Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amb. Dr. Bashiru Ally Kakurwa (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kw akunipa nafasi ya kuongea katika Bunge hili tukufu kwa mara ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru pia kwa kunipa upendeleo wa muda wa dakika 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara ya kwanza kuongea, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuneemesha na kuivusha nchi yetu katika kipindi cha misukosuko baada ya kupata msiba mkubwa ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Na, nina uhakika Mwenyezi Mungu hatatutupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamekuwepo majaribio ya kupitisha maneno na kutuchonganisha na wakati mwingine kudhalilisha watu na kutunga maneno ya uwongo ili nchi itikisike lakini nasema wameshindwa na wamelegea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze viongozi wetu wapya. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu na Dkt. Isdory Mpango Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kushika barabara usukani na hatamu za uongozi wa Taifa letu na kutuwekea mazingira ya matumaini huko tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni Mbunge wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, na ni upendeleo mkubwa kwa sababu ziko nafasi 10 tu za Kikatiba na hadi sasa tuko nane. Nimshukuru sana kwa kuniamini na nimuahidi kwamba sitamuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe kwa kuongoza Bunge letu kwa weledi na kwa umakini na hasa kwa siku hizi mbili tangu jana na leo wakati Bunge hili linajadili bajeti ya Sekta Muhimu kwa uhai wa Taifa letu, Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia Wanasimba, Timu ya Taifa kwa kutufuta machozi angalau ya kurejesha mabao matatu kati ya manne. Niwape moyo haikuwa riziki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nianze kuchangia, tangu jana kusema ukweli nimeandika mengi katika notebook yangu na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo inayoongozwa na mama shupavu Mheshimiwa Dkt. Christina Ishengoma. Naweza nikasema kwamba sina jipya la kuongea, mengi yamezungumzwa. Baadhi yapo kwenye hotuba ya Waziri, mengine yapo kwenye hotuba ya Kamati. Kwa hiyo, nitakachokifanya ni kufanya muhtasari wa yale ambayo nimeyaona yanajitokeza moja kwa moja yanayohitaji kufanyiwa kazi na kamati yetu lakini pia na Bunge lako. Wabunge wamezungumza kwa uhakika, kwa uchungu lakini wametoa mawazo mazuri sana ambayo yanaweza yakatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri au mbaya ninaweza nikasema kilimo chetu kimepata sifa tatu katika mjadala wa tangu jana. Sifa zote tatu ni mbaya, ya nne ndiyo nzuri tu. Sifa ya kwanza ni kwamba kilimo chetu kwa kweli tija yake ni duni. Uduni wa tija hiyo unaathiri uzalishaji wa mazao yote ya kilimo. Hiyo sio sifa nzuri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tubadilishe sifa hii mbaya kwa kuongeza tija na wote tunakubaliana kuhusu sifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sifa ya pili ambayo imesemwa nzuri sana na ni mbaya pia ni kwamba mazao mengi ya kilimo yanayozalishwa yanauzwa bila kuongezewa thamani. Sifa ya tatu mbaya, ni kwamba kilimo chetu hakijapata masoko ya uhakika na yenye manufaa kwa wakulima. Sifa moja nzuri iliyojitokeza ni kwamba Tanzania imejaaliwa kuwa na wakulima wenye huruma, wenye hisani na uungwana, wanazalisha kwa shida na kunyonywa lakini wameweza kuzalisha chakula cha kutosheleza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kilimo chetu kinatuweka katika hali ya kuwa na usalama wa chakula. Hii sio sifa ndogo, tunapo mahali pa kuanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama sifa hizi tatu ndizo tunazotaka kuzibadilisha yamesemwa mengi mapendekezo ya kufanya. Wengine wameelekeza mawazo yao katika uongezaji wa bajeti ya kilimo, nakubaliana nao. Wengine wanataka tubadilishe mbinu zetu katika maeneo ya umwagiliaji, masoko n.k.

