Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yustina Arcadius Rahhi (17 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye matendo haya ya ukatili wanayofanyiwa Watanzania wenzetu. Kwa kweli inasikitisha sana ukiona Watanzania wenzetu na hasa akinamama na Watoto; katika takwimu ambayo Waziri ameisoma kwamba katika matukio 134,310 takribani matukio 106,196 wamefanyiwa akinamama na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hayo tu matukio, kuna matukio mengine yanafanyika huko wala hayarekodiwi popote, lakini jamii hii inaendelea kuteseka, inaendelea kuathirika kisaikolojia, wengine wanapoteza Maisha, wengine wanabaki na ulemavu wa maisha moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita juzi huku Babati na maeneo mengine kuna kesi ambayo mpaka akinamama wa UWT wameishikia kidedea. Kwa mfano jana kulikuwa na kesi pale Babati ya mtoto katika familia mama ana watoto wake na mtoto wa ndugu yakem lakini imepotea shilingi 1,500 alichokifanya ni kuchukua shilingi 200 kuiweka kwenye jiko la mkaa ilivyokuwa nyekundu amemwekea yule mtoto mkononi yule anayetaka kumwadhibu, mkono umeungua, kesi ile imepelekwa polisi, bahati nzuri tumechangia kuwasafirisha wale. Matukio kama haya ni mengi, lakini kinachofanyika, kesi kama hizi ambazo tayari zina ushahidi baadaye watakubaliana zitakwenda kwa wazee, zitaongelewa zitakwisha, pamoja na kesi za ubakaji na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ku-create awareness, watu ambao wanaweza kuisemea wakahamasisha jamii sasa kutokomeza kabisa ni hawa Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo sasa wapo wachache. Wilayani utamkuta Afisa Maendeleo ya Jamii au Afisa Ustawi yupo mmoja, kesi hizi ni nyingi, anashindwa kufuatilia, jamii inashindwa kuona wajibu wake. Naomba sasa Wizara hii kwa sababu kitengo hiki kipo kwao waongeze ajira ya Maafisa Ustawi wa Jamii, wafuatilie ili kwa pamoja tuweze kutokomeza matendo haya ya ukatili wanayofanyiwa Watanzania wenzetu pamoja na kuwasaidia vifaa vya usafiri na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia tena kwenye matibabu ambayo yanatolewa nchini kwetu. Kwanza ninaipongeza sana Wizara na Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba kuna matibabu ya dialysis yalikuwa hayatolewa ndani ya nchi yetu, alikuwa mwathirika au mgonjwa anayetakiwa kutibiwa lazima asafirishwe kwenda nje. Kwa hiyo utaona kwamba ni familia zenye uwezo ndizo zilikuwa zinaweza kumsafirisha mgonjwa wake kwenda kutibiwa nje. Naishukuru Serikali kwamba sasa huduma hii inatolewa nchini, lakini ni katika maeneo machache, ni hospitali kubwa, kwa mfano matibabu haya yanatolewa Benjamin Mkapa, KCMC, Bugando na Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu hayo yanatolewa, mtu akishakuwa anatibiwa anatakiwa kwenda angalau mara mbili, tatu kwa wiki, kwa hiyo kinachofanyika familia yenye mgonjwa kama huyo kama anatibiwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa inabidi wahamie Dodoma wapate pa kuishi, lazima mwanafamilia mmoja akae na mgonjwa na kwa hiyo inaathiri familia nzima kiuchumi na kila kitu na isitoshe matibabu haya ni ghali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara sasa ni kwa nini sasa matibabu haya yasitolewe katika Hospitali zote za Mkoa ili kuwarahisishia Watanzania angalau wapate matibabu haya karibu na mikoani na Hospitali hizi za Kanda. Vile vile waangalie gharama hizi zipunguzwe. Najua kuna changamoto kubwa sana za wataalam wanaoweza kutoa matibabu haya. Namwomba Waziri husika wa Wizara hii awapeleke mafunzo Madaktari pamoja na wataalam ili tuwe na wataalam wengi wa kutosha na matibabu haya yaweze kupatikana angalau katika Hospitali za Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho, naomba nichangie kuhusu bima ya Afya, watu wengi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagongwa Mheshimiwa.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. YUSTINA E. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu ya sasa ni kweli kwamba Tanzania ni ya pili katika Afrika kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia. Mifugo hii mingi hii, asilimia 90 ni kosafu ya asili; na kwamba asilimia 96 ya mifugo hii huchungwa na wafugaji wa kuhamahama na wafugaji wakulima. Hata hivyo, mifugo hii katika tasnia ya nyama inachangia asilimia 90 na maziwa inachangia asilimia 70; na kwamba takribani inatoa vipande vya ngozi milioni tano, kwa maana kutoka ng’ombe vipande milioni 2.6 na wanyama hawa wadogo mbuzi na kondoo vipande milioni 2.6. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na baraka ya namna hii, Tanzania ambayo ni ya pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini ni ya tatu kwa utapiamlo wa udumavu. Inasikitisha, kwa sababu asilimia 45 ya Watanzania wana udumavu; na athari ya udumavu ni kuathiri ukuaji wa akili pamoja na ukuaji wa mwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimehusisha hizi kwa sababu gani? Lengo la msingi la ufugaji halijaweza kutimizwa kwa sababu tunapofuga lengo la kwanza ni kujitosheleza kwa chakula, ni lishe; na lengo la pili ni ziada sasa ili tupate fedha kwa ajili ya kujipatia maisha bora; elimu bora, maji salama, makazi salama na afya nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukija kwenye lishe ndiyo tunaona, kwa mfano, Watanzania wanakunywa wastani wa lita 47 ya maziwa kwa mwaka, badala ya kiasi kinashoshauriwa cha lita 200 kwa mwaka. Watanzania hawa wanakula wastani wa nyama kilo 15 badala ya kilo 50 kwa mwaka kwa mtu mmoja na wanaweza kula mayai takribani 106 badala ya mayai 300 kwa mwaka kwa mtu mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ziko nyingi na changamoto. Unaona kwamba upatikanaji wa bidhaa hii ya mifugo ni mdogo, lakini kwa nini? Kwanza, tunakuja kwenye changamoto ya kosafu, hatuna sehemu yoyote ya kumlaumu huyu mchungaji au mfugaji. Atatoka asubuhi na mifugo yake ataenda kuchunga akirudi jioni anakamua lita moja au lita mbili ya maziwa. Atachunga ng’ombe wake huyu miaka mitano, sita akienda kuuza anaishia kwenye kilo 60, 70 anauza kwa shilingi 200,000/= pamoja na muda wote anaoupoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri sasa mkakati wa kwanza ni kwenye kwenda kubadilisha kosafu ya mifugo. Hii mifugo haina tija. Haya mambo yanawezekana. Nitoe mfano mdogo tu kwa wakulima. Hata hao wakulima zamani walikuwa wakitumia mbegu zao za kienyeji, lakini baada ya Serikali kuleta mbegu ya ruzuku kupitia vocha, wakulima wametoka kwenye kuzalisha ile gunia tano au nane kwa ekari, sasa wanazalisha gunia 15 mpaka 20, hawatarudi huko nyuma. Kubadilisha kosafu faida yake ni kwamba, wakulima watapunguza kundi kubwa la mifugo ambalo halina tija na linaharibu mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ziko nyingi za kuweza kuboresha mifugo; kuna magonjwa ya mifugo ambayo sisi tunaweza kuepukana nayo, ukiacha magonjwa ya milipuko. Kwa mfano, kupe na minyoo ni tatizo kubwa kwa mifugo, lakini kumbe mwarobaini wake ni kuwa na majosho. Tufanye proper dipping. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji siku hizi wengine wanapaka paka tu mifugo kwa kutumia spray, lakini ile sheria ya zamani kwamba ng’ombe wote wa Kitongoji, ng’ombe wote wa Kijiji wanaogeshwa kwa pamoja sasa hivi wameacha. Kwa hiyo, wakiogeshwa kaya fulani, kaya nyingine hawajaogeshwa, ina maana lile tatizo la kupe lipo na ndilo linalosumbua. Ndiyo maana tunaona asilimia ya vifo vya mifugo ni kutokana na magonjwa ya kupe. Kwa hiyo, tuna uwezo mkubwa sana wa kuangamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majosho ya toka zamani ya wakoloni, yamechakaa huko vijijini, ni mabovu. Ni kwa nini sasa Wizara isihakikishe kwamba maeneo yote ya wafugaji wana majosho ya kuogesha mifugo yao ili kuachana na tatizo la kupe na kuondoa minyoo kwa mifugo ambayo pia inachosha mifugo yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili la wafugaji wetu kuhangaika kwa ajili ya ukosefu wa wataalam wa mifugo. Mfugaji siku hizi anatibu mifugo yake mwenyewe, lakini tunatengeneza u-resistance wa magonjwa. Kwa sababu, wanapiga dose kubwa, wanachanganya madawa haya kwa ajili ya kukosa maelekezo. Kuna umuhimu sana wa kuboresha huduma za ugani na wataalam wa mifugo wakakaa karibu. Hili siyo kundi la kudharau, kundi la wafugaji ni wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifikirie namna gani sasa kurejesha; kwanza tulikuwa na veterinary centers kwenye kata, zimekufa; mfugaji hawezi kujua hata mahali pa kwenda, anabahatisha tu. Marafiki wa karibu wa wafugaji sasa wamekuwa ma-agrovet. Akifika kwenye maduka ya wakala ndio ashauriwe dawa hii na dawa hii; na wale ni wafanyabiashara, anaweza akamshauri mfugaji dawa ni hii akachanganya dawa za aina nyingi pengine bila kujijua. Kwa hiyo, utaalam bado ni muhimu kama tunataka kuwasaidia hili kundi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatupati tija kwa sababu usindikaji unafanyika kwa kiwango kidogo sana. Tuna viwanda takribani 81 vya kusindika maziwa; na vingekuwa na uwezo wa kusindika lita hata milioni 276, lakini kwa sasa vinasindika lita milioni 56 hivi kama sikosei. Ni kwamba maeneo ya wafugaji ni maeneo yapo ndani, hizi lita mbili, mbili au lita tano, tano, kama tungeweka collection centers huko kwenye maeneo ya wafugaji vijijini au kwenye Kata, hizi zingeweza kukusanywa, zikapelekwa kiwandani na tukawa na maziwa mengi, tukaongeza hata hiki kiwango cha unywaji wa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tuwaambie kuwa Halmashauri pengine kwa Wakurugenzi, maeneo ya wafugaji mara nyingi wanakaa mbali na soko. Soko ni miji ile midogo, hakuna mtu anaweza kutembea kilomita 30, 40 kupeleka lita mbili au tatu ya maziwa. Kungekuwa na collection center wapeleke maziwa, bado ingekuwa ni kipato kizuri tena hasa kwa akina mama. Maana anajua ukipeleka maziwa kuanzia Jumatatu, Jumanne, Ijumaa anapokea hela yake ya lita tano, tano; ni nyingi ingeweza kufanya kitu kikubwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JUSTINA E. RAHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi collection centers ni muhimu kwa ajili ya… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. JUSTINA E. RAHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya mwaka 2021/2022, bajeti ambayo ina mpango wa namna gani tunakwenda kukusanya mapato na matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni ya kwanza katika Mpango wa Miaka Mitano tuliyojiwekea, ni bajeti ya kwanza ya Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Awamu ya Sita yenye maelekezo mengi, yenye matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inakwenda kujibu kero na vilio vya Watanzania wa aina mbalimbali. Kwa mfano inakwenda kuweka matumaini makubwa kwa watumishi kwa sababu tunaona kuna mpango wa kuwapandisha vyeo watumishi wapato 92,619 pamoja na kwenda kupunguza makali ya Maisha kwa sababu inakwenda kupunguza kodi kutoka asilimia tisa mpaka asilimia nane. Tunamshukuru sana mama, hongera sana. Pia itajenga mazingira mazuri kwa watendaji wa vijiji na makatibu tarafa kwa jinsi ambavyo itawarahisishia kazi zao, kwamba sasa wanakwenda kuwekewa laki moja ili iweze kuwarahisisha katika utendaji wao wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwapa nguvu na confidence viongozi wetu wa siasa, Madiwani kwa kuwa sasa wanaweza wakasimamia miradi ya halmashauri bila kubabaishwa, bila ya kuwanyenyekea wakurugenzi wala wataalam. Wataweza kusimamia miradi ya Wakurugenzi kwa kuwawekea posho zao moja kwa moja kwenye akaunti inayotoka Hazina, hongera sana Mama. Lakini pia inampango mzima wa kuweza kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji waje wawekeze. Pia utaratibu mzuri kwa wafanya biashara kuweze kulipa kodi kwa hiyari yao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa Watanzania walio wengi matumaini ni makubwa kwa sababu bajeti hii imewaonesha jinsi ya kwenda kuboresha huduma za jamii. Kwa mfano itaendelea kutoa elimu bure kuanzia form one mpaka form four. Tunaipongeza sana, lakini mpango mzima wa kwenda kukamilisha vijiji ambavyo havijapata umeme katika mpango huu vijiji vyote Tanzania vinakwenda kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme ni kichocheo cha maendeleo, nimpango mzuri sana. Tunajua umeme umepunguzwa Rural-Urban Immigration ambapo vijana walikuwa hawapenda kukaa vijiji. kwamba ni afadhali akae Machinga Mjini kutokana na kukosa umeme, kwamba anaona ametengwa na dunia anashindwa kuingia internet. Lakini vile vile imeweza kuchochea viwanda vidogo vidogo kama saluni huko vijijini, viwanda vya ma-grill pamoja na pia kuwasaidia kina mama ambao walikuwa wanakwenda mbali kwa ajili ya kwenda kusaga mahidi wakifuata umeme mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile kuna mpango mzima wa kuboresha barabara, hasa hizi za TARURA pamoja na feeder roads; ni kichocheo kizuri sana miundombinu ya barabara. Hata hizi pembejeo tunazo sema zinafika kijijini kwa bei kubwa sana kutokana na miundombinu ya barabara ambapo ni mbovu. Kwa mfano Serikali inatoa bei elekezi kwa ajili ya mbolea, lakini mbolea mpaka ifike kijijini bei yake imekuwa mara dufu kutokana na matatizo ya barabara. kwa hiyo kuna umuhimu sana wa kuimarisha barabara, feeder roads pamoja barabara hizi za TARURA. naompongeza sana Mama yetu kwa kutoa top up licha ya bajeti ya TARURA lakini sasa imeongezwa milioni 500 kwa ajili ya kwenda kuboresha barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, ili kuweza kufikia ndoto hii sasa ya kutoa huduma bora kwa Watanzania pamoja na makundi mengine ni lazima sasa tuweke mkakati wa kupata mapato; kwa sababu bajeti yetu ni cash budget we expenditure kila ambacho tunaki-collect.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaompongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa jinsi ambavyo amekuja na vyanzo mbalimbali vya kukusanya mapato. Kuna vyanzo vya zamani vinaendelea lakini pia nimeona vyanzo vipya. Vyanzo vingine kama jinsi utakapopata property tax, kodi ya majengo watu wamechangia najua ni msikivu atakwenda kuboresha kwa namna gani anakwenda kukusanya mapato hayo ambayo hayana kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ameweka vipaumbele, kwamba namna hii ya kwenda kukusanya mapato kipaumbele cha kwanza ni mapato yetu ya ndani na yanayotokana na kodi, tozo na ushuru, na sehemu nyingine ni mkopo wenye masharti nafuu na misaada. Sasa, kama kipaumbele cha kuendesha miradi yetu ni mapato ya ndani kwa hiyo sisi hatuna budi kuwekeza katika sekta hizi za kiuchumi, ikiwepo kilimo, mifugo, maliasili na madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naipongeza sana Serikali kwa sababu hata bajeti, kwa mfano nikichukulia mfano wa kilimo; tumeongeza bajeti ya kilimo kwa asilimia 22 lakini bado bajeti hii inaonekana haitoshi kwa sababu ukiangalia kwenye gross budget, bajeti yote ya Nchi nzima bado kilimo inakwenda kwenye asilimia 0.8 kwamba iko chini ya asilimia moja. Tunavyoweza kuboresha kilimo; kwa sababu tatizo kubwa kwenye kilimo ni uzalishaji mdogo. Kwa mfano tungeweza kuboresha uzalishaji katika kilimo, faida moja wapo tunayopata ni uhakika wa chakula. Tunapokuwa na uhakika wa chakula basi tunakwenda kumudu inflation, na vile vile tunakwenda kufanya serving, kwamba sasa vyakula ambavyo tulikuwa tunategemea kuagiza kutoka nje ikiwemo mafuta, watu wengi wamechangia, ngano na sukari. Tunatumia hizi fedha kupeleka kwenye miradi ya vitu vingine; kwa hiyo ni faida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunajua kwamba kilimo kinatoa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Kwenye viwanda tutapata ajira, tutakusanya kodi, tutakwenda kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo tutapata fedha. Kwa hiyo hatuna budi kuwekeza katika sekta hizo ikiwemo kilimo pamoja na sekta nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mazao ya kilimo yanakuwa hayajafikia malengo kwa sababu, kwanza kuna upungufu mkubwa wa huduma za ugani. Tumeona kwamba sera ya nchi ilikuwa kila ni kijiji kupata Afisa Ugani mmoja wa kilimo na mmoja wa mifugo. Lakini tukiangalia kuna upungufu mkubwa sana kwa maafisa kilimo, tuna maafisa kilimo takriban 6,700 ilhali wanaotakiwa ni 21,288. Hii inaonesha kwamba ratio ya Afisa Kilimo mmoja ni kuwahudua wakulima 600. Hatuwezi kufanya maajabu au mapinduzi makubwa kwenye kilimo kama tupo hivi.

