Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Esther Edwin Maleko (13 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. ESTHER E. MALLEKO) aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua Kiwanda cha Magunia Moshi Mkoani Kilimanjaro ili kukuza ajira na uchumi kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, magunia yanayotokana na zao la mkonge ni moja ya vifungashio muhimu vya mazao ya kilimo hapa nchini. Tanzania ina viwanda nane vinavyoongeza thamani zao la mkonge. Kati ya viwanda hivyo, viwanda vitatu 3 ni vya kuzalisha magunia ya mkonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Magunia cha Moshi (Tanzania Bag Corporation – TBCL) kilibinafsishwa na Serikali kwa kampuni ya Mohamed Enterprise Tanzania Limited (METL). Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali kiwanda hiki kimeshindwa kuzalisha na kujiendesha kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za viwanda vya magunia ya mkonge ni mtambuka na Serikali inazishughulikia kiujumla kwa tasnia yote ya mkonge. Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za utatuzi wa changamoto ikiwemo kulinda wazalishaji wa ndani na kuwatengenezea mazingira bora ya ufanyaji biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini ya Serikali kuwa jitihada hizi zinazoendelea zitakuwa ni chachu ya kuinua kilimo cha mkonge na ufufuaji wa viwanda vya magunia ya mkonge kikiwepo kiwanda cha magunia cha Moshi na hivyo kukuza ajira na uchumi wa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha makongamano ya Kimataifa ili kukuza utalii wa Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutuamini mimi na Mheshimiwa Waziri kuendelea kuhudumu Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kipekee nikupongeze wewe binafsi kwa kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikiendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo: -

(a) Onesho la Utalii la Kimataifa la Kilifair linalofanyika Mjini Moshi Mwezi Juni kila mwaka;

(b) Mbio za Kilimanjaro (Kilimanjaro Marathon) zinazofanyika Mkoani Kilimanjaro mwezi Februari kila mwaka;

(c) Kushiriki makongamano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo WTM – London, ITB - Ujerumani, Fitur-Hispania na Expo - 2020 Dubai;

(d) Kushiriki makongamano ya kimataifa yanayolenga kuimarisha uhifadhi na kutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro likiwemo Kongamano la Milima Mirefu Duniani (International Mountains Alliance - ITA);

(e) Mlima Kilimanjaro ni moja ya eneo la urithi wa dunia ambapo kupitia mikutano mbalimbali ya UNESCO Mlima huo hutangazwa;

(f) Kuwatumia watalii wanaofika Tanzania kama mabalozi wa kuutangaza Mlima Kilimanjaro;

(g) Kuendelea kutumia matukio muhimu ya Kitaifa kama sherehe za Uhuru kuhamasisha jamii kupanda Mlima Kilimanjaro; na

(h) Kuandaa na kushiriki katika Onesho la Kwanza la Kimataifa la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilofanyika Jijini Arusha ili kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kubuni mikakati zaidi ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa maslahi mapana ya nchi. Ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza mkakati wa ujenzi wa hosteli kwenye shule za kata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa shule kuwa karibu na jamii na kwa muktadha huo Serikali ilielekeza kujengwa kwa shule za kata nchi nzima ili kuwawezesha wanafunzi kusoma karibu na maeneo wanayoishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliopo kwa sasa wa ujenzi wa hosteli kwenye shule za kata ambazo kulingana na jiografia ya eneo hususani umbali kutoka shule na makazi ya watu wananchi wenyewe wamekuwa wakijenga hosteli hizo na kuweka utaratibu wa kuziendesha na kuzisimamia kulingana na mahitaji waliyonayo.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, ni lini mnara wa mawasiliano ya simu utajengwa Kata ya Mamba Kusini Jimbo la Vunjo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mamba Kusini inaundwa na Vijiji vya Mkolowony, Lekura, Kiria, Kimbogho na Kimangara. Katika jitihada za Serikali za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na watoa huduma, Kampuni za Tigo na Vodacom zinatoa huduma za mawasiliano katika kata hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali itafanya tathimini katika Kata hii ya Mamba ili kubaini changamoto zilizopo za mawasiliano ya simu na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuyaingiza maeneo ya kata hii yatakayobainika kuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika katika orodha ya vijiji vitakavyoingizwa katika zabuni zijazo. Ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza wataalam wa saikolojia kwenye jamii ili kutoa huduma za ushauri wa afya ya akili na namna ya kuondokana na msongo?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu na inathamini huduma ya msaada wa kisaikolojia na kijamii ambayo inatolewa na wataalam wa saikolojia kwa lengo la kukidhi mahitaji ya mtu kimwili, kihisia, kijamii, kiroho na kiakili katika mazingira anayoishi. Ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo havina huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Naibu Spika, Mkoa wa Kilimanjaro una jumla ya vijiji 519 ambapo mpaka sasa vijiji 11 tu havina umeme. Vijiji hivi vimepangwa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kilimanjaro una vitongoji 2,260 na kati ya hivyo, vitongoji 286 tu ndiyo havina umeme. Vitongoji hivyo vitaendelea kupatiwa umeme kupitia Miradi ya Ujazilizi kwa kadri fedha zitakavyopatikana, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Uwanja wa Ushirika Moshi ili kukuza utalii wa michezo nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Maleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kinamiliki viwanja mbalimbali vya michezo ambavyo ni uwanja wa mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu na riadha. Viwanja hivyo ni miongoni mwa miundombinu iliyojengwa na Serikali ili kuendeleza michezo na burudani kwa jumuiya ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na wadau wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa viwanja hivyo vipo katika hali nzuri na vinaendelea kutumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa. Aidha, Chuo kina utaratibu wa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi wa Kilimanjaro kwa kumalizia ujenzi wa maboma ya zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi bilioni 1.96 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 37 katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.35 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya vitatu na zahanti 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya vituo vya afya na zahanati nchini kote.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, Serikali ina mchango gani katika kuboresha huduma za Hospitali ya KCMC ambayo inatoa huduma za afya kwa Kanda ya Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeboresha huduma za Hospitali ya KCMC kwa kupeleka fedha za miradi mbalimbali, kulipia mishahara pamoja na ufadhili wa masomo kwa wataalam kama ifuatavyo:-

(i) Serikali inalipa stahiki na mishahara ya watumishi 905 waliopo KCMC ambapo jumla ya shilingi 983,612,500 hutumika kila mwezi.

(ii) Katika Mwaka wa Fedha 2023 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya dawa, vitendanishi na vifaatiba.

(iii) Katika mwaka wa fedha 2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya hospitali na shilingi milioni 263.6 kwa ajili ya uendeshaji.

(iv) Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa ufadhili wa masomo ya ubingwa bobezi kwa watumishi 15 kada ya afya wa KCMC wanaosoma ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawalipa mafao yao watumishi waliokuwa Kiwanda cha Magunia Moshi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ilipokea madai ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Magunia Moshi na kuyashughulikia kwa kuunda Kamati ya Uhakiki. Taarifa ya Kamati hiyo ilibainisha kuwa Watumishi hao walishalipwa mafao yao na kujulishwa kwa barua yenye Kumb. Na. CKB.87/406/02/C/80 ya tarehe 3 Mei, 2019. Hata hivyo, pamoja na kuwajibu, wadai wameendelea kuandika barua kwenda kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali kuwasilisha malalamiko yao; na kwa upande wetu tumekuwa tukiwajibu na kutoa ufafanuzi kuwa walalamikaji hao walilipwa stahiki zao ipasavyo.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, nini utaratibu wa Serikali kutoa msamaha wa kodi ya jengo kwa wale wanaostahili baada ya kodi kuhamishiwa kwenye za LUKU?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya majengo kwa wale wanaostahili unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo Sura 289 ambapo mwenye jengo husika anatakiwa kuwasilisha maombi ya kupata msamaha wa kodi ya jengo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Baada ya TRA kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha kwa mujibu wa matakwa ya sheria, makato yake katika ununuzi wa umeme kupitia LUKU yatasitishwa. Aidha, kifungu cha 7(a) hadi (i) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289, kimeainisha majengo yaliyosamehewa kulipa kodi ya majengo.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya majengo umeainishwa katika Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo, 2020 sehemu ya nne, Na. 16(1) hadi (6).

Mheshimiwa Spika, utozaji wa kodi ya majengo kupitia manunuzi ya umeme wa mfumo wa LUKU hauondoi haki ya msamaha wa kodi ya majengo kwa anayestahili kisheria bali umeongeza ufanisi katika kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha ili kuepuka kuwaondolea makato hata wanaostahili.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, nini utaratibu wa Serikali kutoa msamaha wa kodi ya jengo kwa wale wanaostahili baada ya kodi kuhamishiwa kwenye za LUKU?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya majengo kwa wale wanaostahili unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo Sura 289 ambapo mwenye jengo husika anatakiwa kuwasilisha maombi ya kupata msamaha wa kodi ya jengo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Baada ya TRA kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha kwa mujibu wa matakwa ya sheria, makato yake katika ununuzi wa umeme kupitia LUKU yatasitishwa. Aidha, kifungu cha 7(a) hadi (i) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289, kimeainisha majengo yaliyosamehewa kulipa kodi ya majengo.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya majengo umeainishwa katika Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo, 2020 sehemu ya nne, Na. 16(1) hadi (6).

Mheshimiwa Spika, utozaji wa kodi ya majengo kupitia manunuzi ya umeme wa mfumo wa LUKU hauondoi haki ya msamaha wa kodi ya majengo kwa anayestahili kisheria bali umeongeza ufanisi katika kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha ili kuepuka kuwaondolea makato hata wanaostahili.
MHE. ESHTER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhusisha Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika kulinda miradi mikubwa ya kimkakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alIjibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kulilinda Taifa letu pamoja na Miradi Mikubwa ya Kimkakati kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Makao Makuu ya Jeshi imekuwa ikitoa wataalam mbalimbali wanaoungana na wataalam wa vyombo vingine vya Usalama ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inakuwa salama wakati wote, nashukuru.