Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Esther Edwin Maleko (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ESTHER E. MALEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, niwashukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa nafasi kwa kuteuliwa kugombea. Zaidi niwashukuru akinamama wa Kilimanjaro kwa imani kubwa waliyonipa, wakanipa kura za kishindo na mimi nikaweza kuwa Mbunge wao na kuja kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu. Pia nisiwasahau wazazi wangu, mume wangu, watoto wangu, ndugu jamaa na marafiki, kwa namna walivyonisaidia kwa maombi na kwa ushauri mpaka leo niko hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati anafunga Bunge la Kumi na Moja, lakini wakati anafungua Bunge la Kumi na Mbili Novemba 13. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ambayo imetoa dira, mwelekeo na mustakabali wa Taifa, Mheshimiwa Rais alisema katika ukurasa wa 10 kwamba wataongeza jitihada za kuwasaidia wananchi kiuchumi kwa kuwapa mikopo ambayo haina riba au yenye riba kidogo. Naomba basi niende moja kwa moja kuishauri Serikali yangu sikivu, ifanye utaratibu wa namna gani hiyo mikopo ambayo inatolewa na halmashauri 4% kwa wanawake, 4% kwa vijana na 2% kwa wenye walemavu, iangalie basi ni namna gani mikopo hiyo inaweza kuongezwa. Zaidi ya hapo iangaliwe ni namna gani mikopo hiyo haitatolewa kwa masharti ya kupewa kwa vikundi, ikatolewe kwa mtu mmoja mmoja kwa sababu ni wanawake wengi ambao wanahitaji mikopo hiyo lakini wakati mwingine wanakosa kwa sababu ya masharti ambayo yamewekwa kwamba ni lazima mkakope kwa vikundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu najua Serikali yangu ni sikivu naamini itazingatia suala hilo na kwasababu akinamama wa Kilimanjaro wengi ni wakulima, lakini wengi ni wafanyabiashara wakipatiwa fursa hiyo adhimu wataweza kukwamua familia zao. Kama unavyofahamu mwanamke ndiye anayeinua uchumi wa familia, hivyo mwanamke akiguswa familia itaguswa lakini pia na Taifa litakuwa limeguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisiache kulisema hili pia, kule kwetu Kilimanjaro akinamama wengi wanauza ndizi lakini ndizi haina bei kabisa inapopelekwa sokoni. Mwanamke anapopeleka ndizi sokoni anaenda kuiuza kwa shilingi elfu moja na wakati mwingine wanunuzi wanamkopa, anaweza kukaa na hiyo ndizi ikaiva kwa hiyo hivyo inabidi aitoe kwa wale wanunuzi ambao wao wakienda kuiuza wanaenda kuiuza kwa zaidi ya shilingi elfu ishirini na tano. Basi tuone ni namna gani tunaweza kuwapatia akinamama hawa elimu ya namna gani wanaweza kuchakata ndizi hizo na wakaweza kupata kipato zaidi na siyo kuonewa kwa namna ambavyo wanaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ya hewa ya Kilimanjaro tunaweza kulima kilimo cha mbogamboga, kilimo cha bustani. Naiomba Serikali yangu Tukufu iweze kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo ili sasa wanawake hawa ambao ni wakulima wapate elimu bora juu ya kilimo hicho wanacholima kwenye matunda, kwenye mbogamboga na tukaende kuongeza pato la Taifa. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais amesema leo Tanzania iko nafasi ya 20 kidunia kwa kuzalisha mazao haya, lakini imeingiza zaidi ya dola milioni 412 kwa mwaka 2015; mwaka 2018/2019 imeingiza zaidi ya dola milioni 779. Je, hatuoni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. ESTHER E. MALEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa utekelezaji wa elimu bila malipo kwa sababu kwa sasa wanafunzi ambao wanahitimu wameongezeka na wataendelea kuongezeka kwa kasi kubwa. Sasa ni vyema basi Serikali ijipange ni namna gani basi itaweza kukabili mahitaji haya makubwa ya miundombinu ambayo tayari imeanza kuelemewa. Wizara imeomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi trilioni 1.384 ambazo zina ongezeko la shilingi bilioni 42.