Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Gibson Blasius Meiseyeki (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kabla sijachangia nikiri kwamba mimi ni mfanyabiashara wa utalii kwa takribani miaka 12 sasa kwa hiyo ni field yangu ya experience.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia kwa masikitiko kwa kiasi fulani, wengi wamezungumza hapa kila mmoja anafahamu ni kwa kiasi gani nchi yetu ni nzuri, iko kwenye at least top ten za dunia, lakini tumekaa hapa tunashangilia, wakati fulani Wabunge huku walipiga makofi kwamba tumefikia watalii milioni moja. Watalii milioni moja ni wachache mno, sana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama South Africa ambayo tuko equally beautiful I would say. Wanakwenda sasa hivi watalii milioni 12 kwa mwaka, Misri wako milioni 15, wakati ule kabla hawajagombana sijui sasa hivi iko ngapi. Nchi kama Thailand nazungumzia nchi ambazo hazina uchumi mkubwa kama sisi, wana watalii milioni 25 kwa mwaka, Indonesia, Singapore milioni 15; Tanzania watalii milioni moja tunashangilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa umefika tufanye jitihada za maksudi kuhakikisha kwamba tunanyanyua kiwango hiki cha watalii wanaokuja Tanzania, kiukweli kama sasa hivi wanakuja milioni moja tu wanachangia asilimia 17 ya GDP yetu wangefika milioni tano ingekuwaje, kwa mfano? Ingekuwa ni zaidi ya nusu ya GDP; kwa maana hiyo ingeweza ku-observe shock zote hizi za matatizo ya ajira kwenye Taifa letu, ningekuwa nina mamlaka ningeweza kusema kwamba Serikali yenu hii ya sasa angalau ingechukua vitu vitatu comprehensively. Ingechukua viwanda vya Mheshimiwa Mwijage kama anavyokuja navyo vizuri; amejipambanua vizuri Mheshimiwa Mwijage kwenye viwanda, mchukue Mheshimwia Mwigulu kwenye kilimo, mifugo na uvuvi, ukaweka na utalii hapo tunaweza kuchukua watu wengi ambao hawana ajira katika Taifa letu tukawa-absorb kwenye maeneo haya. Hivyo, ningeshauri tu kwamba tuangalie ni sababu zipi zinapelekea Taifa letu kukosa watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uzoefu nilionao mimi, nimekwenda kwenye trade fair za kutosha na watu wa Mheshimiwa Maghembe wa TTB nimekwenda nao na nina masikitiko makubwa sana kusema kwamba watu wetu wa TTB wanakwenda kwenye trade fair kupumzika, hawaendi kufanya kazi ukilinganisha na mataifa mengine ambayo tunayakuta kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata nilivyosikia mmewanyang‟anya sijui fungu mmelipeleka wapi niliona ni sawa tu, kwa sababu wenzetu wale wanakwenda kupumzika hawaendi kutafuta biashara, mara nyingi nimekwenda nao kwenye masoko mbalimbali nje ya nchi. Kwa hiyo, niseme kwamba tuangalie tena ni maeneo gani ambayo mojawapo ni kwamba Tanzania ni destination ambayo ni very expensive, ni ghali mno kuja Tanzania ukilinganisha na kwenda maeneo mengine ambayo naona watu wanaweza wakawa wanavutika kwenda kutalii maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tu-review tena hizi sababu ambazo zinasababisha tuwe ghali. Kwa mfano, airport zetu wanasema handling fees ni mojawapo inayosababisha tiketi ziwe ghali kwa watalii wanapotaka kuja Tanzania. If that is the case na kwamba kweli tunataka ku-promote utalii Tanzania tufike hiyo namba ya watalii ambayo mmeiweka target kwa sasa hivi ambayo ni milioni tatu ambayo naiona ni wachache, tuangalie hivi sababu vidogo vidogo, handling fees, airport departure taxes zile mnazi-regulate vipi ili kupunguza gharama ya mtu kuja Tanzania, maana yake mtalii anapokuja tusizungumzie ile package tu ambayo anailipa kuja kufanya utalii, lakini zungumzia pia na fedha anazokuja nazo mfukoni nyingi ambazo Watanzania wengi huko mitaani wanazisubiri kuuza bidhaa zao, vitu mbalimbali ambavyo wazungu wanavinunua. Tena wanavinunua kwa kusema mzungu price, tourist price, siyo kama wengine. Sisi tunakunywa soda shilingi 600, shilingi 700; mzungu anakunywa kwa shilingi 2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakifika milioni tano ina maana kutakuwa na dola nyingi ambazo tutazi-retain hapa, ambazo zimekuja indirect. Kwa hiyo, tuangalie mapato ambayo ni indirect, mtalii anaweza kutuletea. Kwa hiyo, tujaribu kuwa-entertain waje kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine vitu vingine vinavyosababisha tukose watalii wa kutosha, kuna hizi issue za viza, tusishindane na Uingereza, Ufaransa sijui na ninyi mnapokwenda kutembea nje mnalipa viza kubwa. Muingereza aki-charge laki mbili kwenda Uingereza, tusishindane nao kwa sababu wale wanapokea watalii karibu milioni 50 kwa mwaka, sisi watalii 1000! Kwa hiyo, tuangalie namna gani tunawa-entertain kupunguza mzigo ili hawa watu waje wakishafika hapa ndiyo tutajua jinsi ya ku-deal nao, mnafahamu pia kwamba mtalii anapofika hapa anachukua precautions nyingi sana.
Mheshimiwa Waziri, nisikitike kwamba figures ambazo umetupa hapa za watalii waliokuja mwaka jana siyo sahihi. Utalii mwaka 2014/2015, ume-drop kwa zaidi ya asilimia 50 mzee. Ugonjwa wa Ebola ilitu-affect sana na tumepunguza wafanyakazi sana kwenye makampuni yetu huko Arusha. Niseme tu kwamba ukitaka kufanya uhakiki vizuri wa hili jambo kesho kutwa week end inayokuja kuna Karibu Fair, nenda pale utawakuta wadau wa utalii, wahoji, waulize biashara ilikuwa vipi bila kujali ninyi mmekusanya kiasi gani, kwa sababu kuna mbinu nyingi za ninyi kukusanya mapato, kwa hiyo, utalii uli-drop sana, toka Ebola ilivyozuka, tulipoingia kwenye uchaguzi pia watalii wanatabia ya kutotembelea nchi, lakini ninyi rekodi zenu zinasema ni 80 percent, siamini kama hiyo ni sahihi na tukafanye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu wanapokuja, sorry kule Arusha tumezoea kusema wazungu, badala ya kusema watalii. Watalii wanapokuja wanameza dawa za malaria, lakini pia kwa baadhi ya nchi wanapofika airport wengine kama hawajadungwa sindano, wanandungwa sindano ya yellow fever, pale panatokea kizungumkuti kikubwa sana unajua siyo kila mmoja anapenda kudungwa sindano, wakija pale maafisa walioko pale wengine hata kwa yale mataifa ambayo hayatakiwi kudunga hizo sindano wanakamatwa wanakuwa harassed, wakati mwingine hongo zinatembea wanaingia bila kudungwa hizo sindano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme kwamba tufanye overhaul ya marketing strategies zetu tukafanye kazi. Ningeshauri kwamba yale mataifa ambayo ni makubwa yanaleta utalii kama Ujerumani, Uingereza, Canada, USA nimesema, Japan tuseme na China; kwanini tusifungue ofisi kule na tukawapa watu kazi na wapewe target ya kuhakikisha kwamba wanaleta wageni Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina ni watu ambao wana uchumi mzuri sana sasa hivi lakini kiukweli tumeshindwa kuwa-reach kwenye soko lile. Pamoja na kwamba kweli tunataka kujilinda wenyewe hapa ndani kwenye suala la utalii wawekezaji kutoka nje ni muhimu sana. Kuna matatizo ya lugha na connection, tukisema kwamba sisi wamatumbi hapa ndiyo tuifanye tu peke yetu hatutafikia hiyo target.