Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yustina Arcadius Rahhi (9 total)

MHE. YUSTINA A. RAHHI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za ugani Mkoani Manyara kutokana na upungufu wa wataalamu wa kilimo na mifugo katika ngazi ya Kata na Vijiji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji na kata kuwa na afisa ugani mmoja. Hadi sasa mahitaji ya maafisa ugani kulingana na vijiji, mitaa na kata zilizopo ni 2,538; na maafisa ugani waliopo ni 6,704 sawa na asilimia 33 ya mahitaji ya uwiano wa afisa ugani mmoja kwa vijiji vitatu. Aidha, kwa taarifa za mwaka 2020 Mkoa wa Manyara kuna jumla ya maafisa ugani 188 sawa na asilimia 49 ya mahitaji ya maafisa ugani 386. Kwa hali hiyo Mkoa wa Manyara una maafisa ugani zaidi ya wastani wa nchi ulioko sasa.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara katika kukabiliana na uhaba wa maafisa ugani tumeanzisha mfumo wa kieletroniki wa Mobile Kilimo uliounganishwa kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na wizara. Mfumo huo unawezesha wakulima kutumia simu za mkononi kutuma ujumbe mfupi na kuomba ushauri wa kitaalamu na kujibiwa na afisa ugani aliyesajiliwa kwenye mfumo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2021 maafisa ugani wote na kaya za kilimo zaidi ya milioni 4.5 wamejisajili kwenye mfumo kati ya kaya za kilimo milioni saba. Kutokana na mfumo huo wakulima wengi wamekuwa wakipata ushauri wa huduma za ugani kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea kuajiri maafisa ugani kadri vibali vya ajira vinavyopatikana, na wagani hao wapelekwe kwenye maeneo yenye upungufu wa Maafisa Ugan ikiwemo Mkoa wa Manyara.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba malambo kwa ajili ya maji ya mifugo katika maeneo ya wafugaji mkoani Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, Serikali imekamilisha ukarabati wa mabwawa matatu likiwemo bwawa la Narakauo lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itaendelea kutenga fedha za kuchimba mabwawa na visima virefu katika maeneo mbalimbali nchini hususan maeneo yaliyoathirika na ukame ukiwemo Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhimiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kutekeleza Waraka wa Rais Na.1 wa Mwaka 2002, unaozielekeza kutenga fedha kiasi kisichopungua asilimia 15 kwa mapato yatokanayo na mifugo ili zitumike kutekeleza shughuli za Sekta ya Mifugo ikiwemo uchimbaji na ujenzi wa miundombinu ya maji kwa ajili ya mifugo. Aidha, Uboreshaji wa miundombinu hiyo ya mifugo uwe Shirikishi kwa kuwahusisha wafugaji.
MHE YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, kuna manufaa gani ya kuunganisha Idara ya Kilimo na Mifugo katika Halmashauri za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekit, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa uandaaji wa muundo na mgawanyo wa majukumu huzingatia mambo mbalimbali ikiwemo Sera, Sheria na maelekezo ya Serikali ya wakati husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muundo na Mgawanyo wa Majukumu ya Halmashauri za Wilaya uliidhinishwa rasmi tarehe 29 Januari, 2022, baada ya kufanya mapitio kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Katika mabadiliko hayo, Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika na Idara ya Mifugo na Uvuvi iliunganishwa na kuwa Idara moja ya Kilimo na Mifugo kutokana na kushabihiana kwa majukumu ya Idara ya Kilimo na Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa ya kuhuisha miundo katika ngazi ya halmashauri na Mikoa ni kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu, kupunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha uratibu na usimamizi. Hivyo, muundo mpya wa halmashauri umepungua kutoka Idara 13 na Vitengo Sita na kuwa na Idara Tisa na Vitengo Tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Taasisi hizo unaweza kufanyiwa mabadiliko inapohitajika bila kuathiri ufanisi ili kukidhi utendaji kazi wa kila siku. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Ndege katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utaratibu wa kutwaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Manyara.

Mheshmiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imeshamaliza kuandaa hadidu za rejea kwa ajili ya kumpata mhandisi elekezi atakayefanya upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina ili kubaini gharama za ujenzi. Hivyo, ujenzi wa kiwanja hicho utaanza baada ya usanifu kukamilika, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara za Dareda – Dongobesh, Katesh – Haydom, Karatu – Mbulu – Haydom – Singida na Babati hadi Orkesumet kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara za Dareda – Dongobesh (km 60), Katesh – Hydom (km 70), Karatu
– Mbulu – Hydom – Singida (km 246) na Babati - Orkesumet (km 145). Kwa kipande cha Mbulu – Garbab chenye urefu wa kilometa 25, taratibu za zabuni ziko kwenye hatua za mwisho za kusaini mkataba. Kwa kipande cha kutoka Garbab – Muslur chenye urefu wa kilometa 25 maandalizi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi yako kwenye hatua za mwisho. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu zilizobaki. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kuhusu Ndoa za Utotoni?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa Muswada wa Sheria ya Ndoa ulifikishwa kwenye Kamati ya Bunge lako Mwezi Februari, 2021, kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani kati kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Gyumi, Rufaa Na.204/2017 iliyotokana na kesi Na.5/2016 ya Mahakama Kuu iliyotaka Sheria ya Ndoa ifanyiwe marekebisho ili umri wa mtoto kuingia katika ndoa iwe kuanzia miaka 18. Kamati ya Bunge baada ya kupitia iliona upo uhitaji wa kushirikisha wadau wengi zaidi ili kupata maoni zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumwarifu Mbunge kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeshakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama vya siasa, wanafunzi, wataalam mbalimbali wa afya, makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu. Aidha, tarehe 26 Aprili, 2023, Wizara imeandaa Kongamano la Sheria ya Ndoa litakalofanyika katika Hotel ya Morena, Jijini Dodoma, kesho saa saba. Naomba niwakaribishe Wabunge wote na itakuwa live TBC kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara tu baada ya Serikali kukamilisha zoezi hili la mwisho, inatarajia kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa Bungeni katika Bunge hili la Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Fidia kwa wahanga wanaoathirika na wanyamapori wakali na waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la kama ulivyonielekeza.

Mheshimiwa Spika, kwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu baada ya Mheshimiwa Rais kunipa heshima hii ya kuniteua kuwa Naibu Waziri, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye imempendeza niweze kutumika kwenye nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipa heshima hii ya kuitumikia nchi yetu. Naahidi kutekeleza majukumu yangu kwa uwezo wangu wote na kwa vipawa vyote alivyonipa Mwenyezi Mungu, naahidi sitamwangusha.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ushirikiano wako na Wabunge wenzangu nawaahidi ushirikiano naomba tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu. Malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Machozi za mwaka 2011 na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, kanuni hizo zilianza kutekelezwa mwaka 2012 ambapo katika kipindi cha kuanzia 2012/2013 hadi 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni 11.3 zimelipwa kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu. Hata hivyo, suala hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika ambapo limesababisha baadhi ya nchi kuondokana na utaratibu wa kulipa kifuta jasho na machozi. Lakini Tanzania imeendelea kuona umuhimu wa kuwafuta jasho na machozi wananchi kwa madhara wanayoyapata kutokana na wanyamapori hao. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha uwekaji wa samani na vifaa vya kufundishia katika Vituo vya Rasilimali za Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilijenga Vituo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata 289 katika Halmashauri 184 kati ya mwaka 2007 na 2011. Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeanza uwekaji wa samani na vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kufundishia katika vituo hivyo na kwa mwaka huu wa fedha Wizara itawezesha Vituo 34 vya Halmashauri 27 za Mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Simiyu, Mwanza, Geita, Lindi, Mtwara, Mbeya, Songwe na Iringa. Kwa ufupi, Wizara itaendelea kuweka samani na vifaa vya kufundishia katika Vituo vyote vya Rasilimali za Kilimo vya Kata vilivyojengwa nchini na kutumika kama Centre of Excellence.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa utambuzi wa mifugo baada ya kusitisha zoezi la utambuzi kwa kutumia hereni za mifugo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti majibu.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2022 Serikali ilisitisha kwa muda zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya hereni ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza ambazo ni pamoja na wafugaji kulalamika juu ya bei ya kuvisha hereni na baadhi ya wafugaji kukosa elimu sahihi ya utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekamilisha kufanya marekebisho ya kasoro la zoezi hilo la utambuzi zilizojitokeza ambapo bei ya kuvika hereni imeshuka kutoka 1,750 hadi shilingi 1,550 kwa ng’ombe na kutoka shilingi 1,000 kwa mbuzi na kondoo hadi shilingi 900. Pia, Wizara imekamilisha kuandaa mkakati wa utoaji elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara kwa kushirikiana na wadau wa mifugo, inategemea kuanza awamu ya pili ya utambuzi wa mifugo kwa kuanza na mashamba makubwa ya mifugo ya Serikali, mashirika, watu binafsi, wawekezaji kwenye vitalu vya NARCO, vituo vya unenepeshaji ng’ombe wa maziwa, wafugaji wakubwa na wafugaji watakaokuwa tayari wakati wa zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.