Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Regina Ndege Qwaray (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. Nami niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyonijalia hadi siku ya leo nimeweza kuwepo hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee pia nikishukuru chama changu kwa kuniteua na kunipendekeza katika ngazi zote na hatimaye leo niko hapa. Pia niwashukuru kwa namna ya pekee sana akina mama wa Mkoa wa Manyara kwa imani kubwa waliyoonesha juu yangu na kuniona natosha kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niishukuru pia familia yangu; mume wangu na watoto wangu ambao wamekuwa bega kwa bega na mimi muda wote wa mchakato na hata sasa wamekuwa wavumilivu kipindi chote ambacho niko katika majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa iliyoifanya kwa miaka mitano ya kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kimaendeleo. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hotuba nzuri iliyosheheni matumaini kwa Watanzania ambayo inaonesha dira kwa nchi yetu. Kwa namna ya pekee, tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema, busara na hekima ili yale yote aliyoahidi na aliyoyasema katika hotuba yake yaweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite katika kipengele cha elimu. Kwanza niipongeze sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo imeona ni vyema kuwa na Watanzania wenye elimu na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania ambaye ana umri wa kwenda shule anaweza kwenda shule na kupata elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne; si kazi rahisi. Ndugu zangu, Tanzania imesonga mbele. Ukiangalia miaka ya nyuma waliokuwa wanapata elimu walikuwa wachache sana lakini leo kila Mtanzania ana uhakika wa kupata elimu na anasoma bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada zote za Serikali bado tuna changamoto ndogo ndogo ambazo Serikali yetu inapaswa ione kwa jicho pevu kwamba bado tuna miundombinu mibovu, madarasa ni machache msongamano ni mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna upungufu mkubwa wa madawati na wataalam kwa maana kwamba walimu ni wachache. Kuna shule ambazo wanafunzi ni wengi darasani, unaweza kuwa na wanafunzi 200 lakini walimu ni wachache sana. Kwa hiyo, uwiano kati ya mwalimu na mwanafunzi bado haujazingatiwa. Hii inabidi Serikali iangalie uwiano huo ili utendaji kazi kati ya ufundishaji na ujifunzaji uwe mrahisi na wanafunzi wetu waweze kufanya vizuri huko madarasani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri Wizara hii ya Elimu iangalie upya mtaala wa elimu unaotumika. Elimu yetu inayotolewa kwa sasa haimuandai mwanafunzi kwenda kusimama mwenyewe na kujitegemea. Kwa hiyo, napendekeza Wizara ione namna gani elimu inayotolewa kwa sasa inaweza kumuandaa mwanafunzi ili aweze kujitegemea. Kwa maana ya kuboresha vyuo vya ufundi, wanafunzi wapate ujuzi wa kutosha ili waweze kujianzishia maisha kwa maana ya kuwa na ujuzi wa kwenda kujitegemea na kuanzisha ujasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi nashauri Serikali iboreshe vyuo vya ufundi vilivyopo, lakini ihakikishe inaanzisha vyuo vya ufundi katika kila wilaya vikiwa na taaluma na ujuzi ambapo kila mwanafunzi anaweza kupata ujuzi tofauti tofauti. Kwa hiyo, wanafunzi wetu wanapomaliza kidato cha nne ni vyema akaamua kujichagulia kuingia kidato cha tano na cha sita ama kwenda kwenye vyuo vya ufundi kujipatia ujuzi hatimaye aweze kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Wizara ya Elimu inapaswa sasa kuanzisha au kusimamia kuwepo na kitabu kimoja cha kiada. Kwa maana kwamba tuwe na kitabu kimoja cha kiada kuanzia shule za msingi za Serikali pamoja na shule za msingi za binafsi. Hii itasaidia kuwa na uniformity katika elimu badala ya kuwa na vitabu tofauti vya kiada mwisho wa siku wanafunzi wanafanya mtihani unaofanana lakini wakiwa wanawezeshwa kwa kutumia vitabu tofauti tofauti. Angalizo kwa Serikali pia iangalie vitabu vinavyotumika katika shule za private viwe na ithibati za Kamishna wa Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Waziri wa