Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Edwin Maleko (21 total)

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, Wizara ina mkakati gani kuongeza watalii kwa sababu kutokana na UVIKO-19, idadi ya watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro imepungua sana kutoka 50,000 mpaka 12,000 kwa mwaka 2020. Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kuweza kuongeza watalii na kusaidia ajira kwa vijana wanaotegemea mlima huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; akinamama wajasiriamali wa Kilimanjaro wanaojishughulisha na shughuli za utalii tunaomba na wao waweze kupatiwa mikopo ili waweze kutangaza zaidi mlima wetu, mbuga zetu na utalii kwa ujumla. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum Kilimanjaro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Esther kwa juhudi nzuri anazozifanya za kuendelea kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro. Nampongeza sana kwa sababu amekuwa ni balozi mzuri wa kuhakikisha eneo hili linaendelea kuvutia watalii wengi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ameuliza kwamba tuna mkakati gani wa kuendelea kuongeza watalii na kuongeza ajira kwa vijana. Eneo hili Wizara imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali zikiwemo kuanzisha marathons mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya hifadhi, lakini lengo ni kuhakikisha kwamba watalii wengi wanakwenda kuviona vivutio lakini pia kuwa mabalozi wa kuendelea kuvitangaza.

Mheshimiwa Spika, hili ni shahidi hata Watanzania wa leo wamekuwa wazalendo na kila mtu sasa hivi anamhabarisha mwenzake kuhakikisha kwamba wanafika kwenye vile vivutio, lakini siyo kufika tu, kuisemea Tanzania ndani ya nchi na maeneo mengine ya nje ya nchi na lengo ni kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa. Ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Katika kuboresha ufaulu katika shule zetu za kata; je, Serikali ina mpango gani sasa kuweza kukamilisha maabara?

Lakini swali la pili, ni lini Serikali itamaliza upungufu wa walimu hasa wa sayansi katika shule zetu za Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kwamba lengo la Serikali kwa sasa ni kuhakikisha shule zote zinakuwa na maabara na ndiyo maana katika kila mwaka wa fedha tumetenga fedha kujenga maabara katika shule zetu za sekondari za kata nchini. Kwa hiyo, hilo ni kipaumbele chetu ambacho Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametuagiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, upungufu wa walimu wa sayansi tunautambua na ndiyo maana katika ajira zote ambazo tumekuwa tukizitoa sasa hivi tunawapa vipaumbele pia zaidi walimu ambao wamesoma masomo ya sayansi na tutaendelea kufanya hivyo ili kuondoa hili tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi katika shule zetu. Ahsante sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwanini Serikali isipunguze riba inapokopesha benki za biashara ili gharama hizo ziweze kushuka na Watanzania wengi waweze kukopa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwanini Serikali isipunguze riba inapouza hati fungani ili Watanzania wengi waweze kupeleka fedha zao katika benki hizo kama fix deposit.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Malleko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, viwango vya riba vimepungua kwa asilimia 16.60 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 16.41, mwaka 2022 ili kuwezesha benki kukopesha wananchi kwa riba nafuu na kupunguza mikopo chechefu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, riba za hatifungani haziwekwi au kupangwa na Benki Kuu ya Tanzania bali ni matokeo ya mchakato wa mauzo na ununuzi wa hatifungani kutoka soko la fedha linaloendeshwa kwa mfumo wa soko huria. Hata hivyo, takwimu za karibuni zinaonesha kuwa riba za hatifungani zimepungua.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Mamba Kusini iliyopo katika Jimbo la Vunjo, kuna shida kubwa ya mawasiliano.

