ranchi ni Mto Kiboroga na Mto Kyaka Kuru unakuwa hujatoa ufumbuzi wowote. Kwa hiyo, huo ni ufumbuzi wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wa pili, iwekwe barabara ya ulinzi na kukagua mipaka kuanzia Mutukula hadi Kakunyu maana ukiwa na mpaka ambao huwezi kuukagua ni kazi bure. Ukiangalia upande wa Uganda wao wana barabara nzuri tu ya kukagua mpaka wao, unapokwenda upande wa Tanzania hakuna barabara. Kwa hiyo, barabara hii ni barabara ambayo lazima tuipe kipaumbele, tuitengeneze kwa haraka na itatusaidia kufanya mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya kwanza imelia, sababu nyingine sitaendelea nazo nimalizie na mambo mengine matatu ambayo nataka kuyaongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu, tulikaa Wabunge wa Kagera na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, tumekubaliana katika kikao mambo ya msingi ambayo yakitekelezwa yatamaliza migogoro ya ardhi Karagwe, Muleba na Misenyi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu amuelekeze huyo Mkuu wa Mkoa amletee makubaliano tuliyokubaliana ili aweze kutusaidia kumaliza mgogoro huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile iliundwa Kamati nzuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu na akatoa hadidu za rejea nzuri tu. Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kwamba atatuletea taarifa ya Kamati hyo, lakini hiyo taarifa siioni na wala haiji Nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu taarifa hiyo ije ili tuweze kumaliza mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa alichangia kuhusu zao la kahawa, nami nizungumze kidogo tu. Zao la kahawa, kuna maamuzi ambayo yamefanyika, ni utaratibu mpya, mzuri tu. Niseme mambo mawili kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, uuzaji wa kahawa ni biashara na mtaalam wa uchumi Adam Smith alishasema, uchumi huendeshwa na mkono usioonekana (invisible hand). Uchumi hauendeshwi na mtutu wa bunduki, wala mizinga. Kwa sababu hiyo, ufunguzi wowote tunaouweka kuendesha uchumi, uuzaji wa kahawa, lazima tulijue hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo napenda kulitoa hapa kwa haraka ni kwamba kama huna muda wa kusoma vitabu, maana duniani vitabu viko vingi. Chagua vichache vya kusoma. Kuna kitabu kimoja kinasema, Why Nations Fail? Moja ya sababu kitabu hicho kinasema Nations fail, yaani Mataifa mengi hushindwa kuendelea kwa sababu ya kutojenga mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaposema unabadilisha mfumo wa kununua kahawa, hujajenga mifumo ya kununua kahawa, ujue utapata matatizo. Kwa sababu unaposema Vyama vya Ushirika kuanzia sasa vinunue na vinunue vyenyewe tu, aah, shughuli ipo. Kwanza ni lazima ujenge hivyo Vyama vya Ushirika viwe tayari kununua hiyo kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata taarifa kwamba wametangaza bei, wakasema watanunua kwa Sh.1,000/= na Profesa amesema hapa, lakini sio wakulima wa kahawa ninaowajua. Hao ninaowajua, hamtakaa mwone kahawa yao. Najua tutajidanganya kwamba tuna wanajeshi, tuna nini, watashughulika, watapambana, hiyo ni kupoteza muda bure, kwa sababu wakulima na wao wanajua soko liko wapi. Mkulima siku zote atapeleka kahawa yake kule ambako anajua atapata soko la uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu. Naomba nianze kutoa pongezi kwa Serikali yetu kwa kazi nzuri sana inayofanyika katika kudumisha na kuboresha huduma za afya, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu sote tumeshuhudia bajeti ya dawa imeongezeka kutoka bilioni 30, mpaka bilioni 270 hili siyo jambo dogo. Nachukua nafasi hii kumpongeza pia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya kusimamia sekta ya afya, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti,achukua nafasi hii pia kuwapongeza Wataalam wetu wanaosimamia MSD kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya ya kusambaza madawa, wamefanya mambo mengi pale, mengi yanaonekana kwa mfano, wakinunua magari kila mtu anayaona, ni rahisi kupongeza magari yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa walilolifanya zaidi ya magari ni kuweka mfumo wa Car Tracking System ambao gari inapobeba dawa za MSD ikisimama popote pale dereva atapigiwa simu hapohapo na kuambiwa mbona umesisima na ulikosimama siyo sehemu tuliyokutuma. Hili ni jambo kubwa na naomba waendele kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza hatua ya pongezi nimpongeze rafiki yangu, lakini pia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Mheshimiwa Profesa Janabi. Mwaka 2000 nilikutana na Profesa Janabi kule Japan alikuwa anafanya PhD yake, nikamuuliza sasa hii PhD unayosoma unasomea nini, aliniambia mambo mawili, moja sitalisema kwa sababu za kitalaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, alilisema, aliniambia angependa siku moja Tanzania waweze kufanya operation ya moyo bila kupasua moyo. Nikamwambia Mzee hii inawezekana, akasema ndiyo maana niko huku na itawezekana. Sasa hiyo ilikuwa ni ndoto yake mwaka 2000 leo hii sote tunakubali hapa Profesa Janabi na wenzake wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu moyo wa Profesa Janabi aliouonesha kwamba unapopelekwa nje kusoma basi ukisoma uwe na jambo ambalo unasema ukirudi Watanzania watanufaika namna gani. Kwa hiyo, nampongeza sana. Nakumbuka wakati ule Profesa Janabi alijaribu kunishauri akasema sasa Mheshimiwa umekuja huku Japan kwa nini usirudi na gari Tanzania nikamwambia na mimi nina ndoto yangu, hizi posho nikizikusanya hapa nikirudi nyumbani ndogo yangu ni kwenda kuwa Mbunge na nikaitekeleza. Kwa hiyo, Profesa Janabi wakati na mimi nakupongeza ukipata fursa na wewe usisite kunipongeza kwamba ndoto zako zilitimia, lakini na ndoto za kwangu zilitimia, ndiyo maana leo hii nipo hapa, nakupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumze kwa haraka nimeshashukuru MSD. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilipeleka ombi langu kwake rasmi, kwamba kituo chetu Bunazi hatuna mashine ya anesthesia breathing machine, leo hii nimepata taarifa za uhakika mashine hiyo imefika kwenye kituo na sasa mambo yote yanaenda vizuri. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kuwa Tanzania tumejaliwa miti ya asili mingi tu yenye uwezo wa kutengeneza madawa, nyote mnafahamu kuna dawa moja maarufu sana inaitwa Cotecxin, lakini dawa ile inatengenezwa kwa miti inayopatikana hapa Tanzania hasa pale Iringa. Wenzetu wanachukua miti wanapeleka kule wanatengeneza dawa wanatuuzia. Tanzania tunasema tunataka kujenga nchi ya viwanda lakini kujenga nchi ya viwanda ni jambo kubwa na hasa viwanda vya madawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Wizara ya Afya ishirikiane na Wataalam wengine kuondoa vikwazo vinavyochelewesha Tanzania kuweza kujenga viwanda vya madawa. Nina rafiki yangu Mchina amekuja kuwekeza Tanzania kwenye kiwanda cha madawa na amewekeza, lakini ilimchukua miaka miwili kupata cheti cha kusajili dawa yake wakati Kenya inachukua siyo zaidi ya miezi sita kupata cheti cha kusajili dawa. Tanzania ya viwanda ina mambo mengi, naomba tushirikiane ili kuweza kuelekea huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango mzuri unatekelezwa unaitwa RBF (Result Based Financing), huu mpango ni mzuri sana unasaidia katika ujenzi wa kutoa miundombinu pamoja na motisha katika vituo vyetu vya afya na hasa kuboresha huduma ya mama na mtoto. Mpango huu nimeupenda sana kwa sababu pamoja na kusaidia miundombinu unatoa motisha kwa wafanyakazi kwa 25%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mango huo umesababisha hata Wakunga, Manesi wao wenyewe wanazunguka kutafuta nani mama mjazito anakaribia kujifungua ili aende akajifungulie kwenye kituo chake cha afya. Mpango huu ni mzuri na nashauri usambazwe kwa Tanzania nzima. Najua hivi sasa unatekelezwa katika mikoa saba, lakini mpango huu kwa kuwa umeonesha mafanikio ukisambazwa Tanzania nzima itakuwa jambo jema.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la Bima ya Afya, natambua nimesoma kwenye hotuba kwamba sasa mpango huu wa huduma ya CHF iliyoboresha utaanza 2018, mwaka 2018 ni sasa, mpango huu utawezesha kutoa ile CHF na wananchi wataweza kutibiwa si tu kwenye kituo kile cha afya, ataweza kutiwa kwenye zahanati kwenye vituo vya afya hadi hospitali ya mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni mzuri naomba utekelezwe kwa haraka na kwa kweli mimi niko tayari hata kusitisha mambo yote lakini mpango huu ukatekelezwe. Ni kwa sababu mpango huu ndiyo utaleta ukombozi mkubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nimalize kwa jambo moja na lenyewe ni kwamba MSD wanajenga pale Kairabwa ujenzi wa Kairabwa Logistics Center. Center hiyo ni muhimu naunga mkono kwa asilimia 100 na namshukuru na Mkuu wa Mkoa wa Kagera anaunga mkono mpango huu. Kwa kweli Wabunge wengi wa Mkoa wa Kagera tunaunga mkono mpango huu, naomba ifanyike haraka itakavyofanyika ili center hiyo iweze kujengwa, tuweze kuboresha huduma za afya, madawa yawafikie wananchi kwa uharaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusisitiza ule mpango CHF iliyoboreshwa, ni mzuri na utasaidia sana katika kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba hii muhimu iliyopo hapa mbele yetu. Nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Profesa kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kusimamia sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo masuala machache ambayo ningependa kuchangia na nitajaribu kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ambayo ningependa kuchangia ni kwamba sote tunaelewa Wizara ya Elimu ndiyo inayotoa sera na miongozo ya kusimamia elimu, lakini pia Serikali inazo shule ambazo nyingi zinasimamiwa na TAMISEMI, kwa hiyo Serikali inatoa sera lakini vilevile inamiliki shule. Huwezi ukawa wewe ndiyo unamiliki shule na wewe mwenyewe ndiyo unatoa sera na unajisimamia. Nadhani wakati umefika wa kuwa na chombo ambacho ni independent cha kusimamia elimu na chombo hicho sasa tukiunde, kitaundwa kwa sheria (Tanzania Education Regulatory Authority) kisimamie shule za Serikali lakini pia kisimamie shule za binafsi na kifanye hivyo kwa usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linawezekana na tukifanya hivyo tutaweza kupiga hatua kwa sababu haiingii akilini unakuta Afisa Elimu anasimamia shule binafsi ina upungufu wa choo kimoja au vyoo viwili inafungwa halafu unakuta shule ya Serikali haina choo lakini inaendelea, hii inakuwa siyo sawa. Jambo hili inabidi tuliangalie, labda niseme tu mimi similiki shule lakini siku zijazo ninaweza nikamiliki shule pia, kwa hiyo sina maslahi yoyote katika hili bali nazungumza kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ningependa kuzungumzia changamoto. Ziko changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya shule binafsi na nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Hussein Bashe kwa taarifa nzuri aliyowasilisha kwa niaba ya Kamati yake. Mheshimiwa Hussein Bashe kati ya jambo ambalo na mimi najivunia kwa sababu nilikufundisha siasa na naona unajifunza vizuri uendelee hivyo na kwa taarifa uliyowasilisha hapa imebainisha mambo mazito ambayo yatasaidia sekta ya elimu, kwa hiyo unapofundisha wanafunzi wako na wakafanyakazi nzuri wapongeze. Mheshimiwa Bashe nakupongeza kwa kuwasilisha vizuri mawazo ya wenzako kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ziko nyingi, changamoto hizi lazima tuziangalie na tuzifanyie kazi. Moja, ukiangalia shule binafsi tuna zaidi ya shule 4,000 sasa na shule za Serikali zipo lakini ukiangalia matokeo ya mwaka jana 2017 shule 100 zilizofanya vizuri kulingana na matokeo yaliyotolewa na Wizara ya Elimu, Serikali ilikuwa na shule nne na shule binafsi ni 96 ukiona hivyo maana yake lazima tuangalie Serikali tuna kazi ya kufanya lakini pia lazima tuendelee kuziunga mkono shule hizi binafsi kwa sababu zinapofanya vizuri ndipo tunajivunia kwamba sasa shule 100 bora, kwamba shule 100 bora hizi, 96 ni binafsi na nne tu ndiyo za Serikali sasa ikishakuwa hivyo ni vizuri kuziwezesha hizi shule na kushughulikia changamoto zinazowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto zinawakabili ni utitiri wa fedha ambazo wanalipishwa. Kwa mfano, ukihitaji walimu kutoka ndani ya Afrika Mashariki kama ni shule binafsi unaambiwa lazima uende Idara ya Labour kule ulipe dola 500 kwa kila mwalimu pia ulipe dola 550 Idara ya Uhamiaji kwa kila mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kati ya jambo ambalo nikiri nadhani na wewe baadae utakiri kati ya jambo ulipokuwa Waziri na mimi nilikuwa Naibu wako tulipokuwa tuna-negotiate common market kati ya jambo ambalo nadhani tulikosea ni pale tuliporuhusu kwamba sasa hizi ada zitaendelea kuwepo na tulisema kwamba ziwe kidogo a token, isiwe chanzo cha mapato, lakini kama unavyofahamu siku hizi mawazo yetu tulifikiri hii haitakuwa chanzo cha mapato watu wamegeuza imekuwa chanzo cha mapato sasa matokeo yake tunaziadhibu shule binafsi bila sababu ni jambo ambalo nadhani liangaliwe kwa sababu linaongeza gharama nyingi bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nadhani tuliteleza ukikosea lazima ukubali makosa tulizungumza wakati ule kwamba tunahitaji tu walimu wa degree peke yao kutoka nje ya Tanzania, tulifikiri tunao walimu wa kutosha ndani ya nchi, lakini ukweli umeonesha kwamba hata ndani ya nchi hatuna walimu wa kutosha ndiyo maana tuna upungufu wa walimu, pia ukianagalia kwa umakini ni kwamba kwa upande wa walimu wa kufundisha hizi za english medium tuna upungufu wa walimu wa sayansi 26,000 na kila mwaka tuna uwezo wa kutoa walimu 2000 sasa tunapozuia kwamba walimu wasitoke nje ya Afrika Mashariki tunajiadhibu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto ambayo ziko na kodi nyingi zimeorodheshwa hili ni jambo la kuangalia kinachotakiwa ni dhamira ya kujua kwamba shule binafsi hizi siyo binafsi, kwangu mimi naweza nikasema hakuna shule binafsi ni kwamba unakuwa na shule mbalimbali nyingine kwa sababu una uwezo unaziendesha mwenyewe ambazo hauna uwezo unakariobisha private sector inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kule kwetu Misenyi tuna Minziro High School tunajenga kule, Bwabuki tunajenga high school pale na Bunazi tumeanzisha high school inafanya vizuri, nichukue nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Waziri tunapoendelea kujenga shule hizi high school ambazo ni muhimu sana basi niombe Wizara yako itusaidie wananchi wa Misenye ili tuweze kuenda kwa kasi ambayo inatarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi pia kuzipongeza shule binafsi zilizo katika Wilaya ya Misenyi, niipongeze Kadea Sekondari ambayo ina headmaster huyu anatoka Uganda, lakini shule hii inafanya vizuri sana karibu kuliko shule zote na kitu kikubwa alichonacho huyu headmaster anasisitiza discipline. Nadhani discipline ni jambo muhimu sana ukiangalia Kadea Sekondari kitu peke inachozishinda shule zote zilizotuzunguka pale ni discipline, wakifanya mitihani wanafanya vizuri kuliko shule zote, lakini kuna shule nyingine pale Kanyigo inaitwa Kanyigo Islamic Seminary na hii inafanya vizuri sana ukiangalia sifa yao kubwa waliyonayo ni discipline, ukienda kule Tweyambe wanafanya vizuri sana ni private hizi sifa kubwa waliyonayo ni discipline. Kwa hiyo, Profesa nadhani eneo hili la kusisitiza umuhimu wa discipline mliangalie jinsi gani na shule zetu za Serikali zinaweza zikatoa kipaumbele kwanye masuala ya discipline ili tuweze kuendelea kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema na kuweka wazi kwamba sitaunga mkono hoja hadi hapo masuala yangu ya kimsingi yatakapopewa majibu na hayo majibu anipatie Mheshimiwa Waziri akiwa anajua ninachokisema na nitayapima majibu yake kadri atakavyoyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza Mheshimiwa Waziri Mkuu aliunda Tume ya kushughulikia mgogoro kuhusu masuala ya ranchi, alieleza humu Bungeni kwamba wananchi wawe na subira, alikuja Misenyi akaeleza wanachi wawe na subira ili tuweze kupata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wananchi wanaendelea kuwa na subira Serikali itoe ufumbuzi wa migogoro ile, viongozi wengine wa nafasi za chini, wala sina sababu ya kuwataja majina na nafasi zao kwa sababu ni wa chini mno kiasi ambacho Mbunge kuwataja ni kuwaonea, wanaandika barua kwa wananchi kwamba waondoke mara moja kwenye maeneo yenye migogoro.

Sasa namuomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu chanzo cha migogoro ni Wizara yake atakapokuwa anajibu aeleze kwanini wanaendelea kufanya mizengwe ya kutaka kufukuza wananchi, kwenye maeneo ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, wakati yapo maelekezo ya Serikali kwamba tusubiri tuwe na subira, wananchi wamekuwa na subira kwanini wao hawahitaji kuwa na subira? Hilo ni jambo la kwanza nitahitaji majibu ya kina.

Mheshimiwa Spika, pili ninayo ramani hapa inaonesha unapovuka Mto Kagera ukaenda mpaka Uganda eneo lote lile ni Misenyi Ranch, hakuna mtu ambaye hata kama ni mtoto angezaliwa leo anayeweza kukubaliana na ramani hii. Kwa sababu ya kanuni sitataja kiongozi mmoja ambaye alishaagiza ramani hii irejeshwe ili ifutwe kwa sababu haiko sahihi. Naogopa kumtaja kwa sababu mwingine anaweza kusimama akasema Kanuni haziruhusu, sasa sitaki kuombewa mwongozo bila ya sababu, lakini ramani hii sio sahihi, kwa sababu unapovuka Mto Kagera unakutana na Makao Makuu ya Wilaya, unapoenda mbele unakuta vijiji, unakuta Kata, sasa unapokuja na ramani unaitumia kugawa blocks Misenyi Ranch ukasema kuanzia Mto Kagera kwenda mpaka Uganda yote ni ranch, ukagawa ukapata blocks 22 siwezi kukubaliana na masuala haya. Ndiyo maana nasema Mheshimiwa akija atoe maelekezo na majibu sahihi.

Mheshimiwa Spika, pia ipo ramani nyingine inayoonesha kwamba Misenyi Ranch imezungukwa na vijiji, ukiangalia nyaraka mbalimbali ambazo nizazo hapa vijiji hivi vina hati, vimesajiliwa na vinatambulika na vilipimwa. Ukisoma taarifa hii kuna sehemu Mheshimiwa Waziri anasema kuna vijiji vimevamia ranch. Napenda niseme mimi kama Mbunge wa Jimbo la Nkenge kwamba ranchi ndiyo imevamia vijiji. Sasa hatuwezi kuruhusu mambo ya namna hii hatuwezi kuruhusu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mtu wa mwisho kupokea mambo ya namna hii. Nikisema hivi, wako wengine walitaka kunipima sitaki kuwataja kwa sababu ukishakuwa Mbunge, Mbunge unasimamia Serikali, wako waliojaribu kunipima, kuna bwana mmoja alinipa barua akasema nenda uwaambie wananchi wako waondoke. Nilimjibu nikasema Mheshimiwa kwa nafasi yako huwezi kuniagiza, mimi naisimamia Serikali na wewe ni sehemu ya Serikali sasa lazima kila mtu aheshimu nafasi yake. Ukiwa Mkuu wa Mkoa, ukiwa sijui nani wewe fanya kazi yako na mimi acha nifanye kazi yangu. Hilo nililisema na naendelea kulisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mtu wa mwisho kuwaambia wananchi waondoke kwenye maeneo yao ambayo wana haki ya kukaa, na mimi nikiwa hapa natamka wananchi wangu katika maeneo yao wakae mpaka hapo nitakaposema kwamba sasa Serikali imeleta taarifa Bungeni na taarifa hiyo nimeikubali, vinginevyo wanapoteza muda wao bure hizo barua wanazoandika wanapoteza muda wao bure na hii vita niko tayari kuisimamia, niko tayari kupambana ndani ya Bunge, nje ya Bunge na kokote kule watakaponipeleka nipo tayari na nitafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nisema kwamba mipaka ya ranchi na Misenyi na vijiji inaeleweka, mwaka 1968 ranchi hiyo ilipokuwa inaanzishwa, walioanzisha ranchi hiyo walienda wakakutana na wananchi na wananchi hao baadhi yao bado wapo wanaendelea kuishi. Walikubaliana kwamba mipaka ya ranchi itakuwa Mto Kiboroga pamoja na Mto Kyakakuru. Mheshimiwa Waziri utakapotoa majibu hapa unieleze hii mipaka kwa nini hamuioni na kwa nini hamtaki kuitambua?

Mheshimiwa Spika, tulifanya operation kubwa ya kuondoa ng’ombe kwenye hifadhi za Serikali, ng’ombe wakaondolewa Biharamulo, jambo la kushangaza baada ya ng’ombe hao kuondolewa Biharamulo sasa wamepelekwa katika Ranchi ya Misenyi. Taarifa nilizonazo kwa mfano katika block No. 15 mwenye kitalu amepokea shilingi 50,000 kutoka kwa wachungaji wawili wenye ng’ombe 600, ukichukua shilingi 50,000 mara 600 unapata shilingi milioni 30. Hizo ni pesa kapokea tu kwa kuwapa ardhi ya vijiji watu wachungie. Nashangaa Waziri anaposema hana hela, hela unazo sema hutaki kuzikusanya.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba kuna vitalu kumi vimefanyiwa tathmini, lakini ukiangalia ramani hii niliyoionesha hapa wao walisemawana vitalu 22, kama una vitalu 22 kwa nini hivi vitalu vingine hutaki kufanyia tathmini unafanyia 10 tu? Hautaki kufanyia tathmini vitalu vyote kwa sababu taarifa zilizopo na nina uhakika hizi ni taarifa za kweli, mkitaka taarifa natoa hapa, ninayo taarifa hapa inaonesha katika Ranchi ya Misenyi katika zile blocks tuliowapa tukifikiri ni wawekezaji siyo wawekezaji ni wachungaji tu. Misenyi Ranch kumejaa ng’ombe za kutoka nchi jirani hakuna asiyejua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeenda kule nimeingia kwenye ranchi nilifanya ziara ya kushtukiza nimeingia mle kwanza ni rahisi kuingia kutambua kwa sababu ng’ombe wote wa Ranchi ya Misenyi wanajulikana. Nilipoingia mle nikakuta kuna ng’ombe wengi tu ambao ni aina ya Ankole. Ranchi ya Misenyi haina ng’ombe aina ya Ankole, wale ng’ombe wote na ushahidi ninao nilipiga picha na hizo picha nimezihifadhi kwenye sehemu mbalimbali na zingine nimeziweka sehemu zingine ili zisiweze kuibiwa, kwa hiyo mtu yeyote asije akaniteka akafikiri akiniteka hizo picha atazipata, hutazipata kwa sababu zimehifadhiwa pengine na watu wana password.

Mheshimiwa Spika, ng’ombe wale cha kushangaza wala hawajapigwa chapa, sasa viongozi wakuu wa nchi wameagiza ngo’mbe wote wapigwe chapa lakini kule Ranchi ya Misenyi ng’ombe wamo, kwanza siyo wa Misenyi Ranch, lakini wanakula kwenye majosho ya Misenyi Ranch wanalindwa, nani anawalinda hao? Lakini kwa mwananchi mmoja tu akijaribu tu ng’ombe wake kuingia kwenye ranch anakamatwa anatozwa faini 50,000.

Mheshimiwa Spika, nasema wazi kabisa hapa, hakuna mwananchi wangu katika Jimbo la Nkenge katika Kata ya Kakunyu na maeneo yote atakayetoka kwenye ardhi hata kwa inch moja hadi hapo nitakaposema. Vita hii nipo tayari kuisimamia, ninazungumza mimi, Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala na katika hili nitaweka Ubalozi kidogo pembeni ili nifanye vizuri kwa sababu kuna rafiki yangu alikuwa ananiambia Mheshimiwa toka umekuwa Balozi umebadilika. Ndiyo nimebadilika kidogo lakini Balozi ni yule yule na Kamala ni yule yule na utaalam ni ule ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa wavuvi wa Kashenye, nazungukwa na Ziwa Victoria, wale wavuvi siku moja nilienda kule nilitaka niangalie wanapata samaki kiasi gani, nikakaa kwenye mwalo pale wakaenda kule, vijana walivyokuja hawakurudi na samaki. Nikauliza vipi samaki wapo wapi? Wakasema Mheshimiwa unajua kwa nini tulete samaki wetu hapa tukishawapata huko kwenye maji tunaenda kuwauza Uganda kwa sababu Uganda kodi zao kimsingi ziko chini, lakini tukikanyaga upande wa Tanzania kodi nyingi mnoo lakini tukiwa tunakuja hivi, kuna operation juu ya operation, kwa hiyo tunaona ni bora tukishapata samaki wetu twende tuuze Uganda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Balozi kwa kweli kama bado una muda wa kukaa hapa, kaa uendelee kusubiri hautaona samaki wowote. Kwa hiyo, nikapiga salute nikawashukuru nikaondoka. Hivyo Mheshimiwa Mpina hizi kampeni unazozifanya hebu ziangalie zisije zikatuletea matatizo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nasema siungi mkono hoja hadi hapo nitakapopata majibu ya kina kuhusu hoja nilizozitoa hapa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii muhimu ya kuchangia bajeti muhimu iliyo mbele yetu; bajeti ya kujenga Tanzania ya Viwanda. Kwa kweli ukiiangalia bajeti, ukiisoma utaona kwamba sasa tumeanza kupaa kuelekea Tanzania ya Viwanda kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa kwenye bajeti, kila mtu anapotazama bajeti, mwingine atapendelea kuona ni fedha kiasi gani zimetengwa na zinaenda wapi? Kwa mchumi atapendelea kuangalia Sera za Kikodi zinasemaje na zinaweza kusaidia nchi namna gani? Hilo ndilo jambo kubwa sana kwenye bajeti. Ndiyo maana nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake kwa bajeti nzuri ambayo imewasilishwa na ukiisoma kwa kina na viambatisho vyake, ni bajeti nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tu nitoe angalizo kidogo tu, hasa kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, awaambie watalaam wake kila jambo linalowasilishwa hapa Bungeni tunasoma kila nukta nakila koma; na mtu mwingine anaweza akasoma kitu kidogo akakitumia kuonesha kwamba bajeti haiko sawa, kumbe ni makosa tu kidogo labda ya Wasaidizi wameshindwa kuweka mambo sawa.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano tu, halafu naomba Mheshimiwa Waziri awaelekeze Watalaam wake na Wasaidizi wake wawe kila jambo linaloletwa ndani ya Bunge hili wahakikishe liko sawa. Vinginevyo linaweza likawa jambo dogo halafu mtu akaanza kushughulika na hilo ikaonekana bajeti yote haina kitu, kumbe ni uzembe wa mtu mmoja kwenye dawati fulani. Huu ni mfano tu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ukisoma kitabu cha Mipango kinaeleza vizuri tu kwamba akiba ya fedha za kigeni, tuna fedha za miezi mitano (5.4). Ukisoma kitabu kingine hiki cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2017, hawa wanatuonesha tuna fedha ya miezi sita. Sasa sita na 5.4 ni vitu viwili tofauti. Sasa makosa madogo madogo kama haya yakikutana na wenzetu wa upande wa pili kule, wanaweza wakashughulika nayo ikaonekana ni jambo kubwa kumbe ni uzembe kidogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bajeti ni nzuri na nisingependa kupoteza muda kwa vitu vidogo vidogo kama hivyo. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tujikite kwenye mambo ya msingi na namwomba Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wawambie Wasaidizi wao wawe wanaangalia vitu hivi visije vikatupotezea muda bila sababu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia kuhusu PPP (Public Private Partnership), naona ni jambo muhimu sana hili. Ni jambo muhimu sana kwa sababu ukiangalia changamoto tuliyonayo, kilio tulichonacho ni kwamba fedha za maendeleo haziendi kwa wingi kama tulivyotarajia, lakini ukiangalia na shughuli za maendeleo tulizonazo, mahitaji ya maendeleo tuliyonayo nayo ni makubwa; tunaingia kwenye Rufiji, tunahitaji fedha nyingi, standard gauge tunahitaji fedha nyingi.

Mheshimiwa Spika, miradi hii kama tungejipanga vizuri, tunaweza tukatafuta fedha kutokana na vyanzo vingine na kwa hiyo, tukatoa unafuu mkubwa sana kwenye bajeti kujikita kwenye shughuli nyingine za maendeleo na shughuli nyingine. Nadhani ni eneo la kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ili tulifanye, tunayo Sheria ya Public Private Partnership. Sheria ile ukiisoma inatoa vivutio lakini haivutii sana wawekezaji kupenda kuingia kwenye Public Private Partnership. Katika Bunge hili tutakuwa tumefanya jambo kubwa kama sheria hiyo Mheshimiwa Waziri akiona inafaa, ikaletwa tukajaribu kuongeza vivutio vitakavyotusaidia kuhimiza watu kuingia kwenye Public Private Partnership. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tulifanye hili, kwa sababu tusipofanya hivyo, tutajikuta miaka mitano inaisha, Watanzania wanaendelea kulalamika kwamba hawaoni fedha kwenye mifuko, tutajikuta tunaendelea kuwa na miradi mikubwa, ambapo utekelezaji wake ni gharama. Kwa kweli mtu akiangalia kwenye mfuko kama fedha haioni, hata uelezee uchumi vipi Mheshimiwa Mpango itakuwia ngumu sana kueleza. Maana watu wanaangalia je, akipeleka mkono kwenye mifuko kuna kitu?

Mheshimiwa Spika, nakumbuka kwa mara ya kwanza nilipogombea Ubunge katika hotuba ya kwanza nikaeleza sera za uchumi zilivyo, mfumuko wa bei na kadhalika. Baadaye kuna Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi moja pale, akaja akasema, kijana unaongea vizuri mambo ya uchumi haya, lakini mbona hatukuelewi? Unazungumza vizuri, mfumuko wa bei na kadhalika, lakini mbona hatuelewi Mheshimiwa?

Mheshimiwa Spika, Katibu wa Chama wa Wilaya yangu Mzee Kamaleki, akaniambia, Mheshimiwa Kamala, unajua kule ulikuwa unafundisha, sasa huku umerudi kwa watu. Sasa unachofundisha darasani na kwa watu, lazima viendane. Nikamwuliza, tunafanyaje? Akasema, wewe subiri nikuoneshe, angalia ninavyoomba kura, mimi Mheshimiwa Kamaleki Masikini Lufufu nisikilize vizuri, kwa style hii ukifanya kama ninavyofanya mimi, watu watakuelewa. Kwa hiyo, taratibu nikabadilika. Kwa hiyo, nikajua kuna kile kilicho kwenye vitabu, lakini kuna kile cha kutekeleza, ni vitu viwili tofauti kabisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango naomba aliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo PPP, nitaenda haraka. Kuna mifano mingi tu. Kwa mfano, ukienda Johannesburg pale, utakuta mradi mkubwa wa Gautrain unaounganisha Johannerburg na Pretoria wa train, wamejenga kwa PPP. Ukienda Marekani unafahamu Mheshimiwa, unaenda mara nyingi kule, New York pale utakuta daraja linalounganisha Manhattan na Queens wamejenga kwa PPP. Naomba Mheshimiwa Mpango waliangalie. Hii PPP, tuleteni ile sheria tuongeze vivutio itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka nilipokuwa Balozi kule Brussels, nilimpigia simu Mheshimiwa Mpango tukazungumza na aliniambia kwamba alikuwa na miradi ya kielelezo, tukazungumza. Nikamwambia nilikuwa nimeandaa mkutano mkubwa kule, bahati mbaya hakuweza kuja. Sasa bahati nzuri sasa ni Waziri wa Fedha, hiyo miradi najua bado anayo na bahati nzuri nami niko hapa, hebu alete miradi yake hapa na Mheshimiwa Spika atalifanyia utaratibu nitarudi tena Brussels niiuze sasa kama Mbunge. Haya yanawezekana; na ile miradi najua bado anayo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo miradi tukiifanyia kazi itatusaidia sana kupaa. Hatuhitaji kutumia shilingi, unahitaji tu utoe fedha kidogo, unipe per diem kidogo hapa, Mbunge anaenda first class, usisahau; haendi economy. Sasa Balozi huwezi kumweka economy. Tukienda hivyo, tutauza hii miradi na nchi itaenda. Ule mradi wa Mkulazi, tunazungumzia mambo ya Kitaifa. Pale Mkulazi kuna mashamba tu, kiwanda bado hawajaanza kujenga. Jana usiku nilikuwa nazungumza na Maafisa Magereza wako pale, wakasema Mheshimiwa pale Mkulazi bado hatujaanza kujenga, kuna store tu peke yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nimalizie kwa kuunga mkono kwa uamuzi wako kuhusu malighafi, kuhusu Crude Palm Oil, ile kodi ya 25% na 35% hatua alizochukua Mheshimiwa Waziri ni sahihi na naomba asiyumbe. Kwenye bajeti amesema kwa mwaka mmoja; isiwe kwa mwaka mmoja, iwe kwa miaka yote. Kwa sababu tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Yuko sahihi, aendelee kufanya hivyo hivyo, asiyumbe na wala asiogope, kwa sababu najua jambo hili lina changamoto nyingi, lakini asimame imara na sisi Wahesimiwa Wabunge tuko imara, tutasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nianze na kusema kwamba naunga mkono hoja lakini pia naomba nijikite kwenye changamoto ya kwanza ambayo Mheshimiwa Waziri ametueleza katika kitabu chake cha hotuba kwamba ndio changamoto kubwa ziko nyingine, lakini yenyewe ni ya kwanza ambayo ilichangia katika kutekeleza vizuri kama tulivyokusudia na changamoto yenyewe ni kwa sababu tuna wafanyabiashara walio kwenye sekta binafsi hawana sehemu maalum, hawatambuliki, kwa hiyo inakuwa ngumu kwa Serikali kukusanya kile ilichokusudia kukifanya. Kwa hiyo, ningependa kushauri mambo yafuatayo kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwanza, naishauri Serikali wakati umefika kwa kutumia Geographical Information System (GIS) katika kuwatambua wajasiliamali katika kukusanya kodi katika kujua nani amelipa na nani hajalipa. Ninaposema GIS sitaki sihitaji kusema maneno mengi kwa sababu ndio mfumo wa kisasa unaotumika, na habari nzuri hapa Tanzania wataalam wa kuandaa mifumo hii wapo na kuna kampuni moja ambayo imeandaa mfumo inaitwa Digital City Services Mheshimiwa Waziri utakuwa unafahamu kwa sababu nina uhakika wataalam wako wanajua kuhusu kampuni hii na kampuni hii imefanya kazi kule Njombe kuhusu property tax walipohamishia zile shughuli kwenda kule Wizarani hiyo project ikasinzia, lakini pia hivi sasa Manispaa ya Iringa ipo mbioni ku-adapt utaratibu huu kwa GIS. Sasa kama hili jambo lipo na linawezekana na mfumo huu ni mwepesi maana tunatumia simu tu, utaalam tuanao Mheshimiwa Waziri nashauri uangalie eneo hili na tuone jinsi gani tukatumia GIS katika kukabili changamoto hii.

Ushauri wa pili, Mheshimiwa Waziri unapoangalia wajasiriamali mfumo wetu wa kodi tatizo ninaloliona moja unavyomuangalia mama ntilie ndio hivyo hivyo unavyomwangalia mfanyabiashara mkubwa au kampuni kubwa kama TBL. Sasa unapokuwa na mfumo unaofanana katika ukusanyaji kodi huo huo unaupeleka kwa mfanyabiasha mkubwa kama TBL mfumo huo huo unaupeleka kwa majasiriamali mdogo, lazima utapata shida Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, ushauri wangu na wataalam wapo wa kusaidia katika hilo tuandae tailor made regime kwa ajili ya informal sector. Tukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri tutakuwa tumepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu ni kuhusu kodi katika economics nyepesi lazima iwe certain, lazima mtu awe anajua akiagiza bidhaa atalipa shilingi ngapi, sio baada ya kuagiza anapofika pale kuanza kulipa anakuta mambo yanabadilika, nasema hivyo kwa sababu tatizo kubwa tulionalo hapa ni kwamba unaweza kukaagiza vitu kwenye kontena lile lile, vitu kutoka sehemu ile ile, waagizaji tofauti lakini kila mtu anaambiwa kodi yake ya kulipa. Sasa hii sio sawa Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo lazima tuweke utaratibu ambao utakuwa certain ili mtu yeyote mfanyabiasha anapoenda Dubai, anapenda China anapoenda popote duniani awe anajua akija pale bandarini alipa shilingi ngapi na hilo lisibadilike badilike. (Makofi)

Kwa taarifa yako Mheshimiwa Waziri wapo wananyabiashara wengi wa Tanzania wamaamua kutumia bandari za nchi nyingine kwa kuogopa kwamba watakapofika pale kwenye bandari yetu wataambiwa bei ambazo ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa nne ni utararibu wetu, hili ni jambo la capacity building tusitarajie kukamua maziwa kutoka kwa mfugo kama unafunga ng’ombe huwezi kukawa unapanga kukamua maziwa mengi bila kumlisha ng’ombe huyo vizuri. Nasema hivyo kwa sababu hawa wajasiriamali wetu hawa watalipa kodi kama wataweza kuwazeshwa masuala mbalimbali mojawapo ni vitu vidogo tu kwa mfano tulikiwapa simple skills za accounting wakazijua, unaweza ukaanzisha programu ya accounting system nyepesi tu ya kufundisha tu hata unawezana ukatumia hata wanafunzi ukitoa elimu hiyo kwa wajasiriamali wetu watawea kutambua nini wafanye ili waweze kulipa kodi vizuri na Serikali inanufaika na utaratibu huo.

Jambo lingine ni elimu ya kodi, tatizo kubwa tunalolipata katika biashara hizi wafanyabiasha wadogo wadogo/wajasiriamali au wataalam wetu wa kodi anapoenda kwa mfanyabiasha huyo anaanza kumwambia hiki mbona hujafanya, hiki hujafanya, kile hujafanya, hiki hujafanya, kwa hiyo na huyo kwa kuwa hajui basi anaishia kukimbia mwingine anaishia kujificha au kulazika kulipa kodi kubwa ambayo siyo, hii ni kwa sababu kutokuwa na elimu hiyo. Sasa kwa kuwa muelekeo Watanzania wengi watakuwa wajasiliamali wakati umefika katika mitaala ya elimu ya msingi kuanza kutoa elimu ya kodi. Mheshimiwa wa Waziri wa Elimu atusaidie katika hili lakini Serikali ijipange tuone ni kwa namna gani vijana katika shule za msingi kuanzia kule wanaweza kuanza kupata elimu ya kodi ili wanapofika kwenye kujiajiri isije kuwa jambo jipya.