Mheshimiwa Spika, bila shaka ni ya kwanza hiyo maana mimi ni form one humu. (Kicheko)

SPIKA: Bado dakika mbili.

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachotaka kupendekeza ni kwamba Bunge lako la Kumi na Moja, limechangia sana kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Madini. Changamoto tuliyonayo kwa Bunge hili la Kumi na Mbili, ambalo nimepata bahati ya kuwa Mbunge, tujipe ajenda Bunge liweze kuwa na mchango wa uhakika wa kubadilisha Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge la Kumi na Moja, katika historia litatambulika kwa kuleta mabadiliko makubwa sana ya kisera na kisheria kwenye Sekta ya Madini na tumeona matokeo yake. Hili la Kumi na Mbili, chini ya uongozi wako na ndani ya Serikali chini ya mama Samia tujipe jukumu la kubadili Sekta ya Kilimo ili sifa hizi mbaya za tija duni, za ukosefu wa masoko na kutoyaongezea thamani mazao yetu ya kilomo zibadilike ili tufanane na Sekta zingine zinazobadilika haraka kama vile miundombinu, mawasiliano n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakuomba ama unaweza ukaelekeza Kamati yetu au kwa busara yako kufikiria namna ya kufanya kujibu maswali matatu yafuatayo. La kwanza, tunajifunza nini kutokana na mafanikio tuliyoyapata katika Sekta ya Kilimo lakini na makosa tuliyofanya katika Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mabadiliko huku nyuma yamefanywa. Tume ya Ardhi ilifanya kazi kubwa ikatusaidia kuweka msingi wa kusimamia ardhi yetu. Tume ya Umwagiliaji Awamu ya Tatu, hata Tume ya Ushirika Awamu ya Nne na Sera zingine. Tusikimbie kufanya mabadiliko bila kujiridhisha kwa kufanya tathmini, wapi tumefanikiwa na wapi tumefanya makosa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili la kuzingatia, Bunge hili la Kumi na Mbili linaweza kutoa mchango gani mpya katika kuchochea mapinduzi ya kilimo. Suala la tatu, tuweze kujibu hoja kwa nini mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini katika sekta za miundombinu, fedha, sayansi na teknolojia, ongezeko la watu, elimu, mawasiliano, havichochei ukuaji wa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake iliyogusa maeneo yote muhimu kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya nchi yetu kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Kwa ufupi, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kama inavyooneshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, unaendelea vizuri sana ingawa kumezuka vikwazo ambavyo havikutarajiwa hususan mlipuko wa virusi vya corona, uhaba wa mvua na vita huko Ulaya Mashariki.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye eneo la hali ya uchumi nchini. Kuhusu hali ya uchumi, naishauri Serikali kuwalinda na kuwawezesha wazalishaji wadogo hasa katika sekta za viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi. Ulinzi wa kisera na kisheria kwa wazalishaji wadogo ujikite zaidi kwenye maeneo ya ulinzi wa masoko dhidi ya walanguzi na wanyonyaji, ulinzi wa kazi za ubunifu na teknolojia na ulinzi wa rasilimali za ardhi na ikolojia zinazotumiwa na wazalishaji wadogo.