Je, ni lini Serikali inaweza kurekebisha tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupokea changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Vunjo ili tukaifanyie tathmini ili sasa tuweze kufikisha mawasiliano katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Ni kweli kabisa Kampuni za Vodacom na Tigo zinatoa huduma katika kata hii, lakini kutokana ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kata hii, maeneo mengi yamekuwa na changamoto ya mawasiliano. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha inashughulikia changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuweza kuwezesha Kampuni ya Airtel na yenyewe inaweka minara katika kata hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Serikali kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya mawasiliano nchini kote. Vile vile kwa kuangalia katika jibu langu la msingi hasa hasa katika Kata hii ya Mamba tayari kuna mnara mwingine ambao unajengwa katika kata hii ambapo naamini kabisa utakapokamilika suala la mawasiliano litakuwa limeboreka kabisa, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ni lini barabara ya Uru Shimbwe itajengwa kwa kiwango cha lami maana imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza itakuwa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha usanifu wa kina wa barabara husika. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ashante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Serikali kupitia vyuo vikuu hapa nchini inatoa mafunzo ya saikolojia. Kwa nini basi isiajiri wataalamu wa saikolojia ili kupunguza tatizo hili kwa sababu kumekuwa kukiongezeka kesi za mauaji na ukatili kila kukicha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa nini Serikali isiwe na mpango wa kusajili chama cha wataalamu wa saikolojia kama ilivyo kwa taaluma nyingine nchini kama udaktari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza ni ajira; Serikali inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata kibali kwa kuajiri wataalamu hao kadri bajeti inavyoruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kuunda bodi ya wataalamu; Serikali ipo kwenye mchakato wa kukamilisha utungaji wa Sheria ya Wataalamu wa Ustawi wa Jamii ili kuona kwamba itakapomalizika basi bodi hiyo itaundwa ili kusajili wataalamu hao wa ustawi wa jamii ikiwemo wanasaikolojia. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru: -

Je, ni lini Serikali itafanya upembuzi yakinifu kwa barabara ya Mwembe-Mbaga na hatimaye kuijenga kwa kiwango cha lami kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakazi wa milimani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, barabara nyingi sana tunategemea kuzifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Tukiwa tunajua tunaelekea mwisho wa utekelezaji wa ilani ya chama, kwa hiyo tunaamini barabara zote ambazo zimeainishwa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tutazifanya kuanzia mwaka huu na mwaka ujao wa fedha, ikiwepo na barabara ya Mheshimiwa Mbunge aliyoisema, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa watu wenye ulemavu wameonekana mara nyingi wakiwa wanaombaomba na wakati mwingine kutumiwa kama chambo katika kuomba; je, ni mkakati upi wa Serikali katika kuwasaidia watu hawa kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kutokana na suala la kuwa ombaomba. Moja ya mikakati ya Serikali ni kutoa elimu; kumekuwa na changamoto sana ya kubadilisha mindsets za watu wetu. Na slogan ya Serikali ambayo inatumika hapa ni disability is not inability; kwa hiyo tumekuwa tukitoa elimu. Sambamba na hilo, Serikali imefungua vyuo vya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha waweze kupata ujuzi wa ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tumekwenda pia kwenye hatua nyingine ya kuweza kutoa mikopo kupitia halmashauri, asilimia mbili, kuwawezesha watu wenye ulemavu. Sambamba na hilo pia tumekwenda katika hatua nyingine ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia watu wenye ulemavu katika kutengeneza miongozo mbalimbali ukiwemo huu wa kuweza kuwa na mfuko maalum pamoja na kuwawezesha na kuwaweka kwenye vyama ambavyo vitawasaidia kuweza ku-raise agenda zao na kuweza kusaidiwa na Serikali kwa ukaribu na kwa umoja zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo la kuendelea kuwa na suala la ombaomba, tayari tumeshaweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuweza kuongeza fedha katika mifuko ya watu wenye ulemavu ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali na kujikwamua zaidi.