Mheshimiwa Naibu Waziri, japo naipongeza sana Wizara kwa sababu pia imetenga fedha kwa ajili kuboresha huduma ya ugani, imeweke bilioni 11.5 kwa ajili ya kununua pikipiki 1,500 kwa ajili pia ya kuwapa maafisa kilimo extension kit pamoja na soil test kit lakini bado hizi 1,500 hata si robo bado vitendea kazi vinatakiwa kwa maafisa ugani. Mimi nilikuwa naomba kama kuna uwezekano kitengo hiki kiongezewe bajeti kutoka kokote itakavyopatikana ili Watanzania walio wengi ambao ni wakulima waweze kufikiwa na huduma za ugani. Lakini vile vile Maafisa Ugani waajiriwe. Kuna halmashauri nyingine hali yao ni mbaya sana kwa ajili ya upungufu wa huduma hizi za ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na tatizo la pembejeo, mimi naisifu sana Serikali kwa sababu imeongeza bajeti ya kituo cha utafiti ili waje na mbegu bora ambazo zitakuja kuzalishwa na ASA, hata ASA imeongezewa bajeti. Bajeti ya utafiti imeongezwa kutoka bilioni 7.5 hadi bilioni 9.9. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Utafiti vina kazi nyingi tunahItaji utafiti kwenye kilimo. Kwa mfano licha ya mbegu pia wanatakiwa kutufanyia utafiti wa agroecological zone, tujue ni mazao yapi yanatakiwa kuzalishwa wapi, tunatakiwa kufahamu hali ya rutuba ya udongo. Wakati mwingine tunamshauri mkulima apande na dup, nani anayefahamu kwamba pale kulikuwa shida ya phosphorus, ndio maana mkulima anaingia gharama kubwa, anatumia hiyo dup lakini at the end of the day bado matokeo ni madogo. Kwa hiyo tunahitaji utafiti tusibahatishe hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imeongeza maradufu bajeti ya Wakala wa Kuzalisha Mbegu (ASA), kutoka bilioni 5.4 hadi bilioni 10.5. Tunaiomba ASA sasa isimamiwe, izalishe ile mbegu inayohitajika. Kuna mbegu kwa mfano za alizeti, mkulima atahangaika atavuna alizeti, lakini gunia zima la alizeti akienda kukamua anaenda kupata lita ishirini, ndoo moja. Kwa hiyo tunahitaji wazalishe mbegu chotara ambazo kweli zinakwenda kukidhi. Mtu anavyotoa jasho kwamba anaenda kufanya kile kilicho bora, pamoja na mbegu ya ngano nashairi, mbegu ya mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu Watanzania wengi kwa mfano Kanda ya Kusini kule wanatumia mbegu za mahindi za Zambia, ambazo ni za Kampuni za SEEDCO na Mosanto pamoja na watu wa Kanda ya Kaskazini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshalia Mheshimiwa.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo. Napongeza kazi kubwa iliyofanyika na Wizara hii, wametuletea bajeti nzuri na kutuonyesha maeneo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama kuna maeneo Tanzania hatutajutia kuwekeza maeneo yenye risk ndogo, basi ni Sekta ya Mifugo. Ukiwekeza katika Sekta ya Mifugo siku zote ujue kwamba risk ni ndogo unaenda kuwekeza na unapata faida ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano, tukanunua meli tukafanya Uvuvi wa Bahari Kuu, si tunanunua, tunavua, tuna- export Samaki, tunapata kipato au tukaamua kunenepesha mifugo, tunanenepesha tunawauza tunapata fedha. Kwa hiyo Sekta ya Mifugo ni sekta ya kuleta uchumi, lakini ni sekta ambayo tukiwekeza hatutajutia. Mheshimiwa Waziri ametuonyesha maeneo ya kuwekeza katika sekta hii ili kuweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji transformation katika Sekta hii ya Mifugo, lakini sasa sijui kwa nini anafanya vidogo vidogo, pengine na bajeti hii ni ndogo, maana na bajeti ametengewa bilioni 295.9. Kwa mfano, ameeleza kabisa kwamba, tija ni ndogo kutokana na mifugo. Tunaona kwamba pato la Taifa bado limebaki kuwa kwa asilimia saba na sekta inakua kwa asilimia kidogo na tija ni ndogo, tumeona sababu mbalimbali, lakini mojawapo ni hili la kwamba aina ya mifugo yetu tuliyonayo hata tungefanya nini bado watakuja na tija ndogo. Aina ya mifugo tuliyonayo ambayo ni mbari za mifugo na kosafu. Kila siku nazisema, hata ungemlisha ng’ombe wa kienyeji namna gani, bado utakamua nusu lita mpaka lita mbili ya maziwa. Tunahitaji kubadilisha aina hii ya kosafu za mifugo yetu, hata ukimlisha namna gani ng’ombe huyu wa kienyeji ataishia kwenye kilo mia, mia na hamsini hazidi mia mbili, hata huwezi kumchagua kwenda kunenepesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona mpango wa Waziri hapa ni kufanya uhamilishaji katika kubadilisha kosafu za mifugo, lakini analenga mifugo laki moja tu, sasa najaribu kuona kwa nini laki moja tu? Laki moja ni kidogo sana, tena na anataka kufanya katika mikoa 26 ya Tanzania. Ukilinganisha na mifugo tuliyonayo milioni 36, laki moja ni wachache na trend ya uhamilishaji naona inazidi kushuka, sijaelewa ni kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu imeonesha kwenye jedwali la Waziri mwaka 2019/2020 alihamilisha mifugo elfu sitini na saba na pointi. Mwaka 2021 alihamilisha ng’ombe 77, lakini mwaka uliopita alihamilisha ng’ombe 60,600. Sasa trend ya Waziri inazidi kushuka. Nafikiri kuliko kutawanya hizi nguvu ndogo katika mikoa yote 26, ni kwa nini wasifanye kampeni, akafanya uhamilishwaji kwenye mikoa miwili au mitatu wakaboresha mifugo ya pale, kwa sababu kuboresha mifugo ni kumbadilisha mfugaji kwenye mitazamo yake. Tukambadilisha mfugaji akaona ubora na wafugaji wenyewe wataazimana, akiona sehemu ambayo mifugo imekuwa bora, wataazimana mbegu, wataazimana madume. Kwa hiyo hili ni muhimu sana na hii ni pointi ya kuleta transformation katika ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tu kwamba mifugo imeongezeka, kuna mmoja amesema mifugo ni kero, mimi sitaki kusema mifugo ni kero. Mifugo ni benki kwa wafugaji, lakini tujue tu kwamba Tanzania ardhi yetu ni ile ile tuliyopewa na Mungu na sisi tunaongezeka na nyanda za malisho haya ndiyo hizi hizi kila siku zinasogezwa zinakuwa maeneo ya kilimo, ndiyo hizi tunaendeleza maeneo ya makazi na zinazidi kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukisema tu kwamba tuko proud pengine na mifugo kuongeza ni nzuri na nakubaliana, lakini bado haijawa mifugo yenye tija na sababu ndiyo hizi hizi. Kwa hiyo kuwabadilisha mitazamo wafugaji ni muhimu, wanatakiwa kuona kwamba watoke kwenye mifugo hii ya kienyeji ambacho kipato chake ni kidogo, waende kwenye dume ambalo wataliona ni zaidi ya kilo mia nne au mia sita kama wanavyoweza kuiona Nane Nane ndiyo watabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo efforts ziongezwe kwenye uhamilishaji kubadilisha kosafu za mifugo, hili ni muhimu sana na nalirudia, lakini pia Waziri ameeleza kwamba atanunua madume 200, sasa madume 200 ni wachache sana. Haya madume 200 kama atagawa tena kwenye mikoa 26, ina maana kila mkoa utaenda na madume saba saba. Hata kama ni Manyara ina maana kila Mbunge ataondoka na dume moja, sasa kweli mpaka hii mbegu ienee ni leo? Hawa wafugaji wakiweza kuwaelekeza ni wapi madume bora wanapatikana na wakawapelekea watakuwa tayari wao wenyewe kuwanunua at least kubadilisha. Pia nimeona kwamba Waziri anaongeza mitamba 1,200, nami natamani Mradi wa Ng’ombe wa Maziwa ungewasaidia sana akinamama waweze kusambazwa, wauze maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenyewe umetoa kibali cha kuingiza maziwa kwa kipindi kilichopita lita milioni 11.6 kwa fedha za Kitanzania bilioni 22. Hii inaonyesha kabisa tu kwamba uzalishaji wa maziwa katika nchi yetu ni mdogo na ndiyo maana tuna-import maziwa, ya kwetu yenyewe hayatoshi kwenye viwanda vya usindikaji, lakini tuna fursa kubwa sana ya kuzalisha maziwa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mtanzania unatakiwa unywe maziwa hata lita 200 kwa mwaka, lakini tunakunywa chini ya kiwango na watoto wetu wanapata udumavu, ujue Tanzania nayo iko kwenye orodha ya udumavu. Tunapaswa kuongeza uzalishaji kwa kuleta madume bora, mitamba bora, lakini pia kwa kufanya uhamilishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kwamba changamoto nyingine iliyoko kwenye mifugo ni hii ya magonjwa. Magonjwa ni mojawapo ya sababu inayorudisha nyuma Sekta hii ya Mifugo. Tunashindwa kuuza mifugo yetu nje kwa sababu wanahitaji kujua background, hii mifugo iliwahi kuugua labda magonjwa ya mdomo na miguu (FMD) na vitu vingine. Mifugo inayoumwa siku zote quality yake ni ndogo, nyama yake ni ndogo, maziwa yake ni kidogo. Sasa inatakiwa kukomesha kabisa au kupunguza magonjwa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kabisa tu kwamba wataalam hatuna. Kwa mfano, kwenye wilaya nzima hatuna Madaktari wa Mifugo, wale wa veterinary per se, kuna kada za mifugo huko ziko za Animal Production, Range Management na zingine, lakini hawa wa veterinary hawapo. Ndiyo maana wafugaji wetu siku zote wanapata shida. Nimeona wafugaji wakihangaika kutibu mifugo yao wenyewe, yaani kwa ugonjwa mmoja mfugaji anatumia uzoefu wake, atatumia aina tatu za dawa, atanunua oxytetracycline (OTC), penicillin, sijui gentamicin zote anakwenda kumdunga ng’ombe mmoja kwa dozi anayoijua kwa sababu hana sehemu ya kupata utaalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeua Veterinary Centers, hata kama haiwezekana kwenye kata, hizi Veterinary Centers ziwepo basi kwenye halmashauri ili tuweze kuchunguza magonjwa hasa ya mlipuko. Ugonjwa wa mlipuko ukitokea katika halmashauri mpaka sample ipelekwe mkoani na ilete majibu ndiyo ianze kushughulikiwa, hebu tuboreshe kwa sababu tatizo limekuwa kubwa. Kwa sababu wataalam hawa ni wachache kwa nini Wizara sasa isifikirie kuwafundisha ma-para professional wengine kwa kila kijiji ili waendelee kusaidia wafugaji, wasiendelee kuhangaika na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili la majosho ili kuweza kupunguza magonjwa ya mifugo. Nampongeza ameweza kujenga majosho ya kutosha na kuwa na majosho ni jambo jema, naomba aongeze majosho kwa sababu ng’ombe hawatakiwi kutembea mbali na maeneo yote ni mashamba, ingewezekana hata kila kijiji kikawa na josho kama siyo kila kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu majosho kuwepo ni jambo moja bado matumizi ya josho hayajawa mazuri, majosho yapo lakini watu hawaogeshi, naomba Mheshimiwa Waziri afanye utafiti tatizo ni nini? Wakipewa dawa ya ruzuku pengine kwa mara ya kwanza wataogesha, baadae wanaacha kwa sababu kuogesha ni kwenye majosho na majosho ndiyo namna nzuri ya kuweza kupambana na magonjwa ya kupe, tujue sababu ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sheria lakini sheria zetu zimekaa kwenye vitabu, mara pengine ni vizuri kutumia sheria kuogesha ili watu wakaogeshe mifugo, kwa sababu kama nyumba moja inaogesha nyingne haiogeshi na sehemu ya malisho ni moja bado mzunguko wa kupe utaendela kuwepo pale, kwa hiyo hilo mimi naomba uliangalie.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine labda ni ubora wa madawa. Hebu tuangalie ubora wa madawa, kwa sababu mifugo hii inaogeshwa ile ratio ya dawa ya kuogesha hii, unaweza ukasema CC Mbili labda kwenye lita moja ya maji, lakini unaogesha ng’ombe au unampeleka kwenye deep anatoka pale bado ana kupe. Tujue tatizo ni nini? Ndiyo maana ukiona kwenye dawa pengine maelekezo ni kuchoma CC 10 kwa ng’ombe, wafugaji wananchoma mpaka 20 na 30 kwa sababu akichoma hiyo 10 kama ilivyo kwenye maelekezo anaona ugonjwa huo hautibiki. Pengine kuna uchakachuaji kwenye madawa haya ya mifugo naomba ufatilie.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Yustina.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi nafasi nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza nampongeza Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu toka tumepata uhuru tunapigana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi pamoja na umaskini, lakini unaangalia toka tumepata uhuru sasa tuna miaka 60, ukikaa saa zingine unafikiria hivi tunatumia silaha gani butu namna hii miaka 60 bado tunapigana na ujinga, magonjwa na umaskini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, silaha pekee ya kupambana na hao maadui ni elimu. Sasa tuangalie mfumo wetu wa elimu kweli umetuandaa kupambana na ujinga? Kama tunasema mtoto wa shule ya msingi angalau ajue KKK (K- Tatu), hivi KKK katika ulimwengu wa sasa wa dijitali wa utandawazi ndiyo umemtoa kwenye ujinga? Kwa hiyo, lazima tuangalie hii mifumo yetu inatupeleka wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wameandaliwa kupambana na magonjwa? Jana Waziri wa Afya alikuwa anahitimisha hapo akasema kupambana na magonjwa ni kubadilisha lifestyle. Achana na mafuta, sukari, chumvi na pamoja na mazoezi. Sasa ni Watanzania wangapi wanaelewa ni namna gani kwa kuelimika kwao watapambana na magonjwa ili siku moja Tanzania Malaria iwe historia kama ilivyo ukoma ni historia, kipindupindu ni historia. Tunahitaji silaha ambayo ni elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ndoto ya kwenda kwenye uchumi wa kati. Tunawategemea hawa vijana watupeleke katika uchumi wa kati. Tunajua demografia nchi yetu asilimia 70 ya vijana ni wana umri kati ya mwaka mmoja mpaka miaka 30. Hao ndiyo tunaowategemea, elimu yetu ni kwa kiasi gani imewaandaa hawa kwenda kujiajiri na kwenda kufanya shughuli ili walipeleke Taifa letu katika uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mama yetu amekumbuka akaliona hili akasema sasa tuangalie upya mitaala pamoja na sera ya elimu ambayo sasa itatupeleka kupambana na hali hiyo ili kijana wa Tanzania sasa aweze kujitegemea, aweze kujiajiri na aweze sasa kuiletea nchi yetu uchumi na tuweze kuvuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napongeza mtaala huu unaonekana utakuwa mtaala mzuri tu, kwa sababu unaonyesha sasa kuanzia form one kutakuwa na mikondo miwili. Kuna mkondo mmoja ambao ni elimu ya jumla hii ambayo wanafunzi wanasoma form one mpaka form four, pia kuna huo mkondo mwingine wa elimu ya awali ambayo ni elimu ya ufundi, itamsaidia kijana kujifunza ufundi wa namna yoyote ili atakavyofika form four aweze kujiajiri na aweze kujitegemea, kwa sababu atakuwa amepata ujuzi na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji maandalizi makubwa. Kwanza wananchi wa Tanzania wenyewe wajiandae kwamba tunavyoenda kwenye mfumo huu ni vitu gani hasa vinatakiwa lakini na vijana tunaowapeleka shuleni wanapaswa kupata elimu. Serikali sasa ndiyo ifikirie tu kwamba tunavyoenda kwenye mfumo huu ambao Mheshimiwa Waziri amesema, ataanza pilot area mwakani, mwaka 2024, ni kwa kiasi gani kwa sababu tunahitaji bajeti ya miundombinu, tunahitaji walimu waliobobea. Isije ikawa tena ni elimu ya nadharia, unamtoa mtoto pale form four, unamtoa mtoto pale form six au hiyo technical school bado ni nadharia akawa hajajifunza kitu. Kwa hiyo, ninawaomba Serikali ifikirie kama tunaanza tentatively mwakani, japokuwa ni pilot area na hili ndiyo tulilokubaliana na ndiyo tunataka sasa tutoke kwenye maadui hawa watatu, basi Serikali itenge pesa za kutosha ili Wizara iweze kujiandaa kwa jambo hili geni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloliona la kurudisha elimu yetu nyuma isiwe bora sana ni suala la miundombinu. Tulikuwa tunaona zamani tukishindanisha shule zetu, shule za private, shule za seminari zilikuwa zikiongoza kwa ufaulu lakini ukiangalia siri ni nini ndani? Mwalimu wa seminari ana wanafunzi 45 tu darasani ukilinganisha na shule za Kata wakati huo mwalimu ana wanafunzi hadi 100 anaowafundisha. Je, anao uwezo wa ku-monitor na kufuatilia mtoto huyu anafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi Taifa limefanya kwa nia njema, kwa mfano suala la elimu bure. Elimu bure imeongeza ufaulu kwa shule ya msingi na kuongeza ufaulu katika shule ya msingi ina maana pia imeongeza udahili wa form one. Imeongeza udahili kwa asilimia 88. Kwa mfano, tukiona mwaka wa 2021, watoto wa form one walikuwa wamedahiliwa 780,376 lakini mwaka jana 2023 wamedahiliwa wanafunzi wa form one 1,073,000. Sasa implication ya hii ina maana kwa sababu wengi wamedahiliwa bado tunahitaji vyumba vya madarasa, bado tunahitaji matundu ya vyoo, bado tunahitaji vitabu, tunahitaji walimu. Sasa Serikali inavyofanya vitu kwa nia njema, tunasema safari moja inaanzisha nyingine, imejipangaje sasa kuendana na hayo matokeo ambayo tuliyatarajia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kazi kubwa sana kuiweka hii katika historia kama tutakubaliana kama upungufu wa madarasa ambao unaenda kwenye 102,000 na hata ripoti ya CAG tumeiona ya mwaka 2021 imeonesha katika Halmashauri 45 imeonesha kuna upungufu wa madawati 158,000, matundu ya vyoo 56,000, nyumba za walimu 35,000, madarasa 27,000 katika Halmashauri hizo 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu kwamba ni afadhali kuachana na hii kwa sababu kwanza tukiingia kwenye huu mfumo ambao utakuwa na madarasa ya kawaida ya elimu na itakuwa na madarasa ya amali bado tutahitaji madarasa zaidi. (Makofi)