Ushauri wangu mwingine ambao napenda niutoe haraka haraka lazima tu-simplify system yetu ya kodi, iwe nyepesi, lakini pia ambapo ni jambo dogo ukiliangalia upokuja kwenye kulipa kodi kuna suala la kandaa returns, kuna suala la manunuzi na mauzo, mfanyabiasha wa mchele kwa mfano anayefanya biashara ya mchele anapoenda kununua mchele wake ananunua maeneo mbalimbali huko vijijini na mara nyingi hizi risiti zinakuwa hazipo. Lakini ukimuuliza ya mauzo risiti atakuwa nayo ya mauzo unapomuuliza risiti ya manunuzi hana tatizo linaanza, lakini kwa mfano ukaenda pale Mwenge ukakutana na wafanyabiasha wa vinyago yule mfanyabiasha wa vinyago ukimuuliza risiti za mauzo anaweza kuwa nazo, lakini ukimuuliza risiti za manunuzi ya kinyago kile mpaka kimefikia pale hana, tatizo linaanza.

Mheshimiwa Waziri uanglie ni kwa jinsi gani tunaweza tukasimplifyeneo hilo ili kuweze kuondoa huo utata ambao unasumbua. Lakini pia ukienda kule Kanda ya Ziwa bidhaa nyingi tunatumia za kutoka nchi za jirani hakuna Special Economic Processing Zone na shauri izingatiwe na nishauri poa kule Kajunguti ambapo tulilikuwa tujenge uwanja wa kimataifa wa ndege sasa hatujengi, lakini tuweke Export Processing Zone, tukifanya hivyo tunaweza tukatumia lile eneo vizuri na kuendelea kupiga hatua.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii muhimu kuchangia hoja tuliyonayo ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa, lakini pia na kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwa kueleza dhana moja; na niseme kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati. Kwa hiyo, hoja ambayo napenda kuanza nayo ni kwamba ukiangalia taarifa mbalimbali za Benki ya Dunia, ukaangalia taarifa mbalimbali zinazotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na taarifa mbalimbali ambazo tumepokea kwenye Kamati, zinabainisha kwamba uchumi wa Tanzania na baadhi ya nchi nyingine ndani ya Sub-Saharan Africa umekuwa ukikua kwa kasi kati ya chumi zinazokuwa kwa kasi. Ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachumi tunafahamu kwamba katika uchumi huwa jambo moja likiwa jema huwa inamaanisha usiangalie hilo tu, huenda kuna jambo lingine jema zaidi. Sasa hatari ya uchumi, ukijikuta sana kufurahia jambo ambalo unaona ni jema ukasahau kwamba kuna lingine ambalo ni jema zaidi, basi unaweza ukajikuta unaendelea kuwa pale pale unafurahia na hilo dogo ambalo unafikiri ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kazi ya Bunge ni kushauri. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali kwamba pamoja na ukweli kwamba uchumi wetu ni kati ya chumi zinazokua kwa kasi zaidi, lakini lazima tujue kwamba suala la uchumi kukua kwa kasi zaidi ni jambo moja, lakini kuna suala lingine uchumi huo una ukubwa kiasi gani? Kwa lugha nyepesi tunasema, the size of the economy matters more. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili ili tuelewane, nitalieleza vizuri. Ukiangalia uchumi wa Marekani kwa mfano, GDP yao size ni 22 trillion US Dollars. Ukiangalia Ubelgiji, nchi ambayo ni ndogo, ukubwa wake ni square kilometers 36,000; ukiangalia Tanzania, ukubwa wa nchi yetu ni karibu 945,000 square kilometers. Kwa hiyo, utaona Wabelgiji wao GDP yao ni 540 billion US Dollars. Tanzania tunajitahidi, lakini ni 60 billion US Dollars.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uchumi wa Ubelgiji ukikua hata kwa asilimia moja, maana yake kwao ni jambo kubwa. Uchumi wa Marekani hata ukikua kwa asilimia 0.5, maana yake hilo ni jambo kubwa. Kwa hiyo, hizi sifa za Benki ya Dunia na mashirika ya fedha duniani na wachumi wengi waliobobea wakikwambia wewe uchumi wako unakua kwa kasi na wewe ukafurahia ukapumzika, inawezekana ukawa haufikirii sawa sawa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachumi tuko ndani ya Bunge hili kushauri, ni lazima tuikumbushe Serikali kwamba ni vyema uchumi ukue vizuri, ni jambo jema, lakini kuna jambo lingine tunaweza tukafanya zaidi. Jambo hili ni lipi? Tuangalie size ya uchumi wetu, tuangalie radical changes zipi tunaweza tukafanya ili walau ku-double uchumi wetu. Tunasema, radical changes. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa kuna neno mara nyingi linaitwa continuous improvement. Mimi sio muumini wa continuous improvement kwa sababu mtu akikwambia uendelee kufanya continuous improvement, maana yake anakwambia uendelee kuonekana unaboresha kidogo kidogo lakini uendelee kukaa pale pale. Tunachohitaji ni kitu kinaitwa radical change. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa radical change mojawapo ambayo tumeanza kufanya ambayo nitaomba niipongeze Serikali, kwa mfano, kufanya maamuzi ya makusudi kabisa kwamba sasa tunataka tuwekeze kwenye Stiegler’s Gorge tuzalishe Megawati 2,100, huo uamuzi ni radical change. Hawa rafiki zetu wa Benki ya Dunia, hawatakaa wakupongeze. Hawa watu wa Mashirika ya Fedha Duniani hawatakaa wakupongeze. Hawa wataalam wetu, wachumi wazuri sana wa huko pengine, hawatakaa wakupongeze, kwa sababu wanajua unachokifanya ni radical change. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine ni standard gauge. Niseme tu, nilipata bahati wakati fulani kuwa Mwenyekiti wa Mawaziri wa Afrika Mashariki, sasa Wajapani tuliwapa kazi ya kutushauri kwamba je, hii standard gauge nchi za Afrika Mashariki tunaweza kufanya au tusifanye? Basi wakatoa fedha za kufanya utafiti ule; Wajapani hao, wakaja na utafiti wakasema, hizi nchi za Afrika Mashariki standard gauge ninyi bado sana. Mwendelee tu na hizo reli zenu mlizonazo msonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikamwuliza Mheshimiwa Rais, unajua ukiwa Waziri wa Afrika Mashariki au Mambo ya Nje, wewe siyo Waziri; Waziri ni Rais. Kwa hiyo, huwezi ukafanya jambo bila kumwuliza Rais wako. Nikamwuliza, tunaenda kufanya uamuzi, tufanyeje? Akaniambia msimamo wa Cabinet si unaujua? Nikasema ndiyo. Akasema, ni standard gauge, hao Wajapani wasiwadanganye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilipofika pale kwenye kikao nikatumia Uenyekiti wangu vibaya, nikamwita Waziri wa Kenya nikamwambia unajua ni standard gauge. Unasemaje? Bwana yule akasema Mheshimiwa, lakini standard gauge nadhani Wajapani hawa wametupa hela, wamefanya na utafiti; nikasema sikiliza, hiyo siyo sahihi, ni standard gauge. Kwa hiyo, tulipoingia kwenye kikao, nilichofanya, nikawapeleka haraka haraka, wala sikuhoji sana, nikapitisha uamuzi ukaja wa standard gauge. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda nichangie ni kuhusu matumizi ya fedha za maendeleo. Ukiangalia taarifa tuliyopokea ya fedha za maendeleo jinsi zinavyotolewa, ukisoma vizuri na ukawa mkweli, lazima ushauri kwamba utolewaji wa fedha za maendeleo zinavyotolewa hazitolewi sawa sawa. Kwa nini? Ukiangalia fedha za maendeleo, kwa mfano, Wizara ya Mambo ya Ndani imepata asilimia 202 ya kile kilichokusudiwa. Sasa ni jambo jema ukiipa asilimia 202, sitaki kuuliza wamefanya nini Mambo ya Ndani, lakini sasa unapoanza kuangalia sekta nyingine ambazo unaona ni muhimu, unaona fedha za maendeleo hatujawapa kama ambavyo tulitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Maliasili na Utalii hatujawapa hata shilingi moja za fedha ya maendeleo; siyo jambo jema hilo. Ukiangalia Wizara ya Afya tumewapa asilimia 14 peke yake, fedha za maendeleo; siyo jambo jema sana; ukiangalia Biashara na Viwanda tumewapa asilimia 6.96. Sasa kama tunajenga Tanzania ya Viwanda, mtu yeyote angetarajia sasa kwenye viwanda fedha ya maendeleo utapeleka nyingi. Siyo jambo jema pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia energy, Wizara ya Madini, tumewapa asilimia 10, siyo jambo jema pia; ukiangalia National Land Use Planning, kitu ambacho ni muhimu, tumewapa asilimia sifuri, siyo jambo jema. Sasa nafikiri kama Mbunge na kama mtu unakuwa mkweli, ni vizuri kuyasema haya. Hatujamaliza mwaka wa fedha, tuna miezi sita mingine inayokuja, basi tumshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha aangalie afanye itakavyowezekana ili hizi sekta muhimu ambazo hazijapata chochote basi ziongezewe zipewe fedha nyingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lugola nadhani yuko humu ndani, ni rafiki yangu ananifahamu, tumefanya wote kazi, hizi asilimia 202 ulizopewa, mimi nadhani zinatosha, hebu sasa tupeleke fedha kwenye sekta nyingine ili tuweze kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambali napenda nilichangie, ni muhimu sana. Ukisoma taarifa tulizopokea, kwenye ongezeko la mikopo, tunasema fedha za mikopo imeongezeka kwa asilimia 63 kwa sekta binafsi, kwenye madini imeongezeka kwa asilimia 9.8 na kwenye viwanda imeongezeka asilimia 4.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? Ukiangalia hii asilimia 63 iliyoongezeka kwenye mikopo binafsi, hii ni mikopo kwa sababu watu ni wafanyakazi wanapewa mikopo ile ya mishahara; na ukiangalia hawa siyo kwamba wanakwenda kuwekeza. Hii ni mikopo ya kujikimu. Sasa kama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii muhimu ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu. Naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kujielekeza katika eneo moja muhimu, nalo ni eneo la uwekezaji. Najielekeza katika eneo hili ili Tanzania tuweze kupiga hatua kuingia kati ya nchi zilizo katika uchumi wa kati kama walivyosema walionitangulia kwa vyovyote vile lazima tujitahidi tuhakikishe tunapanua uwekezaji, tunavutia wawekezaji wa ndani na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa makusudi wa kuanzisha Kitengo cha Uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ni jambo muhimu sana na nampongeza sana. Na siyo tu kwamba kahamasisha kitengo hicho Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini pia kateua Waziri wa kusimamia sekta hiyo. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huo. (Makofi)

Nimesoma kitabu kilichowasilishwa mbele yetu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikaona kwamba kutoka nje tumeweza kuhamasisha, kuvutia wawekezaji kwa ujumla wake kwa ndani na nje dola bilioni 1.84 lakini pia kwenye kitabu hiki kinatuonesha kwamba Tanzania tumeweza kuvutia kutoka nje kuja Tanzania uwekezaji wenye dola bilioni 1.18; kwa hiyo, kwa hesabu ya haraka haraka, nilipochukua ule uwekezaji kwa ujumla tuliohamasisha wa jumla wa ndani na nje 1.84 billion US dollars, nikaondoa dola bilioni 1.18 ambazo zimetoka nje, nikabaini kwamba ndani ya nchi tumeweza kuhamasisha uwekezaji 0.66 billion dollar.

Mheshimiwa Spika, sasa takwimu hazina maana kama hujazifanyia tafsiri. Tafsiri ya haraka haraka ni kwamba wawekezaji wa ndani bado hatujafanya kazi kubwa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa sababu ili Tanzania tuweze kupiga hatua lazima pia tuwe na wawekezaji wa ndani ya nchi. Sasa ili tuweze kuongeza wawekezaji wa ndani ya nchi kutoka dola bilioni 0.6 angalau tupande angalau ifike dola bilioni moja au dola bilioni mbili lazima tufanye kila kinachowezekana siyo kuhamasisha tu wawekezaji wanaotoka nje, lakini pia na wawekezaji wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa moja ambalo umelizungumza vizuri ni kuhusu kuangalia hivi vikwazo vilivyopo na tukavifanyia kazi. Sote tunafahamu kwamba kwa muda mrefu Serikali imefanyakazi nzuri kupitia Wizara ya Biashara kuandaa ile blue print. Blue print inaonesha ni changamoto zipi zipo, ni mambo yapi yapo yanatakiwa kufanywa, lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba ukiisoma ile blue print utagundua kwamba kuna mambo mengi yanahitaji kutungiwa sheria, kuna sheria nyingi zinahitaji kufanyiwa rationalization, sasa naomba kupitia kwako tuishauri Serikali ifanye kila linalowezekana ndani ya muda mfupi ituletee hapa Bungeni sheria zote zinazotakiwa kurekebishwa ili kuendana na blue print ambayo imeandaliwa vizuri na kwa muda mrefu ili hiyo blue print iweze kufanyakazi.

Mheshimiwa Spika, ili tuhamasishe vizuri ndani maana Tanzania kama Tanzania tunasema Tanzania ni gateway ya Afrika Mashariki, lakini nichukue nafasi hii nitangaze ndani ya Bunge hili wakati Tanzania ni gateway ya Afrika Mashariki, Wilaya ya Misenyi na Jimbo la Nkenge ni gateway ya Tanzania kwenda Afrika Mashariki.

Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji ambaye nimemualika tarehe 05 Julai, 2019 aje kuwa mgeni rasmi katika kongamano kubwa la kimataifa la kutangaza uwekezaji na amenikubalia namshukuru sana na nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ukisikia Mheshimiwa Waziri Angellah naomba kwenda Misenyi kufanya kazi hiyo umruhusu aje aifanye kwa sababu ni kazi muhimu sana katika kuvutia wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii nitoe jambo moja la tahadhari. Sote tunafahamu hali ya hewa si nzuri sana kwa sasa, katika maeneo mbalimbali hali ya mvua haikwenda kama tulivyotarajia lakini tuna National Food Reserve Agency taarifa tulizonazo na za uhakika wana tani kati ya 78,000 mpaka 100,000 za chakula tu. Kwa takwimu tulizopewa kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza vizuri tu kwamba Tanzania tumezalisha tani milioni 16, matumizi ni tani milioni 13, kwa hiyo, tumebakiza surplus tani milioni 3.32.

Mheshimiwa Spika, hali ya hewa isipokuwa nzuri kama ambavyo imeanza kuonekana maana yake tutakuwa na upungufu wa chakula ndani ya nchi. Kama itakuwa hivyo litakuwa jambo la hatari kama huyu National Food Reserve Agency ataendelea na mipango yake ya kuuza reserve kidogo ya chakula aliyonayo ili kuweza kupata fedha ya kuongeza reserve ya chakula. Kama una tani 78 kama reserve unataka uuze hicho ili upate fedha za kununua kingine ni changamoto. Nichukue nafasi hii kuomba Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ajaribu kuliangalia eneo hilo ili tuweze kujipanga vizuri kwa sababu ukishakuwa na matatizo ya chakula hata upange mambo yoyote yale hayawezi yakaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, niipongeze Serikali kwa sababu imetoa tangazo maeneo mbalimbali ya Ranchi za Taifa ambayo yalikuwa hayatumiki vizuri sasa yapate wawekezaji wapya, ni jambo jema. Hata hivyo, natahadharisha wale wawekezaji walio wengi wameshindwa kuwekeza kwa sababu ya migogoro mingi kutokana na ukweli kwamba ranchi hizo zilivamia vijiji na kwa hivyo mara kwa mara wawekezaji hao wamejikuta kwenye migogoro ya muda mrefu na migogoro hiyo haijaisha. Kwa hiyo, hata Serikali ikitangaza upya ikapata wawekezaji wapya bila kumaliza migogoro iliyopo yatakuwa yale yale. Kwa hiyo, nishauri tu kwa nia nzuri kwamba ile Kamati iliyoundwa ya Mheshimiwa Rais ifanye kazi yake na ihakikishe ranchi inabaki tu maeneo yake na vijiji vyetu waachiwe wananchi ili hizo ranchi mpya zitakazotangazwa zisianze na migoogoro.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ninayo mambo machache ambayo ningependa kuchangia naomba nianze kwa kusema naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kulichangia, sote tunafahamu kwamba hivi sasa tunajenga Tanzania ya viwanda lakini ili tuweze kujenga Tanzania ya viwanda kada muhimu sana inayoweza kutusaidia kujenga Tanzania ya viwanda ni vyuo vya ufundi (Technical Colleges) hivi sasa tunazo Technical Colleges nadhani tatu, tuna Arusha Technical College, tuna kule Mbeya halafu tuna Dar Technical.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri Mheshimiwa Waziri, aje na mpango wa makusudi na wa dharura ili tuanzishe vyuo vyote kama hivyo kwa ajili ya Kanda ya Kusini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi rafiki yangu hapa nyuma anasema Kanda ya Kati nilikuwa sijalipanga, naomba niongeze pia na Kanda ya Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri tukifanya hivyo tutaweza kujenga Tanzania ya viwanda kwa spidi kubwa zaidi. Uwezekano wa kufanya hivyo upo, na uwezekano wa kupata fedha za kutekeleza jambo hilo upo na Waheshimiwa Wabunge tupo hapo tutakushauri zaidi hizo fedha utazipata namna gani. Jambo muhimu ni kuja na mpango na huo mpango upate baraka za Bunge zima na tutafanya hivyo, tutaweza kujenga Tanzania ya viwanda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimeangalia bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kitu kimoja kilichokuja kwenye kichwa changu ni kwamba shule hizi za msingi na shule za sekondari ni shule ambazo zipo lakini hazina mwenyewe. Kwa sababu unakuta Wizara ya Elimu ndiyo inapanga sera na viwango na kila kitu, lakini inapokuja kwenye kugawa walimu, ukimwambia Mheshimiwa Waziri hapa, shule yangu fulani haina walimu, atakwambia hilo jambo linashughulikiwa na Wizara nyingine. Ukimwambia kuna tatizo la madarasa sehemu fulani, ataniambia jambo hilo linashughulikiwa na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nami naona hizi shule za msingi na sekondari zipo lakini hazina mwenyewe; na mwenyewe ni Wizara ya Elimu. Kwa hiyo, nashauri kwamba wakati umefika Serikali ifikirie kurejesha utaratibu wa zamani, mambo ya elimu yote yasimamiwe na Wizara ya Elimu ili ziwe na mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kuna shule moja inaitwa Shule ya Msingi Kajunguti, iko kilomita 10 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Misenye. Shule hii ina walimu wawili tu, walimu wote wawili hawakai pale. Hii shule haina mwenyewe, maana wakati fulani ilitolewa na KKKT, lakini ukiwauliza KKKT shule hii mlitoaje? Mlitoa nyaraka zinazosema mmeitoa? Wanasema hawakutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni shule ambayo haina mwenyewe. Sasa nikagundua kwamba siyo hiyo tu, ni shule zote za Tanzania zipo, lakini hazina mwenyewe na mwenyewe ni wewe, ndiyo maana nashauri leo hii utaratibu wa zamani urejeshwe ili kuweza kuweka sawa utaratibu wa elimu hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo nimekuwa nikisikia muda mrefu kwamba Waheshimiwa hawa walimu wanaofundisha kwenye shule za msingi, siku moja nilikuta Afisa Elimu mmoja wa Wilaya, aliita Walimu wa Shule za Msingi ofisini kwake, akawa anawakemea, anawatukana kama watoto wadogo. Nikaangalia nikasema aah, huyu Afisa Elimu, hawa walimu nao si wamesoma kama yeye! Unakuta kwamba akishakuwa Afisa Elimu anaona walimu kama watoto wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nilipojaribu kufuatilia zaidi nikakuta na lenyewe halina mwenyewe, kwa sababu mwisho wa siku kumbe wanaosimamia maadili ni watu wengine. Sasa hizi ni vurugu. Ndiyo maana nasema turejeshe ule utaratibu wa zamani na walimu tuwanyime kila kitu ambacho hatuwezi kuwapa, lakini tuwape heshima wanayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine niliseme, tuna uhaba wa walimu tunakubali, lakini uhaba huo wa walimu sawa, lakini wale wachache waliopo tuwagawe sawa. Haina sababu unasema kuna uhaba wa walimu lakini unakuta shule nyingi zina walimu 20, shule nyingie 10, shule nyingine ina wawili, shule nyingine ina mmoja tu, hii sio sawa sawa. Hao wachache waliopo tuwagawe sawa. Sasa hilo nitaliletea hoja maalum kuonyesha ni jinsi gani wale wachache waliopo tuwagawe sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho ningependa kuisisitiza, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyoifanya kule Jimboni kwangu kwa kukarabati Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Natambua mwanzoni fedha hazikutumika vizuri, baadaye alikuwa mkali akaelekeza kwa karibu, akafuatilia, sasa naona kazi imefanyika vizuri. Nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunisaidia na chuo hicho sasa kimekarabatiwa vizuri na mambo yanaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nirudie kusisitiza, turejee kwenye utaratibu wetu wa zamani wa kusimamia elimu. Tukiendelea kama tunavyoendelea sasa, hizi shule zote, sekondari na kila kitu zitakuwepo lakini zitakuwa hazina mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri, utakuta sehemu kubwa amejikita zaidi kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo vikubwa vikubwa lakini kitu ambacho ni cha msingi kabisa walimu, wanafunzi unatakiwa uwaandae tokea kule chini waliko. Sasa Mheshimiwa Waziri anasubiri waje mpaka huku juu, anawapokea kwenye vyuo vikuu na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kuna haja ya kulitafakari hili jambo na kuja na mpango mbadala wa kurejea kwenye utaratibu wetu wa zamani. Bila kufanya hivyo, tutaendelea kuwa tunafikiri tunaendelea mbele lakini kumbe tuko pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii muhimu ya kuchangia Wizara ya Maji. Naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, zipo hoja nyingi ambazo zinaendelea kutolewa, lakini leo ntajikita kwenye hoja mbili, hoja ya kwanza ntatoa sababu za kuwaondolea wasiwasi wale wanaofikiri kwamba tukiongeza shilingi 50 kwenye mafuta petroli na dizeli kwamba inaweza ikasababisha mfumuko wa bei kuongezeka. Na jambo la pili ntakalozungumzia kwa ufupi, ntazungumzia hoja inayohusiana na Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na hoja ya kwanza; wale ambao wanafikiri tukiongeza shilingi 50 kwenye lita ya mafuta ya dezeli au ya petroli itaongeza mfumuko wa bei, nataka nitoe sababu zifuatazo kuwaondolea wasiwasi kwamba hilo halitatokea. Sababu ya kwanza hii shilingi 100 au shilingi 50 ambayo tunataka iwe shilingi 100 sasa, hii kodi kitaalam tunaita specific sio Ad valorem, na mchumi yeyote duniani ukimuuliza atakwambia kama ni specific maana yake haibadilikibadiliki, kama thamani ya kitu fulani inapanda au kushuka kodi yenyewe haibadiliki.