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/2021, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida ni bilioni 480.5 ambayo ni sawasawa na asilimia 34.7 na maendeleo ni bilioni 903.9 ambayo ni sawasawa na asilimia 65.3 tunawapongeza sana kwa uwiano huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kati ya fedha hizo fedha za maendeleo ni bilioni 403, lakini bilioni 500 zinakwenda kwenye mikopo ya elimu ya juu. Sidhani kama ni sahihi fedha za mafunzo au training kuitwa fedha za maendeleo maana matumizi yake ni ya kawaida na matumizi ya fedha za maendeleo hayawezi kwenda kuwekwa kwenye fedha ambazo tunasema zinapelekwa kwenye mikopo ya elimu ya juu. Kwenye mafungu mengine ya fedha za kugharamia mafunzo ziko recurrent, ndio maana fedha zisipotolewa zote kinacho-suffer ni ile miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, katika mwaka huu mpaka Machi, 2021 miradi sita tu kati ya miradi 33 ya mikakati ya maendeleo ndio imepata fedha, lakini hii mingine mpaka sasa haijapata. Miradi hiyo ni EP4R na Equip T haijapata chochote mpaka sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, ni vyema basi zile fedha za mikopo ya elimu ya juu zipewe fungu lake tofauti ya kujitegemea ili zile fedha za miradi zisiweze kuguswa na ziende kwenye ile miradi, ili iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, TAMISEMI tunaomba waboreshe ushirikiano kati yao na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili waweze kushirikiana vyema kutoa huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sina uhakika sana kama Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanajua mahitaji makubwa ambayo yanatokana na kuanzisha utekelezaji huu wa elimu bila malipo. Kwa sababu katika kipindi hiki cha miaka minne tutakuwa tunahitaji madawati 41,333; tutakuwa tunahitaji matundu ya vyoo 75,300; vitabu 18,000,825; na walimu 41,833; na fedha za ruzuku ya wanafunzi bilioni 1,882,000,500; ambayo hiyo ni sawa na trilioni 1.476 ili kuweza kukamilisha shughuli hii ya wanafunzi watakaoongezeka katika kipindi hicho cha miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba ushirikiano bora kati ya TAMISEMI, watakaowasaidia kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye wilaya mbalimbali mfano VETA na vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia hapo, huo ndio mchango wangu. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye Wizara ya hii ya TAMISEMI. Moja kwa moja nijikite kuchangia upande wa elimu. Naipongeza sana Serikali yangu sikivu kwa kuweza kusimamia kujenga shule kwenye kila kata. Suala hili la kuwa na shule kwenye kila kata limetupunguzia adha kubwa ya wanafunzi kupata au kwenda mwendo mrefu kwa ajili ya kwenda shule. Pamoja na Serikali kufanya kazi hii kubwa ikatenga shilingi bilioni 23 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure, imefanya kazi kubwa sana naipongeza sana Serikali yangu. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, naomba kutoa ushauri kwa Serikali yangu sikivu, kwamba baada ya kujenga shule hizi kwenye kila kata, tuangalie sasa ni namna gani tunakwenda kujenga hostel, mabweni kwenye kila kata sasa ili wale wanafunzi ambao wanatoka umbali mrefu wasipate shida njiani. Nasema hivyo kwa sababu wanafunzi wa kike wanakutana na vishawishi vingi wakati wanakwenda shule. Wakati mwingine kutokana na umbali wanaokwenda wanaweza kurubunika katikati hapo wakaingia kwenye mitego mingine mingi kwa sababu wanaona muda wa kwenda shuleni na kufika kwa wakati unakuwa ni kidogo. Kwa hiyo naiomba Serikali yangu sikivu iweze kuangalia ni namna gani sasa tumemaliza kujenga shule za kata, tunatoa elimu bure, lakini namna gani tunaweza kujenga mabweni ili wanafunzi hawa waweze kupata elimu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ule muda wanaotoka shule na kurudi nyumbani wanatumia muda mrefu, lakini wangekuwa shuleni wangeweza kusoma kwa bidii, wakapata muda wa kusaidiana na wenzao, wakapata muda wa kufundishwa zaidi, tofauti na hapa ambapo leo wanatoka shule, wanakwenda nyumbani, wanakuta nyumbani kuna kazi ambazo watasaidia wazazi, kwa hiyo wanakosa muda wa kujifunza kwa muda mrefu. Naomba