Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Gibson Blasius Meiseyeki (3 total)

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Shule za Sekondari na Msingi Mkoa wa Simiyu zina upungufu mkubwa wa walimu. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha katika shule za msingi na sekondari Mkoa wa Simiyu? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali imeendelea kupeleka walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kuanzia ajira za 2021/2022, 2022/2023 lakini pia katika ajira za mwaka huu wa fedha 2023/2024 tutatoa kipaumbele kuhakikisha kwamba walimu zaidi wanaendelea kupelekwa katika shule za Mkoa wa Simiyu, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa Serikali imetenga fedha ya kujenga VETA katika bajeti inayoanza Julai, imetenga fedha ya kujenga VETA 36.

Je, Serikali inaweza ikawaambia nini vijana wa Meatu ambao tayari wameshaandaa eneo la kujenga VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoanza kueleza kwenye majibu ya msingi kwamba Serikali ina sera ya kujenga chuo katika kila wilaya nchini. Katika bajeti yetu ya Serikali ni kweli tumetenga zaidi ya shilingi bilioni mia moja kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 36 au vyuo katika wilaya 36 nchini. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa vile tutaweka vigezo vya namna gani zile Wilaya 36 tunakwenda kuzipata na kwenda kufanya ujenzi na kwa vile ujenzi unafanyika kwa awamu, nimhakikishie tu na niwahakikishie wananchi wa Meatu katika mgao huo ujao tuwahakikishie kwamba na wao Wilaya ya Meatu tutaweza kuzingatia ili tuweze kupata chuo katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba ukienda kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni mara nyingi utakuta sarafu ambazo zimeandikwa ni za baadhi ya nchi kama Ugandan shilling, Kenyan shilling, lakini sina uhakika kama ukienda kwenye zile mbao za kubadilisha fedha utakuta kwamba imeandikwa exchange kati ya pesa ya Malawi Kwacha, Zambian Kwacha na nchi kama Mozambique. Je, kutokana na hali ilivyo ya ukosefu wa dola na jinsi pressure ilivyo kwa sasa hivi, Serikali zetu hazioni kwamba ni wakati muafaka ma-governor wa nchi hizi hasa ambazo tunapakana wakakaa ili waje na utaratibu ambao tutaweza kutumia sarafu za kwetu kupunguza pressure ya hizo dola?
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, wazo la Mheshimiwa Mbunge makini kabisa wa Kalambo ni la msingi. Tutawaelekeza ma-governor wakae waendelee kuangalia hizi njia mbadala ambazo zinaweza zikafanyika, hasa katika nchi zinazofanya biashara mpakani ili kuweza kurahisisha biashara na kupunguza tatizo la uhitaji wa dola.