Mheshimiwa Spika, sasa hii tunasema shilingi 100, hii shilingi 100 bei ya dunia huko ya mafuta ipande ishuke, bei ya mafuta hapa Tanzania ipande ishuke, hiyo haibadilishi hiyo shilingi mia. Kwa hiyo, ntapenda yule atakayekuja kusema itabadilika anieleze yeye uchumi anaousema alisomea wapi na anatumia reference ya wataalam gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, mfumuko wetu tunaouzungumza saa hizi ni wastani wa asilimia 3.1 mpaka Machi kwa takwimu za BOT, lakini BOT lengo lake ambalo wameliweka ni kwamba mfumuko wa bei usizidi asilimia tano, hilo ndilo lengo la BOT. Sasa kama lengo la BOT ambalo ndiyo lengo la Serikali pia ni asilimia tano tusivuke lakini saa hizi mfumuko wa bei ni asilimia 3.1, huu wasiwasi unatoka wapi wa kusema huu mfumuko wa bei utapanda. Ukipanda acha upande tu, sana sana ukipanda utaenda mpaka asilimia 3.5, itakwenda nne, hata ukifika tano uache tu ufike tano, kwani tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu ni kwamba ndani ya Afrika Mashariki tumekubaliana kitu kinaitwa convergence rate, tumlichokubaliana ndani ya Afrika Mashariki ni kwamba nchi zote za Afrika Mashariki zihakikishe mifumuko yao ya bei haizidi asilimia nane. Sasa kama hiyo ndiyo ya Afrika Mashariki tuliyokubaliana tusizidi asilimia nane, sisi tuko asilimia 3.1, huu wasiwasi unatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi kwa nini mfumuko wa bei unaweza ukapanda, unaweza ukapanda ama kwa sababu ya kuongezeka sana kwa aggregate demand au unaweza ukapanda kwa sababu ya cost push, gharama zinaongezeka, lakini hivi kama unasema unaweza ukapanda kwa aggregate demand ikapanda maana yake ni nini; maana yake ni kwamba watu wanakuwa na disposable income kubwa, watu wakiwa na disposable income kubwa kipato kikipanda sana wanaweza wakawa na nia ya kutumia sana.

Sasa unapoongeza kodi kwenye mafuta hauongezi disposable income bali unalenga kupunguza disposable income, sasa wasiwasi huu unatoa wapi kama uchumi hivyo ndivyo unavyotueleza na ndivyo ulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine, EWURA ni chombo ambacho kinafanya kazi nzuri. Mara kwa mara wamekuwa wakitoa takwimu na wanachapisha kwenye magazeti yote, na tunasoma tunaona, na mara nyingi saa nyingine kulingana na mwenendo wa bei duniani wanasema sasa cape itapanda wanaweka cape inapanda kidogo; saa nyingine shilingi 50, saa nyingine 100 saa nyingine inashuka, lakini siku zote EWURA walipopandisha hiyo mfumuko wa bei haukupanda kwa sababu mafuta yamepanda kwa shilingi 50 au shilingi 100. Hata waliposhusha mfumuko wa bei haukushuka kwa sababu wameshusha, kwa maana hiyo kuna vitu vingine vya kuangalia vinavyoweza kusababisha mfumuko wa bei upande au usishuke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine kwa nini nina uhakika haitatokea kama tunavyofikiri; mfumuko wetu wa bei takwimu zinaonesha unachangiwa zaidi na chakula. Sehemu kubwa tunayoangalia ni chakula, sasa kama takwimu tulizonazo kila siku tunaambiwa tuna surplus ya uzalishaji wa chakula ndani ya nchi, wasiwasi huo unatoka wapi tena ya kwamba gharama hizi zitapanda tukiongeza? Kwa sababu sehemu ya kuangalia kwa makini na kwa wasiwasi ni sehemu tu ya ule mfumuko wa chakula usije ukapanda.

Mheshimiwa Spika, wachumi huwa wanaangalia mambo kwa macho mengi, lakini naomba niwaambie sio siku zote kwamba mfumuko wa bei ni jambo baya, hata mfumuko wa bei ukipanda kidogo si jambo baya, na mfumuko wa bei kupanda kwenye uchumi unatakiwa. Tatizo ni watu waliosoma vitabu vile vinavyowafundisha tu kwamba mfumuko wa bei ni mbaya, si kweli, mfumuko wa bei na wenyewe unatakiwa kwenye uchumi kwa sababu ukiporomoka zaidi, ukiwa negative, ni tatizo pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliseme la mwisho; mfumuko wa bei pia unaangalia na interest rates. Kinachotakiwa siku zote mfumuko wa bei usiwe juu ya interest rates. Average ya interest Tanzania ni asilimia 8.3; sasa huu wasiwasi wa mfumuko wa bei unatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie tu kwa ufupi kuhusu Stiegler’s Gorge; ni mradi mzuri sana, lakini mnakumbuka tulikuwa tuna Sheria Na. 5 ya mwaka 1975 ambayo tuliifuta nadhani humu Bungeni kwa sababu tulifuta ile Sheria ya RUBADA, sasa Stiegler’s Gorge ni mradi mzuri na pale tutaweka trilioni 6.3.

Mheshimiwa Spika, ningeomba itungwe sheria ya kulinda mradi ule kwa sababu bila kuwa na sheria maalum ya kulinda ile Stiegler’s Gorge kwa maana ya kulinda chanzo cha maji, tusipokuwa makini tutawekeza hela nyingi halafu baada ya muda maji hayatakuwepo. Kuna sababu ya kuja na sheria maalum ya kulinda ule mradi, ya kulinda vyanzo vya maji. Hili jambo tunaweza tukafikiri si muhimu lakini nadhani lazima tuanze kufikiria sasa na lazima tuchunge sheria hiyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nina mambo machache ambayo napenda nichangie kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, natoa shukrani zangu za dhati kwa fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kukarabati Kituo cha Afya cha Bonazi, nashukuru sana. Mara nyingi huwa nasema mafanikio ni baba wa matatizo kwa sababu unapokarabati kituo cha afya kikawa bora maana yake kitavutia wagonjwa wengi zaidi kukitumia na maana yake ni kwamba kituo kikishakuwa bora zaidi kukitumia na ni kwamba kituo kikishakuwa bora zaidi kikavutia wagonjwa wengi zaidi maana yake unahitaji kuongeza bajeti ya madawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema mafanikio ni baba wa matatizo na huwezi ukaliepuka hilo kwa sababu ukiliepuka hatutaendelea. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Afya na TAMISEMI wafanye kila kinachowezekana kuongeza bajeti ya Kituo cha Afya cha Bunazi na hasa upande wa madawa ili tuweze kukabiliana na ongezeko la wagonjwa ambao sasa watatumia kituo hicho na wameanza kukitumia kwa sababu sasa operesheni pale zinaweza kufanyika na mambo mengine ambayo hapo kabla yalikuwa hayafikiriwi kufanyika pale sasa yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri iliyofanya kwa kujenga Kituo cha Afya cha kisasa Kabyire. Mheshimiwa Waziri niliwasilisha maombi maalum kwa ajili ya kituo hicho cha kisasa ambacho ni bora kuliko vituo vyote katika Mkoa wa Kagera, naweza nikasema, lakini changamoto kubwa ni bajeti, inabidi tutoe bajeti maalumu kwa ajili kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyofahamu Wilaya yetu ni mpya, hatuna Hospitali ya Wilaya, tunatumia Hospitali Teule. Tulishatenga eneo la kujenga Hospitali ya Wilaya, tunaomba sana Serikali ituweke katika awamu itakayofuata ili na sisi tuweze kujenga hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha hotuba Mheshimiwa Waziri ameonyesha fursa mbalimbali za Tanzania katika ununuaji wa madawa na sasa tunawakilisha nchi 15. Pia nampongeza amefuta tozo mbalimbali na ameeleza kwamba wameandaa mwongozo wa uwekezaji katika viwanda vya dawa. Nimejaribu kutafuta mwongozo huo sijauona lakini uzoefu wangu unanituma kwamba mwongozo kama unaeleza tu fursa zilizopo bila kueleza incentive za kisheria zitakazotolewa kwa wale watakaowekeza, bila kutoa ardhi, mimi niseme Halmashauri ya Misenyi tuko tayari kutoa heka 400 kwa ajili ya kujenga viwanda vya madawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge wa eneo hilo nikizungumza na Halmashauri ya Misenyi imezungumza, mje niwakabidhi eneo hilo ili muweke hiyo center ya madawa. Ukijenga center ya madawa Misenyi maana yake umejenga Afrika Mashariki kwa sababu utaenda Uganda, South Sudan, Rwanda, utaenda kokote kule. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuwakaribisha ili tufanye ujenzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake atenge fedha za kutosha za madawa, tunaita noncommunicable disease kwa sababu katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya mara nyingi bajeti zao ni ndogo, madawa ya presha na kadhalika wanakuwa hawana. Mara nyingi nimekutana na watu wengi wako Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wakifuatilia dawa hizo nikawa najiuliza kama ikishajulikana fulani anaumwa na yuko sehemu fulani na dawa anazotumia ni aina fulani na katika Hospitali ya Rufaa zipo, utaratibu ufanywe kuhakikisha dawa hizi zinapelekwa mpaka ngazi ya vijiji na vitongoji ili kuwasaidia wagonjwa hawa kupata dawa ambazo vituo vyetu au zahanati haviwezi kuwa nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilima mia moja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja iliyo mbele yetu. Naunga mkono hoja kwa sababu mbalimbali na nitazitaja chache. Hoja iliyo mbele yetu imeeleza vizuri katika paragraph ya kwanza kwamba tunatarajia kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano kwa sababu sasa tunamalizia huu tunaoutekeleza kwa sasa. Sasa kilichonivutia zaidi kuunga mkono hoja hii ni kwamba dhima inayotarajiwa katika mpango wa tatu utakaoandaliwa ambao inabidi sasa katika mapendekezo tunayoyapitisha leo tuanze sasa kuweka mambo ya msingi yatakayotusaidia kuwa na mpango mzuri wa miaka mitano mingine; na dhima hiyo inasema kama ilivyobainishwa katika paragraph ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza mauzo nje na uwezo wa ushindani Kikanda na Kimataifa. Hili ni jambo jema na dhima hiyo itatusaidia kwa sababu tunapokamilisha huu mpango wa miaka mitano ambao tulijielekeza katika kujenga Tanzania ya viwanda, sasa tukielekea sasa kuongeza mpango wa tatu ukijikita kwenye kuongeza mauzo nje na uwezo wa ushindani Kikanda na Kimataifa itakuwa ni jambo jema. Kuna mambo ya msingi ambayo itabidi yawepo kwenye mpango wetu wa mapendekezo sijayaona na ningependa Mheshimiwa Waziri baadaye angalie ni jinsi gani anaweza akachukua mapendekezo hayo nitakayoyapendekeza kuwa sehemu ya mpango wetu tutakaoupokea na kuupitisha katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ni muhimu sana kama tukitaka kujenga, kuongeza uwezo wa mauzo ya nje na kujenga ushindani lazima tuanze kwa kujenga ushindani wa ndani. Kwa nini ushindani wa ndani ni muhimu? Ni muhimu kwa sababu huwezi ukauza nje, huwezi ukajenga uwezo wa ushindani kama hujajenga uwezo mkubwa wa ushindani wa ndani, nitatumia mfano mmoja tu, mfano wa wine, uzalishaji wa wine; ukiangalia Sekta ya Wine kidunia kwa mfano ukiangalia Italy wao wanazalisha chupa za wine bilioni sita. Tanzania ukichukua kwa makadirio ya juu kabisa tunazalisha chupa za wine laki mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiwa unazalisha chupa za wine laki mbili, ukitaka kujenga uwezo wa ushindani kwamba tuwezeshe sasa wine yetu iweze kushindana hata ndani ya Afrika Mashariki, basi lazima tuanze kujenga ushindani wa ndani kwanza. Sasa kujenga ushindani wa ndani wa wine peke yake ukiangalia kwa mfano wine tulizonazo hapa Dodoma ukiangalia chupa sitataja aina ya wine na kampuni kwa sababu unaweza ukajikuta labda kampuni ukiitaja kwamba haifanyi vizuri inaweza isijisikie vizuri, kwa hiyo sitataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia hizi chupa utakuta kuna nyingine ina lebo ambayo ni water proof hapa hapa Dodoma, lakini utakuta wine nyingine ina lebo ambayo mvua ikinyesha hiyo lebo inaloana hapo hapo. Sasa namna hiyo, ukiangalia Sekta ya Wine tu kwa hapa Dodoma ni kwamba, ukisema unataka kusaidia wine iweze kushindana maana yake uangalie je unawezeshaje hii Sekta ya Wine kwa mfano, kuwawezesha kupata lebo ambazo zinaweza zikajenga ushindani, lakini kwa kuanzia lazima ujenge ushindani wa ndani wakishindana ndani ndiyo unaweza ukapata mtu wa kuweza kushindani nje kwenda kwenye soko la nje. Kwa hiyo huo ni mfano mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano mwingine mdogo, kuhusu soko la kahawa la ndani na soko la pamba la ndani, lazima tujenge ushindani wa ndani, kwa mfano, kwenye kahawa ushindani wa ndani maana yake ni nini? Lazima tuangalie katika mpango huu tunaokuja nao tuangalie nini tunaweza tukafanya kujenga ushindani wa ndani wa ununuzi wa mazao yetu, kushindana ndani. Kwa mfano, mkulima wa kahawa yeye anapenda akiuza kahawa yake apate fedha yake pale pale. Natambua kuna hii dhana kwamba hela itapitia kwenye akaunti, watu wafungue akaunti, lakini mkulima anaangalia, yeye kama anazalisha kilo 10 au 20, unapomwambia utalipwa kupitia benki anakushangaa kwa sababu anaona gharama ya kufuatilia hiyo hela ni kubwa kuliko kile ambacho atakuwa anakifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna uwezekano wa kuweka mazingira ya ushindani ndani. Kwa hiyo ili tufanye hivyo mkulima huyu angependa awezeshwe aweze kuzalisha kwa tija, akiweza kuzalisha kwa tija utaweza kujenga ushindani. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba katika mapendekezo haya sijaona vizuri inavyoweka mazingira ya kujenga ushindani wa ndani kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa nilizungumzie kwa haraka haraka ili kujenga ushindani tunahitaji mkulima kumwezesha kwa mfano, kupata viuatilifu. Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Wizara yake walitenga bilioni kumi nafahamu, lakini baada ya kutenga bilioni kumi LC ikafunguliwa pale BOT, Kampuni ya TFC ikapewa jukumu la kuagiza hiyo viuatilifu. Viuatilifu hivyo mpaka ninavyozungumza hivi sasa viko pale bandarini, bilioni kumi zimetoka lakini viuatilifu mpaka sasa hivi vinaozea bandarini na bilioni kumi zimetumika. Sasa mambo ya namna hiyo hayajengi ushindani, kwa nini? Kwa sababu hivyo viuatilifu vikitoka bandarini vimekuja havijatoka bandarini maana yake tunaendelea kumkwamishwa mkulima na hilo siyo lengo letu. Kwa hiyo Mheshimiwa labda atapokuwa anatoa ufafanuzi nitaomba atueleze hizo bilioni kumi alizotoa na mpaka sasa hivyo viuatilifu viko pale bandarini vimelala pale ni jitihada zipi ambazo amezichukua za makusudi, fedha alitoa lakini viuatilifu vinaozea pale bandarini mambo ya namna hiyo hayatusaidii kujenga ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuzungumzia kwa ufupi kwenye kujenga ushindani kuhusu kilimo. Natambua pale tuna Mkulazi one na Mkulazi two, lakini ukisoma kwenye mapitio ya utekelezaji kwenye vitabu alivyotupa Mheshimiwa Waziri, ukisoma pale huoni kama kuna kitu kinachoendelea kwenye Mkulazi one na Mkulazi two kuhusu uzalishaji wa miwa. Ukisoma pale unaambiwa ekari 3,500 zimelimwa na ekari 750 zimepandwa. Sasa unajiuliza kama umelima 3,500 umepanda 750 maana baada ya miezi sita na zile ulizolima zitakuwa zimeshaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi unapolima miwa halafu kiwanda hakijajengwa wala mitambo haijaja, baada ya miezi 12 miwa iko tayari kiwanda hakipo, maana yake hiyo miwa huwezi kuitumia tena. Ningeshauri kwa kweli Mheshimiwa Waziri umefika wakati Serikali ikajiondoa masuala ya kujenga viwanda badala yake iachie Private Sector. Hapa Tanzania tuna viwanda ambavyo vinafanya vizuri sana katika sukari sitaki kutaja ni kipi, lakini ni vizuri tungeiachia Private Sector ikafanya hivyo na hii Mifuko ya Hifadhi tuiachie iendelee na shughuli zake za mambo ya hifadhi, kwa sababu kwa kuendelea kuiambia Mifuko ya Hifadhi ifanye shughuli za uzalishaji wa miwa tunajenga mazingira ambayo hayana tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tunajenga Tanzania ya viwanda lazima tuweke mazingira mazuri ya kuwa na mikopo ya uhakika, natambua tunayo TIB lakini ukiiangalia unakuta kwamba hii Tanzania Investment Bank uwezo wake ni mdogo, lakini tunayo mabenki mengi huko ya nje ya nchi ambayo yako tayari kuja Tanzania kuwekeza. Nadhani katika Mpango huu wa Maendeleo ujao tungeweka vivutio vya kuwezesha kuvutia investment banks kuja hapa Tanzania kuwekeza na kwa kufanya hivyo tutasaidia kuweka mazingira mazuri ya kuendelea kujenga Tanzania ya viwanda na pia kujipanga vizuri katika kutekeleza ule mpango wa tatu tutakaouandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika taarifa tuliyopewa ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo uliopita, utaona kwamba tulitenga bilioni 123.9 kwa ajili ya kilimo, lakini zilizotoka ni bilioni 56.5 ambazo ni sawasawa na asilimia 45.46. Pamoja na kutenga fedha kidogo na tukatoa kidogo, lakini kilimo ndicho kimechangia kwa asilimia kubwa kwenye pato la Taifa, kimechangia asilimia 28.6. Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tukitenga fedha nyingi zaidi kwenye kilimo tunaweza tukapata matokeo makubwa zaidi na uchumi wa nchi unaweza ukanufaika zaidi, hiyo ndiyo maana yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hivyo ndivyo ilivyo, nimejaribu kusoma kwenye mapendekezo ya Mwongozo, sioni popote ambapo mapendekezo yametolewa moja kwa moja kuagiza sekta mbalimbali, kuagiza Idara mbalimbali, kuagiza halmashauri zetu ili kutenga fedha za kutosha kuelekea kwenye kilimo, sioni ikijitokeza moja kwa moja. Kwa hiyo katika mpango wetu lingekuwa ni jambo jema kama jambo hilo lingeangaliwa na likajitokeza moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ningependa niongelee kabla muda wangu haujakwisha, tunayo East Africa Master Railway Network natambua kwamba tunazungumza hii SGR tunaendelea kuijenga ni jambo jema, natambua kwamba itatoka Isaka itaenda Kigari, lakini ningeshauri ikifika maeneo ya Runzewe au Biharamulo i-branch pale ielekee Kagera, ikifika Kagera ielekee Kampala, ikifika Kampala ielekee South Sudan. Tukifanya hivyo tutakuwa tumejenga uchumi nzuri kwa nchi yetu, pia tutawezesha hata Mkoa wa Kagera kuuandaa kushiriki katika uchumi shindani na kuongeza mauzo yetu ya nje ya nchi na tufikie hata viwanda vyetu mbalimbali vilivyo katika Mkoa wa Kagera viweze kuibuka na kufanya vizuri zaidi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii muhimu ya kuchangia taarifa mbili tulizonazo mbele yetu; taarifa ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.

Katika Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii katika ukurasa wa 44, Kamati imeshauri vizuri, kwamba kuna haja ya kuweka mikakati ya maksudi ya kuhakikisha tunakabili changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya na sekta ya elimu. Ushauri wa Kamati ni mzuri na mapendeklezo ya Kamati ni mazuri. Hii inadhihirisha maeneo mbalimbali kila mtu kwenye eneo lake atakubaliana nami kwamba Kamati inaposema kuna changamoto ya Wataalam katika sekta ya afya na elimu ni kweli, kwa mfano; kwangu kule Wilaya ya Misenyi tuna upungufu wa Walimu katika shule za msingi, upungufu wa Walimu 750; hiyo ni Wilaya moja; na ukienda kila Wilaya tatizo linafanana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia lazima niipongeze Serikali; kwasababu tulikuwa na tatizo pia la upungufu wa walimu upande wa walimu wa sekondari, Tanzania nzima tulikuwa na upungufu mkubwa.Ambacho kimetokea kwa sasa ni kwamba tuna upungufu wa walimu tu wa masomo ya sayansi na hisabati, lakini sasa tuna walimu wa kutosha kwa masomo ya sanaa, wapo wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo ndiyo maana nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya kuondoa tatizo la upungufu wa Walimuy wa sanaa. Naungana na Kamati kama ilivyoshauri kwamba mikakati itafutwe ya kukabiliana na tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niikumbushe Serikali na niiombe Serikali kwamba kwa kuwa mmeweza kuondoa tatizo la upungufu w Walimu wa sanaa, mbinu mlizotumia hizo hizo mzihamishie kwenye kuondoa upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati; nadhani tukifanmya hivyo tutaweza kupiga hatua kwa kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimekuwa nikijiuliza, unakuta maeneo mengi hawa tunaowaita walimu wa sanaa, ukitembelea shule zetu hizi ukaenda ukazungumza utakuta wale walimu wa sanaa wengine watakwambia hapa hatuna mwalimu wa hisabati, hatuna mwalimu wa sayansi; sasa unauliza, kwamba wanafunzi hawafundishwi? Wanasema a‟ a! hawa walimu wengine hawa wa sanaa tunawaomba wanasaidia saidia kufundisha. kuna shule moja ambayo niliambiwa walimu wa sanaa wanaombwa, wanasidia kufundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana walikuwa wana A za hesabu, A za fizikia na A za masomo mengine ya sayansi. Maana yake ni kwamba walimu hawa ambao tunaowaita ni walimu wa sanaa kama wakiweza kuongezewa utaalam kidogo wanaweza pia wakawa walimu wazuri wa masomo ya sayansi. Kwahiyo, naungana na Kamati kama ilivyoshauri kwamba Serikali ifikirie nini kifanyike basi kimojawapo cha kufikiria ni jinsi gani wanaweza wakaandaa mafunzo maalum kwa hao walimu waliopo ili waweze kuwa walimu wa masomo ya hisabati na sayansi wakati tunaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nizungumzie pia suala la wagonjwa wa msamaha. Ni kweli kama ilivyoeleza Taarifa ya Kamati, ni kwamba unakuta akina mama wajawazito, wazee wasiojiweza na watoto wa chini ya miaka mitano wanakuwa ni wengi sana wanpokwenda hospitali; na kwa kuwa sera yetu iko wazi hospitali zinawajibika kuwahudumia hawa. Zikiwahudumia unakuta ndani ya muda mfupi fedha yote iliyotengwa imekwisha. Sasa nilikuwa nafikiria, kwamba kwa kuwa tunayo hoja ya kuanzisha ile bima ya afya kwa wote, basi hiyo sheria itakapoletwa pia izingatie umuhimu wa kutoa bima maalum kwa haya makundi ambayo tulishasema kwamba yapate huduma. Mimi nadhani tukifanya hivyo tutaweza kupata ufumbuzi wa kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika ukurasa wa 53 Kamati imeshauri kwamba ni vizuri Serikali iwekeze na kuboresha vyuo vya ufundi nchini ili viweze kuzalisha mafundi wa kutosha watakjaosaidia katika kuendesha viwanda. Nakubaliana na Kamati kwa mapendekezo hayo, ni mazuri; na nipnde kuchukua nafasi hii kuishukuru Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo imewekeza vya kutosha. Kule kwangu kwa kweli sina cha kulalamika, wamewekeza zaidi ya milioni 700 kwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi-Gera.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa napita pale rafiki yangu mmoja akasema hicho ni Chuo Kikuu kipya, nikasema hiki si Chuo Kikuu, hiki ni Chuo cha Maendeleo ya Wannachi; na nashukuru sana na serikali imefanya hivyo maeneo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatizo tulilonalo maeneo mengi vyuo hivi havitumiwi vizuri. Ukivitembelea vyuo hivi maeneo mengi unakuta hatuvitumii vizuri. Kwahiyo nitoe wito kwa wenzangu Waheshimiwa Wabunge tuliopo hapa kwamba vyuo hivi tuvitumie vizuri, kwasababu tukivitumia vizuri vitatusaidia kutoa mafunzo ya kuweza kupambana na ukosefu wa ajira, kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri pamoja na kuwaandaa na vijana ambao wanaweza wakatusaidia katika kuendesha hii Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna eneo moja ambalo ningependa kulizungumzia kidogo, ni upande wa mikopo ya elimu inayotolewa kwa ajili ya vijana wetu; tunatoa mikopo kwa vijana wanaosoma shahada mbalimbali, lakini kuna kada ambazo tumezisahau. Kwa mfano mimi najiuliza, tuna Chuo chetu cha IJA (Institute of Judicial Administration) kule Lushoto; vijana wanaosoma pale wanasoma mafunzo muhimu sana ya sheria kwa Diploma, Certificate na hawa tunawahitaji sana ili watusaidie lakini wao hawapewi mikopo.

Sasa mimi najiuliza, hivi, hawa tunawahitaji na tunafikiri kwamba watatusaidia katika kutoa haki ndani ya nchi lakini kwanini inapokuja kwenye mikopo tunasema hao wasipewe? Na kwamba wapewe wa Degree peke yake? Mimi nadhani wakati umefika wa kuangalia ni kwa jinsi gani tunaweza tukapanua wigo ili vijna wengi zaidi waweze kupata mikopo ya kuwasaidia kupata elimu kila mtu kadri ya hatua ambayo anasoma. Kwa sababu kusoma Certificate au Diploma siyo dhambi wkamba usimpe mkopo kwasababu anasoma Kada ndogo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umekwisha au bado kidogo?

NAIBU SPIKA: Umekwisha Mheshimiwa, umeshamaliza dakika zako ahsante sana.

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii muhimu iliyo mbele yetu, ni bajeti muhimu sana kwa sababu ndio roho ya uchumi wa nchi, inasimamia roho ya uchumi wa nchi.

Kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja, lakini ninayo mambo machache ambayo ningependa nishauri, ili Wizara iweze kuyazingatia na Serikali iweze kuyazingatia.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukurasa wa 10 Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri kwamba uchumi wa Taifa au pato la Taifa limekua kwa asilimia saba, ni jambo jema na ninampongeza kwa kazi hiyo, lakini alipoanza kubainisha sekta ambazo zimekua kwa kasi; sekta ya kwanza ambayo ameonesha kwenye kitabu, nitatumia yaliyoandikwa tu kwenye kitabu, ya kwanza amesema ni sanaa na burudani imechangia kwa asilimia 13.7. Nikasema hilo ni jambo jema, sanaa na burudani. Sekta iliyofuata ni ujenzi asilimia 12.9, sekta iliyofuata ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 11.8 na sekta nyingine aliyoitaja ni habari na mawasiliano asilimia 9.1.

Mheshimiwa Spika, sasa nilipofika hapo nikastuka kidogo nikasema sasa kilimo vipi, mbona wala hakitajwi hapa? Maana ukiona uchumi sasa sanaa na burudani ndio inachangia kwa kasi, ndio imekua kwa kasi, ni jambo jema, lakini lazima ujiulize kilimo vipi?

Mheshimiwa Spika, sasa kilimo baada ya kuangalia kwenye nyaraka nyingine ni kwamba chenyewe kimekua kwa asilimia 5.3. Sasa kwa nchi yetu hii ambayo wananchi wengi ni wakulima na sehemu kubwa kwa kweli ya Watanzania ni wakulima, ukiona kilimo hakikui vizuri basi ujue hata ukienda kwa wananchi kuwaelezea kwamba uchumi unakua wao watashangaa kwa sababu sio sehemu ya kukua huko. Ndio maana namuomba Mheshimiwa Waziri akija wakati wa kufafanua atualeze kidogo walao na wakulima wasikie na wao wamekua kwa kiasi gani, walau wawe na matumaini kwamba sasa Serikali kuna mambo inayafanya yatakayosaidia na kilimo na chenyewe kukua. Wasanii na burudani barabara, lakini huenda ni kwa sababu tu si kwamba wasanii wamefanya mambo mengi ila kwa sababu sekta zilizo muhimu hazijakua kwa hiyo na zilizokua palepale zinaweza kuonekana kwamba sasa zenyewe ndio zinakua kwa kasi, hilo jambo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia ni mfumuko wa bei. Ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri kinatueleza vizuri kwamba mfumuko wa bei ni asilimia 3.2. Ni jambo jema, nampongeza kwa hatua hiyo, lakini mimi nikajiuliza, nikaangalia huu mfumuko wa bei unachangiwa na nini hasa kutokua, kwa nini tunafanya vizuri?

Mheshimiwa Spika, nikagundua tunafanya vizuri sasa tuwapongeze wakulima kwa sababu mfumuko wa wakulima wa chakula wenyewe umekua tu kwa asilimia 3.2 na ni kwa sababu wakulima wetu hawa wanaweza kuzalisha chakula kwa wingi na cha uhakika na ndio maana wanalinda mfumuko wetu wa bei. Kwa hiyo, lazima tuwapongeze wakulima wetu hawa, lakini nikajaribu kujiuliza sasa ni wapi ambapo sasa huyu Mheshimiwa Waziri ambaye mfumuko wake wa bei unaendelea kuwa mdogo kwa sababu tu wakulima wana mazao, bei hazipandi za mazao ya wakulima kwa sababu tuna sera ambazo zinahakikisha wakulima hawa wanalipwa kidogo.

Sasa kama tuna sera zinazohakikisha wakulima hawa wanalipwa kidogo ili mfumuko wa bei usipande ukaharibu vitu vingine, je, wakulima hawa tunawapelekea ruzuku maalum kiasi gani ya kuwawezesha kunufaika na mfumuko wa wa bei unaoendelea kwa kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana mtu akikutendea jamo jema basi na yeye lazima umpe fadhila na fadhila ya kwanza kabisa ka mkulima ni ruzuku ya mbolea, lakini sioni. Nimejaribu kupitia sana labda kwenye sekta, labda tutaona badae, sijaona ruzuku ya mbolea tunayopeleka kwenye kilimo, sijaona mkakati maalum. Nchi nyingine duniani zinakuwa na mfumuko kidogo wa mazao ya kilimo, lakini kwa mfano kule Ubelgiji wakulima wanaambiwa kwamba bwana tunakuomba wewe usizalishe eneo lako na kwa kuwa hautazalisha sisi tunajua ungezalisha ungeweza kuzalisha maziwa mengi, kwa hiyo, kwa mwaka huu tunakulipa pesa hii ya maziwa ambayo ungezalisha, lakini wewe pumzika usizalishe, ili kulinda bei ya mazao, lakini sasa sioni mikakati ya makusudi ya namna hiyo, ndio maana nashauri Waziri wa Fedha aanze kuangalia ni kwa namna gani huu mfumuko wa bei ambao unakuwa wa chini na anayechangia sana ni mkulima na kwa sababu anazalisha kwa wingi, kwa nini tusimfikirie huyu mkulima kumwezesha, kumsaidia?

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni uhimilivu wa Deni la Taifa; ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri ametuambia deni la Taifa limepanda kutoka trilioni 49.86 mpaka trilioni 51.03 na akatueleza vizuri tu akasema hiyo ni sawasawa na kupanda kwa asilimia 2.35. Sasa na mimi nikasema ngoja na mimi nijifanye nisiyejua hesabu, nijifanye sijui hesabu na sijui hesabu ngumu ngumu; nikasema kama kwa mwaka mmoja Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 3.5 je, kwa miaka mitano deni hili litaongezeka kwa asilimia ngapi? Hesabu zikaniambia litaongezeka kwa asilimia 17.2. Nikapata mstuko kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini namuomba sasa Mheshimiwa Waziri akija baadae anihakikishie kwamba Mheshimiwa Kamala usiwe na wasiwasi, deni hili halitakuwa hivyo kama unavyofikiri, bali litakuwa kidogo. Akishaniambia hivyo, ajiandae kwa sababu nitamuuliza litakuwaje kidogo kwa sababu bado tunaendelea, Stiegler’s Gorge ndio tumeanza na fedha nyingi lazima ziende huko, lakini nitamueleza pia SGR ndio tumeanza na fedha nyingi lazima ziende huko na ametueleza yeye kwamba, fedha katika masoko ya nje, misaada ya wahisani imekua migumu migumu sana kwa hiyo, lazima tuendelee kutafuta fedha ndani na nje, nitamuuliza maswali hayo kwa hiyo, kukopa lazima kuendelee na kukopa si dhambi, cha msingi mnajipanga vipi kulipa na mkopo huo unautumia namna gani?

Mheshimiwa Spika, lakini mambo haya lazima tuyazungumze kwa sababu ndio kazi ya Mbunge. Kazi ya Mbunge ni kuzungumza, ni kutumia microphone na kushauri. Na lazima tushauri kwa msisitizo.