Fedha kwa taarifa yake nzuri aliyoianda. Pia niipongeze Kamati ya Bajeti kwa kuandaa vizuri taarifa yao. Kwa namna ya pekee pia, niipongeze Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha Tanzania inazidi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika sekta ya kilimo. Kilimo ni msingi wa uchumi wa viwanda na uti wa mgongo wa Taifa letu. Wananchi wengi wa Tanzania tunategemea kilimo ili kujikwamua kiuchumi, hasa wananchi wa vijijini wanategemea kilimo kujipatia mahitaji yao. Mwananchi wa kijijini anategemea kilimo kusomesha mtoto, kupata mahitaji yake ya msingi ikiwemo afya, yaani kilimo ndiyo kila kitu kwake. Pamoja na hayo yote bado wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo soko kwa maana kwamba baada ya mavuno, wananchi hawana soko la uhakika. Wanavuna lakini mwisho wa siku mazao yao hayapati soko kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kilimo wanacholima kwanza kinakuwa hakina tija. Wanatumia vitendea kazi vilivyopitwa na muda. Akina mama wengi wa kijijini wanajihusisha sana na kilimo lakini hawana vitendea kazi vinavyowarahisishia kufanya kilimo kile kuwa chepesi zaidi. Hivyo inakuwa vigumu sana kupata tija au kupata manufaa kupitia kilimo. Wamama hao leo wanahangaika kutumia jembe la mkono katika kilimo, hawawezi kulima mashamba makubwa hivyo, wameishia kulima mashamba madogo madogo ambayo sasa mazao wanayoyapata ndio hayohayo wanatumia katika chakula na katika mahitaji mengine, mwisho wa siku wanaendelea kudhoofika kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo bado naendelea kushauri Serikali kuona ni namna gani watainua sekta hii ya kilimo ili wananchi wetu wa vijijini waweze kujikwamua kiuchumi. Kwanza nishauri Serikali iwekeze katika utafiti wa mbegu tunazozitumia. Mbegu zetu nyingi tunazotumia zinatoka nje ya nchi, asilimia kubwa mbegu za mahindi na mbogamboga hazizalishwi hapa nchini hivyo, husababisha wananchi kutumia gharama kubwa kupata mbegu na kutumia mbegu ambazo sio bora katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Serikali ifundishe wakulima wetu kuhifadhi na kusindika mazao ili waweze kuuza bidhaa badala ya malighafi. Pia nishauri pia Serikali kujenga mabwawa ya kuvunia maji ili kuboresha scheme za umwagiliaji. Mfano, katika Wilaya ya Babati kuna Vijiji vya Shauri Moyo, Masware, Kisangaji, Bonde la Kiru, Madunga, Narkash, vyote vinategemea kilimo cha umwagiliaji, lakini hawana uwezo mkubwa au teknolojia ya kutosha kuvuna maji ili waweze kuendesha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wengi hawana elimu ya kutosha. Hawaelewi ardhi yao wanayoitumia ni mazao gani hasa yanastawi, hivyo wanastawisha mazao ambayo wakati mwingine hayaendani na maeneo yao. Maafisa Ugani katika maeneo yetu bado ni wachache sana. Niishauri Serikali kuongeza Maafisa Ugani katika kila kijiji ili waweze kuwaelimisha wananchi wajue ni mazao gani yanastahili kustawishwa katika maeneo yao, lakini pia waweze kutoa shamba darasa. Yale mafunzo ya shamba darasa yanasaidia wananchi kuona kwa vitendo ili waweze kuzalisha mazao yale yanayoendana na maeneo yao na pia yaweze kuwaletea tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia vyuo vya kilimo viboreshwe. Vyuo vyetu vya kilimo haviendi kulingana na ukuaji wa teknolojia. Bado tunatumia mbinu zile za zamani katika kuwapa mafunzo wale wataalam wa kilimo ambao wana kazi ya kwenda kuwaelimisha wakulima hawa, ili waweze kuzalisha mazao kwa kiwango kikubwa. Mfano, Chuo cha Sokoine nashauri Serikali ione ni kwa namna gani kiendelee kubaki na kutoa taaluma inayohusiana na kilimo, uvuvi badala ya kujikita katika kutoa fani ya ualimu. Kama inavyotambulika ni Chuo cha Kilimo, kibaki katika kutoa fani ya kilimo badala ya kujishughulisha na fani nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika Mkoa wetu wa Manyara, tunaomba Chuo Kikuu cha Sokoine kuanzisha shamba darasa katika mkoa wetu, ili wananchi wa mkoa ule waweze kufaidika na mafunzo ya kilimo na mwisho waweze kulima kilimo chenye tija na kufaidika na kilimo hatimaye kuleta maendeleo na mapinduzi katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)