Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Bahati Keneth Ndingo (5 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha uanzishwaji wa hati fungani za Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/22 Waziri wa Fedha na Mipango aliwasilisha kuhusu kuanzisha hati fungani za Halmashauri. Kifungu cha 92 ya hotuba yake ilieleza, katika jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya mapato rasilimali fedha Serikali itaangalia uwezekano wa kutumia hati fungani zitakazotolewa na Halmashauri za Manispaa na Majiji kama njia mbadala ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, hatua hii itapunguza mzigo kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali hasa kwa Halmashauri zenye miradi ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa na uhakika wa uwezo wa miradi hii kurejesha kwa faida kwa maana ya bankable projects.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund – UNCDF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (Capital Markets and Securities Authority- CMSA) imeanza mchakato wa kupitia miradi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji yatakayokidhi vigezo na masharti ya matumizi ya hati fungani yanaanza kutumia utaratibu huu katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Vituo Vya Wazee nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote na kwa kudra za Mwenyezi Mungu, nitatekeleza majukumu yangu ipasavyo katika kuleta maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma, Serikali imeendelea kuboresha majengo na miundombinu ya makazi ya wazee kwa awamu ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021 ukarabati umefanyika katika makazi saba ya wazee ikiwemo; Nunge (Dar es Salaam), Kolandoto (Shinyanga), Njoro (Kilimanjaro), Magugu (Manyara), Kiilima (Kagera), Fungafunga (Morogoro) na Sukamahela (Singida). Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee Wasiojiweza nchini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha zitapopatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka mfumo utakaoruhusu wafungwa kupata haki ya faragha na wenza wao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa haki mbalimbali kwa wafungwa walioko magerezani kwa mujibu wa sheria. Haki ya faragha kwa wafungwa na wenza wao itaanza kutolewa pale ambapo mifumo ya kisheria, na miundo mbinu ya magereza itakapokidhi kutolewa kwa haki hiyo. Masuala mengine yatakayozingatiwa ni usalama, mila na desturi za Watanzania, kwani haki hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa faragha.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea uwezo Wahitimu wa Vyuo nchini ili waweze kushindana katika soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ujulikanao kama, Higher Education for Economic Transformation (HEET), inaendelea na maandalizi ya uboreshaji wa mitaala iliyopo na uandaaji wa mitaala mipya zaidi ya 290 katika programu za kipaumbele cha Taifa ili kuwajengea uwezo wahitimu kuhimili ushidani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayoendelea ni ukusanyaji wa maoni (tracer study and needs assessment) kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mahitaji halisi. Mitaala hiyo iliyoboreshwa inatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2023/2024, nakushukuru.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kujibu swali kama Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba dakika moja niweze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kwa uhai na kila kinachotokea kwenye maisha yangu likiwemo na hili. (Makofi)

Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa imani hii kubwa aliyonipa na nimuahidi ya kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi tuwatendee haki wananchi tunao wahudumia. (Makofi)

Niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono na ushirikiano mkubwa wanaonipa na niwahakikishie Muheza bado Mbunge mnaye na nitahakikisha nawaheshimisha. (Makofi)

Nikushukuru wewe Spika na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ya kila mara, hili ni darasa kubwa na ninaendela kujifunza. Mwisho niishukuru familia yangu mke na watoto wangu kwa mapenzi mengi yanayofanya kichwa changu kiendelee kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, nijibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inachukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na hali hiyo: -

(i) Wizara imeaandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa Mtanzania uliozinduliwa Tarehe 02 Julai, 2022 ambao unaendelea kusambazwa;

(ii) Kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia Vyombo vya Habari. Mathalani, katika kipindi cha Januari – Aprili, 2023 Wizara imefanya vipindi 11. Pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 kati ya Halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya Habari;

(iii) Kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo Viongozi wa Dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na Wasanii. Aidha Wizara inameandaa mdahalo na semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika Mkoani Njombe tarehe 19-21 Mei, 2023;

(iv) Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Viongozi wa Dini, Machifu na Viongozi wa Kimila pamoja na Wizara zenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto na vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja, ahsante.