Mheshimiwa Spika, upande wa elimu, tayari tuna inclusive education ambapo kwa wale wenye uwezo wa kwenda shule Serikali imekuwa ikiwachukua. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, amekwisha kutoa zaidi ya bilioni tatu kwa ajili ya kurekebisha vyuo vya watu wenye ulemavu na kutoa huduma za utengemavu, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana; je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kudhibiti bei ya kahawa, maana imekuwa ikipanda na kushuka kila mara? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, na siyo tu bei ya kahawa, ni mazao yote bei inapanda na kushuka. Serikali haiwezi kudhibiti bei, bali Serikali jukumu letu la msingi ni kuongeza tija ili kupunguza gharama za uzalishaji ili wakulima waweze kupata faida baada ya gharama zao kupungua. Kwa hiyo, tunachukua hatua mbalimbali za kupunguza gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii wakulima wa kahawa wametumia almost asilimia 7.5 ya mbolea yote ya ruzuku iliyosambazwa. Kwa hiyo, ile itawaongezea tija. Mwelekeo wa Serikali ni kuongeza tija kwa kuwapa miche bora ili kuwapunguzia gharama na kuwaongezea uzalishaji waweze kuwa competitive. Hatua ya pili ambayo tunataka kuweka kwenye zao la kahawa ni uhamasishaji wa matumizi ya kahawa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi, tuna-export kahawa kwa wastani wa dola nne, lakini tuna import made coffee kwa wastani wa dola 20. Kwa hiyo, Serikali sasa tunaanza hatua, mtaona kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo, mfano kwenye maeneo ya Kagera tunaanza uwekezaji kwenye Kiwanda cha TANICA ili tuongeze blending na matumizi ya kahawa iliyokuwa processed ndani na kuongeza unywaji wa kahawa ndani ya nchi na kuwaongezea wakulima soko la uhakika na uhakika wa bei.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza.; je, ni vigezo gani vinatumika kupanga ugawaji wa umeme kwa urban peri -urban pamoja na REA?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni upi mpango wa Wizara katika kushughulikia malalamiko ya wananchi juu ya tariff kwa bei za umeme kuwa kubwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Malleko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la kwanza, TANESCO imekuwa ikipanga Mradi wa REA uende wapi na Peri-Urban uende wapi kulingana na taarifa zinazotolewa na TAMISEMI. Pia wenzetu wa TAMISEMI ndio wenye dhamana ya kusema hapa ni mjini na hapa ni kijijini, hapa ni Halmashauri ya Mji, hapa ni Jiji na hapa ni Manispaa. Kwa hiyo, sisi TANESCO tumekuwa tukipata taarifa za TAMISEMI na tunatumia hizo kupeleka Miradi ya Peri-Urban kwenye maeneo ya mijini na Miradi ya REA kwenye maeneo ya vijijini. Pia tumeendelea kushirikiana nao kubaini maeneo jinsi yanavyobadilika ili tuweze kufikisha huduma sahihi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, katika hizi nchi za jirani na Tanzania, watu wenye bei za chini kabisa za umeme ambazo kimsingi kabisa zimewekewa ruzuku na Serikali ni Tanzania. Gharama za uzalishaji na usambazaji wa umeme Tanzania haziko na usawa na uwiano sahihi na gharama zinazolipwa na wananchi katika kupata ile huduma ya umeme na kuunganishwa. Kwa hiyo, gharama zetu ziko chini na sisi tunadhani kuna haja ya kuzitazama vizuri ili shirika liweze kuendelea kujiendesha na kuweza kutoa huduma sahihi kwa wananchi na kwa wakati.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na Serikali kutenga fedha za ukarabati kila mwaka, lakini vyumba vya kubadilishia wachezaji ni chakavu, pia chumba cha marefarii kipo karibu sana na chumba cha timu pinzani ambayo inaleta wakati mwingine sintofahamu. Je ni lini sasa Serikali inaweza kutatua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je nini mpango wa Serikali kuongeza nguvu katika kujenga Uwanja wa Majengo ambao unajengwa kwa fedha za ndani ili uweze kukamilika mapema? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malleko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishaeleza katika majibu ya swali la msingi kwamba ni wajibu wa Serikali kupitia Chuo chetu cha Ushirika kwa maoteo ya bajeti kwa ajili ya ukarabati. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na nilithibitishie Bunge lako Tukufu tutaendelea kufanya hivyo na hivi sasa tutatupia macho maeneo hayo aliyoyataja katika vyumba hivyo vya kubadilishia nguo pamoja na hiki chumba cha marefarii, tutafanya hayo marekebisho labda katika bajeti ijayo ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, anataka kufahamu vile vile mkakati wa Serikali kuhusiana na Uwanja huo wa Majengo. Naomba nimthibitishie Mbunge kwamba uwanja huo tunafahamu kwamba uko chini ya Manispaa ya Moshi. Kwa hiyo tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, lakini vile vile Wizara yenye dhamana ya michezo kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na maswali mazuri sana na Serikali lakini nilitaka kujua, je, ni lini katika ajira hizi zilizotangazwa watumishi hawa wataingia kazini ili waende wakawatibu Watanzania wengi ambao wanahitaji huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira hizi zilizotzngazwa zote 21,300 katika sekta ya elimu na afya zitaanza kutumika au wataingia kazini baada ya mchakato wa ajira hizi kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo muda siyo mrefu Mheshimiwa Malleko kule Kilimanjaro lakini na Waheshimiwa Wabunge wote hapa wataanza kuona wale watumishi wapya wanaaanza kwenda kwenye maeneo yao.
MHE. ESTHER E. MALEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika kutekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda, nini mkakati wa Serikali kufufua viwanda vilivyopo katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kuwapatia wananchi wetu ajira, lakini pia kuongeza uchumi wa Mkoa wetu wa Kilimanjaro? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama nilivyosema nia ya Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kutekeleza sera ya kuwa nchi ya viwanda na kama tulivyosema tuwe na uchumi unaoendeshwa na viwanda hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kutafuta wawekezaji kwa sababu, tunaondokana na uchumi hodhi, kwa maana ya Serikali kufanya biashara au kuendesha viwanda. Kwa hiyo, Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa mingine ambako kuna viwanda vyenye changamoto, vile ambavyo vitakuwa vimebinafsishwa, lakini havijaendelezwa au vingine ambavyo tunaona havifanyi kazi, tutaendelea kutafuta wawekezaji kwa kuweka kwenye masharti nafuu, pia vivutio mbalimbali ili kuvutia uwekezaji wa ndani, hata wawekezaji kutoka nje ili kuhakikisha viwanda hivyo vimefanya kazi na kupunguza nakisi ya bidhaa mbalimbali ambazo zinatumika nchini kuagizwa nje, lakini pia kutoa masoko kwa malighafi ambazo zinatumika kwenye viwanda hivyo ambavyo vinzalishwa hapa nchini, nakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itatekeleza maombi ya kibali cha mabadiliko ya mishahara katika hospitali ya KCMC ambacho wameomba tangu mwaka 2011?