sana dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu sina mashaka naye, najua yeye pamoja na wasaidizi wake wataliangalia hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema kuhusu wanafunzi, niseme kuhusu Walimu. Walimu hawa wanatusaidia kuangalia watoto wetu, tunaenda makazini na tunafanya kazi zetu kwa sababu tunajua wapo walimu ambao wanatunza watoto wetu, lakini walimu hao hao wamesahaulika, kiwango chao cha malipo kipo chini. Ni lazima sisi kama Bunge Tukufu tuweze kuangaliana kuwapigania Walimu hawa ili waweze kuongezewa mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, Walimu hawa wanakwenda masomoni wakiwa shuleni. Wanapokwenda masomoni wengine wanaobaki shuleni ambao wanaendelea na kazi wanaongezwa mishahara au kupandishwa vyeo, lakini hawa walikwenda kujiendeleza pamoja na kwamba wanajiendeleza kwa pesa zao, tena kwenye kima kile cha mshahara mdogo wanaolipwa, wanaweza kwenda kujiendelea ili wafanye kazi kwa ufanisi mkubwa, lakini shida inatokea wao wakiwa masomoni wenzao wanapandishwa mishahara, wanapandishwa madaraja, lakini wao hawapandishwi wakiwa masomoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu sikivu iweze kuwaangalia hao Walimu, imekuwa ni kada ambayo imeachwa nyuma, ni kada ambayo haiangaliwi, wengine wakienda masomoni wakirudi mishahara yao inaongezeka, lakini kwa hao walimu ambao wanatuangalizia watoto wetu, hao walimu wanaotusaidia kufuta ujinga, wamesahaulika. Kwa hiyo naiomba Serikali iangalie pia suala hilo la Walimu. (Makofi)

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika. Taarifa.

SPIKA: Uko wapi?

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, niko hapa!

SPIKA: Endelea.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, suala la mishahara na suala la kutokupandishwa vyeo wakiwa shule sio Walimu tu ni watumishi wote Tanzania. Naomba kumpa taarifa hiyo.

SPIKA: Unaipokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Esther E. Malleko.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante naipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, kero nyingine kwa Walimu, ni kero kubwa kwa wale Walimu wanaostaafu. Baada ya kustaafu anapotakiwa kubeba mizigo yao na kurudi nyumbani kwao inakuwa wanacheleweshewa kupata yale malipo na hii inaendelea kukatisha tamaa kwa sababu hao watu wamefanya kazi hiyo kubwa kwa maisha yao yote, lakini wanapofika wakati wa kustaafu bado hata ile hali ya kuangaliwa waweze kurudi nyumbani kwao imekuwa ni shida.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ESTER E. MALEKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya Kilimo. Kwanza naipongeza Wizara kwa hotuba nzuri, lakini nijikite moja kwa moja kwenda kuzungumzia changamoto zinazokabili sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ya kilimo inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na pia inatoa pato la asilimia 29 kwenye pato la uchumi wa Taifa, lakini hii ndiyo sekta yenye changamoto kubwa kuliko sekta nyingine zozote. Tunategemea tutapata ajira kutoka kwenye sekta hii, lakini hatujaweka mkazo mkubwa kwenye hii sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2022 katika ukurasa wake wa 33 imeeleza kwa kirefu mikakati ya kukifanya kilimo cha kisasa na cha kibiashara chenye tija na ambacho mazao yake yatakuwa yameongezwa thamani, lakini shida kubwa pamoja na hayo, ni masoko. Wakulima wengi wanalima lakini hawajui mahali pa kuuza mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka Mheshimiwa Rais wetu Hayati John Pombe Magufuli alipokuwa anahutubia Bunge tarehe 13 Novemba, 2020 alisema anaomba Wizara ya Kilimo, Wizara ya Biashara na Wizara ya Mambo ya Nje ikishirikiana na Mabalozi waweze kukutana ili kuangalia ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zinazokabili kilimo. Ninaamini kabisa Wizara hizi zikikutana zikaweza kuweka mawazo yao ya pamoja tutaenda kutatua changamoto kubwa ya kilimo inayowapata wananchi wa Tanzania. Wengi wanalima lakini hawajui watauza wapi mazao yao.

