Contributions by Hon. Bahati Keneth Ndingo (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri na nzito ambayo wameendelea kuifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 7 kuhusiana mambo ya masuala mazima ya wazee. Kwa kweli, hotuba ile iliwapa matumaini makubwa wazee na tunashukuru kwa kutambua thamani kubwa ya wazee wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua tuna Sera ya Wazee iliyotungwa mwaka 2003 lakini mpaka sasa hatujaitengenezea sheria ya kusimamia utekelezaji wake. Hata kama tuna mipango mizuri na mikubwa kwa ajili ya wazee wetu kama tunakosa sheria ya kusimamia utekelezaji wa sera hizi, itakuwa ni ngumu sana changamoto za wazee kupata muarobaini. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja ku-windup atuambie ni lini ataleta Bungeni sheria ya kusimamia utekelezaji wa Sera hii ya Wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze sasa kwenye vituo vya kulelea wazee vinavyomilikiwa na Serikali. Nitambue kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kwa ajili ya wazee wetu na sasa hivi tuna vituo takriban 16 nchi nzima vya kulelea wazee, lakini hali ya vituo hivi kwa kweli inasikitisha. Mimi binafsi nimeshatembelea baadhi ya vituo vya kulelea wazee, niliwahi kwenda pale Fungafunga Morogoro miundombinu ya pale si rafiki. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza kwamba wataenda kukarabati vituo 5 kama ifuatavyo: Kituo cha Kolandoto (Shinyanga); Kituo cha Nunge (Dar es Salaam); Kituo cha Njoro (Kilimanjaro); Kituo cha Magugu (Manyara) na Kituo cha Fungafunga (Morogoro). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wanapokwenda kufanya maboresho ya vituo hivi pia waangalie sana miundombinu ambayo itakuwa rafiki kwa wazee. Kwa mfano, pale Fungafunga (Morogoro) ukiangalia kile Kituo cha Wazee vyoo vyao viko nje kabisa ya sehemu wanazolala na wale wazee wanahitaji kusaidiwa kwa sababu ni watu ambao umri wao umekwenda sana.
Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo, niombe sana wanapofanya marekebisho ya vituo hivi waangalie miundombinu rafiki ambayo haitakuwa vikwazo kwa wazee wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na miundombinu kuwa rafiki vifaa vya kuhudumia wazee kwenye hivi vituo hakuna, hata gloves za kuwasaidia wale wazee hakuna. Kwa hiyo, niombe sana sana Serikali vifaa viwepo kwenye vituo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye vituo hivi vya Serikali huduma zinazotolewa mle ndani ni huduma za kwanza yaani mzee atapewa tu Panadol, ndio zinazokuwepo pale lakini ile huduma angalau inakuwa ni ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vingi vyao vipo nje sana ya miji na kusababisha wazee wengi kupoteza maisha kwa sababu ya umbali. Kwa mfano, hiki cha Fungafunga (Morogoro) kwa sababu nimeshakwenda hata barabara ya kufika pale kituoni hakuna, watu wanapita chini ya lile bomba la reli, hata gari zikifika pale kuleta dawa wanaenda na pikipiki wanavuka wanachukua ndio wanakuja kuzileta kituoni. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri muangalie sana miundombinu ya hivi vituo vya wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifurahi kusikia kwamba mna utaratibu wa kuanzisha uniform kwenye vituo vyetu vya afya, kwamba watu wanaohudumia wazee mtatoa uniform maalum ili mzee akifika pale ajue hawa ndio wanaohudumia wazee. Naomba katika utaratibu huo mwaangalie pia walemavu na viziwi ili wajue kabisa, kama mtaweka sare hizo kwa wazee muweke na sare pia kwa watu wengine ambao wanauhitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, naomba niongelee kuhusu mambo ya vyoo. Magonjwa mengi sana yanatokana na ukosefu wa vyoo; usambazaji wa uchafu kutoka vyooni. Kuna kampeni moja ilikuwa inaongelea “Nyumba ni Choo.” Kampeni ile ilifanyika, lakini kwa vijijini kule bado suala la vyoo ni shida. Kwa hiyo, naomba sana, kampeni hizi za nyumba ni choo iendelezwe ili iweze kuleta tija mpaka kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule vijijini hakuna vyoo na maradhi mengi yanatokana na kukosa vyoo. Endapo Serikali mtaichukulia uzito hii Kampeni ya Nyumba ni Choo na vyoo vikawepo kwenye kila maeneo, itatusaidia sana kupunguza magonjwa mengi na itaisaidia pia Serikali kutopoteza fedha nyingi kwa sababu ya kukosekana magonjwa ambayo ni hatarishi. Kwa hiyo, niwaombe sana Serikali mjitahidi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagonga.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kupata fursa nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuipongeza Serikali ya Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa bajeti yake hii ya kwanza, nzuri kabisa ambayo imepokelewa kwa bashasha kubwa huko mtaani. Lakini pia niendelee kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kutuletea bajeti ambayo inakuwa ni chachu ya maendeleo kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani. Tunaona bajeti hii inayokwenda kuisha tarehe 30 Juni, tulikuwa na vyanzo vya mapato ya ndani kwa asilimia 69, sasa kwenye bajeti hii tunatarajia kuwa na vyanzo vya mapato asilimia 72. Kwa hiyo ina maana tunakwenda kupunguza utegemezi wa bajeti na mikopo ya nje na wahisani kwa asilimia tatu. Siyo kazi ndogo niwapongeze sana kwa ubunifu wa kuibua vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubalina na mimi na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba kwa takribani miaka mitano iliyopita kuanzia 2014 mpaka 20219 Halmashauri zetu bado zimekuwa na changamoto ya kuweza kupata mapato ya kutosha. Kwa hiyo tumekuwa tukiipa Serikali Kuu mzigo mkubwa kwenye Halmashauri zetu. Tumeona kwamba kwa takriban kuanzia mwaka 2014 mpaka 2019 zaidi ya asilimia 85 ya Halmashauri zilishindwa kujigharamia matumizi yake ya kawaida. Hivyo zilipelekea kwamba Serikali Kuu iendelee kuzisaidia hizi Halmashauri. Kwa hiyo, utaona kwamba bado Serikali Kuu ina mzigo mkubwa ambao ni lazima kama Taifa tuje na mbinu mbadala za kuendelea kutafuta vyanzo vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kuishauri Serikali, niliona katika Mpango wa Pili wa Serikali mliongelea Hati Fungani za Manispaa (Municipal Bonds) lakini pia niliona katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Mheshimiwa Waziri wa Fedha kipindi hicho ni Makamu Rais sasa, alisisitiza kuendeleza Mpango ule wa kuanzishwa kwa Hati Fungani za Manispaa, ilielezwa Bunge lako Tukufu kwamba mmekwenda kufanyia training karibia Manispaa ya Mwanza, Arusha na nyinginezo na Tanga. Sasa, naona hili jambo pia limekuwa kama linasinzia. Hii nchi ni kubwa lazima tubuni halmashauri hizi zijiendeshe kibiashara. Tukisema halmashauri zote nchini ziweze kujiendesha kwa kutegemea Serikali Kuu tutakuwa tunajidanganya. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iweke mkazo kwenye kuhakikisha wanamalizia uanzishwaji wa hizi Hati Fungani za Manispaa au Municipal Bonds.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, kwenye bajeti tukatoe kipaumbele kwenye miradi ambayo itakwenda kuchochea uchumi kwa haraka. Leo hii tuna mradi mkubwa unakwenda kuanza wa Liganga na Mchuchuma lakini kama Serikali imeandaa mazingira ambayo yatakuwa wezeshi kwa mradi huu kutopatikana kwa vikwazo. Barabara zipo, miundombinu rafiki kwa ajili ya mradi huu ipo? Ni vitu ambavyo kama Serikali lazima tuhakikishe tunatoa vipaumbele kwenda kutekeleza bajeti yetu kwenye vyanzo ambavyo vitakwenda kuchochea uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kule kwenye barabara za huko vijijini utaona jinsi kuna uwekezaji mkubwa kwa mfano, kuna uwekezaji mkubwa ulifanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu kule kwetu Madibila, Mbarali. Waliwekeza zaidi ya bilioni 28 lakini leo hii hata barabara kufika kwenye yale mashamba hakuna. Ni jinsi gani Serikali inapoteza mapato kule kwa kukosekana tu barabara ile barabara ipo tangu Serikali ya Awamu ya Tatu imeahidiwa kwa wananchi kilomita 151 kutoka Rujewa, Madibila mpaka Mafinga kule kuna wakulima wa mbao, kuna uwekezaji mkubwa Serikali imetengeneza skimu za umwagiliaji kubwa lakini hakuna barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana Serikali, leo hii lango kubwa la biashara kwenye nchi za Southern Africa, Kusini mwa Afrika, (SADC) leo hii lango kubwa la biashara ni kule, barabara ile haifai kutoka pale Igawa mpaka Tunduma ni shida. Kwa hiyo, ni lazima kama Serikali tutoe vipaumbele kwenye maeneo ambayo yataweza