Kwa hiyo, lakini uhimilivu wa deni mwingine wanasema mauzo ya nje sasa tumeweza kufikia asilimia 157.3 hii tuko chini ya ukomo ambayo ni asilimia 240, lakini kwa hesabu ya haraka haraka ni kwamba asilimia 82 tu ndio zimebaki, hiyo maana yake hiyo. Nikaangalia na kutumia mapato ya ndani kulipa deni nikaona sasa ni asilimia 15 na ukomo ni asilimia 22 nikajua sasa kumbe tumebakiza asilimia sita. Kwa hiyo, hivi viashiria vya ukomo wa deni pamoja kwamba ni vizuri hapa, lazima tukubaliane kuna taa ya njano imeanza kuwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ukiwa unaendesha gari ukakutana na taa ya njano lazima kwanza ushike brake kidogo na kama gari lako ulikuwa hujakagua brake usiendeshe tu, uanze kukagua brake ziko namna gani, na kama mafuta yameanza kwisha ile taa ya mafuta ikiwaka basi simama kwenye kituo cha karibu ujaze mafuta ili uendelee na safari. Ukiyadharau haya ukasema gari halijasimama ukaendesha tu, utapata tatizo na uendeshaji wa gari wa style hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho naomba niseme niko kwenye Kamati ya Bajeti na ninakushukuru Mheshimiwa Spika ulinipeleka kwenye hiyo Kamati, nakushukuru sana, nimejifunza mambo mengi. Moja nililojifunza ni kwamba tunakusanya saa nyingine fedha ambazo tunajua hizi fedha hatukutakiwa kuzikusanya, tunasema tuta-refund, lakini hatu- refund.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye madini peke yake wanadai bilioni 600, ukienda kula TBL wanadai-refund bilioni nyingi tu, ukienda viwanda vya soda wanadai fedha. Sasa shida ya fedha ambazo humrudishii mtu na ulitakiwa umrudishie fedha yake unapokaanazo ni kwamba unakuwa umeshikilia mtaji. Unaposhikilia mtaji ni kwamba unakuwa umeshikilia ajira; unaposhikilia mtaji, unaposhikilia fedha za kampuni maana yake umeshikilia ajira za Watanzania. Huyu badala angeweza kuwa na mipango ya kuajiri zaidi inabidi asitishe ajira ili aweze kuendelea kiwanda chake kwenye …, kwa hiyo, nasema eneo hili ambako ni mabilioni ya fedha nyingi tu yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hakuna kinachoshindikana katika Bunge. Kama Serikali inaona zile fedha lazima aendelee kuzitumia basi ituletee hapa turekebishe sheria kwamba wasisubiri chochote fedha hizi sasa zinakuwa rasmi za Serikali na wajipange vizuri kwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Sehemu kubwa ya mpaka kati ya Tanzania na Uganda iko Wilaya ya Misenyi – Kagera. Kama unavyofahamu kuna mambo mengi yanayoendelea katika mpaka huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwe karibu zaidi na ifuatilie kila siku yanayoendelea kwenye mpaka huo kwa nia ya kuimarisha ulinzi, ujirani mwema na kuimarisha utangamano. Aidha, suala la ng’ombe wanaoletwa kutoka nchi jirani (Uganda) na kuja kula majani Tanzania inabidi liangaliwe kwa umakini na lidhibitiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo uwe kwamba ardhi ya Tanzania itumiwe na Watanzania tu na kwamba wanaoleta mifugo kutoka nchi jirani wadhibitiwe na watumie ardhi ya nchi zao. Jambo hili la kudhibiti mifugo kutoka nchi jirani litawezekana tu kama wale tunaowapa majukumu ya kulinda mipaka wakizingatia miongozo wanayopewa na kuzingatia maadili ya Tanzania. Aidha, usalama wa Watanzania wanaoishi maeneo ya mipakani na mali zao upewe kipaumbele pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate orodha ya wawekezaji wenye vitalu vya kufuga ng’ombe katika ranchi ya Misenyi. Nitashukuru sana nikipata orodha yao ikibainisha na uraia wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko taarifa kwamba wafugaji wengi wanaofuga ng’ombe Misenyi ranchi haijulikani wanakouza ng’ombe wao. Je, Serikali inazo taarifa kuhusiana na jambo hili? Kwa mwaka ng’ombe wangapi wanauzwa Misenyi ranchi na nani ni wanunuzi wakuu? Pia je, Serikali inatumia shilingi ngapi kupambana na magonjwa yanayosumbua ng’ombe katika ranchi ya Misenyi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa samaki Ziwa Victoria unazinufaisha sana nchi jirani isipokuwa Tanzania. Kwa upande wa Tanzania mfugaji wa samaki akitaka kufuga samaki Ziwa Victoria anatakiwa kufanya nini? Hapa Tanzania kwa hivi sasa tunao wafugaji wangapi wa samaki katika Ziwa Victoria? Je, kuna samaki ambao hivi sasa wamepotea au kutoendelea kupatikana katika Ziwa Victoria? Samaki hao kama wapo ni aina gani? Tanzania tuna mpango gani wa kuhakikisha chakula cha samaki cha viwandani kinapatikana kwa gharama nafuu na je Tanzania tuna viwanda vingapi vinavyozalisha chakula cha samaki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nibainishe kwamba naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nkenge kuna miradi ya maji ambayo tayari imepokea fedha zote za miradi husika ya maji lakini maji hayajapatikana. Miradi hiyo ni Mradi wa Maji wa Ruzinga, zimetumika zaidi ya shilingi milioni 400 na mradi wa maji wa Igurugati ambao umetumia zaidi ya shilingi milioni 300. Aidha, kuna miradi mingine ambayo nayo haitoi maji kama ilivyotarajiwa. Miradi hiyo ni miradi ya maji Kilimililite, Kakunyu, Kenyana na Kibeho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ifuatilie kwa karibu miradi tajwa na hasa mradi wa Maji wa Ruzinga na Mradi wa Maji wa Igurugati ulio katika Kata ya Bugandika. Pia mradi wa Maji wa Kakunyu nao umeshindwa kutoa maji. Miradi yote tayari ilipokea fedha ya Benki ya Dunia lakini maji hayajapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru nikipata maelezo ya kina kuhusiana na miradi niliyobainisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukumbushia ahadi za viongozi wakuu zifuatazo ambazo utekelezaji wake haujaanza Wilayani Misenyi, Jimbo la Nkenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya lami ya Katoma hadi Bukwali; barabara ya lami Kajai – Hospitali ya Magana (Hospitali Teule ya Wilaya); barabara ya lami ya Matukula hadi Minziro; barabara ya lami ya Kituo cha Afya Kabyaile hadi Gera; kilometa tatu za lami Makao Makuu ya Wilaya – Bunazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu Serikali ilisimamisha shughuli za maendeleo katika eneo la Kajunguti. Baada ya Serikali kufanya maamuzi ya kutojenga tena Uwanja wa Ndege – Kajunguti ni dhahiri wananchi walioacha kuendeleza maeneo yao ya Kajunguti watakuwa wamepata hasara kubwa. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwapa chochote wananchi kufidia hasara waliyoipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naomba kutoa mchango katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vyuo vikuu vyote duniani huwa na kazi tatu ambazo ni training, research na consultancy. Research grants hutolewa kwenye vyuo vikuu kwa kuzingatia ubora wa research zinazofanyika na publications kwenye Four Stars Journal. Utaratibu huu huhamasisha vyuo kufanya tafiti bora na kuchapisha makala mbalimbali kwenye journals za Kimataifa. Nashauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutumia utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya zilizo nyingi hapa nchini kuna upungufu mkubwa wa walimu katika shule za msingi na sekondari pia katika Wilaya ya Misenyi tuna upungufu wa walimu 750 katika shule za msingi. Pamoja na utaratibu huu mkubwa, utaratibu unaotumika kugawa walimu wachache wanaopatikana hauko sawa. Kwa mfano, mwaka 2014 katika Wilaya tatu Mkoani Kagera zilizopangiwa zaidi ya walimu 700 kila Wilaya huku Wilaya nyingine zikipangiwa chini ya walimu 10, jambo hili siyo zuri lazima uwekwe utaratibu mzuri wa kugawa vizuri walimu katika shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la wakaguzi kutotembelea shule za msingi. Kwa mfano, shule ya msingi Kajunguti iliyo Wilaya ya Misenyi kwa muda mrefu Wakaguzi hawajatembelea shule hiyo. Aidha, shule hiyo ina walimu wanne tu na walimu hao hawakai kwenye kata hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera kina changamoto nyingi. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Elimu alitembelea Chuo hicho na kutoa maelekezo mbalimbali ya kusaidia kuboresha ukarabati wa chuo hicho pamoja na maelekezo hayo mazuri hakuna utekelezaji wowote uliofanyika hasa kuhusiana na VETA kutakiwa kutumia fedha zao kukarabati baadhi ya majengo ya chuo hicho, baada ya VETA kutumia vibaya milioni 100 kukarabati baadhi ya majengo chini ya kiwango. Naomba Wizara ifuatilie suala hili kwa karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, katika Wilaya ya Missenyi, Kata ya Kakunyu nimepokea malalamiko mengi ya baadhi ya watu kupewa PI - Persona non grata na kutakiwa kuondoka ndani ya saa 24.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anipatie orodha ya majina ya Utaifa wa watu waliokuwa wanakaa Kata ya Kakunyu na wakapewa ‘PI’. Katika mikutano yangu ya hadhara katika Kata ya Kakunyu nilipokea malalamiko mengi, pia ya baadhi ya wananchi kukamatwa usiku nyumbani kwao na kupigwa viboko na kulazimishwa wakubali kwamba wao si Watanzania. Naomba Mheshimiwa Waziri afafanue kama vitendo vya kukamatwa watu usiku na kuwapiga viboko ndiyo utaratibu mpya wa kuwatambua Watanzania na wasiokuwa Watanzania hasa katika Kata ya Kakunyu, Wilayani Misenyi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Katika Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi tuna ahadi tano muhimu za viongozi wetu ambazo zilitolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano achukue hatua za haraka kutekeleza ahadi hizo. Ahadi hizo ni pamoja na:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, kuongeza kasi ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Katoma hadi Bukwali. Barabara hii ni muhimu sana na inaunganisha Tanzania na Uganda. Ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, pili, kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kajai hadi Hospitali Teule ya Wilaya ya Mugane. Ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Spika, tatu, barabara ya Mutukula hadi Minziro, kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahadi hii ilitolewa na Mheshimiwa Rais alipozindua one boarder post ya Mutukula.

Mheshimiwa Spika, nne, barabara ya kutoka Kituo cha Afya cha Kabyaile hadi Gera. Ahadi hii ilitolewa na Mheshimiwa Rais alipotembelea Kituo cha Afya cha Kabyaile.

Mheshimiwa Spika, tano, ujenzi wa kiwango cha lami wa kilometa tatu za lami Makao Makuu ya Wilaya (Kyaka – Bunazi). Ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, chimbuko la hoja mbalimbali za kwamba fedha za Serikali zinatumika nyingi pasipokuwa na sababu, mara nyingi tumekuwa tukisikia viongozi mbalimbali wakisema huu ni mfano tu, kwamba pen ingweza kununuliwa shilingi 100 au 200, lakini kwa sababu ya Sheria ya Procurement tunalazimika kununua pen hiyo kwa shilingi 1000, 2000, 3000 au hata 10,000. Sasa chimbuko la tatizo hilo ni kifungu namba 50 na 56 kilichoanzisha Mamlaka ya GPSA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko yote haya tunayoyafanya kwa lengo la kuhakikisha tunaokoa fedha ya Serikali isitumike pasipokuwa ya lazima, bila kufanya marekebisho ya makusudi kuhusu utaratibu unaotumiwa na GPSA tutakuwa hatujafanya lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana wale wachache wanaofanikiwa kuingia kwenye GPSA; Taasisi mbalimbali na hasa kwa hizi items ambazo zinatumika kununua kwa utaratibu wa GPSA ni zile items zinazotumika kila siku, computer, masuala ya pen, uchapishaji na mambo mengine madogo madogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa GPSA inakuwa imeshaweka orodha kwamba hawa ndio wanahusika nchi nzima, na Taasisi kama iko Kagera ikijikuta kwamba kati ya wote waliobanishwa ndani ya orodha ya GPSA hakuna anayetoka eneo hilo, maana lazima watalazimika kufuata ile bei ambayo imewekwa na GPSA. Hili ni tatizo kubwa ambalo kama hatutaligusia katika mabadiliko haya huenda tukaendelea na matatizo kama tuliyokuwa tukiyazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia katika kifungu cha 4A(1) ambapo inasema; all public procurement and disposal by tender shall be, lakini neno by tender nashauri liondolewe kwa sababu njia ya manunuzi by tender ni njia mojawapo, zipo njia nyingine nyingi tu, ambazo sheria inazitambua. Zipo taratibu kama vile restricted system, shopping, single source, direct contracting, minor value sasa zote hizi zinatambulika. Ukisema by tender maana yake hizi nyingine zote zinazotambuliwa na sheria umeziweka pembeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo ningependa iangaliwe, ukienda katika kifungu cha 6(c) replace monitor and evaluate with advice with on performance, sheria inashauri tuweke maneno advice on performance na tuondoe monitor and evaluate katika kifungu 6(c).
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho ningependa kusema hapa ni kwamba hiki kifungu nashauri chote kifutwe, kwa sababu masuala ya advice and performance tayari sheria inatambua yako kwenye sheria na yanasimamiwa na PPRA. Sasa masuala ya advice and performance tayari tumeshaweka utaratibu mzuri wa kuyashughulikia na sheria inatambua kuwepo kwa PPRA; kwa hiyo tutakuwa tunarejesha kazi ambazo tayari tulishawapa PPRA zinarejeshwa kwenye taasisi zingine jamba ambalo litaleta mgongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ukurasa namba 3 wa Mheshimiwa Waziri alipokuwa akiwasilisha hoja ya mapendekezo, nikaangalia wadau wakubwa waliokutana na Wizara nikaona kuna TANESCO, TANROADS na taasisi zingine, lakini kwa masikitiko makubwa sikuona National Board of Materials Management watu ambao ndio muhimu, ndio wataalamu wanaotakiwa kuongoza katika masuala ya procurement. Sasa sijui ni kwa bahati mbaya Mheshimiwa Waziri alisahau au hawakuwa consulted au wao wenyewe walishindwa kutoa ushauri wao. Lakini sababu hiyo iliyosababisha hawa National Board of Materials Management wasio consulted, inapelekea wanaopanza kutaja sifa za Mkurugenzi Mkuu wa PPRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kifungu 23 kinataja sifa za Mkurugenzi Mkuu wa PPRA. Lazima tukubali katika dunia hii, kwa mfano mimi kama mchumi siwezi kuomba hata siku moja kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PPRA. Waliosomea mambo hayo watanishangaa na watanidharau.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hiki kifungu kinachopendekezwa kinasema mwanasheria, mchumi, mwanamuziki anaweza kuwa. Sasa hii sikubaliani nayo ushauri wangu ni kwamba lazima tuheshimu profession za wataalam. Tunayo Board ya Materials Managementi na wataalam walio bobea katika masuala ya procurement, basi ni vizuri sifa hizi hata tunapozitaja, tuanze kutaja. Hapa Tanzania tuna bodi nyingi, kwa mfano tuna Professional Board ya Madaktari, huwezi ukakuta kule mwanasheria eti ndio anakuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, ukienda kwa wakandarasi, utakuta kuwa Mwenyekiti wa hiyo Bodi au Mtendaji Mkuu lazima awe mkadarasi aliyesomea, ukienda kwa wahasibu kule, ili uweze ku-add ile professional body lazima uwe mtaalamu wa Uhasibu. Lakini unapokuja kwenye Materials Management inakuwa tofauti; naomba niseme tunalo tatizo katika nchi hii ambapo kila mtu anafikiri anaweza kufanya kazi za procurement hiyo siyo sawa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia haraka haraka kuna utaratibu wa kuweka lots unapo-advertise tender, kama tender ni bilioni 40, 50 ni vizuri kuweka lots ili upate watu wengi wanaoweza kufanya kazi hiyo na ifanyike kwa haraka. Najua hapa Tanzania kuna taasisi moja ilijaribu kufanya hivyo, tulipongeza kwa hatua hizo lakini tulikuwa tunapongeza hatua ambazo walifanya kwa ubunifu wa watu waliokuwepo wakati huo siyo utaratibu ambao sheria ilikuwa inaruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo ningependa nishauri ukienda kifungu kinachozungumzia suala la kwamba tender board ikutane mara moja kwa quarterly. Lakini Sheria ya Manunuzi ukiiangalia inaitaka Procurement Management Unit (PMU) wakutane kila mwezi na taarifa yao waiande kwaajili ya kuiwasilisha kwenye tender board na PMU lazima wakutane na wanashughuli nyingi za kufanya, lakini wakati huo huo tumeamua sasa kwamba tender board ikutane mara moja kwa miezi minne ili kubana matumizi. Maana yake ni kwamba ule urasimu tunaoukwepa tunarejea kwenye urasimu huo huo kwa sababu PMU itakaa kulingana sheria inavyotaka, lakini haitaweza ku-reporti kwenye tender board mpaka baada ya miezi minne ambapo sasa tender board ndipo inapokaa. Kwa hiyo tunaondoa urasimu mmoja, tunarejesha urasimu wa aina nyingine
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa hili ni la kisheria zaidi, nitaomba Serikali ilitizame tunawataja katika sheria hii kwamba kifungu cha 83, tunapendekeza kufungua kampuni itakayojihusisha na rushwa si chini ya miaka kumi; ukishasema itapewa adhabu si chini ya miaka kumi maana yake itategemea siku hiyo Hakimu ameamkaje, anaweza akatoa hata miaka 50, hata 100. Sasa hilo kwangu ni changamoto. Lakini pia nchi hii, tunazo sheria nyingine zinazoshughulikia masuala ya rushwa, juzi tumepitisha mabadiliko hapa, tumeanzisha na mahakama ya kushughulikia masuala ya uhujumu uchumi. Kama kuna sheria nyingine zinazoshughulika na masuala ya rushwa kwa nini basi tusiache sheria hizo zikafanya kazi kuliko kufanya mabadiliko hapa, ambayo tunampa Hakimu uamuzi ambao ni pendulous box huwezi kujua anachukua hatua zipi? Lakini kwa sisi ambao siyo wanasheria tunajua kwamba pale inapotokea kuna sheria iliyotungwa awali inashughulikia jambo hilo hilo; unapokuwa unatunga sheria mpya lazima uhakikishe sheria hiyo unayotunga isigongane na zile sheria nyingine ambazo tayari zipo. Mimi nadhani wanasheria wanalielewa hili na wataweza kulifanya kazi kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, la mwisho kabisa ni dogo tu, ukiangalia corruption mult-practice ni ipi kuna sehemu wametoa definition hawakuweka comma wamesema giving receiving sasa nimejaribu kutafuta kwenye dictionary zote za kiingereza nini maana ya giving receiving nimekuta hana maana, kwa hiyo ninashauri koma iongezwe pale, giving ni jambo moja na receiving ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu muhimu ulio mbele yetu. Ni Muswada muhimu kwa sababu bajeti tuliyopitisha na miongozo mingine inayoendana na hiyo bajeti, utekelezaji wake utategemea nguvu za kisheria za sheria ambayo tutaipitisha leo na ambayo naiunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini gazeti la Citizen la leo limeandika habari ambayo sitatumia muda mrefu kuisoma. Kuna wakati nilishazungumza hapa Bungeni kwamba suala la mitumba linapoelekea litatuletea changamoto kubwa. Kwa sababu kuna petition imepitishwa kule Amerika ambayo sasa inalenga kuzuia biashara kati ya nchi za Afrika Mashariki na Amerika na kuondoa kabisa nchi za Rwanda, Tanzania na Uganda na nchi nyinginezo katika list ya AGOA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jambo kubwa hilo, kwa sababu tunapojenga Tanzania ya viwanda na yote mengine tuliyopitisha, tunapoondolewa kwenye orodha ya AGOA maana yake sasa kutakuwa na mtikisiko lakini hata bajeti yetu ambayo tulitarajia kuna baadhi ya kodi tutakusanya, hatutazikusanya. Kwa hiyo, ni jambo ambalo nitaomba wahusika walitazame na waone ni hatua zipi zinaweza zikachukuliwa na kama kuna lolote tunaweza tukafanya, basi tulifanye ili kuweka mambo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda nilisema na hili ni la jumla, mwaka 2007 nchi za Afrika Mashariki tulikubaliana kwamba bajeti ya nchi za Afrika Mashariki itasomwa siku moja na wakati wa kuisoma ni uleule. Lengo ni kwamba tulipooanza kutekeleza Customs Union asilimia kubwa ya maamuzi ya kibajeti yanafanyika katika vikao vya Afrika Mashariki. Maana yake ni kwamba muda mwingi tunaoutumia hapa tunazungumza kodi zile tu ambazo tunakuwa hatuamui sisi wenyewe na zilizo nyingi zinaamuliwa katika ngazi ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikubaliana iwe siku moja, lakini kinachoendelea kutokea hivi sasa ni kwamba baadhi ya nchi zinaamua kusoma bajeti zinavyotaka. Nyote mnafahamu na mnatambua kwamba bajeti ya mwaka huu ni kwamba Rwanda, Uganda na Tanzania ndiyo pekee tulisoma kwa siku moja waliobaki hawakuweza kusoma kwa siku moja kwa sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lina implication kwenye masuala ya sera. Jambo hili lina implication kwamba mambo yote unayokuwa unayatoa kisera hapa ya kodi na hatua wengine wenye akili wanakuwa wameshajipanga kwenye magodauni yao ili kufanya mambo ambayo yata- sabotage kile ambacho unajipanga. Kwa hiyo, nimeona niliseme hilo kwa sababu lina implication kubwa kisera na kwenye utekelezaji wa bajeti siyo baadaye tunalaumia tu, haitekelezeki lakini kumbe kuna mambo ambayo tungeweza kuyajua na tukayafanyia kazi yangetusaidia kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho la jumla ni kwamba ukiisoma hii amendment, mimi siyo mwanasheria nitangaze hiyo interest siyo mtaalam wa sheria, nilipoitwa kusoma na nikapewa nafasi kabisa kwa bahati mbaya niliitwa sehemu nyingine na nikapewa offer kubwa zaidi kwa hiyo nikaachana na sheria. Nilipewa offer kubwa zaidi kwamba niende sehemu nisome digrii ya kwanza na nikimaliza pengine nisome ya pili na nisome ya tatu na nipate na ajira. Kwa hiyo, nikaamua kuachana na haya mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho nakisema na naomba wataalam wetu waandishi wa sheria watusaidie, ni la jumla hili tuone kama inawezekana, unaposoma hizi amendments zote kwa mfano amendment of section 63, huu ni mfano tu, inasema:-