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Immigration waangalie namna gani tuna collaborate na hawa watu wanaotoka nje, maana hawa ndiyo wana access na masoko ya kule kwao. Tuwarahisishie utaratibu wa kuingia hapa na wao watakapoleta wageni wakifika hapa kwetu na sisi tutapona hapo. Lakini tukisema tufanye wawekezaji wa ndani na nini? Kumchukua mzungu kutoka ya kuwekeza kwetu, tuwawekee mazingira mazuri, na yawekwe rahisi kama Rwanda wanavyo fanya, Tanzania tumekuwa na bureaucracy kubwa sana, ningeshauri kwamba tuangalie hivyo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Airlines, pamoja na kwamba mnakwenda kununua ndege zenu ambazo ni chache kwa kweli na ningeshauri pia kwamba tununue na zile ndege ndogo kama hizi za Precision Air - HR kwa ajili ya kuweza kuhudumia viwanja vyetu vidogo vidogo hapa ndani, kulikoni kuwaachia private sectors ambao flight charges zao ni ghali sana. Kutoka tu Arusha kwenda na kurudi Serengeti shilingi 800,000. Kwa hiyo, tuwe na ndege za Serikali au ambazo tunaweza tukawa na ubia ili tuweze ku-regulate price za fares. Tuweze kutoa wageni Arusha kuwapeleka Ruaha, Katavi na maeneo mengine kama Mikumi, kufanya hivyo sasa hivi ni tatizo, mgeni akileta enquiring kwenye makampuni yetu anataka kwenda Kusini na sisi tuko Kaskazini huwa hatufanyi hiyo biashara, kwa sababu ya jinsi ya kufika kule gharama ni kubwa sana na pengine kwa sababu ya uchache wao tunakuwa hatuna contacts. Kwa hiyo, tuboreshe maeneo hayo ili tuweze kutanua huu uwigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini airlines za kimataifa…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimefurahi jinsi ulivyolipatia jina langu, limekuwa likiwapa shida sana watu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza pia kuzungumza katika Bunge lako, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wangu wa Arumeru Magharibi kwa kura nyingi za kishindo ambazo wamenipatia. Labda tu ili uweze kuweka rekodi zako, mimi ndiyo niliyeshinda kwa tofauti ya kura nyingi kuliko Mbunge mwingine yeyote, takribani kura 62,000; siyo kidogo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti nakwenda moja kwa moja kwenye mchango. Nimefurahia, hotuba ya Waziri ilikuwa nzuri kama ambavyo zimekuwa zikitolewa hotuba nyingi nzuri humu ndani, lakini kwa kweli nina mashaka sana na utekelezaji wake. Takribani miaka kumi iliyopita, Wizara yake ya Kilimo ilikuwa ndiyo wimbo wa Serikali iliyopita, Kilimo Kwanza, lakini mpaka sasa hivi tumeshindwa kujua kilimo hicho kimetufikisha wapi na sasa kwa Serikali hii ambayo hatuoni namna gani ina-incorporate Kilimo Kwanza na Serikali hii ya viwanda ambayo mnakwenda kuifanya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi pia katika hotuba ya Waziri unanijia ni jinsi gani, sijapata kuona ni kwa namna gani anakwenda kumaliza matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji; na wafugaji kwa wafugaji wenyewe? Ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yangu kuna triangle moja ambayo sisi Monduli na Longido, wafugaji ambao wote ni Wamasai wanajeruhiana kila kukicha, wanagombania mpaka, kwamba ng‟ombe akitoka Arumeru Magharibi akaenda upande wa Monduli ni tatizo; akitoka Monduli akaja Arumeru Magharibi ni tatizo; akitoka Longido akaingia kwenye mashamba, sasa tunashindwa kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii migogoro ya namna hii ni kweli kwamba Serikali imeshindwa namna ya kumaliza matatizo haya ya wafugaji? Inakuwa vipi ng‟ombe wanaweza kutoka Arusha kwenda mpaka Morogoro, wakazunguka mpaka Mkoa wa Pwani; ukiondoa ile migogoro yao na wakulima; wafugaji kwa wafugaji hawagombani kwenye maeneo hayo, lakini wale ambao wanakaa, wako settled wanagombania mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali ingekuja na kauli kama ambavyo tulivyo sisi Watanzania ambao tunaweza kuingia kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kama ni maeneo ya wafugaji kwa wafugaji, hakuna sababu ya kupigana kugombania nyasi, nchi hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ambayo ina ukubwa kuzidi nchi karibu nne za Afrika Mashariki; Kenya, Uganda na Rwanda ukiziweka pamoja bado Tanzania ni kubwa kuliko hizo nchi. Hizo nchi zina watu karibu milioni 100, sisi tuna milioni 50 tu. Nchi hii ni kubwa, ni nzuri ina karibia kila kitu kinachotakiwa. Hii ndiyo nchi ile ambayo ni ya asali na maziwa, lakini Serikali imeshindwa kuwatenga wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kutenga maeneo ya wanyamapori, tumeweza kutenga maeneo ya misitu, lakini tumeshindwa kuwatengea wakulima maeneo yao, wafugaji maeneo yao. Ni masuala ya kutoa kauli tu, tutengeneze corridor. Tutengeneze corridor ambayo wafugaji watakuwa wanaitumia bila kujali ni wa asili gani; awe Mmasai, Msukuma, Mnyamwezi, nani, kama kuna malisho na hayo maeneo yawe kama ni ya Serikali vile. Maana ni vigumu sana kwa wafugaji kupata hatimiliki kwa ajili ya kulisha mifugo mingi ambayo wanaifuga. Kwanza mifugo yenyewe inakwenda kulingana na malisho yanavyopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungetengeza corridor, kama ambavyo tumetengeneza Game Reserves kama ilivyozungumzwa hapo awali, tutengeneze corridor ambayo itakua ni ya wafugaji. Kama alivyosema Mbunge mwenzangu ambaye alitangulia awali, maeneo hayo yawe ni maeneo ambayo kuna maji, watawekewa miundombinu ya majosho na pia kuwa na maeneo ya masoko pia ili wafanyabiashara waweze kupata access ya kununua mifugo hiyo. Hii nchi ni kubwa na ina kila kitu. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kiukweli hotuba hii ya Waziri kama hataidadavua vizuri namna gani anakwenda kukabiliana na tatizo la migogoro kwa kushirikiana na mwenzake Waziri wa Ardhi na pengine na Waziri wa Maliasili, ili tuweze kupata maeneo sasa na kuhitimisha suala hili la migogoro ya ardhi ambayo inalitia Taifa letu aibu, Taifa hili ni kubwa lina kila kitu tunashindwa kuvigawa. Kwa hiyo, Mawaziri hawa wakae pamoja na watuletee mpango ambao utatuonyesha ni kwa namna gani wakulima wetu wanakuwa safe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa hatimiliki za ardhi kwa ajili hata ya hawa wakulima. Mimi kama nilivyosema, wakati mwingine ni mkulima lakini pia mfugaji. Ni mkulima wa ukweli, nalima kweli kweli, lakini tumekuwa tukipata shida sana ya kupata hatimiliki ya maeneo ambayo tumeomba na pengine hata Serikali ilitoa kabisa kwa ajili ya kulima lakini kuipata hatimiliki inakuwa ni shida sana. Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakae na wakubaliane kwa sababu bila hati pia unashindwa kupata misaada kwenye mabenki.
Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakubaliane namna gani wanaweza kuharakisha wakulima waweze kumilikishwa ardhi ili waweze kupata pia access ya mikopo ambayo inatolewa na mabenki na taasisi nyingine za kifedha. Kwa hiyo, tungependa tupate hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la mbegu bora kwa ajili ya mazao ambayo wenzangu wamezungumza sana. Labda niseme tu Mheshimiwa Waziri, hii picha uliyoipiga hapa kwenye cover yako; hii picha ya dume inanipandisha mori kidogo. Hii ndiyo mbegu ambayo nilikuwa nasema tunataka tuzipate; mbegu bora ya ng‟ombe wa nyama, ndiyo kama hii. Mbegu hizi kwa kweli kwenye taasisi zako zinazozalisha mbegu bora, wanaziuza ghali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dume kama huyu akiwa mdogo tu na mwaka mmoja, anauzwa shilingi 800,000 au shilingi milioni moja na kuendelea. Hii ndiyo bei halisi iliyopo. Kwa dume kama hili lililopo kwenye picha yako Mheshimiwa Waziri, mimi nimetoka mnadani juzi tu, shilingi milioni moja, shilingi milioni moja na nusu unapata hili dume, lakini ninyi mbegu mnauza shilingi 800,000, shilingi milioni moja. Hii mbegu ni kubwa na haionyeshi ile commitment ya Serikali kuwasaidia wakulima kuweza kubadilisha mbegu zao ambazo ni zile tunaita katumani. Kama ni mahindi tuite katumani; unalisha miaka mingi sana haifikishi kilo 100.
Kwa hiyo tusaidie tena, ulinijibu juzi kwenye swali lakini nisisitize tu kwamba bei mnayouza bado ni ya juu sana, mtusaidie ili tupate ng‟ombe wa namna hii ikiwezekana nchi nzima. Kwa hiyo, hilo naliomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alizungumzia ushuru wa mazao kutozwa sokoni. Naomba kabisa kwamba ikiwezekana ushuru huu utozwe shambani inapotoka. Kwa sababu haiwezekani Maafisa wa Halmashauri zetu wawasaidie wakulima lakini wakati wa kuvuna tozo inakwenda kuchajiwa Kariakoo; itakuwa mmetupunja. Kwa hiyo, naomba ushuru uchajiwe mara moja tu; kama ni mashambani au kwenye road block zilizopo kwenye Halmashauri na sokoni wasitozwe tena; kwenda kuitoza sokoni utakuwa umewadhulumu Halmashauri ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chakula cha njaa; enzi za Mwalimu kulikuwa na ile programu ya kwamba kila mkulima ni lazima awe na akiba ya chakula anapokuwa amevuna. Hiyo imekwisha, siku hizi hakuna na Serikali inahangaika na vigaloni au vidumu, chakula kiasi kidogo ambacho inakwenda kuwadanganyia wananchi na tunaona kama hii ni siasa ya kura. Serikali ije na mpango kama ule wa Mwalimu, kwamba kila mtu anapovuna awe na kichanja cha kuhifadhi chakula ili wakati wa njaa aweze kukabiliana na njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wanavuna halafu wanauza yote, halafu kesho Serikali inaanza kuhangaika kuwagawia kilo mbili mbili au tatu tatu za mahindi, kitu ambacho hakiwasaidii. Kwa hiyo, tuwe na mpango wa kisera kwamba wakulima waweze kushawishiwa kuhifadhi chakula baada ya kulima na tuepukane na hii kusambaza chakula ambacho hakiwatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyeikiti, kwa hiyo ningependa pia kuishauri Wizara, nilipata fursa, nilikuwa Diwani hapo awali, nikatembelea nchi moja ya jirani hapo, sitaitaja. Kwa kweli tuliona wana mpango mzuri sana wa kuwasaidia wakulima. Wakulima wanapovuna kwa fujo, wamebahatika kupata mazao, wanakwenda kuyahifadhi vizuri kwenye maghala ya Serikali; na yale maghala yanakuwa yanathaminisha kile chakula au yale mazao ambao mkulima ameyazalisha na anapewa hati. Nafikiri nilishasikia hapa, sijui mnasema sijui ghala sijui nini, kitu kama hicho. Ile hati inamwezesha mkulima kwenda kukopa benki wakati anasubiria bei ya mazao yake yaweze kupanda value. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamsaidia yeye kuweza kusomesha watoto wake au kujiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo na kwa maana hiyo halazimiki kuyauza kwa bei ya haraka haraka. Tena anakuwa ameweka sehemu ambayo ni salama kimatunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisema hapa kwamba kuna dawa ambazo unawanyunyizia wadudu lakini wanaogelea tu na kutokea upande wa pili. Sasa kwenye maghala ya Serikali watapata fursa ya kuweza kuyatunza vizuri na kwa maana hiyo anakuwa na uhakika wa uhifadhi wa chakula kile na wakati huo Serikali ikimtafutia bei nzuri ya mazao hayo. (Makofi)
Naishauri pia Serikali, kama ambavyo ina kitengo kinachoshughulikia kutafuta ajira ndani na nje ya nchi, kuwe na chombo, kuwe na bodi kama ilivyo Bodi ya Utalii ambayo itakwenda nje ya mipaka yetu kutafuta masoko ya bidhaa ambazo tunazizalisha hapa nchini ili tuweze ku-entertain wananchi wengi kuingia kwenye kilimo kwa maana ya kwamba masoko yatakuwa yanapatikana. MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa bahati mbaya siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuchaguliwa tena kuongoza Wizara hii, hakika anaweza. Nampongeza pia na kumshukuru kwa ziara aliyoifanya Jimboni kwetu kwani ilitupa mwanga wa utatuzi wa migogoro mingi ya ardhi iliyotuzunguka. Bado tunamhitaji Mheshimiwa Waziri Arumeru ili tuweze kumaliza kabisa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya sababu ambazo zinasababisha migogoro ni Serikali kuwapa wawekezaji maeneo makubwa mno kuliko uwezo wao na kuyaendeleza. Hii hupelekea wawekezaji kufanya biashara kukodisha ama kugawia wananchi mashamba hayo ambayo baadaye hushindwa kuwaondoa pindi wanavyotaka kufanya shughuli nyingine katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo kama haya hasa katika shamba ya Fill Estate na Tanzania Plantation yote katika Jimbo la Arumeru Magharibi, Kata ya Bwawani. Wananchi wameumizana sana na vyombo vya dola na zaidi ya watu 11 wapo rumande kwa miezi miwili sasa kwa kubambikiziwa kesi ya wizi wa kutumia silaha eti kwa sababu tu wanagombania shamba na askari polisi ambao wawekezaji wakawakodisha katika shamba ambalo wananchi tayari walikuwepo kwa lengo la kuwatoa kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Arumeru karibu sasa yote inakuwa mji, hivyo mashamba mengi ya wawekezaji yamemezwa na idadi kubwa ya wananchi wanaoongezeka kila kukicha na hivyo mashamba haya yanalimwa mjini na bado hayajaendelezwa vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huchukua muda mrefu sana kubatilisha haki za umiliki za wawekezaji zilizopita muda wake na kupelekea wananchi kuvamia mashamba hayo na kuanza kujigawia. Serikali sasa ichukue hatua madhubuti kutengua hati za ardhi ambazo muda wake umeisha. Hii ni pamoja na kuwatafutia maeneo mengine wawekezaji ambao mashamba yao yameingia ndani ya miji kuepusha migongano zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu linaelekea pabaya hasa jinsi suala la migogoro ya ardhi inavyoshughulikiwa, Taifa linaelekea Zimbabwe. Kwa Mkoa wetu wa Arumeru hali siyo shwari kwa wawekezaji na hivyo wapo kwenye hofu kubwa sasa, wananchi kila wanapoona shamba kubwa basi hulazimisha wanasiasa kufanya liwezekanalo ili wanyang‟anywe na wapewe wao, jambo ambalo siyo zuri kwa ustawi wa Taifa letu ambalo bado linahitaji wawekezaji kwa ustawi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwa Serikali, hasa kwa Mkoa wa Arusha kuboreshewa miundombinu inayounganisha mikoa mingine hasa Manyara, Wilaya ya Simanjiro ili kuwaunganisha wananchi hawa na maeneo hayo ambayo bado ardhi ni virgin. Mashamba yaliyo mjini na muda wake umekaribia kwisha, Serikali iyatwae na kufanya mipango mipya ya ardhi/mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanasiasa siyo rahisi kutoa elimu ambazo siyo rafiki kwa wananchi kuhusu umiliki wa mipango ardhi, Serikali kwa kutumia vyombo vyake, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi kuhusu sera za ardhi na umiliki mashamba ili wananchi waache tabia ya kuvamia mashamba ambayo nyaraka zake ziko thabiti/genuine ili kuhakikisha kwamba wawekezaji ambao Serikali inahangaika kuwaalika wanakuwa salama na wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninamwalika tena Mheshimiwa Waziri Jimboni Arumeru Magharibi ili tumalizie migogoro iliyopo once and for all. Ahsante sana, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri. Pamoja na pongezi hizo, kwa kifupi, lazima niwaombe mambo mawili, matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Ambulance mbili kwa Halmashauri ya Arusha DC kwa ajili ya Kata zangu mbili za Oldonyowas na Kata ya Bwawani. Hali za wanawake na watoto kwa maeneo haya ni mbaya. Panapotokea dharura, wanataabika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yetu ya Mkoa haina mashine za X-Ray, CT-Scan na MRI na hata huduma ya Utra sound haitolewi hospitalini hapo. Umuhimu wa vifaa hivi katika


hospitali kama Mount Meru, wote tunaujua. Mheshimiwa Waziri atusaidie wakazi wa Arusha na viunga vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba huduma za Bima za NHIF na CHF ziboreshwe ili wananchi wawe na imani nayo, ili waweze kujiunga kwa wingi na mifuko hii iweze kuwa na tija na iweze kupata uwezo zaidi. Kwa sasa hata sisi wanasiasa tunaogopa kuwahimiza wananchi kujiunga na mifuko hii, kwani changamoto za matibabu ni nyingi mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haya tu kwa sasa.