Sasa tungeachana na huu upungufu. Kwa vile tunafahamu kwamba darasa moja linajengwa kwa shilingi milioni 20, Serikali ingeongeza bajeti basi katika Wizara hii ili tujenge madarasa at least 25 kwa mwaka ambapo itaenda kwenye shilingi bilioni 500 kwa mwaka ili katika historia tutakuwa tumekamilisha upungufu wa madarasa, tukapambana na jambo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kuangalia Bajeti ya Wizara ya Elimu, naipongeza Wizara kwa sababu bajeti imefika shilingi trilioni 1.6, lakini ninaangalia bajeti iliyoenda kwenye maendeleo ambayo ni shilingi trilioni 1.1, lakini asilimia 67 ya bajeti hii ambayo ni sawasawa na shilingi bilioni 738.7 inaenda kwa mkopo wa elimu ya juu na asilimia 33 ambayo ni sawasawa na shilingi bilioni 363.1, ndiyo inayoenda kwenye investment. Sasa najaribu kuangalia, watu wanaweza wakaona kwamba bajeti kubwa ya elimu ya maendeleo imefika Shilingi trilioni moja, lakini fedha za investment hapo bado ni kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone kama kweli tuna nia njema ya kuboresha elimu, tuangalie kwamba bajeti inayoenda perse kwenye investment. Kwa sababu ukiangalia fedha inayoenda kwenye mkopo ambayo pengine wanafunzi watakuja kudaiwa, mimi binafsi najaribu kuona labda iwe revolving fund kama siyo hivyo, iwe capacity building. Ingefaa zaidi hata iitwe capacity building, lakini tukiweka kama ndiyo fedha za maendeleo, kama ndiyo investment, kwa vyovyote vile tutakuwa sijui tunajidanganya au tunaiumiza Wizara, kwa sababu uwezo wa kufanya kazi ni mdogo, fedha zinazobaki kwenye investment ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahitaji kufanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na utafiti, kujenga miundombinu. Naona mara nyingi Waheshimiwa Wabunge mkiuliza kujengewa VETA kwenye majimbo, mkoani, lakini pesa za Wizara ndiyo hizi, kidogo, pamoja na kuwafundisha walimu na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee pia ruzuku ambayo Serikali inatoa kwa shule ya msingi zaidi, inatoa ruzuku ya shilingi 10,000 kwa mwaka. Katika fedha hiyo, shilingi 4,000 inaenda kwenye vitabu, na shilingi 6,000 ndiyo inaenda shuleni. Ukigawanya hiyo shilingi 6,000 kwa mwaka ina maana kwa mwezi ni shilingi 500 kwa mwanafunzi. Hivi mwalimu anaweza kufanyaje kwa shilingi 500 kwa mwezi kwa mwanafunzi mmoja? Ruzuku hii ni kidogo. Kuna walimu wanajiongeza. Kuna clip moja ilikuwa inatembea, mwalimu anafundisha mambo ya kemikali, ameleta maziwa ya mgando, limao, na kadhalika; hivi mwalimu akitaka ku- demonstrate, anataka kufundisha kwa vitendo, ukamwachia shilingi 500 kwa mwezi, anaweza kufanya kitu gani? Kwa hiyo, ruzuku hii ni ndogo, Serikali ifikirie tu kuongeza basi angalau ifike hata shilingi 20,000 au shilingi 25,000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naona linarudisha nyuma ubora wa elimu ni uhaba na ubora wa walimu. Tumeona uhaba wa walimu ni mkubwa. Kwa shule ya msingi tunaenda kwenye 100,958 na shule ya msingi tunaenda kwenye 74,000, ukijumlisha unapata 175,000. Naipongeza Wizara ya TAMISEMI na Mheshimiwa Rais kwa kutoa kibali hicho cha kuajiri walimu 13,000, lakini kiukweli speed hii ni ndogo, mpaka kuja ku-overcome hiyo gap ya 175,000.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina, muda wako umekwisha.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kunikumbuka na kunipa nafasi ya kuchangia sekta hii nyeti ya kilimo, ungetoa nafasi kwa kila Mbunge hapa angekuwa na jambo la kusema kuhusu sekta hii nyeti sana inayogusa maisha ya Watanzania na ni kwa sababu aidha kila mmoja hapa alikuwa na kura yake moja ya mkulima au mfugaji, na huenda karibu Wabunge wengi hapa ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ya Kilimo inagusa maisha ya Watanzania wengi kwa asilimia zaidi ya 60 tukiongelea asilimia 65 hii ni kwa sababu ya wastani wa vijijini na miljini.

Mheshimiwa Spika, lakini ukienda kwenye Majimbo ya vijijini huko asilimia zaidi ya 90 ni wakulima lakini ndio sekta iliyokumbwa na changamoto nyingi tu ukiangalia katika hatua zote za mnyororo wa thamani katika sekta hii ya kilimo kwanza uzalishaji una changamoto nyingi kwasababu kuna uzalishaji mdogo kwa hekari, ukisogea kwenye usindikaji kuna changamoto ukienda kwenye masoko kuna changamoto kibao.

Mheshimiwa Spika, hatujaweza kuwekeza vya kutosha katika sekta ya kilimo ili kumtoa mkulima huyu katika hatua aliyonayo kumsogeza katika mapinduzi na kumtoa katika umaskini kwa sababu changamoto hizi zote zina dawa. Tunaongelea habari ya mbegu lakini kuna dawa, inatakiwa tutoe fedha katika mafiga matatu ya kuweza kutuletea mbegu bora wakiwepo TOSCI, TARI na ASA ili wakulima hawa wapate mbegu bora wanazozihitaji.

Mheshimiwa Spika, watu wanaongelea kuhusu habari ya alizeti, mbegu zinazotolewa na ASA ya record huwezi kufananisha na mbegu ya hybrid ambayo inauzwa bei ya juu takriban Sh.35,000 kwa kilo kwa sababu mbegu zinazotakiwa na wakulima ni mbegu bora na chotara. Ni kwa nini sasa tusitatue changamoto hii ya kutokuwa na mbegu bora wakati tuna fursa nyingi na za kutosha?

Mheshimiwa Spika, katika uzalishaji mdogo mimi naenda kugusa zao la ngano. Tabia ya ulaji ya Watanzania sasa imebadilika na kwamba ngano ni kati ya mazao muhimu ya chakula. Ngano sasa ni zao namba nne ikifuatiwa na mahindi, mihogo na mchele. Ukitaka kuhakikisha kwamba ngano utaona Tanzania sasa bakeries nyingi zimefunguliwa kila mtaa na ukienda kwenye vioski vya vijijini wanauza mikate na maandazi.

Mheshimiwa Spika, lakini inasikitisha sana kwamba Watanzania ngano tunayokula siyo ya kwetu, tunaingiza ngano kwa dola nyingi za Marekani. Sisi tunatafuta foreign currency kwa ajili ya kununua vitu vingine lakini kumbe tunaagiza chakula. Hii haikubaliki kabisa. Watanzania kwenye miaka ya 70 hadi 80 we were good producer of wheat…

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Longido unakata katikati ya mwongeaji na Spika, endelea Mheshimiwa.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunilinda. Naendelea kuelezea masikitiko yangu kwamba kwa kweli si sahihi na haikubaliki kwa Watanzania kuingiza ngano kwa fedha za kigeni kwa sababu tulikuwa na mashamba makubwa….

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa, nimekuona Mheshimiwa Asia.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kumpa taarifa mchangia hoja kwamba hata Wilaya ya Hanang ambapo ndiyo sehemu kubwa ya kilimo hiki cha ngano tunaiomba Wizara ije kuona kwa sababu mashamba mengine yamepewa wawekezaji lakini wawekezaji wale wanalima kiwango kidogo sana na eneo kubwa linabaki kuwa pori.

Mheshimiwa Spika, hata Serikali yenyewe ina eneo la ekari 12,000 ambapo halmashauri imechukua eneo dogo kwa ajili ya kukodisha wananchi lakini eneo lingine Serikali imeliacha limekuwa pori. Sasa tuombe kwa sababu Serikali ilishaamua kukikuza kilimo hiki cha ngano na kukifanya kuwa cha biashara basi waje wawekeze kweli kweli kuanzia kwenye mashamba ya wawekezaji lakini hata kwenye mashamba yenyewe ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa Yustina unaipokea?