“The Principal Act is amended in section 63 by- (a) deleting paraghaph (d)”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili kwa wanasheria waliobobea ni jambo jema kwao na kwa wale ambao wana ofisi zao Wabunge zenye nyaraka zote, maana ofisi ya Mbunge ni kwamba unakuwa na wasaidizi, unakuwa na nyaraka zote na kila kitu, kwa hiyo ukitaka kitu chochote unapata. Hata hivyo, sisi hapa sote hakuna mwenye ofisi hapa Dodoma na sote hapa hakuna ambaye anaweza akasema anajua hiyo Principal Act inasema nini, inabidi uende library utafute uiangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kushauri kwamba kama itawezekana wataalam wetu wa kuandika sheria pale wanapotaja kifungu kinachoondolewa wakitaje chote pale ili ninapopitisha hapa nijue kinachoondoka ni hiki na kinachowekwa ni hiki vinginevyo ni jambo gumu kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mtaalam wa sheria unajua kwamba inakuwa ngumu sana unapokuwa unapitisha amendment lakini unachopitisha hukijui. Ni kama unafanya mchezo tu lakini waliobobea wao wanajua na wenye nyaraka zote na wanaotunza hivi vitu wanakuwanavyo. Mwingine anaweza kusema nyie Wabunge mnakuwa wazembe, lakini hali halisi ndiyo hiyo, hivyo, inabidi tuangalie tuone tunafanyaje kurekebisha hali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia kwa haraka ni kwamba ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha kuna kitu kinaitwa stay of application. Stay of application unakuta mtu anaomba na tunakubaliana ndani ya Afrika Mashariki kwamba fulani anaruhusiwa asitekeleze jambo fulani, wanakubaliana kwamba fulani ameruhusiwa asitekeleze hili kwa muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kingine wataalam wanaita duty remission wanakwambia hiyo kodi uikusanye au kama huikusanyi itakusanywa baadaye irejeshwe. Hata hivyo, uzoefu umeonesha hata zile kodi zinazosemwa zitakusanywa, Waziri wa Fedha atakuwa anaelewa wala hawazikusanyi tena, ikishatoka imetoka, hazitakusanywa na wala hazitarejeshwa. Mambo haya ukiyatazama maana yake ni kwamba tuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunaelewa na Waziri wa Fedha anaelewa kuna kitu kinaitwa Uganda list ambapo Uganda tuliipa msamaha mkubwa sana wa kodi na matokeo yake ni kwamba kuna vitu vingi vinaingia Uganda na vinatakiwa viuzwe Uganda tu lakini vinaishia kuja hata Tanzania. Unapokuwa unafanya hivyo maana yake huku tunapoimba wimbo wa kujenga viwanda tutakuwa hatuwezi kuvijenga kwa sababu mtu atakwambia kuna vitu vya gharama nafuu vinakuja. Kwa hiyo, ni eneo la kuangalia, sijui tutafanyaje lakini ni eneo gumu sana ambalo nimeona niliseme hapa ili tuone tunajipanga namna gani, kwa sababu vinginevyo tutaishia kusema bajeti haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mmoja. Tunataka kujenga mtambo mzuri wa liquid gas cylinder, lakini wakati tunakubaliana kufanya hivi na hapa Tanzania kuna watu wameshawekeza wanazalisha hizi cylinder, kuna nchi moja sitaitaja kidiplomasia yenyewe imeamua kufuta asilimia 25 ya kodi imeweka zero. Maana yake yenyewe inataka hizi cylinder zisitoke ndani ya East Africa maana yake zisitoke Tanzania, maana yake initiative zetu za kuwezesha kuwa na viwanda ndani ya Tanzania hazitawezekana, sasa hii inaleta tabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye sekta ya chuma. Hapa Tanzania kuna viwanda vingi vimewekeza kwenye chuma lakini wakati tunasema ukitoa chuma kilichokuwa processed kutoka nje basi tulipe asilimia 10 na tumeeleza kwenye sera zetu za kodi lakini wengine wao wanasema ni sifuri. Wanaweka sifuri kwa sababu wana interest ya kuvitoa nje, wakivitoa nje wakaleta kwao maana yake viwanda vya chuma vilivyopo Tanzania havitaendelea, maana yake hata hiyo Mchuchuma tunayozungumza, hata hao wawekezaji hatutawapata. Haya ni mambo ambayo lazima tujiulize mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma yako mambo mengi hayaishii tu kwenye bidhaa za chuma yanaenda kwenye textile, ngozi, garments na vitu vingine vingi. Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa ambapo tusipoitazama, tukachukua juhudi za makusudi, basi hatutaweza kujenga uchumi wetu kama tunavyotarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia utalii ni jambo muhimu na tumechukua measures za kusaidia kuboresha utalii lakini nadhani katika bajeti ijayo pia tujipange kuchukua hatua kubwa zaidi. Kwa sababu ukiangalia hapa Tanzania tuna changamoto ya kuwa na taasisi nyingi zinazoshughulikia ku- regulate utalii. Wenzetu Kenya wao wameanza kuwa na taasisi moja tu inayoshughulika utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia tumetenga shilingi ngapi za kusaidia utalii, sioni ikijitokeza moja kwa moja lakini ukiangalia kwa wenzetu unakuta wao wametenga kwa mfano shilingi bilioni moja kwa ajili ya tourism recovery, wametenga pia shilingi bilioni nyingine moja kwa ajili ya kutunza yale masoko ya zamani yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja nilishangazwa na wataalam wetu wa utalii walikuja na mkakati wao wa kutangaza utalii pale Brussels nikauliza mbona Ubelgiji haimo? Wakasema hii haipo kwa sababu hapa utalii tulishaanza tunaenda sehemu mpya. Nikawaambia usiende tu sehemu mpya ukasahau ya zamani, ya zamani kama unayo mfano Uingereza, Ujerumani lazima uendelee kuwatunza, usiache tu ukakimbilia pengine. Haya nayasema tu kwa sababu pamoja na kwamba bajeti yetu tumeiweka vizuri, lakini najua lazima tujipange kuweka vizuri zaidi katika bajeti ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa muda ulionipa na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na naunga mkono mapendekezo ya Serikali ya kufuta RUBADA, kwa sababu kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 13 ni kwamba uendeshaji wa taasisi hiyo na uwepo wa taasisi hiyo unaongeza gharama zisizokuwa za lazima za uendeshaji wa Serikali kama ilivyoelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kama mnavyofahamu tulipopitisha bajeti hapa tulipitisha pamoja na mambo mengine, trilioni 9.2 kwa ajili ya mishahara peke yake. Sasa kama tunatumia trilioni 9.2 kwa ajili ya mishahara peke yake, maana yake sehemu kubwa ya bajeti inaelekezwa huko, maana yake sasa ukubwa wa Serikali umepanuka mno, ndiyo maana jitihada nyingi ambazo zimefanyika za kuondoa wafanyakazi hewa na mambo mengine, lakini bado tu tunajikuta tunahitaji trilioni 7.2 huenda ikaongezeka siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uamuzi huu wa Serikali wa kuondoa RUBADA kwa sababu taasisi nyingine zilizopo za Kiserikali zinaweza kufanya kazi hii iliyokuwa ikifanywa na RUBADA ni vizuri tukamulika na maeneo mengine. Kwa leo sitapenda kuyagusia hayo kwa sababu sote tunayafahamu. Kuna suala la utitiri wa taasisi zinazofanya mambo yanayofanana, kuna changamoto za masuala ya Wakala, yote haya yaangaliwe kwa upana wake ili tuone zile taasisi ambazo zipo lakini hazina tija basi tuziondoe na shughuli hizo ziweze kuendelea kufanywa na Serikali, tupunguze matumizi yasiyokuwa ya lazima. Kwa hiyo, naunga mkono uamuzi wa kuondoa RUBADA sina shaka shughuli hizo zitaweza kufanywa na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo tu ni kwamba, tunapoondoa RUBADA zile mali zilizokuwa chini ya RUBADA lazima tuwe makini ili isije ikawa RUBADA imeondoka na mali zikaondoka, kwa sababu kwenye transition ya kipi kilikuwa chini ya RUBADA sasa kitaenda wapi, tusipoangalia basi mambo mengi yanaweza yakaendelea hapo katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kuhusu kumpa uwezo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusu masuala ya kutoa misamaha hasa kwa miradi ambayo tunapata fedha ya wahisani na makubaliano kati ya Serikali yetu na wahisani mbalimbali. Ni jambo muhimu kwa sababu, unaposema mradi fulani ulipe kodi lakini fedha hizo ni za mradi ama tumepata sehemu ya fedha hizo kutoka kwa wahisani maana yake unawatoza walipa kodi wa ile nchi ambayo umepata fedha hizo kwa ajili ya miradi yako ya maendeleo, si jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uamuzi wa Serikali wa kuliona hilo ni jambo jema, tumerudi kwenye mstari. Kwa hiyo naunga mkono hoja hiyo kwa sababu itasaidia kuongeza moyo wa wahisani kutusaidia, lakini pia itapunguza gharama za miradi, pia itaharakisha utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo na tutaweza kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kama ilivyowasilishwa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia
mada iliyo mbele yetu, hii mada muhimu sana katika kuboresha Sheria ya Public Private Partnership ambayo ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa viwanda katika kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi, na katika kuweka mazingira mazuri kuwezesha Serikali kutumia rasilimali kidogo ilizonazo katika shughuli nyingine za sekta ya umma nakuachia sekta binafsi kujihusisha na masuala mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba tulitoa ombi wakati fulani hapa Bungeni, kwa kutaka tunapokuwa tuna-amend sheria fulani (Principal Act) ingekuwa vizuri Waheshimwia Wabunge tupatiwe nakala za hiyo sheria tunayo i-amend. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tusipofanya hivyo tunaweza kutumia muda mwingi hapa kushauri kumbe unaishauri Serikali kwa sheria ambayo siyo hiyo inayofanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti wewe kama Mwanasheria unafahamu kwamba sheria inapotungwa tunasema tuna Principal Act, lakini Principal Act hiyo inakuwa inapata mabadiliko ya mara kwa mara na kwa bahati mbaya mabadiliko haya yanapofanyika hayawi integrated kwenye hiyo Principal Act, hatari iliyopo ni kwamba tunaweza tukamtumia muda mwingi hapa unashauri, una-amend kumbe jambo unalo amend siyo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajua siyo hilo na wanasheria wengine wanajua lakini sisi tuliosomea general principal in law kusoma sheria kidogo ya kuwezesha kuongoza, tunajua kwamba watunga sheria ni chombo hiki. Sasa wale wataalam ambao ndiyo wanatunga sheria wanatakiwa wakati wote watushauri vizuri, wasitumie utaalam wao kutupoteza au wasitumie utaalam wao kututegea ili baadae tukitoka hapa tunafikiri tumetunga sheria kumbe hatujatunga lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na definition ya Public Private Partnership; ukisoma vitabu na makala mbalimbali kuhusu hiki kitu kinaitwa Public Private Partnership ni nini, wengine wanakwambia Private Partnership ni pale ambapo Private Sector inapowekeza kwa kushirikiana na Serikali. Walio wengi watakwambia siyo hiyo watakuambia PPP ni pale ambapo kunakuwepo na agreement kati ya private sector pamoja na public katika kufanya jambo fulani. Kama maana yake ndiyo hiyo basi, wale wanaofikiri kwamba sasa PPP maana yake ni kwamba private sector aje awekeze halafu na Serikali iwekeze kidogo tuweze kuendelea, unakuwa unafikiria kitu ambacho sicho. Kumbe PPP ni pale ambapo Serikali ina transfer risk ya ku–invest, risk ya ku-design, risk ya kusimamia project, risk ya ku-operate. Haya ni mambo mawili tofauti. Ndiyo maana nasema ni sheria ipi tunayoi- ammend? Ingekuwa vizuri tukawa na principle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipojaribu kuangalia sheria ambayo ni principle act ya PPP niliyoweza kupata inasema Public Private Partnership means investment through private sector participation in a project undertaken in this term, ndiyo definition waliyotoa. Lakini ukienda pengine ukiangalia inasema it is all about transfer of risk in terms of project design, project management, project operations. Sasa ndiyo maana nikasema ombi letu la Waheshimiwa Wabunge kupewa principle act tunayo-amend ni ipi na ni vizuri tukawa tunafanya hivyo, itatusaidia kushauri vizuri Serikali na kujua ni jambo gani tunafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nililotaka kushauri ni kwamba ukiangalia PPP ile format ambayo sasa inashauriwa kwamba itatumika itapunguza na ukiritimba tunaambiwa kwamba ukiangalia kwenye Taarifa ya Kamati imetuchorea mchoro pale, kiambatanisho namba moja inaonesha hatua kama moja, mbili, tatu, nne na tano. Ukiangalia hatua hizi zinazooneshwa hapa ni kwamba kuna hatua nyingine pale ambapo inatakiwa wakishamaliza kazi pale kwenye Kamati ya Uidhinishaji wa miradi ya ubia basi wapeleke kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nafikiri utaratibu mzuri tungefanya kama Uganda. Wao walichofanya, ile committee inayopitia miradi ya PPP na Attorney General ni Mjumbe wa Kamati ile, sasa Attorney General akishakuwa Mjumbe wa Kamati ile unapunguza urasimu usiokuwa wa lazima wa watu kufanya kazi chini ya Wizara ya Fedha halafu baadae wakimaliza kazi wapeleke kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili na wao waangalie. Niseme tu kwamba hakuna kuna ofisi yenye ukiritimba mzuri kama ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kurahisisha mambo haya, basi huyu Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe mjumbe kwenye Kamati inayoangalia hizi PPP. Wanapomaliza kazi pale pale Wizar aya Fedha hakuna tena sababu ya kusema sasa tunasubiri Mwanasheria Mkuu wa Serikali apitie ashauri kwa sababu tunakuwa tunapoteza muda bila ya kuwa na sababu yoyote ile na tunaongeza ukiritimba juu ya ukiritimba na bahati nzuri kwa utaratibu wa nchi yetu tunaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini pia tunae na Waziri wa Katiba na Sheria.