Shukrani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, labda tu nirekebishe majina yangu kidogo, naitwa Gibson Blasius Ole -Meiseyeki, ni gumu kidogo jina la Kimasai hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, kwa sababu ya muda ni mfupi nitazungumza in a bulletin form ili Profesa pale aweze kunipata kidogo. Nina-declare tena interest kwamba mimi ni mdau wa utalii wa zaidi ya miaka 15 ya utalii wa picha lakini ni mwekezaji pia kwa maeneo fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamezungumza na tuliishauri Serikali kwenye bajeti mwaka jana kwamba VAT is going to kill us na hasa kwa namna ambayo Serikali ilikuwa imeileta, iliileta ghafla na ikaanza implementation pale pale. Kwa hiyo, ilituathiri na niseme tu kwamba introduction ya VAT ilishusha sana biashara yetu ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, statistics ambazo Mheshimiwa Profesa pale ametupa, pengine ni wale Watalii ambao wanakuja kusaka kazi Tanzania lakini siyo wale Watalii wa Photographic Safari’s kama ambavyo tunawategemea. Wakati mwingine anapotuletea record atuambie waliokuja kutafuta kazi ni hawa ambao wao wanawaita watalii na wale wanaokuja kwa lengo la kutembelea mbuga zetu watupe record zake pia kwa sababu wanatupotosha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuleta VAT biashara ya Utalii ilianguka na mbaya zaidi iliharibu sana image ya Taifa letu katika forum za Kimataifa. Mheshimiwa Waziri wao hasa ndiyo wanaorudisha nyuma jitihada za TTB nirekebishe kutoka mchango wangu wa mwaka jana, tumegundua kwamba policy za nchi ndizo zinazoshusha au zina-demoralize kazi nzuri ambayo TTB inafanya ya kuitangaza hii nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wanapokuja hapa Tanzania hawawi treated katika ile namna ambayo inapaswa kuwa. Hospitality yetu ni poor sana pia tozo hizi ambazo ni za kuibuka ibuka halafu mnaanza ku-implement immediately, zinashusha image ya nchi Kimataifa. Wakienda kwenye forum mbalimbali za Kimataifa wataona jinsi gani ambavyo watu wa utalii wameizungumzia Tanzania, wameizungumzia negatively. Sasa hiyo inasababisha tena baadaye tuanze kutumia fedha zilezile ambazo wamewanyang’anya kwenda kufanya utangazaji mwingine ili kuweza ku- stabilize wageni ambao wanatembelea nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunapoleta tozo hizi tuwe na grace period maana VAT watu hawakuikataa lakini ku- introduce leo na kuanza ku -implement kesho that was a problem na anafahamu Mheshimiwa Profesa Maghembe alishapambana sana na waongoza utalii miaka ya nyuma mlivyokuwa mnabadilisha rates katikati ya msimu. Wana-introduce wakati ule Ngorongoro crater service fee, wakataka ku- impose immediately, wakapambana na waongoza utalii wakabadilisha, lakini walipoleta VAT this time wali-implement immediately.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ilituletea shida sana na ikalazimika kama alivyosema Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Wawekezaji wakalazimishwa wao ndiyo walipe hizo fedha siyo kumchaji mteja ila makampuni ndiyo walitoa fedha mfukoni kuwalipa VAT. Wale watu mliwanyang’anya fedha kwa sababu hatukuwachaji clients, wako sensitive sana hawa waongoza utalii unapoleta mabadiliko ya gharama katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, nizungumzie pia suala la entry fees kama nilivyosema mimi ni Mwekezaji na ni muathirika, lakini hapa nazungumzia pia in a National perspective kwamba, Introduction ya single entry lengo lenu ilikuwa hasa kuwakandamiza wawekezaji wadogo ambao hawana ubavu wa kuwekeza ndani ya hifadhi. Kwa hiyo, mnawabeba wale wakubwa ambao wamewekeza hoteli zao kubwa ndani ya hifadhi, wanaenda kuwaminya wale wadogo wanyonge ambao wamewekeza kwenye vijiji vyetu na wanasaidia sana maendeleo kwenye vijiji kwa kuwalinda watu wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu waka-review tena hiyo single entry system kama alivyozungumza Mheshimiwa Marwa Ryoba asubuhi, inawaumiza sana na sasa hivi wale watu wote waliowekeza nje ya hifadhi wanashindwa kufanya biashara. Kwa sababu imekuwa ni gharama sana kwenda kumlaza mgeni nje kuliko kumlaza ndani. Mjue kwamba hakuna mgeni wa utalii ambaye anapenda kulala nje ya hifadhi. Wamefanya hivyo tu ile ilikuwa ni mpango wa Serikali kwamba kwa sababu changamoto ya vitanda vya kulala wageni ilikuwa ni kubwa sana miaka ya nyuma, Mheshimiwa Maghembe anakumbuka alikuwa ni Waziri wakati ule miaka ya 2000. Kulikuwa na changamoto kubwa ya vitanda vya kulala wageni, kwa hiyo, kukawa na a sort of kuwahamasisha watu wajenge tented lodges nje ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wamejenga wamewekeza, all of a sudden wanafanya gharama iwe kubwa sana kuwalaza wageni kule nje au wana wa-equate, wanataka hao watu wawe na gharama zinazofanana, siyo sahihi. Hiyo kitu ime-affect sana uwekezaji hasa wa watu ambao wana mitaji midogo. Kwa hiyo, ningeshauri ni vema tukarudi kwenye zile tozo za masaa. Kwa sababu, haiwezekani mtu anayelalala ndani ya hifadhi alipe kidogo na yule anayelala nje alipe zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia suala la Ikoma, kwa hiyo hebu waka-review hapo hizi fees ziwe timely, iwe ni kwa saa, kama ni masaa 12 iwe ni masaa 12 nje na ndani, kama ni masaa 24 iwe ni hivyo nje na ndani. Siyo kwamba anayelala nje alipe mara mbili, wanafahamu kabisa kwamba jiografia kama alivyosema mwenzangu asubuhi kwamba ili uweze kuingia Serengeti wengi wanatokea Arusha kuingia Serengeti, sasa anapitiliza kwenda kulala upande wa pili wa Serengeti maeneo ya Ikoma. Ameshalipa park fees unamwambia kesho akirudi tena akiingia kufanya full day game drive alipe tena park fees halafu akitoka akirudi tena kesho wakati anaenda Arusha analipa tena, hawa watu wanawabana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia la leseni, wafanyabishara wetu wadogo wenye gari moja, gari mbili, wanawatoza leseni sawa na mwenye magari 400. Hayo nimeyasikia sana Arusha na tunaomba wawe wasikivu wanaposhauriwa. TATO ameongea na ninyi mara nyingi, siyo sahihi kumtoza mtu leseni dola 2000 sawa na mwenye gari moja na mwenye magari 20 ama 200 wanatozwa fee ambayo ipo sawa, siyo sahihi. Kwa hiyo waingalie na hiyo, waje na utaratibu ambao utawatenganisha mwenye mengi alipe zaidi na mwenye magari machache alipe kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri pia kwenye Shirika letu la Ndege la ATCL badala ya kujaza zile Bombardier ifikirie pia kuleta ndege ndogo kama LET zile za kubeba watu ishirini. Hizi ndege ndogo ndiyo zinaweza kusambaza watalii kwenye Mbuga zetu hizi nyingine ndogondogo zilizozunguka nchi hii. Ruaha, Mikumi, Katavi