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana mdogo wangu Asia, naipokea taarifa yake kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna historia kwa mfano kama alivyotoa mfano mdogo wangu Hanang tukishirikiana na Canada miaka hiyo yale mashamba yote sasa hivi yamegawanywa kwa wafugaji, wakulima wadogo wadogo na private sector wame-fragment mashamba yale makubwa katika vipisi vidogo vidogo hatuwezi tena kulima ngano. Kilimo cha ngano ni lazima kifanyike katika mashamba makubwa kwa sababu kilimo hiki ni mechanical agriculture kwa sababu ngano utapanda kwa planter, utapalilia kwa mashine na utakuja kuvuna kwa combine harvester, hatuwezi kuachia wakulima wadogo wadogo. Mashamba ya NAFCO yale wamechukua wawekezaji, yamekuwa privatized katika sekta binafsi na hatukuwapa incentive kwa sababu ngano ilikosa bei. Naishauri Wizara ije na mpango kwamba sasa hatutaendelea kulishwa ngano na nchi za nje na kwamba tutaokoa hela hizo za kigeni zinazoenda kununua ngano na kwamba mpaka miaka mitatu kuanzia leo tutakuwa tumejitosheleza kwa soko la ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine unaenda kwenye upotevu wa mazao baada ya mavuno. Ni kweli kabisa tumeacha wakulima hawa wakihangaika. Nashukuru Wizara na naipongeza kwamba imekuja na teknolojia ya kutumia vifungashio ambavyo haviingizi hewa (hermetic). Kuna serial za chuma, plastics lakini na mifuko hii ya PICS. Hii ni namna pekee ambayo wakulima hata sisi walaji wa chakula tutakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya wakulima hawa kutumia viatilifu vingi vya unga mara nyingi wanakuta mahindi yao yamepekechwa na kwa ajili hiyo wanachanganya madawa mengi kina Actel, Duduba, unawakuta mahindi yako mazima sokoni kumbe tunaenda kula sumu. Kwa ajili hiyo hii mifuko ya PICS na vifungashio vingine ambavyo sasa vinauzwa ghali, serial ya chuma ya kuweka magunia matano inaenda mpaka laki na kitu, mifuko hii inauzwa Sh.5000, tunaomba sasa Serikali ifanye namna yoyote ya kuweza ku-subsidies ili angalau mifuko hii basi wakulima wapate kwa Sh.2,500 hadi Sh.3,000 waachane na kutumia viatilifu hivi ambavyo vina kemikali nyingi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.(Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia hoja hii ya Azimio la Kuridhia Itifaki ya viwango vya Afya ya Mimea, Usalama wa Wanyama pamoja na vyakula vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Community Sanitary and Phytosanitary Protocol).

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na tumeingia kwenye Jumuiya hii tukakubaliana mikataba, tukasaini mkataba toka mwaka 1999. Kati ya Mikataba hii inataka tushirikiane Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mambo mbalimbali kwa usawa na haki kwa ajili ya manufaa ya nchi wanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele kimojawapo ambacho kipo kwenye mikataba hii ni kipengele namba 151 ambacho kinataka Nchi Wanachama kutengeneza Itifaki ya Kuridhia Afya ya Mimea na Usalama wa Wanyama pamoja na chakula na sisi Tanzania tulisha iandaa hii na kuitayarisha toka mwaka 2013.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba sisi ni Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki vile vile sisi ni Wanachama wa Shirika la Biashara la Dunia (World Trade Organization), sisi kuwa wanachama wa Jumuiya ya World Trade Organization imetulazimu vile vile kutekeleza baadhi ya makubaliano ambayo mojawapo ndio hii Itifaki ya Afya ya Mimea na Usalama wa Wanyama pamoja na Usalama wa Chakula, imebidi tutekeleze kwa sababu na sisi ni wanachama ambapo sasa makubaliano haya yanaitwa The Agreement on the Application of Sanitary and Phytosanitary Protocol. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Itifaki hizi lengo lake kubwa ni kulinda afya ya mlaji popote pale. Ndio maana sisi sasa tunatekeleza makubaliano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo makubaliano ya usalama wa chakula ambayo inaitwa the Codex Alimentarius Commission na vilevile ya usalama wa mimea ambayo ni International Plant Protection Convention na pamoja na hii ya usalama wa wanyama World Organization for Animal Health.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwa kuingia au kuridhia Itifaki key ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa vyovyote vile tuna faida mbalimbali ambazo kama Nchi Tanzania tutaweza kuzifuata na moja wapo ni kukua kwa biashara ya mazao, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyoona kwamba kijiografia sisi tuko vizuri, sisi ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula. Kwa hiyo kuwa na document ya pamoja, Itifaki itatusaidia sisi kuweza kuingia kwenye biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tunafahamu kwamba sisi soko letu kubwa la mahindi lilikuwa Kenya lakini hivi karibuni tumeona vizuizi kwamba mahindi yetu walisema yana sumu kuvu. Sasa tungekuwa tayari tuna hii Itifaki inayokubali kiwango gani cha sumu kuvu ambayo tumekubaliana katika Itifaki hii pengine hiki kizuizi kisingekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile sisi Tanzania ndio wafugaji wakubwa, ndio tuna mifugo mingi katika nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo moja kwa moja hii inatupa fursa sisi Watanzania, kwamba sasa tunaweza tukaingia kwenye soko la Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, faida nyingine kubwa ni kwamba sasa Itifaki hii itatoa hamasa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na taasisi mbalimbali kwamba sasa wakazalishe kwa viwango vinavyotakiwa ku-win biashara hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Kimataifa. Kwa mfano tu, wafugaji wanapaswa kuogesha mifugo yao pamoja na kuwapa chanjo pengine labda ya ugonjwa wa midomo na kwato, kwa sababu hii mara nyingi imekuwa kizuizi ili kwamba mifugo yao pamoja na mazao ya mifugo kama nyama na maziwa iweze kupata soko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nawashauri na Wabunge wenzangu kwa sababu kuna round table kuweza ku-harmonize mambo fulani kama GMO ambayo sisi kwa kisera tulishayakataa, Itifaki hii ipite na tuweze kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na biashara ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naelekeza mchango wangu kwenye changamoto hii kubwa ya ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wanamaliza kusoma katika madaraja mbalimbali, lakini wanapata changamoto kubwa sana ya kutafuta ajira ili waweze kujikimu kwa maisha. Tunafahamu kwamba kwa demokrasia ya nchi yetu idadi kubwa ni vijana, asilimia 35 ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 35. Hao ndio nguvu kazi tunayoitegemea, hao ndio wenye ari na morali wa kuijenga nchi yetu ambayo tunafikiria tunaingia kwenye uchumi wa kati, lakini hautajengwa na wazee utajengwa na vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, crises ya ajira ni kubwa sana na sisi wenyewe tunaiona, hebu ona ukitangaza nafasi 100 ya ajira, applicants walivyo wengi ni elfu na zaidi, sisi wenyewe tukija huku Bungeni tumebeba mabahasha ya vijana wetu, wanataka kazi. Wengine wanao-sustain maisha pengine wanafanya kazi ya boda boda au wenye miamala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, boda boda wanakaa vijana kwenye kituo kimoja 20 au 40 akisubiria mteja akiwa na stress ya kufikisha mahesabu ya tajiri wake na ndiyo maana pengine wanapata ajali na wanaishia kukatwa viungo vyao. Nafikiri tuliangalie vizuri hii crises ya ajira na tunaona kwamba kwa mahesabu Word Bank kwamba kila mwaka Tanzania kuna vijana kama 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira, fikiria kuna mwaka juzi hawajapata ajira, wa mwaka jana, mwaka huu na hatuwezi kuepuka kwa sababu tunawasomesha na tunaendelea kuzaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kuna fursa kubwa pengine kwenye kilimo, kama tutakifanya kilimo kikawa kizuri na kikavutua kwa vijana na kilimo kitakachovutia vijana ni kilimo cha bustani ya mboga mboga na maua, kwa sababu ni kilimo ambacho atapata fedha haraka sana. Nafikiria hivyo, lakini changamoto ya vijana hawana ardhi, changamoto ya vijana hawana nyenzo, wala hawana mtaji. Sasa ni kwa nini basi Serikali nilikuwa nafikiria kwa kusaidiana pengine na halmashauri, wakaweza kutafuta ardhi ya kilimo hata kwenye halmashauri, wakawapa hawa vijana kwa kuwasimamia wakazalisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano nilikuwa naangalia kijana ukampa nusu heka ya kuzalisha labda mchicha tu ambao anaweza akapata fedha kila baada ya wiki tatu maana mchicha unaweza kuiva haraka. Katika nusu heka anaweza akapata tani nne, sawa sawa na kilo elfu nne, akiuza kwa elfu mbilimbili ana uwezo wa kupata elfu nane, fikiria ni katika wiki tatu, akitoa gharama za uzalishaji anabaki na kiasi cha fedha cha karibu shilingi elfu tano. Sasa ni kwamba sisi tuangalie hiyo namna kuwasaidia hao vijana tukawajengea mazingira mazuri ya upatikanaji wa maji, sehemu ambayo tunaona ni muhimu na maji ni kidogo tukawafungie ile mirija ya kufanya dripping irrigation. Ofisi ya Waziri Mkuu imejenga kitalu nyumba kwenye halmashauri lakini tunaona zile haziko sustainable pengine kwa sababu wangeendelea kujenga vitalu nyumba pengine huko vijijini, lakini vijana wanashindwa kwa sababu ya hizi changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwaacha hawa vijana wakajikatia tamaa kesho ndiyo watajiingiza kwenye makundi ya majambazi na baadaye tutakuwa hatuna usalama na sisi na nchi yetu. Kwa hiyo naomba Serikali itupe jicho la pekee, wakati inaendelea kujenga fursa na ajira pengine kwenye sekta maalum basi waweze ku-accommodate hiki kikundi cha vijana katika kilimo kwa sababu kilimo ndiyo kina fursa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kwenye majanga au maafa. Najaribu kufikiria namna ambayo nchi yetu inashughulikia maafa, Tanzania kama nchi nyingine duniani tunapata maafa mengi, tunapata maafa ya ukame, mafuriko, vimbunga, magonjwa na kadhalika. Sasa kuna sehemu ambayo kwa kweli naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na nchi yetu kwamba kwa kweli wanashughulikia maafa tunaona. Kwa mfano yakija maafa labda ya ukame na mazao kukauka pengine kukawa hakuna chakula, Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga na nchi yetu imejipanga na nina imani kubwa kabisa kwa jitihada ya Rais wetu hakuna Mtanzania atakufa na njaa, kwa sababu kuna chakula cha kutosha kwenye maghala ya Taifa NRFA imenunua chakula, kwa hiyo hapo nawasifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasifu pia Kamati za Maafa zilizoko kijijini kama kule kwangu ni mfano mzuri tu Kamati za Maafa Vijijini wamejipanga, wakipata maafa ya misiba wana namna yao wanasaidiana, wamejiwekea level yao ya michango, wamenunua viti, maturubai, masufuria na kila kitu. Kwa hiyo wako well equipped, utaona kwamba ni namna gani sasa watu wameelewa namna ya kusaidiana kwenye maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shida yangu ni namna ambayo tunapambana na maafa tunapokuja kwa upande wa mifugo ambao hawajui kusema. Nchi yetu imekuwa ikipata maafa ya kufa mifugo karibu kila wakati ikijirudia rudia. Kama tunafahamu tu kwamba kipindi cha ukame na bahati nzuri watu wa hali ya hewa huwa wanatuelekeza kwamba kipindi fulani kitakuwa cha maafa, hivi mfugaji anapopoteza mifugo yake 10, 20, 30 au hata zizi lake lote boma lake likaisha, hivyo anakosa gani mpaka hapo na hatuna mpango mkakati, hatuna coping strategic kama ambazo tunafanya kwa binadamu, maana kwa binadamu chakula kikipungua tunapeana coping strategic tutakula mara chache chakula chetu tutahifadhi, tusipikie pombe, lakini tunapokuja kwa wanyama, tunawaacha wale wafugaji wana-suffer peke yao, mfugaji anapoteza mifugo yake anabaki maskini. Mifugo hii ni chakula, mifugo hii ni benki yao, mifugo hii ndiyo bima ya afya akiugua mtu ndiyo inatumika, mifugo hii ni kila kitu lakini tunawaachia wanahangaika wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiria kwa nini tusiwe na mkakati coping strategic kwenye mifugo ni nini? Kwa nini hata wakati mwingine basi tusiruhusu pengine mifugo ikaenda kuchungwa pengine kwenye buffer zone au sehemu ambayo ni reserved kwa wakati ule wa mwezi mmoja au miwili ili ku-risk mifugo yetu isife kama tunavyowaachia wanakufa mizoga imezidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tufanye utaratibu mzuri hata wafugaji wakalipia kuliko wajanja wachache wachache wao wanaweza wakaingiza mifugo kwenye game reserved, wakatoa rushwa lakini wengine huku wakiwa na stress ya ukame, mifugo ikisogea kwenye hizi buffer zone wanakamatwa na askari na wanashughulikiwa vya kutosha.

Kwa hiyo, nafikiri Serikali sasa iangalie kwa upande mwingine jinsi ya kupambana na haya maafa. Hata hivyo, nafikiria hivi huyu mfugaji anayepoteza mifugo yake yote akabaki maskini Serikali ina mpango gani? Kwa nini isimfidie sasa mfugaji ambaye amerudi kwenye zero point, ndiyo wafidiwe kwa sababu siyo kosa lake, ana kosa gani kama ni hali ya ukame, yeye ametimiza wajibu wake, amepewa mifugo yake amekwenda kuchunga amerudisha jioni, kwa hiyo anapopata maafa kama haya, Serikali ijipange na ikawafidie wafugaji ambao wanapoteza mifugo yao katika ukame wa namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, yanapokuja maafa haya kwa watu binafsi, pengine ya mafuriko, yakachukua nyumba pengine tena za wazazi wetu, ndiyo nyumba ambazo siyo bora au mapaa yakachukuliwa na vimbunga, ninachoona pale ni utashi wa mwanasiasa ambaye yuko pale au ndiyo uwanja wa mwanasiasa, akienda pale na bati mbili au tatu akapigapiga picha ndiyo unafikiri ni solution, kumbe yule mhanga pale pengine amepoteza chakula, amepoteza mavazi, amepoteza kila kitu.