kuchochea uchumi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze TAMISEMI kwa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge katika miradi mbalimbali inayoendelea. Niombe sana na Wizara nyingine zifanye hivyo kama Wizara ya Ujenzi wakae na Waheshimiwa Wabunge, Wabunge hawa wanajua barabara ambazo zitakwenda kuchochea uchumi kwenye Majimbo yao. Kwa hiyo niwaombe sana na Wizara nyingine muwape kipaumbele Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo yao ili waweze kujadiliana nanyi na kuwapa kipaumbele ambacho kitasaidia kujua ni nini kipaumbele cha vitu ambavyo vitachochea uchumi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana kwa kupata fursa, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata fursa. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, management yote ya Wizara na taasisi zake kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nita-base kwenye vitu viwili kuishauri na kutoa maoni yangu kwenye Wizara hii. Kwanza ni Chuo chetu cha Utumishi wa Umma na vile vile mafunzo kwa Watumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona kuna upokwaji mkubwa wa taasisi hii kufanya majukumu yake, kwa sababu chuo hiki kilianzishwa kwa ajili ya kuwafunda watumishi wa umma, lakini sasahivi tumekuwa na utaratibu wa kawaida kabisa kwa mtumishi kuingia ofisi ya umma pasipo kupitia kwenye chuo hiki, na ndiyo maana tunayaona haya ambayo yako kwenye mitandao. Utaona si dhambi sasahivi kuona document ya Serikali ambayo imendikwa siri kwenye Instagram, tunaona kabisa unaingia kwenye ofisi ya umma mtu amevaa kama anaenda disco, ni kawaida kabisa kwa sababu wameacha kukitumia ipasavyo Chuo cha Utumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo zamani ilikuwa kwamba, ili mtumishi yeyote aanze kazi ni lazima apite kwenye chuo hiki kufanyiwa induction program. Kwenye induction program utaelezwa mipaka yako kwa nafasi yako, bosi wako umuheshimu vipi, mipaka yako inaishia wapi. Sasahivi ugomvi mwingi ulio kwenye taasisi mbalimbali ni kwa sababu watu hawapikwi kwenye chuo hiki. Mtu anaona jambo hili napaswa kufanya mimi pasipo kufanya huyu. Kwa hiyo mgongano ni mkubwa. Ni lazima Wizara ikipe msisitizo chuo hiki kuwafunda watumishi wa umma, la sivyo vitu vya kwenye mitandao na tabia za ajabuajabu za kwenye utumishi wa umma hazitakoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kwenye hili suala la training tunaona TAMISEMI wanaajiri, wanapeleka watumishi wao Chuo cha Hombolo. Chuo cha Kodi wakiajiri wanapeleka watumishi wao chuo chao cha kodi. Wakiajiri bandari wana chuo chao cha bandari, kila taasisi zina vyuo vyao, lakini kule wakienda ukiangalia program wanazozisoma si za utumishi wa umma, wanasoma program za kama job description zao. Mfano kama bandari utakusanyaje kodi, utafanya hivi, Hombolo vilevile wanafanya hivyo. Sasa utumishi wa umma haupati fursa ya kuwafunda wale watumishi wa-behave vipi kwenye nafazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe coordination ndani ya Serikali. Hawa watumishi wanavyowekwa kwenye hivi vyuo; kama wakiwa Hombolo mfanye coordination mchukue chuo hiki kina wataalam wengi waende wakawape training ya utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu mafunzo kwa watumishi. Ni mashahidi humu ndani ili gari hata liwe zuri ni lazima ufanye service. Unakuta mtumishi wa umma anakaa five years, haendi hata kwenye mafunzo, Kwa sasa mambo yanakwenda yanabadilika, technology zinabadilika. Ni lazima mafunzo nyawe si hiyari yawe ni lazima na wawepo na program maalum, kila baada ya muda fulani watumishi wawe wanaenda kwa kupokezana kupata mafunzo mafupi ili kuwajengea uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutapunguza matatizo mengi ambayo yanawakumba watumishi wa umma na utumishi; lakini vilevile Mheshimiwa Waziri ni lazima uwe na wivu na utumishi. Utumishi wowote ndani ya nchi hii uko chini yako. Wewe ndiye unayeteuwa kwenye idara nyingine, Wizara nyingine; kwa hiyo ni lazima kuhakikisha kuna coordination ya kutosha. Hata kama TAMISEMI wanaajiri, lakini wale waishaajiriwa ni watumishi wa umma, lazima wafanye kazi kwa kufuata misingi ya utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)