mpaka Gombe kule, lazima tuwe na feeder planes zile ndogo ambazo zinaleta watalii kutoka kwenye mbuga na kuleta kwenye viwanja vikubwa, hivyo ndiyo tunaweza kuwasambaza wageni katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naizungumza hii based on my experience, ni vigumu sana kumtoa mgeni Serengeti ukampeleka Ruaha, gharama za hizi ndege za binafsi ni ghali sana. Tungependa kama wangeweka ndege kama tatu hivi za Shirika la Ndege la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri ana-wind up, ningependa kujua pia ni namna gani alilishughulikia suala la mauaji ya wananchi wangu watano yaliyotekelezwa Arusha mapema mwaka huu. Nataka kujua walishiriki vipi na imefikia hatua gani na nini hatua zaidi ambazo zinachukuliwa kwa Askari wa Mheshimiwa Waziri ambao waliwauwa wananchi wangu watano kwa kuwapiga risasi kama wanyama mapema mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na incidence ya Januari watu wanne na mwezi Aprili aliuawa mtoto wa miaka 15 kwa kupigwa risasi nne mgongoni akiwa anaongoza ng’ombe watatu ambao walikuwa pembezoni mwa misitu ya Meru USA kule Arusha. Ningependa kufahamu kwamba walishiriki vipi na ni nini kauli rasmi ya Serikali hapa kuhusiana na mauaji hayo yaliyofanyika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni uvunaji wa misitu na mazao ya misitu kwa ujumla. Tunaomba waondoe contradiction iliyopo kutoka Wizara za Kilimo, Ardhi na Maliasili ya namna gani kilimo kinaweza kikafanyika nchini humu. Kwani kuna watu wana mashamba yenye mazao ya misitu miti, sasa mtu anataka kuendeleza shamba lake lakini ruhusa ya kuvuna miti inatoka kwenye Wizarani na kuna urasimu mkubwa sana kwenye …

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na zaidi pia kwa kulipatia jina langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maombi kwa Mheshimiwa Waziri; nimkumbushe tu kwamba, kuna kile kilio chetu ambacho wananchi wa Kata yangu ya Bwawani walilia mbele ya Waziri Mkuu na wakaahidi kwamba mgogoro ule wa ardhi wangeufanyia kazi na yeye alikuja pale na akaagiza vijana wake waweze kufanya kazi ile. Hata hivyo, mpaka sasa ni zaidi ya miezi sita hatujapata mrejesho wowote. Kwa kweli wananchi wananisumbua sana kuhusiana na mgogoro ule wa ardhi ulioko pale Kata ya Bwawani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wananchi wangu wa Kata za Oldonyosambu na Olkokola ambao ardhi yao ilitwaliwa na Jeshi na ilikuwa wapewe fidia, lakini baadhi yao hawakupata. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba badaye atuambie mahali ambapo imefikia, ili tuweze kupata majibu ya kuwapa wananchi wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Arusha DC imezunguka Jiji la Arusha kwa pande zote. Kiukweli, influx ya wananchi sasa hivi katika Mji wa Arusha ni kubwa sana na wote asilimia zaidi ya 80 wanakuja Arumeru, hasa Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Ardhi kule inazidi kuwa finyu na ninachokiona huko mbele ni migogoro zaidi za ardhi ikiwa kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuhakikisha kwamba, wananchi wale wanaokuja maeneo yale ama wale wakazi wa maeneo ya Arusha ambao wengi wao ni wafugaji na wanapenda kulima, ardhi inazidi kuwa finyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwamba, kuwe na mpango wa kupata mapori au mashamba pori yale ambayo yapo, hayajaendelezwa, ili vijana hawa ambao wako tayari kufanya kazi za kilimo waweze kutengewa maeneo kule na ikiwezekana taarifa ziwafikie maana wako tayari kwenda mashambani popote, maporini kule, kwenda ku-establish mashamba ili kujipatia riziki zao. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kwa sasa hivi mazingira ni kama vile wanabaniwa sana kiasi kwamba wanashindwa kupata mwelekeo kwamba ni namna gani wanaweza kupata maeneo kwa ajili ya kujiendeleza kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa kwenye Semina hapa ambayo Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alituandalia. Wataalam wale maprofesa walikuja hapa walituambia kuwa nchi hii haina tatizo la ardhi. Hatuna matatizo ya ardhi ukilinganisha kilichopo na idadi ya watu na lilikuwa ni jambo la aibu sana, wamesema hapa tunachokikosa sisi ni mipango. Aliilinganisha Tanzania na akina Vietnam jinsi ambavyo wako kwenye eneo dogo, watu wengi na hawana migogoro hii ambayo kama sisi tuliyonayo na wale watu wanazalisha chakula mpaka sisi tunapewa huku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana tulikuwa na matatizo ya njaa, nchi yenye ardhi kubwa kama Tanzania halafu watu tunalialia na vibakuli vya kuombaomba chakula? Ifike wakati sasa Waheshimiwa muamue sasa kwamba, mnaipanga hii nchi ili Watanzania wengi ambao wana nguvu za kufanya kazi waweze kupata maeneo ya kufanya kazi za kilimo na mifugo, tena bila kugombana. Kuna nchi nyingi tu ambazo ni ndogo kwa size, zina watu wa kutosha, wengi lakini hawana migogoro kama tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba, Waheshimiwa Mawaziri, kama tulivyoomba katika bajeti iliyopita wakati ule Mheshimiwa Mwigulu akiwa kwenye kilimo yeye akiwapo hapo na Mheshimiwa Maghembe pale, kwamba washirikiane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mizengwe mingi sana katika nchi hii; yametengwa kwa ajili ya kilimo lakini maeneo hayo yana misitu, kuna miti lakini watu wananyimwa kukata miti, eneo la kulima utalimaje sasa kwenye miti, si lazima uikate? Likishakuwa declared kwamba ni eneo la maendelezo ya kilimo na mifugo basi Wizara ya Maliasili na Utalii isiende tena kupeleka pale wataalam wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wana chokochoko nyingi sana, wako aggressive na wakati mwingine wanafanya biashara ambazo ni kichaa kule kwenye mashamba. Kwa hiyo, Waheshimiwa Mawaziri ningewaomba washirikiane. Maeneo ya kilimo kama kuna misitu, kama kuna miti huko na tayari wamesha-declare ni eneo la kilimo na ufugaji basi watu wa maliasili wasiwe wanaingia sana kule, hii mizozano hii inaleta fracas kwa wananchi wanashindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningewaomba wakae pamoja ili wananchi waweze ku-explore na ku-enjoy matunda ambayo nchi hii inaweza ikawapa. Tuna ardhi kubwa, maeneo ni mengi, hakuna sababu ya sisi kugombana. Viongozi ama tuseme watu wanapokaa kwenye madawati yao wasiwe wanakaa pale wanakuwa kama obstacles, watu wamekaa tu! Mtu akishakaa anakuwa bwanyenye kazi yake ni kuzuia watu wengine wasi-develop, wanakosa nafasi ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kila mmoja kwenye nafasi yake awe ni chachu ya mtu mwingine kunufaika na chochote ambacho kinapatikana kwenye nchi hii na asikae pale anakuwa kama kizingiti kuzuia mtu. Kuna wivu sana wa kimaendeleo kwenye nchi hii. Kwa hiyo tusaidiane, vijana wapewe nafasi na vijana wako wengi na hawana kazi, tutengeneze ajira ili watu waweze kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ni Shirika la Nyumba na Mheshimiwa Angela Kairuki hapa inaweza ikamhusu pia. Tunawapeleka Walimu, Madaktari, na Manesi vijijini; maeneo yetu mengine kwa kweli ni maeneo ambayo si mazuri kwa maisha ya binaadamu. Kule hakuna nyumba, hakuna maji. Kuna kata zangu nyingine kwa kweli ni za ajabu sana, hakuna barabara, hakuna umeme, hakuna maji, Kata za Bwawani, lakini bado kuna shule kule, kuna zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwomba Mheshimiwa Waziri Shirika lako la Nyumba, ikiwezekana lifanye makubaliano, sisi Halmashauri ya Arusha DC tuko tayari kama ataruhusu tuingie mikataba, watujengee nyumba nzuri kwa ajili ya wafanyakazi kwenye maeneo yale, halafu sisi kwa kutumia vyanzo vyetu vya ndani tuweze kuwa- fund, kuwalipa kama ni kodi, kama ni kulipa instalment ya kununua zile nyumba, pengine baada ya miaka 10 kadhaa hivi tutakuwa tumeshazinunua na wafanyakazi wanakuwa wako comfortable kule vijijini. Maana sasa hivi huwezi kumchukua mtu ana degree yake nzima, nzuri safi tu, hajachakachua cheti wala nini halafu unampeleka kwenye nyumba za udongo, nyingine hazina madirisha, hakuna umeme, hakuna solar, hakuna kitu halafu unataka afundishe shule yetu ya kata iliyoko kule! Kwa hiyo, wanapata shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Serikali iangalie utaratibu badala ya kujenga majumba tu mijini huku ambako tayari watu binafsi wamewekeza na nyumba bado si tatizo sana, tukawekeze hizi nyumba kwenye maeneo ambayo yana challenges nyingi ili nyumba ziwe nzuri, wataalam angalau wawe comfortable kwenda kufanya kazi vijijini na huduma ziweze kutolewa ambazo zinaeleweka kwenye vijiji vyetu. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba kwamba, miingiliano ile ya kwenye Wizara kidogo iwe controlled ili tuweze ku-enjoy matunda ambayo yako kwenye nchi hii. Kwa hiyo kwa leo niseme tu Mheshimiwa Waziri ningefurahi sana kama akinijibu yale maombi yangu ya Kata yangu ya Bwawani na wale ambao wanahitajika kufidiwa katika eneo ambalo jeshi limechukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na ningefurahi siku moja nisimame hapa nimsifu kama alivyosifiwa na akina Mheshimiwa Mdee; mimi bado hajanigusa, kwa hiyo naomba na mimi aniguse ili nikija hapa Bunge lijalo na mimi nimsifie kidogo. Arumeru tuna shida sana, nikimpa nafasi Mheshimiwa Nassari hapa ataongea mpaka asubuhi, ni kwa sababu ya ongezeko kubwa la wananchi katika Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tu watutanue, mapori yako mengi ambayo hayana hata mipango mingine hamna…

Yes! Tutanuliwe kule, kwamba yale maeneo ambayo yako wazi yanafaa kwa kilimo kwa sababu kiukweli hata sehemu za kuzikia siku hizi ni tatizo. Katika viunga vya Mji wa Arusha sasa hivi tunakwenda kuzikana Manispaa kwa sababu, ardhi imekuwa ni finyu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu machache kwa leo. Nakushukuru sana kwa kunipa fursa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuunga mkono maoni ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara hii. Kama alivyosema mwenzangu, Waziri achukue muda kwenda kupitia mapendekezo hayo kutoka Kambi hii, wataalam wetu wamepitia na kuja na mapendekezo ambayo yangeweza kumsaidia sana kuweza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuiasa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kufuata utawala wa sheria. Tutapona sana na itakuwa na manufaa makubwa sana kwa nchi yetu kama tutaongozwa kisheria. Hivi karibuni tumekuwa tukiongelea sana masuala ya Sheria zetu za Madini, kumekuwa na maneno ya ajabu ajabu kupinga wengine ambao wanatoa mapendekezo lakini tunashukuru kwamba kwa namna fulani Serikali imechukua mapendekezo ya baadhi ya watu ambao wanaitwa waropokaji na sasa tunaona kwamba sheria hiyo inataka kuletwa hapa Bungeni kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba wataalam wetu wa sheria, Waziri wetu wa Sheria asisite kutumia rasilimaliwatu walioko upande huu katika kuleta marekebisho ya Sheria hiyo ya Madini ili tuweze kupata sheria ambayo italinusuru Taifa hili katika kutokupoteza rasilimali madini tuliyonayo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sitasita kumshukuru Mheshimiwa Lissu kwa uelewa wake katika eneo hili. Ningependa kama inawezekana Serikali bila kuona aibu isisite kuchukua maarifa ambayo wataalam au kwa watu ambao wamebobea kwenye maeneo hayo wakatengenezea kitu ambacho tukija hapa kama ilivyo desturi yetu tutapitisha tu kwa ‘ndiyo’ tupitishe kitu ambacho kimefanyiwa kazi vizuri na kiko balanced ili tuweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Maazimio yalikuja hapa ya kumpongeza Rais, lakini mimi niseme kwa uelewa wangu msingi mkubwa wa hasara ambayo tumeipata kwenye madini na matatizo yote haya yamejikita kwenye Katiba yetu, ni sheria lakini na Katiba pia. Ningekuwa mtu wa kwanza kabisa, tena na kubeba mabango ikiwezekana nitaingia huku na vuvuzela kumpongeza Rais kama angetuletea Mapendekezo ya Warioba, ile Rasimu ya Pili ya Warioba ikaletwa hapa Bungeni tukapitisha kama Katiba yetu. Tutakuwa tumelitatua hili tatizo pale kwenye kiini chake lakini haya mazingaombwe ambayo naona yanataka kufanyika hapa katikati hayatatufikisha popote kwa sababu msingi wa makosa yote umejikita sehemu ambayo hatutaki kuigusa. Kwa hiyo, mimi ningeomba tukali-attempt hili maana Wazungu wanasema you can not solve a problem with the same mind that created it. Nasema kwamba tuilete Katiba, tuibadilishe hapa, tutakuwa tumetatua kwa kiasi kikubwa sana mlolongo wa haya matatizo ambayo yako kwenye sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme hivi karibuni kumekuwa na kulipukalipuka kwa watu kutekeleza mapendekezo au tuseme sheria mbalimbali zilizopo. Hivi majuzi nimeona watu wakiingilia kwenye mashamba ya wawekezaji tena moja la Mwenyekiti wetu, wakaenda wakafanya uharibifu mkubwa. Nasema huko ni kukurupuka na tukikurupuka tutaipeleka nchi hii kama walivyosema wenzangu, wataipeleka kama ilivyo Zimbabwe sasa hivi ambako wote tunafahamu kwamba Zimbabwe haitumii currency yake sasa hivi kwa sababu, kwa bahati mbaya neno ambalo lilikuwa linakuja sio zuri, wamejiharibia wenyewe. Ilifika wakati wanaenda kununua kilo ya sukari kwa mfuko wa fedha na sasa hivi wanatumia fedha za kigeni kama bill of exchange kwenye nchi yao. Sasa tukikurupuka kurupuka na sisi kwenda kuvamiavamia watu nadhani tutaishia pabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ambayo yana sifa