Kwa hiyo nafikiria, Ofisi ya Waziri Mkuu ione namna gani ipambane kwa sababu kwenye shida Watanzania ni sisi na kwenye raha Watanzania ni sisi, tusiache kikundi cha Watanzania wachache wanaokuwa wahanga na majanga haya, wakapata mateso siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ndiyo mchango wangu na naiunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nikachangia Mapendekezo ya Mpango huu wa Taifa wa Mwaka 2023/2024. Mpango huu ni wa tatu katika mpango wa miaka mitano wa 2022 mpaka 2025/2026 na mpango wetu huu unadhima ya kukuza uchumi shirikishi na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunalenga kukuza uchumi wa viwanda na uchumi shirikishi tunategemea mpango wetu huu ungeangalia zaidi catalyst (vichachua uchumi). Vichachua uchumi vyetu hivi ni viwanda ni nishati ni usafiri na usafirishaji ni muhimu sana. Toka tumesema Tanzania ya viwanda bado hatujafanya vizuri kwa viwanda. Viwanda ni kichachua uchumi kwa wazalishaji wote; kwa wakulima kwa wafugaji na hata kwa wachimba madini. Wakiwa na uhakika kwamba viwanda vipo pale kwa ajili ya kusindika, uzalishaji utaongezeka kwa sababu ya uhakika wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini viwanda ndivyo vingeenda ku-solve changamoto ya aijra ya vijana tunayoisema kila siku. Vile vile, viwanda hivi ndio vingesaidia kuongeza kipato kwa mkulima kwa kuongeza mnyororo wa thamani. Wenzangu wamesema, tunazalisha na tunauza malighafi kwa wenzetu. Tunazalisha korosho, pamba, mahindi vinaenda kama malighafi, tunaenda kujenga viwanda vya wenzetu wanasindika na sisi ndio walaji wanaturudishia. Sasa tubadilike na sisi tukatafute masoko ya vitu ambavyo tayari tumeshavi-process kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati ya umeme ni muhimu sana kama kichochezi cha uchumi katika Taifa letu. Niwapongeze tu Wizara tu kwamba wameweza kufikia vijiji 9,160 kati ya vijiji 12,400 na kitu. Umeme ni kichochea uchumi muhimu sana, ni haki ya kila Mtanzania kupata nishati ya umeme. Umeme ambao tayari umekwisha kupelekwa unaishia katika center za vijiji ambapo unapaswa umeme kufika kwenye vitongoji kama ilivyo dhima yetu ili kila mtu a-enjoy kuwa na umeme katika eneo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unatoa ajira kwa vijana walioko vijijini watatengeneza visaluni vyao watukuwa na viwanda vidogo vidogo vya welding wengine watamwagilia kwa kutumia pump. Vile vile ungepunguza hii rural-urban migration, kwa sababu vijana wanaomaliza chuo kikuu ukawapeleka kwenye vijiji ambavyo havina umeme wasingeweza kukaa huko. Umeme tunahitaji wa kuaminika, unajenga fursa ya wawekezaji nikivutio kwa wawekezaji kuja kama kuna umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani mpango huu sasa utuambie, pengine uhakika wa umeme, tungeweza kuupata baada ya kukamilisha mradi mkubwa huu wa Julius Nyerere ambao tulitarijia kupata mega watts 2,115. Mradi huu umeanza tangu Disemba 2018 nawapongeza kwamba tumefikia sehemu nzuri asilimia 77 lakini tumekwisha kuwekeza 1.2 trilioni. Sasa ili weze kutoa output tunakila budi kuona kwamba mpango ukoje na mpango kazi ukoje, kwamba katika mpango unaokuja, tukamilishe ili tuweze kupata umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafirishaji ni changamoto kubwa sana. Usafirishaji huu ndiyo sababu kina mama zangu kule wanalalamika bei kubwa ya vifaa wanavyovitumia, bei kubwa ya pembejeo, kwa sababu barabara na vivuko ni ngumu. Nategemea mpango huu uwekeze vya kutosha kwa TARURA na TANROADS ili barabara zetu na vivuko vipitike mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shida sana, wakulima wamezalisha kule, kuja kuleta mazao yao mjini ni kazi kubwa na yanaharibika mwengine ni perishable foods, zinakaa pengine kwenye usafirishaji siku nzima au siku ngapi baada ya magari kukwama, unakuta kwamba uharibifu wa mazao ni mkubwa sana. Kwa hiyo, tuangalie hizi pillars katika mpango wetu huu. Kwamba lazima tuboreshe hizi viashiria ili kwamba tuweze kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpango huu nategemea pia utaendelea kuwekeza katika sekta za kiuchumi ambayo ni kilimo, mifugo, maliasili pamoja na madini. Mimi nawapongeza sana kwamba tumeshafanya vizuri kwa kuongeza bajeti iliyopita, tumeongeza bajeti zaidi ya mara tatu na tumeanza kuona matokeo makubwa. Sasa ninafikiri uwekezaji huu lazima tuone ni maeneo gani hasa tutawekeza kwenye kilimo. Sehemu ambayo ina - risk kidogo na sehemu ambayo tukiwekeza miradi mikubwa, tukawekeza fedha nyingi itaweza kurudisha kwa mapema, yaani pay back period iwe ndogo. Kwa mfano, naipongeza Wizara kwa mpango wake, sasa hivi tunatakiwa tuhamie kwenye uwekezaji wa mashamba makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Wizara imekwisha kupata ekari 183,000 hapa Chamwino. Mimi nawapongeza kwa sababu kuwekeza katika mashamba makubwa ya pamoja (block farming) ina faida kubwa kwa sababu ni mashamba yapo pamoja uzalishaji utafanyika kwa gharama ndogo, itakuwa economical of scale lakini rahisi kusambaza teknolojia. Vile vile sasa kuweza kupata soko, mazao yanayotakiwa kwa ile quality. Kwa mfano shamba lilipo hapa kama tunawapata assignments watazalisha soya itaenda kuzalisha ile soya ambayo tayari tuna soko lake nje. Basi jitihada hizi zifanyike kwa zone. Kila zone agro-zone, kwa mfano hata Manyara tungeweza kupata mashamba Kiteto, basi yapatikane mashamba yaangaliwe hali ya udongo hata tuka - assign pengine ikazalisha hata mahindi ya njano ambayo tayari tunasoko Misri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mpango huu ni mzuri nawapongeza. Kwamba hatuna risks zozote za kuwekeza katika kilimo kama hicho, na kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ambacho risks zake ni ndogo. Fursa ni nyingi kwenye kilimo, tumeona kwamba maeneo yanoyofaa kwa kilimo ni zaidi ya hekta milioni 44 na ambazo tumeweza kulima asilimia 38 mpaka 40. Kwa hiyo zaidi ya asilimia 60 ya eneo linalofaa kwa kilimo bado halijatumika. Kwa hiyo, bado tunaweza kuweka wawekezaji ambao unalima na ambao hauna risks kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikifikiria kwamba tungeweza kuwekeza pia kwenye mifugo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia ahsante sana. Tungeweza kuweka kwenye ranch zetu kule tukanenepesha mifugo au tukazalisha malisho ya mifugo kwa matumizi ya ndani na nje tungeweza pia kufanya vizuri. Nakushuru sana, naunga hoja mkono. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nami nafasi hii niweze kuchangia taarifa nzuri sana ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uzalishaji maana taarifa imejieleza vizuri.

Mheshimiwa Spika, Watanzania bado tuna- cerebrate, tunaona maono ya nchi yetu sasa ni kwenda kutufikisha pale ambapo maazimio yetu; Azimio la Malapo, Azimio la Maputo siku moja tunakwenda kuifikia asilimia 10 kuwekeza katika sekta hizi za kiuchumi ili tuweze kuimarisha uchumi wetu. Kwa sababu nyongeza ya bajeti hii mpaka bilioni mia tisa na kitu ni sawasawa na na asilimia 1.8 ya bajeti kuu. Tunategemea bajeti tunayoenda pengine tutasogea kwenye trilioni mbili na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kutenga bajeti ni kitu kingine, lakini utoaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pengine ikawa ni tatizo. Nasema hivyo kwa sababu kwa bajeti ya maendeleo hadi kuifikisha tarehe 31 Desemba bajeti hii ya kilimo imeweza kutekelezwa kwa asilimia kumi na tisa na pointi. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sasa kama tumeazimia kweli kuwekeza kwenye kilimo basi Serikali iendelee kutoa fedha ili miradi hii ya kilimo iliyotengewa fedha ipate kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo niseme tu kwamba changamoto kubwa kwenye miradi hii ya kiuchumi yote kilimo, mifugo na uvuvi, changamoto kubwa tulikwishasema ni uzalishaji mdogo na tumeona sababu mbalimbali. Kwa mfano kwenye kilimo ilikuwa ni upatikanaji wa pembejeo kwa ajili ya bei, pamoja na kuweza kufikika kwa muda. Lakini vilevile kilimo cha kutegemea mvua ikiwepo pamoja na matatizo ya utoshelevu wa ugani.

Mheshimiwa Spika, safari hii Serikali imewaunga mkono wananchi kwa kuweza kutoa ruzuku kwa pembejeo ya kilimo ambayo ni mbolea. Pamoja na changamoto lakini tumeona nia nzuri ya Serikali jinsi ambavyo itaenda ku-solve haya matatizo yaliyotokana na usambazaji wa mbolea ya ruzuku. Hii tunaiachia Serikali, imekwisha weka utaratibu maghala yote ya Halmashauri ambayo yapo yatapelekewa mbolea kwa muda. Nafikiri kwa musimu unaokuja mbolea itasambazwa kwa vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumeona impact, toka ruzuku imewekwa katika mbolea, matumizi ya mbolea yamepanda sana na kama kweli Serikali ingewahisha kwa awamu nyingine maana mbolea nyingi iliyotumika ni ya kupandia, pengine mbolea ya kukuzia ikafika kwa muda, tutaona kwamba kuna ongezeko kubwa sana la mbolea ya viwandani ambayo wakulima walikuwa hawajakubali hiyo teknolojia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tunajua kwamba kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa mbegu na ni kwa sababu asilimia kubwa ya mbegu tunazotumia kwa zaidi ya asilimia 60 zinatoka nje hasa kwa mahindi, tunatumia zaidi mbegu za Seedco, Decay, Pan, Pioneer, Zamseed zote hizi tunaziingiza kutoka nje na mbegu hizi ni ghari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ikae na iangalie namna gani inatoa unafuu katika upatikanaji wa mbegu na kwa bei nafuu. Nasema hivyo ili Serikali iweze kutoa bajeti. Ilitenga shilingi bilioni 43 kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na bajeti hii mpaka tarehe 30 imetekelezwa kwa asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, katika kuzalisha mbegu tunaomba Serikali iwezeshe taasisi ya ASA pamoja na vituo vya utafiti iweze kuwajengea miundombinu hasa miundombinu ya umwagiliaji ili mbegu hizi uzalishaji wa mbegu pia tusitegemee mvua. Tuhakikishe kwamba kuna miundombinu ya kutosha ili tuweze kupata mbegu za kutosha wananchi na zile mbegu zinazotakiwa. Kwa hiyo tunaomba Serikali iendelee kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme kwenye umwagiliaji; changamoto kubwa imekuwa ni kutegemea mvua. Tunajua kilimo cha watanzania kinatekelezwa na wakulima wadodgo wadogo kwa asilimia 90. Pia wakulima kila siku wanabaki kwenye dimbwi la umasikini kwa sababu ya kutegemea zaidi mvua. Kilimo ni ghari, mkulima atalima kwa gharama kubwa, atanunua pembejeo kwa gharama kubwa, ametimiza wajibu wake, lakini mwisho wa siku kama mvua zitakuwa haba ndio inaishia kwenye mazao yake kukauka. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile inamrudisha kwenye njaa na kwa vyovyote vile inamrudisha kwenye umaskini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba kwa kipindi kilichopita Serikali imetekeleza kweli miradi ya umwagiliaji midogo midogo ya kukarabati scheme. Sasa tutegemee tena baada ya bajeti kutoka shilingi bilioni 46 mpaka shilingi bilioni 361 sasa ikawekeze kwenye miradi mikubwa ya umwagiliaji ambayo itasaidia wananchi iweze kusogea sasa kutokutegemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu mifugo; tumeona pia chanagamoto kubwa sana kwenye mifugo na tatizo la mifugo ni kuwa na uzalishaji mdogo vilevile. Mifugo ya Tanzania inakumbwa na upungufu mkubwa wa malisho na maji, lakini na magonjwa. Tunaomba sasa Serikali iendelee kuchimba mabwawa pamoja na kuimarisha malisho kwa ajili ya mifugo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya malisho shilingi bilioni 8.5 mpaka mwezi Desemba ilikuwa imetolewa hela kidogo sana kama shilingi milioni 100.

Mheshimiwa Spika, tuwasaidie pia wafugaji, wamekuwa wakihangaika na wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa nini sasa nyanda za malisho zikaendelea kutambulika, zikawekewa GN kama ilivyo maeneo ya hifadhi na maeneo mengine ili wafugaji hawa wasiendelee kuhangaika. Tunaiomba Serikali iwasaidie wafugaji watoke hapo, lakini vilevile na magonjwa. Magonjwa yamekuwa ni tatizo kubwa, Serikali iendelee kujenga majosho ili mifugo iogeshwe, kwa sababu magonjwa mengi ya mifugo yanatokana na Magonjwa yanayosababishwa na kupe na tunatumia fedha nyingi za kigeni ambazo tunategemea takribani bilioni 100 kununua dawa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwa chanjo, ni kwa nini tusiimarishe kituo chetu cha Kibaha kikaweza kutengeneza chanjo za kutosha na kupeleka chanjo kwa wafugaji? Tumekuwa tegemezi. Vilevile tumeua veterinary centers ambazo zilikuwepo katika kata, wafugaji wamekuwa wakihangaika wakitibu mifugo yao wenyewe bila kuelewa na ndio maana tunapata usugu wa magonjwa ya mifugo.

Vilevile huko kwenye Halsmashuri unaweza ukakuta Halmashauri kadhaa haina hata daktari wa mifugo. Hebu sasa Serikali ikawekeze kwa sababu kweli Tanzania tuko proud kwamba sisi ni wa pili kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia, lakini Tanzania bado sisi tuna-suffer na udumavu, Tanzania hatu-export mazao yoyote ya mifugo badala yake bado tunaingiza mazao. Sasa kama tumekubali kuwekeza kwenye mifugo tuone matokeo makubwa ili na sisi sasa tuwe na mifugo iliyo bora, tuweze kupeleka mazao ya mifugo nje kuweza kupata fedha za kigeni na kuongeza GDP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sanakwa kunipa fursa hii, kwamba leo nimekuwa mchangiaji wa kwanza katika bajeti hii ya Wizara ya Maji, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla yayote naomba kumpongeza Waziri wa Maji pamoja timu yake kwa kazi kubwa anayoifanya ya kujenga miradi mikubwa na kusimamia kwa weledi mkubwa, nampongeza sana Waziri kazi yake inaonekana na akijua wazi kabisa kwamba maji ni uhai na kwamba amekwishasema maji hayana mbadala na kwakweli anatendea haki, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba hilo niseme tu, tumshukuru Mungu kwa Tanzania bado tunarasilimali ya maji ya kutosha. Kwa mfano maji yanayoweza kupatikana kwa mwaka ni lita za ujazo bilioni 126, na kati ya hizo bilioni 105 zipo juu ya usawa wa ardhi na bilioni 26 zipo chini ya ardhi; ni maji ambayo yanaweza kupatikana kwa mwaka. Hii inafanya Mtanzania kuweza kutumia maji wastani wa lita 2,250 kwa mwaka, ambapo kiwango cha kimataifa ingekuwa ni lita 1700, na chini ya hapo tungeingia kwenye water stress. Kwa hiyo, tunaona kwamba tunabahati pengine kazi kubwa ni namna gani tunaweza kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo nitoe wito, nimuombe na Waziri kabisa kwamba tunapaswa kuhifadhi vyanzo vya maji ili kwamba kiwango hiki kiendelee kuwepo. Kwa sababu kwa kuharibu vyanzo vya maji pengine kiwango hiki kinachoweza kupatikana kikapungua. Kwa hiyo, akishirikiana na mabonde ya maji nitoe rai kabisa kwamba hifadhi ya vyanzo vya maji ifanyike ili maji yaweze kupatikana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo Mkoa wa Manyara una changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Wakati tukiongelea kwamba Taifa tunaenda kwenye asilimia 72 pengine na kuendelea, ya coverage ya upatikanaji wa maji lakini Mkoa wa Manyara bado tuna asilimia 58 pengine na chini. Hali hii ni mbaya zaidi kwa maeneo ya pembezoni, maeneo ya kanda za chini na maeneo ya wafugaji maji ni machache na ukizingatia vyanzo vya kudumu za maji tiririka hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba tu-focus sasa ya Waziri iende kwenye maeneo hayo kwa sababu kuna mama zangu kule bado wanatembea kilometa nyingi kutafuta maji. Kwa mfano tu kwenye Wilaya ya Mbulu, ukienda kwenye ukanda wa chini wa Yaeda Chini, Endamilay, Eshkeshi, Masieda hali ya maji kule ni mbaya. Nampongeza kwamba huko pia ameweka bajeti ya kuchimba visima. Mimi nimuombe tu kabisa kwamba fedha hizi azitoe na visima hivi vichimbwe ili mama zangu waliopo kule waki-Wabarbeig, Wakiiraki wapunguze huu mwendo, kwa sababu kule bado kuna kuamshana wakati wa jogoo la kwanza ili kwenda kukinga maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nimpongeze tu kwa sababu hata Hanang’ ana mpango wa kuchimba visima tisa kwenye maeneo magumu kama hayo. Maeneo ya Endagau, Wareta, Dumbeta pamoja na mengine. Maeneo haya ni korofi kwa upatikanaji wa maji na kwamba hakuna vyanzo vya maji tiririka. Vilevile anampango wa kuchimba visima 13 katika Wilaya ya Simanjiro pamoja na kufanya extension na mradi mkubwa kabisa ule wa Orkesument ambao alizindua Makamu wa Rais kwamba sasa anapeleka maji Ruremo kutoka mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu kabisa kwamba, katika Wilaya ya Kiteto kuna changamoto kubwa ya maji kwa binadamu hata kwa mifugo na ndiyo maana tunapata vifo vingi vya mifugo. Watu wa Kiteto wameomba kuchimbiwa Bwawa kubwa la Dongo. Bwawa hili lipo kwenye mpango wako na ninaona kwamba miongoni mwa mabwawa ambayo umeyatambua kwamba yanaweza yakachimbwa ni pamoja na Bwawa la Dongo. Mimi nikuombe sana, Bwawa hili la Dongo ni suluhisho kwa watu wa Kiteto wameomba zaidi ya miaka minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bwawa hili faida yake kwanza ni kunusuru mafuriko yanayotokea kule Dumila. Can you imagine mvua inanyesha Manyara lakini mafuriko yanaenda mpaka Morogoro, ikiharibu mazao ya watu wa Dumila, miundombinu pamoja na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bwawa hili litakapokamilika lina uwezo wa kusaidia maji katika Wilaya ya Kongwa pamoja na Wilaya ya Gairo; na inakuwa na kazi kubwa, tutapata maji ya binadamu na maji ya mifugo. Mimi unasikia kila siku nikilia na mifugo ya Kiteto inavyokufa wakati wa ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile itatumika katika kilimo cha umwagiliaji tukawa na uhakika wa chakula; na tukijua kwamba Kiteto ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula lakini ndiyo yenye idadi kubwa pia ya mifugo. Vilevile itasaidia katika ufugaji wa samani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba hili uliweke katika mpango mkakati kama unavyofanya mikakati ya Farkwa na Kidunda. Hili Bwawa la Dongo ninakuomba sana; litakuwa suluhisho kubwa kwa watu wa Kiteto wote changamoto ya maji itakuwa imeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ninahamasisha uvunaji wa maji. Nimeona Wizara wamejitahidi wametengeneza mwongozo wa uvunaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taasisi zetu maji ni ya shida, na lakini ukiona maji ya mvua ni rasilimali muhimu. Kama tungekuwa na tabia ya kuvuna maji ya mvua tungekuwa na uwezo wa kupata maji ya kutosha na kuongeza kiwango cha maji kinachopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule hizi tunakutana na wanafunzi, unaona wanavyobeba maji wakipeleka shuleni, hatujui wamepata wapi vyanzo hivyo vya maji. Lakini uvunaji wa maji ni project rahisi wana, miundombinu ya kutosha ya paa, kinachotakiwa pale pengine ni kuweka ma- tank ya kuvuna maji na ikawasidia wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye taasisi za afya, ukienda katika zahanati zilizopo pembezoni bado changamoto ya maji ni kubwa na maji ni muhimu sana kwenye taasisi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana, kwa mwongozo huo utaratibu wa uvunaji wa maji katika taasisi uwe kipaumbele na uendelee; lakini utaratibu wa uvunaji wa maji pia kwa wananchi wa kawaida uendelee kuhamasishwa kupitia kwenye halmashauri zao. Maji ya mvua yakivunwa inaweza kuwa suluhisho kwa maji ya mifugo pamoja na matumizi ya binadamu. Sisi tunaona kabisa pengine miradi ya TARURA na TANROADS ikipita wakichimba udongo wao wakaacha yale mashimo kipindi cha kiangazi kinasaidia mifugo, ndiyo maji ambayo yanapatikana.

Sasa kumbe na sisi ukihamasisha wafugaji hata na wakulima wanauwezo mkubwa kabisa wa kuchimba vilambo vidogo vidogo wakaweza kuifadhi maji na kwa hiyo, ikawasaidia kipindi cha kiangazi. Naomba sana, mwongozo huo ukipita kwenye taasisi, lakini vilevile mwongozo huo ufike halmashauri ili wananachi kwa pamoja waweze kuhamasishwa kuvuna maji ya mvua yaweze kutumika kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga hoja mkono kwa mchango wangu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora. Ukiangalia majukumu ya Msingi ya Wizara hii ni kutengeneza Miundo, Sera na Nyaraka ambazo ni rafiki zinazotoa hamasa kwa watumishi wetu. Hata hivyo, kuna Miundo ya Utumishi ya muda mrefu, Muundo wa toka mwaka 2002 na miundo mingine. Hii miundo imebaki kuwanyanyasa watumishi au kuwa threat kwa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu watumishi wa umma kila mmoja anaajiriwa kwa muundo wake. Kwa mfano, watumishi wanaoajiriwa kwenye wa Muundo Mwandamizi, nitoe mfano kama Maafisa Kilimo, anaajiriwa kama Agriculture Field Officer au Afisa Kilimo Mwandamizi ana mahali pake akifikia bar, kwa mfano TGS G hawezi kuendelea ndio mwisho wa muundo wake. Mtumishi huyo akienda kujiendeleza akasoma, pengine ametoka diploma ameenda degree, badala ya kupata promotion sasa kama alikuwa TGS G atoke pale aende H muundo unamrudisha mpaka pale kwenye TGS D. Sasa TGS D mpaka kwenda TGS E anahitaji miaka mitatu, kama kweli muundo utampandisha smoothly. Akitoka D kwenda E miaka mitatu, akitoka D kwenda hiyo G yake miaka mitatu mingine. Sasa mpaka kwenda kumvusha mpaka kwenye H ni miaka tisa mpaka 12. Hivi Muundo huu ni rafiki kwa wafanyakazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa unam-frustrate mfanyakazi ambaye tayari alishajiendeleza mwenyewe na anajiendeleza kwa ajili ya kutoa huduma bora. Iko hivyo hivyo hata kwa watumishi wa Afya. Ma-nurse wetu wanaosoma RNDA au train nurse darasa la saba amehamasishwa ameenda kusoma form four amemaliza, ameenda kuchukua diploma, wanapopata diploma akirudi kwenye utumishi, muundo ule una-frustrate wanashindwa kwenda mbele na wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kushangaza, sijui kwa nini tunatenga watumishi? Muundo huu ukienda kwa Walimu, Mwalimu mwenye diploma akienda kusoma degree, yeye anahama moja kwa moja na ule muundo wa watu wenye degree, hakuna kinachomrudisha nyuma kama maeneo mengine. Sasa ifike muda basi niiombe Wizara hebu wa- review hii miundo. Miundo ambayo sio rafiki kwa watumishi, miundo inayokandamiza watumishi na kuwa-frustrate. Kama sasa hivi sio hitaji, umefika muda sasa ku-review na kuachana nayo na kuangalia namna nyingine ya ku-motivate mtu ambaye ameamua kujiendeleza, ukitegemea sasa hivi dunia inaenda na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, lakini inakuwa mbaya zaidi kama mtumishi wa Idara tofauti ameenda kusomea kitu tofauti, hapo ndipo unammaliza kabisa. Kwa mfano, Mwalimu, yeye toka mwanzo wito wake ulikuwa unamtuma labda kusomea kitu kingine Afisa Utumishi au Mwanasheria, akajiendeleza yeye mwenyewe, maana huko nyuma atakuwa alisaidiwa na wazazi, pengine fursa ilikuwa ni kwenda Chuo cha Elimu na fursa ya kupata utumishi ilikuwa ni hiyo, lakini atakapokuwa mkubwa na mshahara wake amejiendeleza na pengine halmashauri imempa nafasi ya kuwa labda Mwanasheria, anarudishwa kwenye muundo ule wa kuanza wa degree, lakini hata ile personal salary yake inafutwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshawahi kuona mtumishi anapunguziwa mshahara, anaenda kuanza kwenye mshahara wa chini. Hii miundo mingine naomba sasa ufike muda tu-review, tuone ni namna gani ambapo watumishi sasa wawe na furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili muundo wa hivi karibuni wa Halmashauri sijui restructuring maana nilishawahi kuuliza huko nyuma kama swali. Pengine nia ni njema halmashauri kwa ajili ya kubana matumizi imebadilisha muundo, ilikuwa na idara 13 na vitengo, sasa hivi imebana zile idara zimebaki idara tisa. Kwa maana hiyo kuna Idara zimeunganishwa kama za Kilimo na Vitengo vingine kama vya Uchaguzi vimefutwa, Idara kama ya Fedha imekuwa kitengo, can you imagine idara ya fedha ndio mkono wa Mkurugenzi pale. Sasa pengine sio shida, sijui kama kuna utafiti wa kutosha uliofanywa kuunganisha Idara za Kilimo na Mifugo pamoja na zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa stress zinatoka kwamba mtumishi ambaye alishawahi kuwa Mkuu wa Idara sasa unampoeleka chini ya Mkuu wa Idara nyingine, it is enough torture to him (psychological torture) yaani hawezi kuwa happy kufanya kazi chini ya idara nyingine. Vile vile na ufanisi utakuwa chini, kwa sababu taaluma ya kilimo ni tofauti na taaluma ya mifugo. Haiwezekani mtu wa mifugo ukimpa asimamie kilimo kwa vyovyote vile atakuwa bias. Niombe wafanye review. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu tatizo ni kwamba, kama tulikuwa tunabana matumizi, hawa Wakuu wa Idara na Vitengo ambao vitengo vyao vimefutwa kwa mfano Afisa Uchaguzi, huwezi kumnyang’anya mshahara wake na stahiki zake za Mkuu wa Idara, ataendelea kubaki nayo. Kwa hiyo, ataendelea kupata mshahara wa Mkuu wa Idara na zile stahili ambapo hakuzifanyia kazi na huwezi kumwacha pale kwa sababu atakuwa hayuko happy. Sasa sijui wamejipangaje kumjengea job satisfaction huyu mtu aweze kuwa happy sasa kuendelea? Kama alikuwa ni Mwalimu, utamrudisha kwenye chaki, alishakuwa Mkuu wa Idara, fikiria ukimrudisha kwenye chaki, ni kweli ataenda kufanya utumishi vizuri? Napendekeza, pengine ikibidi kwa hawa watumishi ambao idara zao zimefutwa labda wapelekwe kwa RS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, nataka kusema kuhusu watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wanavyopatikana. Watumishi hawa RS (Sekretarieti ya Mkoa) kazi yao kubwa ni kusimamia watumishi pamoja na Wakuu wa Idara katika halmashauri. Hata hivyo, hebu ona unamwajiri mtu kijana aliyetoka chuo unamweka pale kwenye Sekretarieti ya Mkoa. Anatoka huko anaenda kusimamia miradi ya halmashauri. Kama ni Engineer wa Umwagiliaji anakuja yule technician wa umwagiliaji aliyeko kule kwenye halmashauri ana knowledge kumshinda yeye. Ndio maana wakija wakubwa, akija Waziri Mkuu au Waziri mwingine kukagua miradi anakuja kukuta miradi mingine iko chini ya kiwango na lazima ina mapungufu. Sasa jiulize kama RS (Sekretarieti ya Mkoa) ilikuwepo pale walitoa ushauri gani huko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza wa-review utaratibu wa kupata Sekretarieti ya Mkoa kwa sababu wao ni wasimamizi wa miradi yote ya halmashauri pamoja na Wakuu wa Idara, wafanyiwe kama wanavyofanyiwa Wakuu wa Idara, wawe na experience ya kufanya kazi kwa miaka sita kama Wakuu wa Idara na wafanyiwe vetting, halafu wapate promotion ya kwenda Mkoani. Hii itawa-motivate pia watumishi wetu wengine kwenye halmashauri wajue kwamba watumishi wakifanya vizuri kuna promotion ya kwenda Mkoani. Hiyo itasaidia sana, naomba hilo waliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza na kusema ukweli nampongeza na Mama, kipindi hiki ndipo tumepata nafasi za ajira kuliko kipindi kingine chochote. Nashukuru kwamba ajira nyingi zimekwenda kwa Walimu pamoja na watumishi wa afya, lakini kuna Wizara tunazisahau…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina Rahhi kwa mchango wako, unaweza kuunga mkono hoja kama ulidhamiria. (Kicheko)