Sasa kwa kuwa tunaye Waziri wa Katiba na Sheria basi ni vizuri Mwanasheria Mkuu wa Serikali akafanya kazi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, asione tatizo kukaa na Makatibu Wakuu wenzake wakafanya kazi. Wakimaliza kazi pale wamemaliza tunapiga hatua tunakwenda mbele kuliko kujichelewesha sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kushauri kwenye muswada huu ukiangalia PPP modals zinazotumika kote duniani kuna aina tano. Aina ya kwanza inaitwa design, finance, build, operate and transfer. Hii ukiangalia nchi nyingi zaidi ya asilimia 9-0 ya miradi inayotekelezwa kuhusu PPP ni ile inayotekelezwa kwa utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina nyingine ni design, finance and operate. Hii ni asilimia 10 tu ukiangalia kwa ujumla wake ambayo inapitia utratibu huu na inatekelezwa. Kuna nyingine ya design, build, operate and transfer, hii ni asilimia mbili tu ya miradi yote, nazungumzia generally ya miradi yote ambayo inatekelezwa kwa utaratibu huo. Kuna nyingine wanaita equity partnership project, hii ni asilimia moja tu na nyingine wanaita facilities, management project na hii ni asilimia moja. Kwa maneno mengine, sheria yetu hii ingeweza kuwa na nguvu zaidi kama tungejikita zaidi katika kuwezesha utaratibu wa design, finance, build, operate and transfer kwa sababu ndiyo umeonekana kufanya kazi maeneo mengi waliyojaribu kutekeleza hii miradi ya PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu wa Uingereza, William Hague alikuwa mara nyingi anapenda kusema ukiamini katika kila kitu maana yake hauamini katika chochote. Sasa nasema hivyo kwa sababu ukiangalia ile Public Private Partnership Act ambayo tunasema ndiyo Principle Act, inataja ni miradi ipi ambayo inaweza ikaingizwa kwenye PPP lakini ukisoma ile sheria inataja miradi yote, miradi ya barabara…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. BALAZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa naomba nianze kwa kutoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa jinsi ambavyo alishiriki tarehe 19 kule Misenyi katika kuhitimisha kampeni kubwa dhidi ya UKIMWI pamoja na mimba za utotoni. Mheshimiwa Waziri uliyemtuma akuwakilishe, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Eva Maria, alifanya kazi nzuri, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Muswada huu, nimesoma ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho, The Tanzania Teachers Professional Board. Ukiangalia jina la Muswada unaona kwamba hili ni jambo kubwa lakini unapoenda sasa kwenye Muswada wenyewe kifungu hadi kifungu, unakuta umejikita zaidi katika kuangalia maadili ya mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu hapa ni kwamba, tumejaribu kumechukua neno professional likawa sawasawa na ethical. Huu Muswada ungekuwa mzuri sana kama tungeuita The Tanzania Teacher’s Ethical Board or whatever, unajikita zaidi kwenye ethical kwa sababu profession ya mwalimu kama taaluma, ina mambo mengi zaidi ya kuangalia maadili. Tunaangalia huyu mwalimu alisoma chuo gani, syllabus alizokuwa akisoma ni zipi na anafundisha namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo yote ukisoma Muswada huu huyaoni. Kama huyaoni, tafsiri yake ni nini? Maana yake kuna vyombo vingine vinavyoshughulikia mambo hayo. Kwa mfano, suala la kuajiri walimu hutalikuta kwenye Muswada huu. Maana yake kuna chombo kinachoshughulikia ajira za walimu. Ukisoma Muswada huu, hutaona moja kwa moja masuala yanayohusiana na ile taaluma yenyewe ya ualimu. Maana yake ni kwamba kuna chombo kingine kinachoshughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muswada ni mzuri tuupitishe kama ulivyo, lakini naishauri Serikali basi ijiandae kuleta Muswada mwingine utakaotusaidia kupunguza utitiri wa taasisi mbalimbali zinazosaidia sekta ya elimu. Nasema hivyo kwa sababu ukizungumza na mwalimu mmoja mmoja, walichokitaka kimsingi na maombi yao ya awali waliyowasilisha Serikalini, ilikuwa kuomba chombo kitakachosimamia masuala ya elimu yote, nadhani ndiyo yalikuwa maombi yao. Kwa sababu sisi kama Wabunge tunaongea nao hawa walimu na juzi juzi nilipata bahati walinialika, nikajifunza na mambo mengi ambayo nilikuwa siyajui. Napenda kusema, kwa sasa huu Muswada tuupitishe kwa sababu ni hatua, lakini Serikali ijiandae kushughulikia kile kilio cha walimu ambacho wamekua nacho muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye kifungu cha 43 kinaanzisha Committee of Inquiry. Ukiangalia sasa wajumbe ambao wanaingizwa kwenye Committee of Inquiry unakuta kuna wajumbe wawili registered teachers, professional hao; mjumbe mmoja kutoka public service; mjumbe mmoja kutoka TAMISEMI; na mjumbe mmoja senior lawyer. Ukingalia wote hawa, walimu wana vyama mbalimbali vinavyowawakilisha, huoni mwakilishi wao hata mmoja. Inapokuja kwenye principle of natural justice utakuta kwamba hawa ambao watakuwa wanakaa kujaribu kutatua matatizo mbalimbali, wanakosa yule mwakilishi anayewakilisha vyombo vyao. Sasa hili ni jambo ambalo kama lingeangaliwa lingeweza kutusaidia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba unaposema professional au skills za mwalimu, ufundishaji, hizi ziko dynamic hazipo static. Kwa hiyo, unapoamua kuzungumzia suala la professional ya ualimu, lazima uwe na mfumo ambao siyo tu unatoa leseni, unatoa leseni kwa mtu ambaye unajua ameandaliwa namna gani na ukishampa leseni, lazima umfuatilie huyo mtu anafundisha namna gani akiingia darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tulifundisha ingawa lazima nikiri kwamba mimi sikuwa mwalimu bali nilikuwa lecturer, lecturer siyo mwalimu, lakini ukiamua siku moja unaweza kuingia darasani ukaeleza jinsi ulivyosoma Uingereza, Japan dakika arobaini zikaisha, lakini umefundisha. Kuna Kitengo ambacho kinaitwa Udhibiti wa Ubora. Sasa hawa wadhibiti wa ubora ambao Mheshimiwa Waziri anawafahamu, ni watu muhimu sana, nami ningefurahi kama tunasema tunaanzisha chombo cha kusimamia ubora, basi wale wanaodhibiti ubora, wanaofanya kazi nzuri sana, wangeweza kuonekana kuwa sehemu ya Muswada huu jambo ambalo hatujalifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo moja ambalo ni muhimu. Ziko center za TRC. Center hizi ni muhimu sana kwa sababu zimekuwa zikisaidia kumfanya mwalimu awe mwalimu kweli, aendane na wakati na ajue kwamba ufundishaji unabadilika. Sasa hizi TRC zilizo nyingi Tanzania nzima zimesahaulika. Muswada huu ungetenda haki kama ungegusia jinsi ya kuboresha hizo Teachers Resource Center, (TRC) na kuzi-link jinsi ambavyo zitatusaidia kuongeza ubora wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Muswada huu kama ulivyo tuupitishe, lakini tuanzishe chombo ndani ya Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo hapa, tunayo changamoto kama nchi, gharama za uendeshaji Serikali zinaongezeka kila siku, lakini kila siku tunaanzisha vyombo vya namna hii. Kama kuna chombo ambacho kinaweza kufanya kazi hiyo, niwe mkweli, hakuna sababu ya kuanzisha chombo kingine. Majukumu yote haya tunayoyapa Bodi hii tungeweza kuyapeleka Tanzania Teacher’s Service Commission na yakafanywa vizuri kabisa bila kuanzisha chombo kingine na kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali. Tusipokuwa makini, siku moja tutakuta tuna vyombo vingi vinavyofanya kazi ile ile na hiyo haitatusaidia sana kupata kile tunachokitaka, lazima tutumie rasilimali kidogo kufanya mambo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii muhimu ya kuchangia Miswada miwili iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Muswada kuhusu Meteorological, ukiangalia kifungu cha 7 ambacho kinaanzisha Bodi, kinabainisha kwamba kutakuwa na wajumbe nane lakini ukiangalia kwa umakini unaona kwamba NEMC, taasisi ambayo inafanya kazi muhimu sana zinazoendana na shughuli za meteorological na kule Zanzibar tuna ZEMA, hatujatambua uwepo wa taasisi hizi mbili muhimu zinazofanya kazi muhimu kama ambayo itakuwa inafaywa na hii Mamlaka mpya. Kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu wa kutambua uwepo wa hizo taasisi mbili, lakini pia na kwenye bodi wawepo wawakilishi wawili mmoja atoke NEMC na mwingine atoke ZEMA ili kuingia kwenye taasisi hii. Jambo hilo likifanyika litasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Meteorological imeelezwa katika kifungu cha 11(1)(a) kwamba awe na Ph.D. Labda tu niseme sina tatizo la kusema mtu awe na Ph.D kwa sababu wengine tunazo mbili na nyingine wala hatuzifanyii kazi, hoja yangu hapa haya mawazo ya kufikiri kwamba mtu anapokuwa na Ph.D basi huyo ndiyo amebobea na ni mtaalam sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tungesema tu walau awe na Masters akishakuwa na Masters hata Masters sio lazima sana kimsingi degree ya kwanza ndio huwa inamtambulisha mtu ni mtaalamu wa kitu gani degree ya kwanza. Ndio maana hata Wanasheria wengi ambao wamebobea huwa hawahulizi Masters wala Ph.D wanaangalia degree ya kwanza. Sasa unapoangalia shughuli zote za hii Taasisi tunayounda Mamlaka unaposema Mkurugenzi Mkuu lazima awe na Ph.D maana yake kuna watu unawajua wana degree za kwanza au za pili ni wazuri lakini unajua hawana Ph.D kwa hiyo, unaiweka hapa Ph.D ili kuwa-exclude bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda katika schedule ya kwanza A inaeleza Wajumbe wa Bodi, wawe na degree ya kwanza inayotambulika sasa kama Wajumbe wa Bodi wale umewapa sifa ya kuwa na degree ya kwanza, inakuwaje sasa Mkurugenzi Mkuu pekee ndio unasema na yeye lazima awe na Ph.D wakati Mkurugenzi Mkuu huyo naye pia ni Mjumbe wa Bodi, kwa hiyo unakuwa una Sheria moja ile ile ambayo inajipinga yenyewe, huku inatambua kwamba huyu Mkurugenzi Mkuu, lazima awe na Ph.D huku inasema kwamba kwenye Bodi unapoangalia nani wenye Bodi na Mkurugenzi Mkuu yuko kwenye Bodi. Kwa hiyo Mheshimiwa nadhani tuweze tuka-harmonize nikiangalia eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia kuna kifungu cha 22 kinabainisha kwamba ukichukua takwimu hizi za kama unataka kufanya utafiti au unafanya assessment ya Miradi lazima takwimu hizo zitolewe na Meteorological ambayo ni jambo jema. Lakini tunasahau kwamba tunasheria inayoanzisha NBS (National Bureau of Statistics) ambayo tulishakubaliana hapa kwamba data zinazotolewa na ile Taasisi ndio official. Kwa hiyo, mtu kama anafanya assessment ya Mradi akitumia takwimu kutoka NBS kufanya assessment ya Mradi halafu baadaye ukawa na Sheria nyingine inayosema haitambui taarifa yoyote ile isipokuwa zitakazotoka Meteorological ni kwamba unakuwa unashindwa kutambua kwamba tayari kuna Taasisi iliyoanzishwa kwa kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi Wajumbe wa Kamati ya Bajeti tulitembelea NBS walituonesha kazi nzuri ambayo wameshaifanya katika utafutaji wa takwimu na takwimu zinazohusisha na masuala ya hali ya hewa, wenzetu wameshapiga hatua wanatumia satellite wanazo taarifa ambazo ni bora kuliko na hii Taasisi ambayo tunaianzisha leo hii. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tutambue kwamba NBS hapo tutambue ndio chombo ambacho kimehalarishwa kwamba kinapotolewa takwimu ndio takwimu halali kisheria sasa hata kama chombo kipya kinaanzishwa ni vizuri chombo hicho kitambue uwepo wa chombo kingine ambacho official ndicho kimeshakipa hayo mamlaka, tusipofanya hivyo tutaleta migongano ya Utendaji isiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii, ukiangalia Kifungu cha 42 kina jaribu kubainisha mtu akiruhusu watu kuingia kwenye eneo ambalo liko protected kwamba hili ni eneo liko protected kwa ajili ya kuweka Miundombinu ya masuala ya Meteological basi anaweza akatozwa faini kubwa. Nilikuwa najiuliza hapa hivi unatambuaje kwamba eneo hili liko protected na alama zipi zinawekwa kwenye eneo hilo kwamba liko protected kama huwezi ukajua maeneo yote yaliyo protected kama hata alama hazijawekwa basi utajikuta watu wanachukuliwa adhabu wanapewa adhabu kali kwa sababu tu ya kuonekana wamevunja sheria na kwa sababu tu ya kutojua, vinginevyo Sheria hii lazima iendane na kutambua hayo maeneo yabainishwe na alama ziwekwe ili watu wengine wasije wakajikuta wanapewa adhabu zisizokuwa za lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 46, kinasema ukitoa taarifa za hali ya hewa kwa kutumia redio kutumia, kutumia magazeti na nyinginezo unakuwa unavunja Sheria lazima utumie zile ambazo wanasema ni latest methodology. Lakini Sheria haitaji hizo latest Methodology ni zipi, ambazo maana sote tunaelewa hapa ukitoa taarifa kupitia redio ni jambo ambalo linajulikana ukitumia magazeti ni jambo ambalo linajulikana lakini unapokuwa na Sheria unasema usipotumia zile ambazo ziko official utachukuliwa hatua kali bila kuzitaja hizo ambazo zinaitwa official ni zipi tutakuwa tunauziwa mbuzi kwenye gunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri atakapokuwa ana-windup Mheshimiwa Waziri atueleze hizo anazosema ndizo zinatambulika na ndizo zitumike, ni zipi kwa sababu mode of communication tunazijua ziko za magazeti yapo, redio, televisheni zipo lakini unaposema atakayetumia hizo amevunja Sheria atumie zile zinazotambulika wakati hatujui hizo zinazotambulika ni zipi, kama mtunga Sheria hapo unakuwa sijaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Muswada wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini Muswada mzuri na nimeupenda sana kwa sababu ukiangalia pale sifa za Mkurugenzi za Mkuu wa Mamlaka hiyo, wanasema awe na Masters, Postgraduate pamoja na uzoefu wa miezi nane, nadhani hili ni jambo jema kabisa, na sifa hizi ndiyo zingepelekwa hata kwenye Mkurugenzi wa ile Mamlaka nyingine tunayoianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia Kifungu cha 7(1b) kinataja wajumbe wa bodi, mbali na wengine kinawataja wengine sita, mmoja anatoka ofisi AG ni jambo jema, lakini inataja wengine sifa zao inasema wale watano wengine, walau awe na Engineering, Management, Finance or Accounts imesahau professional muhimu sana kwenye haya mambo na Mchumi, Transport Economics haitambui kabisa hapa, ingawa inapoenda kwenye panel ya ku-review ndiyo inakumbuka Wataalamu wa Economics inawaweka kwenye panel review.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri hata kwenye Bodi akawemo Mchumi ili hata yule aliye kwenye panel review atakapopelekewa jambo basi jambo hilo, liwe kweli limepitia kwa wachumi katika hatua. Na jambo lingine tunaona representative kwenye hiyo Bodi sijaona TABOA, sijaona TATOA hizi ni Taasisi muhimu sana kwenye masuala ya usafiri na hawa watu wamekuwepo muda mrefu kabisa sasa unapoanzisha mamlaka kama hii, kwenye Bodi ukashindwa kuwatambua kwamba TATOA wapo ukashindwa kutambua kwamba TABOA wapo nadhani tunakuwa hatujatenda haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni la elimu, elimu ya utumiaji wa barabara ni muhimu, kwa watumiaji kwa waendeshaji wa vyombo hivi watembeaji kwa miguu na ningependa na lenyewe lipewe liwe jukumu mojawapo la mamlaka hii ili waweze kusimamia utoaji wa elimu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni alama za barabarani ambazo huwa zinachangia sana katika ajali za barabarani tusiende mbali ukiangalia barabara inayopita hapa mbele ya Bunge unapokuwa unatoka Dar es Salaam kabla hujafika kwenye geti la Bunge pale kuna inabidi, gari kubwa haziruhusiwi kuingia mjini, inabidi zikate kulia.

MWENYEKITI: Asante maliza.

MHE. DKT. BALOZI DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sasa utakuta Trafiki wamesimama kule gari kubwa ikienda wanaikamata lakini kumbe barabarani hakuna alama zinazoelekeza mtu apite wapi aende wapi, hakuna sababu ya kufanya hizi shughuli kwa kutegeana, tuweke mambo wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini wa Mwaka 2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii muhimu ya kuchangia Miswada miwili iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Muswada kuhusu Meteorological, ukiangalia kifungu cha 7 ambacho kinaanzisha Bodi, kinabainisha kwamba kutakuwa na wajumbe nane lakini ukiangalia kwa umakini unaona kwamba NEMC, taasisi ambayo inafanya kazi muhimu sana zinazoendana na shughuli za meteorological na kule Zanzibar tuna ZEMA, hatujatambua uwepo wa taasisi hizi mbili muhimu zinazofanya kazi muhimu kama ambayo itakuwa inafaywa na hii Mamlaka mpya. Kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu wa kutambua uwepo wa hizo taasisi mbili, lakini pia na kwenye bodi wawepo wawakilishi wawili mmoja atoke NEMC na mwingine atoke ZEMA ili kuingia kwenye taasisi hii. Jambo hilo likifanyika litasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Meteorological imeelezwa katika kifungu cha 11(1)(a) kwamba awe na Ph.D. Labda tu niseme sina tatizo la kusema mtu awe na Ph.D kwa sababu wengine tunazo mbili na nyingine wala hatuzifanyii kazi, hoja yangu hapa haya mawazo ya kufikiri kwamba mtu anapokuwa na Ph.D basi huyo ndiyo amebobea na ni mtaalam sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tungesema tu walau awe na Masters akishakuwa na Masters hata Masters sio lazima sana kimsingi degree ya kwanza ndio huwa inamtambulisha mtu ni mtaalamu wa kitu gani degree ya kwanza. Ndio maana hata Wanasheria wengi ambao wamebobea huwa hawahulizi Masters wala Ph.D wanaangalia degree ya kwanza. Sasa unapoangalia shughuli zote za hii Taasisi tunayounda Mamlaka unaposema Mkurugenzi Mkuu lazima awe na Ph.D maana yake kuna watu unawajua wana degree za kwanza au za pili ni wazuri lakini unajua hawana Ph.D kwa hiyo, unaiweka hapa Ph.D ili kuwa-exclude bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda katika schedule ya kwanza A inaeleza Wajumbe wa Bodi, wawe na degree ya kwanza inayotambulika sasa kama Wajumbe wa Bodi wale umewapa sifa ya kuwa na degree ya kwanza, inakuwaje sasa Mkurugenzi Mkuu pekee ndio unasema na yeye lazima awe na Ph.D wakati Mkurugenzi Mkuu huyo naye pia ni Mjumbe wa Bodi, kwa hiyo unakuwa una Sheria moja ile ile ambayo inajipinga yenyewe, huku inatambua kwamba huyu Mkurugenzi Mkuu, lazima awe na Ph.D huku inasema kwamba kwenye Bodi unapoangalia nani wenye Bodi na Mkurugenzi Mkuu yuko kwenye Bodi. Kwa hiyo Mheshimiwa nadhani tuweze tuka-harmonize nikiangalia eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia kuna kifungu cha 22 kinabainisha kwamba ukichukua takwimu hizi za kama unataka kufanya utafiti au unafanya assessment ya Miradi lazima takwimu hizo zitolewe na Meteorological ambayo ni jambo jema. Lakini tunasahau kwamba tunasheria inayoanzisha NBS (National Bureau of Statistics) ambayo tulishakubaliana hapa kwamba data zinazotolewa na ile Taasisi ndio official. Kwa hiyo, mtu kama anafanya assessment ya Mradi akitumia takwimu kutoka NBS kufanya assessment ya Mradi halafu baadaye ukawa na Sheria nyingine inayosema haitambui taarifa yoyote ile isipokuwa zitakazotoka Meteorological ni kwamba unakuwa unashindwa kutambua kwamba tayari kuna Taasisi iliyoanzishwa kwa kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi Wajumbe wa Kamati ya Bajeti tulitembelea NBS walituonesha kazi nzuri ambayo wameshaifanya katika utafutaji wa takwimu na takwimu zinazohusisha na masuala ya hali ya hewa, wenzetu wameshapiga hatua wanatumia satellite wanazo taarifa ambazo ni bora kuliko na hii Taasisi ambayo tunaianzisha leo hii. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tutambue kwamba NBS hapo tutambue ndio chombo ambacho kimehalarishwa kwamba kinapotolewa takwimu ndio takwimu halali kisheria sasa hata kama chombo kipya kinaanzishwa ni vizuri chombo hicho kitambue uwepo wa chombo kingine ambacho official ndicho kimeshakipa hayo mamlaka, tusipofanya hivyo tutaleta migongano ya Utendaji isiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii, ukiangalia Kifungu cha 42 kina jaribu kubainisha mtu akiruhusu watu kuingia kwenye eneo ambalo liko protected kwamba hili ni eneo liko protected kwa ajili ya kuweka Miundombinu ya masuala ya Meteological basi anaweza akatozwa faini kubwa. Nilikuwa najiuliza hapa hivi unatambuaje kwamba eneo hili liko protected na alama zipi zinawekwa kwenye eneo hilo kwamba liko protected kama huwezi ukajua maeneo yote yaliyo protected kama hata alama hazijawekwa basi utajikuta watu wanachukuliwa adhabu wanapewa adhabu kali kwa sababu tu ya kuonekana wamevunja sheria na kwa sababu tu ya kutojua, vinginevyo Sheria hii lazima iendane na kutambua hayo maeneo yabainishwe na alama ziwekwe ili watu wengine wasije wakajikuta wanapewa adhabu zisizokuwa za lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 46, kinasema ukitoa taarifa za hali ya hewa kwa kutumia redio kutumia, kutumia magazeti na nyinginezo unakuwa unavunja Sheria lazima utumie zile ambazo wanasema ni latest methodology. Lakini Sheria haitaji hizo latest Methodology ni zipi, ambazo maana sote tunaelewa hapa ukitoa taarifa kupitia redio ni jambo ambalo linajulikana ukitumia magazeti ni jambo ambalo linajulikana lakini unapokuwa na Sheria unasema usipotumia zile ambazo ziko official utachukuliwa hatua kali bila kuzitaja hizo ambazo zinaitwa official ni zipi tutakuwa tunauziwa mbuzi kwenye gunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri atakapokuwa ana-windup Mheshimiwa Waziri atueleze hizo anazosema ndizo zinatambulika na ndizo zitumike, ni zipi kwa sababu mode of communication tunazijua ziko za magazeti yapo, redio, televisheni zipo lakini unaposema atakayetumia hizo amevunja Sheria atumie zile zinazotambulika wakati hatujui hizo zinazotambulika ni zipi, kama mtunga Sheria hapo unakuwa sijaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Muswada wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini Muswada mzuri na nimeupenda sana kwa sababu ukiangalia pale sifa za Mkurugenzi za Mkuu wa Mamlaka hiyo, wanasema awe na Masters, Postgraduate pamoja na uzoefu wa miezi nane, nadhani hili ni jambo jema kabisa, na sifa hizi ndiyo zingepelekwa hata kwenye Mkurugenzi wa ile Mamlaka nyingine tunayoianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia Kifungu cha 7(1b) kinataja wajumbe wa bodi, mbali na wengine kinawataja wengine sita, mmoja anatoka ofisi AG ni jambo jema, lakini inataja wengine sifa zao inasema wale watano wengine, walau awe na Engineering, Management, Finance or Accounts imesahau professional muhimu sana kwenye haya mambo na Mchumi, Transport Economics haitambui kabisa hapa, ingawa inapoenda kwenye panel ya ku-review ndiyo inakumbuka Wataalamu wa Economics inawaweka kwenye panel review.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri hata kwenye Bodi akawemo Mchumi ili hata yule aliye kwenye panel review atakapopelekewa jambo basi jambo hilo, liwe kweli limepitia kwa wachumi katika hatua. Na jambo lingine tunaona representative kwenye hiyo Bodi sijaona TABOA, sijaona TATOA hizi ni Taasisi muhimu sana kwenye masuala ya usafiri na hawa watu wamekuwepo muda mrefu kabisa sasa unapoanzisha mamlaka kama hii, kwenye Bodi ukashindwa kuwatambua kwamba TATOA wapo ukashindwa kutambua kwamba TABOA wapo nadhani tunakuwa hatujatenda haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni la elimu, elimu ya utumiaji wa barabara ni muhimu, kwa watumiaji kwa waendeshaji wa vyombo hivi watembeaji kwa miguu na ningependa na lenyewe lipewe liwe jukumu mojawapo la mamlaka hii ili waweze kusimamia utoaji wa elimu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni alama za barabarani ambazo huwa zinachangia sana katika ajali za barabarani tusiende mbali ukiangalia barabara inayopita hapa mbele ya Bunge unapokuwa unatoka Dar es Salaam kabla hujafika kwenye geti la Bunge pale kuna inabidi, gari kubwa haziruhusiwi kuingia mjini, inabidi zikate kulia.

MWENYEKITI: Asante maliza.

MHE. DKT. BALOZI DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sasa utakuta Trafiki wamesimama kule gari kubwa ikienda wanaikamata lakini kumbe barabarani hakuna alama zinazoelekeza mtu apite wapi aende wapi, hakuna sababu ya kufanya hizi shughuli kwa kutegeana, tuweke mambo wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)