Swali la pili; kuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika Hospitali hii, je, Serikali imejipanga vipi kuweza kutatua changamoto hiyo, ikizingatiwa hospitali hii ni ya Kanda?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoshirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro na namna ambavyo anafanya kazi yake. Swali lake la kwanza kuhusu ni lini Serikali itafanya maombi yale ya kupandisha hadhi na kuongeza mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali la kwanza la kuhusu Mbeya Mbeya pamoja na KCMC ni hospitali ambazo ziko kwenye mchakato ambao kuna mjadala kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Utumishi kwa ajili ya kufikia kiwango hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge unakitaja. Wiki hii tumepanga tufanye kikao na utumishi ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kujikwamua na kusaidia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni suala la upungufu wa watumishi. Kama ambavyo nimesema kuna watumishi 905 ambao wanalipiwa na Serikali, lakini wao wenyewe wanalipa kwa mapato yao ya ndani zaidi ya watumishi 400. Maana yake ukiangalia wanao watumishi karibu 1,300 sasa huo upungufu labda tutaenda kuangalia upungufu umetokana na nini. Inawezekana huko nyuma kweli kulikuwa na upungufu unaoletwa na hospitali yetu ya Mawenzi ilikuwa haifanyi vizuri, sasa hospitali yetu ya Mawenzi sasa inafanya vizuri kwa hiyo, wagonjwa wengi watazuiliwa Mawenzi, wataenda wale wanaohitaji kwenda kwenye Hospitali ya Kanda kwa hiyo, huo upungufu unaweza usionekane. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la nyani na ngedere ambao wamekuwa ni waharibifu sana kwa mazao ya wananchi: Je, Serikali haioni sababu ya kuwahamisha au kuwauza nje ya nchi ili kujipatia fedha za kigeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya miongoni mwa wanyamapori ambao tunawatumia sana kwa shughuli zetu za utalii na kivutio cha watalii kwa ajili ya kuingiza mapato katika nchi yetu ni hao kima na wengine. Hata ukiangalia kwa mfano kwa upande wa Zanzibar, kule kuna wale kima ambao nadhani dunia nzima wanapatikana tu Zanzibar. Kwa hiyo, kwa kusema kwamba tuwachukue tuwasafirishe nadhani hili tulichukue tuende tukalifanyie kazi tukafikirie zaidi. (Makofi)

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ninaomba kuuliza, je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa rheumatic heart disease ambao unaonekana unaongezeka kwa kasi kubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho naweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge moja ni elimu, watu kuangalia afya zao kila wakati na kupata tiba stahiki mapema, ndiyo maana unaona leo, hata Taasisi yetu ya Jakaya Kikwete keshokutwa inakwenda Pemba kwenda kabisa kule vijijini kuhakikisha watu wanafanyiwa uchunguzi na kuhakikisha haya matatizo yanagundulika mapema na watu kupata tiba stahiki mapema. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina ushahidi kupitia kwa Mwenyekiti na Katibu wa Wastaafu hawa, na pia wamepeleka vielelezo vyao kwa Waziri Mheshimiwa Ndalichako kwamba mpaka sasa hawajalipwa stahiki zao;

Je, nini kauli ya Serikali kuweza kuwalipa wastaafu hawa haki zao?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, hii Kampuni ya Magunia mwaka 1996 baada ya kuona haiendeshwi kwa faida iliamua kuwapumzisha au kuwastaafisha wafanya kazi hao lakini pia mwaka huo huo iliingia mkataba wa hiari kwa watumishi hao baada ya kukubaliana kustaafu kwa maana ya kupata mshahara wa mwezi mmoja, malimbikizo ya likizo, malimbikizo ya mishahara, gharama za kusafirisha mizigo na malimbikizo ya michango mingine baada ya kuingia mkataba wa hiari kwamba watalipwa kama vibarua kwa siku shilingi 1,000 na wangelipwa marupurupu mengine kama kiwanda kingepata faida.

Mheshimiwa Spika, lakini kiwanda hiki baada ya kuona kinashuka faida mwaka 1998 kilibinafsishwa kwenda kwenye kampuni ya TPM ambayo ni Kampuni tanzu ya Mohamed Enterprises. Kwa hiyo, maana yake madai haya nadhani ndio hayo ambayo walidhani watalipwa kama kiwanda hiki kingeweza kupata faida kwa wakati huo, nakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina maswali mawili ya nyongeza; mwaka jana wakati wa Waziri wa Fedha akihitimisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2021/2022 alisema kwamba wale wote ambao wana haki ya kupata msamaha huo watapata msamaha wa kodi hiyo, lakini mpaka sasa wanaendelea kutozwa.

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka TRA na TANESCO kuweza kubadilisha mifumo hiyo ili watu hawa waendelee kupata msamaha wa kodi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha fedha hizo ambazo wamekuwa wakiwakata watu hawa ambao tayari walikuwa wamewaahidi kwamba fedha hizo hazitaendelea kukatwa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kilimanjaro, shemeji yangu huyu kwa kuwatetea sana Watanzania hasa wanyonge.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wiki moja iliyopita alisimama kidete kuhusu ruzuku ya kahawa na Serikali tumechukua jambo hilo. Hata hili alilolileta, ni kweli tulipoanza tulianza tukiwa tuna ujaribisha mfumo huku tukiwa tunatekeleza sheria ya Bunge, kwa maana hiyo ni kweli kulitokea baadhi ya watu waliendelea kukatwa huku wakiwa wanastahili kusamehewa. Lakini tulirekebisha kwa kiwango kikubwa mifumo hiyo, kwa hiyo kama bado wapo ambao wamebakia wachache ambao wameendelea kukatwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalifanyia kazi na nielekeze Mamlaka ya Mapato kufanya haraka kumalizia wale ambao bado hawajanufaika na msamaha huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka wa fedha unakwenda kuanza tutafanyia kazi na hilo la kimfumo ili kuweza kufanya sorting zote ili tunapoanza mwaka mpya tuwe tumekamilisha jambo hilo kikamilifu, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, kwanza nachelea kusema kiendacho kwa mganga hakirudi kwa sababu Kilimanjaro hata waganga walishakwisha, ninachoweza kusema tu ni kwamba kwa wale ambao kumbukumbu zao zinaonesha wamekatwa na walitakiwa wasilipe wawasiliane na Mamlaka ya Mapato kwa sababu kwenye kodi huwa kuna utaratibu wa kufanya offsetting kile ambacho ulishakilipa in advance ili kiweze kuwa offsetted wakati unalipa kinachofuata. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina maswali mawili ya nyongeza; mwaka jana wakati wa Waziri wa Fedha akihitimisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2021/2022 alisema kwamba wale wote ambao wana haki ya kupata msamaha huo watapata msamaha wa kodi hiyo, lakini mpaka sasa wanaendelea kutozwa.

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka TRA na TANESCO kuweza kubadilisha mifumo hiyo ili watu hawa waendelee kupata msamaha wa kodi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha fedha hizo ambazo wamekuwa wakiwakata watu hawa ambao tayari walikuwa wamewaahidi kwamba fedha hizo hazitaendelea kukatwa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kilimanjaro, shemeji yangu huyu kwa kuwatetea sana Watanzania hasa wanyonge.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wiki moja iliyopita alisimama kidete kuhusu ruzuku ya kahawa na Serikali tumechukua jambo hilo. Hata hili alilolileta, ni kweli tulipoanza tulianza tukiwa tuna ujaribisha mfumo huku tukiwa tunatekeleza sheria ya Bunge, kwa maana hiyo ni kweli kulitokea baadhi ya watu waliendelea kukatwa huku wakiwa wanastahili kusamehewa. Lakini tulirekebisha kwa kiwango kikubwa mifumo hiyo, kwa hiyo kama bado wapo ambao wamebakia wachache ambao wameendelea kukatwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalifanyia kazi na nielekeze Mamlaka ya Mapato kufanya haraka kumalizia wale ambao bado hawajanufaika na msamaha huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka wa fedha unakwenda kuanza tutafanyia kazi na hilo la kimfumo ili kuweza kufanya sorting zote ili tunapoanza mwaka mpya tuwe tumekamilisha jambo hilo kikamilifu, nakushukuru.

SPIKA: Swali lake la pili lilikuwa linataka kujua kama wale ambao sasa baada ya msamaha wameendelea kukatwa fedha, je, watarejeshewa zile fedha zao? (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nachelea kusema kiendacho kwa mganga hakirudi kwa sababu Kilimanjaro hata waganga walishakwisha, ninachoweza kusema tu ni kwamba kwa wale ambao kumbukumbu zao zinaonesha wamekatwa na walitakiwa wasilipe wawasiliane na Mamlaka ya Mapato kwa sababu kwenye kodi huwa kuna utaratibu wa kufanya offsetting kile ambacho ulishakilipa in advance ili kiweze kuwa offsetted wakati unalipa kinachofuata. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza au kuajiri vijana wengi zaidi na kuwapa mafunzo hayo ili waweze kusimamia ile miradi mikubwa inayotolewa kwenye mikoa na wilaya, kwa sababu mingi imeonekana ikihujumiwa sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa madhumuni kama aliyoyaeleza Mheshimiwa Mbunge Malleko, ni kweli kwamba Serikali ina dhamira na imekuwa ikiajiri vijana kwa ajili ya kujiunga na vyombo vyetu vingi vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi, Fire na Uokozi pamoja na Magereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vyote hivi hushiriki katika shughuli za ulinzi na usalama wa miundombinu inayoendelezwa kwenye maeneo yetu kupitia Kamati za Usalama za Wilaya na Kamati za Usalama za Mikoa, nashukuru.