Mheshimiwa Spika, inawezekana kutokana na uelewa mdogo au kutokujua namna gani ya kuongeza thamani ya mazao yao, wanakuja wafanyabiashara kutoka nje ya nchi; nchi za Jirani hapa, wananunua mazao yanayolimwa hapa Tanzania, wanakwenda wanayaongezea thamani, wanauza nchi za nje na wanapata fedha nyingi, lakini wakulima wanaolima ambao wanatoka Tanzania wanaendelea kubaki nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba sana Wizara ya Kilimo inayoongozwa na kaka yangu Mheshimiwa Prof. Mkenda, ninajua wewe na ndugu yangu Mheshimiwa Bashe ni viongozi makini sana, muende mkaliangalie suala hili kwa makini, wakulima wetu wanapata changamoto kubwa sana, wanaishia kufanya kilimo ambacho hakina tija, wanaishia kulima lakini hawana faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Benki ya Kilimo haiwasaidii wakulima wadogo. Inanufaisha wakulima wakubwa na wakulima hawa wadogo ndio tunaotegemea waende kuinua kipato chao na kuchangia kwenye pato la Taifa. Wanachangiaje sasa ikiwa hata hii benki ambayo imewekwa mahususi kwa ajili ya kuwasaidia, haiwasaidii?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa ambalo linakwaza kwenye kilimo ni upatikanaji wa mbegu bora. Wizara ya Kilimo, nimesikia kwenye hotuba yenu, mmetenga bajeti na mtasimamia kuhusu upatikanaji bora wa mbegu za kilimo, tunaomba mwahamasishe wakulima ni namna gani wanaweza kwenda kulima mbegu bora na sisi tukaweza kupata mbegu zinazohitajika hata tukaacha kulia kama tunavyolia leo nchi haina mafuta, tunaenda kuagiza nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, leo tukilima kilimo hiki cha alizeti, ninaamini suala hili la kulia mafuta, mafuta, litakwisha. Haiwezekani nchi kubwa kama Tanzania yenye zaidi ya asilimia 44 ya ardhi yake inafaa kwa kilimo, lakini bado sisi tunaendelea kuagiza mafuta nje ya nchi. Ni aibu kubwa sana. Naomba sana Wizara ya Kilimo iangalie namna ya kuwapatia wakulima mbegu bora na ziwafikie kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pia suala la Maafisa Ugani, hili ni tatizo lingine. Leo hii Chuo cha Kilimo SUA kinatoa wataalam, lakini kwa sababu wanaona sekta hii haiwalipi, wanaenda kuajiriwa benki badala ya kwenda kusaidia wakulima hawa ambao ndiyo tunasema tutapata ajira, tutakomboa vijana, tutakomboa wanawake ambao wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, katika mazao saba ya kimkakati yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025, kuna zao la mkonge. Zao hili linalimwa pia Kilimanjaro, lakini asilimia kubwa ya wananchi hawa wa Kilimanjaro hawajui vizuri juu ya suala hili. Naiomba basi Wizara iangalie namna ya kuwapatia akina mama na vijana fursa ya kuweza kulima zao hili. Zaidi ya yote, tunalima hili zao la kimkakati, lakini pia tunahitaji kufufua kiwanda cha magunia kilichoko Moshi, kwani kimekufa. Tunasemaje tunaenda kutafuta mazao ya kimkakati, tunaenda kuzalisha bidhaa, lakini kile kiwanda ambacho kinatumika kuzalisha bidhaa hizo, hakipo; lakini tuna malighafi na hatuna mahali pa kwenda kuzipeleka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwanda cha Magunia cha Moshi ni tatizo. Kimechukuliwa na mwekezaji, lakini mpaka sasa hakijaendelezwa, lakini leo tunasema zao hili ni la kimkakati na pale Kilimanjaro tunataka wakulima wetu waende kulima zao hili. Wapolima, tunategemea wakauze pale na kiwanda kile kiweze kuboreshwa kisitengeneze tu magunia, kikatengeneze na vitu vingine ambavyo vinatokana na zao la mkonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kufufua kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools. Huko tutapata vipuri vya matrekta, ma-Power Tiler, lakini hivi hivi ndiyo vitakavyoenda kuwasaidia wakulima wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, Kilimanjaro tunalima ndizi na parachichi. Katika kulima ndizi, wakulima wetu mfano wanaotoka Jimbo la Hai wanauza mazao yao ya ndizi katika soko la Kwa Sadala, lakini soko hili limekwisha kabisa, hawawezi hata kuhifadhi vitu vyao. Mvua ikinyesha, ni shida hata mchuuzi kuingia kwenye lile soko kwenda kununua bidhaa. Ninaiomba Wizara iangalie kwa jicho la tofauti soko hili la Kwa Sadala ambalo linawasaidia akina mama wengi na vijana, kujikwamua kiuchumi waweze kupata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ESTER E. MALEKO: ahsante sana naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ESTER E. MALEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii nyeti ya Maliasili na Utalii. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pia nitoe pongezi za dhati kwa timu nzima ya Wizara kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye kuchangia kwa sababu mud ani mfupi sana. Naomba nichangie kupitia utalii kwa sababu kwa kwetu sisi Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya asili ikianza Brazil ambayo ni nchi ya kwanza duniani kuwa na vivutio vingi vya asili. Pamoja na hayo sekta hii ya utalii inachagia pato la 17% katika pato la Taifa. Si hivyo tu, inachangia ajira zisizopungua milioni 1.6, zile za moja kwa moja na ambazo siyo za moja kwa moja. Kwa hiyo, Wizara hii ni nyeti kwa sababu pia inaingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye kuchangia kwenye vivutio vyetu vya asili. Tuna kivutio kikubwa sana katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro. Kivutio hiki ni mlima Kilimanjaro, mlima huu kwa takriban watalii 45,000 mpaka 50,000 wanapanda kwa mwaka. Hata hivyo, kiikolojia mlima huu unaweza kupokea takriban watalii 300,000 kwa mwaka mmoja. Hivyo, unaona idadi ya watalii wanaopanda mlima huu ni 45,000 mpaka 50,000, ina maana kuna nafasi hapo ambayo hatufanyi vizuri. Nadhani hatutangazi vizuri mlima wetu au matangazo yako chini sana, kwa hiyo tujitahidi sana kutumia media. Leo media ni kitu kikubwa sana, watu wanashinda kwenye media, tukiweza kutumia tu Instagram kuutangaza mlima wetu, ambapo hatutumii gharama yoyote kubwa, tunaweza kuutangaza kwa kiasi kikubwa lakini pia hatuwezi kutumia gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tukachukua watu maarufu mfano Ronaldo, Messy na wengine wengi tukawafanya wao wakaja Tanzania, tusiwatoze hata senti tano, tukachukua wao wanapokuja Tanzania wakalala bure wakapata huduma zote bure, lakini yule mtu aka-post tu kwenye page yake yenye followers zaidi ya milioni 50 kwamba yuko Kilimanjaro, tayari tumetangaza mlima wetu na hatutumii gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, nimeona Wizara inafanya vizuri sana, wamemleta Mamadou kama balozi wa utalii, lakini si hivyo tu jana amekuja Zari the boss lady kama balozi wa utalii. Namshukuru Mungu nilipata nafasi ya kuzungumza naye na kubadilishana mawazo. Kama Mbunge ninayetoka Kilimanjaro nilimwalika aweze kuupanda Mlima Kilimanajro na amekubali, hivyo nawahamasisha Wabunge tuungane pamoja kwenda na Zari kuupanda Mlima Kilimanjaro kwa sababu sisi ni vivutio na sisi ni wawakilishi wa wananchi. Wananchi wakiona sisi tunaenda kupanda mlima Kilimanjaro, nao watahamasika na wataenda kupanda mlima. Kwa hiyo nawaomba Wabunge tuungane pamoja kupanda mlima Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, tunapaswa pia kuboresha rescue system katika mlima wetu wa Kilimanjaro. Watalii wanapokuja wakapata shida wakiwa kule mlimani wanapaswa kupata huduma sahihi. Ninaposema rescue system iboreshwe, naamini Wizara inajua namaanisha nini. Kwa hiyo ninaomba Wizara iboreshe rescue system iwape wale watoa huduma elimu bora zaidi ili iweze kuwahudumia watalii wanaopata shida wakiwa kule mlimani.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu tuwe na information center…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga.

MHE. ESTER E. MALEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Ester hujatuambia kama na wewe utakuwa unapanda, kwa sababu wako Wabunge hapa ambao watatamani kujua kama na wewe unapanda ili waambatane na wewe.

MHE. ESTER E. MALEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nimewahamasisha kwa sababu na mimi nitakuwa mmojawapo kwa sababu nimemhamasisha Zari apande Mlima Kilimanjaro, nitakuwa pamoja nao. Ahsante sana. (Makofi)