Aidha, wazalishaji wadogo wanahitaji pia kuwezeshwa na Serikali hasa kwenye masuala ya upatikanaji wa mitaji ya gharama nafuu, utafiti na mafunzo, upatikanaji wa pembejeo na ujenzi wa miundombinu ya uhifadhi wa mazao, usafirishaji, nishati na umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, hali ya kiuchumi kwa wazalisaji wadogo inaweza kudorora zaidi pengine kwa muda mrefu kutokana na athari za UVIKO-19, mabadiliko ya hali ya hewa na mfumuko wa bei ya mafuta duniani. Kwa muktadha huu, Serikali inatakiwa kufanya tathmini ya haraka ili kuweza kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu za kulinda na kuwezesha sekta ya wazalishaji wadogo kulingana na mazingira yaliyopo sasa. Kwa kuwa sekta ya wazalishaji wadogo ndiyo mhimili wa uchumi wa nchi yetu hasa katika nyanja za ajira, usalama wa chakula, kodi na tozo na kwa kuwa kuna changamoto mpya zilizozuka ghafla katika sekta hii, ipo haja kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kuilinda na kuiwezesha sekta ya wazalishaji wadogo kwa maslahi ya taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa mchango huu naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa sababu ya ufinyu wa muda nianze kwa kuunga mkono mapendekezo yote na taarifa nzima ya Kamati ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Maji ambayo mimi ni Mjumbe. Nitakayoyazungumza yameshajadiliwa kwenye Kamati na baadhi ya Wajumbe kazi yangu itakuwa ni kuweka msisitizo.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, mwaka jana tulikuwa na matatizo makubwa mawili kama Taifa, ukame na mfumko wa bei hasa za vyakula. Kwa hiyo nitagusia kidogo kwenye eneo la ukame kwa Sekta ya Maji lakini mchango wangu kwa sehemu kubwa utagusa Sekta za Uzalishaji, kwa maana ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali na hasa Wizara ya Maji na Shirika letu la DAWASA kwa namna walivyoshughulikia tatizo kubwa la uhaba wa maji hasa katika Jiji la Dar es Salaam. Tatizo hilo limetupa mafunzo mengi kwamba uwezo wa Serikali kukabiliana na majanga ni mkubwa na kama Serikali inamiliki vyombo vya kufanya kazi hiyo inakuwa salama zaidi na hapa tujifunze kwamba, mawazo ya kubinafsisha huduma za maji hayafai katika nchi maskini kama ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tatizo lile lingetokea wakati watoa huduma ya maji wangekuwa ni Sekta Binafsi tungetafutana, lakini uratibu, ufuatiliaji na juhudi na hatua za haraka ziliwezekana kwa sababu jambo hilo lilishughulikiwa mia kwa mia na Serikali. Kwa hiyo tujifunze kwamba katika maeneo nyeti ya huduma za kiuchumi na za kijamii, vyombo vya Kiserikali ni muhimu sana. Hilo ni funzo pia kwenye eneo la nishati na umuhimu wa kuimarisha Shirika letu la TANESCO na mashirika mengine ambayo yanaweza yakatusaidia wakati nchi inapoingia kwenye mtikisiko wa dharura usiotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, funzo la pili ni kwamba, DAWASA walibaini kwamba kama matatizo ya maji kwa Ruvu Juu ni makubwa na Ruvu Chini ina nafuu, wanaweza wakaunganisha mifumo ilhali ikiwa mbaya Ruvu Juu, Ruvu Chini iweze kusaidia, maana yake nini? Maana yake kuna haja ya kufikiria kuwa na mfumo ambao unafananafanana na Gridi ya Maji ya Taifa. Kwa sababu vyanzo vyetu vimetawanyika, kuna maeneo yenye ziada na kuna maeneo yenye uhaba. Kwa hiyo miundombinu yetu ikizingatia namna ya kusaidiana kwenye maeneo ya ziada na uhaba, tunaweza tukawa na mpango mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie dakika zangu tatu zilizobakia kwenye eneo la uzalishaji. Nitasema kwa ufupi tu kwamba, njaa inadhalilisha heshima na uhuru wa nchi na njaa inatweza utu wa binadamu. Kwa hiyo tatizo la mfumko wa bei za vyakula ni tatizo ambalo tutake tusitake lazima tuongeze kiwango cha ubunifu kukabiliana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu ametuwezesha kama binadamu hakuna ukomo wa ubunifu. Wananchi wanakabiliana na tatizo hili, nilikuwa nazungumza na baadhi yao, mmoja anasema wamepanga milo kwa kupiga pasi. Kwa maana ya kwamba staftahi ya asubuhi na chakula cha mchana vinaunganishwa kwenye majira ya saa 5.00 na saa 6.00 mchana halafu na mlo wa usiku unaunganishwa kati ya majira ya saa 11.00 na saa 12.00 jioni, hawasubiri kujadili mambo ya Ukraine na tabianchi na kadhalika wameanza kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, mwingine ananiambia pesa aliyokuwa anaitumia kunua unga ni ileile na chanzo cha mapato yake hakijaongezeka, lakini bei ya unga imeongezeka kwa hiyo unga aliokuwa anaununua kwa pesa ileile kusonga ugali, ameamua kukoroga uji. Sasa kama wananchi wanakabiliana na hali hiyo na nchi inaenda, miradi ya maendeleo inaendelea haijasimama. Kwa nini Serikali isipanue wigo wa kufikiri na ubunifu kukabiliana na tatizo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuacha maswali machache kuongezea ulipotuongoza, je, ruzuku ya mbolea na mafuta na mbegu imepunguza makali kiasi gani ya mfumko wa bei ya vyakula? Je, kutokuwa na lockdown kumepunguza kiasi gani makali ya mfumko wa bei za vyakula? Je, udhibiti wa kuuza vyakula nje ukiwepo unamnufaisha nani na pia vyakula vikiuzwa nje kwa uwazi hiyo ruksa inamnufaisha nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, uwekaji wa mazingira ya wananchi wanaozalisha chakula na hapa nikisema chakula namaanisha wavuvi, wafugaji na wakulima. Nadhani tuna kazi ya ziada ya kuboresha mazingira ya wananchi wa aina hii. Kwa nini tumeshindwa kudhibiti lumbesa? Lile tamko la Serikali la kuruhusu mwananchi asafirishe vyakula kwenda sokoni bila kusumbuliwa ili mradi havizidi uzito wa tani moja lipo au halipo?

