Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mariam Madalu Nyoka (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MARIAMU M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kwani ni mara yangu ya kwanza leo kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuiona siku hii ya leo. Pili, naomba niwashukuru wazazi wangu, familia yangu, watu wangu wa karibu, Chama changu cha Mapinduzi na wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kunipa moyo na kuniamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Awamu ya Tatu wa miaka Mitano 2021/2022 - 2025/2026 wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Katika Mpango huu, mambo muhimu yamezingatiwa kama kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapitio ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 na 2020/ 2021, tumeona jitihada kubwa za Serikali za kuwashirikisha wanawake katika nyanja mbalimbali ili kuleta usawa na kuondoa ukatili wa kijinsia, kuongeza fursa za kiuchumi, kuwajengea uwezo wa kufanya biashara, upatikanaji wa mitaji, upatikanaji wa masoko na upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa baadhi ya mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati sasa wanawake wa mikoa yote wapate fursa sawasawa wakiwemo wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ili na wao waweze kujikimu kimaisha pamoja na familia zao kwa kuwapatia mikopo hiyo yenye riba nafuu na fursa nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya Mpango wa Tatu, naomba kushauri mambo matatu yafuatayo. Moja, ianzishwe kanzi data itakayokuwa na vikundi vya wanawake nchini kimkoa ikionesha madaraja ya vikundi, mahitaji yao na namna ya kuyafikia mahitaji hayo kwa mfano mikopo yenye riba nafuu. Mbili, itolewe taarifa ya Benki ya Wanawake iliyohamishiwa Benki ya Posta, ni namna gani fursa za mikopo kwa akina mama zinatolewa kwa madaraja tofauti na fursa hizo zinapatikanaje kupitia benki hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nitamke kama ifuatavyo. Wanawake hawa ili waweze kuchangia uchumi wanatakiwa wajengewe uwezo wa kujiamini kwa kuendeleza juhudi zao za kujitegemea na hatimaye waweze kuchangia Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo ameendelea kuzifanya, naipongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri na bila kusahau Kamati ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Daniel Sillo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti yetu ni bajeti ambayo itaondoa changamoto nyingi za wananchi wetu. Hakuna Serikali inayotekeleza miradi yake bila ya kulipa kodi, hivyo niwaombe wananchi wenzangu tulipe kodi kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ni kwenye eneo la miradi ya kimkakati; miradi hii ya kimkakati ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba kila Halmashauri inajitegemea yenyewe kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali wakati wa upembuzi yakinifu wa miradi hiyo ni vyema tukawashirikisha wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kwenye maeneo hayo badala ya ilivyo hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa mfano Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Songea Mjini kuna mradi mkubwa wa mabasi kule umejengwa wenye umbali wa takribani kilometa 21, kama wananchi wale pamoja na wadau wake wangeshirikishwa mradi ule ungejengwa lakini sio kwa umbali ule. Hivyo niiombe Serikali kufanya ushirikishwaji jamii wakati wa utekelezaji na hiyo ndio dhana ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi viporo; ninaipongeza Serikali kwa kufanya mabadiliko ya Kanuni ya 21 ya Sheria ya Bajeti, Sura Namba 439 ya kuondoa urejeshwaji wa fedha za miradi kila ifikapo tarehe 30 Juni kila mwaka, na hivyo kusababisha fedha zile zitekeleze miradi yake kama ilivyokusudiwa. Niiombe Serikali kuhakikisha kwamba miradi ile iliyopangwa itekelezwe kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kuimarisha Kitengo chake cha Monitoring and Evaluation (Tathmini na Ufuatiliaji) kwa kuunda timu ya kikanda na ya kitaifa katika kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo, kila robo mwaka ikiwashirikisha Madiwani pamoja na Wabunge wa maeneo husika kwa kila sekta. Kwa kufanya hivyo tutajua tumetoka wapi, tupo wapi na tunaelekea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwisho ni kwenye eneo la ajira; ajira ni changamoto, asilimia 80 ya Wabunge katika kipindi hiki tumeshuhudia wananchi wetu wakitupigia simu za kuomba tuwasaidie kupata ajira. Ninaiomba Serikali yetu iweke uwiano katika utoaji wa ajira kwa kila Mkoa lakini kwa kuzingatia sifa za waombaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba nchi yetu hii ni kubwa sana na hivyo wananchi wake wapo vijijini na Mikoa ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama na kuchangia bajeti ya Serikali leo hii. Pili nimpongeze Mheshimiwa Rais Mpendwa, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kuzifanya. Pia, niipongeze Wizara ya Fedha ikiongozwa na Waziri wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na timu yake kwa bajeti nzuri ya Serikali na bila kusahau Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Daniel Sillo kwa bajeti yao nzuri ambayo imeendelea kutekelezeka na hatimaye kufikia muafaka hapo itakapopitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni bajeti ambayo itaondoa changamoto nyingi za wananchi wetu wakiwemo wananchi wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimba madini na makundi mengineyo. Pamoja na haya ninaomba nieleze kwamba, wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo Serikali hii haiwezi kutekeleza miradi yake bila wananchi hawa kulipa kodi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni eneo la miradi ya maendeleo viporo, eneo la pili miradi ya kimkakati na eneo la tatu ni eneo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo hili la miradi ya kimkakati. Miradi hii lengo la Serikali kuleta miradi ni zuri sana ambalo litaiwezesha kila Halmashauri kutekeleza miradi yake yenyewe wakati huo wakiwa wanajielekeza katika kukuza uchumi wa kila Halmashauri yake. Pamoja na lengo hili, dhamira ya Serikali ni nzuri, lakini utekelezaji wa miradi hii kule kwenye Halmashauri imekuwa ni kinyume na matarajio ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali wakati wa kufanya upembuzi yakinifu wa miradi hii ni vema tukawashirikisha wanancbhi wetu wa maeneo yale pamoja na wadau wa maendeleo wa kila eneo husika. Eneo hili la miradi ya kimkakati lina changamoto zake nyingi sana, changamoto hizo tumeona wakati miradi hiyo imeshakamilika na kuanza kutumika. Tukija mfano wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Songea Mjini, Mheshimiwa pale kuna changamoto kubwa sana. Mradi mkubwa wa kituo cha mabasi umejengwa lakini mradi huu unashindwa kufanya kazi vizuri kulingana na ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo yale pamoja na wadau wake wa maendeleo wa Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini ya kwamba, kama tungewashirikisha wananchi katika utekelezaji wa mradi ule, eneo lile la mradi uliojengwa kilometa 21 kutoka Songea Mjini usingejengwa mradi ule kule, badala yake mradi huu ungejengwa kwenye eneo rafiki na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma. Kwa kweli, wakati wa utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo ni vema dhana ya ushirikishwaji wa jamii iwe ni nyenzo muhimu katika dhana nzima ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo la miradi viporo. Kwanza niipongeze Serikali kwa dhamira yake nzuri ya kuweza kubadilisha eneo la Kanuni ya 21, Fungu Namba 439, ambalo changamoto hizo zitaondolewa kwa kutorejeshwa fedha katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na badala yake fedha hizi zitatumika kuendeleza miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa. Changamoto hii tumekuwa tukiipata kila mwaka kwenye kila Halmashauri, inapofika tarehe 30 ya Juni ya kila mwaka fedha hizi hurejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na badala yake miradi ile husimama au kutoendelezwa kabisa kwa changamoto ya kuwa hii imekuwa ni miradi viporo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuondoa changamoto hiyo na sasa miradi yote ya maendeleo itakuwa inatekelezwa kama ilivyopangwa. Niiombe Serikali sasa kuhakikisha ya kwamba, miradi yote ambayo imeanza kutekelezwa ikamilishwe kama ilivyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye eneo la ajira. Ajira ni changamoto hapa nchini. Kwa kipindi hiki chote ambacho tuko hapa Bungeni ninaamini ya kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Wabunge wamepigiwa simu na wananchi wao wakiomba kupata msaada wa kupata ajira. Wakati huo changamoto hii tunaweza kuitatua tu kama Serikali yetu itaweka uwiano wa ajira kwa kila Mkoa kwa kuzingatia sifa au vigezo vya muombaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu nchi yetu hii ni kubwa sana, lakini wananchi wake wengi wapo maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi. Hivyo, basi niiombe Serikali hii iweze kuhakikisha kwamba, wananchi walioko vijijini na maeneo ya pembezoni wanapatiwa ajira badala ya wananchi wale kuona usumbufu kubakia kule vijijini na kuona ni vyema waje mjini kwa ajili ya kutafuta ajira hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)