Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Thea Medard Ntara (15 total)

MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Taifa Kusini mwa Tanzania na Kanda nyingine ambazo hazina Vyuo Vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea M. Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taratibu za uanzishwaji wa Vyuo Vikuu vya Umma hazilengi kuanzisha Vyuo Vikuu vya Kikanda, Kimkoa au Kiwilaya. Vyuo Vikuu vilivyopo nchini, vikiwemo vya Serikali na Binafsi, vinapokea wanafunzi kutoka Kanda zote za Tanzania Bara na Visiwani; na kutoka nje ya nchi. Huu ndio utaratibu wa Vyuo Vikuu Duniani kote. Katika Kanda ya Kusini kuna vituo vitatu vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) vilivyopo katika Makao Makuu ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Aidha, kipo Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris STeMMUCO kilichopo Mkoa wa Mtwara na Taasisi ya Uhasibu Tanzania TIA Kampasi ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mpango wa Serikali ni kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia. Tunafanya hivyo ili kuongeza nafasi za udahili na ubora wa elimu itolewayo na hivyo kukidhi mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Sheria ya Ajira na kuweka mazingira mazuri ili maprofesa wa kigeni waweze kufanya kazi nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuboresha utoaji ajira kwa wageni ilitunga Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni, Namba 1 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Kuratibu Ajira za Wageni za mwaka 2016 ili kuratibu ajira za raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini ikiwa ni pamoja na kulinda ajira za wazawa na kuruhusu ujuzi adimu kutoka nje kuingia na kurithishwa nchini. Serikali kwa sasa inaendelea na mapitio ya sheria ili kuifanyia maboresho kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, ili kuweka mazingira mazuri ya kuruhusu uwepo wa wafanyakazi wa kigeni nchini, Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na ukaazi kwa raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini na mfumo husika umeanza kutumika kwa majaribio (piloting) kuanzia tarehe 23 Aprili, 2021. Mfumo huu utaongeza Ufanisi katika kushughulikia maombi husika.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu pia utaondoa changamoto ya upatikanaji wa taarifa unganishi za kisekta za kurahisisha upatikanaji wa vibali vya wageni wakiwemo Maprofesa kwa wakati kwa kuzingatia uhitaji.

Mheshimiwa Spika, kulingana kwa taarifa zilizopo mpaka sasa jumla ya vibali vya kazi 74 vimetolewa kwa Maprofesa na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania na vinginevyo.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kusomesha Wahadhiri wengi zaidi katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (Ph.D) kwani waliopo sasa ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango mkakati wa kuongeza rasilimaliwatu katika taasisi za elimu ya juu ikijumuisha wahadhiri, wakutubi na wataalamu wa maabara na karakana ili kukidhi mahitaji ya viwango na ubora wa Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwezi Julai, 2021 Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) ina mpango wa kusomesha jumla ya wahadhiri 430 katika kipindi cha miaka mitano (2021-2026) ili kukabiliana na upungufu huu katika fani za kipaumbele (Priority Programs) katika vyuo vikuu vya Serikali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mpango huo mahsusi, vyuo vikuu navyo vinaendelea kusomesha wahadhiri wao kupitia vyanzo vingine, ikiwemo mikataba ya kitaalam ya utafiti (collaborative research projects) na scholarship mbalimbali tunazopokea kutoka nchi rafiki ambapo wahadhiri hupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mipango hiyo, Jumla ya wahadhiri 621 katika ngazi ya shahada ya Uzamivu (PhD) na 241 katika Shahada ya Umahiri wanaendelea na masomo. Aidha kwa mwaka wa masomo 2021/2022 jumla ya wahadhiri 48 wanaendelea na masomo katika nchi mbalimbali. Kwa mfano katika nchi ya China wapo wanafunzi au wahadhiri 30, Uingereza 12 na Hangaria wahadhiri sita. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika sekta ya kilimo kwa kuwa mikopo ya elimu ya juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu zinaongezeka hususan katika sekta ya kilimo, Serikali imetekeleza mipango ifuatayo: -

(i) Kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini, ambapo jumla ya vijana 12,580 katika Mikoa 17 nchini, wakiwemo wahitimu wa fani ya kilimo wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na sasa wapo tayari kuanza biashara ya kilimo na kutumia teknolojia na ujuzi wa kitalunyumba.

(ii) Kuwezesha wahitimu kupata uzoefu wa kazi nje ya nchi (internship), ambapo Serikali kwa kushirikiana na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO), wamewezesha wahitimu 703 kwenda nchini Israeli na Marekani. Kati ya hao, wahitimu 311 wamerudi nchini na wamejiajiri katika maeneo mbalimbali nchini.

(iii) Kupitia Benki ya TADB na mikopo ya Halmashauri, baadhi ya wahitimu waliopatiwa mafunzo nje ya nchi wamepatiwa mikopo ya jumla ya Shilingi Milioni 170 na wanaendelea na shughuli hizo.

(iv) Kupitia Vituo vya Uatamizi kwa wahitimu (Incubator Centres) katika Mikoa ya Morogoro na Pwani, wahitimu 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uanzishaji shughuli za kilimo na ujasiriamali na;

(v) Kupitia kilimo cha vizimba (block farming), wahitimu 39 wamepatiwa fursa ya kuanzisha shughuli za kilimo. Kati ya hao, wahitimu 30 wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la hekari 1,500 lililopo Mkoani Morogoro Mvomero. Aidha, wahitimu Tisa wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la kahawa Mkoani Songwe.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wahitimu wengi zaidi wanaendelea kuwezeshwa kuajirika lakini pia kujiajiri, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 54 ili kuwawezesha wahitimu 1,500 kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi ikiwemo fani ya kilimo. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa Wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika Sekta ya Kilimo kwa kuwa mikopo ya Elimu ya Juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu zinaongezeka hususan katika sekta ya kilimo, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo: -

(i) Mpango wa Taifa wa Kukuza Ujuzi nchini ambao unatoa mafunzo ya ujuzi na uzoefu katika kilimo cha kisasa cha kutumia teknolojia ya vitalu nyumba. Kupitia mpango huo, hadi sasa jumla ya vijana 12,580 wakiwemo wahitimu wa fani ya kilimo wamepatiwa mafunzo ili waweze kujiajiri;

(ii) Mpango wa mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship) kwa wahitimu wa elimu ya juu nchini kupitia waajiri wa ndani na nje ya nchi, ambapo jumla ya wahitimu 6,624 wamepatiwa mafunzo husika;

(iii) Mpango wa Vituo vya Uatamizi kwa Wahitimu (Incubation Centres) ambao tayari umeanza kutekelezwa katika Mikoa ya Morogoro na Pwani. Hadi sasa, jumla ya wahitimu 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uanzishaji wa shughuli za kilimo na ujasiriamali;

(iv) Mpango wa kilimo cha vizimba (Block Farming), ambapo tayari wahitimu 39 wamepatiwa fursa ya kuanzisha shughuli za kilimo katika mashamba mbalimbali nchini;

(v) Mpango wa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu, ambapo Serikali kwa kushirikiana na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO) imewawesha wahitimu 703 kwenda nchini Israel na Marekani kupatiwa mafunzo katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeanzisha Mpango mpya uitwao ‘Building a better Tomorrow’’ unaowalenga vijana wahitimu na wasio wahitimu. Katika mpango huu, Ofisi ya Waziri Mkuu itakua na jukumu la kuwapatia mafunzo vijana hao na Wizara ya Kilimo itakua na wajibu wa kutoa ardhi, mitaji, kuweka miundombinu katika mashamba tengwa ya Agro Parks/Blocks pamoja na kuwaunganisha na masoko. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaridhia Mkataba Na.189 wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P.
KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Mkataba huu wa Kimataifa wa kuhusiana na haki za wafanyakazi wa majumbani haujaridhiwa ambapo Serikali inafanya tathmini ya kina kuona kama kuna umhimu wa kuridhia na kuwa masuala mengi yaliyoko katika Mkataba huu yanatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019. Aidha, siyo kila Mkataba wa Kimataifa unaridhiwa. Tunaridhia mikataba ya msingi (Core Conventions) ambapo kwa Mikataba isiyo ya lazima (Other Conventions) uridhiaji wake utazingatia mila, desturi na hali ya uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushauriana na wadau katika suala hili. Nitumie fursa hii kuwaomba wadau kuendelea kutoa maoni ya njia bora ya kuendelea kuboresha maslahi na haki za wafanyakazi wa majumbani kwa kuzingatia mila, desturi na hali ya nchi yetu. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni Vyuo Vikuu vingapi vimepewa fursa ya kuajiri watumishi wake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo Vikuu kama zilivyo taasisi nyingine za Umma huajiri watumishi baada ya kupata vibali vya ajira kutoka Wizara yenye dhamana na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumla ya Vyuo Vikuu vya Umma 13 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2018-2019 mpaka 2020/2021) vilipata vibali vya kuajiri watumishi 618 ambapo wanataaluma ni 333 na waendeshaji ni 285.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fursa hizo za kuajiri watumishi zilizotolewa, bado Serikali inaendelea na taratibu za kuwahamisha watumishi wenye sifa kutoka sehemu mbalimbali kujiunga na utumishi katika Vyuo Vikuu. Aidha, Serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira katika Vyuo Vikuu kwa lengo la kuviongezea fursa ya kuajiri watumishi kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatangaza kima cha chini cha mishahara kwa Wafanyakazi wa Serikali na mashirika binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa kima cha chini cha mshahara kwa sekta ya umma kilitangazwa tarehe 13/5/2022 na utekelezaji wake ulianza tarehe 1 Julai, 2022. Kwa upande wa sekta binafsi kima cha chini cha mshahara kilitangazwa tarehe 25/11/2022 kwenye Gazeti la Serikali Na. 687 baada ya Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara kukamilisha utafiti na kutoa mapendekezo ya viwango kwa Sekta Binafsi ambayo yaliridhiwa na Baraza la Ushauri kuhusu Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO). Utekelezaji wake unaanza rasmi Tarehe 1 Julai, 2023.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuamua kuwa wasichana wasiolewe chini ya miaka 18?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatvyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inatambua mtu mwenye umri chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto, hivyo ni kosa la jinai kumuhusisha na mahusiano ya kimapenzi pia kumuozesha. Kwa upande mwingine Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu mtoto wa kike kuingia kwenye ndoa akiwa na miaka 14. Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeshakusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu upi ni umri sahihi wa kuoa na kuolewa.

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa maoni hayo umeshakamilika na yatawasilishwa ndani ya Bunge ili yajadiliwe na mabadiliko kufanyika kadri Bunge litakavyoona inafaa ili kumlinda mtoto wa kike afikie ndoto zake. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vyenye taaluma ya sayansi na tiba vinakuwa na hospitali za kufundishia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKINOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara Mbunge wa Viti Maalaum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala ya Mafunzo ya Sayansi ya Utabibu (Medical and Health Training) vyuoni hutekelezwa kwa mafunzo ya nadharia na vitendo ambavyo hufanyika katika hospitali zenye wagonjwa halisi. Kwa vyuo ambavyo havina hospitali za mafunzo kwa vitendo, upo utaratibu wa makubaliano kati ya vyuo na hospitali za rufaa, mikoa, wilaya pamoja hospitali za watu binafsi zenye kukidhi vigezo kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo kufanya mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vikuu vyenye taaluma ya sayansi na tiba kuwa na hospitali za kufundishia; ambapo kwa sasa inaendelea na ujenzi wa Hosipitali ya Mloganzila kama hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kujenga hospitali za kufundishia katika vyuo vikuu vingine vyenye taaluma ya sayansi na tiba ambavyo havina hospitali hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta muswada wa sheria ya adhabu kali kwa wanaobaka na kulawiti watoto na wanawake?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa vifungu 130, 131, 131A na 154 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, ni makosa ya jinai kwa mtu kubaka na kulawiti. Makosa yote haya adhabu yake ya juu ni kifungo cha maisha jela, na adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela. Aidha, kwa makosa yote hayo yakitendeka dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela. Pamoja na adhabu hizo, Mahakama ina mamlaka ya kutoa amri ya ziada ya kumlipa fidia mwathirika chini ya kifungu cha 131(1) cha Kanuni za adhabu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Bunge, inafanya utafiti zaidi ili kuona kama kuna hitaji la kufanya maboresho au marekebisho ya sheria hiyo, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia wapi katika mpango wake wa kurudisha Reli ya Mtwara – Mbamba Bay na eneo la Mchuchuma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu ilipendekeza kuwa mradi huu utekelezwe kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP).