SPIKA: Sekunde thelathini, malizia.

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, la mwisho hilo, je, haki ya ardhi ya wakulima na wafugaji imelindwa kwa kiasi gani na wana uhakika kwa kiasi gani kuitumia ili kujilisha wao wenyewe na kulilisha Taifa?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya bajeti ya TAMISEMI iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Bashungwa kwa umakini. Kwa kiasi kikubwa TAMISEMI imefanya kazi ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ufanisi na hasa katika maeneo ya utoaji bora wa huduma katika sekta za miundombinu ya barabara za mijini na vijijini kupitia TARURA, elimu ya msingi na sekondari na sekta ya afya. Aidha, utekelezaji wa mpango wa mapambano dhidi ya UVIKO kwa ufanisi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi na uongozi bora wa watendaji na viongozi walioko TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo wa kudhibiti UVIKO ili tuainishe maeneo ambayo tunaweza kujifunza. Kwa maoni yangu, baadhi ya mafunzo yaliyojitokeza waziwazi kutokana na mpango huo ni kiwango cha hali ya juu cha utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ubunifu katika uandaaji wa mipango ya maendeleo na ushirikishaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti iliyopita, napenda kutoa ushauri kwa ufupi kwa TAMISEMI katika maeneo mawili kama ifuatavyo: -

(a) Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziwe kitovu cha uzalishaji katika sekta za viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwa wazalishaji wadogo wako chini ya mamlaka hizo. Fursa nyingi za uzalishaji bado hazijatumiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki kigumu kiuchumi duniani kote, mamlaka zilizoko chini ya TAMISEMI zinatarajiwa kuchangia katika kutafuta suluhu ya matatizo ya ajira kwa vijana, tishio la mabadiliko ya tabianchi linaloweza kusababisha upungufu wa chakula, tija duni katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo na ukosefu wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

(b) Ushirikishaji wa wananchi katika kuongeza kiwango cha uzalishaji na kupambana na umaskini unategemea uwezo wa kiuongozi na kiutendaji wa vyombo vya wananchi hasa vyama vya ushirika vya wazalishaji na vyama vya akiba na mikopo. Pamoja na kwamba kisheria na kisera, vyama vya ushirika viko chini ya Wizara ya Kilimo, TAMISEMI ina jukumu la kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuboresha utendaji na uongozi wa vyama vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja.