Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Regina Ndege Qwaray (7 total)

MHE. REGINA N. QWARAY Aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya kuboresha elimu katika Vyuo vya Ufundi (VETA) Mkoani Manyara ili kuboresha utoaji wa elimu ya ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiongeza wigo wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza mipango mbalimbali ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini. Mkoa wa Manyara ni moja kati ya mikoa inayonufaika na ongezeko hilo la bajeti. Katika kipindi cha mwaka 2018 – 2020, Serikali imetumia kiasi cha shilingi 1,925,438,420.13; kati ya fedha hizo shilingi 600,000,000 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shilingi 505,159,420.00 zimetumika kununua nyumba za watumishi katika chuo cha VETA Manyara kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika Chuo cha VETA Gorowa, kiasi cha shilingi 337,081,677.13 kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa karakana, ofisi ya utawala na madarasa. Vilevile, katika Chuo cha VETA Simanjiro Serikali imetumia kiasi cha shilingi 223,981,323.00 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kujenga bweni la wasichana. Aidha, shilingi 259,279,000.00 zimetumika kugharamia mafunzo ya muda mfupi katika Vyuo vya VETA Manyara na Gorowa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi katika mkoa wa Manyara na mikoa mingine kwa ujumla kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Ndege cha Mwada Mkoani Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege yaani TAA na kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara wameainisha eneo la Mwada katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege katika mkoa huo. Aidha, Serikali imeendelea na taratibu za kutwaa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja hicho cha ndege. Baada ya hatua hii, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yaani Sekta ya Ujenzi kupitia TANROADS, itatangaza zabuni ya kumpata Mshauri Mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo hapo juu, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ina nia thabiti na imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa uwanja huo unajengwa ili kuweza kutoa huduma muhimu katika Mkoa huo wa Manyara na maeneo ya jirani. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka na kuongeza vifaa tiba na wataalam katika vituo vya afya ilivyojenga vikiwemo vifaa tiba maalum kama vile “incubator beds” na taa maalum kwa ajili ya kukabiliana na homa ya manjano kwa watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vituo vya afya unaenda sambamba na mpango wa ununuzi wa vifaa tiba. Kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2020/2021 Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 68.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyojengwa na kukarabatiwa ili kuwezesha utoaji wa huduma za dharura na upasuaji kwa akinamama wajawazito na wananchi kwa ujumla. Vifaa vilivyonunuliwa vinajumuisha vifaa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda (Infant Radiant Warmers).

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali mpya 67 za Halmashauri zilizojengwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mei, 2017 hadi Mei, 2020 Serikali imeajiri na kuwapanga watumishi 9,531 wa kada mbalimbali za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Aidha, mwezi Mei 2021 Ofisi ya Rais - TAMISEMI imetangaza nafasi 2,726 za kada mbalimbali za afya. Wataalam hao watapangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini na kipaumbele kitakuwa kwenye vituo vyenye uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba na kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante sana.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia kikamilifu Sera ya Afya ili akinamama wajawazito na watoto wasitozwe gharama katika vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo kwa sera na miongozo inayotaka huduma itolewe bure, kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya wananchi walio katika makundi hayo katika maeneo mbalimbali kudaiwa fedha katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Ili kuepukana na malalamiko hayo, Serikali inawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Bodi za Afya na watoa huduma za afya kutekeleza Sera na miongozo inayohusu matibabu bure kwa mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inawakumbusha Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi kuwa ni jukumu lao pia kusimamia miongozo inayotolewa na Serikali. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuchimba mabwawa ya kuhifadhia maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo katika kila Kijiji nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yenye mifugo mingi na yale yaliyoathirika na ukame mara kwa mara yanakuwa na miundombinu ya maji yakiwemo mabwawa kwa ajili ya maji ya mifugo. Katika kutekeleza mkakati huo, mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.146 kwa ajili ya uchimbaji na ujenzi wa mabwawa au malambo na visima virefu vya maji kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha za kuchimba, kujenga na kukarabati mabwawa ama malambo na visima virefu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, napenda kutoa wito kwa Halmashauri za Wilaya, wafugaji na wadau wengine kuchimba na kujenga malambo au mabwawa, visima virefu kwa ajili ya maji ya mifugo. Pia, nahimiza wafugaji kuwa na vyanzo vyao binafsi vya maji kwa ajili ya mifugo yao.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mabweni yaliyoanzishwa na wananchi kwa michango yao katika shule za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali iliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 9.21 kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni 461, kati ya hayo mabweni 28 ni kwa ajili ya shule za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mabweni ili kuunga jitihada zilizofanywa na wananchi za kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mabweni kila mwaka kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza kiwango cha mikopo ya vikundi vya watu watano inayotolewa na Halmashauri kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 9 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2019 imeelekeza kwamba fedha za mikopo zitakazotolewa zitatumika kwa miradi iliyoidhinishwa na Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi kwa kuzingatia ushauri na mapendekezo ya Timu ya Menejimenti na Kamati ya Huduma za Mikopo. Hivyo, ni jukumu la kikundi husika kuomba mkopo kulingana na mahitaji ya mradi husika.