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kuwa marekebisho ya Sheria ya PPP yatakayofanyika hivi karibuni yatasaidia kuwapata wawekezaji kwa ajili ya kujenga reli hii muhimu. Naomba kuchukua fursa hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mtwara na Ruvuma kuwa na subira wakati Serikali inashughulikia kwani suala hili litapewa kipaumbele na Serikali katika mwaka 2023/2024 ili kukamilisha taratibu za kumpata mjenzi, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanafunzi wote waliomaliza kidato cha sita wanapata mkopo wa elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka hadi mwaka ili kuongeza wigo wa wanufaika. Bajeti ya mikopo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 570 mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 654 mwaka 2022/2023. Pia mwaka 2022/2023 shilingi bilioni tatu zilitengwa kwa ajili ya Samia Scholarship iliyonufaisha wanafunzi 593 waliohitimu kidato cha sita wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kupanua fursa za mikopo kwa wahitimu wa kidato cha sita, Serikali imeingia mkataba wa mahusiano na Benki ya NMB ili kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia tisa kwa wazazi/walezi kwa ajili ya kugharamia elimu ya watoto wao katika ngazi ya elimu ya juu na kati. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fursa za mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mhitimu wa kidato cha sita mwenye sifa anapata mkopo kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu, nakushukuru.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, nani anahusika kukamilisha ujenzi wa viwanja vya michezo Nelson Mandela University ili shughuli za michezo ziendelee?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanja vya michezo katika Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia umefanywa na Mkandarasi Elerai Construction Company Ltd. chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi. Hata hivyo, wakati ujenzi unaendelea kulijitokeza dosari na hivyo ujenzi haukukamilika na kusimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ndiyo inayohusika na ukamilishaji wa ujenzi huo. Hivyo mwezi Machi, 2021 Wizara iliitisha kikao cha wahusika wote wa mradi huo ambao ni Wizara ya Fedha na Mipango, Pension Property Ltd., Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia, Mshauri Elekezi na Mkandarasi kujadili suala hili. Katika kikao hicho ilikubalika kuwa Chuo Kikuu cha Ardhi kiendelee kumsimamia mkandarasi Elerai na kuhakikisha anakamilisha kazi ya ujenzi wa viwanja hivyo. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itathibitisha Mkataba Na. 189 wa Wafanyakazi wa Majumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kuridhia Mkataba Na. 189 ulianza mwaka 2011 hadi 2016 ambapo ulifika hatua ya kuridhiwa kwa kuwasilishwa Bungeni. Hata hivyo, kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi na utekelezaji wa Mkataba tajwa, iliamuliwa kuwa wadau waendelee kupewa elimu kuhusu Mkataba huo kabla ya hatua za uridhiaji kuendelea. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani CHODAWU imetoa elimu kuhusu Mkataba husika kupitia Makongamano na vikao 90 ambao ni wafanyakazi wa majumbani, Viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali imeanza hatua ya uchambuzi wa Mkataba Na. 189 kwa kupitia Sheria na Kanuni zinazosimamia wafanyakazi wa majumbani. Baada ya hatua hizo na mapitio kukamilika, hatua inayofuata ni ya kushirikisha wadau kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu maeneo ambayo Serikali inapendekeza kuridhia katika mkataba husika. Aidha, Serikali itazingatia umuhimu wa vipengele vya mkataba ambavyo vitazingatia mila, desturi na uwezo wa nchi katika kutekeleza Mkataba husika, ahsante. (Makofi)