kama alilokuwa nalo Mheshimiwa Mbowe yako mengi sana na kama Wakuu wengine wa Wilaya wao hawatatekeleza kama alivyotekeleza yule pengine siku moja wendawazimu wengine kama sisi au mimi tutaenda kuwasaidia kuharibu. Maana katika Wilaya yetu ya Arumeru wawekezaji wenye mashamba ya maua ambayo yamekaa pembezoni mwa maji au mito ni karibu mashamba yote lakini sijui ni nani huyo na akili zake ziko vipi amekurupuka ameenda kuvunja shamba la Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mienendo kama hii haitatupeleka pazuri. Kama ni operesheni ya kuondoa mashamba ambayo yako pembezoni mwa mito basi mashamba mengine yote ya maua, miwa, mpunga nafikiri ni vyema yakahakikiwa na yenyewe ili hii kama ni sheria basi ile pande zote lakini tuwe na tahadhari, tusije tukaipeleka nchi yetu kwa akina Zimbabwe na Venezuela. Nilitaka niseme hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka kwenda kwenye bajeti nianze kwa usemi wa mwanamuziki hayati Bob Marley maarufu kwa taste ile ya reggae, aliwahi kuimba kwenye wimbo wake wa get up, stand up akasema, you can fool some people sometimes but you can not fool all the people all the time. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti iliyoletwa hapa inataka kututegatega. Watanzania wa sasa hivi ni werevu sana, tusidhani ni kama wale watu wa miaka ya 60, 70, watu wamezidi kujanjaruka kwa hiyo huwezi kutudanganya. Nimwombe tu Waziri wa Fedha hili suala mnalosema elimu bure kwa bajeti hii tuanze kulifuta kwa sababu umedanganya kwa upande huu halafu sasa kwa upande huu unakuja ku- balance. Watoto wengi ambao wanasoma kwenye shule zetu za msingi ni zile familia ambazo kiukweli hata umeme wanausikia tu hawajawahi kuuona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapowawekea hizi Sh.40/= kwa kila lita moja ya mafuta hao ni kwamba unaenda kuwatoza zile hela zako ulizosema elimu bure, kwa hiyo tuifute. Utapitisha bajeti yako hii kwa Sh.40/= kwa kila lita moja ya mafuta ya taa, nazungumzia mafuta ya taa, petroli na dizeli tutajua huko mbele lakini mafuta ya taa, maana yake ni kwamba unakwenda kuwatoza Watanzania ile pesa ya ada ya shule waliyokwenda kuilipa, ndiyo maana yake na wajanja wameshajanjaruka. Kwa hiyo, hapa hamna elimu bure, you are charging us. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri mwaka jana tulizungumza mengi kuhusiana na bandari.

Walikwenda pale wakasema hata zikiingia meli mbili kama zile nyingine haziingii, sasa kule kumetetereka amekuja hapa anatuambia kwamba uchumi wa dunia umeyumba, sio kweli! Siku hizi tunakaa na simu zetu hapa, tunaangalia Beira, Mombasa, Tanzania sasa hivi Bandari yetu ya Dar es Salaam inakaribiana na Kismayo Somalia kule kwenye ma-pirates kwa jinsi ambavyo hakuna meli sasa hivi. Sasa wasituambie kwamba uchumi umetetereka, hapana! Walizinyima hizo meli jana kuja na tuliwaambia wakakataa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia tena kuhusiana na VAT kwenye utalii, wameleta ndege sijui nani atazipanda hizo Bombadier ambayo tunajua moja tayari iko grounded na ilikuwa mpya. Hawawezi wakaleta ndege, apande nani wakati utalii huku kwao wana-discourage? Wenzetu wa nchi za jirani wamefuta VAT, wao wamekomalia. Sasa utalii utaanguka halafu mwakani atakuja kutudanganya kwamba kuna mtikisiko wa kiuchumi. Hii tunai-note na mwakani sijui atatuambiaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii naomba tunapo-set priorities tuzisimamie. Rais alipokuwa anaomba kura hata na sisi wote tatizo la maji tuliliona tumeli-address na akasema anaenda kuleta suluhu ya shida ya maji nchini. Hata hivyo, wameingia madarakani cha ajabu ni kwamba hela nyingi wamezipeleka kwenye kuleta ndege mpya ukilinganisha na walizozipeleka kwenye maji. Pesa za kununua ndege zimezidi karibia bilioni 50 pesa walizopeleka kwenye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida ya maji, Arumeru yangu tuna kiu sana ya maji tuangalie priority zetu, tunapopata fedha tusikengeuke, twende kwenye zile areas ambazo tulisema kwamba tunaenda ku-accomplish. Kwa hiyo, naomba tu-stick kwenye bajeti kama tulivyokuwa tumeipendekeza ili tuweze kumaliza kero nyingi ambazo wananchi wanazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida sana, tunahitaji barabara, mwaka jana swali langu moja lilijibiwa na Naibu Waziri, nafikiri ni wa Ujenzi, akasema kwamba barabara yetu inayounganisha Arusha na Simanjiro inafanyiwa upembuzi yakinifu. Walisema shilingi milioni 600 imeshapelekwa pale isije ikawa tena miaka mitano. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja. Ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, labda ni-declare interest kwamba ni mfanyabiashara wa utalii takribani miaka 20 sasa.

Mheshimiwa Spika, sitatofautiana na wengi ambao wamenitangulia kwa maeneo mengi niseme wameni-pre- empt some how. Lakini niseme idadi ya watalii tunayoipata nchi hii ni ya kusikitisha sana. Ni watalii wachache sana ukilinganisha na uzuri na natural gift ambayo tumeijaliwa kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema ni wachache kwa sababu kuna nchi kama Thailand ambayo haina kabisa vivutio ambao naweza kusema wana robo tu ya tulichonacho sisi. Wao wanapata watalii milioni 35 kwa mwaka na wanaongezeko la watalii milioni moja na nusu kila mwaka. Sisi ongezeko letu ni tena kwa namba ya kuchakachua maana yake Mheshimiwa Dkt. Chegeni hapa amenigusa mahali. Kila siku tunaambiwa hapa tunaambiwa hapa imeongezeka lakini kiukweli mahoteli yetu yanalala bila wageni. Sasa tunashindwa kuelewa hawa wageni wanaoongezeka huwa wanakwenda kulala wapi. Sasa wanaongezeka angalau kwa namba hizi za kuchakachukua 100,000 kwa mwaka. Kwa hiyo, ili tuweze kufika watalii milioni tatu kwa mwaka tunahitaji miaka at least 15. Thailand kila mwaka wanaongezeko la watalii milioni moja na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ulinifurahisha sana juzi uliposema kwamba hatuwezi kuwa na Mawaziri ambao wanakaa tu humu bila kwenda nje kujifunza. Basi kama kuna mmoja ambaye anatakiwa ahamie huko ili akajifunze kweli kweli sio kutalii kwenda kujifunza kweli kweli ili tujue kwa nini Thailand wao kwa miaka kumi wameongeza watalii zaidi ya milioni 15. Sisi tunahitaji miaka 15 ili kuongeza watalii milioni moja na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kiukweli tuwapigie chepuo hawa wakajifunze, Thailand wanafanyaje mpaka wapata watalii kiasi hicho. Sisi na uzuri wote huu tumezidi kulia lia tu na hii nchi tumekuwa wa ajabu sana kila mahali tunalia, kila sekta tunalia, wakulima wanalia, wavuvi wanalia kama watu walivyosema hapa na sisi humu Bungeni tunalia. Sasa mpaka wakati mwingine tunashindwa.