MHE: YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii. Kwa sababu ya muda mfupi naomba kuungana na wenzangu wote waliochnagia kuhusu bajeti ya Wizara hii, kwa sababu haswa ndio kilichofanya nisimame kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunathamini maana saa nyingine tunasema hii Wizara ipo kwa bahati mbaya au kwa kitu gani? Michezo, Sanaa na utamaduni ni jambo mtambuka inayowagusa kuanzia watoto wa miaka miwili, mitatu, ukiona wale watoto wadogo mpaka wana-act namna gani, Mayele anafunga goli na wengine wana-act kama Joti anavyotembea ina maana wame wa-inspire watoto toka wakiwa wadogo, lakini mpaka wazazi mpaka wazee huku tunashabikia michezo, tunafatilia tamthiliya ili tupate amani, lakini ukiangalia bajeti inayotengwa kwenye Wizara hii kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemei bajeti kuu ya bilioni 35, naangaliaga bajeti ya maendeleo kwa sababu Serikali kama imeajiri watendaji sehemu ya mishahara ikaenda kama mishahara zingine kama oc zinaenda akama oc. Lakini bajeti hii ya maendeleo ambapo kwa mwaka uliopita ilitengewa bilioni 15 lakini mpaka mwezi Februari wizara hii imepata bilioni 5 peke yake na sijui kama sasa hivi wameongezewa sawa na 31%. Tunaongea habari ya kuboresha viwanja, tunaongea habari ya kujenga vyuo, tunaongea habari ya kufufa chuo cha sanaa cha Butimba sijui wizara inaweza kufanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea habari ya kuweza kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Afrika kwa bajeti hii ndogo kwa sababu Waziri wa Fedha yupo na Serikali hii iko hapa, nafikiri hilo watakuwa wameshalichukua. Lakini vinginevyo nampongeza sana Waziri, nampongeza pia na Naibu wake pamoja na watendaji wa Wizara kwa kweli tuseme kama ni upele umepata mkunaji. Tumeona kwa namna gani michezo Tanzania inapanda, hawa ni wachapakazi nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaona ni kwa kiwango gani amepaisha michezo Tanzania. Mama Samia Suluhu Hassan Mungu ampe uwezo, Mungu amlinde kwa sababu kwa kweli watanzania wameona kwa namna gani ametoa motisha kubwa. Kila mtu anafahamu ameanza ku-motivate wachezaji mara milioni tano, ameongeza dau milioni 10 ameongeza dau milioni 20, ametoa usafiri, anakaa na wachezaji wanakaa wanakula pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa sana la kuiga kutoka kwa viongozi wetu. Nampongeza sana lakini siyo yeye tu nawapongeza na Mawaziri. Nampongeza Waziri Mkuu kule kwake utasikia Namungo FC, nawapongeza Mawaziri huku ukienda kwenye majimbo yao michezo mingi, vipaji vingi vya wachezaji vinabebwa na Wahehsimiwa wengi Wabunge pamoja na Mawaziri. Ukienda huku utasikia Gekul Cup utasikia Issaay Cup, utasikia sijui Massay Cup. Wanatoa jezi, wanatoa mipira, chakula na nafikiri Wabunge wengi kwenye maeneo yetu ndio tunachokifanya na kuwasaidia wasanii kurekodi miziki na kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawapongeza sana lakini kwa kweli bajeti iongezwe tuone ni namna gani wanaweza wakafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kuwa–support tumeona michezo Tanzania nawapongeza hata wanayanga wameweza kuibeba sifa ya nchi kwa kuweza kuingia fainali hongera sana, tunaendelea kupongeza timu nyingi wamekuja huku Serengeti Girls tumewapongeza wamepata sifa ya kuingia kwenye World Cup, Tembo Worriors, wamekuja vijana wa riadha Gabriel Geay, kina Isumbi yaani kwa kweli nawapongeza, hii yote ni kwa sababu tunawa–support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba vipaji hivi vinaanza toka utotoni. Hawa watoto wadogo kama timu kubwa inapata makocha hivi kwa nini hawa watoto wadogo tusianze kuwajenga kuanzia leo. Sisi zamani tulikuwa na maeneo ya wazi ambayo tunacheza michezo kama rede sijui hata inapotelea wapi? Lakini ni michezo ya kuwajenga watoto hasa kwa akili. Sasa maeneo yote yale ya wazi yamejengewa hakuna maeneo ambayo watoto wanacheza wanafungiwa ndani. Michezo ingesaidia Watoto kuwajengea akili pamoja na kuweka mahusiano na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Waziri katika kuhitimisha pengine uwaelekeze sasa kama ni Wakurugenzi au kwenye maeneo yote huko ya kata ya vijiji, waendelee kutenga maeneo wazi watoto wanacheza barabarani, wengine wanafungiwa ndani. Ili kutoka pale waendelee kujengewa uwezo lakini wapo taluma ya michezo, sanaa na utamaduni waanze kufundisha, waingie kwenye mitaala wafundishwe kuanzaia shule za msingi, sekondari, mpaka vyuo vikuu. Tuweze kupata vipaji kwa sababu hii ni ajira tosha. Ukichukua vijana watano wa Tanzania ukaambiwa chagua wangapi Kwenda shamba wengine kwenye michezo, kwa kweli watatu wataenda kwenye michezo. Kwa hiyo, michezo ni ajira kwa vijana wengine wanapotea kwa kukosa support na kwa hiyo hii ingia kwenye mitaala vijana wafundishwe, wawe-couch kuanzia huku chini siyo timu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kusemea ni bahati tuliyopata Tanzania ya kuwa center ya kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika. Hapa naomba tu kwamba tunamuenzi Baba wa Taifa yeye ndio aliyesema Tanzania haiwezi kuwa huru, mpaka Afrika yote iwe huru na kwa heshima hii, sisi tumekuwa center ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tujenge hili ambalo limeanza kujengwa kutoka 2003 kwa msaada wa UNESCO na Tanzania kwa kweli ni center nzuri ya utalii wa kiutamaduni na tunapata wageni wengi wa kuja kujifunza kwetu, hasa hawa ambao sisi tumewasaidia katika Ukombozi wa Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watakwenda kupata kumbukumbu zao kuna maeneo mengi ya kuhifadhi ikiwepo Dar es Salaam, Mazimbwi, Kongwa pamoja na sehemu zingine. Kwa hiyo, kote huku kuhifadhiwe ijengwe kumbukumbu nzuri, wahifadhi makaburi, watafute zile documents za zamani kuwe na maktaba kubwa na ukumbi ili wenzetu wakute hizi historia. Tanzania ni nchi ya pekee iliyokuwa na uzalendo kusaidia nchi za Afrika Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa uletwe Muswada wa kisheria wa kuweza kuhifadhi hizi kumbukumbu za kiutamaduni ili utamaduni huu usiweze kupotea.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Nitakuwa mchache wa shukrani, wa fadhila kama sitatambua na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kuiheshimisha nchi ya Tanzania na kuwaheshimiwa wakulima wa Tanzania kwa kuweka bajeti hii ya kihistoria mwaka huu. Nampongeza pia Waziri pamoja na watendaji wake kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa tatizo kubwa katika kilimo ni uzalishaji mdogo kwa eneo na uzalishaji huu mdogo unasababishwa na upungufu au ukosefu wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu, mbolea pamoja na viuatilifu. Tunafahamu kabisa ikifika wakati wa msimu upatikanaji wa mbegu unakuwa wa shida kabisa na zikipatikana bei yake inakuwa juu na wakati huo ndiyo wakati ambapo wakulima wanakimbizana na unyevunyevu wa mvua. Naomba kuishauri Serikali kwa bajeti kubwa iliyoipata ya uzalishaji wa mbegu, mbegu nyingi tuzizalishe huku Tanzania, tupunguze mbegu tunazoziagiza kutoka nje ili wakulima wetu waweze kumudu bei ya mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile watu wameongea kuhusu bei ya mbolea, tunafahamu changamoto tulizozipata kipindi kilichopita, lakini mwarobaini wa tatizo hili ni kuwa na viwanda vyetu wenyewe huku ndani, hatuwezi ku-control bei ya mbolea tunazoagiza kutoka nje na ruzuku iwekwe katika viwanda vinavyozalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kuchangia kidogo kuhusu kilimo cha umwagiliaji. Tuna fursa kubwa sana katika kilimo cha umwagiliaji. Tuna maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji, potential area zaidi ya hekta milioni 29 na pointi, lakini japokuwa sasa hivi tumeweza kuendeleza hekta kwenye 700,227 na lengo la kwenda kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ni hekta 1,200,000. Bado eneo hili ni dogo na Serikali haiwezi kufanya kila kitu, naomba kuishauri kwamba, Wizara ikaweke fursa katika eneo hili ili kuwahamasisha wawekezaji waweze kuweka mchango wao katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo hiki ndiyo kilimo ambacho nategemea kitajenga mazingira mazuri kwa vijana, kiweze kuwafanya vijana wawekeze katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu anaweza kupata mapato mapema zaidi hata kuanzia wiki tatu, mwezi au miezi miwili. Hapo vijana watapata kipato kutokana na kilimo cha umwagiliaji. Nimeona mpango wa Wizara unaoitwa National Strategy for Involvement of Youth in Agriculture, mahali hapa nategemea Wizara itawatafutia vijana mashamba kwa kufidia maeneo na kuweza kuwakodisha vijana ili waweze kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea pia katika bajeti hii kubwa iliyowekwa kwenye kitengo hiki cha umwagiliaji wataenda kuchimba mabwawa na kuvuna maji ya mvua ambayo mara nyingi yanasababisha mafuriko, vile vile kwenda kuboresha miundombinu. Kuna miradi mingi ya mabwawa ambayo yameshachimbwa ambayo bado ufanisi wake haujawa mkubwa kwa sababu ya kutokuweka miundombinu ya kupeleka maji katika mashamba na mifereji mingine tunajua inapoteza maji. Kwa hiyo mifereji hiyo pamoja na miundombinu ingesakafiwa na kutengeneza miundombinu mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kule Manyara, Mradi wa Bwawa la Dongobesh umekamilika lakini hauna miundombinu ya kupeleka maji mashambani. Naomba uwe mmojawapo pamoja na kuchimba mabwawa. Naomba bwawa ambalo limewekwa katika mpango wa Mheshimiwa Waziri, Bwawa la Dawi, lipate kuchimbwa. Vile vile kuna wakulima wanapenda kilimo cha umwagiliaji lakini mashamba yao yako juu ya mifereji wanatumia pump na generator kumwagilia mashamba yao. Niiombe Serikali kabisa kwa nia njema waweze kutoa kodi kwenye vifaa hivi ili wakulima wengi waweze kununua pump hizi na waweze kumwagilia maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kidogo, kwa sababu tumepata bajeti hii kubwa ya kihistoria, katika ufanisi naomba kushauri tu kwamba, Wizara iajiri watendaji wa kutosha, kwa mfano, Wahandisi wa Umwagiliaji kule kwenye halmashauri hawapo na ndiyo wanaoenda kusimamia miradi hii. Vile vile kuna vitengo kwa mfano Kitengo cha Agro-mechanization ambacho kilikuwepo, wale waliokuwepo baada ya kustaafu Serikali imeacha kuwaleta watu hawa, ndiyo maana wakulima wanabaki kwenye kilimo cha mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wamenunua trekta zilizoharibika, hakuna mtu wa kuwashauri. Kuna power tiller tulihamasisha, wakulima wana ma-power tiller yameharibika hakuna mtu wa kuwasaidia. Kwa hiyo katika ajira ijali tusiangalie tu labda pengine ma-agronomist, kuna vitengo hivi vya agro mechanisation, kuna wakulima bado wanalima kwenye miteremko mikali, lakini kulikuwa na washauri, hawa watu wa land use, tunaomba tu Wizara ikaangalie hivyo vitengo muhimu ili kwenda kuwasaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha, tayari kengele imepiga.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana na mimi kupata fursa hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Mifugo. Nami vilevile nitoe pongezi kubwa kwa Rais wetu Mama Samia Suluhu kuweza kuweka bajeti kubwa katika Wizara hizi za kisekta za uzalishaji kwa kuwatia moyo Watanzania kujikwamua na umaskini ambao umekuwa kikwazo kikubwa kwa wafugaji na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa kubwa sana katika sekta hii ya mifugo kuweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kuweza kutusogeza katika uchumi wa kati, kwa sababu kwanza ukiona Tanzania tumezungukwa na Maziwa Makuu ambapo tungeweza kufanya uvuvi katika Maziwa Makuu na tungeweza kupata tija samaki tukaweza pengine kuwauza nje na ikachangia katika Pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha ni kwamba sekta hii bado haijafanya vizuri, kwamba mchango wake kwa Pato la Taifa bado ni chini ya asilimia 10, bado inachangia kati ya asilimia Saba mpaka Nane, sasa hebu ona jinsi tulivyo nyuma lakini tukiwa proud tu kwamba Tanzania sisi ni wa pili kuwa na mifugo mingi, sasa pia hatujaweza kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni wa pili katika kuwa na mifugo mingi Afrika lakini Tanzania hii pia ni ya pili katika kuwa na udumavu wa mifugo, sasa hii ina-reflect nini? Ina-reflect tu kwamba ulaji au upatikanaji wa mazao ya mifugo bado upo chini na ubora wake upo chini, ndiyo maana hata bado tunaingiza mazao haya ya mifugo kama nyama tunaingiza kutoka nje, maziwa, Samaki sasa tuone kwamba tunapaswa kufanya nini, bado ukienda hoteli za kitalii, ukienda supermarket, utakuta kwamba mazao ya mifugo bado tunaingiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri ameweza kuona ni kwanini tuna kipato kidogo kutokana na mazao ya mifugo, amesema mojawapo ni kuwa na kosafu za mifugo yetu, tuna asilimia 90 ya mifugo ni mifugo yetu ya asili ambayo kosafu ndiyo sababu pengine ya kuwa na tija ndogo, vilevile magonjwa ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bado hatujawa na sheria, kwa mfano tunamajosho huko sheria ya kuogesha mifugo bado hatujaweza kuisimamia na ndiyo maana majosho sehemu nyingine pia yapo hayatumiki ni bahati tu kwamba mifugo ya kienyeji ina ustahimilivu mkubwa, lakini inang’atwa na kupe, inatembea na kupe, inakuwa na minyoo, ndiyo maana mifugo yetu haina ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni la malisho pamoja na maji. Naipongeza Wizara kwa intervention inazofanya katika matatizo haya. Kwa mfano, Wizara imetenga karibu bilioni 3.9 katika kubadilisha kosafu za mifugo kwa kufanya uhimilishaji. Sasa uhimilishaji huu namuomba tu Waziri kama kweli ana nia njema, kazi hii ambayo itafanywa na Maafisa Ugani huko kwenye Halmashauri kwa wafugaji, kwa kuwa amenunua pikipiki za Maafisa Ugani wa Mifugo basi angewapatia kabisa mitungi ya kubeba liquid nitrogen ili huko kwenye makundi haya ya mifugo ya asili waweze kufanya uhimilishaji ambao kwa vyovyote vile ni ngumu kufanya uhamilishaji kwa sababu mifugo hii ya asili inachungwa pamoja, mitamba pamoja na madume. Pengine basi angeweza kusambaza hata madume labda madume bora ya mbegu kuweza kufanya uhimilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nakisemea kituo cha NAIC kinachozalisha hizi artificial insemination tunachokituo kimoja kiko Arusha na hali yake si nzuri, uwezo wa kuzalisha mbegu za kutosha za kusambaza Tanzania nzima bado ni mdogo, pengine Waziri ningeshauri tu kwamba kama kuna uwezekano wa kufanya extension, kwa mfano mifugo iliiyopo Dodoma kutegemea NAIC iliyopo Arusha peke yake bado haiwezi kutosheleza, mifugo iliyopo Shinyanga, Mwanza utegemee NAIC peke yake na kwa sababu umewekeza kidogo huko NAIC uhimilishaji gharama yake ni kubwa. Kwa mfano, kwa sasa hivi ukimpandisha ng’ombe mmoja unampandisha kwa elfu ishirini pengine hata asiwe na mimba urudie. Kwa hiyo, na gharama hizi zipunguzwe ili wafugaji wengi waweze kutumia hizi artificial insemination. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna nyingine ambayo umeona ni kubadilisha kosafu ni kuzalisha mitamba kwenye mashamba ya Sao Hill pamoja na NARCO na kwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii mitamba sasa isambazwe huko vijijini kwa akina mama, tunaweza tukawashauri akina mama zetu ile asilimia kumi ya mkopo anaopata mapato ya ndani kutoka Halmashauri wanaweza wakawekeza huku wakajenga mabanda mazuri ili sasa Wizara mitamba hiyo isambaze kwa akina mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna asasi isiyo ya Kiserikali kama Heifer International imefanikiwa sana katika kusambaza mitamba kwa namna kwamba ukipeleka mitamba hiyo hata mitano katika kijijini kimoja itasambaa na kijiji kizima itajaa kwa maana ya kukopesha mtambo, utampa mama akizaa anampandisha yule ndama na akishampandisha anampa jirani yake. Kwa hiyo, mifugo hii itazunguka na kwa ajili hiyo akina mama watapunguza umaskini. Kwa hiyo, hilo moja naomba tu isambazwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, intervention nyingine uliyofanya ni katika kuzalisha malisho ya mifugo. Ni kweli wazo hili ni zuri lakini uzalishaji huu kwa maeneo ambayo hakuna miundombinu ya umwagiliaji, malisho haya yatazalishwa kama mazao mengine wakati wa masika kwa maana hiyo wakati wa masika malisho yatakuwa mengi, tukirudi kwenye kiangazi changamoto ya malisho itakuwa palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sambamba na kusambaza hii ambapo umetenga karibu Bilioni 1.2 umesema utaweka na mashamba darasa kwenye Serikali za Mitaa, mimi nishauri tu kwamba usambazaji wa mbegu za malisho ziendane na kuwawezesha wafugaji kuweza kuhifadhi sasa malisho ya mifugo ili ije iwasaidie kipindi cha kiangazi, wakatengeneza ma-bell ya hay wasile kile kipindi cha kiangazi iwasaidie, vinginevyo tutafika kiangazi bado kutakuwa na changamoto ya malisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi cha kiangazi ng’ombe mpaka wanakorogewa uji na wengi wanakufa, kwa hiyo hii ni hatari sana lazima tupeleke teknolojia kuhifadhi malisho kwa wafugaji wetu tukitaka tuwasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mchango wangu mwingine ni kwenye vituo vya kukusanya maziwa. Kiukweli maziwa kipindi cha masika maziwa ni mengi sana na kwa sababu maziwa ni mengi kina mama au watu waliopo vijijini wanashindwa kuyapeleka kwenye masoko hii ni kwasababu pengine mifugo yetu ya asili hii anakamua labda nusu au mpaka lita mbili sasa hizo chache hawezi kwenda kilometa chache kufuata soko la maziwa. Tungeweza kuweka hivi vituo bado hizi zingekuwa payroll za akina mama kama ameweza kupeleka hata lita mbilimbili kwa wiki ana hakika tu kabisa kwamba anazo pesa za kuweza hata kununua supplement, hata dawa za mifugo kama Serikali inashindwa pengine kupeleka vituo vingi vya kukusanya maziwa hata inaweza ikashawishi ushirika ulioko kijijini hata SACCOS lakini hii ni muhimu sana, asilimia karibu 66 au theluthi ya maziwa tunayotumia humu ndani yanatoka kwa mifugo. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kipindi kilichopita tulikuwa tunapanga pia vipaumbele na kupitisha bajeti yetu, lakini Mheshimiwa Rais ametoa fedha za utekelezaji wa mpango ambao sasa hivi unaendelea kutekelezwa na ametoa fedha nyingi sana. Nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa hivi tukiweka mpango wetu vizuri na vipaumbele vizuri kwa vyovyote vile utapata fedha na utatekelezeka. Pia, nampongeza kwa maono aliyonayo tulikuwa tumetamani sana irejeshwe Wizara ya Mipango na Uwekezaji ambayo sasa amewekeza na tunaomba isimamie rasilimali za Watanzania ziweze kutumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kupanga ni kuchagua. Tuna mahitaji mengi sana ya wananchi na hasa ukienda vijijini mahitaji ni mengi, kuna barabara ni mbovu zinatakiwa zitengenezwe, kuna vivuko, kuna zahanati na kuna elimu lakini kwa sababu rasilimali hizi ni chache, hizi resource ni scarce, ni lazima tuwe makini kuona kwamba ni vipaumbele vipi vinatakiwa viingie katika mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza Waziri kwa sababu amekuja na mapendekezo ya mwongozo, kwamba kati ya vipaumbele, kwanza ni kukamilisha miradi mikubwa iliyokuwa inaendela ikiwemo mradi wa reli, wa viwanja vya ndege na hasa huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ili tuweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni hitaji kubwa sana katika kuendeleza uchumi wa Tanzania, lakini sasa nchi mara nyingi tunaingia kwenye mgao wa umeme. Hili jambo ni baya sana, umeme unahitajika, kuna vijana kule wana viwanda vyao vidogo vidogo vya kuchomelea na kadhalika, sasa tunavyokata umeme, tunavyoweka mgao kwa kweli ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe tungeweza kuweka kipaumbele kikubwa kwa kuachana na hii changamoto ya upungufu wa umeme, kwa sababu kwanza rasilimali za kuzalisha umeme tunazo, tumebarikiwa na Mungu tunaweza kuzalisha umeme hata kutoka kwenye vyanzo vya jua, akazalisha mtu mmoja mmoja tukaingiza kwenye gridi ya Taifa. Tunaweza kupata umeme pia kutoka kwenye vyanzo vya upepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaongea kila siku habari ya gesi asilia ambayo pia inaweza ikazalisha umeme. Tunaongea habari ya gesi kule Mchuchuma na Liganga ambapo watafiti wanasema kuna takriban shilingi bilioni mbili potential ambazo pia tungeweza kufua umeme kutoka huko wa kati ya megawatt 600 mpaka 900 tukaweza kuingiza kwenye gridi ya Taifa, tena kwa gharama ndogo ya shilingi 103 mpaka 108 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kipaombele changu kingine ni kuwekeza katika viwanda. Tumeona nchi zote zilizofanya vizuri katika uchumi wamewekeza kwenye viwanda na sisi tunasema dhima ya uchumi wetu ni uchumi shindani. Tunawezaje kwenda kwenye uchumi shindani kama hatufikirii habari ya viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingi kwenye viwanda, tuna viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vinachukua karibu asilimia 98. Kwa mfano, tuna viwanda vidogo vidogo sana 62,400 ambayo ni asilimia 77 ya viwanda vyetu. Tuna viwanda vidogo 17,274 ambayo ni sawa na asilimia 21, tuna viwanda vya kati 684 ambayo ni asillimia 0.8 na tuna viwanda vikubwa 618 ambayo inaenda asilimia 0.76. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vidogo bado vina mahala pake. Tunajua umuhimu wa viwanda, vinaweza vika-absorb nguvu kazi kubwa ambayo kila siku inakimbizana na ajira. Vilevile, viwanda hivi vinasaidia, kwa mfano agro-processing viwanda, kufanya value chain ya mazao yetu na tukapata faida. Changamoto kubwa ya viwanda hivi vidogo vidogo ni mitaji. Serikali iwasogelee hao wenye viwanda vidogo vidogo, pengine ni vikundi vya kina mama, wengine wanafanya usindikaji wapate mitaji, skills na knowledge pamoja na masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nasema habari ya viwanda hivi vya kati na viwanda vikubwa kuviboresha, kwa mfano viwanda ambavyo mahitaji yake ni makubwa Tanzania. Kwa mfano, kiwanda cha mbolea tuna viwanda viwili tu vya mbolea, kiwanda cha Minjingu pamoja na Intracom ambapo inazalisha mbolea kidogo. Minjingu kinazalisha tani 100,000 na hiki kingine kinazalisha tani 250 mpaka tani 300 na mahitaji ya mbolea ni zaidi ya tani 1,000,000. Sasa tunaagiza na kuweka mbolea ruzuku, natamani nguvu zote hizi tungewekeza katika kujenga viwanda vya mbolea ili tuweze kujitosheleza kwa mbolea.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna viwanda vya saruji pamoja na chuma. Nasema Watanzania wamekubali kupata maendeleo na kujenga makazi bora, lakini saruji na chuma bado bei yake imekuwa ni kubwa sana. Naiomba Serikali iweze kuwekeza katika viwanda hivyo ili Watanzania waweze kwenda kwenye makazi bora. Tunajua ni matokeo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi katika lower level ambapo imeongeza mzunguko wa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule ambapo Mama Lishe, vijana na maduka madogo madogo wameweza kuzungusha hizi hela na kwa ajili hiyo watu wameamua kujenga makazi bora, lakini ukienda saruji inauzwa ghali, chuma inauzwa ghali. Tuna uwezo mkubwa sana wa kuweza kuzalisha saruji yetu wenyewe pamoja na chuma kwa sababu malighafi zote ziko huku. Changamoto ni kusafirisha hizi malighafi kutoka kule kusini, kwa mfano gesi asilia inayotoka kwenye makaa ya mawe, huko chini tunaomba reli ijengwe. Wameongea sana Wabunge wa Songea na wote wa Kusini, kuna umuhimu sana wa kujenga reli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, kengele ya pili imepigwa, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
The Water Resources Management (Amendment) Act, 2022
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi ya kuchangia hoja hii ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza sana Wizara ya Maji kwa kuja na Muswada huu wa kufanya marekebisho katika Usimamizi wa Rasilimali za Maji. Ninasema hivyo kwa sababu maji ni rasilimali muhimu sana. Tunasema maji scarce resource, lakini maji ni muhimu sana katika maisha yetu, maji ni uhai kwa binadamu, maji ni uhai kwa Wanyama, maji ni ustawi wa mimea pamoja na mazao. Kwa hiyo, tunaweza tukasema hapa bila maji sasa kumbe hakuna uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu umekuja wakati mzuri sana. Tunaona kwamba rasilimali maji imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka. Kama tunakumbuka, kwamba kipindi nchi yetu inapata uhuru kulikuwa na wastani wa maji wa lita za ujazo takribani 10,000 kwa mwaka kwa kila Mtanzania. Lakini kwa sasa na kwa takwimu iliyopita wastani wa upatikanaji wa maji kwa Mtanzania ni mita za ujazo 2,250. Sasa nategemea kwamba hata tukipata takwimu ya sensa ya mwaka huu bado inaweza ikaonesha upatikanaji wa maji unazidi kupungua. Sababu ni nyingi tu, kwamba moja wapo ni hilo la ongezeko la binadamu lakini la rasilimalimaji ipo pale pale, wanyama rasilimalimaji ipo pale pale, shughuli za kilimo, lakini uharibifu wa vyanzo vya maji na hasa maeneo tengefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea usimamizi wa rasilimali za maji tunaongelea muundo wa kitaasisi pia na mamlaka na wajibu katika kusimamia rasilimali za maji pamoja na kudhibiti uharibifu. Sasa tumeona kwamba tuna mabonde tisa, na mabonde haya yalikuwa yakisimamiwa na maafisa mabonde. Sasa katika usimamizi mzuri tunafikiria tu kwamba tupate muundo mzuri wa taasisi wa kuweza kusimamia haya mabonde; na ndiyo maana tukasema mabonde haya sasa yasimamiwe na wakurugenzi kabisa wenye mamlaka. Sifa za kuteua hawa wakurugenzi zimeainishwa kwenye muundo huu. Kwamba, angalau basi wawe na degree za hydrological, ideological degrees na fani zinazosimamiwa na hapa. Muundo wa kazi pamoja na majukumu yanayotakiwa kufanya yameelekezwa pale ili kuwe na usimamizi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taasisi hizi zikishuka mpaka huku chini kwenye jumuiya ya watumiaji wa maji (water uses associations) zilizoko vijijini na kwingine, tulikuwa tunaona kwamba nyingi zinaundwa na wanaume, au nyingine wanasema at least kuwe na wanawake wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sasa ninapendekeza kwamba muundo huu uletwe sheria inayotaja kwamba uwakilishi wa wanawake katika taasisi hizi unakaaje. Napendekeza angalau isiwe chini ya asilimia 30, na hata ikiwezekana wawekwe wanawake wote kwenye kamati hizi za usimamizi wa maji. Hii ingependeza kwasababu ni watumiaji wazuri wa maji, lakini pia wapo makini katika kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia nakubaliana na faini mbalimbali zilizotajwa. Ninasema hivyo kwa sababu kuna makosa kwa kweli yameelekezwa hapo. Kwa mfano, kuvamia maeneo tengefu, ndiyo tunayotegemea kulinda vyanzo vya maji, lakini watu wanavamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona wakulima wetu wanaenda kulima mpaka kwenye vyanzo vya maji au wanapitisha mifugo huko. Sasa maana ya faini siyo kuwakomoa Watanzania. Tukiacha mambo haya yakaenda holela, tena hasa kwa ndugu zangu wafugaji, watavamia haya maeneo, ukimpiga faini ndogo, atalipa na kesho bado atapeleka mifugo. Anayelima anajua atalima mazao yake, ukimpiga faini ndogo, atalipa, ataendelea kulima. Kwa hiyo, nafikiri faini katika Muswada huu ni sahihi, lakini tuangalie faini ambazo zinaweza zisiwaumize sana Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faini hizo zimetajwa katika vifungu mbalimbali vya sheria hii inayorekebishwa kuanzia kifungu 44, 55, 64 na kuendelea. Ni faini inayoanzia kwenye Shilingi 300,000/= mpaka Shilingi milioni tano, maana kwa kila kosa kuna faini yake; au kifungo cha miezi mitatu mpaka miezi sita. Sasa kwa kweli imeelezwa katika makosa mbalimbali; ukichungia mifugo kuna adhabu yake, pia kuna wanaochepusha tu maji; kuna mto au bwawa anaamua kuchepusha, anamwagilia labda eneo lake anavyotaka au kuchimba visima bila kupata kibali cha mabonde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa faini hii pia imeangalia mambo mengi. Faini hii inatofautisha kati ya taasisi, hawa tunaosema legal person, anapaswa kuwa na faini kubwa kuliko watu wa kawaida ambao huku wanasema natural person; au mtu anayerudiarudia makosa, basi atakuwa na faini kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana kabisa kwamba faini hizi ziwepo kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu, kwa ajili ya hifadhi ya mabonde haya ya maji, kwa sababu maji tunayahitaji. Pamoja na faini hizi, jambo kubwa la muhimu ni kuwaelimisha wananchi, elimu ya kuhifadhi mabonde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwenye Sera ya Maji wamesema kila kwenye mradi wa maji lazima miti ipandwe. Hata kwenye Wizara ya Ardhi nimesikia ukipewa hati ya ardhi ya nyumbani kwako, sharti mojawapo ni kupanda miti. Kwa hiyo, nafikiri tutoe wito kwa Watanzania na elimu itolewe, tuhifadhi vyanzo vya maji lakini pia tuhifadhi mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)