Mheshimiwa Spika tusaidie kama kuna kitu tunaweza kufanya ili hivi vilio vipungue kwenye nchi hii basi tufanyeni kama Wabunge kwa sababu kulia kumezidi. Unda, wamesema watu hapa hizi sekta zote ambazo zinamatatizo ambao Wabunge wengi tumekubaliana humu ndani ikiwezekana unda tume mbalimbali ili tufanye kazi yetu kama Wabunge tuunde tume mbalimbali kwa kila Idara ambayo tumeona kwamba tumekubaliana humu ndani ili ukafanyike upembuzi yakinifu na tuje hapa na maamuzi ya Kibunge ili kulia lia kuishe humu ndani ya hii nyumba, tunalia tu toka mwaka juzi. Kwenye Wizara hii ya Maliasili kwa miaka mitatu mfululizo tumekuwa tukilia hivi hivi na inaelekea tutaendelea kulia mpaka mwisho wa maisha yetu ni kulia tu humu ndani. Ifike mahali tuchore mstari, maamuzi yafanyike ili tuone kama yanaweza kuleta mabadiliko yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Kigwangalla na wenzake pengine na Wabunge humu ndani iundwe tume tukaifanyie ovehaul hii idara ya Utalii ili tuweze kufaidika maanake utalii huu unaweza kutumalizia shida nyingi sana katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nimwombe Mheshimiwa Waziri sasa nilishamwomba Waziri aliyekuweko hapo kabla kwamba mwaka jana mwanzoni mliweza kuwapiga watu wangu watano risasi mkawaua na wengine zaidi ya nane kujeruhiwa na mmojawapo ni mtoto ambaye amepata ulemavu wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, watu hawa toka wameuawa baada ya msaada wa mazishi hamjaenda kwenda tena kuwaona wala hakuna kifuta machozi. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri ukawaone watu wale na uwafute machozi ikiwezeka na tukio hilo lisirudie tena kwa sababu kwa kweli hali ilikuwa ni tete wakati ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Nianze kwa kusema kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo ya viwanda na biashara lakini pia mimi ni mjasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye vikao vyetu hivyo vya Kamati wakati mwingine tunapatwa na bumbuwazi kwa jinsi ambavyo kero hizi ambazo wafanya biashara na wawekezaji wanazipata katika nchi yetu. Kwa kweli hali ni mbaya ya kibiashara sasa hivi nchini na sisi humu ndani tumezidi kulia. Tumekuwa kama watu wa kulia tu na narudia kusema kwa sababu nimeshasema hivyo kipindi cha nyuma, ifike mahali tuisaidie Serikali na tuisaidie nchi yetu humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wamechangia kwa masikitiko sana humu ndani ya Wizara hii, sasa ufike wakati baadaye wakati tunapitisha hapa tumsaidie Waziri, baadhi ya kero hizi ambazo wafanyabiashara wamekuwa wakilia zitatuliwe humu humu ndani, tusiipitishe hii Bajeti leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wanalalamikia sana, kwa mfano, suala la ETS hizi electronic stamp, ni kazi ya TRA lakini wanaogharamia ni wazalishaji, kwa nini msilipe wenyewe? Kwa sababu hizo stamp ni kwa faida yenu nyie kujua production za viwandani. Wanalalamika kwamba hizi fedha ni nyingi zinasababisha wanashindwa kukuza mitaji yao. Leo Waziri na Serikali humu ndani ifute hiyo ili tuweze kusonga mbele. Wengine wanasema hata matangazo ya biashara zao wanaweka mabango barabarani, TRA wanakusanya kama ni maeneo ya TARURA na wenyewe wanakuja wanakusanya fedha, sasa hawa watu watakuza mitaji yao lini? Kama inawezekana achaji mmoja mwingine abaki, kwa sababu TRA na TARURA ni organ ambazo zinaweza kufanya kazi pamoja kwa nini wanadaidai wafanyabiashara? Hivi viwanda vyetu vya ndani visipotangaza biashara zao watapataje masoko? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Komu hapa, kama siyo yeye ni nafikiri ni Mheshimiwa Japhary alisema ng’ombe ili aweze kupata maziwa lazima umlishe, lakini sisi hapa hatuwasaidii wafanyabiashara, tunawakwamisha na in fact na hali ya nchi yetu sasa hivi Kimataifa siyo nzuri kwa maana ya uwekezaji, is not good. Sasa tunaongea, tunalia halafu tukiondoka, mwakani tena tunaendelea hivyo hivyo. Nashauri kwamba Bunge hili leo liisaidie Serikali, tuwasaidie wananchi wetu, tuna vijana wengi wanamaliza Vyuo Vikuu kama wenzangu walivyotangulia kusema, hatujui wakitoka hapo wanakwenda wapi. Uwekezaji tunau-discourage badala ya kuu-promote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba kwamba leo tumsaidie, maana najua alikuwepo hapo Mheshimiwa Charles sasa hivi tunaye Kakunda, kuna wakati unaongea anakuangalia tu. Kuna namna hawawezi, wanashindwa, hawana cha kufanya. Kuna wakati umefika hapa tukafikiria pengine na wafanyabiashara wa nchi hii tuwakutanishe na Rais ili baadhi ya kero wazimalize pale pale on the spot maana yake hapa ndani tunaona tunazungusha tu, muda unakwenda, hakuna uwekezaji, tunaendelea kuzalisha vijana, hawapati ajira, sasa naona sisi kama Wabunge tuna nafasi yetu hapa badala ya kulialia tu tunaweza tukahitimisha haya mambo humu humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hapa Waziri wa Fedha atuambie ETS wanaifanya vipi, habari ya mabango na kero nyingine hizo za kodi ambazo zimetamkwa hapa ndani, hizo kodi tu-harmonize akina OSHA na nashukuru Rais alivyokuwa kusini mwa nchi hii alishangaa nay hii OSHA maana yake ni nini. Anatoka OSHA, anaingia sijui mtu wa levy, msururu wa watu, kila siku wapo maofisini kwa watu. Wawekezaji tulionao hapa nchini kama hawatuzungumzii vizuri hatutapata wawekezaji wapya. Ni lazima tuhakikishe hawa tulionao tunawa-contain vizuri ili wanapoulizwa kuhusu uwekezaji Tanzania waweze kutu-advertise, waweze kuitangaza Tanzania kama ni sehemu nzuri ya kuwekeza, lakini sasa hivi tunapata negative comments kwamba Tanzania siyo sehemu nzuri ya kuwekeza. Sasa tutakwenda wapi na watoto ambao tunawazaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa zetu za ndani; najaribu kupata picha hivi watu wote humu ndani tungekuwa Wamasai tukawa tunavaa yale mashuka ya Kimasai ni viwanda vingapi vingekuwepo sasa hivi Tanzania vingekuwa vinajaribu kutuvalisha hizo nguo? Humu ndani tumevaa masuti tu hizi siyo products za Tanzania. Ifike mahali tuwe na utashi wa kisiasa na tuanzie humu Bungeni. Hebu tuondoeni haya matai tai na masuti ambayo ni ya kuagiza tuvaeni nguo za kwetu... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)